Kuna MOU tu - IGA upo ndani ya 1 yr then wakishakubaliana ndiyo utakuja mkataba wa Operations ndiyo utakuwa na duration.
1
AZIMIO LA BUNGE NA. ….. LA MWAKA 2023
AZIMIO LA BUNGE KUHUSU MAPENDEKEZO YA KURIDHIA MAKUBALIANO KATI
YA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA SERIKALI YA
DUBAI KUHUSU USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA KIJAMII KWA AJILI YA
UENDELEZAJI NA UBORESHAJI WA UTENDAJI KAZI WA BANDARI TANZANIA
LA MWAKA 2023 (INTERGOVERNMENTAL AGREEMENT – IGA, BETWEEN THE
UNITED REPUBLIC OF TANZANIA AND THE EMIRATE OF DUBAI CONCERNING
ECONOMIC AND SOCIAL PARTNERSHIP FOR THE DEVELOPMENT AND
IMPROVING PERFORMANCE OF PORTS IN TANZANIA)
KWA KUWA, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iliingia Makubaliano ya Awali (Memorandum of
Understanding - MOU) na Kampuni ya DP World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya
Dubai mnamo tarehe 28 Februari, 2022. Makubaliano hayo yalikuwa na lengo la
kubainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa
miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na Maziwa Makuu, maeneo maalum ya
kiuchumi (special economic zones), maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo (logistics
parks) na maeneo ya kanda za kibiashara (trade corridors);
NA KWA KUWA, Makubaliano hayo ya Awali yalitokana na kudhihirika kwa tija, na
ufanisi mkubwa uliopatikana kwenye Bandari mbalimbali duniani ambapo, Kampuni ya
DPW imewekeza kama vile Dubai, Senegal, Msumbiji, n.k na kupelekea huduma za
uchukuzi kwa njia ya maji kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la eneo au nchi
husika;
NA KWA KUWA, katika kuhakikisha Tanzania inapata tija stahiki kupitia huduma za
bandari, mnamo tarehe 25 Oktoba 2022, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Dubai zilisaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii
kwa ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji kazi wa Bandari;
NA KWA KUWA, Mkataba unaolengwa kuridhiwa unabainisha vipengele muhimu ikiwa
ni pamoja na: Mawanda ya Ushirikiano na Taasisi za Utekelezaji; Haki za Kuendeleza,
Kusimamia na Kuendesha shughuli za bandari; Ridhaa za Serikali; Ushirikishaji wa
Wazawa, Ajira na Majukumu kwa Jamii; Kodi, Tozo na Ushuru nyinginezo; Utatuzi wa
Migogoro; Sheria zitakazosimamia Mkataba; Muda wa Mkataba na Usitishwaji wa
Mkataba; Kuanza Kutumika kwa Mkataba; Utekelezaji wa Mkataba (IGA) Ndani ya
Sheria za Nchi; na Ubadilishanaji wa Hati za Uridhiaji.
2
NA KWA KUWA, Mkataba huu baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Serikali ya Dubai ni miongoni mwa jitihada za dhati ambazo Serikali ya Awamu ya
Sita imeendelea kuzichukua kwa lengo la kuendeleza na kuboresha utendaji na ufanisi
wa bandari ili kuendana na dira ya Serikali kuhusu kazi za bandari kuwa na mchango
mkubwa katika mapato ya nchi na kuchagiza ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi
nchini, sambamba na mabadiliko ya usimamizi na uendeshaji wa shughuli za kibandari
duniani;
NA KWA KUWA, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo uwekezaji
mkubwa katika miundombinu ikijumuisha Mradi wa Maboresho ya Bandari Dar es
Salaam, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na uboreshaji wa usafiri kwenye maziwa kwa
lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha ustawi wa Watanzania kwa ujumla;
NA KWA KUWA, maboresho katika sekta ndogo ya bandari yataiwezesha Serikali
kuendelea kutumia fursa ya kijiografia ya nchi yetu kuzungukwa na bahari na maziwa ili
kupata masoko na kuzihudumia nchi zisizo na bahari ikiwa ni pamoja na kuimarisha
ushindani wa huduma za bandari na kuboresha shughuli za kijamii na kuichumi;
NA KWA KUWA, kuridhiwa kwa Mkataba huu kutakuwa na manufaa yafuatayo kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania:
(a) kuongeza fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana
na uwekezaji mkubwa na ongezeko la Shehena ya Mizigo itakayopitia Bandari ya
Dar es Salaam;
(b) kuongezeka kwa ufanisi katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi na
kuleta tija stahiki katika mnyororo wa thamani wa huduma za bandari nchini;
(c) kuongezeka kwa pato la Taifa kutokana na uboreshaji wa shughuli za kibandari;
(d) kuongeza tija na kuwezesha mwendelezo wa miradi mikubwa ya kimkakati
ambayo imekuwa ikijengwa na Serikali kama vile Mradi wa ujenzi wa Reli ya
Kisasa (SGR), ujenzi wa meli za mizigo katika Maziwa Makuu, na Mradi wa
uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam; na
(e) kuchagiza na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi (Multiplier Effect)
zikiwemo Kilimo, Utalii, Viwanda, Mifugo, Uvuvi, Biashara na Usafirishaji na hivyo
kuboresha ustawi wa Watanzania kwa ujumla.
HIVYO BASI, kwa kuzingatia manufaa ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
itayapata kutokana na Mkataba huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika Mkutano wake wa 11 na kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, linaazimia kuridhia Makubaliano kati ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai Kuhusu Ushirikiano
wa Kiuchumi na Kijamii kwa ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi katika
Bandari Tanzania (The Intergovernmental Agreement Between the United Republic
of Tanzania and the Emirate of Dubai Concerning Economic and Social
Partnership for the Development and Improving Performance of Sea and Lake
Ports in Tanzania).