Maridhiano, msamaha, ni lazima vitanguliwe na ukweli. Wahusika ni lazima wakiri makosa waliyoyafanya, kisha waombe msamaha, na hatimaye wasameheane. Na hayo ndiyo yanakuwa maridhiano. Fikiria kuwa nimekupiga nikakuumiza, halafu nasema sijawahi kukupiga au nasimama na kusema ilikuwa sahihi kabisa kukuumiza, halafu nasema turidhiane! Inaingia akilini hiyo?
Tujifunze maridhiano yale ya Afrika Kusini: Serikali ya makaburu ilieleza kwa kina juu ya mauaji ambayo ilifanya kwa miaka mingi, mpaka wakaeleza namna walivyowaua baadhi ya watu, wengine waliokuwa wamepotezwa kama wanavyopotezwa hapa kwetu. ANC ilieleza pia baadhi ya maovu waliyokuwa wamefanya, na hata kuharibu mali za makaburu. Hata makundi binafsi na watu binafsi walieleza jinsi walivyokuwa wamewafanyia uovu baadhi ya watu. Na kila kundi, baada ya kueleza ukweli, liliomba msamaha. Kisha wakasameheana na kuridhiana.
Kwetu hapa maridhiano yanakuwa magumu kwa sababu wahusika wakuu hawataki kuwa wakweli, hawajawahi kuomba msamaha, zaidi wamebariki uovu!
Anayekwamisha maridhiano ni CCM na Serikali ya Samia, kwa sababu hawataki kukiri kuwa walichokifanya, kama walinzi wa usalama wa wananchi, kilikuwa ni uharamia wa ajabu. Wauaji wangekiri makosa yao, wakaomba msamaha, waliotengeneza matokeo bandia ya kura wangekiri uovu wao, wakaomba msamaha, ndipo yangefuata makundi mengine ambayo vitendo vyao vilikuwa triggered na vitendo viovu vya CCM na watawala.