Ripoti ya LHRC yarejea mauaji ya Oktoba 29, yayaita kipindi cha giza

Ripoti ya LHRC yarejea mauaji ya Oktoba 29, yayaita kipindi cha giza

Elias Msuya

Platinum Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
267
Reaction score
1,014

Okt 29.png

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2025 kikiyataja mauaji ya Oktoba 29, 2025 kuwa kipindi cha giza katika ulinzi wa haki za binadamu Tanzania.

Mauaji hayo yalifanyika baada ya maandamano kuzuka katika mikoa mbalimbali nchini, ambapo waandamanaji walisema wanaupinga uchaguzi huo na walikabiliwa na nguvu za kijeshi kwa kupigwa risasi, huku kukiwa na ripoti pana za mauaji yasiyo halali, vifo vya watu wengi, na madai ya matumizi makubwa ya nguvu kupita kiasi na vyombo vya usalama wakati wa maandamano hayo.

Mashirika ya haki za binadamu, wachunguzi wa kimataifa na mashuhuda wanasema mamia ya watu waliuawa katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku makadirio yakitofautiana kutoka mamia kadhaa hadi maelfu, ingawa serikali haijatoa takwimu rasmi.

Kukatika kwa intaneti ​

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, siku ya uchaguzi, serikali iliweka vizuizi vya intaneti nchini kote, hali iliyozuia upatikanaji wa majukwaa ya kidijitali wakati wa maandamano yaliyopangwa.

“Huduma za mtandao ziliporejeshwa siku kadhaa baadaye, picha na video zenye maudhui ya kushtua zilianza kusambaa mitandaoni zikionyesha miili ya marehemu, majeruhi, na hali ya vurugu katika miji kadhaa ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Geita, Mara na Songwe.

“Mashuhuda wanasema maafisa wa usalama walitumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji na pia raia wasiohusika na maandamano. Katika baadhi ya matukio, wanajeshi waliovaa kiraia pia wanatuhumiwa kuhusika katika ufyatuaji risasi,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.

Uchunguzi wa kimataifa na madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi​

Ripoti hiyo imeangazia taarifa za mashirika kadhaa ya kimataifa yaliyochunguza na kufanya uchambuzi huru wa ushahidi wa video na picha za machafuko hayo.

Imeripoti shirika la habari la CNN katika ripoti yake na uchambuzi wake wa kitaalamu ulioonesha maafisa wa usalama wakifyatua risasi kwa raia wasio na silaha, ikiwa ni pamoja na matukio ndani ya makazi ya watu na wakati wa msako wa nyumba kwa nyumba.

Pia imerejea ripoti ya Shirika la Centre for Information Resilience (CIR) pia lililothibitisha zaidi ya picha na video 180, likihitimisha kuwa risasi za moto zilitumika mara kwa mara na maafisa wa usalama. BBC nayo ilithibitisha uhalisia wa baadhi ya video kwa kutumia teknolojia ya kutambua maeneo na picha za satelaiti.

Limetaja pia ripoti ya Shirika la Amnesty International, Human Rights Watch na wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa walioeleza wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa mauaji yasiyo halali na kufichwa kwa miili ya marehemu.

Madai ya vifo vingi, makaburi ya siri​

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kuwa angalau watu 700 wanaweza kuwa wameuawa kinyume cha sheria, huku vyanzo vingine vikisema idadi inaweza kuwa kubwa zaidi. Muungano wa mashirika zaidi ya 40 ya kiraia Afrika ulidai kuwa takriban watu 3,000 waliuawa, pamoja na madai ya kuwepo kwa makaburi ya pamoja maeneo kama Mabwepande Dar es Salaam.

Kimegusia taarifa za Chama cha upinzani CHADEMA kilichosema kimeandika vifo hadi 1,000 katika mikoa kadhaa na kikatoa tuhuma za miili kutupwa maeneo yasiyojulikana.

“CNN na CIR pia ziliripoti uwezekano wa makaburi ya pamoja katika maeneo ya Kondo (Dar es Salaam) na Tengeru (Arusha).”

Watu mashuhuri​

Ripoti hiyo imetaja watu mashuhuri waliouawa wakiwamo watoto, wanawake, waandishi wa habari, viongozi wa dini na wataalamu mbalimbali.

Imetaja tukio la, mwanamke mjamzito aliyeuawa jijini Arusha kwa kupigwa risasi akiwa anakimbia, huku mkoani Mbeya, mtoto aliyedaiwa kuuawa na maafisa wa usalama akiwa njiani kwenda dukani.

Pia kwa Dar es Salaam, Wakili Peter Makundi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika aliuawa kwa kupigwa risasi siku ya uchaguzi.

Waandishi wa habari kadhaa pia waliripotiwa kuuawa, wakiwemo waliokuwa wakiripoti maandamano Mbeya na Dar es Salaam.

Hospitali kuzidiwa na miili kupotea​

Ripoti hiyo imeangazia video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha mochwari za hospitali zikiwa zimefurika, hasa Dar es Salaam na Mwanza, zikidaiwa kuwa na miili mingi iliyolundikana kutokana na nafasi finyau, huku familia zikieleza changamoto ya kuwapata ndugu zao, huku baadhi zikisema miili iliondolewa kabla ya kutambuliwa.

Hata hivyo, ripoti hiyo imesema Serikali ilikanusha madai ya kuficha miili, huku baadhi ya hospitali zikisema video hizo ni za uongo. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa ulisema umepokea taarifa za kuaminika kuhusu uwezekano wa miili kuhamishwa au kufichwa.

Changamoto za demokrasia

Ripoti hiyo imeeleza mwelekeo wa Tanzania katika kulinda misingi ya haki, uhuru na demokrasia.

Moja ya maeneo yenye mjadala mkubwa ni uhuru wa kisias, ambapo ripoti hiyo inaashiria kuwa uwanja bado hauko sawa kwa washindani wote.

Vyama vya upinzani vinaendelea kukumbana na vikwazo vya mikutano na wakati mwingine hatua kali kutoka kwa vyombo vya dola.

Kwa upande wa uhuru wa habari, waandishi wa habari na wanaharakati wanatajwa kukumbana na vitisho, huku sheria zilizopo zikitumiwa kwa namna inayoweza kudhibiti mtiririko wa taarifa.

Uchambuzi wa kina unaonesha kuwa udhibiti wa habari hauishii tu kwenye vyombo vya habari vya jadi, bali pia unaenea kwenye majukwaa ya kidijitali.

Hii ina maana kuwa hata sauti za wananchi wa kawaida zinakabiliwa na vikwazo visivyo rasmi kama vile kujidhibiti (self-censorship) kwa hofu ya hatua za kisheria au kiusalama.

Matokeo yake ni jamii ambayo taarifa zake zimepunguzwa, na hivyo kufanya maamuzi ya umma kujengwa juu ya taarifa zisizo kamili au zenye upendeleo.
 

Attachments

Siasa za kibongo kuanzia taasisi mpaka mtu mmoja mmoja wote chawa tu. Hawa wanasheria waliandika barua kuhoji uhalali wa wabunge wa jumuiya ya afrika mashariki kurudi bungeni tena, wakajibiwa kwa barua yenye vifungu vinavyojitosheleza.

Wapo kimaslahi wakivizia fursa zinazojitokeza.
 
Back
Top Bottom