Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

narudi buzwagi.jpeg

96

Bila ubishi nikainuka, tukakumbatiana na kuanza kucheza. Nilipomkumbatia tu nikahisi kama chaji za umeme zinapita mwilini mwangu pale kifua cha Jamila kilichobeba chuchu laini kilipogusana na kifua changu. Kadiri muziki ulivyokuwa ukienda ndivyo tulivyojikuta tukikumbatiana kwa nguvu zaidi. Muziki ulimalizika lakini bado tuliendelea kukumbatiana kwa nguvu.

Taratibu Jamila akaupeleka mkono wake wa kulia chini kidogo ya kiuno changu na kukutana na kitu kigumu kilichotuna. Taratibu na kwa ufundi akakishika kitu kile kilichotuna na kunifanya nianze kuhema kwa nguvu kisha nikampiga busu zito lililomfanya aweweseke.

Nikataka kulianzisha pale pale sebuleni lakini Jamila akanitaka tuelekee chumbani, na mara tu tulipoingia chumbani hatukuchelewa, kukawa na mpambano mkali wa mechi ya kukata na shoka huku safari hii nikiwa naipangua mitego ya Jamila aliyoniwekea kiasi kwamba katika mizunguko mitatu tuliyokwenda nilimwonea kupita maelezo na kwa kuwa nilikuwa ndiyo mchezeshaji mkubwa wa mechi Jamila alijikuta akimwagikwa na machozi, na sikujua kama yalikuwa ya furaha au karaha!

Kiukweli, pasipo kujali maumivu ya mguu wangu nilimpagawisha sana Jamila hadi ikafikia wakati alikuwa akizungumza maneno ambayo sikuweza kuyaelewa, na baadaye aliniomba apumzike kwani hali ilishakuwa mbaya. Na hadi kunakucha wote tulikuwa hoi. Hakuna aliyekuwa na hamu na mwenzake.

Ukimya mkali ulitawala kati yetu huku kila mmoja akiyasikilizia mapigo yake ya moyo yalivyokwenda. Jamila alijinyanyua taratibu na kulaza kichwa chake kiduani kwangu huku akinikumbatia, alikuwa analia kilio cha kwikwi, wasiwasi ukaanza kunivaa.

“Baby mbona unalia?” nilimuuliza kwa wasiwasi.

“Jason, nakupenda sana hadi nahisi kuchanganyikiwa, nahitaji uwe mume wangu halali wa ndoa,” Jamila alisema huku akijitahidi kuyazuia machozi yaliyozidi kumtoka.

“Hilo haliwezekani kwa sababu ya tofauti zetu za rangi na dini. Ndugu zako hawawezi kukubali uolewe na Mbantu kama mimi.”

“Nalijua hilo Jason, ila najua nitalimaliza vipi na lazima utanioa,” Jamila alisema na kunifanya niogope mno. Nilianza kujilaumu kukutana naye.

“Jamila!” niliita kwa wasiwasi.

“Mmh!”

“Kubali tu kuolewa na mume uliyetafutiwa na ndugu zako ili usije ukakosa radhi ya wazazi,” nilijaribu kumshawishi.

Jamila alikaa kimya kwa kitambo fulani akionekana kuzama kwenye lindi la mawazo, kisha akainua uso wake kuniangalia. Machozi yaliendelea kumtoka.

“Jason, naomba unisikilize, kuna kitu nataka nikwambie ila naomba usikasirike,” Jamila aliniambia kwa sauti ya kunong’ona.

“Niambie tu siwezi kukasirika,” nilisema huku mapigo ya moyo wangu yakienda mbio isivyo kawaida.

“Hutokasirika?” Jamila aliniuliza huku akiniangalia machoni.

“Ndiyo.”

“Nina mpango wa kutoroka kabla ya harusi, tafuta nchi nzuri twende tukaishi kama ni fedha ninazo za kutosha,” Jamila alisema huku akifuta machozi.

“Nadhani unajua kwetu tumezaliwa watatu, kaka yetu Selemani na sisi wa kike wawili. Dada yangu Salma kwa sasa yupo Uarabuni ameolewa. Kwa upande wa baba yangu wao walizaliwa wawili tu, yeye na kaka yake, baba yetu mkubwa…” Jamila alizungumza katika hali ya utulivu, muda huo alikuwa amenikumbatia huku akiendelea kulia.

“Baba mkubwa hakubahatika kupata mtoto na alikuwa na mali nyingi… alinipenda sana na kabla hajafariki aliacha wosia kuwa mimi ndiye mrithi wa mali hizo… kwa hiyo mimi ni tajiri ila kwa kweli siyafurahii maisha ya nyumbani kwetu, nimekuwa ni mtu wa kuchungwa chungwa kiasi kwamba ninakosa uhuru wa kufanya mambo yangu,” alisema huku akiendelea kutiririkwa na machozi.

“Basi usilie, baby,” nilimwambia kwa sauti tulivu, hata hivyo nilikuwa najilaumu kukutana na Jamila.

“Hapana Jason, ndugu zangu wananionea sana, hawanipi uhuru… na mbaya zaidi huyo mwanaume wanayetaka kuniozesha kiumri ni sawa na baba yangu.”

“Kwani ana umri gani?”

“Sijajua ila hata wewe ukimwona utashangaa! Kisa tu ni tajiri mkubwa na anamiliki visima vya mafuta!” Jamila alisema huku akizidi kunikumbatia na kulia.

“Jason!” Jamila aliniita kwa sauti ya kunong’ona.

“Mmh!”

“Naomba uniambie ukweli, unanipenda?” aliniuliza huku akiniangalia machoni.

“Kwa nini unaniuliza hivyo?”

“Nisikudanganye, mimi nina wivu sana na nipo tayari kupoteza fedha yangu ili kumkomesha yeyote atakayeingilia uhusiano wetu…”

“Kivipi? Si unajua kuwa nina mchumba na karibuni tutaoana?” nilimuuliza Jamila huku nikimtazama kwa umakini.

“Nitafanya kila linalowezekana umsahau…” Jamila alisema huku akiniangalia machoni na kuchia tabasamu.

“Usiniulize nitafanyaje kwani hiyo ni siri yangu ya moyo. Na ukiachana na Rehema, msichana mwingine yeyote atakayejitokeza atanitambua mimi ni nani? Naomba tu tusije tukalaumiana!”

Dah. mwili wote uliingiwa ganzi. Nilizidi kumwogopa Jamila. Nikatamani kumfukuza halafu nimwambie asije tena nyumbani kwangu. Wazo jingine likanijia kuwa akiondoka tu nihame pale na nikaishi kwenye nyumba nyingine au nimfuate Rehema huko wilayani Misungwi.

“Lakini Jamila, naomba usijaribu kufanya jambo lolote litakalomuumiza Rehema sitakuelewa kabisa,” nilimpa onyo huku nikiidhibiti hasira yangu. “Pia sidhani kama ndugu zako ni wajinga kukuchangulia mume, wanajua kuwa ndiye atakayekufaa…” nilijaribu kumsihi.

“Mambo ya kuchaguliana waume yamepitwa na wakati, nakuapia hakuna mwanaume atakayenioa ila wewe. Ikishindikana basi nitajua cha kufanya na sitataka kuolewa tena maishani mwangu. Wewe ndiyo mume wangu, wewe ndiyo mwanga wa maisha yangu.”

Maneno ya Jamila yalikuwa yamenitisha mno, kila nikimwangalia sikuona yakini kwenye macho yake. Asubuhi ile tulinyanyuka kiuvivuvivu tukaingia bafuni na kuoga, kisha nilibadilisha shuka na kutandika vizuri kitanda changu na wakati huo Jamila alikuwa anaandaa kifungua kinywa.

Ilikuwa siku mpya, siku ya Jumatatu na asubuhi ile tuliagana nikaenda kazini huku Jamila akielekea kwa shangazi yake kwa ajili ya safari ya Masumbwe.

Siku ile nilifanya kazi nikiwa na mawazo mengi na nusura mawazo hayo yaharibu ufanisi wangu wa kazi. Hatimaye nilipanga kubadili namba ya simu na kuihama ile nyumba niende nikajifiche Mwime kwenye nyumba niliyojenga ambayo hadi wakati huo haikuwa ikikaliwa na mtu.

Jioni ya siku ile baada ya kutoka kazini nilibadilisha namba ya simu na kuwajulisha watu wangu wachache akiwemo Rehema kisha nikapanga kwenda kwanza Nyasubi kumtafuta Asia kisha baadaye niangalie utaratibu wa kuhamisha vitu kupeleka Mwime. Nilishukia Chattle Restaurant kisha nikaanza kutembea taratibu nikiambaa ambaa kando kando ya barabara kuelekea eneo alilokuwa akiishi Asia. Mtaa ule haukuwa na msongamano mkubwa na hivvyo sikupata taabu wakati nikitembea.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

97

Nikiwa hatua zipatazo 100 kuifikia nyumba aliyoishi Asia nikawa navuka barabara pasipo kuangalia nyuma ili nipite upande wa pili wa barabara na mara nikashtushwa na sauti ya breki kali za gari nyuma yangu. Niliogopa sana nikajikunja na kuruka juu huku nikitua kando ya ile barabara nikiwa nimefumba macho yangu, kisha nikageuza shingo yangu kutazama nyuma yangu.

Nikaliona gari ndogo aina ya Toyota Mark X la rangi ya bluu bahari likiserereka na dereva akijitahidi kunikwepa, kisha lile gari likasimama kando mbele yangu.

Nilisimama huku nikihema kwa hofu nikamtazama yule dereva ambaye muda ule alikuwa akinitazama kwa hasira. Macho yangu yakatua kwenye uso wa yule dereva na mshtuko nilioupata ulikuwa hauelezeki. Dereva wa lile gari alikuwa ni Asia. Tuliangaliana kwa kitambo kifupi kila mmoja akiwa kimya, kisha nikamsogelea na kusimama usawa wa mlango wake.

“Asia!” niliita kwa mshangao huku nikimkazia macho yangu, lakini hofu ilikuwa bado inanitambaa mwilini mwangu kutokana na kukoswa koswa kugongwa.

Asia alishtuka sana na kunikazia macho kwa mshangao, hata hivyo, nikaachia tabasamu laini. “Nadhani sijakosea jina, wewe ni Asia…” nilisema tena huku nikiendelea kumtazama Asia kwa tabasamu pana.

Nikamwona Asia akishusha pumzi ndefu. “Ndiyo hukukosea… ni mimi…” alisema lakini akasita kidogo na kunikazia macho huku akinitazama kwa makini, “Lakini, ni nani amekwambia naitwa Asia?”

“Niliambiwa na yule kijana wa pale dukani siku ile ulipokataa ofa yangu ya soda,” nilisema huku nikiachia kicheko hafifu.

Asia aliguna kabla hajaachia tabasamu, “Ahsante kwa kuonekana kunijali, Mr Jason.”

“Na wewe ahsante kwa kulikumbuka jina langu!” nilisema huku moyoni nikifarijika sana baada ya kuona kumbe Asia alikuwa akilikumbuka jina langu.

“Hamna shaka, Mr Jason, na pole sana kwa kutaka kukusababishia ulemavu.”

“Usijali, yote ni mapenzi ya Mungu,” nilisema huku nikiendelea kutabasamu, nikavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku nikijikuna kidevu changu.

Asia aliniangalia kwa umakini kisha akataka kuondoka, lakini nikamzuia kwa ishara ya mkono. Akasita kuondoka lakini hakuzima gari lake, alinitazama kwa mshangao huku akionesha wasiwasi kidogo usoni kwake.

“Kuna nini tena, au bado unataka kuninunulia soda?” Asia alisema kwa utani huku akinikazia macho.

“Ni hivi… mimi na wewe tuna bahati ya kukutana katika maisha yetu, kwa nini basi tusiwe marafiki?” nilisema huku nikimtazama Asia kwa makini.

“Urafiki wa vipi unaoukusudia?” Asia aliniuliza akiwa amekunja uso wake, hakuacha kunitazama usoni kwa umakini.

“Unajua Asia … tangu siku ile ya kwanza tulipokutana Masumbwe nimeshindwa kabisa kukutoa akilini mwangu,” nilisema huku nikimkazia macho, nikamwona ameshtuka sana na kunitazama usoni kwa mshangao mkubwa.

“Lini mimi na wewe tumekutana Masumbwe?”

“Siku ya mgomo wa madereva kisha tukasafiri kwenye gari moja aina ya Prado tukiketi nyuma na baadaye yakatokea mauaji kule porini wakati mimi na wewe tukijificha kwenye kichaka…”

Oh my God!” Asia alishtuka sana na kuachia yowe kubwa la mshangao na mshtuko usioelezeka. Nilimwona akiinua mikono yake juu na kushika kichwa chake huku akinitazama kwa mshangao mkubwa kana kwamba alikuwa ameona kitu cha ajabu sana. Alikuwa anahema kwa nguvu.

“Hukumbuki? Ni mimi niliyekusaidia kujificha pale kwenye kichaka. Ni mimi niliyekulinda muda wote hadi pale Polisi walipokuja. Ni mimi niliye…” Asia alinikatisha akionekana kuchanganyikiwa.

Please, stop it!” alisema huku akihema kwa nguvu. Kisha kikapita kitambo fulani cha ukimya, alinitumbulia macho yake kwa mshangao. Nikaiona michirizi ya machozi mashavuni kwake japo alijaribu kuyazuia machozi lakini alishindwa, akabaki kimya akiniangalia bila kusema chochote.

Kisha alitoa leso yake laini na kufuta machozi huku akipenga kamasi zilizoanza kumtoka, akashusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani na kujiegemeza kwenye siti yake, akafumba macho. Hadi muda huo hakuweza kuongea neno lolote bali alikuwa anahema kwa nguvu kama aliyekuwa akipigania pumzi ya mwisho.

“Nashukuru sana kwa kunijali,” hatimaye Asia aliweza kusema baada ya kitambo fulani kisha akayafuta machozi.

Niliachia tabasamu na kuangalia kando. Asia alizidi kuniangalia kwa namna ambayo sikuijua tafsiri yake, alikuwa bado haamini macho yake. Kwa kitambo kirefu tuliangaliana pasipo kusema neno, kisha alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu. Hakuweza kusema tena neno lolote baali aliliondoa gari lake kwa mwendo wa kasi akiniacha nimepigwa butwaa.

Gari halikwenda mbali nikashuhudia akifunga breki kali kisha gari likarudi nyuma hadi pale niliposimama. Asia alipenga kamasi kwa kutumia kitambaa chake laini na kuniashiria niingie ndani ya lile gari. Sikujivunga, nilizunguka upande wa pili nikaufungua mlango wa mbele wa abiria na kuingia. Hiyo ilikuwa nafasi muhimu niliyokuwa naingoja siku zote.

Asia akaliondoa gari lake taratibu na hatukuweza kuongea chochote, alinitupia jicho mara mbili akiwa bado haamini. Kisha tulifika nyumbani kwao, kwenye nyumba kubwa na nzuri ya kifahari iliyozungukwa na miti mizuri ya kivuli. Ilikuwa imezungukwa na ukuta mrefu usiomwezesha mtu kuona ndani na ulifungwa mfumo maalumu wa umeme.

Hiyo ilikuwa ni moja ya majumba makubwa ya kisasa ya watu wakwasi katika eneo lile yaliyozungushiwa uzio na mageti makubwa yenye vifaa vyote vya usalama vya kuwahakikishia wakazi wake ulinzi na usalama wa hali ya juu.

Mbele ya lile geti kubwa jeusi Asia alipiga honi na mara mlango mdogo wa lile geti ulifunguliwa kidogo, nikamuona mdada mmoja ambaye kiumri alikuwa amemzidi Asia akichungulia na kuliona lile gari. Akaachia tabasamu na kulifunga lile geti dogo, kisha akalifungua lile geti kubwa. Asia akaliingiza lile gari ndani ya uzio wa ile nyumba na kuliegesha kwenye eneo maalumu la maegesho, jirani na gari jingine aina ya Toyota Hilux double cabin lililokuwa na rangi nyeupe.

Alitulia kidogo kisha akazima injini ya lile gari na kushuka huku akiniashiria nami nishuke. Nilishuka kisha Asia akaifunga vizuri milango ya lile gari kwa rimoti na kuniongoza ndani ya ile nyumba. Yule mdada aliyetufungulia geti alitusalimia kwa unyenyekevu mkubwa, nikamwitikia salamu yake, na hapo nikagundua kuwa alikuwa ni mdada wa kazi.

Wakati nikiongozana na Asia nilikuwa natupa macho yangu kuangalia huku na huko kuyatazama mandhari ya kupendeza ya ile nyumba. Ilikuwa ni nyumba kubwa ya kisasa ya ghorofa moja. Ilikuwa na madirisha makubwa ya kisasa na baraza kubwa mbele yake iliyopangwa seti moja ya makochi ya sofa. Nje ya nyumba hiyo upande wa kushoto kulikuwa na banda la wazi la kuegeshea magari.

Tulipofika kwenye mlango wa barazani wa kuingilia ndani nililazimika kupigapiga miguu yangu kwenye zulia dogo lililokuwa pale nje mlangoni ili kukung’uta vumbi kwenye viatu vyangu kisha nikavivua na kubaki na soksi miguuni, nikaingia ndani nikimfuata Asia. Pale sebuleni nilitulia kidogo huku nikiyatembeza macho yangu kuitazama ile sebule kubwa yenye samani zote muhimu na za kisasa.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

98

Asia aliniangalia kwa umakini kisha akaniashiria niketi kwenye kochi. Niliketi juu ya kochi dogo la sofa, Asia akaketi kwenye sofa la jirani na lile nililoketi.

“Karibu sana, Jason, hapa ndiyo nyumbani kwetu,” hatimaye Asia aliongea kwa mara ya kwanza tangu nilipompa taarifa zilizomshtua sana kuhusu mauaji ya kule porini.

“Nashukuru kupafahamu,” nilijibu huku nikiendelea kuzungusha macho yangu kuyatazama mandhari ya kupendeza ya ile sebule. Asia alishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Sijui utatumia kinywaji gani?” Asia aliniuliza huku akinikazia macho yake ya upole.

“Chochote.”

“Nasikitika kuwa tunazo soda, juisi, kahawa, chai, maji… lakini hatuna chochote!” alisema Asia kwa utani huku akiangua kicheko hafifu na kunifanya nami niangue kicheko.

“Basi nipe juisi na itapendeza zaidi kama itakuwa ya passion,” nilimwambia huku nikitabasamu.

Asia hakusema kitu bali aliinuka na kwenda kwenye ule ukumbi wa chakula, akafungua jokofu na kutoa jagi kubwa la juisi, kisha alifungua kabati na kutoa bilauri mbili ndefu, boksi lenye mirija na trei ndogo. Akaweka lile jagi la juisi, ile bilauri na boksi lenye mirija juu ya lile trei na kuja nilipokuwa nimeketi. Aliweka lile trei juu ya meza ya kioo na kuisogeza mbele yangu. Kisha akamimina juisi kwenye bilauri moja na kutoa mrija mmoja, akauweka ndani ya bilauri hiyo na kunitazama kwa tabasamu. “Karibu, bwana mkubwa.”

“Nashukuru, bi mdogo,” nilijibu huku nikiachia tabasamu kabambe.

Asia aliondoka haraka akaelekea jikoni na baada ya sekunde chache akarudi pale sebuleni akiwa amebeba sahani yenye sambusa tatu na soseji mbili na kuiweka pale juu ya ile meza ya kioo. Anakikaribisha kisha akachukua sambusa moja, akawa anakula.

“Samahani Jason, nakuacha kidogo na n’tarejea baada ya dakika mbili hivi, jisikie huru,” aliniambia na kusimama akisubiri ruhusa yangu.

“Usihofu juu yangu, unaruhusiwa kiroho safi,” nilimwambia huku nikiachia tabasamu. Asia akaniwashia runinga iliyokuwa imetundikwa ukutani na kuweka chaneli ya filamu kisha akaondoka haraka na kuufuata mlango mmoja wa kioo, akaufungua na kupotelea ndani.

Nilibaki pale sebuleni nakunywa juisi taratibu na “vitafunwa” nikajikuta navutiwa na sinema iliyooneshwa kwenye runinga, ilikuwa ni sinema ‘Catch Me If You Can’ kuhusu kisa cha tapeli mmoja mwenye akili sana ambaye hajawahi kutokea duniani.

Niliwahi kuiona sinema hiyo mara kadhaa lakini sikuwahi kuishiwa hamu, kwani huyo tapeli aliyefahamika kwa jina la Frank W. Abagnale Jr. alikuwa amefanikiwa kuwakwepa FBI na askari wengine kwa miaka mingi kiasi cha kuamua kumpa ajira alipoamua kuachana na utapeli.

Baada ya muda Asia alitokea tena akiwa kabadilisha nguo na kuketi juu ya kochi jingine huku akiniangalia kwa tabasamu. Safari hii alionekana kuchangamka zaidi na mkononi alikuwa kashika simu yake kubwa ya kisasa.

“Natumaini hujajisikia vibaya kubaki peke yako muda mrefu. Unajua tena…” Asia alisema huku akijiweka vizuri kwenye lile sofa. Nikaachia tabasamu huku nami nikijiweka vizuri pale kwenye sofa.

“Hapana… hiyo sinema imenichangamsha sana” nilisema huku nikiachia tabasamu.

Asia naye aliachia tabasamu na kuchukua ile bilauri nyingine na kujimiminia juisi, kisha akafyonza ile juisi kidogo huku akiisikilizia jinsi ilivyokuwa ikipita kwenye koo lake na kutua tumboni huku akionekana kutafakari jambo. Nilitamani sana kujua alichokuwa akiwaza. Nilimwona akifyonza tena kisha akapiga mwayo mrefu huku akijinyoosha, alionekana kuchoka mno.

Nami nikafyonza funda kubwa la juisi kinywani mwangu na kuisikilizia juisi ilivyokuwa inasafiri kwenye koo langu na kuingia tumboni kisha nikashusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani.

“Unaonekana umechoka sana au pengine hukupata usingizi usiku!” nikamwambia Asia huku nikimtazama kwa makini.

Asia aliguna huku akiachia tabasamu pana. “Ni kweli sikupata usingizi usiku, hata hivyo usijali sana, nipo sawa!”

“Punguza mawazo,” nilisema huku nikimwangalia kwa umakini katika namna ya kutafuta mazungumzo zaidi.

“Ahsante kwa ushauri wako! Ila mawazo ni sehemu ya maisha ya binadamu, sometimes unajikuta unawaza tu na hauna namna ya kukwepa. Hata hivyo ushauri wako nitauzingatia,” Asia alisema na kisha kikafuata kipindi kingine cha ukimya mrefu, Asia alionekana kuwaza mbali sana.

“Halafu hujanieleza chochote kuhusu siku ile ya tukio kule porini… sijajua ilikuwaje baada ya mimi kupoteza fahamu!” nilisema huku nikimkazia macho Asia.

Asia aliniangalia kwa kitambo kirefu kisha akaachia tabasamu lililoonekana ni la kulazimisha na lililoficha huzuni ndani yake.

“Kwa kweli sipendi kabisa kukumbuka lile tukio maana halikuniacha salama…” Asia aliongea kwa huzuni huku machozi yakimlengalenga machoni. “Nilichanganyikiwa kabisa na ilibidi nipewe tiba maalumu ya kisaikolojia kutoka kwa wataalamu wa saikolojia na afya ya akili ndipo nikaweza kukaa sawa. Nisamehe sana Jason sikukumbuka tena kuja hospitali kukuona.”

“Usijali, hata hivyo Mungu kaniponya na hatimaye katukutanisha tena tukiwa hai,” nilimwambia Asia katika namna ya kumfariji.

Muda huo huo nikaona mlango mkubwa wa barazani ukifunguliwa na mwanamke mmoja wa makamo, mnene wa wastani, akaingia pale sebuleni. Hakuwa mfupi wala mrefu bali alikuwa na kimo cha wastani na alikuwa mweupe. Hakuwa mwanamke wa kumtazama mara moja tu. Ingawa alionekana kuwa na umri mkubwa wa takriban miaka hamsini lakini ilikuwa ni vigumu mno kumtofautisha na wasichana wenye umri mdogo kutokana na jinsi alivyoonekana.

Umbo lake lilikuwa ni umbo ambalo lingeweza kulifanya kila jicho lililomuona kumtazama mara mbilimbili. Wakati namwona nikawa najiuliza kama alikuwa mrembo kiasi kile katika umri huo, je, alionekanaje enzi za usichana wake?

Kisura alifanana sana na Asia na alikuwa na macho makubwa na mazuri sana yaliyokuwa ya aina yake, ni aina ya yale macho yaliyoita kwa mng’aro sadifu, yakiambatana na kope nyingi nyeusi ambazo ziliachia nafasi kwa nyusi ili zipate kujidai. Midomo yake ilikuwa minene yenye kingo nyepesi na mikunjo midogo midogo.

Na hata tembea yake ilikuwa ya aina yake kabisa, ilishindwa kumtofautisha na wasichana vigoli. Ilikuwa ni adimu kuipata kwa wasichana wengi ambao pamoja na kujikwatua vilivyo, bado walishindwa kupata miondoko mizuri kama yake!

Yule mama alisimama na kuachia tabasamu pale alipotuona tumeketi sebuleni, akashusha pumzi ndefu na kwenda moja kwa moja alipoketi Asia, akaketi. Nikamwona Asia akimlalia yule mwanamke kama kitoto kinachodeka kwa mama yake. Nilibaki kimya nikimkodolea macho pasipo kusema neno lolote, kama niliyekuwa nimepigwa na shoti mbaya ya umeme, na bila kuambiwa nikahisi kuwa yule alikuwa ni mzazi wa Asia.

Asia alinitazama kwa makini na kuachia tabasamu kisha akaweka mkono wake mmoja juu ya paja la yule mama.

“Kutana na Bi Aisha, mama yangu mkubwa,” Asia aliniambia kisha akamgeukia Bi Aisha, “Mama, kutana na Jason…” akasita kidogo huku akinikazia macho.

“Jason Sizya,” nikawahi kusema.

“Ni rafiki yangu ambaye Mungu kanikutanisha naye katika mazingira ya ajabu sana. Huyu ndiye aliniokoa kule porini siku ya mauaji,” alisema Asia na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.

Bi Aisha alionekana kushtuka sana, alinitumbulia macho na kuanza kulengwalengwa na machozi. Alisimama na kunipa mkono wake wa kulia kwa bashasha, tukakutanisha mikono yetu huku machozi yakizidi kumlengalenga machoni.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

99

“Nimefurahi sana kukufahamu mama… shikamoo!” niliwahi kumsalimia kwa bashasha huku nikiachia tabasamu.

“Marhaba baba, nami nimefurahi sana kukufahamu na pole kwa yote yaliyotokea…” alisema, sauti yake ilikuwa ya upole sana alipoongea nami.

“Nimekwisha poa, mama,” nilijibu kwa unyenyekevu.

“Karibu sana mwanangu, niliambiwa kuwa ulilazwa VIP pale Hospitali ya Wilaya, lakini tusamehe sana hatukuweza kuja kukuona,” alisema Bi Aisha kwa huzuni huku akifuta machozi yaliyokuwa yakimtoka.

“Usijali mama,” nilijibu huku nikihisi mwili wangu ukinisisimka sana. Mbali na urembo aliokuwa nao yule mama lakini niligundua kitu kingine kikubwa zaidi kilichokamilisha uzuri na mvuto wake, ni upole wake.

Alikuwa mpole pindi aongeapo, alionekana mpole atembeapo na pengine hata alipokuwa katika shughuli zingine.

“Ule mkasa ulimfanya mwenzako achanganyikiwe kabisa, wazimu si wazimu basi ni shida tupu, hata hivyo tunamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea,” aliongea Bi Aisha kwa upole.

“Ni kweli mama, tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kila jambo, maana ni mapenzi yake hadi leo tuko hai,” nami nilisema kumuunga mkono yule mama.

Yule mama alirudi kuketi na kukatokea ukimya wa kitambo kifupi, kila mmoja akizama kwenye mawazo, kisha kama aliyegutuka, Bi Aisha aliitazama saa yake ya mkononi na kuinuka.

“Karibu mwanangu, jisikie huru mimi nipo ndani kuna kitu nafanya,” alisema huku akiondoka.

“Nashukuru, mama,” nilijibu huku nikimsindikiza kwa macho hadi alipopotelea kwenye mlango wa kioo. Kisha niligeuka kumtazama Asia kwa makini.

“Inaonekana mama yako ni mcheshi sana?” nilimuuliza nikiwa nimekazia macho.

“Sana… kitu kingine ni kwamba mama yangu ni mzungu, si mtu wa kufuatilia fuatilia mambo yangu…” Asia alisema huku akiachia kicheko hafifu.

Kikapita tena kitambo kifupi cha ukimya, nikainywa ile juisi yote iliyobakia kwenye bilauri huku nikiwaza namna ya kumuanza Asia maana pepo mbaya wa ngono alikuwa ananisumbua sana. Asia alinitazama kwa umakini kama aliyehisi kitu.

“Vipi maisha?” Asia aliniuliza huku akiniangalia usoni.

“Maisha ni kama hivi, namshukuru Mungu kwa kuwa nipo hai, vinginevyo…” nikasita kidogo na kubaki kimya. Asia akaniangalia kwa udadisi.

“Vinginevyo kitu gani mbona huendelei?” aliuliza kwa shauku. Nikajifanya natafakari kidogo kisha nikashusha pumzi ndefu.

“Asia, naomba nikuulize,” hatimaye nikamwambia kwa sauti ya utulivu.

“Niulize tu kaka yangu.”

“Je, wewe umeolewa?”

Asia akaniangalia kwa makini kwa kitambo kirefu kisha akaachia tabasamu huku akitingisha kichwa chake kukataa. “Ningekuwa nimeolewa usingenikuta naishi hapa kwa mama yangu!”

“Mchumba je, huna mchumba?”

“Hapana sina mchumba!”

“Boyfriend?”

“Pia sina! Ila kwa sasa Mungu amenipatia friend boy na siyo boyfriend, na si mwingine ni wewe Jason.”

Nikashusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikihisi faraja, sikujua faraja hiyo ilitokana na nini. Nikajiegemeza kwenye kochi.

“Kwa hiyo huna mume, huna mchumba, huna boyfriend, je mvulana ambaye labda… unampenda au…”

Asia akanikazia macho kwa mshangao huku akikunja uso wake. Ni dhahiri alionekana kukerwa na maswali yangu yaliyomjia mfululizo.

“Samahani Jason, kwani unatakaje! Sipendi kukulazimisha kusema kwa namna ninavyopenda, lakini naona kama nimekwisha jibu vya kutosha maswali yako kuhusu uhusiano wangu na wanaume. Sina uhusiano na mwanaume na wala sijawahi kuwa na uhusiano na mwanaume yeyote, sijui unahitaji nini zaidi?”

Maneno yake yakanifanya nibaki kimya kwa muda nikimkodolea macho huku nikijilaumu sana kwa kukosa uvumilivu na kuporomosha maswali mfululizo kana kwamba nilikuwa polisi ninayehitaji taarifa muhimu za kiintelijensia.

“Naomba usinielewe vibaya Asia, kama unakumbuka niliomba tuwe marafiki… ukweli ni kwamba nilikupenda tangu siku ya kwanza tu nilipokuona!” niliamua kufunguka.

Muda huo nilihisi msisimko wa aina yake ndani yangu ingawa ukweli kulikuwa na sauti ndani yangu iliyonieleza kuwa sikuwa nampenda kutoka moyoni bali nilitaka kumchezea… nilimtamani kwa ajili ya ngono tu, akishanivulia nguo zake tukashiriki tendo hamu yangu ingeisha na ningeachana naye.

Ndiyo, ningeachana naye kwa sababu nilikuwa nimeingia agano na Rehema na sikuhitaji kuishi na wanawake wawili kwa kuogopa kupata presha.

“Ni kweli unanipenda?” sauti tulivu ya Asia ilinizindua kutoka kwenye mawazo yaliyokuwa yakipita kichwani kwangu, nilimtazama nikamwona akinikazia macho, na kabla sijajibu akaendelea, “Kwanza ni upendo wa aina gani huo unaouzungumzia?”

“Upendo unaozidi urafiki, unaozidi wa kaka na dada. Upendo wa mke na mume. Yaani… nahitaji kukuoa Asia, sijui unasemaje?” nilijikakamua kuzungumza ingawa moyoni niliamini kuwa ule ulikuwa uongo mtupu.

“Huoni tuna kikwazo cha dini? Wewe Mkristo na mimi Muislamu!”

“Najua lakini kwangu si tatizo, kama utaridhia niwe na wewe.”

Asia alishusha pumzi ndefu na kuinamisha uso wake chini, alionekana kufikiria sana.

“Una hakika unanipenda na unataka kunioa, Jason?” aliniuliza akiwa kanikazia macho.

“Ndiyo, tena niko tayari siku yoyote, na ndiyo maana nilikuwa tayari kuutoa uhai wangu kwa ajili yako!” niliongea kwa kujiamini huku nikimtazama Asia bila kupepesa macho. Wanaume tunapotaka jambo letu huwa ni waongo mno.

Asia alinitazama kwa umakini sana kwa kitambo kirefu, ilikuwa ni kama vile alikuwa akiyasoma mawazo yangu kisha alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu.

“Sijaelewa, mwanzo ulitaka tuwe marafiki lakini sasa unaongelea kunioa, hivi haya unayoyasema yanatoka wapi, au unataka kunichezea tu umalize haja zako kisha…”

“Najua ni vigumu kuniamini, sijui niseme nini ili uniamini,” nilimkata kauli wakati alipokuwa akiendelea kuongea.

“Okay, naomba nikuulize maswali machache,” Asia alisema huku akiendelea kunikazia macho.

“Niulize tu,” nilijibu kwa kujiamini.

“Kwa nini unadhani kuwa unanipenda?”

“Kwa sababu nakupenda, penzi halina sababu,” nilijibu kwa kujiamini.

“Una uhakika kuwa hunipendi kwa sababu yoyote ile nyingine?”

“Kama zipo sababu, basi nakupenda kwa sababu unazo sifa zote za mwanamke ninayetaka kumuoa.”

“Ahsante!” Asia alisema na baada ya hapo kikapita kitambo kirefu cha ukimya. Nilimuona akiwa anawaza na sikujua alikuwa anawaza nini. Nikawa najiuliza ni wapi nilikotoa ule ujasiri wa kuyatamka yale yote niliyoyatamka kwa Asia wakati nikijua kabisa ni uongo mtupu.

“Lakini, hujaniambia bado kama inawezekana au vipi!” nilivunja ukimya baada ya kuona Asia yupo kimya.

“Unataka kuniambia hujaoa hadi sasa?” Asia aliniuliza huku akinitazama kwa udadisi.

“Sijabahatika,” nilimjibu kwa sauti tulivu.

“Kwa nini?”

“Kwa sababu Mungu alikuwa hajanijaalia bado.”

“Na wala huna girlfriend?”

“Ninaye!” nilijibu huku nikimkazia macho Asia, nikamuona kashtuka kidogo ingawa hakutaka kuuonesha mshtuko wake.

“Sasa… kama una girlfriend nini tatizo hadi uanze kutanga tanga?”

“Wala sijatanga tanga kwani leo ndiyo mara ya kwanza naongea naye na hajui ni kiasi gani nampenda. Girlfriend wangu ni wewe Asia!”

Asia akataka kusema neno lakini nikamuona akisita. Aliyakwepa macho yangu yaliyokuwa yakimtazama kwa umakini na kuangalia kando, kisha akashusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Jambo unalohitaji kwangu ni jambo linalohusu maisha… yangu na yako vile vile, kwa hiyo halihitaji uamuzi wa papara,” alisema Asia na alionekana kumaanisha kile alichokisema na kuendelea.

“Nahitaji muda wa kutafakari zaidi, nahitaji kukufahamu zaidi na kuufahamu ukoo wako kabla sijakubali au kukataa ombi lako. Najua hata wewe hunifahamu vya kutosha…”

“Ni kweli,” nilikubaliana na maneno yake ingawa moyoni sikuona sababu ya kuanza kuchunguzana wakati nilijua kabisa sitaweza kumuoa bali nilitaka kushiriki tendo tu na kumwacha kama wengine.

Asia alitabasamu tu bila kusema neno. Nikataka kusema neno lakini nikasita baada ya kumuona Bi Aisha akiingia pale sebuleni na kuketi kwenye sofa, kisha mazungumzo ya kawaida ya kufahamiana zaidi yakatawala maongezi yetu.

Baada ya mazungumzo marefu niliaga ili niondoke lakini Bi Aisha hakuniruhusu, aliniomba nisubiri chakula ya jioni nile ndipo niondoke. Kwa kweli yule mama alikuwa mcheshi na mzungumzaji mzuri. Nilipoondoka pale ilikuwa yapata saa 2:30 usiku, nilielekea moja kwa moja nyumbani kwangu nikiwa nimefarijika sana.

Nilipoingia tu ndani ya nyumba yangu moyo wangu ukapiga kite baada ya kukumbuka kuwa nilipaswa kuhama katika nyumba ile haraka iwezekanavyo kabla Jamila hajanikuta. Hata hivyo, nilijiuliza ningemwelezaje Rehema; kwamba nimehama kwa kumkimbia Jamila? Ilibidi nipate muda mzuri wa kutafakari kabla sijachukua hatua yoyote.

* * *

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

100

Kwa Heri!


Saa 11:00 jioni…

ILIKUWA siku ya Alhamisi, siku tatu tangu nilipotoka nyumbani kwa akina Asia na kukutana na mama yake, Bi Aisha. Nilikuwa nimewasiliana na Asia na nilimwomba aje anitembelee nyumbani ili apafahamu. Hakupinga. Na hata alipomweleza mama yake hakumkatalia.

Baada ya kutoka kazini nilielekea kwao moja kwa moja, nikamchukua hadi kwenye nyumbani yangu ya Mwime, ambayo ilikuwa na samani chache nilizonunua kwani sikuweza kuhamisha vitu vilivyopo kwenye ile nyumba ya Mbulu.

Tuliingia ndani tukaketi sebuleni kwenye sofa, nikamletea juisi kisha tukaongea mengi sana. Alishangaa kuona nyumba ilikuwa bado mpya na vitu vichache lakini nilijitetea kuwa kwa kuwa sikuwa na mke sikuona sababu ya kuwa na vitu vingi. Asia alikuwa akiniuliza maswali mengi kuhusu maisha yangu binafsi na maisha ya familia yangu, nami nilikuwa nikimjibu kila swali alilouliza kwani nilijua alichokuwa akikitafuta. Hata hivyo, nilikuwa makini sana katika majibu yangu.

Pamoja na kuwa na wakati mzuri wa kuongea na kufurahi nilijaribu sana kumwonesha kuwa nilimhitaji kwa ajili ya kushiriki tendo lakini Asia alionesha msimamo wa kutokuwa tayari, nami niliheshimu msimamo wake kwa kuogopa kuonekana nilikuwa na papara. Siku ile ukawa ndiyo mwanzo wa kuwa karibu zaidi na Asia.

Siku iliyofuata Rehema alirudi toka Misungwi, akafikia nyumbani kwangu katika nyumba ya Mwime baada ya kumwambia kuwa niliamua kuhamia Mwime huku nikifikiria kununua samani zingine. Tayari nilikuwa nimewasiliana na wazazi wangu kuwataarifu suala langu na Rehema na wakaniambia walikuwa mbioni kutuma washenga kwa wazazi wa Rehema. Siku hiyo Rehema alilala pale na kesho yake akaelekea Ushirombo kwa ajili ya kuchukua vitu vyake ambavyo alivileta pale nyumbani kwangu Mwime.

Baada ya siku mbili aliondoka asubuhi kurudi Misungwi. Mchana wa siku hiyo niliwasiliana na Asia na kumwomba aje nyumbani jioni, hakukataa. Aliwasili nyumbani kwangu muda wa saa 11:300 jioni, na alinikuta nikiwa nafanya kazi zangu kwenye tarakilishi yangu. Nikamkaribisha ndani kwa bashasha.

Hakuonesha kukaa sana lakini nami sikutaka kuipoteza nafasi ile, hivyo tukiwa katikati ya maongezi nikaanzisha tena mazungumzo yaliyohusu uhusiano.

“Unajua Asia, sifurahii aina ya maisha ninayoishi, ni ajabu kwamba katika maisha ni vitu vichache kati ya unavyovitaka ambavyo unavipata, vingi huvipati!”

“Hebu niambie Jason, ni vitu gani katika maisha yako ambavyo hujavipata? Una nyumba nzuri, una kazi nzuri, una maisha mazuri… ni nini hujapata?” Asia aliniuliza huku akiniangalia usoni kwa udadisi.

Niliinamisha uso wangu kidogo nikijifanya kutafakari ingawa kimsingi sikuwa natafakari chochote, kisha nikanyanyua uso wangu kumtazama huku nikishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Ni kweli, nashukuru Mungu nimesoma vizuri, nina shahada ya teknolojia, nina kazi nzuri yenye mshahara mkubwa, nina nyumba hii na viwanja kadhaa, na ninapata mahitaji yangu yote muhimu. Lakini bado zipo haja nyingine zilizomo ndani ya nafsi yangu ninashindwa kuzipata!”

Asia akacheka kidogo. “Kama zipi hizo?”

“Upendo…” nilijibu huku nikimtazama kwa makini.

“Unataka kuniambia kuwa familia yako hawakupendi?” Asia aliniuliza huku akinitazama kwa mshangao.

“Familia inanipenda sana, lakini pendo ninalozungumzia hapa ni lile ambalo… ni tofauti na la baba, mama, dada au kaka!” nilisema huku nikimkazia macho.

Asia aliguna na kuangalia kando akijaribu kuyakwepa macho yangu, hata nilipojaribu kumchunguza sikuiona tashwishwi usoni kwake. Kisha nikamwona akiinuka, akaaga na kuanza kuondoka.

“Keti kwanza,” nilimwambia Asia huku nikimzuia asiondoke.

Asia alinitazama kwa makini kwa kitambo fulani kisha alitii na kurudi kwenye sofa, akaketi huku akiniangalia kwa makini. Tukabaki tunaangaliana kwa kitambo.

Nilivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku nikiuma midomo yangu, nikajifanya nafikiria kidogo kisha nikamkabili Asia kwa sauti tulivu.

“Najua umenisisitiza kuwa na subira, lakini naomba tu nikwambie ukweli, moyo wangu umeshindwa kufanya hivyo ingawa umekuwa mvumilivu mno… Nilihisi kuna wakati pamoja na matendo yangu kwako ningefanikiwa kubadilisha hisia zako lakini naona unazidi kunikatisha tamaa!” nilisema kwa huzuni. Asia akaniangalia kwa umakini sana na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Niwie radhi… nakuthamini, nakuheshimu na nakupenda vile vile, lakini siko tayari kwa jambo hilo kwa sasa… huo ni msimamo wangu na sidhani kama unaweza kubadilika,” Asia alisema kwa sauti yenye utulivu lakini akimaanisha kile alichokisema.

“Lakini…” nilitaka kusema lakini Asia alinikatisha kwa ishara ya mkono.

“Suala la kufanya ngono kwa sasa halipo moyoni mwangu na wala halipo akilini mwangu… nasikitika Jason!”

“Naheshimu msimamo wako, lakini nimeomba jambo ambalo naamini limo ndani ya uwezo wako… nikiamini mimi na wewe ni wachumba! Sasa… bado hujanipa sababu za wewe kukataa!” nilimwambia Asia huku nikiwa nimekunja sura yangu.

Asia aliinamisha uso wake chini akaonekana kutafakari sana na alipouinua uso wake alinitazama kwa makini. Uso wake ulisheheni maumivu na huzuni kubwa iliyoonekana wazi.

“Sababu… sababu zipo, kwanza dini hairuhusu!” alisema huku akiuma mdomo wa chini.

Nikatingisha kichwa changu kukataa. “Hicho ni kisingizio tu. Kwa vyovyote utakuwa na mtu wako, ila mimi unanizuga tu!”

“Sina mwanamume na wala sifikirii kuwa na mwanamume mwingine yeyote. Nimetokea kukupenda wewe tu… wewe ndiye mwanamume wa maisha yangu!” Asia aliniambia. Nikamtazama kwa makini na kuuona ukweli wa maneno yake kwenye macho yake.

Nikajiuliza, ingekuwaje siku uongo wangu ukijulikana? Hiki sasa kilikuwa kioja. Rehema alijua mimi ndiye mwanamume wa maisha yake, Jamila pia alidai mimi ni mwanamume wa maisha yake. Hata Asia pia amedai hivyo hivyo! Sasa akili yangu ilianza kwenda kasi, nilianza kujiuliza ni shetani gani aliyekuwa ameniingia hadi kujikuta nikishindwa kutosheka na mtu mmoja? Ni shetani gani aliyenifanya nitamani kila mwanamke mrembo niliyekutana naye?

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

101

Nikahisi kizunguzungu na jasho jepesi likaanza kunitoka. Hata hivyo, nilijikakamua nikamsogelea karibu zaidi nikamtazama moja kwa moja machoni.

“Thibitisha kama kuna ukweli katika maneno yako vinginevyo nitaamini vipi?”

Asia alinitazama kwa makini kwa kitambo kirefu kidogo, kisha akashusha pumzi zake huku akinyanyua mabega yake juu.

“Sioni kwa nini niongope. Kama huniamini sawa, sina namna ya kukufanya ukubaliane na kila kitu nisemacho. Ila ninachojua ni kuwa wewe ndiye mwanamume wa maisha yangu, basi.” Asia alisema na kuinuka.

Nikabaki nikimwangalia kwa makini nikiwa sijui niseme nini. Mara nikamwona Asia akiinuka. Nami nikainuka kutaka kumzuia.

“Kwa heri!” alisema na kuondoka haraka akiniacha nimepigwa butwaa.

Donge la hasira lilinikaba kooni, nikarusha mikono yangu hewani kama ishara ya kukata tamaa kisha nikajibwaga juu ya sofa na kushusha pumzi ndefu huku nikisonya kwa hasira.

“Aende zake na asinibabaishe. Kwani yeye nani hadi nimbembeleze sana!” nilijiambia na kusonya kwa hasira.

Japo Asia alikuwa amenikasirisha kwa kukataa ombi langu lakini ukweli niliujua kuwa sikuwa mtu sahihi kwake, pamoja na kunihakikishia kuwa alinipenda bado nilimhitaji kwa sababu moja tu, ngono! Nilitegemea akinivulia nguo zake tukashiriki tendo hamu yangu ingeisha na ningeachana naye.

Yaani nilitaka kuwa katika uhusiano na Asia kwa sababu ya ngono tu na kilichoniudhi ni yeye kutotaka kushiriki ngono na mimi. Alinikwepa sana hadi nikajisikia vibaya. Nikahisi huenda alikuwa ana mtu mwingine.

Sasa nikajikuta pepo mbaya wa ngono akinivagaa, nikapanga kumwonesha Asia kuwa nilikuwa na wanawake wengine. Usiku wa siku ile Asia alinipigia simu lakini sikupokea, hata alipotuma ujumbe mfupi kwenye simu yangu wa kuniomba msamaha kutokana na kitendo alichokionesha kwangu sikuujibu, nilitaka kumwonesha kuwa nilikuwa nimechukia sana.

Kitendo cha kutokupokea simu wala kujibu jumbe zake kilinifanya niwe na uhakika kwamba kingemuumiza sana na kwa vyovyote kesho yake angekuja nyumbani kwangu, hivyo nilimpigia simu nesi Hilda kumwomba tuonane nyumbani kwangu. Nilimwelekeza na kumtaka achukue teksi nami ningelipa.

Hilda hakuwa na pingamizi lolote kwani aliisubiri nafasi ile muda mrefu ndiyo maana hakupinga na bahati nzuri siku ile alikuwa ameanza mapumziko baada ya kumaliza zamu ya usiku.

Hilda alikuwa karibu zaidi na mimi muda wote alipokuwa zamu wakati nikiwa nimelazwa pale hospitali baada ya mkasa wa mauaji kule porini. Alijitolea kwa kila hali kunihudumia hata pale alipokuwa hayuko zamu, jambo lililonivutia sana.

Ukawa mwanzo wa urafiki ambao baadaye ukazaa penzi. Ingawa Hilda alijua kabisa kuwa nilikuwa na mchumba lakini hakikuwa kipingamizi cha kutokubali ombi langu, alitokea kunipenda. Nilipotoka hospitali tuliendelea kuwasiliana na alikuja nyumbani kwangu kule Mbulu mara mbili kwa ajili ya kunijulia hali ingawa hatukuwahi kushiriki tendo.

Usiku wa siku ile niliupitisha nikiwa na Hilda nyumbani kwangu Mwime na siku iliyofuata tuliamka saa 3:00 asubuhi tukiwa hoi. Siku hiyo wote tulikuwa na mapumziko na hivyo hatukuwa na haraka ya kuamka. Tulipotoka kitandani tuliingia bafuni kisha Hilda aliandaa chai na baadaye tukaketi sebuleni kwa ajili ya kifungua kinywa, na tulipokuwa tukinywa chai, nilishtushwa na mlio wa gari lililosimama ghafla huko nje. Nikajua tayari mambo yalikuwa yamekwenda kama nilivyopanga.

Hilda alinishtukia akaniuliza, “Vipi baby, kuna nini?”

“Hakuna kitu… Vipi kwani?” Nilimjibu huku nikijaribu kusikilizia vizuri kama ni Asia au alikuwa mtu mwingine.

“Nimesikia muungurumo wa gari, sitaki watu wako wanikute hapa. Wakija waondoe mapema maana leo nataka tukimaliza kunywa chai tulale, bado nina hamu na wewe,” Hilda aliniambia kwa utani huku akijitahidi kuangalia nje kupitia ukuta msafi wa dirisha lakini hakuweza kuona kwani ukiwa katika ukumbi wa chakula huwezi kumwona mtu aliyepo barazani. Alikuwa na wasiwasi.

Nilimwangalia nikatabasamu bila kusema neno. Mara nikaisikia sauti ya hatua za haraka zikija hadi kwenye mlango wa barazani, kisha zikasimama.

“Nani?” Hilda aliniuliza kwa sauti ndogo huku akifinya macho yake. Nilibetua mabega yangu na sikusema neno japo nilikwisha mjua aliyekuwa kasimama barazani.

Taratibu mlango wa barazani ulifunguliwa. Asia akiwa amevaa sketi ndefu nyeusi yenye miraba myeupe, blauzi ya bluu ya mikono mirefu na viatu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio akaingia. Alikuwa amejimwagia mafuta mazuri yaliyosambaa sebule yote hadi kule kwenye ukumbi wa chakula. Alipoingia alisimama akizungusha macho yake kabla hajatuona pale mezani, akatutazama kwa makini.

“Karibu Asia,” niliongea huku nikiachia tabasamu. Sauti yangu ilikuwa tulivu sana. “Kutana na best wangu, Hilda…” nilimwambia Asia kisha nikageuza shingo yangu kumtazama Hilda, “Huyu ni dada yangu mpenzi, Asia.”

Asia aliachia tabasamu japo nilihisi halikuwa tabasamu halisi ila lilificha huzuni au hasira fulani ndani yake, alipiga hatua akaja kuketi kwenye kiti tupu karibu yangu huku akiniangalia usoni kwa makini kisha akayahamishia macho yake kwa Hilda. Hilda akageuza shingo yake kuniangalia kwa jicho la kuuliza lakini hakuthubutu kusema chochote.

Niliachia tabasamu nikionekana kutobabaika kabisa. Kikapita kimya kirefu, huku wanawake wote wawili wakinitazama kwa makini.

“Sijauelewa vizuri utambulisho wako, Jason… unaweza kunitambulisha tena huyu ni nani na mimi ni nani?” Asia aliniuliza kwa sauti tulivu.

“Huyu ni mwanamke na wewe ni mwanamke,” lilikuwa jibu langu.

“Najua kuwa sisi ni wanawake, lakini nataka kujua yeye ni nani?”

“Nimeshakwambia anaitwa Hilda, hayo mengine wayatakia nini?” niliongea kwa kufoka.

Asia aliniangalia kwa makini, nikayaona machozi yakimlengalenga kwenye macho yake, hakutaka kuendelea kukaa pale aliinuka na kuondoka haraka, akafungua mlango na kutoka kisha nikasikia muungurumo wa gari lake lilipokuwa likiondoka kwa kasi na kupotelea mtaani.

Kwa kiasi fulani moyo wangu ulikuwa umeridhika kwa kitendo nilichomfanyia Asia nikiamini kuwa baada ya siku ile angeniheshimu maana nilijua kuwa alikuwa ananiona bwege. Moyoni mwangu nikaahidi kuendelea na vimbwanga vya hapa na pale hadi anyooke.

Muda wote Hilda alikuwa akiniangalia bila kusema neno, nilijua kuwa alikuwa amejisikia vibaya sana kwa kile kilichomtokea mwanamke mwenzake, japo sikujali. Nilijitahidi kumsemesha lakini alibaki kimya akiniangalia kwa umakini. Kisha alishusha pumzi ndefu.

“Jason, najua wewe ni kijana mtanashati sana na kila mwanamke angependa kuwa na wewe, lakini nimehuzunika sana kwa kuwa sipendi kugombanisha wawili wapendanao. Usingefanya uliyofanya, mimi ningeweza kuwapisha badala ya hiki kilichotokea!” Hilda alisema kwa uchungu.

“Kwani mchumba wangu humfahamu? Asia si mpenzi wangu bali tumezoeana tu kwa kuwa nilimsaidia kwenye lile tukio la kule porini.” nilimwambia Hilda katika kumtoa wasiwasi. Kisha nilimsimulia kuhusu tukio zima lilivyokuwa na jinsi nilivyomuokoa Asia.

Hilda aliamua kukubali yaishe lakini hakuonekana kuridhishwa na maelezo yangu. Baada ya chai hakutaka kuendelea kuwepo pale kwa kuwa alijisikia vibaya, nilimkubalia kwa kuwa nilikuwa nimefanikisha lengo langu. Hilda akaondoka zake akiwa amenyong’onyea.

Baada ya siku ile zilipita siku tatu nikiwa sina mawasiliano na Asia ingawa ukweli sikutaka uhusiano wetu uishie katika hali ile, niliamini kuwa Asia alikuwa ananipenda ingawa sikujua kwa nini hakuwa tayari kushiriki ngono, bila sababu zozote za msingi.

Kila nilipolikumbuka chozi lake nilijikuta roho yangu ikiniuma sana japo siku ile nilijifanya sikujali. Niliumia lakini nikaamua kukaza kamba, kwa nini alikuwa ananinyima penzi? Nilijiuliza nikakosa majibu. Hatimaye nikafikia uamuzi wa kuachana naye. Lakini tatizo lilikuwa ningeachana naye vipi bila kuonja ladha yake? Nilijiapia kuwa jambo hilo lisingewezekana hata kidogo, mimi kama mwanamume kamili angenitangaza kwa rafiki zake kuwa sijawahi kulala naye tukafanya tendo. Ingekuwa aibu kubwa kwangu!

* * *

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

102

Anajigonga
?

Saa 9:30 alasiri…

HALI ya hewa ilikuwa baridi kiasi na iliambatana na upepo wa wastani. Nilikuwa natembea taratibu kwenye barabara ya kutokea Chattle Restaurant kuelekea nyumbani kwa akina Asia. Siku hiyo niliamua kuondoka mapema zaidi kazini ili nikamtafute Asia.

Ilikuwa ni siku ya nne tangu Asia amkute Hilda nyumbani kwangu na kuondoka, hii ilikuwa baada ya kuona Asia hajanitafuta niliamua kujishusha kwa kuamua kwenda kwao kumtafuta. Nilipokuwa nakaribia kufika nyumbani kwa akina Asia mita chache mbele yangu nikawaona wanawake wawili waliokuwa wanatokea upande niliokuwa naelekea.

Nilipatwa na mshtuko mkubwa nikiwa siamini macho yangu. Nilitamani ardhi ipasuke ili niingie na kupotelea humo. Nilihisi kuchanganyikiwa maana niliowaona mbele yangu walikuwa Jamila na mama mmoja aliyekuwa na umbo kubwa lililovutia. Mwanamke yule alikuwa Mwarabu na mrefu kama alivyokuwa Jamila.

Mara moja nikagundua kuwa huyo ndiye yule shangazi yake aliyekuwa akinielezea habari zake kwani mama yake nilikuwa namfahamu. Mama yule alikuwa na macho makubwa mazuri yaliyoambatana na kope nyingi nyeusi ambazo ziliachia nafasi kwa nyusi ili zipate kujidai, na midomo yake ilikuwa minene yenye kingo nyepesi na mikunjo midogo midogo.

Jamila aliponiona alishtuka sana na kukunja sura yake kisha akaongea jambo kwa yule mwanamke kwa sauti ya chini na kumfanya yule mwanamke aniangalie kwa umakini huku akiachia tabasamu. Hata hivyo sikuona tashwishwi usoni kwa Jamila.

“Jason!” Jamila aliita huku akiniangalia kwa umakini, “Leo umepote njia?”

“Tusalimiane kwanza,” nilimwambia Jamila huku nikilazimisha tabasamu.

“Najua hujambo ndiyo maana upo barabarani saa hizi!” Jamila alisema kwa sauti ya hasira huku chuki ya wazi ikijionesha usoni kwake. Kisha aligeuza shingo yake kumwangalia yule mama aliyekuwa naye.

“Shangazi, huyu ndo yule mwanaume aliyeamua kunitenda, anaitwa Jason Sizya…” Jamila alisema huku akiniangalia kwa chuki. Nikaiona sura ya shangazi yake ikichanua kwa tabasamu.

Alinisogelea na kunyoosha mkono wake kunisalimia kwa bashasha zote huku uso wake ukiendelea kupambwa na tabasamu pana.

“Nimefurahi sana kukufahamu Jason. Mimi ni shangazi yake Jamila, naitwa Bi Aisha maana naona hataki kunitambulisha kwako…” shangazi yake Jamila aliongea kwa sauti ya kishambenga. “Huwezi kuamini, kila siku Jamila haachi kukutaja taja hadi nikawa najiuliza huyu Jason yukoje hasa… maana hatuli wala hatulali, kila saa ni Jason! Jason!”

“Shikamoo!” nilimwamkia shangazi yake Jamila baada ya kukosa neno la kuongea, huku nikiwa na haya usoni kwangu. Nilikuwa nimeinamisha sura yangu na macho yangu yakiangalia chini.

“Marhaba… na pia pole sana kwa mkasa uliokupata,” shangazi yake Jamila aliitikia huku akiniangalia usoni.

“Ahsante, nimeshapoa.”

“Nadhani mguu huu ulikuwa unakuja nyumbani kwetu. Karibu!” shangazi yake Jamila alisema huku akinionesha kwa kidole e ilipo nyumba yao.

Nilishtuka sana maana nyumba aliyokuwa akinionesha ilikuwa imepakana na nyumba aliyokuwa akiishi Asia na mama yake mkubwa Bi Aisha. Pia nilishtushwa sana kwa kuwa hata shangazi yake Jamila pia aliitwa Bi Aisha. Muda wote Jamila alikuwa akiniangalia kwa umakini, macho yake yalionesha chuki.

“Jason, ujue nimekasirishwa na use**e wako ulionifanyia. Wewe si mtu wa kunifanyia hivyo au kwa sababu nilikuonesha nakupenda sana na kuamua kuuvua utu wangu kwako basi ukaniona mjinga, siyo? Umeamua kunizimia simu na hata nyumbani kwako umepakimbia!” Jamila aliongea akiwa amefura kwa hasira.

Nilishangaa sana! Jamila aliwezaje kuongea maneno kama yale mbele ya shangazi yake.

“We Jamila, hebu acha hasira zako za kijinga bwana, hapa tupo njiani usitake kuwapa watu faida!” yule mama alimwambia Jamila huku akiwa amekunja sura yake.

“Shangazi we hujui tu alichonifanyia huyu mwanaume. Amefikia hatua ya kunizimia simu na hata nyumbani kwake amepakimbia…”

“Unajua alikuwa na matatizo gani hadi akawa hapatikani? Unakimbilia tu kusema amekukimbia. Kwa nini umeshindwa kumuuliza kistaarabu hadi mpandishiane? Si vizuri bwana!” yule mama alimwambia Jamila kwa hasira.

“Ndiyo kanikimbia. Leo nilikwenda hadi kazini kwake kuna mtu akanielekeza alikohamia,” Jamila alisema na kunifanya nishtuke sana.

“Mzowee tu mwenzio. Twende ukapaone nyumbani kwetu, au kuna sehemu ulikuwa unaelekea?” yule mama aliniuliza baada ya kuachana na Jamila aliyekuwa amefura kwa hasira.

Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani, nikatingisha kichwa. “Kuna mtu ninakwenda kumwona mara moja hapo mbele, ni muhimu sana maana muda wote ananisubiri mimi tu,” niliamua kuongopa ingawa ukweli nilikuwa nakwenda nyumba ya jirani kwa Asia. Jamila aliniangalia kwa umakini.

“Sasa leo nakuja nyumbani kwako huko ulikohamia na nisipokukuta nitajua cha kufanya. Wewe si umeianzisha vita basi umeipata nitakufanyia kitu ambacho hutokuja kunisahau katika maisha yako,” Jamila aliongea kwa hasira na kuanza kuondoka. Shangazi yake alimwangalia kwa makini na kutingisha kichwa chake huku akisonya.

Mwili wangu wote ukajikuta ukilowa jasho na midomo kunitetemeka kwa hasira. Sikujua kwa nini alithubutu kuongea maneno makali mbele ya shangazi yake pasipo hata uoga. Pia nilijiuliza ni nani aliyemwelekeza makazi yangu ya Mwime? Nikajikuta naanza kukata tamaa.

“Mkwe, we mzowee tu, bado ana mambo ya kitoto sana!” yule shangazi aliniambia kisha akaondoka kumfuata Jamila.

Nilisimama palepale nikiwashuhudia wakiingia ndani ya uzio wa ile nyumba kisha nikaondoka nikiwa na maswali mengi kichwani kwangu, sikuwa nimefikiria kabisa kukutana na Jamila katika mazingira yale. Pia sikutegemea kuona kuwa Jamila na Asia walikuwa majirani na pengine walifahamiana!

Sikuwa na hamu tena ya kwenda kumtafuta Asia, na sikutaka kurudi nyumbani muda huo, hivyo nikaamua kwenda Kahama Tulivu Garden, sehemu tulivu sana, kwa ajili ya kupunguza mawazo. Sikutaka kwenda sehemu zenye mkusanyiko mkubwa wa watu bali nilihitaji mahala ambako ni tulivu, nitakapopata wasaa, japo kwa muda mfupi, wa kuyasahau masahibu yangu.

Kahama Tulivu Garden ilikuwa moja kati ya sehemu zenye utulivu sana kama lilivyo jina lake, club ya kisasa yenye kila kionjo cha zama za leo. Ilikuwa sehemu iliyopendwa sana na wageni wengi toka katika miji na nchi mabalimbali waliofika hapo Kahama kutokana na utulivu wake na mandhari ya kuvutia mno.

Niliifahamu sehemu hiyo na ndiyo maana nikachagua kwenda hapo kwa sababu ilikuwa ndiyo sehemu pekee niliyoamini ingeweza kunisaidia kunisahaulisha na dhahama iliyonikumba japo kwa saa chache. Sikutaka kunywa kilevi lakini kwa hali niliyokuwa nayo niliagiza mvinyo mweupe aina ya Dodoma Wine.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

103

Maneno ya Jamila yalinifanya niwe mwenye wasiwasi mkubwa japo shangazi yake alijaribu kunitoa wasiwasi lakini sikutaka kuipuuzia kauli ile. Nilijiuliza ni kipi kilichokuwa kikimpa jeuri ya kunitishia maisha? Kwa nini niendelee kuishi maisha ya uoga namna ile sababu ya binti mdogo kama Jamila?

Baada ya kitambo fulani cha kuwepo pale Club nikitafakari hili na lile hatimaye nilijikuta nikipata majibu ya maswali yangu na hivyo, kama mwanamume nilikuwa tayari kukabiliana na chochote.

Jinsi nilivyoendelea kunywa ule mvinyo ndivyo kilevi kilivyozidi kunipanda kichwa na kujikuta nikipata hamu ya kuwa na mwanamke wa kustarehe naye, kama kawaida yangu nilijikuta nikivutiwa na binti mmoja mhudumu aliyekuwa akipita karibu yangu. Sikujua kama ilikuwa ni pombe au ndivyo alivyokuwa, kwani machoni kwangu alikuwa mrembo sana, alikuwa mrefu na mwembamba wa wastani mwenye sura nzuri na alisuka nywele zake katika mtindo wa rasta zilizomkaa vyema. Alikuwa nadhifu akiwa ndani sare za kazi; suti safi ya samawati, shati jeupe na tai ya buluu.

“Samahani binti, sijui unatoka kazini saa ngapi?”

“Mimi ndo kwanza nimeingia jioni hii hivyo muda wa kutoka ni hadi saa sita usiku,” yule mhudumu aliniambia na kunikata maini.

“Mmh, sawa!” nilijibu huku nikichukua bilauri ya mvinyo na kuugida mvinyo wote uliobakia kwenye ile bilauri.

“Kwani vipi?” yule mhudumu aliniuliza huku akiniangalia kwa umakini.

“Basi…” nilimjibu nikiwa nimekata tamaa. Hata hivyo nikakumbuka na kumtupia swali kabla hajaondoka. “Hapa Kahama unakaa wapi?”

“Nyihogo,” alinijibu huku akiniangalia kwa udadisi.

“Unaitwa nani?”

“Saida Mhando.”

“Umeolewa?”

“Wanaume waoaji wapo wapi? Kila mwanamume atataka akufunue tu na akikuchoka anaachana na wewe!” yule mhudumu alisema na kunifanya nisitake kuendelea na maongezi. Nikamruhusu aondoke na wakati akiondoka nilimsindikiza kwa macho yaliyojaa ubembe.

Sasa sikutaka kuendelea kukaa pale, nikaamua kuondoka. Nilifika nyumbani kwangu Mwime saa 12:30 jioni na nilipoingia ndani nilisimama pale sebuleni huku nikiupima utulivu ndani ya ile nyumba kana kwamba ilikuwa mara yangu ya kwanza kuwepo pale.

Nikiwa nimesimama pale sebuleni nikahisi kama kulikuwa na mtu amejibanza mlangoni kwangu, nikauendea mlango na kuufungua kwa tahadhari, na kweli kulikuwa na mtu. Si mwingine ila Jamila. Alikuwa amesimama pale mlangoni na wakati akijiandaa kuufungua mlango ndipo na mimi nikawa nimeufungua na kumshtua sana. Hata mimi nilikuwa nimeshtuka ingawa sikutaka kuuonesha mshtuko wangu.

“Vipi?” nilimuuliza Jamila huku nikimkazia macho.

“Vipi kuhusu nini? Ndo nimekuja!” Jamila alisema huku akiniangalia kwa macho ya kisasi. “Au ulidhani sitapaelewa ulipohamia?”

“Kwa hiyo umekuja kunisimanga au kufanya nini?” nilimuuliza huku nikijitahidi kuizuia hasira yangu. Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yakienda kasi na damu ilichemka na kukimbia kwenye mishipa ya damu.

“Nimekuja kama nilivyoahidi au umesahau tuliongea nini?”

“Zaidi ya matusi yako hata sikumbuki, hebu nikumbushe,” nilimwambia Jamila huku donge la hasira likianza kunikaba kooni.

“Nikukumbushe? Nipishe kwanza niingie ndani halafu nitakukumbusha,” Jamila alisema huku akinisukuma. Sikuwa na namna nikampisha, akaingia na kusimama katikati ya sebule huku akiiangalia kwa makini.

Wow! A nice house!” Jamila alisema huku akizungusha macho yake kuyatazama mandhari ya sebule yangu.

Sikumjibu bali nilibaki kimya nikimwangalia kwa makini. Kasha nikaufunga mlango na kwenda kuketi kwenye sofa.

“Nini kimekuleta hapa? Unajua sijapenda kabisa maneno yako leo, nilimheshimu sana shangazi yako…”

“Samahani kama nilikukera, zile zilikuwa hasira tu!” Jamila alisema huku akisogea na kuketi jirani na pale nilipoketi. Akaniangalia kwa pozi la kimahaba huku akiachia tabasamu.

“Hata hivyo nimekuletea habari njema, nadhani itakusisimua kidogo.”

“Habari ipi?” niliuliza kwa shauku.

“Nina mimba,” Jamila aliongea kwa sauti ya kunong’ona huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wangu.

Ilikuwa ni kama pigo la kisu ambalo lilipenya mwilini mwangu na kuujeruhi moyo wangu, nilihisi kama moyo wangu ukicharangwa kwa visu vikali na kubanikwa katika moto mkubwa! Kati ya yote niliyoyatarajia jioni ya siku hiyo, jambo hilo, la ujauzito, halikuwamo kabisa akilini mwangu.

Bila kujua nitendalo, nilijikuta nikimshika Jamila mkono kwa vidole vyangu vikubwa na kumbana huku akimuuliza kwa sauti iliyoonesha mshtuko, “Mimba? Mimi nahusika vipi na hiyo mimba yako?”

Jamila aliniangalia kwa hofu huku akijaribu kujitoa katika mkono wangu. Ilikuwa ni kama kujaribu kujitoa katika pingu. Badala yake ndiyo kwanza vidole vyangu vilizidi kudidimia katika ngozi yake laini. Akanitazama usoni kwa mshangao zaidi ya hasira.

“Unaniumiza Jason!” Jamila alilalamika huku akifinya sura yake kwa maumivu.

Ndiyo kwanza nikagundua kuwa nilikuwa nimemshika Jamila mkono kwa nguvu. Nilimwachia na kuiona damu ikianza kutoka katika michubuko iliyosababishwa na vidole vyangu. Nikashusha pumzi.

“Sipendi utani, Jamila!” nilimwambia huku nikihisi mwili wangu mzima ukimwagikwa na jasho na mikono ikinitetemeka kama niliyepigwa na shoti ya umeme.

“Wala si utani. Nimepima jana na kugundua nina ujauzito…”

“Kwa hiyo ukaona uje kunibambika mimi!” nilimkatisha Jamila kwa hasira huku donge la hasira likinikaba na kusimama kwenye koo langu. Joto kali la hasira lilikuwa limeibuka ndani yangu na sofa nililokalia lilikuwa kama lenye moto. Hapakukalika tena, mara niliinuka mara niliketi kana kwamba nilikuwa nikikalia kaa ambalo lilikuwa likiniunguza.

“Nikubambike wewe kwa lipi! Kwani tulipokuwa tunashughulika ulikuwa unamwaga nje?”

“Nitaamini vipi kama huo ujauzito ni wangu? Unaishi Masumbwe, kumbuka!”

“Kwa hiyo nikiishi Masumbwe ndiyo nini?” Jamila aliongea huku akiinuka na kunisimamia mbele yangu na kunishikia kiuno.

“Nawajua vizuri vijana wa Masumbwe, wanajua sana kuimbisha na kufuatilia mwanamke utadhani wanatafuta kazi. Mimba hiyo itakuwa ya kijana mmoja wa huko huko,” nilimwambia Jamila huku nami nikiinuka. Nilitamani ardhi ipasuke ili nitumbukie.

“Usitake kukataa Jason, huu ujauzito ni wako. Sijatembea na mwanaume mwingine zaidi yako…” Jamila alinitazama kwa jicho kali la hasira huku akinipandasha na kunishusha.

“Mbona sikukukuta ukiwa bikira?”

“Ni kweli, lakini kwa sasa sina mwanaume mwingine ila wewe tu.”

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

104

“Mimi nitaamini vipi?” nilimuuliza Jamila huku nikiwa nimetahayari japo nilijifanya sijali.

“Kwa hiyo unataka kuniambiaje?” Jamila aliniuliza huku akinikazia macho, machozi yalianza kumlengalenga.

“Haiwezekani kabisa. Kwani mwanaume rijali ni mimi peke yangu? Kwanza kwa tabia yako nani atakuamini?” nilisema kwa sauti kali na hapo nikamwona Jamila akibadilika rangi na kuwa mwekundu.

“Kwa hiyo ushaniona malaya, eh! Au kwa sababu nilikupanulia mapaja yangu ndiyo maana sasa unaniona malaya? Umewahi kuniona wapi nikiwa na mwanaume mwingine?” Jamila aliniuliza kwa sauti ya juu. Sasa alianza kulia kilio cha kwikwi kama mtoto mdogo.

Nilitaka kuongea lakini nikashindwa, kitu fulani kilinikaba kooni na kunifanya nishindwe kuongea.

“Naomba usitake kuyafanya mambo yawe makubwa zaidi, Jason. Jambo la watu wawili lisiwe la wengi, nitakujazia watu sasa hivi na najua aibu itakuwa kwetu wote. Kumbuka mimi nipo tayari kwa lolote,” Jamila alisema huku akiendelea kulia kwa uchungu kama mtoto mdogo.

Mh! Mambo yalikuwa mazito, nilishindwa nifanye nini. Nilijiona nipo kwenye mtihani mzito sana na hivyo sikuona sababu ya kuendelea kugombana na Jamila bali nilitakiwa kutumia busara. Nilijishusha na kuanza kumbembeleza nilivyojua ili baadaye tufanye mpango wa kuitoa hiyo mimba. Niliona heri lawama kuliko fedheha, nikamkubalia kuwa ni ujauzito wangu ili tupange namna ya kufanya maana nilikuwa sina jinsi.

Niliketi kwenye sofa kisha nikamuomba Jamila akae, akakaa karibu yangu. Kabla sijamweleza nilichokusudia akaniambia kitu kingine kilichonimaliza zaidi, kuwa hata shangazi yake alikuwa anajua kila kitu kuhusu ujauzito huo na kwamba ndiye msiri wake kwenye mambo yaliyotuhusu. Aliniambia kuwa alifurahia sana kuwa nami na kwamba masuala ya harusi yake hayakuwa na umuhimu tena!

Nikiwa bado nimechanganyikiwa taratibu Jamila akajiegemeza kifuani kwangu huku akinitazama kwa macho malegevu. Muda huo macho yake yalikuwa mekundu. Kisha akaanza uchokozi wa kunipapasa papasa, nilitaka kumzuia lakini hakutaka kunielewa.

Sikuwa na ujanja kwa jinsi Jamila alivyojiweka kifuani kwangu nikajikuta nikitulia na kumwacha afanya yake. Baada ya kuridhika aliinuka na kutoa baibui lake na gauni jepesi na kubakiwa na nguo ya ndani tu. Akasimama mbele yangu huku akijichekesha chekesha. Nilitaka kunyanyuka akanirudisha kwenye sofa kwa kunisukuma.

“Usiwe na haraka, acha nikuoneshe mambo.”

Nilibaki nimekaa kwenye sofa huku nikihema kwa nguvu kama simba aliyemkimbiza swala na kumkosa. Akaanza kufungua vifungo vya shati langu na kulivua kasha akalirusha kando huku muda wote nikiwa sijui nini nifanye kwake. Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yakinienda mbio huku jasho jembamba likinitoka.

Kisha mikono yake ikahama toka hapo na kushuka chini, akaanza kufungua mkanda wa suruali yangu na kuivuta chini. Kufumba na kufumbua nikajikuta nikiwa nimebakiwa na boksa tu, Jamila akapiga magoti mbele yangu kama mtoto anayetambaa huku akiuchukua mkono wangu na kuniwekea kifuani mwake. “Niminye chuchu.”

Nikaanza kuziminya chuchu zake na kumfanya aanze kutoa miguno ya raha huku akitweta kwa ashki, alionekana kuhisi faraja iliyopenya hadi kwenye mishipa yake ya damu.

Mara nikahisi kusikia muungurumo wa gari likifunga breki nje ya nyumba lakini akili yangu ilikuwa haifanyi kazi sawasawa muda huo. Muda wote nilikuwa nafikiria namna ya kumfanya Jamila akubali kuitoa mimba, kama kweli alikuwa nayo.

Sikujua ni muda gani yule mtu aliyekuja na gari alishuka, nilishtuka baada ya kuhisi nyayo za mtu zikikija na kupanda kwenye ngazi za barazani, nikatulia nikisikiliza kwa makini lakini sikusikia chochote maana ukimya ulitawala, nikadhani labda yalikuwa mawazo yangu tu na hakukuwa na chochote.

Nikaanza tena kumpapasa Jamila huku nikiupeleka ulimi wangu kwenye sikio lake, akaonekana kusisimkwa tena na kuachia kicheko. Muda ule ule mlango wa sebuleni ukagongwa taratibu na kukatiza kicheko cha Jamila.

Mimi na Jamila tukashtuka sana na kukodolea macho kwenye ule mlango, kisha Jamila akanitazama katika namna ya kuniuliza kama nilikuwa namjua mtu aliyekuwa anagonga ule mlango. Sikuwa na jibu. Kwa sekunde kadhaa kukazuka ukimya mzito. Mlango ukagongwa tena, safari hii kwa nguvu zaidi.

“Nani?”

Hakuna aliyejibu. Nikashangaa zaidi na kumtupia jicho Jamila ambaye alibaki kimya akinitazama kwa makini.

“Wewe nani?” niliuliza tena huku hasira zikianza kunipanda.

Lakini mgongaji aliendelea kukaa kimya, kisha nikaona kitasa cha mlango kikinyongwa na mlango ukasukumwa na kufunguka. Bila kusita Asia akaingia sebuleni na kusimama huku akitupa macho yake kuangalia pale kwenye sofa, akapigwa butwaa.

Jamila alishtuka sana kumwona Asia. Wakabaki wametazamana kwa mshangao kama majogoo yaliyotaka kupigana. Nilimwona Asia akiwa katika mshtuko mkubwa na midomo yake ilikuwa inamtetemeka.

Kwa nukta chache moyo wangu ulisahahu mapigo yake na yalipoanza tena nilivuta pumzi ndefu, nikazishusha. Nilimtupia jicho Asia huku nikijaribu kuzuga.

“Jamila!” Asia aliita kwa mshangao mkubwa huku akimkodolea macho Jamila akiwa haamini kumwona pale.

“Asia!” Jamila naye aliita huku akiendelea kuonesha mshtuko mkubwa sana usoni kwake, kisha akageuza shingo yake kunitazama kwa umakini akionekana kuwa na maswali mengi.

Mimi nilibaki kimya nikiwa nimetahayari sana. Ingawa sikushangaa sana kuona kuwa Asia na Jamila walikuwa wanafahamiana lakini sikutegemea kuwa wangekutana nyumbani kwangu.

“Unasemaje, Asia?” hatimaye nikajikakamua na kuumuliza Asia.

Asia alibaki kimya, midomo yake ilikuwa inamtetemeka. Machozi yakaanza kumtiririka mashavuni. Jamila alishindwa kusema chochote na kubaki anashangaa, alitutazama mimi na Asia kwa zamu akiwa haelewi kilichokuwa kinaendelea, kisha akajiinua na kuketi kitako kitandani huku akiufunika mwili wake kwa shuka.

“Jason, mbona sielewi, kwani kuna nini kinaendelea hapa? Au…” Alishindwa kumalizia sentensi yake akashusha pumzi akiwa hajui aseme nini.

Nilibaki kimya nikiwa nimetahayari. Asia akashusha pumzi za ndani kwa ndani, alijaribu kuyazuia machozi yaliyokuwa yanaendelea kumtiririka bila mafanikio. Akajikuta akilia kwa uchungu mbele yangu na Jamila.

“Jason kwa nini hukuniambia kama wewe na Jamila ni wapenzi? Kwa nini siku zote ulikuwa unaniongopea kuwa unanipenda kumbe una wapenzi wengi tu! Juzi nimemkuta mwingine leo tena una Jamila!”

Niliendelea kuwa kimya nisijue la kufanya. Jamila alinitupia jicho kali akionesha kukasirika sana, lakini alikuwa akiyakwepa macho ya Asia.

“Ndiyo maana huoneshi kujali hisia zangu bali unachotaka wewe ni ngono tu! Ni bora ungenieleza ukweli wala nisingesumbuka kuja hapa…”

Sasa Asia alikuwa analia kwa uchungu mbele yangu, kisha aliniambia kwa uchungu kabla hajatoka, “Nakupenda sana Jason, na wewe unajua hilo… wewe ni mwanaume wa maisha yangu, ila kwa hiki ulichonifanyia nashukuru sana na kwa heri.”

Asia alisema na kugeuka, akatoka taratibu na kuufunga mlango nyuma yake. Chozi lake liliniumiza sana na kwa mara nyingine tena nilihisi hatia moyoni mwangu lakini sikuweza kuonesha chochote mbele ya Jamila.

Asia alipotoka tu Jamila akasimama huku akiniangalia kwa hasira na kushika kiuno. “Naomba uniambie ukweli, nini kinaendelea kati yako na Asia?”

“Sina uhusiano wowote na Asia. Nilimwokoa siku ile ya mauaji kule porini na tukazoeana basi lakini hakuna kinachoendelea. Naona anajigonga tu kwangu!”

“Anajigonga? Siyo Asia ninayemjua! Asia hawezi kujigonga kwa mwanaume na huwa hana mpango na wanaume. Kwanza nimeshangaa kumwona hapa!” Jamila alisema kwa mshangao huku akinikazia macho.

“Kwa hiyo huniamini au vipi, nakwambia sina uhusiano wowote na Asia ila anajigonga tu…” niliongea kwa sauti bila kujua kuwa kumbe Asia hakuwa ameondoka, alikuwa amesimama barazani nje ya mlango.

“Nashukuru sana, Jason. Kumbe najigonga kwako!” sauti ya Asia tokea barazani ilinishtua sana. Sikuwa nimetarajia kama angekuwa bado yupo eneo lile akitusikiliza.

Nilijisikia vibaya sana ingawa nafsi nyingine ilinikumbusha kuwa nilikuwa katika uhusiano na wasichana wale kwa sababu moja tu… ngono, na kwa kuwa Asia hakutaka kushiriki ngono na mimi na alionesha kunikwepa sikuona kwa nini anionee wivu kiasi kile.

Niliinuka na kufungua mlango wa barazani, nikachungulia pale barazani na kuliona gari aina ya Mark X jeusi likiondoka taratibu toka eneo lile nje ya nyumba yangu. Kumbe wakati huo Jamila alikuwa anavaa nguo zake kasha alikuja kusimama nyuma yangu huku akinitazama kwa hasira, machozi yalikuwa yanamtoka. Nilipogeuka nikashtuka na kumfuata huku nikilazimisha tabasamu.

“Jamila, naomba unisikilize basi, bado hatujaongea…”

“Tuongee kuhusu nini? Sina haja ya kuongea na wewe… mfuate Asia labda atakusikiliza!” Jamila alisema kwa hasira huku akinikwepa.

Nilimsogelea karibu zaidi na kuupeleka mkono wangu wa kulia kwenye uso wake kwa uangalifu huku nikiachia tabasamu la kumlainisha, si kwa kulazimisha. Jamila aliusukuma mkono wangu kwa hasira na kurudi nyuma hatua moja huku aking’aka. “Usiniguse! Vinginevyo nitakachokufanya utajuta kuzaliwa.”

Niliminya midomo yangu huku nikimtazama Jamila kwa uchungu. Nilikuwa nafikiria ni namna gani nitaweza kuongea naye kuhusu suala la ujauzito kabla hali haijawa mbaya.

“Sikiliza Jamila…” nilianza kusema huku nimejiegemeza kwenye ule mlango kumzuia Jamia asiweze kutoka. Jamila alinitazama kwa chuki. “Tunatakiwa tuzungumze kuhusu suala la ujauzito wako, kumbuka siku si nyingi utafunga ndoa na kwenda Omani…” nilisema huku nikimkazia macho.

“Tena naomba usinikere kabisa. Wala sina mimba ya mwanaume kama wewe usojua kupendwa!” Jamila alisema kwa hasira na kunifanya nipatwe na mshangao mwingine. “Kama nina mimba ni bora niitoe… kwanza nilikuwa nakupima akili yako tu nione kama mwanaume kweli!”

“Unasemaje?” nilimuuliza huku nikimkazia macho.

“Ndo kama ulivyosikia, siwezi kurudia kwa kuwa haya si matangazo ya vifo!” Jamila alisema huku akishusha pumzi ndefu.

“Kwa hiyo huna mimba?” nilimuuliza tena huku nikiwa nimemtulizia macho usoni. Nilihitaji kuhakikishiwa kuwa hakuwa na ujauzito. Jamila alinikata jicho kali la hasira kisha akaachia msonyo mkali. Akaanza tena kulia kwa uchungu huku akipumua kwa nguvu.

Nilimfuata nikaanza kumbembeleza huku nikimpapasa mgongoni. Alisonya kwa hasira na kunisukuma kisha akauendea mlango, akaufungua na kutoka. Nilibaki nikiwa nimepigwa butwaa nisijue nini cha kufanya. Sasa ingalau niliweza kupumua kidogo kwa kujua kuwa Jamila hakuwa na ujauzito ila alitaka kunipima akili yangu. Na niliamini kwa kile kilichotokea muda mfupi asingeweza kurudi tena nyumbani kwangu.

Nilikwenda mlangoni na kufungua kisha nikachungulia nje, sikumwona Jamila na hivyo nikajua kuwa alikwisha ondoka. Nilirudi sebuleni na kujipweteka juu ya sofa huku nikishusha pumzi za ndani kwa ndani.

* * *

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

105

Hata Hungoji Kutambulishwa?


Saa 4:30 usiku…

NILIKUWA nimeketi pale kwenye sofa hadi saa nne na ushee usiku, sikuhisi njaa na mawazo yalikuwa yakizunguka kichwani kwangu. Nilikwenda chumbani, nikapanda kitandani lakini sikuweza kupata usingizi. Usiku ule sikulala. Ilikuwa shida sana kupata usingizi. Nilijawa mawazo mengi kuwa Asia asingenielewa tena.

Niliwaza mambo mengi kuhusu lile tukio la Asia na Jamila kufumaniana nyumbani kwangu. Dah! Nilijilaumu sana kwa kushindwa kudhibiti tamaa zangu katika kipindi kile ambacho nilikuwa kwenye mchakato wa kumuoa Rehema.

Sikupenda kuwa na uhusiano na Jamila maana alishaanza kuonesha ukorofi, ila nilitamani sana nimtafute Asia ili nimuombe msamaha maana niliamini kuwa machozi yake yalikuwa yamebeba laana fulani. Usiku mzima nikawa namuwaza Asia tu.

Ilipofika saa nane za usiku uvumilivu ulinishinda, nilichukua simu yangu na kupiga namba ya Asia, simu iliita kwa muda mrefu na kukata bila majibu, nikapiga tena, baada ya muda mrefu wa kuita nikasikia simu ikipokelewa upande wa pili.

Hello… Asia!” nilisema mara baada ya simu kupokewa upande wa pili.

“Unasemaje?” Asia aliniuliza kwa sauti tulivu.

“Asia, samahani sana kwa yote yaliyotokea… naomba…” simu ikakatwa kabla sijamaliza kuongea! Nilipiga lakini simu ya Asia ilikuwa haipatikani, nikasonya na kuitupa simu yangu kando.

Kwa kweli sikuweza kupata usingizi, niliinuka nikaelekea sebuleni na kuwasha runinga, hata hivyo, pamoja na kukodoa macho yangu kwenye runinga lakini sikuwa naelewa chochote.

* * *



Saa 3:25 asubuhi…

Nilikuwa nimeketi mbele ya tarakilishi ofisini kwangu na macho yangu yalikodolea kioo cha tarakilishi kana kwamba nilikuwa natafuta jambo. Hata hivyo mawazo yangu hayakuwa pale bali nilikuwa nawaza mbali sana, mezani kwangu kulikuwa na kikombe cheupe cha chai iliyokwisha poa. Nilikuwa nimechoka sana kutokana na kukosa usingizi usiku, muda wote nilipiga miayo.

Nilikuwa nimeingia kazini tangu saa moja na nusu nikiwa mwenye mawazo mengi na nilionekana kama mtu aliyechanganyikiwa, muda mwingi nilihisi macho ya wafanyakazi wenzangu yalikuwa yakinitazama kwa kuibia na baadhi yao walionesha kushangazwa na mabadiliko ya tabia yangu.

Muda wote nilikuwa mwenye wasiwasi huku nikiitazama saa yangu, niliwaza kumpigia simu Asia lakini moyo wangu ulisita. Nikawaza kuwa huenda angenipigia simu. Niliendelea kuitazama saa yangu mpaka mishale ifike kunako tatu na dakika therathini.

Bila ya sababu, moyo wangu ulianza kunienda kasi sana. Dakika moja ilipita, ya pili… ya tatu! Sikujua nilichokuwa nikikisubiri. Simu ya Asia? Asia yupi? Yule aliyenifumania jana na Jamila kisha nikamkana! Au Asia mwingine? Moyo wangu ulipiga mshindo mkubwa, ukanipasuka niliposikia simu yangu ya mkononi ikiita, niliiangalia kwa makini nikaiona namba nisiyoifahamu ikionekana kwenye kioo. Niliipokea haraka na kuipeleka kwenye sikio langu, kwa sauti ya kutetemeka nikasema, “Hello!”

“Hi, Baby!” sauti tamu ya mwanamke ilipenya vyema kwenye ngoma yangu ya sikio na kunisisimua mwili.

“Hi! Nani mwenzangu?” niliuliza kwa sauti yenye mashaka kidogo.

“Mimi Rehema, bwana! Hii inamaanisha kuwa una wanawake wengi, siyo?” Rehema alisema kwa msisitizo na kunishtua sana. Jasho jepesi lilianza kunitoka mwilini na mapigo ya moyo wangu yakazidisha kasi.

“Aa, nimeshangaa maana namba ni mpya!” nilijaribu kujitetea huku nikishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Hata kama namba ni mpya, inamaana hata sauti yangu huitambui au umezongwa na mawazo?” Rehema aliniuliza kwa sauti iliyojaa udadisi.

“Samahani baby, unajua mambo ni mengi na wakati mwingine yananichanganya,” nilisema huku nikijitahidi kuifanya sauti yangu kuwa ya kawaida.

“Mbona unaonekana kama una jambo linalokusumbua. Nini kinakusumbua, mpenzi wangu?”

“Wala hakuna…”

“Usinidanganye Jason, nakufahamu vema. Unaonekana kama hujalala usiku… ulikuwa na nani?” Rehema aliniuliza swali lililonishtua sana. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kusoma hisia za mtu kwa kuisikia tu sauti yake kwenye simu!

“Ni kweli sikupata usingizi usiku lakini sikuwa na mtu yeyote,” nilishindwa kumbishia, nikamjibu na hapo hapo nikaamua kubadilisha mada haraka.

Tukaanza kuongea mambo mengine hasa kuhusiana na maandalizi ya ndoa yetu huku nilimwelezea jinsi nilivyokuwa sipati usingizi kutokana na umbali uliokuwepo kati yetu na kwamba nilitamani ndoa yetu iwe mapema zaidi. Hadi tunamaliza mazungumzo yetu Rehema bado alionesha wasiwasi.

Baada ya mazungumzo yetu kwenye simu nilijikuta nikizama tena kwenye mawazo ya kumfikiria Asia. Siku hiyo nilikuwa mkimya kuliko kawaida, na kwa ukimya wangu nilihisi wafanyakazi wenzangu walikwisha tambua nilikuwa na mawazo fulani. Hata hivyo, wasingeweza kujua ni mawazo gani kwani kulikuwa na mengi ambayo yangeweza kunisumbua kijana kama mimi.

“Jason,” nilisikia sauti ya bosi wangu ikiniita, nikainua macho yangu kumtazama.

Macho yangu yakatua kwenye uso wa mwanamume wa kizungu, mrefu na kipande cha baba akiwa amesimama mbele yangu akinitazama kwa umakini sana. Umri wake wa miaka hamsini na mbili ulikuwa haujazipokonya nguvu zake mwilini. Macho yake makali yalinitazama kwa tuo huku akionekana kuipa utulivu akili yake.

Mzungu huyo aliitwa Dawson Peters na alikuwa Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu na Huduma za Kampuni. Asubuhi ile alivaa suti maridadi ya kijivu na miwani mikubwa ya macho.

Jason, are you okay?” (Jason, uko sawa?) Peters aliniuliza huku macho yake yakiendelea kunitazaama kwa tuo pasipo kupepesa.

I think… ah, I’m fine!” (Nadhani… ah, nipo sawa!) nilibabaika kidogo katika kujibu.

Are you sure?” aliniuliza kwa msisitizo huku akinikazia macho.

Yeah!” nilimjibu kwa kifupi.

Tulibaki kimya kwa nukta chache tukiangaliana, kisha akaniuliza swali nisilolitegemea. “I've been here for a while trying to talk to you but you seem to be far away. Did you argue with your fiancé?” (Nimesimama hapa kitambo najaribu kukusemesha lakini naona uko mbali. Kwani umegombana na mchumba wako?)

No.” (Hapana).

Has there not been any conflict between you? You don’t have to tell me if you think there is no need!” (Hakujatokea mzozo wowote kati yenu? Si lazima unieleze kama unadhani hapana haja!) aliniambia huku akiachia tabasamu. Mr. Peters alimfahamu Rehema na alijua kuwa nilikuwa mbioni kuoa.

We couldn't argue…” (Tusingeweza kuzozana…) niliongea kwa sauti ya chini. “She is currently not here, she has been transferred to Misungwi.” (Kwa sasa hayupo hapa, amehamishiwa Misungwi).

Has she been transferred to Misungwi?” (Amehamishiwa Misungwi?)

Nilibetua kichwa changu kukubali.

Why did they take her away from you while you are in the process of getting married?” (Kwa nini wamempeleka mbali nawe wakati mpo kwenye process ya kuoana?)

She has been promoted to the position of District Commissioner.” (Amepandishwa cheo, kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya).

Okay! And you’ve missed her a lot?” (Sawa! Na umemkumbuka sana?) Peters aliniuliza huku akinikazia macho. “It is a very stupid question but its answer can help me find a solution to your problem.” (Ni swali la kijinga sana lakini jibu lake laweza kunisaidia kutafuta suluhu ya jambo lako). Alinyamaza na kunitazama kwa makini akingoja jibu langu.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

106

Nilishindwa kumwambia kuwa jambo lililokuwa likinisumbua akili yangu si kuwa mbali na Rehema bali suala la Asia. Hata hivyo nilibetua kichwa changu kukubali. Peters aliniangalia kwa kitambo kisha akaachia tabasamu huku akibetua kichwa chake. Bila ya shaka alitambua kuwa hicho ndicho kilichonifanya kuwa na mawazo.

I can understand,” alisema kisha akanyamaza kwa nukta chache kabla hajaendelea. “I know your leave is next month but maybe you wanna start this week? Could it help you to manage your own affairs, or what do you say?” (Najua likizo yako ni mwezi ujao lakini pengine wapenda kuanza likizo yako wiki hii? Yaweza ikakusaidia kushughulikia mambo yako, au wasemaje?)

I’ll be very grateful.” (Nitashukuru sana).

Okay, you can follow up on your leave form and fill it out, then bring it to my office,” (Sawa, fuatilia fomu ya likizo uijaze, kisha niletee ofisini kwangu) alisema kisha akaanza kuondoka.

Alipofika mlangoni akageuka na kunitazama. “Would you like to be paid your full salary?” (Ungependa ulipwe kabisa mshahara wako?)

I'd like that, Sir,” (Ningependa hivyo, bosi) niliongea huku nikiachia tabasamu dogo.

Good,” Mr. Peters alisema, “Ask Salma to prepare everything for you. Okay?” (Mwambie Salma akutayarishie likizo na mshahara wako. Sawa?)

Nilibetua kichwa, nikainuka na kuufuata mlango, nikatoka kuelekea masjala.

* * *



Saa 3:00 asubuhi…

Zilipita siku tatu pasipo kumwona Asia wala kuwasiliana naye. Kipindi cha siku hizo kilikuwa kirefu na kigumu sana kwangu. Muda mwingi nilikuwa nakunywa mvinyo nikijitahidi kujisahaulisha kuhusu Asia lakini nilishindwa. Yaani kadiri nilivyojitahidi kutomfikiria na kadiri Asia asivyonitafuta au kunipigia simu ndiyo nilivyozidi kumfikiria.

Kwa kuwa nilikuwa nimeanza likizo sikutaka kwenda mbali na nyumbani kwangu, muda mwingi nilikuwa najifungia ndani nikipata mvinyo huku nikitazama filamu na vipindi vingine vya burudani kama mpira katika runinga kubwa ya ukutani.

Katika muda ule wa saa tatu za asubuhi nilikuwa nimeketi sebuleni nikiwa sijui nifanye nini. Jambo kubwa nililoamua kulifanya ni kujisahaulisha kuhusu Asia, kufanya jitihada nitoke kwenye mawazo yanayomuhusu Asia ili niweze kuendelea na maisha yangu na Rehema. Hata hivyo, nilijikuta muda wote picha ya Asia ilikuwa ikijivinjari akilini mwangu. Waswahili husema mapenzi ni upofu, japo hatukuwahi kujivinjari kwenye ulimwengu wa huba lakini moyo wangu ulikuwa umezama kwa Asia.

Baada ya kuona nimeshindwa kujizuia niliamua kuchukua simu yangu, nikatafuta namba ya Asia na kumpigia. Simu yake iliita, nikashusha pumzi huku nikipanga maneno ya kumwambia. Simu yake iliita kwa muda mrefu pasipo kupokelewa na mwishowe ilikatika, nilipopiga kwa mara ya pili nilisikia ujumbe kuwa simu haipatikani. Nilipogundua kuwa alikuwa amenikatia simu nilichanganyikiwa.

Kama kuna jambo linaweza kumpa msongo wa mawazo mtu basi ni pale anapopenda lakini huyo anayependwa asioneshe mrejesho chanya au kuingia mitini. Mawazo yalizidi kunisumbua. Mwishowe niliamua kwenda nyumbani kwa akina Asia. Potela mbali liwalo na liwe.

* * *



Saa 4:30 asubuhi…

NILIFIKA nyumbani kwa Bi Aisha na kusimama nje ya uzio wa nyumba, karibu ya lango la mbele la kuingilia, nikiwa na wasiwasi mwingi, niliangalia huku na huko kwa wasiwasi na kushusha pumzi za ndani kwa ndani kisha nikabonyeza kitufe cha kengele kilichokuwa kando ya lile geti.

Nilipoona kimya nikabonyeza tena kile kitufe cha kengele na muda uleule nikaisikia sauti ya Bi Aisha kutoka ndani ikinikaribisha. Mara geti dogo lililokuwa kando ya lile geti kubwa likafunguliwa na Bi Aisha akachungulia nje na kuniona, nikamwona akiachia tabasamu la makaribisho.

“Karibu, baba,” alinikaribisha huku akisogea kando kunipisha niingie ndani. Nilisita kuingia, nikashusha pumzi huku nikibabaika kidogo.

“Sh’kamoo, mama!” nilimsalimia Bi Aisha nikiwa bado nimetahayari.

“Marhaba. Karibu ndani Jason!” Bi Aisha alijibu huku akinitazama kwa udadisi.

Nilionekana kusita sana, nikayatupa macho yangu kuangalia ndani ya ule uzio wa nyumba kupitia upenyo mdogo wa mlango uliokuwa wazi huku nikijaribu kubashiri iwapo Asia alikuwepo ndani au katika mazingira yale. Bi Aisha alizidi kunitazama kwa udadisi zaidi.

“Vipi Jason, kuna tatizo?” aliniuliza huku akinikazia macho.

Nilitingisha kichwa changu taratibu kukataa huku nikiendelea kuchungulia ndani ya ule uzio. Bi Aisha aliguna huku akiniyatuliza macho yake usoni kwangu kwa udadisi zaidi kisha akageuza shingo yake kutazama nyuma yake, sehemu ambako macho yangu yalikuwa yameelekea.

“Asia yupo?” hatimaye nilimuuliza Bi Aisha.

“Hayupo, amekwenda Hospitali ya Dk. Memba,” Bi Aisha alinijibu huku akinikazia macho. Jibu lake likanishtua sana.

“Hospitali! Kuna nini?” niliuliza kwa wasiwasi.

“Tangu juzi aliporudi toka kwako alianza kulalamika kuwa hajisikii vizuri,” Bi Aisha alinijibu huku akiendeelea kuniangalia kwa umakini, niligundua kuwa macho yake yalionekana kuficha kitu. Sikujua kitu hicho kilikuwa hasira, chuki au huruma.

Sikutaka kuendelea kusimama pale, niliondoka haraka nikashika njia ya kuelekea Hospitali ya Dk. Memba bila hata kuaga, nilikuwa naifahamu hospitali ile kwani ilikuwa eneo la Majengo, si mbali na nyumbani kwa Eddy. Wakati naondoka nilimsikia Bi Aisha akiguna lakini sikujali wala kugeuka, niliendelea na safari yangu nikimwacha akinisindikiza kwa macho yenye mshangao.

Nilifika kwenye kituo cha bodaboda, nikachukua bodaboda moja na kumwambia mwendesha bodoboda hiyo aniwahishe Hospitali ya Dk. Memba. Dakika saba baadaye nilikuwa nimeshafika pale hospitalini na nilikuwa naingia kwenye geti la kuingilia katika hospitali hiyo. Macho yangu yakavutwa kumwangalia msichana mrembo aliyekuwa akitembea taratibu lakini kwa madaha kuelekea kwenye maegesho ya magari pale hospitalini.

Alivaa kigauni kifupi kilichoishia juu ya magoti na hivyo kufanya miguu yake mizuri na minene kidogo kuonekana kwa uzuri. Msichana yule alilifikia gari moja jeusi aina ya Toyota Mark X na kubonyeza rimoti, milango ikafunguka, aliufungua mlango wa dereva ili aingie lakini kabla hajaingia aligeuza shingo yake na macho yake yakakutana na yangu, nikamwona akishtuka sana. Akabaki ameduwaa. Msichana huyo alikuwa Asia. Nilipata nguvu za ghafla, nikamsogelea na kusimama mbele yake.

“Umefuata nini hapa?” Asia aliniuliza huku kakunja uso wake.

“Nimekufuata wewe! Ni nani anayeweza kuendelea na kazi zake wakati ampendaye yuko hospitali?” niliongea kwa utulivu huku nikijitahidi sana kutabasamu.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

107

Asia hakujibu kitu, alinitazama kwa dharau kuanzia chini hadi juu, akinipandisha na kunishusha kisha akaangalia kando kwa muda akionekana kuwaza mbali. Alikuwa anapumua kwa nguvu.

“Asia, najua nimekuudhi sana, nimekukosea sana na nimekuumiza sana… lakini sasa nimetambua kuwa mimi na wewe tunapendana kwa dhati, hivyo naomba unisikilize, usinihukumu kabla hujanipa nafasi nikuelezee…”

Asia alionesha ishara ya kunitaka nisiendelee kuongea. “Huna unachoweza kunieleza, Jason… au unadhani sijui kilichotokea huko nyuma baada ya mimi kuondoka nyumbani kwako? Please leave me alone!

Nilishtuka sana kusikia yale maneno kutoka kwa Asia lakini sikutaka kuonesha mshtuko wangu, nikamkazia macho. “Kilitokea nini?”

“Hata ukijidai kuficha lakini najua, na hata mama yangu anajua, pia shangazi yake Jamila anajua kila kitu. Kama ulifikiri unaweza kutuchanganya basi sahau,” Asia alisema huku kanikazia macho. Nikaduwaa.

“Wewe si wa kutembea na dada wa rafiki yako wakati unajua kabisa kuwa anaolewa hivi karibuni, hadi umempa ujauzito!” Asia aliongeza na kunifanya nishtuke sana.

“Najua kakwambia kuwa hana mimba lakini ukweli ana mimba yako na hayuko tayari kuitoa,” Asia aliongeza na kuingia ndani ya gari yake.

Nilishtuka sana lakini nikaamua kujikaza kisabuni huku nikimzuia Asia asiondoe gari lake. Alinitazama kwa umakini kwa kitambo fulani huku akionekana kuzuia hasira zake kisha akashusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Naomba nikuulize jambo, Jason,” Asia alisema huku akitoka ndani ya gari na kusimama mbele yangu, alinitazama moja kwa moja machoni kwa macho makali yaliyokuwa yakiwaka kwa hasira.

“Ruksa, niulize!” nilijibu huku na mimi nikimtazama moja kwa moja machoni kwa umakini. Kwa kitambo kifupi tukabaki tumetazamama kama majogoo yaliyotaka kupigana.

“Hivi, wewe unaamini kama kupenda kupo?” Asia aliniuliza akiwa anaendelea kunitazama moja kwa moja machoni pasipo kupepesa macho.

Nilitulia kwa sekunde kadhaa nikimtumbulia macho huku nikijaribu kufikiria kidogo, kisha nikashusha pumzi ndefu.

“Mapenzi yapo. Wapo wanaopenda na wapo wanaopendwa… yule anayependa huwa yumo mashakani, kwani anao uwezo wa kuyafanya mambo yasiyowezekana yakawa ya kweli kwa sababu ya kupenda, na yule anayependwa… yeye nadhani, mara nyingi… apendwaye huwa hajali!” nilijibu huku nikishangaa nilitoa wapi yale majibu.

Sikujua kabisa kwani kwa miaka mingi sikuamini kama kulikuwa na mapenzi ya kweli. Ila sasa nilikuwa nimenasa. Asia aliminya midomo yake na kushusha pumzi.

“Ni kweli, mara nyingi anayependwa huwa hajali! Lakini unajua kama kuna tofauti kati ya mtu anayependa na anayetamani?” Asia aliniuliza tena akiwa bado ananitazama moja kwa moja machoni pasipo kupepesa macho.

“Mimi namzungumzia mtu anayependa, si mtu anayetamani,” nilisema na kumfanya Asia aangue kicheko cha dharau kisha akaingia ndani ya gari lake na kufunga mlango.

“Sidhani kama mimi na wewe tunasafiri kwenye boti moja. Ingawa nakupenda sana lakini sioni namna nyingine ya kufanya. Kama ni uvumilivu nimefika mwisho, kwa heri Jason na ninaomba usinitafute tena!” Asia alisema na kuwasha injini ya gari lake kisha akaanza kuliondoa taratibu.

Nililisindikiza gari la Asia kwa macho ya huzuni huku nikiwa nimekata tamaa. Nilihisi donge la uchungu likinikaba kooni na kunifanya nishindwe kupumua vizuri, machozi yalianza kunitoka machoni na kuwafanya watu waliopita eneo lile wanitazame kwa mshangao.

Mara nikaliona lile gari likisimama. Asia alishusha kioo cha gari na kutoa kichwa chake nje kisha akaniashiria kwa mkono nimfuate. Nilimfuata kwa unyonge huku nikipangusa machozi yaliyoendelea kunitoka, nilipomfikia akaniashiria niingie ndani ya gari, nami sikujivunga niliufungua mlango wa mbele wa gari kushoto kwake na kuingia.

Asia alinitupia jicho mara moja na kuliondoa gari lake bila kusema chochote, gari likatoka kwenye geti la kuingilia la hospitali na kuchukua uelekeo wa upande kulia kisha tukaifuata barabara ya lami iliyokwenda kuungana na barabara ya kuelekea Uhindini. Hadi wakati huo sikujua tulikuwa tunaelekea wapi, nilibaki kimya tu nikimtazama Asia kwa kuibia.

Asia aliongeza mwendo wa gari na mbele kidogo tukaifikia barabara ya Mhongoro, akakunja kuingia kushoto na mbele tukaikuta barabara ya kuelekea stendi ya mabasi, nikamuona akiongeza mwendo hadi tulipofika usawa wa majengo ya Hospitali ya Wilaya, akakunja na kuingia upande wa kushoto akiifuata barabara iliyoelekea katika Hoteli ya Pine Ridge, kisha akaliingiza gari lake kwenye geti la kuingilia katika ile hoteli ile.

Tulipoingia ndani ya uzio wa ile hoteli Asia aliniangalia kwa kitambo huku akiliacha gari lake liungurume taratibu kisha akazima injini ya garina kufungua mlango, akashuka. Nami nikashuka na kumfuata kimya kimya, tukatafuta sehemu nzuri ya kukaa kwenye mgahawa wa kisasa uliokuwa ndani ya hoteli ile.

Kwenye mgahawa ule tulikuta wateja wachache wakiwa wameketi, Asia aliagiza mchemsho wa kuku wa kienyeji na chapatti moja. Mimi niliagiza kahawa ya maziwa, sambusa mbili na soseji moja. Sikuwa nikihisi njaa lakini pia sikutaka kubaki bila kula.

Mhudumu alipoondoka kwenda kuleta oda zetu takabaki tukiwa kimya kila mmoja akiwaza lake, na baada ya kitambo tuliletewa chakula, tukaanza kula taratibu huku kila mmoja akiwa kimya. Wakati tunakula Asia alikuwa akinitupia jicho mara kwa mara akionekana kuwa makini zaidi na mimi.

“Asia… najua nimekukosea sana, lakini ni vizuri kama tutazungumza kuhusu matatizo yetu kuliko ukimya huu! Ni pepo mbaya tu alinipitia lakini naahidi sitorudia tena…”

“Kwani unatakaje?” Asia alinikata kauli huku kakunja sura yake.

“Tafadhali naomba uniahidi kuwa umenisamehe,” nilisema huku nikimwangalia kwa macho ya kuomba msamaha.

“Nilikwisha kusamehe hata kabla hujanitafuta kuniomba msamaha, ingawa nashindwa kusahau yote uliyonifanyia,” Asia aliniambia kwa sauti ya chini huku akiendelea kula chakula taratibu.

“Nashukuru kama umenisamehe, na ninashukuru kwa kuwa umethibitisha kuwa unanipenda… hata hivyo naomba kujua kwa nini umekuwa hutaki tufanye mapenzi?” nilimuuliza tena huku nikiwa siyatoi macho yangu kwenye uso wake.

“Je, ni lazima swali lako nilijibu sasa hivi?” Asia aliniuliza huku na yeye akinikazia macho.

“Ikikupendeza unaweza kunijibu sasa hivi, vinginevyo naweza kukupa muda!” nilisema kwa sauti tulivu nikiendelea kumtazama.

“Basi nipe muda, kwani ni swali gumu lililoulizwa katika wakati mbaya na mahali pagumu!” Asia alisema huku akitafuna kipande cha nyama ya kuku.

“Hebu tuwe wakweli Asia, msichana mrembo kama wewe unaweza kuishi bila kufanya mapenzi? Hii hainiingii akilini… wanaume wangapi wanakutongoza, kwani wewe ni nani hadi usiingie majaribuni?” nilimuuliza kwa wasiwasi huku nikimkazia macho kujaribu kuyasoma mawazo yake.

Asia alinitazama kwa makini kwa kitambo kirefu, nikagundua kuwa alikuwaa amekerwa sana na kauli yangu ingawa alijitahidi kuzuia hasira zake.

“Unanikosea sana heshima, Jason, kwa nini uongeee vitu usivyovijua? Naomba uelewe, mimi siko kama unavyodhani!” Asia aliongea kwa huzuni.

“Kumbuka ni wewe pekee niliyeamua kukuweka kwenye moyo wangu wa nyama. Najua huwezi kuamini ila siku nikipotea jumla ndiyo utajua kuwa nilikuwa nakupenda kiasi gani!” Asia alisema na kuinamisha uso wake chini akionekana kuwaza mbali sana. Machozi yalikuwa yakimlengalenga machoni.

Nilishtuka sana kwa maneno yake. Nilitaka kusema neno lakini nikasita baada ya kuhisi kulikuwa na mtu aliyefika eneo lile na kusimama nyuma yangu. Nikageuza shingo yangu na kumwona mwanadada mmoja aliyekuwa na umbile kubwa lakini lililovutia sana.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

108

Kwa yeyote awaye mwanaume rijali hapana shaka kama angemwona angekiri kuwa alikuwa na umbo zuri sana la kibantu na alikuwa ni moto wa kuotea mbali. Kwa mlingano wa macho tu, alitoa tafsiri ya kuwa na ule uzuri usiomithilika, uzuri kama wa mdoli.

Nywele zake zilikuwa nyeusi tii zilizotumwa vema sambamba na sura yake ya kitoto yenye mvuto wa asilimia mia moja. Nyusi na kope zake zilikuwa ndefu zilizong’ara na kuyafanya macho yake yawe wazi nusu. Pua yake ilikuwa ndefu kiasi, nyoofu ya wastani na midomo yake ilikuwa minene. Alikuwa na rangi angavu yenye ung’avu wa kuteleza.

Japo alikuwa na umbo kubwa lakini kifua chake kilibeba matiti ya wastani na tumbo lake lilikuwa flati huku kiuno chake kikiwa chembamba mithili ya dondola. Miguu yake ilikuwa mizuri mno iliyotazamika. Mwanadada yule alikuwa amevaa gauni zuri la kitenge na alikadiriwa kuwa na umri usiopishana na wa Asia.

Alisimama pale akimtazama sana Asia kama aliyekuwa akimfananisha. Mara Asia akainua uso wake na kumtupia jicho yule mwanadada kisha akanitazama kwa makini.

Nilimtazama tena yule mwanadada kwa makini lakini sikumfahamu kabisa na hivyo sikuwa na hofu kama angeweza kuwa mmoja wa wasichana niliowahi kutoka nao kimapenzi. Nikageuza tena shingo yangu kumtazama Asia ambaye aliendelea kumtazama yule mwanadada katika namna ya kumfananisha. Wakaendelea kutazamana kwa makini zaidi kwa kitambo fulani.

“Unamfahamu?” nilimuuliza Asia huku nikimkazia macho.

“Kama namkumbuka hivi, ila sura yake inanijia na kutoka,” Asia alisema huku akiendelea kumtazama yule mwanadada.

Yule mwanadada akatafuta kiti akaketi huku akigeuka tena kumtazama Asia, kisha akaachia tabasamu pana na kuinuka akitufuata pale tulipoketi.

“Asia, umenisahau?” yule mwanadada aliuliza huku akiketi kwenye kiti karibu ya Asia.

Rehema akaachia tabasamu. “Sura naikukumbuka lakini umen’toka kidogo. Nikumbushe basi.”

“Miye Joyce.”

Asia akamtazama kwa makini na kuonesha kumkumbuka. “Joyce… Mgaya, siyo?”

“Ee… Joyce Mgaya. Si tulisoma darasa moja pale Kahama School au umesahau?”

“Ndiiiiyooo! Mtumeeee! Ndiyo uko hivi babu wee! Umekuwa bonge!” Asia alisema kwa mshangao na kumfanya Joyce acheke sana huku akimshika Asia begani.

“Ndiyo hivyo tena! Nimeridhika mwenziyo!” Joyce alisema na kugeuza shingo yake kunitazama kwa umakini huku akiendelea kuangua kicheko cha kishambenga. Asia alitabasamu tu. Nilimtupia jicho la wizi Joyce hukunami nikitabasamu.

“Vipi, ndiye shemegi huyu?” Joyce alimuuliza Asia kwa bashasha huku akinikazia macho.

“We nawe! Hujaacha tu tabia yako! Hata hungoji kutambulishwa?” Asia alisema huku akigeuka kunitazama kisha akaachia tabasamu.

“Aa babu, ngoja ngoja yaumiza matumbo ati!”

“Ndiyo… ni shemeji yako mtarajiwa,” Asia alisema huku akinishika mkono wangu wa kushoto na kuviminyaminya vidole vyangu vya mkono.

Joyce akanyoosha mkono wake kwa bashasha kunisalimia. Na mimi nikanyoosha mkono wangu na kukutanisha na mkono wake. Tukasalimiana.

“Ooh shemegi, nimefurahi sana kukufahamu!” Joyce alisema kwa uchangamfu mno. Nikaachia tabasamu huku nikibetua kichwa changu bila kusema neno.

“Umeshaolewa, Joyce?” Asia alimuuliza Joyce huku akimtazama kwa makini.

“Hee! Zamani gani! Lile balaa lilipokwisha tu nikaolewa. Si uliyasikia yaliyonikuta mwenziyo baada ya kifo cha mama yangu?”

“Niliyasikia! Pole sana mwaya! Halafu nikasikia sakata lile lilikufanya ukalazwa hospitali. Ni kweli?”

“Kweli! Yule mama aling’ang’ania mpaka baba akanipeleka bila ya miye mwenyewe kupenda. Lakini sikukaa siku nyingi nikatoroka,” Joyce alisema na kuachia kicheko cha kishambenga.

“Lo! Pole sana, na yule kaka’ako… Michael, yuko wapi siku hizi?”

“Yupo zake Sauzi Afrika! Yule ndiyo basi tena, nasikia ana jimama la Kizulu linamlea!” Joyce alisema na kuachia tena kicheko cha kishambenga.

Waliendelea kuongea na kukumbushana mengi tangu walipoachana mara ya mwisho, wakati huo mimi nilikuwa kimya tu nikiwasikiliza. Joyce alikuwa mcheshi na mwongeaji sana, kiasi kwamba ilikuwa vigumu kumchoka.

* * *

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

109

Nilikuwa Nakutania!


Saa 12:00 jioni…

Nilikuwa nimetulia sebuleni nyumbani kwangu, juu ya sofa nikiwa nawaza sana hasa baada ya kuachana na Asia, kwani pamoja na juhudi zote za kumshawishi sana lakini aliendelea kusisitiza kuwa ni bora awe mbali nami. Pale sebuleni nilikuwa nimeweka chaneli ya Safari iliyoonesha vivutio vya utalii. Japo nilikuwa nimetulia na macho yangu yalikodolea kwenye runinga lakini ukweli sikuwa nikiona chochote kwenye ile runinga.

Muda wote nilikuwa namfikiria Asia tu na sikuweza kumtoa mawazoni. Sikujua nifanye nini ili kuurudisha moyo wake kwangu.

Mbele yangu juu ya meza ndogo ya kioo kulikuwa na chupa kubwa ya mvinyo mwekundu na bilauri moja. Nilikuwa nimeshakunywa robo na niliendelea kumimina pombe kwenye bilauri na kunywa kisha nikaikita ile bilauri juu ya meza huku nikisisimkwa.

Kijasho kilikuwa kikinitoka usoni, nikaijaza tena ile bilauri kwa kilevi na kuitazama kwa makini lakini kabla sijainywa nikasikia sauti ya mtu akigonga mlango wa mbele taratibu. Nilinyanyuka na kwenda kuufungua ule mlango kisha nikachungulia nje.

Asia alikuwa kasimama mbele yangu huku akiniangalia kwa wasiwasi jinsi ambavyo jasho lilikuwa linanitoka usoni kutokana na ule mvinyo niliokunywa. Alikuwa amevaa gauni fupi jepesi la rangi ya pinki lililohifadhi vema umbile lake na ndani ya lile gauni alivaa suruali ya buluu ya. Miguuni alikuwa amevaa sendozi ngumu za kike zilizotengenezwa kwa ngozi imara ya mamba.

Nilimkodolea Asia macho ya kilevi nikishangaa alifika pale muda gani maana sikuwa nimesikia muungurumo wa gari lake. Asia alinitazama kwa umakini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Kisha nikakumbuka jambo, nikampisha aingie ndani, bila kujivunga Asia aliingia sebuleni na kuketi kwenye sofa huku akinitazama kwa makini.

“Jason, unakunywa pombe?” aliniuliza kwa mshangao mkubwa.

Sikumjibu, niliinua tena ile bilauri nikaigida ile pombe yote na kuikita ile bilauri juu ya meza huku nikisisimkwa sana. Asia alitingisha kichwa chake kwa huzuni huku akiinuka na kuichukua ile chupa ya mvinyo na bilauri akaviondoa pale mbele yangu na kwenda kuviweka jikoni, kisha akarudi na kusimama akinitazama kwa wasiwasi.

“Kwa nini unakunywa pombe? Ni kipi kibaya nimekifanya hadi uchukue uamuzi huu wa kunywa pombe?” Asia aliniuliza huku akiendelea kunitazama kwa wasiwasi. Sikumjibu bali nilitulia tu kama sanamu huku nikimwangalia kwa matamanio.

Akiwa bado amezubaa akinitazama kwa mshangao niliinuka nikamshika na kumvutia pale juu ya sofa kisha nikapeleka mikono yangu na kuipapasa shingo yake. Asia aliendelea kunitazama, nikashusha mikono yangu na kuanza kumgusa matiti yake madogo yaliyosimama wima yakijitahidi kunidhihaki. Na yalifanikiwa hasa hasa kunikebehi.

Nikamgusa huku na kule akiwa ametulia tu akinitazama. Nilipotaka kumvua nguo akanizuia na alipogundua nilichokuwa nataka kufanya akagutuka na kujaribu kujitoa kwenye mikono yangu. Sikutaka kumpa nafasi, nikazidi kumng’ang’ania.

Nilikuwa nimekunywa pombe kiasi hivyo sikuwa na aibu, nikaamua kutumia nguvu, nia yangu ilikuwa kumbaka kama angeendelea kushikilia msimamo wake na kutoniruhusu kuzitoa nguo zake kistaarabu. Pepo mbaya wa ngono alikuwa amefanikiwa kuikamata nafsi yangu, sikutaka tena kungoja, nilitamani kuzirarua nguo zake ili nimbake kwani harufu nzuri ya manukato yake ilinishawishi kufanya ngono.

Nilihisi msisimko mkubwa wa mapenzi ukinitambaa mwilini mwangu na sasa mapigo yangu ya moyo yalikuwa yakienda mbio isivyo kawaida. Nilimtazama kwa uchu kama vile fisi atazamavyo mzoga. Ni kama alikuwa ameyasoma mawazo yangu, aliongea kwa sauti ya kubembeleza.

Jason please! Najua wewe ni mtu mzuri sana, naomba usifanye hivyo…” Asia alisema kwa sauti ya kubembeleza. “Ujue historia yangu si nzuri na hivyo haitokuwa vizuri kufanya mapenzi maana unaweza ukaja kujutia maisha yako yote.”

Nilishtuka sana kwa kauli ile ingawa sikutaka kuuonesha mshtuko wangu, nilimwangalia Asia kwa wasiwasi kidogo. Nikayaona macho yake yakimaanisha kile alichokuwa akikisema, ila sikujua alimaanisha nini.

“Usishangae, nimekupa tu angalizo maana naona unavyonishika shika mwenzio nina ugwadu wa miaka yote…” Asia alisema kwa sauti tulivu.

Nilitulia kidogo huku nikimwangalia kwa umakini ingawa kuna sauti fulani ndani yangu ilinihimiza nisimpe nafasi na nizirarue nguo zake. Ikajitokeza sauti nyingine ikinitaka nimsikilize kwanza kabla sijafanya lolote.

“Mmh, msichana mzuri kama wewe huwezi kuwa hujakutana na mwanamume, kwani huko hakuna wanaume?”

“Wapo ila ndo kama hivyo, mimi sijawahi tangu nizaliwe.”

“Mmh! Kwa hiyo njia bado haijafunguliwa?”

“Najua huwezi kuamini lakini huo ndiyo ukweli! Labda niseme hivi… naweza kukupa unachotaka kwa kuwa wewe ni mwanaume pekee uliyeuteka moyo wangu na kujikuta nikiwa mtumwa wa mahaba yako japo umeniumiza sana kihisia kwa kutembea na Jamila lakini sijaacha kukupenda…” Asia alisema kwa sauti dhaifu ya kinyonge huku akijitahidi kudhibiti donge la hasira ya wivu kooni mwake, na hapo hisia zangu zilinitanabaisha kuwa alikuwa msichana mwenye wivu mkubwa juu yangu.

“Ni kweli mimi bado bikira, sijawahi kulala na mwanamume yeyote kwa kuwa nina kasoro kubwa ambayo hainipi hadhi ya kulala kitanda kimoja na wewe… hivi unadhani mpapaso wako haunisisimui? Nasisimkwa sana na natamani nikutimizie kwa hiari kile unachotaka… pengine mimi ni muhitaji kuliko wewe mpenzi, lakini…” Asia alishindwa kumaliza, akajitupa kifuani pangu na kunikumbatia kisha akaanza kulia kwa uchungu.

Kilikuwa kilio cha dhati kabisa kilichotoka rohoni, ambacho aghalabu huisha chenyewe pindi uchungu unapopungua au kuisha kabisa. Kilio cha kwikwi! Machozi yake hayakuonesha ukomo na sasa yalikuwa yakimwagika kwa fujo na kunilowesha kifua changu. Mwili wake ulikuwa ukitikisika kutokana na kilio. Ni dhahiri Asia alishindwa kujizuia kulia.

Loh! moyo wangu ukaingiwa na ganzi na hali ile ilinitisha sana kwani sikutaraji kitu kama hicho kutokea. Maswali mengi nayo yalianza kupita ndani ya kichwa changu, nilijiuliza ni kipi kilichomfanya kulia kwa uchungu nkiasi kile? Je, ni kasoro ipi kubwa iliyokuwa ikimfanya asiwe tayari kulala na mimi?

Kwa mara ya kwanza niligundua kuwa moyo wangu ulikuwa umetekwa na mapenzi na sasa niliyaona mapenzi yakinivaa mzima mzima na kunifanya niugue, ubongo ukiwa hospitali na nafsi kwa Mungu.

Nafsi yangu ilianza kuzongwa na mawazo mengi juu ya mustakabali wangu na Rehema. Moyo wangu ulianza kusononeka sana baada ya kujikuta nikiwa njia panda, kati ya kuchagua niendelee na Rehema au nianzishe uhusiano mpya na Asia!

Huku nikijiuliza ningeanzaje kumwacha Rehema na kuwa na Asia, na je, maisha yangu yangekuwaje? Vipi kama Rehema angegundua kuhusu uhusiano wangu na Asia nini kingetokea?

Hatimaye kilio cha Asia kilipungua taratibu na sasa ilibakia ile hali ya kuweweseka. Hapo ndipo nilipoanza kumbembeleza na kumtamkia maneno yote mazuri na ya kumfariji. Ilimchukua muda, Asia kujikusanya pamoja ili aweze kurudi katika hali ya kawaida, kisha akainua uso wake kuniangalia.

“Jason…”

“Naam Asia.”

“Nakupenda sana kutoka moyoni na ninapenda uishi miaka mingi…”

“Mimi pia nakupenda…”

“Hapana, wewe hunipendi ila unanitamani,” Asia alisema kwa sauti ya kinyonge iliyobeba uchungu.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

110

“Usiseme hivyo Asia, nakupenda na nitakupenda hadi kifo kitakapotutenganisha,” niliongea kwa utulivu huku nikiruhusu tabasamu langu kuchanua usoni.

“Unanidanganya Jason, unachofanya ni kunifariji kama mtoto. Kwa kweli nafsi yangu inajuta kukufahamu. Umeuteka moyo wangu na sasa nashindwa kabisa kukuacha.”

“Nakuhakikishia kuwa nipo tayari kwa lolote mpenzi. Wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu,” niliongea huku nikizichezea nywele zake na hapo nikaona tabasamu hafifu likichanua usoni mwake.

“Kweli mpenzi?” Asia aliniuliza huku akiniangalia machoni. Sasa tabasamu liliupamba uso wake.

“Kweli kabisa nakuhakikishia,” nilimhakikishia.

“Lakini tuna tofauti kubwa, mimi ni Muislamu na wewe ni Mkristo, sasa tutaoana vipi?” Asia alisema. Nikafikiria kidogo.

“Vyovyote utakavyopenda wewe, ikiwa Kiserikali, Kikristo na hata Kiislamu pia… niko tayari kubadili dini kwa ajili yako!” nilisema kwa kumaanisha. Hata hivyo bado kauli yake kuwa alikuwa na kasoro kubwa iliyomfanya asiwe tayari kulala na mimi ilizidi kuniumiza kichwa, nikaona nimalize utata.

“Asia, sasa naomba uniambie ukweli… kwa nini hauko tayari kulala na mimi?”

Asia alionesha kushituka na uso wake ulionesha maumivu kiasi fulani. Tabasamu lililokuwa limetawala likayeyuka ghafla. Alibaki akiniangalia kwa kitambo kirefu akionekana kujishauri. akijaribu kutabasamu, alitaka kuendelea lakini hakufanya hivyo. Ilimchukua muda kujikusanya pamoja ili aweze kunieleza yaliyomsibu.

“Kwa kweli hata sijui nianzie wapi kukueleza… lakini kwa kifupi ni kwamba, nimekuwa nikiishi na Virusi vya Ukimwi kwa muda mrefu baada ya kuambukizwa na wazazi wangu…” Asia alisema sauti ya unyonge.

Habari ile ilikuwa kama pigo la kisu ambalo lilipenya mwilini na kuujeruhi moyo wangu. Nilishtuka sana na moyo wangu ulipiga mshindo mkubwa kama uliotaka kupasuka kwa mshtuko. Masikio yangu hayakuamini kile ambacho yalikuwa yakikisikia na ubongo wangu uligoma kabisa kukubaliana na kile nilichokisikia toka katika kinywa na Asia.

Jambo hilo lilikuwa kubwa mno na nilishindwa kulibeba kabisa. Nililiona jahazi la mapenzi yetu likienda mrama na mimi kama nahodha nilikuwa sina uwezo wa kulinusuru toka katika gharika lile kubwa.

“Jason, Wazazi wangu walishindwa kufuata taratibu za kiafya hasa ukizingatia kuwa kipindi kile bado wanasayansi walikuwa hawajagundua mbinu mbadala za kumfanya mtoto asipate maambuikizi ya ukimwi. Nilizaliwa nikiwa na virus vya ukimwi, na mama yangu kabla ya kufa alinikanya kuwa ni heri nife peke yangu kuliko kuua yeyote asiyekuwa na hatia ndiyo maana pamoja na kuwa nakupenda sana lakini nimekuwa nikisita kulala na wewe…” Asia alisema huku akiniangalia usoni.

Nilivuta pumzi ndefu kisha nikazishusha taratibu. Jasho jepesi lilikuwa likinitoka mwilini na mapigo yangu ya moyo yalikwenda kasi sana. Hata hivyo nilijikuta nikimhurumia sana Asia.

“Nakupenda sana Asia, nakupenda kutoka ndani ya moyo wangu japo umeniambia unaishi na virusi vya ukimwi, lakini tambua si mwisho wa maisha yako. Bado kuna mambo mengi ambayo tunaweza kufanya bila kuathiri maisha yetu,” nilimwambia Asia kwa sauti tulivu lakini iliyobeba huzuni kubwa ndani yake. Machozi yalikuwa yananilengalenga machoni.

“Lakini kwa tatizo langu sina hadhi ya kulala kitanda kimoja na wewe…” Asia alisema kwa huzuni, nikamkatisha.

“Hapana, usiseme hivyo. Ungekuwa huna thamani kwangu nisingekuwa na wewe muda huu. Ni kwa sababu una thamani ndiyo maana unaona niko na wewe…” nilimwambia Asia kwa sauti tulivu.

“Unachokifanya sasa ni kunipa moyo tu. Hilo tu basi! Si zaidi ya hivyo,” Asia alisema kwa huzuni.

“Nikuombe kitu?” nilimuuliza huku nikimtazama moja kwa moja machoni.

“Ndiyo.”

“Naomba uniruhusu nikuoe, najua kuwa tukifuata ushauri wa kitaalamu tutaishi vizuri kama…”

“Jason!” nilikatishwa na sauti kali ya Jamila iliyotushtua sote, mimi na Asia, wakati tukiwa bado tumekumbatiana pale kwenye sofa tukipeana faraja.

Nikainua kichwa na ghafla nikakutana na kitu ambacho sikukitarajia kabisa. Jamila alikuwa amesimama mlangoni na alikuwa akitusogelea taratibu na kisha akasimama hatua kadhaa toka mahala tulipokuwa tumeketi kwenye sofa. Mkononi kwake alikuwa ameshika bastola. Sikujua aliitoa wapi na alikuwa amefika hapo muda gani.

“Jamila!” niliita kwa mshangao.

Asia naye alimwona na kunitazama, tukatazamana pasipo kusema chochote. Muda huo Jamila alikuwa anatetemeka kwa hasira.

Jamila please… huhitaji kufanya hivyo tunaweza kuzungumza…” Asia alisema kwa sauti ya kutetemeka.

Shut up! Nakuheshimu sana Asia na usitake nikufanyie kitu ambacho hutakisahau… tena usinieleze upumbavu wako wowote la sivyo nitaanza na wewe,” Jamila alisema kwa ukali kisha akaikoki bastola yake na kuielekeza kwa Asia.

“Jamila hebu acha utani na silaha za moto,” nilisema kwa sauti tulivu katika namna ya kumsihi Jamila. Hata hivyo macho yake hayakuonesha masihara hata kidogo.

“Nakujua vizuri Jamila, najua wewe si muuaji na huwezi kuniua, tafadhali weka bastola chini,” niliendelea kumsihi Jamila.

“Unanijua vizuri eh? Kwa taarifa yako huujui upande wangu wa pili… sasa leo nitakuonesha mimi ni nani!” Jamila alisema kwa hasira huku akiihamishia bastola yake kwangu, midomo ilikuwa inamtetemeka kwa hasira.

“Jamila tafadhali naomba upunguze hasira unaweza kufanya kitendo ambacho utakijutia maishani mwako. Tafadhali punguza hasira na uiweke chini bastola yako tuongee…” nilijitahidi kumsihi Jamila.

“Hakuna tena kitu cha kuongea mimi na wewe Jason. Umekwisha nionesha wazi kwamba mimi na wewe tumefikia mwisho bila hata kujali kama nimebeba mtoto wako tumboni. Hakuna kitu tunachoweza tukaongea tena. It’s over Jason… it’s over!” Jamila aliongea huku machozi yakimtoka, ni wazi alikuwa ameumia sana moyoni.

“Una roho ya kikatili sana Jason, pamoja na kujiweka wazi kwako bado umeamua kunigeuka na kunitupa kama takataka! Nimeumia sana kiasi ambacho sikutegemea. Maisha yangu yote niliyakabidhi kwako na sioni kama kuna sababu ya kuendelea kuishi hapa duniani bila ya kuwa na wewe…” Jamila alisema huku machozi yakiendelea kumtiririka.

Sasa aliishika vyema bastola yake na kuielekeza kwenye kichwa changu huku kidole cha shahada kikielekea kwenye triga tayari kufyatua risasi.

“Jamila tafadhali acha utani, hiyo ni silaha za moto,” Asia alimwambia Jamila huku akipiga hatua za taratibu kumkaribia.

Stop! Unaona nafanya utani we malaya? Unaona kama nawatania eh?” Jamila alisema kwa ukali na mara akaielekeza bastola kwa Asia na mlipuko mkubwa ukasikika. Wote tukaanguka na kulala sakafuni. Baada ya nukta kadhaa nikafumbua macho yangu taratibu, pembeni yangu alilala Asia na damu nyingi zikimtoka.

“Shetani mkubwa wewe! How could you do this?” nilijikuta nikifoka kwa ghadhabu.

“Usihofu Jason. Hata wewe utamfuata malaya wako muda si mrefu,” Jamila alisema huku akiachia tabasamu la kifedhuli. Ni wazi alikuwa amechanganyikiwa maana alianza kucheka pasipo sababu. Kisha akanyamaza na kunitazama kwa macho makali yaliyojaa chuki huku akiukaza mkono wake kuielekeza bastola yake kwangu.

Hapo akili yangu ilianza kufanya kazi haraka. Nilimtazama kwa umakini machoni nikijaribu kuyasoma mawazo yake. Kufumba na kufumbua nikajinyanyua toka pale sakafuni na kumrukia lakini kabla sijamfikia nikashtukia kitu fulani cha moto mkali kikipenya kifuani kwangu na kunitupa sakafuni kwa kishindo kikubwa.

Nikajikuta nikiwa katikati ya maumivu makali sana yasiyoelezeka, nilianza kutetemeka kama niliyekumbwa na ugonjwa mbaya wa degedege. Maumivu makali yalinitawala katika kifua changu, nikajishika kwenye kifua na kugundua kulikuwa na damu zikinitoka, ikanibidi niukaze mkono wangu ili kuzuia damu nyingi isiendelea kuvuja katika sehemu ambayo risasi ilipita.

Jamila alinitazama kwa hofu, akawa kama aliyerudiwa na fahamu zake, akaanza kuweweseka huku akiwa haamini kwa tukio alilolifanya. Aliitupa bastola yake sakafuni na kunisogelea, akapiga magoti na kunikumbatia huku akiangalia kifuani kwangu kisha akaanza kulia kwa uchungu.

“Jason, nilikuwa nakutania! Tafadhali usiniache…” Jamila alisema huku akilia kwa uchungu, alionekana kuchanganyikiwa sana kwa kitendo alichokifanya. “I’m sorry Jason! Please forgive me!”

Mara mlango wa sebuleni kwangu ukapigwa kumbo na hapo nikasikia sauti ya vishindo vya watu waliokuwa wakija mbio pale sebuleni, niliinua uso wangu kuangalia nikaona watu watatu, wanaume wawili na mwanamke mmoja aliyewafuata kwa nyuma. Niliweza kumtambua yule mwanamke, alikuwa mchumba wangu Rehema na alivaa gauni zuri la kitenge na kilemba kichwani.

Oh My God! We binti umemuua Jason? Kwa nini umemuua Jason?” niliisika kwa mbali sauti ya Rehema akipiga ukelele.

Muda huo huo nikamwona Jamila akiniachia haraka na kuinuka huku akiwa ametahayari.

Taratibu nikahisi nguvu zikiniishia huku mwili ukizizima kwa kukosa uwezo wa kufumbua macho na hapo nikajikuta nikiwa katika hali nzito ambayo sikuwahi kuipata katika maisha yangu ikiutawala moyo wangu. Na mara giza zito likaanza kutanda kwenye mboni zangu za macho na mwili wangu ukilegea, mapigo yangu ya moyo nayo yakaanza kudorora, mwishowe nikahisi roho yangu ikifika njia panda.

“Wewe simama na usijaribu kupiga hata hatua moja! Wewee, hebu mkamate!” kwa mbali nikasikia sauti ya mwanamume ikisema kwa ukali.

“Jason! Jasoon! Jasoooon amkaaa!” kwa mbali sana niliisikia sauti ya Rehema akiniita huku akilia.

Nilitaka kuinuka lakini badala yake nikaanza kujiona nikitumbukia kwenye shimo refu sana lilikokuwa na kiza. Nilijaribu kupiga kelele za kuomba msaada lakini nilihisi sauti yangu haikuweza kutoka bali niliisikia akilini mwangu…

* * *

Mambo yanazidi kunoga. Endelea kuufuatilia mkasa huu wa kusisimua...
 
Dah! Ila inakatisha tamaa sana kutokana na mwitikio wa wasomaji humu, wanawaona wawili tu kama si watatu. Kuna
Dah! Ila inakatisha tamaa sana kutokana na mwitikio wa wasomaji humu, wanawaona wawili tu kama si watatu. Kuna wakati nafikiria kuikatisha...

nafikiria kuikatisha...
Usiikatishe boss wafuatiliaji mbona tupo??!
 
Back
Top Bottom