Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka wakuu wa mikoa walioteuliwa na kubadilishwa vituo vya kazi kwenda kujirekebisha na kuwatumikia wananchi ipasavyo. Akizungumza Septemba 2, 2026, katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa na Katibu Tawala wa Mkoa, Rais Samia amewakumbusha viongozi hao kuwa wao ndio "jeshi lake" na asingependa kuona jeshi lake likichafuka au kuharibu kazi nzuri iliyokwisha fanyika.
"Nilisema kuwa wakuu wa mikoa nyie ndio jeshi langu. Sasa hakuna anayependa jeshi lake lichafuke"-Amesema Rais Samia
Rais Samia amebainisha kuwa uamuzi wa kuwabadilisha vituo vya kazi badala ya kuwaondoa umelenga kuwalinda na kuwaondosha katika matatizo na tuhuma mbalimbali alizokuwa akipokea kutoka katika maeneo yao ya awali. Amesisitiza kuwa vituo vipya walivyopangiwa vinatoa fursa mpya ya kujirekebisha na kuacha tabia mbaya au kuingilia majukumu yasiyowahusu, ili wajikite kikamilifu katika kuwahudumia wananchi.
"Sasa kama ulikuwa unajijua unatabia mbaya au yoyote kule ulikotoka, kupya unakokwenda ni nafasi mpya kajirekebishe. Kajirekebishe tumikieni wananchi kama inavyotakiwa. Ni kuwasevu au kuwalinda, kuwahami na yale ambayo nimekuwa nikipokea. Kwa hiyo nenda kajirekebishe."-Amesema Rais Samia