Wakuu,
Kuna taarifa nzito sana imetolewa na Bunge la Ulaya (European Parliament) kuhusu mahusiano yetu ya kidiplomasia na hali ya haki za binadamu hapa nchini.
Kwa mujibu wa chapisho rasmi kutoka kwenye tovuti ya bunge hilo, Serikali ya Tanzania imeikatalia kamati ya Wabunge wa Ulaya kufanya ziara yao rasmi iliyokuwa imepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu wa Mei.
Kwa ufupi, haya ndiyo yaliyo kwenye hii taarifa:
- Lengo la Ziara: Ujumbe huu kutoka Kamati Ndogo ya Haki za Binadamu (MEPs) ulipanga kuja Tanzania kufuatilia masuala ya demokrasia, utawala wa sheria, na haki za binadamu kufuatia sintofahamu ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025. Pia, walitaka kukagua miradi inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutembelea Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu iliyopo Arusha.
- Sarakasi za Tarehe: Awali, ziara hii ilipangwa kufanyika mwezi Februari mwaka huu (2026). Hata hivyo, Serikali ya Tanzania iliomba isogezwe mbele ili kupisha Tume ya Uchunguzi wa vurugu za uchaguzi ikamilishe kazi yake. Baada ya Tume hiyo kutoa matokeo yake Aprili 24, Kamati ya Ulaya ikapanga kuja mwishoni mwa Mei.
- Kuzuiliwa Kabisa: Ghafla, bila kutoa maelezo yoyote ya msingi, Mamlaka za Tanzania zimekataa kabisa kupokea ugeni huu, ikiwemo kuwazuia wabunge hao kuonana na asasi za kiraia (CSOs) pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini.
Kauli ya EU: Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mounir Satouri, ameeleza kusikitishwa sana na hatua hiyo, akisema kitendo hicho ni sawa na kukataa waziwazi ushirikiano. Amesema hatua hii inawazuia kufanya ufuatiliaji wa fedha za walipakodi wa Ulaya zinazofadhili miradi hapa nchini, huku akikemea kile alichokiita "muendelezo wa kudorora kwa haki za binadamu na kuminywa kwa upinzani."
Maswali yangu:
- Sovereignty vs Uwazi: Je, Serikali yetu ipo sahihi kuwazuia hawa wawakilishi wa EU kwa kisingizio cha kulinda mamlaka (sovereignty) na kutokuingiliwa mambo ya ndani, au kuna jambo zito tunaficha kuhusu uchaguzi wa 2025?
- Athari za Kidiplomasia na Kiuchumi: Nini athari za hatua hii ikizingatiwa EU ni mmoja wa wafadhili wakubwa wa miradi yetu ya maendeleo? Tunajiandaa vipi na uwezekano wa vikwazo?
- Ripoti ya Uchunguzi: Kwenye ile ripoti ya Tume ya Uchunguzi iliyotolewa Aprili, kuna nini hasa ambacho Serikali haitaki wageni waje kukichokonoa?
- Je, ni wakati muafaka kwa nchi za Afrika kukataa misaada inayoambatana na masharti ya ufuatiliaji wa kisiasa?
Nawasilisha kwenu wakuu, ulingo ni wenu.
Chanzo: Tovuti Rasmi ya Bunge la Ulaya - Soma Habari Kamili Hapa
View attachment 3585719View attachment 3585721View attachment 3585722View attachment 3585724