"Wanawake ambao saa yao ya kuamka ni kilio cha mtoto. Wamefundishwa kuwa mama lakini maisha yakawalazimisha kuwa baba pia. Wanabeba mabegani mtoto, mkononi mfuko wa mboga, moyoni deni na usoni tabasamu ambalo halisemi ukweli.
Jamii imekuwa na haraka ya kuwahukumu kuliko kuwasaidia. "Mumeo yuko wapi?" Kana kwamba hilo swali lingeweza kulisha mtoto. Hakuna anayetaka kujua kuwa wengine walitelekerezwa, wengine walifiwa, wengine walikimbia jehanamu iliyoaitwa ndoa, lakini wote tunawaita kwa jina moja la single mother.
Single mother anafanya kila kitu kwa mtoto wake ili mtoto wake amini kuwa dunia bado ina upendo. Hamjui ni mara ngapi mtoto alilala akimwita baba, na yeye akageukia ukuta akafuta machozi kabla mtoto hayayaona. Watu wanaona mtoto anatembea na mama yake, wanahesabu kile ambacho mtoto hana, baba hayupo. Lakini hawahesabu kile mama alichokifanya ili mtoto huyu awepo. Hawajaona alivyogawanya kipande cha chakula mara mbili, akampa mtoto sehemu kubwa halafu akasema mimi sina njaa.
Single mother, labda dunia haijawahi kuwaambia, lakini leo niseme mimi: mmefanya kazi ya watu wawili kwa moyo wa mtu mmoja. Wakati dunia ilikupa sababu mia za kulia, ulimtazama mtoto wako ukafuta machozi. Ulikuwa baba alipokosekana, ulikuwa mama ulipochoka, ulikuwa bega wakati hakuna bega la kuwegemea. Na huenda mtoto wako hajui ni mara ngapi ulilala na mawazo ukiamka kesho bila kujua utaanzia wapi. Lakini siku moja atajua, atajua kwamba maisha hayakuwa mepesi, ila mama yake hakuwahi kuwa mwepesi wa kukata tamaa.
Single mother, kama leo hakuna aliyewahi kukushukuru basi nisikilize mimi. Asante kwa kubaki, asante kwa kupambana, asante kwa kumlea mtoto wako hata wakati wewe mwenyewe ulihitaji mtu wa kukulea, na kama machozi yanakutoka yatowe, umeshapigana vya kutosha".
Anaitwa Raiffa Abdallah.