18th Portion:
Baada ya kuachana na Mzee Dingi, nilirudi gheto direct. Siku hiyo hiyo mida ya jioni, yule mama mstaafu akanipigia simu;
Mstaafu: "Hujambo mwanangu?"
Analyse: "Mzima mama, shikamoo"
Mstaafu: "Marahaba. Vipi utakuwepo mjini mpaka lini?"
Analyse: "Kuna vitu naweka sawa, vikikamilika nitaondoka. Inaweza ikawa Jumatatu au Jumanne"
Mstaafu: " Tunaweza kuonana kabla hujaondoka?"
Analyse: "Sawa hakuna shida, nadhani Jumatatu jioni nitakuja".
Baada ya kuongea na yule mstaafu, jioni hiyo hiyo, Mzee KY nae akanipigia simu, kuniambia tuonane siku ya Jumatatu jioni bila kukosa, ili tuweke sawa mambo kadhaa. So, ndani ya siku moja nikawa na appointments mbili, na zote jioni.
Wa kwanza kuonana nae ni Mzee KY, tulikutana mida ya saa kumi kumi.
Mzee KY: "Umeshaongea na yule mama au kuonana nae tokea ufike mjini?"
Analyse: "Hapana, kwanini?
Mzee KY: "Ulimwambia chochote labda kuhusu huu mpango?"
Analyse: "Hapana, vipi kwani?"
Mzee KY: "Oky Vizuri, sasa shika hizi hesabu" (akatoa hela na kunipa).
Nikahesabu, zikafika laki 3 na nusu. Nikamuuliza za nini hizi?
Mzee KY: "Huo ndio mgao wako, kwenye ili dili haupo tena"
Nikabaki nimeshangaa, sipo Kivipi?. Maana kama sipo basi dili limekufa, ila yeye mbona anaongea as if dili bado lipo?.
Ni kama vile aliyasoma mawazo yangu, akaniambia "Wewe ulikuwa plan A, haikuwa plan pekee. Kwahiyo kama nilivyokwambia, naomba ukae pembeni, dili litaenda bila uwepo wako. Na usije kumwambia chochote yule Mama"
Nikabaki na mwangalia tu. Hapa ndio alikuja kunipa maelezo ambayo nilikuja kuhitimisha kuwa, uwepo wangu kwenye lile dili haikuwa coincidence, kila kitu kilikuwa planned. Aliifahamu connection yangu na yule mama, na dhumuni la kunifanya Mimi kuplay role ya mwenyekiti, ili niweze kugain trust ya yule mama Kwa urahisi. Na hata kile kitendo cha Mzee Dingi Kuni unblock na kunitaka nipige nao kazi, yote ilikuwa ni maandalizi ya ili dili. Halikuja ghafla kama nilivyodhani. Baadhi ya maelezo aliyonipa, ndiyo niliyaelezea jana. Japo kuna mengine niliyaelezea jana, ila yeye alikuja kuniambia mbeleni kabisa wakati dili limeshafanyika.
Baada ya kumaliza mazungumzo yetu, tukaagana. Sikuwa na sehemu nyingine ya kwenda zaidi ya kule kwa mstaafu, ikabidi nielekee kule.
Nikiwa zangu mdogo mdogo nishakaribia kwa yule, Sina ili wala lile. Kumbe Mzee KY alikuwa ameniungia tela. Sikujua kama dhamira yake ilikuwa kupajua ninapoishi au alitaka kujua nitaelekea wapi baada ya sisi kuachana pale kwenye ile Pub. Naingia tu kwenye ile nyumba, na yeye huyu hapa. Kwa haraka haraka, mtu angeweza kuhisi kuwa tulikuwa tumeongozana wakati tunaenda pale.
Nilishtuka kumuona, japo sikuwa na uwezo wowote wa kumzuia yeye kuwa pale. Yule Mama mstaafu alipotuona wote alifurahi sana;
Mstaafu: "Naona watu muhimu mmeamua kunijia kwa pamoja, karibuni sana"
Analyse: "Asante sana"
Mzee KY: "Kijana alinipigia simu niungane nae kuja kukuona. Vipi za tokea siku ile?
Mstaafu: "Salama tu, Tunamshkuru Mungu uzima upo kama unavyotuona"
Kisha akanigeukia Mimi;
Mstaafu: "Karibu tena nyumbani, ila this time karibu kama mwenyekiti"
Aliniambia hayo maneno huku anacheka, Mzee KY nae akacheka kidogo. Tukaingia na kukaa sebleni kwake. Maongezi yote kayatawala yule mama tu. Kuna muda akaingia chumbani huko, kisha akatoka na hela;
Mstaafu: "Nilikwambia nitakurudishia hela ya Kodi uliyoacha, chukua laki mbili yako. Sitaki dhulma Mimi, najua kijana ndio kwanza unaanza kujijenga".
Mzee KY akamakinika kuona nitafanya nini. Binafsi nikaamua kuzikataa zile hela;
Analyse: "Hapana mama, nilihama kwa hiari yangu hii hela wala sio deni kwako"
Mstaafu: "Chukua mwanangu, hii haiusiani na kule kusainishiana, maana kule najua huwezi kuniangusha. Nakupa kama kijana wangu tu".
Unajua siku zote wakati nakua, kuna methali ilikuwaga maarufu sana.
"Sikio la kufa halisikii dawa"
Ukikanywa, usiposikia lazima uambiwe. Siku zote nilikuwa naichukulia kama methali tu, lakini in a real sense kwa mara ya kwanza nimekutana na ilo "Sikio la kufa". Unajua ili umuokoe mtu anayezama, sharti awe mtulivu vinginevyo mtazama wote. Au la, basi mpe kijiti, akishike umvute. Sasa huyu mama kila nikimpa kijiti, anakikataa. Kimoyo moyo nikajisemea atajijua mwenyewe.
Analyse: "Usijali mama, hiyo hela wewe Kaa nayo. Nimeondoka kwa amani kabisa, nikiichukua nitajisikia vibaya".
Akabaki na hela yake. Baada ya maongezi ya hapa na pale, Mzee KY akaomba niwapishe waongee kidogo. Sikuwa na namna, nikatoka zangu nje, wakaongea mambo yao kwa takribani nusu saa au dakika arobaini na tano. Baada ya hapo Mzee KY akatoka nje, tukaondoka wote.
Baada ya kutoka pale, akatafuta sehemu. Akaniweka kikao tena;
Mzee KY: "Sikia kijana, hivi unaweza kukadilia gharama kiasi gani imetumika kuandaa Ili dili?".
Ni kama alikuwa anaongea peke yake, maana kabla sijamjibu akaendelea tena;
"Mlivyokuja kule site, uliwaona wale majirani niliosalimiana nao?. Wale wote nimetoka nao huku. Uliwaona wale watu wanaolima pale?. Sijui hata wanalima nini, ila nao nimewaweka Mimi."
Akaendelea;
"Dili lifanikiwe au lisifanikiwe, hao wote lazima wapate hela yao. Sasa hebu niambie, lisipofanikiwa hela za kuwalipa zinatoka wapi?"
"Kuna watu huwezi kuwasaidia hata ufanye vipi, they are destined to lose. Hata ukisema umuache na hela zake akanunue eneo halali, still zile hela ataenda kuzifukia chini akitegemea zitachipua, ila ataambulia hasara. Najua hukuchukua ile laki mbili yake, sio kwamba huitaki au unamuonea huruma, bali you feel guilty. Nitakupa Mimi ile laki mbili, soon after dili kufanikiwa, ila for now naomba usinizibie njia, maana siwezi elezea nitakachokufanya. Umenisikia..........?'' Akataja jina langu halisi.
Nikashtuka, amelijuaje jina langu?.
Mzee KY: "Wote mliopo kwenye Ili dili hakuna nisiyemjua, kuanzia anapokaa au sehemu zake za kwanza kukimbilia hapa mjini, kwahiyo kabla hujafanya jambo utakalokuja kulijutia, ni heri ujifikirie mara mbili"
Nikabaki nimeduwaa tu Kwa muda, sielewi what next. Akaniambia, "Huna haja ya kuendelea kubaki hapa, wahi ukapange vitu kwenye makazi yako mapya, japo nakushauri hama". Hakusubiria jibu langu, akaondoka.
So, he knows me well?. Why nihame wakati ndio kwanza nimehamia au kuna msala unanisubiria? Wazo likanijia, kwanza yule mstaafu tumejuliana mjini hapa hapa, atajijua mwenyewe, ngoja nijihangaikie Mimi.
Nilivyofika ghetto, Yale maneno ya Mzee KY kuwa nihame pale, yakawa yananijia. Nikajikuta njia panda, nipange vitu au nijiandae kuhama?. Ila nimetoka kulipa Kodi ya miezi 6 siku chache tu zilizopita, nahamaje? Mbona ntakuwa nafaidisha wenye nyumba?. Lakini taswira ya Mzee KY ikawa hainipi picha nzuri ya yajayo. Akili ikaniambia nisipange vile vitu, nihame.
Nikampigia simu mwenye nyumba, kumuomba kesho tuonane kama ataweza. Akakubali.
Asubuhi nilivyoonana nae, nikampanga kuwa nimepata dharura natakiwa kusafiri haraka nje ya mkoa, anirudishie hata nusu kodi. Akanijibu "Mwanangu Cha kukusaidia hapa, labda nikuhifadhie vitu vyako kwahiyo miezi 6 utakayokuwa unapambana na hiyo dharura yako"
Nikaona hapa siwezi ambulia hata mia, cha zaidi nitapoteza muda tu kumbembeleza.
Kipindi Mimi nawaza namna ya kuhama pale. Mzee Dingi akanipigia simu na kuomba tuonane.
Nikafikiria huyu nikutane nae maeneo yapi?. Kipindi kile maeneo ya Tabata kuna mashindano ya mpira wa miguu yalikuwa yanaendelea. Viwanja vilivyokuwa vinatumika ni kile Cha Sigara na cha Tabata shule. Nikaona option ya Tabata shule ndio sahihi, maana ni mbali kiasi na ninapoishi. Lakini sababu nyingine iliyofanya nisione shida kukutana nae Tabata, ni kwavile nilikuwa natarajia kuhama.
Nikamwambia tukutane Tabata shule. Mzee Dingi akagoma, na hii ni kwavile pale ni karibu sana mitaa anayoishi yeye. NilivyΓ³ona bado anakomaa tuchange location, nikamwambia basi sitaki kuonana na wewe. Endelea na mishe zako.
Nilipata ujasili wa kumwambia vile kutokana na sababu Kuu mbili, kwanza kwenye dili lao sipo tena, alafu pili sijui anataka tuongee nini. Alivyoona nimekataa kuonana nae, hakuwa na choice zaidi ya kukubali tukutane maeneo yale.
Mida ya jioni nikasogea pale Tabata shule. Mzee Dingi alikuwa ameshafika kabla yangu. Mara zote ambazo tumekuwa tukikutana, vikao vilikuwa vinafanyikia either bar, pub or kwenye mgahawa. Ila this time hakutaka tukutane maeneo hayo. Akapendekeza tukutane kwenye yale majengo ya shule ya Kijapan (kuna shule ilijengwa na Wajapani maeneo yale). Nikajiuliza mara mbili mbili, why kachagua kule?. Ila kimoyo moyo nikajisemea akileta za kuleta, nitamfumua. Hasira zangu zote ziishie kwake.
Akanielekeza alipokuwa amesimama, nikamfata. Kufika pale, navikuta vizee vyote vitatu vipo. Mzee Dingi, Mzee Kidevu na Mwanasheria feki. Nikajiuliza vinanitakia nini?.
Nilivyowaona, sura zao zote ziliakisi shari, ila sikuwa na namna zaidi ya kuwasogelea. Zikapigwa story za hapa na pale, lakini Unaona kabisa hapa kuna jambo litatokea muda sio mrefu. Na Mimi kwa hasira nilizokuwa nazo, nikawa nasubiria kwa hamu ilo jambo litokee. Kwa jinsi tulivyokuwa tumejipanga, Mzee Kidevu alikuwa nyuma kidogo upande wangu wa kushoto, alafu mwanasheria feki na Mzee Dingi walikuwa mbele, tupo face to face. Tukiwa tunaendelea kuongea upande, kwa ghafla sana yule Mzee Kidevu akanirukia horizontally na kunipiga kichwa cha mbavu. Ni kitu ambacho sikuwa nimekitarajia, nikajikuta nayumba yumba. Kitendo cha kuyumba yumba, wale wazee wote wakanivamia kwa pamoja.
Nikajisemea hapa ndio nilikuwa napataka, ngoja nipunguze hasira zangu. Unajua Kwa jinsi nilivyokuwa nawakadiria, nilihisi dakika 10 nyingi wangesanda kwenye lile valangati. Ila yule Mzee Kidevu sijui hata anakulaga nini aisee, maana kuna muda nilimrushia ngumi, lengo nimpige shingoni, ila at the same time nae akanirushia ngumi. Ngumi kwa ngumi zikakutana, nilipatwa na maumivu kiasi kwamba nikahisi nimepiga mti. Kibaya zaidi yule Mzee hata akuugulia chochote, ndio kwanza anakuja tu.
Kipindi hicho chote, Mzee Dingi na Mwanasheria feki wameshasanda, wameniacha Mimi na Mzee Kidevu. Raia wamejaa wanauliza kuna nini?. Mzee Dingi linawajibu "Mambo ya kifamilia, tuachieni wenyewe". Yule Mzee Kidevu kama angekuwa na pumzi ya kutosha, angeniaibisha pale, kitu pekee kilichofanya akachemka ni pumzi. NilivyΓ³ona kazidiwa, nikaanza kumpelekea punch mfululizo. Kumbe bwana vile vizee vilikuja na back up. Muda wote tokea nimewakuta, kuna jamaa kipande alikuwa amekaa kwa pembeni anachezea simu.
Walivyoona hadi Mzee Kidevu kazidiwa, Mzee Dingi akaita "We Beka fanya kazi yako". Aisee nilivyomuona huyo Beka mwenyewe, sikuwa na namna zaidi ya kukimbia. Nilifungua turbo kuelekea kwenye makazi ya watu, yamekaa kama kota hivi. Nilidhani watanipotezea, nashangaa Beka kaniungia tela, Mzee Kidevu na wale wazee wengine nao wakaanza kuja nyuma yetu. Raia nao hawana dogo, baadhi wameacha kuangalia mpira, wametuungia tela.
Nikipiga hatua zangu mbili, ndio hatua moja ya Beka. Sikwenda mbali sana akanishika. Nikataitishwa. Mwanasheria feki akawa anafanyakazi ya kufukuza watu walau wasogee mbali ba tulipo. Nilivyokuwa chini pale, Mzee Dingi akawa anasema;
Mzee Dingi: "Mvue hivyo vitu alivyovaa ndio vinamtia kiburi"
Beka akanichukulia ile pete yangu yenye kihirizi. Kisha akataka kunivua na kacha niliyokuwa nimevaa mkononi
Mzee Dingi: "Hiyo muachie, haina madhara. Yupo nayo hata kabla hajaoneshwa Dunia ilivyo"
Baada ya kuichukua ile pete, akamkabidhi Mzee Dingi, alafu wakaanza kuondoka. Kwenye wallet nilikuwa na 70k, hawakuigusa kabisa. Yani Wazee shida yao ilikuwa ile pete tu. Nilikuwa bado nimekaa chini nikiwa na hasira, maana yule kipande aliniumiza. Ghafla kuna wazo likanipitia kichwani, sikujiuliza mara mbili, nikanyanyuka na kuanza kuwafata. Nilivyowakaribia nikainama chini na kuchota mchanga, Mzee Kidevu akawa ameniaona;
Mzee Kidevu: "Apostle umenichota unyayo, apostle umenichota unyayo?"
Kiukweli nilifanya vile kama kuwatisha tu, ila Mzee Kidevu akalichukulia serious.
Mzee Kidevu: "Apostle unachotaka kukianzisha unakimudu?. Kumbe mtoto mshenzi sana wewe"
Kabla sijamjibu kitu, yule Beka kipande akawahi kunikamata, akaniminya mkono hadi nikaachia ule mchanga. Nikabaki nimesimama tu. Kila Wakitaka kuondoka, natishia kama nainama kuzoa mchanga, wanarudi.
Mzee Dingi: "Huyu mtoto sio wa kumfanyia mzaha kabisa"
Jamaa kila wakipiga hesabu, walipoacha gari yao ni mbali lazima watembee. Lakini hapo hapo wanahofia huku nyuma naweza fanya jambo baya. Ghafla Mzee Kidevu akanirukia, tukaanguka wote chini. Kisha wakamwambia Beka anibebe mpaka kwenye gari yao.
Muda huo wote raia full kucheka, kelele na kuzomea. Jamaa ikabidi wanipe lift kwa lazima, wakaenda kunishushia Ilala Boma.
Nilichokuja kugundua, kumbe ile Jana nilivyoacha na mzee Kesho Yetu, alimpigia Mzee Dingi na kumwambia Mimi sitoshiriki tena kwenye lile dili, nikiendelea kuwepo kuna uwezekano mkubwa sana wa dili kufeli. Ndio maana kina Mzee Dingi wakaamua kuja kunishikisha adabu na kunipora kile kihirizi, maana waliona sihitajiki tena.
Ambacho Mimi na wale wazee hatukujua ni kwamba, wakati sisi huku tunashikana mashati, upande wa pili Mzee Kesho Yetu alikuwa anakamilisha dili. Jana yake wakati tupo kwa yule mstaafu, walivyo baki peke yao sijui hata alimwambia nini, ila chochote alichomwambia ndicho kilichopelekea wao kwenda kukamilisha dili.
Walau Mimi nilishajua kuwa kwenye lile dili sipo tena, ila kina Mzee Dingi wao walikuwa wanasubiria siku mbili mbele wakakamilishe dili.
Wamechukua pete yangu, na kuondoka kishujaa, kumbe upande wa pili Mzee Kesho Yetu anasepa na mkwanja peke yake.
Kibaya zaidi, anaacha msala ambao ni wetu wote, ilhali sisi wengine hatujajiandaa....