KCWW MASWALI YA RAMADHANI XVI
Tarehe 20 Ramadhani, 1438, sawa na 15 Juni, 2017.
SEHEMU YA KUMI NA SITA
Nimeulizwa, NANUKUU:-
Salam alaykum Shareef Abdulqadir. Hakika tunaelimika sana kutoka kwako juu ya Dini yetu! Mwenyezi Mungu akulipe kheri duniani na akhera. Naomba kuelimishwa zaidi, Alhabib.
Je, inajuzu kwa wafanya kazi wa viwanda vya kufua vyuma, kama chuma cha pua, au migodi ya kuyeyusha madini, ambako wanafanya kazi karibu na matanuri ya moto mkali sana, unaowaka masaa 24, siku nenda siku rudi, bila ya kusita, na hivyo inakuwa shida kubwa sana kwao kufunga Ramadhani.
Je, wanaweza kufidia kwa kulisha masikini, badala ya kufunga? Maana likizo yao ni kama wiki mbili au tatu tu, katika mwaka mzima, hivyo hawana muda wa kutosha kuja kulipa, Ramadhani yote. Nini hukumu yao? Wanaweza kutoa fidia, tu, badala ya kufunga?
JIBU
BISMILLAH
Haijuzu! Wenye kufanya kazi za sulubu, sulubu yoyte ile, yenye mazingira magumu kama hayo uliyoyataja , ambao wanafanya kazi karibu na matanuri ya moto mkali -au vibarua na mafundi wa ujenzi wa barabara, majumba na kadhalika, chini ya Jua laki, na khasa katika mataifa yenye joto kali- haiwajuzii kuacha kufunga Mwezi wa Ramadhani kwa hoja ya kwamba mazingira ya kazi zao ni magumu sana, na hivyo watoe fidia ya kulisha masikini. Haijuzu. Sharia ya kufunga inawahusu kama inavyo mhusu mtu yeyote mwengine. Hivyo, haiwezekani kutolewa fatwa ya jumla jamala kwamba wenye kufanya kazi za sulubu, mchana wa Ramadhani, wanaweza kuacha kufunga, na badala yake watoe fidia ya kulisha masikini mmoja kwa kila siku moja. Haiwezekani.
Sharia, kama wanavyo sema- ni msumeno. Na Sharia za Mwenyezi Mungu nazo vile vile ni msumeno, tena wenye makali pande zote mbili. Mwenyezi Mungu amesema: فمن شهد منكم الشهر فاليصمه! : Ataye shuhudia kuingia mwezi afunge!” Yaani atayekuwepo aishipo unapoingia mwezi wa Ramadhani, basi afunge.
Hivyo basi, ni wajibu wa kila aliyekuwepo hai kufunga isipokuwa wale wachache tu, walioruhusiwa kutokufunga na baadala yake ama kulipa baada ya Ramadhani, au kutoa fidia kutokana na ugonjwa usiotazamiwa kupona au wazee wasiomudu kufunga kabisa. Wengine wote, lazima wafunge, na kama kuna udhuru wa muda, basi ataruhusiwa kutokufunga, lakini LAZIMA alipe baadae, baada ya kuondoka udhuru huo, kama maradhi ya muda.
Wafanya kazi za sulubu hawamo humo. Na hivyo, ni suala la mtu mmoja mmoja na jinsi ya kukabiliana na kazi hiyo, siku hadi siku. Hakuna leseni ya jumla jamala, kwa sababu zifuatazo.
1. Kila mfanya kazi ana uwezo wake wa kuhimili uzito; hawawiani kwa nguvu wala uzima. Kila mmoja na uwezo wake na uzima wake.
2. Kila mfanya kazi, anaweza - akidhamiria kikweli- kuomba doria\shifti ya usiku, katika Ramadhani, badala ya mchana. Lilio muhimu ni kujipanga itakikanavo, ili aweze kufanikiwa.
3. Kila mmoja ana likizo katika mwaka. Kama hawezi kufunga katika hali kama hiyo, aombe kuchukua likizo yake katika Mwezi wa Ramadhani ili afunge.
4. Kila mtu, anapaswa kuamka kwa nia ya kufunga, na afunge kama kawaida. Endapo itamtokea baadaye, katika siku hiyo hiyo, kushindwa kuendelea na swaumu, basi inamjuzia WAKATI HUO, kufungua na kulipa siku nyengine baadae. Lazima alipe baadae kwa sababu udhuru wake ni wa muda; hivyo haingii katika wasioweza kufunga maisha yao.
Kwa maneno mengine, wafanya kazi za sulubu, kama wafanyakazi za viwanda vya kufua vyuma, madini, wachoma mikate kwenye matanuri, wahunzi, wajenzi wa barabara, wamwa-zege na kadhalika, wote hao LAZIMA WAAMKIE NA NIA YA KUFUNGA, na WAFUNGE, kikomo cha uwezo wao. Inapofikia kutoweza kuendelea na swaumu, katika siku maalumu, basi HAPO ndipo MWENYE tatizo hilo ndiye anaye ruhusiwa kufungua na anapaswa kulipa siku nyengine, nje ya Ramadhani. Lakini KAMAWE haingii katika kuacha kufunga na hivyo kufanya mbadala wa kulisha masikini.
Hivyo, hata akifikia hali hiyo, na akajikuta anapaswa kufungua, basi siku ya pili LAZIMA anuwie kufunga na aamke akiwa amefunga, na aendelee na kufunga kikomo cha uwezo wake, kwa mtindo huo huo, hadi mwisho wa Ramadhani. Siku atayohemewa, kikomo cha kuhemewa, basi afungue siku hiyo, na alipe siku nyengine baada ya Ramadhani. Hakuna kutoa fidia.
Ndiyo maana, hata madereva wa mabasi ya abira ya masafa marefu; kutoka mji mmoja hadi mji mwengine, wanawajibika kuamka wakiwa wamefunga; maana wao SI WASAFIRI, bali wamo kazini. Na hakuna basi au teksi inayosafiri, masaa 12 mfululizo, pasi na kutoweza kusimama katika miji mbali mbali. Hata mafuta ya gari hilo yataisha, na kupaswa kusimama kujaza mafuta.
Hivyo, madereva wa mabasi ya abiria hawamo safarini, wamo kazini. Na kama ilivyokuwa wafanya kazi kwenye migodi ya kufua vyuma na madini, wamo kazini, basi na madereva wa mabasi ya abiria, au treni, au ndege, au meli, na kadhalika, na wao wamo kazini. Si wasafiri. Wanasafiri ama na vyakula vyao, ndni ya vyombo hivyo, au wanajuwa wasimame wapi kupata chakula na wapi pa kupumzikia na kadhalika. Hivyo, lazima waamke na nia ya kufunga, na wafunge kikomo cha uwezo wao. Na hivyo, kufungua au kutokufungua ni kwa mujibu wa siku hadi siku, na kwa mujibu wa mtu na mtu mwengine; siyo kwa kuamua kuwa mwezi mzima hatofunga, na hivyo atowe fidia. Hapana.
Mfano wao ni zima-moto. Wafanyakazi wa kuzima moto, wanapaswa kuamka wakiwa wamefunga. Iktokea ajali ya moto, wakapaswa kwenda kuuzima moto huo, na mmoja wao akajikuta anapaswa kuvaa mavazi maalumu na kujitoma kwenye ndimi za moto, ili kwenda kumuokoa mtu ndani ya jumba linalowaka moto na kuweko moshi mkubwa, basi huyo anaweza kufungua ili akatekeleze wajibu huo, kwa wakti huo, kwa ajali hiyo, na atalipa siku nyengine. Lakini kama ataweza kuifanya kazi hiyo pasi na kufungua, basi aifanye na swaumu yake.
Maswahaba wa Mtume ﷺ na yeye mwenyewe, walipigana vita vya vikli vya Badr huku wakiwa wamefunga, hawajui hata watafuturia nini. Hivyo, unafunga kikomo cha uwezo wako, na unafungua unapokaribia kufika kikomoni. Katika hali kama hiyo, hakuna junaha kufungua na kulipa swaumu siku nyengine, nje ya Ramadhani. SI kulisha masiiini, kama mbadala wa kufunga.
Fidia ni kwa mgonjwa asiyetazamiwa kupona ugonjwa wake, au mzee, kikongwe, hawezi kabisa kufunga, na hana rajwa ya kurudia ujana, hadi kufa kwake. HAO, peke yao, ndio wanaoruhusiwa kutoa fidia ya kumlisha masikini kwa kila siku moja, badala ya kufunga. Akifariki, kati kati ya Ramadhani, basi fidia yake ni kwa siku alizokuwa hai tu, siku zinazo fuata kifo chake, hawajibiki, na hivyo halipiwi. Maana hana deni kwa siku hizo.
Kwa ufupi, kila mwenye kumuanini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, anapaswa kuamka, katika Ramadhani akiwa amefunga, isipokuwa wale waliopewa ruhusa kuamka pasi na kufunga. Hawa, peke yao, ndio inawajuzia kuamka bila ya kufunga, na badala yake kulisha masikini kwa kila siku moja inayo wapita, katika Ramadnani. Wengine wote, lazima waamke na nia ya kufunga, na wafunge kuanzia alfajiri hadi kuchwa Jua. Atakaye tokewa na udhuru wa kisheria, kati kati ya mchana wa Ramadhani, basi anaruhusiwa kufungua siku hiyo, na alipe baadae. Vile atayeharibu swaumu yake, makusudi, kwa tendo la ndoa, mchana wa Ramadhani anapaswa siyo kulipa siku hiyo tu, bali na kutoa KAFARA yaa kuhuaribu swaumu yake kwa makusudi.
********
2. Habib Abdulgadir! Assalamu alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh. Naomba msaada wako kunifafanulia jambo moja geni kabisa nimelikuta ughaibuni nilipokuja kufanya kazi. Niko mataifa ya joto kali (nchi imetajwa jina). Na nimekuta kuwa ni kawaida kwa watu wa nchi hii, mwenendo wao katika mwezi wa Ramadhani, ni kwamba mchana kwao ni kama usiku na usiku ni kama mchana. Kulingana na shughuli zao za kila siku. Yaani mchana wanalala kwa muda mrefu sana, na kama wanaenda kazini, basi kwa masaa machache sana. Wakitoka makazini wanarudi majumbani na wanalala hadi magharibi. Mchana mzima barabara ni tupu, na maduka karibu yote yanafungwa, hata yasiyokuwa ya kuuza vyakul. Lakini, ikiingia magharibi, wanaamka, wanafungua kinywa kwa kitu kidogo tu, kisha wanaanza kwenda mabarazani kwa mazungumzo, au kwenda madukani, hadi usiku wa manane. Kisha wanarudi majumbani mwao au kwenda kwenye makaramu na huko wanakula kila aina ya vyakula, mpaka ikiingia alfajiri, wanaaza kufunga kama jana. Wengine hata hawaendi msikitini. Yaani mchana wa Ramadhani kwao ni usiku, na usiku wa Ramadhani kwao ni mchana. Je, nini hukumu yao?
JIBU
BISMILLAH
Ni kweli, zipo badhi ya jamii zenye watu kama hao, na wanafanya hayo uliyoyasema na zaidi ya hayo. Na watu kama hao wapo siyo tu hapo ulipo, bali hata nje ya eneo ulipo. Ila si wote. Bado wapo waja wema wanaofunga Ramadhani kama itakikanavyo, na yumkini hao ndio wengi. Ila, kama kawaida, wapo vile vile wanaofanya munkari huo, hadharani, na kama utamaduni unaokubalika na kuzoweleka katika jamii husika, licha ya wanazuoni mbali mbali kukemea tabia hiyo. Hao ni miongoni mwa wenye kujidanganya na kuvuruga thawabu za swaumu yao. Ila swaumu zao ni swahihi. Kulala hakubatilishi swaumu, isipokuwa kwa kuzimia mchana kutwa. Hapo ni kuzimia na kutokwa na fahamu mcahan kutwa ndiko kunako batilisha swaumu. Ama kulala hakubatilishi swaumu, kwa sababu hakuna anayelala fofoforo mchana kutwa, pasi na kuzindukana hata kama ni sekunde chache.
Hivyo, kimsingi, usingizi haubatilishi swaumu. Na ni makuruhu sana, kulala mchana wa Ramadhani kwa makusudi kwa muda mrefu, hata kama kulala hakufunguzi swamu. Bali kunaweza kuwa ni haramu, iwapo vipindi vya swala vitampita bila ya kuamka na kuswali swala za faradhi za machana. Ataingia katika dhambi za kupuuza swala, na dhambi za kupuuuza swala ni kubwa.
Hivyo, ni vibaya sana, tena sana, kwa Mwislamu kugeuza mchana wake wa Ramadhani kuwa ndio usiku, na usiku wake wa Ramadhani kuwa ndio mchana, wake. Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa ibada, kuomba maghfira, kutenda amali njema, kukithirisha kuswali, kusoma Qur’ani, kutoa sadaka na kadhalika. Si mwezi wa kualal, wala si mwezi wa kufakamia na kula kila aina ya vyakula; utadhani mtu ametangaza vita vya vyakula aina kwa aina.
.
Naam, kama mtu ni mgonjwa, na ugonjwa wake hauhitaji kula dawa mchana, bali unahitaji kupumzika, kikamilifu, au kwa muda mrefu, basi hakuna junaha kwa mtu kama huyo kulala mchana wa Ramadhani, pasi na kupuuza kuswali swala za faradhi utapo wadia wakati wake. Na endapo itamwia shida kufunga na ugonjwa huo, basi anaruhusiwa kufungua na kulipa siku nyengine, nje ya Ramadhani.
******
3. Alhabib, Sayyid Abdulqadir. Nina suali. Baba yangu mzazi amefariki katikati ya Ramadhani. Je inajuzu nimlipie Ramadhani yote, au siku anazo daiwa tu? Na je inajuzu nimlipie kwa kumtolea fidia tu ya kulisha masikini?
JIBU
BISMILLAH
Endapo amefariki katikati ya Ramadhani, pasi na kuwa na deni la swaumu, basi hakuna cha kumlipia kitu; maana hawajibiki kufunga baada ya kifo chake. Lakini endapo amepitisha siku kadhaa, katika Ramadhani, bila ya kufunga, kutokana na udhuru wa kisheria, basi unaweza kumfungia, baada ya Ramadhani, kwa siku anazodaiwa, tu. Mtume ﷺ ameseam: من مات وعليه صم صام عنه وليه (متفق عليه)
“Ataye fariki, akiwa na deni la swaumu, basi anaweza kufungiwa na walii wake.” Muttafaq ‘Alayhi.
Hivyo, anaweza kulipiwa deni lake, tu, si asichodaiwa. Na kama hakuna wa kumfungia, hasa miononi mwa watoto wake au jamaa zake, basi inajuzu kumlipia fidia kutokana na mali aliyo acha, au kama hakuwacha mali, basi anaweza kulipiwa na jamaa wengine, hata watoto wake. Ila atatolewa fidia kwa siku anazodaiwa tu.
والله أعلم
وبالله التوفيق
السيد عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم
Imejbiwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chchote, na kuweka kwenye FB yako au kwenye WhatsApp na kwenye Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, kwa lengo la kusambaza na kuelimisha Dini. Changia kusambaza Dini, ujipatie thawabu.
kcwajawema@gmail.com