Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ametangaza rasmi kuwa timu ya Coastal Union ya Tanga, maarufu kama "Wagosi wa Kaya," sasa itaanza kutumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kama uwanja wake wa nyumbani. Hatua hii inalenga kukuza mchezo wa soka mkoani Arusha, huku pia ikileta manufaa makubwa kiuchumi kupitia sekta mbalimbali, ikiwemo hoteli na biashara za kitalii, kutokana na ongezeko la wageni wanaokuja kutazama mechi.
Wagosi wa Kaya wanatarajiwa kuanza rasmi kuutumia uwanjani leo, Oktoba 18, wakati watakaposhuka dimbani dhidi ya Dodoma Jiji FC saa 2:00 mchana, katika mechi ya Ligi ambayo itatoa ladha ya kwanza kwa mashabiki wa soka wa Arusha kuona Coastal Union ikitumia uwanja huo.
Mbali na mechi hiyo ya leo, mashabiki wa soka wa Arusha wana hamu kubwa ya kuona mtanange mwingine utakaowakutanisha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Yanga SC na Coastal Union, mechi ambayo itachezwa Oktoba 26.