SEHEMU YA 40
Brenda Brebre aliyetegemea kuwa Tembo atamsindikiza na kumwacha barabarani alishangaa safari inaenda hadi Mlimani City. Tembo akaegesha gari lake.
“Kumbe na wewe ulikuwa unakuja huku?.” Brebre alimuuliza Tembo. Tembo akaachia tabasamu kabla ya kujibu, “Hapana nimefanya hivi kwa sababu yako Bre. Naamini hakuna kinachoharibika”
Brenda akajisikia ufahari mkubwa sana kufikishwa pale Mlimani city na gari binafsi. Alijua lazima watu watamkodolea jicho. Ni kweli magari yapo mengi Mlimani city na ya kifahari lakini wapo wanaokuja kwa miguu, pikipiki ama bajaji, hawa ndio Brenda aliwafikiria jinsi watakavyomshangaa.
Na alipenda sana kutazamwa na watu… kimoyomoyo akajipongeza kwa kuvaa nguo nzuri na kupendeza.
Tembo alikuwa makini katika mahesabu yake. Kile kitendo cha kujibiwa majibu ya ajabuajabu na Mamamia kilikuwa kinamsumbua kichwa hakutaka kuzichanga karata zake vibaya kwa Brenda. Huku akaamua kuwa mtulivu na kwenda kwa hatua za kunyatia. Huku kichwani akiamini kuwa simba mwenda pole…….
Bado kile kithembe cha Brenda kilikuwa kinampa mshawasha.
Wakaingia ndani. Kwanza wakaanza kung’arisha macho wakitazama wapi pa kuanzia. Tembo akawa mtulivu akimtazama Brenda.
Brenda akaanza kuelekea mashariki, Tembo akafuata. Mara wakaingia katika mlango mmoja, humo ndani wakakutana na Vitabu mbalimbali, Brenda akawa anavitazama bei bila kuulizia.
Tembo akamshtukia kuwa alikuwa akiogopa zile bei.
Kosa kubwa sana kumwonyesha Munyama Mukubwa kama Tembo udhaifu wako ilihali ana pesa ambazo anaamini kuwa ni kamba ya kuvutia vitamu vingi vya duniani!!
“Unapenda sana kusoma vitabu eeh!!.”
“Yaani sana, napenda novels na kuwatch movies.” Brenda akatupia kiswanglish matata.
“Tena kama riwaya za huyu nani hu…Hadley Chase, dah!” alizidi kutiririka.
Tembo akatumia muda kidogo akaziona hizo riwaya alizozitamani Brenda.
Elfu kumi na nane kitu gani kwa Tembo mwenye ajira bab kubwa isiyotoa jasho sana. Tembo akachomoa kitabu akalipia.
Wakatoka hapo. Sasa wakaifikia Supermarket. Mara Brenda aseme natamani marashi yale, Tembo analipia, mara ile poda, Tembo analipia. Kama mchezo wa kuigiza vile.
He!! Hiyo thabuni jamani!!!! Tembo analipia usiwe na wasiwasi.
“Huo mthwaki umenivutia jamani..”… Tembo atalipa!!
“Hathani angalia ile thimu. Mh!! Kuna thimu kali jamani.” Alijisemesha Brenda. Tembo akagundua kuwa anatakiwa kununua.
Kosa kubwa sana!!!
“Unaipenda eeh!!” Tembo akamuuliza.
Brenda hakujibu. Akajidai hakusikia. Tembo hakuuliza tena.
Kila alichokitaka Brenda sasa alikuwa amenunuliwa.
Wakatoka nje!! Haoo Garini.
Safari ya kumrudisha Brenda nyumbani.