Rostam azua mapya
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti
KAULI alizotoa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM) wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam juzi, zimepokewa kwa maoni na mtazamo tofauti na watu wa kada mbalimbali, wakiwamo wanasiasa na wasomi waliozungumza na Tanzania Daima.
Wakizungumza katika mahojiano ya ana kwa ana na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wasomi na wanasiasa walizielezea kauli hizo za Rostam kuwa zinazofungua ukurasa mpya katika mwenendo wa mahusiano ya kisiasa na kijamii nchini.
Mmoja wa wanasiasa maarufu ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) na mshauri wa karibu wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Jussa Ismail Ladhu, alieleza kuguswa na kauli zilizotolewa na mbunge huyo ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa akiandamwa na jinamizi la ufisadi.
Akifafanua, Jussa alisema hoja ya Rostam kuhusu kuanza kuwapo kwa ubaguzi katika masuala ya siasa kwa upande wa Tanzania Bara, ni jambo la hatari kwa umoja na mshikamano wa kitaifa kwani ndilo limekuwa likivitafuna visiwa viwili vya Pemba na Unguja kwa miaka mingi, na tayari athari za jambo hilo zimekuwa zina madhara makubwa.
Ninaungana naye kusikitika kwamba, tatizo la ubaguzi wa rangi ambalo limekuwa linatukwamisha sana huku Zanzibar, sasa limeanza kuingia Tanzania Bara. Hii ni hatari, alisema Jussa.
Alisema kauli hiyo ya Rostam inapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka na kwamba, iwapo itathibitika kuwa alichokisema si jambo la kweli, basi atalazimika kuwajibika kwa kulieleza taifa uongo.
Jussa alieleza kwamba, tamko la juzi la Rostam limekumbusha masikitiko ya watu wengi, ambao waliguswa na uamuzi wa Spika wa Bunge, Samuel Sitta wa kumzuia kutoa utetezi wake kuhusu uhusiano wake na Richmond na Dowans, tena baada ya Bunge lenyewe kumtaka afanye hivyo awali.
Inasikitisha kwamba leo Rostam anatoa maelezo hayo miezi kadhaa baada ya Spika kumzuia kutoa utetezi wake bungeni, kuhusu Richmond na Dowans, hata kusababisha hivi sasa Watanzania kubakia kizani kwa sababu tu ya kukosekana kwa fursa hiyo ambayo ilitokana na agizo la Bunge hilo hilo, alisema Jussa.
Mbali ya hilo, Jussa alieleza kusikitishwa na kile alichokielezea kuwa ni unafiki wa wanasiasa, kama ule unaoonyeshwa na Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye wanaita baadhi ya watu mashetani na wao wenyewe wakawa wa kwanza kwenda kwao kuomba.
Lililotia aibu katika mazungumzo yale ya Rostam, ni hili la kuwa na wanasiasa wanafiki kama Mtikila. Watu wa namna hii wamekuwa wanaitukanisha siasa na wanasiasa. Huyu mtu anamwita mwingine ibilisi, halafu fedha ya huyo huyo anayemwita shetani unaichukua. Kama mtu ni shetani, basi hata fedha yake pia ni ya shetani. Kama haikuwa safi kwa kuomba, pia haitakuwa safi kwa mkopo, alisema akionyesha kukerwa na kitendo cha Mtikila kuchukua fedha kutoka kwa Rostam.
Mbali ya hilo, alisema kikubwa katika kauli aliyoitoa Rostam juzi, ni ule wito wake wa tahadhari kwamba taifa linaelekea kubaya, hasa kutokana na kuanza kuibuka kwa watu wanaozushia wengine uongo.
Alisema alikuwa akikubaliana na Rostam kwa asilimia 100 kwamba, juhudi kubwa inayofanyika hivi sasa kwa watu kuzungumzia watu, kama ingeelekezwa katika masuala mengine yenye tija, basi taifa lingepiga hatua kubwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliuelezea mjadala unaozingira suala hili zima kuwa usio na msingi, na ambao unapaswa kukomeshwa.
Hata hivyo, Zitto alisema Rostam alipaswa kutambua kuwa, mbegu za ubaguzi ambazo zinajionyesha leo hii katika taifa, chimbuko lake ni kundi la mtandao ndani ya CCM, ambalo mbunge huyo wa Igunga alikuwa mmoja wao.
Alisema harakati za kibaguzi zilizoendeshwa na kundi hilo la mtandao dhidi ya mwanasiasa na mwanadiplomasia Dk. Salim Ahmed Salim, wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala, ndiyo msingi wa vitendo vya kibaguzi leo hii.
Baadhi yetu tulipata kuonya mapema kuhusu utamaduni wa kibaguzi, uliokuwa ukiratibiwa na kundi la mtandao, ambalo Rostam ni mmoja wao, wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2005. Tuliwaeleza mapema kabisa kwamba ipo siku mambo haya yatawarudia, alisema Zitto mmoja wa wanasiasa wanaoheshimika nchini.
Hata hivyo, Zitto alisema alikuwa akiamini kwa dhati kuwa, kama Mtanzania, Rostam Aziz alikuwa na haki ya kualikwa na kwenda katika hafla ya Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri.
Alisema angepata nafasi ya kumshauri Rostam kabla ya kwenda pale, angemtaka aende akashiriki katika shughuli ile na kutoa mchango wake na kuondoka pasipo kusema neno.
Kilichowastua watu wengi ni yale maneno aliyoyasema alipokuwa kanisani, na si kwenda kwake pale kwani mimi naamini kama Mtanzania alikuwa na haki ya kuitikia wito na hata ikibidi kuchangia, alisema Zitto.
Alipoulizwa kuhusu matamshi ya Rostam kuwa kuna kundi la watu maarufu na wazito ambao wana ajenda ya kuchafua baadhi ya watu, Zitto alikuwa na haya ya kusema: Mbona unaniuliza kitu ambacho hata wewe unakijua? Ni jambo la kweli kwamba kuna makundi, na wewe unalijua hilo. Ninachosema mimi mjadala mzima huu hauongezi tija yoyote.
Kuhusu mjadala wa ufisadi kuteka ajenda zote nyingine muhimu, Zitto mbali ya kusema hoja hiyo ina ukweli, alisema suala hili linalojadiliwa ni muhimu sana na linapaswa kujadiliwa hadi hapo hatua zinazostahili zitakapochukuliwa.
Alisema kushindwa kwa serikali kuchukua hatua za mara moja juu ya mambo yanayohusu ufisadi, ndiyo chanzo kikuu cha kuendelea kushamiri kwa hoja hizi za ufisadi kila kukicha.
Ni kweli mjadala wa ufisadi umechukua muda mrefu sana. Hata hivyo, ni jambo ambalo hatuna budi kuendelea kulipigia kelele hadi hapo serikali itakapochukua hatua. Kushindwa kuchukua hatua za mara moja kwa serikali, ndiyo chanzo kikuu cha kuendelea kwa kelele na meneno mengi, alisema Zitto.
Alieleza kushangazwa kwake na kushindwa kwa serikali kuchukua hatua zinazopaswa hata katika suala kama la Richmond, ambalo Kamati Teule ya Bunge ilishatoa ripoti yake Februari mwaka huu.
Alisema ni jambo jema kwamba katika historia ya Tanzania, tatizo la ufisadi ambalo lipo, halijapata kuzungumzwa kwa uwazi na kwa mapana kama ilivyo sasa, hatua aliyosema tulipaswa kuipitia.
Hata hivyo, alisema kushindwa kuchukuliwa kwa hatua za haraka kuhusu ufisadi, ni moja ya mambo ambayo yamesababisha watu kama aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daud Ballali afariki dunia kabla hajaeleza kile alichokuwa akikijua kwa upande wake, juu ya wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Suluhisho ni kwa masuala haya kushughulikiwa mara moja, na matokeo ya kuchelewa huku ndiyo yaliyosababisha mtu kama Ballali afariki dunia kabla hajapata haki ya kujitetea au kueleza upande wake. Utamaduni wetu wa kukalia mambo umetufikisha hapa tulipo leo, alisema Zitto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia, alisema sasa nchi inaelekea kubaya zaidi kwani watu wameajikita zaidi katika kuzungumzia masuala ya mtu mmoja mmoja badala ya kuzungumzia masuala ya kitaifa.
Alisema hivi sasa nguvu nyingi inaonekana kutumika kuzungumzia ugomvi wa mtu mmoja mmoja badala ya kuzungumzia umasikini uliokithiri wa wananchi.
Mbatia alisema kama hali hiyo itaendelea, kuna hatari ya taifa kukatika vipande vipande, na huo ndiyo utakuwa mwisho wa Tanzania inayosifika kuwa ni nchi yenye amani na utulivu.
Ndugu yangu, nilishawaeleza kuwa kama waandishi, mna jukumu kubwa sana la kuhakikisha taifa linarejea katika mstari wake, na wala si kuendekeza vita vya watu wasioangalia matatizo ya wananchi, alisema Mbatia.
Alisema vielelezo alivyovitoa Rostam ni ishara tosha ya kile kinachofanyika katika nchi hii, ambayo kila kukicha, watu wamekuwa wakiangalia namna ya kuendeleza mapambano yanayotishia ustawi wa maisha ya Watanzania walio katika lindi la umasikini.
Kwa upande wake, Profesa mstaafu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Issa Shivji, alisema mchakato wa kisiasa hivi sasa unaelekea kubaya zaidi, kwani watu wameshaanza kukosa mwelekeo wa kulipeleka taifa sehemu inayotakiwa.
Alisema alichokisema Rostam ni maoni yake, na hata vielelezo alivyovitoa vipo wazi, hivyo yeyote mwenye kupinga au kuwa na hoja nyingine, atumie utaratibu wa kisheria.
Nionavyo, siasa haielekei pazuri hata kidogo, na hiyo ni ishara mbaya kwa taifa, sina cha kusema katika kile alichokisema Rostam, alisema Shivji.
Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema yeye alimtaka Mchungaji Christopher Mtikila na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kumuomba radhi Rostam kwa kudai hawatapokea fedha zake ilihali wamekuwa wakifanya hivyo kwa muda mrefu.
Mrema ambaye ni Mlutheri kiimani, alisema ili Mtikila na KKKT wajisafishe, ni vema wakarejesha fedha za mbunge huyo ambaye tangu zamani amekuwa bega kwa bega akishirikiana nao katika shughuli zao za maendeleo ya makanisa yao.
Alisema ni udhalilishaji wa hali ya juu na kumkosea heshima Rostam ambaye anatumia fedha kutoa misaada kila anapoombwa kufanya hivyo na KKKT na Mtikila.
Wao kama wanaona hawataki fedha za Rostam, ni vema wakarudisha fedha zake tangu alipoanza kuwasaidia, lakini si vema kumdhalilisha kama wanavyofanya hivi sasa, alisema Mrema.
Alisema Mtikila kamwe hawezi kuepuka lawama, kwani amekuwa akipiga kelele kuhusu ufisadi, wakati yeye mwenyewe amekuwa akiwazunguka watu kwa kwenda kupokea fedha za Rostam, ambazo ni hivi karibuni tu alidai zilitokana na ufisadi.
Mrema alisema vita ya ufisadi kamwe haiwezi kutokomezwa kama watu wanazungukana na kutumia fedha zinazotokana na mazingira yanayolalamikiwa.
Aidha, kuhusu kauli ya Mtikila kukopa fedha kwa Rostam, Mrema alisema hoja hiyo haina nguvu, bali kinachotakiwa hivi sasa ni kwa Mtikila kuzirejesha, na si kuanza kuwaambia watu kuwa fedha hizo ni za serikali au alikopa kwa mradi binafsi.
Kwani Mtikila hajui vyombo vya kukopa fedha mpaka akaenda kwa Rostam, tena kwa nguvu ya kusema ni za ujenzi wa kanisa? Azirejeshe ndipo awe na nguvu ya kuukemea ufisadi, alisema Mrema.
Pia aliigeukia KKKT kuwa haina haki za kuuambia umma kuwa wanasiasa waliache kanisa kwani lenyewe ndilo lililojiingiza katika siasa mwaka 2005, pale walipotagaza kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu.
Nimeshangazwa kweli na tamko la KKKT kuwa, wanasiasa waliache, wao ndiyo wanaojiingiza katika siasa kwa kuwaaminisha Watanzania kuwa kiongozi fulani ndiye anayefaa, alisema Mrema.
Alisema wanasiasa ndiyo watu wanaopaswa kuliambia kanisa liachane na masuala ya siasa, lakini si kanisa ambalo limeonekana dhahiri kuwa na upendeleo.