325
“Pia inasemwa kuwa, mfanyabiashara huyo ambaye kwa sasa ametengana na mkewe aliijenga nyumba hii kwa siri sana kiasi kwamba hata mkewe Ummi Mrutu hakufahamu kama mumewe alimiliki nyumba hii, na aliitumia kwa mambo binafsi ya siri sana! Kwa nini hakutaka mkewe ajue? Hakuna aliye na majibu…”
“Siri ndani ya nyumba ya Rashid Mrutu! Hapa kuna kitu, naomba mniamini… hii code imefungua kila kitu kuhusu upelelezi wetu juu ya kifo cha mama Ummi Mrutu!” nilisema kwa kujiamini. Kisha nikaongeza, “Hata hili suala la wanausalama kuniwinda kila mahali ili waniue ni kwa kuwa wana hofu ninaweza kunusa taarifa hizi, kwani wanashirikiana kwa karibu sana na mtandano huu hatari na ushahidi tayari tunao kuwa wanalipwa mamilioni ya fedha kuvujisha siri za serikali na za kiusalama kwa mtandao huu.”
“Unadhani huyu mfanyabiashara Rashid Mrutu anaweza kuwa ndiye aliyeidhinisha mamilioni ya fedha kwa wanausalama kupitia akaunti ya Kangaroo Group?” mkurugenzi mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa aliniuliza huku akinikazia macho.
“Sidhani, nina uhakika! Kwa mujibu wa taarifa tulizozipata kule Alpha Commercial Bank, fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ya Kangaroo Group zimetokea kwenye benki mama iliyopo nchini Afrika Kusini, na sasa tunaambiwa kuna siri ya hatari ndani ya nyumba ya Rashid Mrutu ambaye baada ya kutofautiana na mkewe akahamishia makazi yake nchini Afrika Kusini! Hamuoni kama hapa kuna uhusiano fulani kati ya mambo haya?” nilisema kwa kujiamini kisha nikaongeza.
“Waziri Ummi Mrutu aliaminika kuwa mtu mwadilifu sana asiyeweza kumvumilia mtu yeyote asiye mwadilifu, na zipo taarifa kuwa mumewe alikuwa na makando kando kibao akiwa pia mmoja wa ma-
tycoon wakubwa wa mihadarati duniani ndiyo maana wakatengana. Upo uwezekano kuwa waziri alikuwa anatishia mustakabali wa biashara zake ndiyo sababu akaamua kummaliza.”
Maneno yangu yaliwafanya watu wote mle ofisini kwa mkurugenzi mkuu wanitazame kwa mshangao mkubwa. Kwa namna fulani walistaajabia wepesi wa akili yangu katika kuhusisha mambo. Niliamini kabisa kuwa hayo ndiyo yalikuwa majibu ya fumbo lile gumu lililotushinda kulifumbua.
Na hapo Pamela akasema, na kwa mara ya kwanza tangu kulipokucha, alinitazama usoni, “Kwa maana hiyo, mwandishi wa ujumbe huu alikusudia kukufikishia taarifa za kukutaka uende Mbezi Beach kwenye nyumba nambari 70 iliyopo kwenye bikoni nambari 2603 ambayo ni mali ya Rashid Mrutu… huko kuna siri kubwa ambayo huenda ndiyo imesababisha kifo cha waziri, hili ni jambo moja… na la pili kuna hatari ofisini, hatujui ni ipi na katika ofisi ipi, yako binafsi au Idarani kwenye Taasisi za SPACE!”
Sasa kila kitu kilianza kuwa wazi, ulikuwa ni ukweli mchungu kuwa baadhi ya wanausalama wenzetu walikuwa mawakala wa mtandao huu hatari na walikuwa wakilipwa fedha nyingi.
Hata hivyo tulijikuta tukiwa na maswali lukuki; Ni nani aliyeuleta ule ujumbe nyumbani kwangu? Na ilikuwaje baadaye usiku akaonekana akiwa na Daniella ambaye tuliamini alikuwa mmoja wa wanausalama waliopo kwenye mtandao huu hatari, na ushahidi ulijionesha pale alipofanya jaribio la kutaka kutuua kwa bomu lililotegwa kwenye gari letu?
Nilipoanza kujiuliza ni nani ambaye angeweza kuwa ameuleta ule ujumbe nyumbani kwangu mara nikamkumbuka Sajenti Mambo. Nikakumbuka jinsi alivyotuokoa na kifo cha bomu lililotegwa kwenye gari kule benki. Na hapo ile picha ya mtu niliyemwona nyumbani kwangu usiku akiwa amevaa koti refu na kofia pana ya pama iliyoficha uso wake akiwa na Daniella kisha wakaondoka na gari aina ya Lexus ikajifunua. Sasa nilikuwa na uhakika kuwa mtu huyo alikuwa Sajenti Mambo!
Nikaamua kuwashirikisha maofisa wenzangu kuhusu hisia zangu, na wote tukakubaliana kumtafuta Sajenti Mambo ili tupate majibu ya maswali yetu, kwani ilionesha Sajenti Mambo aliyafahamu mengi kuhusiana na tukio lile la kigaidi.
“Kumbukeni kuwa Sajenti Mambo ni mmoja wa maofisa waliopo kwenye
payroll list ya kulipwa mamilioni ya fedha toka akaunti ya Kangaroo, lakini mimi kwa sasa simwangalii kama mshukiwa bali kama shahidi anayeweza kutupatia majibu ya maswali yetu na mwanga zaidi kuhusiana na kazi hii,” nilisema na kushusha pumzi. Kabla sijaendelea Luteni Lister akaingilia.
“Nakubaliana na wewe, Jason. Tukimpata Sajenti Mambo tutakuwa tumepata mwanga wa nini kinaendelea. Nadhani tusipoteze muda zaidi, inatakiwa tuingie kazini sasa kumtafuta Sajenti Mambo kwa kutumia vyanzo vyote vya taarifa… tumpate kabla ya jioni ya leo,” Luteni Lister alisisitiza.
Mkurugenzi mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa alibetua kichwa chake kuafiki kisha akanyanyua kikonyo cha simu iliyokuwa mezani pake na kupiga namba fulani halafu akaiweka sikioni. “Victor, nakuhitaji haraka ofisini kwangu,” alisema na kukata simu kisha akairudisha mahala pake.
“Msemayo vijana nakubaliana nayo
a hundred percent, Sajenti Mambo ni mtu muhimu sana kwenye kesi hii,” mkurugenzi mkuu wa Idara aliunga mkono hoja. “Lakini pia tunatakiwa kwenda mbele zaidi ili kubaini hii akaunti ya Kangaroo inamilikiwa na nani, na nani aliyezituma fedha zote hizi toka huko Afrika Kusini.”
Nilitaka kusema neno lakini kabla sijasema lolote mlango wa ofisi ya mkurugenzi mkuu ukagongwa mara moja na kufunguliwa, wote tukageuka kutazama mlangoni na kumwona ofisa mmoja, mwanamume mwenye umri wa takriban miaka arobaini akaingia ndani. mara moja nikatambua kuwa huyo ndiye Victor.
Victor alitusalimia kisha akasimama mbele ya mkurugenzi mkuu wa Idara kwa unyenyekevu mkubwa.
“Victor, fanya kila unaloweza nipate taarifa za akaunti hii ya Kangaroo iliyopo Afrika Kusini kabla ya jioni ya leo,” mkurugenzi mkuu wa Idara alimwamuru Victor akimwonesha karatasi ya taarifa za fedha za akaunti ya Kangaroo. “Nataka kujua kampuni hii imeanzishwa lini na wapi, nani hasa mwenye kampuni hii, na kila unachoweza kupata. Tumia njia zote unazoweza kupata taarifa. Sawa?”
“Sawa, mkuu,” Victor alijibu kwa unyenyekevu huku akiipokea ile karatasi na kuitazama mara moja tu kisha akayarudisha macho yake kwa mkurugenzi mkuu wa Idara. Kisha akapiga saluti na kuondoka.
Muda huo huo simu yangu ilianza kuita, nikaitazama na kuona namba ngeni. Bila kusita nikaipokea na kuiweka sikioni. “Hallo!”
“Jason!” sauti ya kiume upande wa pili wa simu iliita kwa wasiwasi.
“Ndiyo. Nani mwenzangu?” niliuliza kwa sauti tulivu huku nikikunja sura yangu.
“Albert Mambo hapa…” yule mtu upande wa pili wa simu alisema na kunifanya nishtuke kidogo kwani sikutegemea kumpata Sajenti Mambo kirahisi hivyo.
“Sajenti Mambo?” niliuliza kwa mashaka kidogo katika kutaka kupata uhakika. Watu wote mle ofisini kwa mkurugenzi mkuu wa Idara waliposikia nikilitaja jina la Sajenti Mambo wakawa na shauku ya kutaka kusikiliza. Nikaweka sauti kubwa (
loud speaker) ili kila mmmoja aupate ujumbe moja kwa moja.
“Ndiyo, ndugu yangu. Kama hutojali naomba tukutane jioni ya leo kwa maongezi maana mambo hayako sawa kabisa katika nchi hii. Kama mimi na wewe hatutaweza kuwa wazalendo na nchi yetu tusitegemee mtu toka nje aje aipende nchi hii,” Sajenti Mambo alisema kwa huzuni na kushusha pumzi.
“Tutaonana vipi sasa?” niliuliza kwa shauku.
“Nitakujulisha baadaye wapi na muda gani tuonane, ila naomba iwe siri sana na uje peke yako maana kuna usaliti mwingi sana sasa hivi kwenye vyombo vyetu vya ulinzi na usalama,” Sajenti Mambo alisema.
“Kwa hiyo… ni wewe uliyeuleta ule ujumbe nyumbani kwangu?” nilimuuliza kwa shauku.
“Ndiyo. Naamini umeuelewa na kuufanyia kazi!” Sajenti Mambo alisema.
“Nimeuelewa ila bado kuna mambo yananitatiza kidogo…” nilisema.
“Usijali, tutaongea baadaye, nitakujulisha kila kitu. Kwa kifupi hali si shwari kabisa, kuna mambo makubwa yanaendelea chini ya zulia,” Sajenti Mambo alisema na kukata simu. Sauti yake ilionesha wasiwasi mkubwa.
Dah! Baada ya simu kukatwa ukimya ukatawala kwa muda ndani ya ile ofisi kisha mkurugenzi mkuu akavunja ukimya, “Kwa sasa Mambo ndiye ‘sosi’ wetu mkubwa, naomba tusiipoteze nafasi hii. Namfahamu vizuri, ni mzuri sana kwenye kuchambua taarifa na upembuzi wake wa mambo ni wa kiwango cha juu.”
Tulibaki kimya tukijaribu kutafakari. Mkurugenzi mkuu akaongea jambo ambalo siku zote nilikuwa na shaka nalo, “Labda niwamegee siri, Mambo ni mmoja kati ya maofisa wa Usalama wa Taifa waliopenyezwa kwenye Jeshi la Polisi, hivyo mtaona ni kwa namna gani anaweza kuwa mtu muhimu kwetu.”
* * *
Endelea kufuatilia...