Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete ameshangazwa na mikutano ya machifu inayofanyika nchini, akisema utawala huo ulishafutwa nchini.
Hayo ameyabainisha Dar es Salaam leo Juni 8, 2022 akiwa mgeni rasmi kwenye kongamano la 13 la Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo amesema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipinga ukabila na kuwaaunganisha Watanzania kutumia lugha moja.
“Sikuhizi nasikia kuna mikutano ya machifu siajua wanaitoa wapi? Sijajua akina Mangi Mkuu watarudi tena na watemi wale, na babu yangu ni mkuu wa kabila langu lakini akinialika kwenye mikutano hiyo sivutiwi nayo,” amesema Kikwete.
Amesema anachojua yeye suala la uchifu lilishakwisha nchini na kwamba hajui hata wakikutana huwa wanaenda kujadiliana kitu gani, huku akieleza kwamba hatamani kuona watu wanarudi nyuma na kuanza kufikiria kuhusu masuala ya ukabila.
Kikwete ambaye pia ni mkuu wa Chuo hicho Kikuu cha UDSM, amesema ili kufanikiwa kuishi katika misingi aliyoishi Mwalimu Nyerere, kuna umuhimu wa kizazi cha sasa kujifunza historia yake.
Awali akizungumzia kongamano hilo, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema chuoni hapo wataendelea kuchapisha mashapisho mbalimbali kuendeleza falsafa za kiongozi huyo ili wanafunzi wanaokwenda kusoma waelewe.
“Vijana wengi wanakuja kusoma hapa na wanasambaa nchi nzima kwakutambua hilo tutaendelea kutoa elimu kwao kwa kuchapisha matangazo yatakayokuwa yanaelezea kazi aliyofanya baba wa taifa wajifunze kwa sababu tunawategemea kuwa viongozi wa baadae,”amesema Profesa William Anangisye
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk John Kalage amesema Mwalimu Nyerere mambo mengi aliyokuwa anayazungumza falsafa zake bado zinaendelea kuakisi maisha ya sasa huku akibainisha aliweka mkazo kwenye kuhakikisha vijana wanapata elimu
Source: Mwanachi