Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #101
79
Kabla sijajua nifanye nini mara nikasikia milio mingine kadhaa ya risasi ikirindima kama radi kuelekea kule tulikokuwa na hapo nikashuhudia kile kioo cha mbele cha gari letu kikitawanywa na kusambaa huku vipande vidogo vidogo mfano wa chenga chenga vikitumwagikia mwilini na kuendelea kuzua hali ya taharuki.
Kwa nukta chache nilihisi kama vile moyo wangu ulisahau mapigo yake, nilichoweza kusikia muda ule ilikuwa ni yowe dogo la hofu kutoka kwa yule dereva wa gari letu kisha nikamwona akiangukia kwa mbele kwenye usukani wa lile gari na kutulia kimya huku kifo kikiwa tayari kimemchukua. Waswahili wangeweza kusema kuwa “wala hakuomba maji”.
Muda ule ule abiria wenzangu ndani ya lile gari walianza kupiga mayowe ya hofu, hata hivyo ule haukuwa muda wa kushauriana kwani nilijua fika ni nini ambacho kingefuatia baada ya pale. Niliweza kushuhudia zile risasi zilizorindima zikiwa zimekifumua kichwa cha yule dereva wa gari letu na kutoboa bodi la lile gari.
Risasi nyingine zilikuwa zimeacha matundu mawili yakivuja damu katika sehemu ya kifua cha abiria mtu wa makamo aliyekuwa ameketi siti ya mbele upande wa kushoto kwa dereva na nyingine ilipita hadi kwa abiria mwingine aliyekuwa ameketi nyuma ya yule abiria wa mbele katika ile siti ya katikati.
Kwa kweli sikuwahi kuingia na hofu kubwa maishani mwangu kama hofu iliyonipata siku ile, hata hivyo, katikati ya hofu ile sikuona namna nyingine yoyote ya kujiokoa haraka katika mkasa ule, hivyo nilichokifanya ilikuwa ni kuvuta haraka kabali ya ule mlango wa nyuma ambako tulikuwa tumeketi.
Niliivuta ile kabali ya mlango na kuinyonga huku nikijaribu kuusukuma ule mlango kwa nguvu, lakini haukufunguka kwa kuwa ulikuwa umepinda kidogo na kubonyea kwa ndani kutokana na gari lile kugonga ule mti mkubwa, hivyo nikaamua kuufungua kwa teke moja la nguvu.
Ule mlango ulisalimu amri na kufunguka, lakini kabla sijashuka kutoka ndani ya lile gari nikajiwa na wazo la kumwokoa yule mrembo ambaye muda ule alionekana kama aliyekuwa amepigwa bumbuwazi na presha ilikuwa imepanda na hivyo kumfanya asijue la kufanya.
Sikuona sababu ya kujiokoa mwenyewe huku nikimwacha yule mrembo auawe kinyama katika mazingira ambayo nilidhani ninawajibika kufanya hivyo. Bila kuchelewa nikamshika mkono na kumsukumia nje ili ashuke, lakini alionekana kuendelea kushangaa.
Nilipotupa macho yangu kule barabarani muda ule nikawaona majambazi wawili kati ya wale watatu waliokuwa wameruka kutoka ndani ya lile Land Cruiser Pick-up wakikimbilia kuja kule tulikokuwa huku wakiwa wameshika vyema bunduki zao mikononi. Sikutaka kuendelea kushangaa, nikamnyanyua yule msichana mrembo kutoka kwenye siti yake kisha nikaruka naye nje ya lile gari na kutua chini kwa miguu yangu kama paka.
Kutokana na kiza kilichokuwa kimetanda katika eneo lile nilishindwa kuona vizuri sehemu niliyorukia na kujikuta nikitua kwenye bonde dogo na hivyo mguu wangu wa kushoto ukashtuka na hapo nikasikia maumivu makali sana kwenye kifundo cha mguu wangu wa kushoto yaliyopanda hadi juu ya goti.
Hata hivyo, sikujali yale maumivu makali ya mguu wangu niliyoyahisi, nilimbeba juu juu yule msichana mrembo na kujitahidi kuondoka haraka kutoka eneo lile huku nikikimbilia kichakani. Sikuweza kufika mbali kwani nilihisi kama mguu wangu ukipinda kidogo, kisha nikaanguka huku nikiwa bado nimembeba yule msichana mrembo. Hata hivyo, kwa namna ya ajabu nilijikuta nikimwinua juu yule mrembo huku nikijipinda na kulalia mgongo huku yule mrembo akiangukia juu ya kifua changu.
Kitendo kile cha kuanguka chini na yule mrembo kunilalia juu kikamzindua kutoka kwenye lile bumbuwazi, na hapo nikamwona akiangalia huku na kule kwa hofu kubwa na kutaka kupiga kelele. Niliwahi kumziba mdomo wake huku nikimsukuma haraka kumwondoa eneo lile.
“Kimbilia kichakani kabla hawajafika,” nilimnong’oneza sikioni yule mrembo huku nikimsukuma aondoke haraka eneo lile na kwenda kwenye kichaka kikubwa ambacho hakikuwa mbali kutoka pale chini tulipokuwa tumeangukia. Yule msichana alionekana kuganda juu yangu kama sanamu akiwa ameanza kuchanganyikiwa na hivyo kumfanya asijue lipi la kufanya na kwa wakati gani.
Muda ule abiria wengine walikuwa wametaharuki na kuanza kutimua mbio ovyo wakikimbilia barabarani huku wakipiga kelele ovyo kwa hofu. na hapo milio mingine kadhaa ya risasi ikavuma tena hewani, kufumba na kufumbua nikawaona watu watatu miongoni mwa wale abiria wakitupwa hewani na kupiga mayowe ya uchungu.
Wale watu walipoanguka chini walitulia kimya huku uhai ukiwa mbali na nafsi zao, kwani zile risasi zilizofyatuliwa zilikuwa zimepenya kwenye maeneo nyeti na kuacha matundu makubwa yaliyokuwa yanavuja damu.
Milio ile ya risasi ikamzindua tena yule msichana mrembo, nami nikazidi kumsisitiza kwa sauti yenye kusihi na kushawishi sana kuwa akimbilie kichakani kabla wale majambazi hawajafika pale na kutuona tukiwa katika hali ile. Maneno yangu yakamfanya anitazame kwa makini kama vile alikuwa amesikia habari mpya kabisa masikioni mwake.
Nikamsukuma kwa nguvu nikimtaka aondoke haraka eneo lile, safari hii aliinuka haraka pasipo upinzani wowote, nikamwona akitimua mbio huku akiwa ameinamisha mgongo wake kuelekea kwenye kichaka.
Nikiwa bado nimelala pale kwenye majani, nilimtazama yule msichana mrembo namna alivyokuwa akipotelea kwenye kile kichaka hadi alipotoweka kabisa machoni kwangu, nami nikaubana mguu wangu wa kushoto uliokuwa na maumivu makali na kuanza kutambaa kama nyoka, haraka nikapotelea gizani huku nikielekea kwenye kile kichaka.
Muda ule abiria wengine wanne waliobaki walisambaratika kwa hofu kila mmoja na njia yake wakikimbilia porini na hivyo kusalimisha roho zao. Nilifanikiwa kufika pale kwenye kichaka japo kwa taabu nikamkuta yule mrembo akiwa kajikunyata kwa hofu kubwa huku akilia kwa uchungu kilio cha kwikwi.
Sikuwa na shaka kabisa kuwa alikuwa amechanganyikiwa kutokana na hali ile ya taharuki aliyokuwa ameishuhudia na kuna wakati alitaka kupiga yowe la hofu lakini niliwahi kumziba mdomo wake baada ya kuhisi hatari ambayo ingetukabili pindi wale wauaji wangelisikia yowe lake.
Wale wauaji wawili waliisogelea ile gari yetu kwa tahadhari wakati yule jambazi wa tatu alikuwa amesimama kwa mbali kule barabarani akionekana kulinda eneo lile pamoja na kuwalinda wale wawili endapo hatari yoyote ingetokea.
Mara nikamwona mmoja kati ya wale wauaji wawili waliokuwa wamesimama kwenye lile gari akianza kusogea taratibu kuelekea pale kwenye kile kichaka tulipokuwa tumejificha mimi na yule msichana mrembo huku akielekeza mtutu wa bunduki yake pale kichakani.
Yule mrembo akaingiwa na kiwewe na kutaka kutoka ili akimbie lakini niliwahi kumdaka na kumzuia kwa mikono yangu yenye nguvu ili asikimbie, kisha nikamziba mdomo wake kwa nguvu ili asipige kelele. Ni wazi kabisa kuwa kwa muda ule alikuwa amechanganyikiwa na hakujua hatari ambayo ingempata endapo angejaribu kukimbia.
Wakati nikiwa nimemziba mdomo yule mrembo nikaamwona yule muuaji akizidi kusogea pale kwenye kichaka kwa kupitia uwazi wa matawi na majani katika kile kichaka, niliweza kumwona vizuri yule mtu wakati akitembea kwa tahadhari kusogea pale.
Kiza kilichokuwepo katika eneo lile hakikunizuia kumtambua yule muuaji kutokana na umbile lake na hata utembeaji wake, alikuwa ni yule jamaa aliyeshuka kwenye lile Land Cruiser Pick-up pale jirani na kituo cha kujazia mafuta cha Masumbwe na kuja kwenye gari letu kuulizia usafiri wa kwenda Kahama.
Nilimtazama kwa mshangao akiwa ameishika vyema bunduki yake huku misuli ya shingo na mikono yake ikiwa imetuna kwa ukomavu. Mwonekano wake ukanitanabaisha kuwa alikuwa ni mtu hatari sana na aliyependa matata.
Yule muuaji akaendelea kutembea kwa tahadhari akikikaribia kile kichaka na wakati huo yule mwenzake alikwenda moja kwa moja hadi kwenye siti ya mbele kushoto kwa dereva alipokuwa ameketi yule mzee wa makamo mwenye suti maridadi, nikamwona akiuchukua ule mkoba kutoka kwenye mikono ya yule marehemu.
Itaendelea...