213
Maofisa hao wa JWTZ walikamatwa na kufunguliwa kesi ya uhaini iliyosikilizwa mwaka 1985.
Kama hiyo haitoshi, mnamo Aprili 12, 1984, Idara ya Usalama wa Taifa ilipata pigo kubwa baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine kufariki dunia katika ajari ya gari iliyotokea eneo la Wami - Dakawa, nje kidogo ya Mji wa Morogoro baada ya gari aina ya Land Cruiser lililokuwa linaendeshwa na Dumisan Dube, mkimbizi wa kutoka Afrika ya Kusini aliyekuwa akiishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Mazimbu kugongana uso kwa uso na gari la Waziri Mkuu.
Msafara wa Waziri Mkuu uliokuwa ukilindwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ulipata ajali hiyo ukitokea Dodoma alikokuwa amekwenda kuhudhuria kikao cha Bunge. Kifo hicho kilizua mtafaruku mkubwa miongoni mwa wananchi na hasusan wanasiasa ambao waliituhumu Idara ya Usalama wa Taifa kwa kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kupanga mauaji hayo, kwa lengo la kuteka nafasi ya urais iliyoonekana kumwangukia Edward Sokoine.
Wapo pia waliowatuhumu baadhi viongozi wa juu hususan waliokuwa mawaziri wakuu wastaafu kuwa walitumia nguvu za giza kumuua kiongozi huyo. Lakini pia wapo waliovumisha kuwa mauaji hayo yalipangwa na kiongozi mkuu mwenyewe baada ya kuona Edward Sokoine angeipeleka nchi pabaya.
Hata hivyo, kadri muda ulivyokwenda tuhuma hizo zilipuuzwa na kuthibitika kuwa zilikuwa uzushi usiokuwa na ushahidi, huku Idara ya Usalama wa Taifa ikifanya kazi kubwa ya kujisafisha na kuzuia kifo hicho kisisababishe machafuko nchini.
Katika miaka ya 1983 hadi 1995, Idara ya Usalama wa Taifa ilifanya kazi chini ya Meja Jenerali Imran Kombe na kupata mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano kutoka kwa wananchi.
Idara iliwatumia vyema vijana waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria, na wazee waliopitia mafunzo ya mgambo katika kukusanya na kutoa taarifa kwa hiari (
informers), na wakati mwingine bila wao kujua. Kimsingi mawazo, misingi na itikadi za ujamaa na kujitegemea vilikuwa vikiwasukuma Watanzania wengi kujivunia utaifa wao, na kuonesha uzalendo kwa kujitolea kulitumikia taifa kwa hali na mali.
Hali ilianza kubadilika baada ya Mzee Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani alifanya kazi kubwa ya kubadilisha mfumo wa siasa na uchumi kutoka ujamaa asilia na kwenda kwenye mfumo wa biashara huria, kupitia Azimio la Zanzibar (ruksa).
Sasa Tanzania ikafungua mipaka yake, wafanyabiashara wakaruhusiwa kuingiza bidhaa za nje nchini na kuuza bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa chini ya usimamizi wa
Board of External Trade (BET). Uamuzi huu ulisaidia sana kupunguza ugumu wa maisha ya Watanzania uliotokana na kukosekana kwa bidhaa muhimu.
Mwaka 1989 Idara ya Usalama wa Taifa ikakumbwa na jinamizi lingine baada ya magaidi wa
The Mozambican National Resistance (MNR) wa Msumbiji kuvamia maeneo ya Kusini mwa Tanzania. Magaidi hao ambao pia hujulikana kwa jina la
RENAMO (
Resistência Nacional Moçambicana) au
BANDITO walianza kukipinga chama tawala cha Msumbiji, FRELIMO, miaka ya 1970 kabla hata nchi hiyo haijapata uhuru.
Magaidi hao walipata nguvu zaidi mwaka 1975 baada ya kuungwa mkono na idara ya ujasusi ya makaburu wa Rhodesia (sasa Zimbabwe) iliyojulikana kwa jina la
Rhodesian Central Intelligence Organization (
CIO) ambayo ilikuwa na lengo la kutokomeza ukomunisti Afrika.
Rhodesian Central Intelligence Organization ilifanya kazi zake kwa maelekezo na kwa kushirikiana na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) lililokuwa likitekeleza sera za kudhibiti kuenea kwa ukomunisti.
Hivyo, uvamizi wa RENAMO ndani ya ardhi ya Tanzania hakikuwa kitu kilichotarajiwa. Kwa muda mrefu magaidi hawa walikuwa wakipigana na majeshi ya FRELIMO ndani ya nchi ya Msumbiji bila kusababisha madhara kwa Watanzania. Mambo yaligeuka baada ya magaidi hao kupokea kipigo kikubwa kutoka kwa majeshi ya Serikali ya Msumbiji, na kukosa sehemu ya kukimbilia ndani ya nchi yao.
Ndipo walipovuka mpaka na kuingia Tanzania wakiwa na uhakika kuwa majeshi ya Msumbiji hayawezi kufanya vita ndani ya nchi nyingine. Wakiwa ndani ya ardhi ya Tanzania, magaidi wa RENAMO walijikuta wakiishiwa chakula, dawa, sigara, na vitu vingine muhimu walivyokuwa wakihitaji kuweza kuishi, ndipo walipoamua kuvamia vijiji vya mipakani na kupora chakula, dawa hospitalini, mavazi ya kiraia, na kisha kubaka wanawake kabla ya kurudi msituni kujificha.
Hali hii ilisababisha taharuki kwa wananchi wa maeneo hayo. Wengi wao waliamua kukimbia makazi yao na wengine kukubali kuishi na baadhi ya magaidi hao waliojivika kofia ya ufanyabiashara au uvuvi.
Ili kudhibiti hali hiyo Idara ya Usalama wa Taifa ilifanya kazi kubwa na kwa ushirikiano wa karibu na Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika operesheni iliyofanywa sambamba na nyingine (Operesheni Uhai) ikihusisha makomando wa Idara ya Usalama wa Taifa na makomando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania toka 92KJ Ngerengere.
Baada ya kazi ngumu iliyodumu kwa zaidi ya miezi tisa makomando hao walifanikiwa kuwatokomeza kabisa magaidi wa RENAMO na kurejesha amani katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.
Baadaye Idara ya Usalama wa Taifa ilijikuta ikiwa katika ‘sintofahamu’ baada ya kufumuka kwa mageuzi makubwa ya kisiasa na kiuchumi duniani. Mageuzi haya yaliyochochewa na
‘perestroika’ yalisababisha kuvunjwa kwa ukuta wa Berlin (mwaka 1989), kusambaratika kwa dola ya Urusi (
United Soviet Socialist Republic – USSR) mwaka 1991, na kumalizika kwa vita baridi kati ya Ulaya Magharibi na Ulaya Mashariki.
Pamoja na kutotajwa sana katika historia ya Tanzania, mageuzi haya kiuhalisia ndiyo yaliyochangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya jumla ya mfumo wa siasa na uchumi wa Tanzania, ikiwa pamoja na mfumo, muundo na utendaji wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Miaka mingi kabla ya mageuzi, Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa inafanya kazi katika mlengo wa kijamaa, kwa kufuata mfumo wa siasa wa chama kimoja, chini ya mwamvuli wa Ofisi ya Rais. Baada ya mageuzi Idara ya Usalama wa Taifa ilijikuta ikilazimika kubadilisha mfumo na malengo yake ili kwenda sambamba na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi, na kutengeneza muundo wa kuiwezesha kufanya kazi zake kwa kujitegemea.
Miezi michache baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, Idara ya Usalama wa Taifa ilipeleka mapendekezo ya marekebisho ya mfumo na muundo wa Idara kwa Rais Ali Hassan Mwinyi. Hata hivyo mapendekezo hayo yalikataliwa.
Mwaka 1995 Rais Benjamin Mkapa alimteua Cornel Apson Mwang’onda kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa badala ya Meja Jenerali Imran Kombe aliyestaafu. Cornel Apson Mwang’onda alitumia nafasi ya ukaribu wake na Rais Mkapa kupendekeza kwa mara ya pili mabadiliko ya mfumo na muundo wa Idara ya Usalama wa Taifa. Rais Mkapa aliridhia mapendekezo hayo na kuagiza uandaliwe muswada ili uweze kupelekwa bungeni.
Miezi michache baadaye muswada wa Sheria ya Usalama wa Taifa (
Tanzania Intelligence and Security Service Act No. 15 of 1996) ulipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusainiwa na Rais Benjamin Mkapa mnamo Januari 20, 1997.
Kupitishwa kwa sheria hiyo ndiko kunatajwa kuwa mojawapo ya mafanikio makubwa ya Cornel Apson Mwang’onda, ambaye wakati wa uongozi wake Idara ya Usalama wa Taifa ilikumbwa na misukosuko mingi, ikiwa pamoja na kulipuliwa kwa ubalozi wa Marekani.
Kuanzia Agosti 20, 2006 hadi Agosti 19, 2016, Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa chini ya Othman Rashid (OR) kama mkurugenzi wake mkuu baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuchukua nafasi iliyoachwa na Cornel Apson Mwang’onda. Kabla ya uteuzi huo Othman Rashid alikuwa Mkuu wa Utawala na Utumishi wa Idara hiyo ya Usalama wa Taifa (
Director of Administration and Personnel – DAP) baada ya kufanya kazi nzuri iliyomwezesha kuteuliwa kushika nafasi hiyo.
Katika kipindi hiki yalianza kujitokeza malalamiko kutoka kwa wabunge kuwa Idara ilishindwa kuzuia uhujumu uchumi na badala yake ikaanza kujikita kwenye siasa za kukipendelea chama tawala.
Ni kipindi hiki kulijitokeza matukio kadhaa ya ufisadi wa kutisha ikiwemo wizi wa zaidi ya Shilingi bilioni 133 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ununuzi wa rada ya kijeshi na ufisadi uliodaiwa kufanywa katika kampuni za Meremeta, Tangold na Deep Green Finance. Na bila kusahau ufisadi wa Tegeta Escrow.
Pia nchi ilishuhudia kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya, ujangili, rushwa na hata uvujaji wa siri za serikali. Mwaka 2013 Othman Rashid alikuwa astaafu kwa mujibu wa sheria lakini aliongezewa mkataba wa mwaka mmoja na kisha nafasi yake ikakaimiwa na Mkurugenzi wa Operesheni za Ndani wa Usalama wa Taifa (
Director Of Internal operations - DOI), George Madafa.
Kati ya Novemba 24, 2016 hadi Septemba 2019 Idara ya Usalama wa Taifa iliongozwa na Dk. Modestus Kipilimba, mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano aliyeteuliwa na Rais John Pombe Magufuli kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Othman Rashid.
Katika kipindi chake Idara ya Usalama wa Taifa iliendelea kushutumiwa na vyama vya upinzani kuwa ilikuwa ikikipendelea chama tawala, na kwa mara ya kwanza, liliibuka lindi la uhalifu wa kutisha uliofanywa na kundi la watu waliopewa jina la “wasiojulikana” ambapo watu kadhaa walipotea katika mazingira ya kutatanisha huku maiti zikiokotwa kwenye viroba kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi.
Pia ziliibuka tuhuma kuhusu mfumo wa ajira kwamba zilitolewa kwa upendeleo kwa ndugu na jamaa wa vigogo na kusababisha kuathiri sana ufanisi wa kazi huku baadhi ya maofisa usalama “wakijiumbua” kwa makusudi kwa kutaka sifa ili waogopwe mtaani. Na hapa ndiyo ile kauli ya “Unanijua mimi nani?” ilipokuwa maarufu mtaani.
Ni katika kipindi hiki pia nchi ilishuhudia kushamiri kwa matukio ya mauaji ambayo wengine waliyahusisha na ugaidi huko Mkuranga, Kibiti na Rufiji katika Mkoa wa Pwani, ambapo watu 40 wakiwemo askari polisi 15 waliripotiwa kuuawa kwenye kadhia hiyo.
Hata hivyo Idara ilifanya kazi kubwa sana na kubaini kuwa waliokuwa wakifanya mauaji hayo walikuwa wameingia kwenye maeneo hayo miaka nane kabla ya kuanza mauaji hayo, wakijipenyeza kwa njia ya kuendesha mafunzo ya dini kumbe walikuwa na mambo tofauti; wakifundisha
karate,
judo na namna ya kutumia silaha.
Kwa kushirikia na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kama Polisi na JWTZ, Idara ya Usalama wa Taifa ilipata mafanikio makubwa baada ya operesheni iliyofanywa maeneo husika kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa kadhaa wa mauaji hayo na wengine kukimbilia nchi jirani ya Msumbiji.
Halafu, Septemba 12, 2019 kulitokea mabadiliko ya uteuzi wa mkurugenzi mpya wa Idara ya Usalama wa Taifa na nafasi kuchukuliwa na Diwani Athuman Msuya. Ni katika kipindi hiki Idara ya Usalama wa Taifa ilipata pigo jingine kubwa kitaifa baada ya kifo cha Rais John Magufuli aliyekufa akiwa madarakani mnamo Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena. Kifo cha Rais Magufuli kilisababisha Idara ya Usalama wa Taifa kulaumiwa kwamba ilikuwa inaficha taarifa za afya ya Rais…
Dah! Nilijikuta kichwa changu kikianza kuwa Kizito, mambo yalikuwa mengi sana na ndiyo kwanza nilikuwa nimesoma utangulizi tu wa Idara. Bado kulikuwa na mambo mengi mno ya kusisimua na hata kuogofya kuhusu mazingira ya ufanyaji kazi kwa wausalama na mengineyo.
Kufika hapo nilijikuta nikishindwa kuendelea kusoma kwani nilihisi akili yangu ikishindwa kufanya kazi sawa sawa, nikaamua kuachana kwanza na kitabu hicho na sasa mawazo yangu yakahamia kwenye mambo mengine huku hisia fulani zikinijia, hisia zilizonifanya kuanza kujenga picha fulani kichwani kwangu, picha ambayo nisingeweza kuielezea vizuri kutokana na mshawasha niliokuwa nao…
Hata hivyo, nilikuwa na matumaini makubwa juu ya kile kilichokuwa kikinisubiri mbele ya safari.
* * *
Inaendelea...