236
Aidha, aliongea kwa maneno na vitendo. Mara kwa mara mikono yake iliruka na kutua hapa na pale katika mwili wangu. Mara achezee vidole vyangu. Mara mkono utue na kutulia juu ya paja langu. Kama mwanamume rijali sikuwa na uwezo wa kustahimili hali ile na kama nisingekuwa makini nami ningejikuta pia nikiingia katika mchezo wa mikono, nikimshika hapa na pale.
Lakini sikutaka hali ile ijitokeze kwani akili yangu muda huo ilikuwa kikazi zaidi, nilifikiria kuhusu kazi ya kumsaka Rahma wa Singida na Abshir. Ilikuwa inaniuma sana kwa kuwa niliamini kuwa kwa namna moja au nyingine nilikuwa nimeshindwa kutimiza wajibu wangu.
Wakati Zuena akiendelea na mbwembwe zake mara wimbo wa taratibu wa mwanamuziki wa Marekani,
Mariah Carey uitwao
My All ukaanza kupigwa ukisisika kutoka katika spika zilizotundikwa maeneo fulani kwenye kona za ukumbi ule. Wimbo huo niliupenda sana kwa kuwa sauti tamu ya mwanamama huyo ilikuwa inanisisimua sana mwili.
Nikiwa natafakari kuhusu Rahma nikamwona Zuena akiigida pombe yote iliyokuwemo kwenye bilauri yake kama maji kisha akainuka na kunishika mkono. “
Can we go?” (Tunaweza kwenda?) aliniuliza.
“Wapi?” nilimuuliza kwa mshangao huku nikimtazama kwa umakini usoni.
“
Can we dance?” (Tunaweza kucheza?) Zuena aliniambia huku akiwa bado ameushika mkono wangu akinitazama usoni. “Twende tukacheze bwana.”
Ilinishangaza kuona kuwa pamoja na mwili wangu kusisimkwa na matarajio, roho yangu ilikuwa nzito sana. Hisia fulani za kijasusi, ambazo sikuweza kuzifafanua vizuri ziliashiria shari badala ya heri. Nikashusha pumzi.
“
Thinking of your wife?” (Unamfikiria mkeo?) Zuena aliniuliza huku akiendelea kunitazama usoni.
Nami nikamtazama usoni na kusema, “
I don’t have a wife.” (Sina mke).
Zuena akacheka huku macho yake yakienda moja kwa moja kwenye kidole changu cha mkono wa kushoto chenye pete ya ndoa kisha akauliza, “
What’s that ring for?” (Na hiyo pete ni ya nini?).
Nikayapeleka macho yangu kukitazama kidole changu chenye pete ya ndoa na kuachia tabasamu. Japo nilighafirika kidogo lakini sikutaka kuonesha mshtuko. Kisha tabasamu langu likageuka kicheko kidogo na wakati nikitaka kujieleza Zuena akawekea kidole chake cha shahada kwenye mdomo wangu kwa namna ya kunizuia nisiongee.
“
Never mind… it’s okay,” (Usijali… ni sawa) Zuena alisema huku akiangua kicheko. Na baada ya kile kicheko akanitazama tena machoni, “Kwa hiyo unasemaje, tunakwenda kucheza, au?”
“
I don’t feel like dancing,” nilimwambia huku nikimtazama usoni kwa udadisi.
Zuena alinitazama moja kwa moja machoni kisha akaangua tena kicheko. “Acha mzaha, Slim. Unajua… leo imetokea kama bahati tu kukutana na wewe… naweza kusema leo ni bahati ya pekee, kwa nini tusifurahie maisha!”
“Dah, kwa leo sijisikii kucheza, labda siku nyingine kwa kuwa bado upo,” nilisema kwa sauti tulivu.
Zuena akaachia tabasamu huku akijinyonga nyonga kwa mbwembwe na kulamba midomo yake katika namna ya kunivutia kimahaba. “Siku nyingine! Lini?”
“Hata kesho. Kwani kuna ubaya?” lilikuwa jibu langu.
“Daah! Kesho tutaonana wapi na saa ngapi? Natamani sana tupate wakati mzuri ili tufahamiane zaidi. Tumekutana na tumefahamiana juu juu tu, nafikiri kuna kila sababu ya kujuana kwa undani kidogo, kama hutajali,” Zuena aliniambia huku akirudi kuketi kwenye kiti. Alionekana kufadhaika kidogo.
Taaluma yangu ya ujasusi ilinifanya kuwa makini mno, niliamini kuwa kupanga muda ni kati ya makosa makubwa. Unaweza kuwa unashirikishwa kupanga muda wa kifo chako. Nikajifanya kufikiria kidogo kisha nikamtazama Zuena usoni, “Ratiba yangu ya kesho inaonesha kuwa mchana nitakuwa na shughuli nyingi, tuombe Mungu…” nilisema huku nikiinua mkono wangu wa kushoto kutazama saa yangu, nikajitia kushtuka kidogo.
“Inakaribia saa tano za usiku. Nikiendelea kukaa na wewe hapa tunaweza tukafika asubuhi.
It’s time to go now,” nilimwambia Zuena kwa sauti tulivu halafu nikainuka toka kwenye kiti. Sikutaka kuendelea kukaa pale maana zile hisia zilizoashiria shari badala ya heri ziliendela kunijia.
“Bado hujaniambia zilipo ofisi zako,” Zuena aliniambia huku akiinuka kisha kabla sijasema lolote akatoa simu yake. “Nipe basi namba yako ili nikutafute kesho kujua ulipo na ratiba zako.”
Niliitarajia kauli ya kuombwa namba na nilikuwa nimejiandaa kwa hilo, hivyo bila kusita nikamtajia Zuena namba zangu. Namba ambazo nilikuwa nimezisajili kwa kazi maalumu na kuziingiza kwenye mfumo maalumu wa kiulinzi uliozifanya zisiweze kudukuliwa au kutambuliwa na chombo chochote baada ya kuziwekea
msimbo fiche (
code number).
Ingekuwa vigumu sana kwa mtu mwingine kutambua mahali nilipo au hata kuingilia mawasiliano yangu. Kama mtu angejaribu kudukua mawasiliano yangu kwa siri asingefanikiwa kwa kuwa taarifa zake zilikuwa zinalindwa. Ingehitaji mtu awe mtaalamu aliyebobea mno kwenye masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano na mwenye ufahamu mkubwa sana wa masuala ya mawasiliano kuweza kuzifungua
code number hizo.
“Ahsante, kwa hiyo ofisi zako zipo wapi?” Zuena bado aling’ang’ana kutaka kujua zilipo ofisi zangu huku akizipiga zile namba katika namna ya kutaka kuhakikisha kama zilikuwa namba sahihi, na hapo hapo simu yangu ikaanza kuita mfukoni mwangu.
“Utakaponipigia kesho nitakuelekeza,” nilisema huku nikiitoa simu yangu toka mfukoni na kuzitazama namba za Zuena. Nikabetua kichwa changu kuonesha kuridhika halafu nikaanza kupiga hatua fupi fupi za kuondoka.
“Sawa, naamini bado tutakuwa na muda wa kutosha wa kuongea na kufurahi. Hakika leo nimefurahi sana.
I had a very great time with you,” Zuena alisema akinisindikiza kwa maneno wakati naondoka.
“Usijali,” nilisema kisha nikaongeza mwendo nikielekea kwenye lango la kutokea pale Lamada Hotel, nia yangu ilikuwa kwenda kulifuata gari langu kwenye kituo cha mafuta kilichokuwa ng’ambo ya pili ya Barabara ya Kawawa nilikoacha kwa sababu za kiusalama. Sikuwa nimeingia pale Lamada Hotel na gari langu.
Mara tu nilipotoka nje ya lile geti la Hoteli ya Lamada sikutaka kwenda moja kwa moja kule nilikokuwa nimeegesha gari langu, bado hisia mbaya zilizoashiria shari badala ya heri ziliendela kunijia. Nikaamua kujipa tahadhari maana kwenye kazi ya ujasusi kila mtu kwako ni adui na hutakiwi kumwamini yeyote.
Hivyo mara tu baada ya kutoka nje ya lile geti la Hoteli ya Lamada nikashika uelekeo wa upande wa kulia nikawa naambaa ambaa na ukuta wa uzio wa ile hoteli ya Lamada nikitembea kwa mwendo wa tahadhari hadi mwisho wa uzio ule, huku mara kwa mara nikigeuka na kutazama nyuma kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia. Niliwaona watu kadhaa wakitembea lakini sikumwona mtu yeyote niliyehisi kuwa alikuwa akinifuatilia, hivyo niliamini hali ilikuwa shwari.
Nilipofika mwisho wa ule ukuta nikasimama kutathmini hali ya usalama wa eneo lile na niliporidhika nikakata kulia kuufuata Mtaa wa Mafao uliokuwa na mwanga hafifu ukiwa unapita kando ya maghorofa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kanda ya Ilala. Kisha nikachepuka na kuvuka barabara upande wa pili. Nikiwa upande ule wa pili wa ile barabara nikaendelea kutembea kwenye barabara ile yenye mwanga hafifu huku nikimtafakari mwanamke huyo aliyejitambulisha kwangu kama Zuena wa Mombasa.
Nilijikuta nikimweka Zuena wa Mombasa kundi moja na Rahma wa Singida. Sikujua kwa nini nilifanya hivyo lakini hisia zangu ziliniambia hivyo! Hata nilipozidi kujiuliza bado jibu sikulipata ila hisia zangu ziliniambia kuwa kwa kumfuatilia Rahma wa Singida nilikuwa nimejiingiza kwenye mkasa hatari.
Niliendelea kutembea kando ya ile barabara hadi nilipojikuta nimetoka kwenye barabara ya Uhuru iliyokatisha kutoka Buguruni kwenda mjini, eneo la Kituo cha Vijana cha Amana (AVC), hivyo nilipoifikia ile barabara nikaingia upande wa kushoto kuifuata barabara ya Uhuru huku nikiendelea kutembea kwa tahadhari na mara kwa mara nikawa nikigeuka na kutazama nyuma kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia.
Bado sikumwona mtu yeyote aliyeonesha kunifuatilia nyuma yangu, hivyo nikaendelea kuamini kuwa hali bado ilikuwa shwari. Nilizidi kuifuata ile barabara ya Uhuru na kulivuka jengo la Mafao linalomilikiwa na NSSF, lililokuwa upande wangu wa kushoto, na soko la Ilala Boma kwa upande wa kulia, nikazidi kunyoosha mbele hadi nilipofika kwenye jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Nikachepuka kuivuka Barabara ya Kawawa hadi upande wa pili wa soko la Mchikichini, nikawa naambaa ambaa na barabara ile nikitembea kando ya soko la Mchikichini kisha nikakata kuingia kulia nikiufuata mtaa mwingine uliokuwa ukielekea eneo la ndani la Mchikichini, kando ya maghorofa ya Mchikichini. Niliendelea kuwa makini nikimchunguza kila mtu niliyepishana naye au aliyekuwa akinijia nyuma yangu.
Niliuzunguka ule mtaa na kwenda kutokea kwenye kituo cha mafuta nilipoacha gari langu, na wakati nikilifikia lile gari nikachepuka kidogo na kujibanza kwenye kona moja ya ukuta wa kile kituo cha mafuta katika namna ya kuchunguza hali ya usalama wa eneo lile na niliporidhika kuwa hali bado ilikuwa shwari nikaelekea kwenye gari langu kwa tahadhari huku mkono wangu wa kushoto ukiwa umekikamata vyema kilimi cha bastola yangu kwenye mfuko wa koti langu tayari kukabiliana na rabsha yoyote ambayo ingejitokeza eneo lile.
Hatimaye nikalifikia gari langu na baada ya kulizunguka kidogo kukagua usalama wake na kuridhishwa nikamfuata mlinzi wa kituo hicho cha mafuta na kumpa noti ya shilingi 2,000 kama asante kisha nikafungua mlango wa dereva na kuingia mle ndani. Bila kupoteza muda nikawasha gari na kuondoka eneo lile huku mawazo mengi juu ya Rahma wa Singida, na Zuena wa Mombasa, yakipita kichwani mwangu.
* * *
Inaendelea...