8th Portion:
.... Mtaji wa hela taslim aliokuwa nao Mzee Dingi ni milioni 3, japo tulivyopiga mahesabu tulitakiwa walau tuanze na milioni 5. Akasema hakuna shida, tunaweza anzia hiyo, then million mbili ataiongezea baadae. Nilitamani kumuuliza ataitoa wapi hiyo hela ya kuongezea, ila nikaamua kukausha.
Biashara ikaanza. Mkaa nikawa nachukulia Iringa, Mufindi, kuna Kijiji kinaitwa Usokani, huko ndio nikawa nachukulia mzigo. Nikiufikisha town, Mzee Dingi anaukabidhi kwa madalali wake, Kisha anasimamia makusanyo ya hela mpaka mzigo uishe. Ukiisha, narudi tena porini.
Mwanzoni wakati tunaanza, ilikuwa tunaleta trip moja, ila biashara ilivyo changanya, ikawa trip moja ikishafika town ikapokelewa na Mzee Dingi, kule kijijini naanza kukusanya mzigo mwingine. Sometime demand ikiwa kubwa, nilikuwa naenda hadi vijiji vingine kukusanya mzigo, mara nyingi nilipendelea kwenda maeneo ya Nyololo, kuna Kijiji kinaitwa Mzizi. Kutokana na kuzoeleka, ikafikia wakati tunaweza kusanya mzigo wa gharama kubwa hata kama hatuna hiyo hela. Mwanzoni usafiri tulikuwa tunatumia fuso moja ambayo ilibeba gunia 170, ila ikafikia wakati tukawa tunatumia kipisi chenye kubeba gunia 280, na sometime trip moja ingeweza kuwa na vipisi viwili.
Waliosemaga Ex ni kama furushi la miba, hatakiwi kurudiwa hata akija analia, maana ukimpa nafasi lazima atakuchoma tena, hawakukosea. Biashara ikiwa imenoga, vipisi viwili vipo town vinafaulisha mzigo, muda huo nipo kijijini najaza kipisi kingine nacho kiende mjini, Mzee Dingi akanipigia simu, kuwa uhitaji umekuwa mkubwa, hivyo nifanye mchakato wa kipisi kingine (Yani jumla viwe viwili) Kisha niviagize mjini. Kwavile hela ilikuwa haitoshi, iki kipisi nilichokuwa nasimamia muda huo, na kingine ambacho nimeambiwa nikiongeze, vyote ukiachana na gharama za usafirishaji na gharama za barabarani (ushuru, mizani,nk), gharama zingine zote hasa za mkaa wenyewe, kujaza, kushona na kupakia, zikawa ni Kwa Mali kauli, nikiwa naimani tutazilipa pindi mzigo ambao ushafika mjini utakapoisha.
Ila Cha ajabu, mzigo mwingine hadi nao unafiki mjini, ule wa mwanzo hela haijatumwa. Nikimchek Mzee Dingi, sound zinakuwa nyingi. Sikutilia mashaka kabisa. Kwavile hapakuwa na cha kufanya kule kijijini, nikawa nimesogea maeneo ya Mafinga ili kupumzisha mwili. Ila zikapita siku mbili bila kupewa feedback yoyote na Mzee Dingi. Nikimpigia, anasema nitulie atanipigia muda sio mrefu. Ila nikikaa kimya, hanitafuti.
Kule kijijini nao wakaanza kunipigia simu, wanataka hela zao. Nikimpigia Mzee Dingi, akawa hapokei simu zangu. Nikaamua kumfata Dar. Mpaka nafika, bado alikuwa hapokei simu zangu. Kesho yake mapema sana nikaamkia nyumbani kwake. Kufika pale naambiwa pale alishahamaga, kuuliza alipohamia, wanasema hawajui.
Nikajaribu kumpigia kwa namba ngeni. Alivyopokea na kujua ni Mimi, akanikatia simu. Akili ikaniambia nishapigwa!. Kule kijijini nao hawaishi kunipigia simu, na vitisho vikaanza kuwa vingi. Nikaona isiwe kesi, kwavile Mzee Dingi hapokei simu zangu, basi ngoja nianze kumsaka manually kwenye vijiwe vyake vyote. Kote nilimkosa, ila inaonekana kuna mtu akamfikishia taarifa za Mimi kumtafuta.
Akaamua kunipigia simu. Kupokea, namuuliza inakuwaje anafanya mambo ya ajabu kama yale?.
Mzee Dingi: "Sikupanga iwe hivi, ila kuna changamoto ilijitokeza, sikuwa na jinsi"
Analyse: "Hukuwa na jinsi? Wale jamaa wenye mkaa wao kule kijijini nawaambiaje?"
Mzee Dingi: "Wewe ni msomi mjanja apostle, wanakijiji hawawezi kukushinda. Tafuta namna yoyote ya kuwaelezea, au la, wapotezee, maana kule ushaondoka"
Analyse: "Tuachane na wanakijiji, kwahiyo Mimi sina mgao kwenye hela ambayo nimeisotea kule porini?"
Mzee Dingi: "Matatizo yaliyonikuta yanahitaji hela nyingi sana apostle, hii yenyewe unayoiona, bado haijatosha"
Analyse: "Kwahiyo unaniambiaje?"
Mzee Dingi: "Mungu ni wetu sote apostle, riziki yako haiwezi kupotea, itachelewa tu. Nitakuja kulipa, Alafu wewe bado kijana, nguvu na akili unavyo, pambana tu"
Aisee lilinitoka povu la kutosha, mpaka akaamua kukata simu. Nikapiga, akakata. Nikapiga, akakata. Kupiga tena nakuta kaniblock. Sijakaa sawa, yule jamaa mwenye mkaa wake akanipigia simu kutaka kujua kama nimewadhurumu au vipi?. Kila nikimpanga, haelewi. Huyu jamaa alikuwa mrefu, ana shingo ndefu pia. Alaf shingoni kwenye koromeo pamevimba kiasi. Huyu jamaa alikuwa na sauti ndogo/nyembamba sana japo ni mwanaume, hivyo watu wengi walipenda kumuita Kisauti, japo jina lake halisi ni Mbwana. Na Mimi humu nitakuwa natumia jina ilo la Kisauti. Sasa nikataka kuweka ahadi kwa Kisauti ya kulipa, ila nikifikiria hela wanayodai, nikaona sitoweza, maana Mzee Dingi ndio kaamua kunikataa. Kisauti alivyoona nipo kimya, akaamua kuniambia "Umeyataka mwenyewe mdogo wangu, sitolaumiwa kwa lolote nitakalofanya". Nikamuuliza utanifanya nini? Akajibu "Sikwambii, ila nataka ujionee". Kabla sijamjibu, akakata simu.
Nikampotezea!. Zikapita kama wiki mbili, nikiwa naendelea kumtafuta Mzee Dingi bila mafanikio. Nikaanza kupatwa na tatizo la mwili kuchoma choma. Yani inakuwa kama mtu yuko ndani ya mwili wangu, kashika sindano au pini, alafu ananichoma kwa kutokea ndani kuja nje. Ile hali ilianza taratibu sana, ila baada ya muda ikawa mwili mzima nausikia hivyo. Yani inaweza kunitokea kwa mfululizo ndani ya masaa matatu au manne, alafu inapoa kwa nusu saa au zaidi kidogo. Na hapo ikipoa, nakuwa nachomwa kidogo kidogo kwa mbali.
Yani kuna muda naweza kuwa nimelala au kupumzika, ghafla mwili unaanza kuchoma choma mfululizo, najikuta nasimama naanza kuzunguka tu gheto bila kujua nijikune wapi, inabidi nivue nguo,kisha nitumie ukuta kujikuna. Na ubaya yale maumivu yanatokea ndani kuja nje, sina namna ya kuyadhibiti. Kwa hali hiyo nikawa nashinda ndani tu, na ikitokea nahitaji kitu nje, basi mwendo ni kukimbia tu, tena nilikuwa naenda dukani na chenji kamili, ili nisipoteze muda dukani, na nikifika naanza kutoa hela kabla hata sijapewa nilichofata. Maana nilifikiria what if muuza duka kanipa bidhaa kabla sijampa hela alaf mwili ukaanza kuchoma, nikikimbia si wataniitia mwizi?. Just imagine nje watu wanakupiga, na ndani mwili unachoma, nitadeal na maumivu yapi, ya nje au ya ndani? Sikutaka hizo fedhea.Yani kiufupi nikiwa natoka dukani alaf ikatokea nikakutana na mtu anayenidai, angeweza hisi namkimbia yeye, kumbe mwenzie wala nawahi zangu ndani nikajikune ukutani.
Hali ilivyozidi kuwa mbaya, ikabidi niwajulishe home. Mama akaniambia niende. Aisee, sijawahi kusafiri safari chungu kama ile, maana bus ilikuwa ikipita kwenye matuta, hasa yale ya rasta, kwangu inakuwa mateso tupu. Maana narushwa rushwa, huku kwa ndani mwili unachoma.
Mpaka nafika destination ya lile bus, nilikuwa hoi hoi. Alafu kutokea pale, nikapanda kihiace cha kunifikisha kijijini kwetu. Njia nzima nailaani CCM Kwa kutotengeneza barabara, maana hapakuwepo na matuta, ila njia nzima kihiace kinatingishika, kokoto hazina uwiano.
Hali niliyofika nayo nyumbani, hadi bi mkubwa alijikuta chozi linamlenga lenga. Maana sikuwa hata na wiki tokea tatizo lianze, ila tayari uso ulishaanza kupoteza nuru.
Kijijini kwetu kuna zahanati kubwa tu ya kanisa, palivyokucha nikapelekwa pale. Fanyiwa vipimo vyote, ila halikuonekana tatizo lolote. Nikapelekwa hospital nyingine, nako majibu yanaonesha Sina tatizo. Ikabidi nirudishwe nyumbani, Mama muda wote majonzi tu.
Nikiwa nimelala kwenye kiti pale sebleni Kisauti akapiga simu. Kwavile sikuwa na hali nzuri, Mama hakuruhusu niongee na simu, akaipokeka yeye.
Kisauti akaulizia mwenye simu yuko wapi? Mama akamwambia nimelala. Kisauti akamuuliza Mama "Hali yake ipoje lakini?". Mama akamjibu kuwa hajisikii vizuri, amelala. Kisauti akacheka sana, alaf akamwambia Mama "Huyo ndio basi tena, hata msisumbuke nae, mtapoteza hela zenu bure". Ile kauli ikamchanganya Mama, ikabidi atake kujua sababu ya Kisauti kusema vile. Kisauti akamjibu "Sikutishi Mama angu, ila kama mna mashamba nyie uzeni tu, maana akiba mliyonayo haitotosha". Na kile kisauti chake, anazidi tu kumpanikisha Bi Mkubwa. Mwisho wa siku akamwambia "Nyie muulizeni mwenyewe anajua vizuri alichofanya, ila nawashauri msijisumbue nae". Akakata simu. Jamaa maneno anayoongea, na kile kisauti chake lazima ukereke.
Kipindi hayo mazungumzo yanaendelea, simu ilikuwa loudspeaker. Baba, Mama na Mimi wote tulikuwa tunayasikia yale mazungumzo, japo ni Mama pekee ndio alikuwa anaongea nae.
Simu ilipokatwa, wote wakawa wamenikodolea macho. Mama akaniuliza "Umefanya nn tena safari hii mwanangu? Mbona wewe huishiwi hizi sekeseke lakini?". Baba akanifyonya, alafu akasema "Mimi sio mtabiri, ila hapa lazima mwanamke anahusika, Yani kama hajatembea na mke wa mtu huyu, sijui"
Nikabaki kimya, namuwaza Kisauti na Mzee Dingi....