WAKALA WA SIRI S2 EP 02
Mtunzi; Robert Heriel
0693322300
ILIPOISHIA
Yule Mtu akiwa anaongea mara simu yake iliyokuwa mezani ikaita, jambo lililowafanya wote waitazame na kimya kidogo kitawale. Yule mtu akaichukua simu yake akapokea na kuiweka sikioni.
“ Hallo! Kweli! Upo wapi! Sawa nakuja sasa hivi” Yule mtu akasema akiongea na mtu wa upande wa pili simuni, kisha simu ikakatika.
“ Samahani nimepata dharura hapa, simu hii imetoka kwa moja ya viungo wetu waliopo maeneo mbalimbali hapa jijini, mambo yanazidi kunyooka, nafikiri niwaache muendelee na kikao mimi nikakutane na kiungo wetu huyu ili mambo haya yasilale. Mr. Gombe utaendelea kuendesha kikao hiki alafu utanipa maazimio” Yule mtu akasema kisha akatoka akiwaacha wenzake wakitamani kujua anaenda wapi.
ENDELEA
Ni katika chumba ambacho kulikuwepo na kitanda cha futi 3*6, pembeni lilikuwepo dirisha lenye pazi jeusi, kuta za chumba kile zilikuwa za rangi ya maziwa, sakafu ilikuwa ya vigae. Pembeni ya kitanda kulikuwa na stuli ambayo juu yake ilkuwepo taa ya sola iliyokuwa ikiwaka na kutoa mwanga uliotosha watu kuonana ingawaje haukuwa mwanga mkali. Juu ya kile kitanda alikuwa amelazwa Fernanda aliyekuwa hajitambui kwani alikuwa amepotza fahamu. Hapakuwa na mtu mwingine.
Muda kidogo ulipita, Fernanda akarejewa na fahamu, alijikuta akiwa amelala kwenye kitanda kisicho na godoro akiwa amefungwa mikono na miguuni huku mdomoni akiwa kawekwa kitu ili asiweze kupiga kelele.
“ Sasa hapa nitakuwa nipo wapi, yule mtu aliyeniteka kaenda wapi? Simu! Simu! Ile simu ndio ya muhimu. Kama wameichukua watakuwa wamenirudisha nyuma maili kadhaa” Fernanda akawaza huku akigeuza shingo yake upande huu na upande huu kukagua chumba kile. Kwenye kona kabisa akaona kimeza chenye droo, lakini hakuona vilivyopo juu yake kwani mwanga haukuwa na nuru ya kutosha kumfanya aone
“ Yule mtu aliyeniteka atakuwa ni nani? Anashida gani na mimi? Au ni hawa wanaomtafuta Sajenti, kwa kweli mambo haya yamenichosha, kila siku kusumbuliwa, nashindwa kufanya kazi zangu kisa kuwafahamisha alipokimbilia Sajenti. Hata kama ningekuwa nafahamu naapa nisingewaambia ng’oo” Fernanda akawaza lakini mawazo yake yalikatishwa baada ya mlango wa kile chumba kufungulia/ Akatangulia mwanaume mmoja aliyevaa tisheti iliyombana iliyochora kifua chake, akiwa kavalia na suruali ya kadeti, kisha akafuatia mtu aliyevalia suti ya kijani iliyomkaa vyema uso wake ukiwa nyuma ya miwani ya macho. Ndiye yule aliyekuwa akiongoza kikao cha siri.
“ Umefanya kazi nzuri sana. Alafu kumbe ni binti mrembo kabisa. Sasa inakuwaje binti mrembo kama huyu kujiingiza katika kazi za hatari namna hii?” Mtu yule akasema huku akisogea karibu na kitanda alichokuwa amelazwa Fernanda.
“ Embu washa taa nimuone vizuri” Yule mtu akasema na jambo hilo likafanyia, nuru ya taa ya umeme ikakijaza chumba chote na kuimeza nuru ya taa ya sola.
“ Waooh! She is an angel. Yuko na uzuri wa ajabu. Naweza muona vizuri sasa” Yule mtu asiye na jina akasema huku akitazamana na Fernanda.
“ Huyu Baba vipi, maneno yake ni dhihaka yananitia kichefuchefu” Fernanda akawaza huku akimtazama mtu yule mwenye asili ya kiarabu.
“Habari msichana mzuri, jina langu naitwa Abidin Wahid, ningependa kukufahamu. Sijui jina lako nani?” Abidin akasema akimtazama Fernanda kwa macho ya mtu mwenye kufurahia kuona kitu kizuri. Fernanda hakumjibu kitu, alikaa kimya huku akimtazama kwa hasira.
“ Msichana mzuri! Nimekuuliza unaitwa nani? Mbona hujibu, je wewe ni Bubu huwezi kusema?” Abidin akasema huku akimshika Fernanda kwenye kingo cha nywele zake usoni.
“ Hivi hawa wanaakili kweli? Kama machizi, Wameniwekea kitu mdomoni mimi nitaongeaje” Fernanda akawaza huku akiwa kaukunja uso wake.
“ Embu mfungue hiyo kamba mdomoni” Abidin akasema, yule mtu aliyejazia akamfungua Fernanda ile kamba mdomoni. Fernanda akavuta pumzi na kuiachia kama mtu aliyekuwa amebeba mzigo mzito.
“ Haya sasa tunaweza kuzungumza. Wewe ni nani, ulifuata nini kwenye nyumba ya Meja Venance, usiku wa manane kama huu?” Abidin akasema akimtazama Fernanda kwa macho ya upole kana kwamba ni mtu mwema. Fernanda bado alikuwa kimya zaidi ya yote akageukia upande wa pili kuwakwepa wasimtazame, Jambo hilo halikumfurahisha Abidin na yule Mwanaume mwenye mwili wa mazoezi.
“ Usitulazimishe kuwa watu wabaya, sisi ni watu wema, unapogeukia upande huo ni dalili ya dharau na kutupuuza, kamwe hilo siwezi kulivumilia na wote waliowahi kunionyeshea dharau walijutia maamuzi yao” Abidin akasema mara hii sauti yake ilikuwa mbali na sauti ya mwanzo aliyokuwa akizungumza, alizungumza kwa mitetemo ya hasira.
“ Haya msichana mzuri naomba unieleze, wewe ni nani na pale nyumbani kwa Marehemu Venance usiku huu ulikuwa unaraka nini?” Abidin akasema wakati huu akiwa amekishika kichwa cha Fernanda na kukigeuza kwa nguvu ili watazamane.
“ Mkuu huyu atatupotezea muda, kama hataki kwa hiyari tunaweza tumia nguvu” Yule mwanaume akasema.
“ Hapana Morris, Msichana huyu ni mzuri, tunapaswa tumuhoji kwa njia nzuri kama uzuri wake ulivyo, si ndivyo msichana?” Abidin akasema akimgeukia tena Fernanda pale kitandani.
“ Mnafiki Mkubwa wewe..” Fernanda akamtemea mate Abidin kisha akaendelea kusema;
“ Kama ningekuwa mzuri usingenifunga hivi, tangu lini Malaika akafungwa na pingu namna hii. Kama wewe usivyovumilia dharau ndivyo na mimi nisivyoweza kuvumilia kejeli na dhihaka” Fernanda akasema huku uso wake ukiwa umekasirika ungedhani jinni pori. Abidin alitoa kitambaa cha kujifutia mfukoni akajifuta, kisha kwa upesi kama umeme akamzaba kofi la uso Fernanda, lilikuwa kofi maridadi kabisa lililomfanya Fernanda aone Nyota na mwezi kwa wakati mmoja.
“ Unafanya makosa ambayo yataweza kukugharimu, ninaweza kukufanya uonekane kinyago watu wanaokufahamu wakakushangaa, nitakurarua..!” Abidin akafoka huku akimtolea maneno makali Fernanda huku akimkazia macho yake ambayo Fernanda aligundua ni yakidhalimu baada ya Abidin kutoa miwani usoni.
“ Mfungue hizo pingu” Abidin akasema,
“ Hapana Mkuu, huyu ni mateka hatari..”
“ Hatari? Kwa hiyo unamuogopa. Sivyo?” Abidin akasema akiwa kamkatisha Morris.
“Hapa sio kama namuogopa..”
“ Nimesema Mfungue hizo pingu” Abidini akasema kwa sauti ya juu yenye amri. Morris hakuwa na jinsi akamfungua Fernanda.
“ Mkuu, usidanganywe na uzuri wa huyu dada, huyu dada ni hatari kubwa, kama ungemuona mtu aliyemuua kule kwenye nyumba ya Meja Vennace nakuhakikisha wala tusingemfungua hizi pingu” Morris akasema akiwa tayari kamfungua Fernanda pingu za miguuni na mikononi. Fernanda alijisikia kaunafuu, mwili wake ulikuwa huru ingawaje alikaa kinyonge.
“ Hapa lazima nicheze na akili za hawa mbuzi, nijiweke kinyonge, nijilegeze na kulendea lendea ili wasiwe na hofu juu yangu, alafu baadaye niwashtukize. Mbona wataonja joto la jiwe” Fernanda akawaza huku akiwa bado kajilaza akiwa kafunguliwa pingu.
“ Unaweza kukaa ewe msichana mzuri” Abidin akasema huku akimtazama Fernanda na kumuashiria kwa macho akae. Fernanda akakaa akiwa kajinyong’onyesha”
“ Ni kweli tulifanya makosa kumfunga pingu Malaika, We made a mistake, please forgive us. Haya Bilashaka sasa tunaweza kuzungumza” Abidin akasema akiwa kairejesha sauti yake mfukoni kama awali akiongea kama mtu mwema anayepaswa kutumainiwa. Kisha akatoa Sigara Mfukoni akampa Fernanda, akaingiza tena mfukoni akatoa sigara nyingine na kiberiti cha gesi. Wakati huo Fernanda alikuwa keshaweka sigara mdomoni, Abidin akawasha kiberiti na kuiwasha sigara ya Fernanda aliyokuwa kaiweka mdomoni, kisha Abidin naye akaiweka sigara mdomoni mwake, akakiwasha kiberiti na kuiwasha sigara yake. Kimya kidogo kilipita wakati wawili hao wakiwa wanavuta sigara, Morris akiwa makini kuzichunga nyendo za Fernanda asijeleta hila yoyote.
“ Naomba nijitambulishe tena, Niite Abidin Wahid, huyu ni kijana wangu anaitwa Morris. Nafurahishwa kuwa nawe usiku huu mnene, nilipokuwa mdogo nilisomaga kitabu kilichokuwa kinajina “Angels descend during the great night” kilikuwa kitabu kizuri sana. Kilieleza kuwa Malaika wazuri hushuka nyakati wa usiku mkuu kama huu. Miaka kadhaa imepita leo nimethibitisha maneno ya kitabu kile. Naamini hata malaika wanamajina, tena majina mazuri. Haya embu nambie jina lako waitwa nani?” Abidin akasema kwa sauti iliyotulia, hakika maneno yake kwa mwanamke dhaifu huweza kuuchota moyo wake, lakini haikuwa kwa Fernanda.
“ Ninaitwa Fernanda, malaika jike mtoa roho” Fernanda akasema huku akiangaza macho yake huku na huku. Maneno hayo yakamfanya Abidin atabasamu,
“ Mwanamke huyu ni mzuri kama nini, lakini pia anasauti zuri mithili ya ndege waimbao asubuhi” Abidin akawaza.
“ Malaika mzuri mtoa roho, nini ulichokuwa unakitafuta katika nyumba ya Meja Venance?”
“Labda ningetangulia kwanza kuwauliza ninyi, jambo gani limewafanya mnikamate nikiwa katika nyumba ya Marehemu Meja Venance? Ninyi ni kina nani? Mkinijibu hayo basi nitawaambia kilichonipeleka kwa Meja” Fernanda akasema, kisha wote wakapeleka sigara mdomoni wakavuta pafu ndefu kisha wakaachia na kutoa moshi mzito mdomoni na puani ulioziba nyuso zao kwa kitambo.
“Ninyi ndio mlimtuma yule mwenzenu niliyemuua kule kwa Meja Venance?” Fernanda akauliza baada ya kuutupa moshi nje yam domo na pua zake.
“ Umeua! Hivi kumbe ni kweli..” Abidin akakatishwa na Morris
“ Mkuu nilikuambia nilipofika kule kwa Meja Venance, baada ya kumzimisha huyu, niliingia kwenye nyumba ya Meja, nikakuta mwanaume wa miraba minne ameuawa muda mfupi tuu. Nikajua aliyemuua ni huyu mwanamke hapa..” Kabla Morris hajamaliza kuongea Fernanda alimpulizia Morris moshi mwingi usoni uliompata sawia, na kwa upesi akamrukia Abidin na kumpiga ngumi mbili mfululizo zilizomfanya Abidin aanguke chini, lilikuwa shambulizi la kushtukza ambalo kamwe yeyote kati yao hakuwa amelitarajia. Bila kupoteza nafasi huku akijua kuwa anacheza na mdomo wa mamba, Fernanda akamrukia yule mwanaume mgongoni na kumpiga visukusuku vya kichwa kama vitatu, yule mtu akaanguka chini. Abidin akiwa pale chini akawaa anahangaika kuitoa bastola yake ili ampige Fernanda lakini kabla hajaikoki aachie risasi bado akiwa amemnyooshea bastola Fernanda, masikini alikuwa kachelewa, Fernanda alimrukia Free Kick na kuupiga mkono bastola ikaruka juu na kabla haijafika chini Fernanda akaiwahi kuidaka, wakati huo Morris alikuwa akija nyuma kwa kasi ili ampige Fernanda, kama paka akajibetua ili amkwepe Morris, ndio alifanikiwa kumkwepa lakini aliparazwa kidogo na mkono wa morris jambo lililomfanya apepesuke na kupoetaza muelekeo akaangusha bastola. Morris akaenda kumuangukia Abidin pale chini. Kama mtu mmoja wakaamka kwa pamoja Morris na Fernanda wakawa wanatazamana kwa hasira na uchungu wa kuuana, macho yao yakaenda pamoja mpaka ilipoandukia Bastola. Bahati mbaya bastola ilikuwa karibu zaidi ya Morris kuliko aliposimama Fernanda. Morris alivyoona hivyo akatabasamu huku macho yake bado yakiwa makini kutazamana na Fernanda.
Morris akafyatuka kama mshale kuiwahi ile bastola lakini akiwa kainama kabla hajaiokota, Fernanda akainyanyua stuli ambayo juu yake ilikuwepo taa ya sola. Akampiga nayo ya kichwa, Morris akaanguka na damu zikamtoka mdomoni, wakati huo Abidin alikuwa akinyanyuka kwa upesi kuifuata ile Bastola lakin naye alikuwa kachelewa, Fernanda alimrukia akampiga teke la uso Abidin akaangukia upande ilipomeza akaigonga ile meza na mara vitu vilivyokuwa juu ya meza vikaanguka. Macho ya Fernanda yalihamanika alipoiona ile simu ya Meja Venance aliyoichukua kule nyumbani kwake. Kwa upesi Fernanda akachukua bastola akamuelekezea Abidin aliyekuwa pale chini akimtazama Fernanda kwa macho ya kuomba msaada. Kabla Fernanda hajataka kumpiga risasi akasikia kuna sauti ya mtu akija, kwa upesi akaiokota ile simu. Kisha akamnyanyua Abidin na kumkaba akiwa kamuwekea risasi shingoni. Mlango ukafungulia akatokea mwanaume aliyevalia suti nzuri iliyosimama. Yule mwanaume alikuwa hajajiandaa vyema kwani hakujua kuna hatari yoyote, hivyo alikuwa amekuja mzima mzima kama kifurushi kinachopelekwa na maji. Fernanda hakutaka kupoteza muda akampiga risasi ya kichwa yule kijana akadondoka chini.
Jambo hilo likazidi kumuogopesha Abidin, lakini pia likampa wasiwasi Fernanda kwani bastola haikuwa na kiwambo cha kuzuia sauti, hima hima Fernanda akatoka akiwa kamuweka Abidin kama ngao yake. Akafungua mlango na kuchungulia upande huu na upande huu, hapakuwa na mtu isipokuwa korido ndefu sana.
“ Njia ya kutoka humu ni ipi?” Fernanda akauliza.
“ Hautafanikiwa kutoka humu ndani. Upo gorofa ya chini kabisa katika jengo hili. Umejiingiza katika matatizo makubwa sana Fernanda” Abidin akasema. Fernanda akampiga na kitako cha bastola,
“ Nimekuuliza njia ya kutoka humu ni ipi? Sitaki maelezo mengine” Fernnda akasema akiwa amekasirika. Kabla hajajibu sauti za watu wanaokimbia zikasikika zikija mkukumkuku upande walipo wakina Fernanda. Hapo Fernanda akajua sauti ya risasi waliisikia.
“ Nimekuambia hautafanikiwa kutoka hapa, ni bora ujisalimishe huenda ukaonewa huruma lakini kwa kitendo ulichokifanya cha kuua vijana wangu sina uhakika kama hilo litawezekana” Abidin akasema huku akitabasamu, sauti yake sasa ilijawa na nguvu baada ya kusikia wenzake wakija kumuokoa. Fernanda bila kupoteza muda akamkokota Abidin upande mwingine wa korido ambao hakusikia watu wakija.
“ Huku unaenda wapi msichana mzuri? Huku hakuna njia” Abidin akasema lakini Fernanda hakuwa akimsikiliza alimkokota wakatokea sehemu yenye mgawanyiko wa njia mbili zenye korido ndefu pia.
“ Nambie njia ya kutokea ni ipi, nitakuua usiniletee upuuzi. Sema njia ni ipi?” Fernanda akampiga Abidin risasi ya paja, abiding akapiga ukulele wa maumivu.
“ Unaniua! Unaniua wewe shetani! Nakuhakikishia utalipia” Wakati Abidin akisema hayo mara wale watu waliokuwa wakija wakatokea wakiwa na silaha za moto, Fernanda akawarudisha kwa kupiga risasi jambo lililowafanya wajibanze. Fernanda akazidi kumkokota Abidin akisonga kuwakimbia watu wale, punde jengo zima likaanza kulia alamu ya kuashiria kuna hatari,
“Kumekucha! Kazi ndio imeanza hapa, hawa mbuzi wanaitana humu. Lazima niharakishe kuondoka, nikileta mchezo inaweza kuwa hatari kwangu, hii ndio nafasi ya pekee ya kujiokoa ambayo naamini haiwezi jirudie tena” Fernanda akawaza huku akimkokota Abidin kama mzigo, Hata hivyo akaona Abidin anamuelemea.
“ Chagua nikuue au unasema njia ilipo?” Fernanda akamsukuma Abidin akaanguka chini alafu akamuwekea bastola kichwani.
“ Subiri Fernanda, usiniue. Pita njia hii itakutoa” Abidin akasema kwa maana macho aliyoyaona kwa Fernanda hayakuwa macho ya kibinadamu, yalimuambia kuwa akileta mchezo yatafyonza roho yake. Fernanda akampiga Abidin kitako cha bastola, Abidin akapoteza fahamu. Fernanda akampekua Abidin mifukoni lakini kabla hajafika mbali sauti kali ya amri ikitokea mita kama hamsini ikasikika ikisema;
“ Tulia hivyo hivyo”
ITAENDELEA.
Kitabu hiki kinamahusiano makubwa na Kitabu cha " MLIO WA RISASI HARUSINI" ambacho tayari kipo sokoni.
Jipatie Hardcopy kwa bei ya Ofa Tsh 10,000/= Ikatayodumu mpaka tar 14/10/2021
OFA hii isikupite!
MLIO WA RISASI HARUSINI
Kitauzwa Kwa Tsh 10,000 badala ya Tsh 15,000.
Mwisho WA OFA ni tarehe 14/10/2021
TUMA PESA KWA NAMBA
0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel