Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Mkuu wangu kwanza nashukuru sana kwa heshma umoja na amani ulionipa,.japo kama utaamua kutubariki hata sasa tupo tayari tuuu...wako mtiifu
Leo n'takuongopea, sina access ya stori maana hapa natumia simu wakati stori zipo kwenye computer ambayo sitembei nayo. Vumilieni tu hadi keshokutwa...
 
ufukweni mombasa.JPG

233

Rahma wa Singida…




Saa 6:30 mchana…

MCHANA huo ulinikuta nikiwa naliegesha gari langu kwenye eneo maalumu la maegesho ya magari ng’ambo ya pili ya barabara mkabala na jengo la Benki ya NBC makao makuu, eneo la Posta baharini. Nililiegesha gari langu jirani kabisa na gari moja la kifahari aina ya Range Rover SV Autobiography LWB la rangi nyeusi lililokuwa na vioo vyeusi visivyomruhusu mtu kuona waliomo ndani nililolikuta hapo.

Kisha nikateremka na kukatiza barabara kuelekea kwenye ngazi za baraza ndefu ya jengo la benki hadi kwenye mlango wa kuingilia ndani ya Benki ya NBC. Mlango ule ulikuwa mkubwa wa vioo.

Nikiwa kwenye ile baraza kabla sijaufikia mlango mkubwa wa vioo wa kuingilia ndani ya lile jengo la benki niliwaona askari wawili wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) wakiwa wamesimama kikakamavu na mkononi wamebeba bunduki aina ya SMG. Nikawasalimia na wakati huo huo nikazidisha hatua nikielekea ulipo ule mlango mkubwa wa kioo.

Wakati najiandaa kuingia ndani mwanamke mmoja aliyekuwa anatoka kwa mwendo wa haraka huku macho yake yakiwa kwenye karatasi alizozishika mkononi akanigonga, na karatasi zake zikaanguka na kutawanyika pale sakafuni.

Alikuwa mwanamke mwenye asili ya Kiarabu, kwa makadirrio tu umri wake ulionekana kuwa kati ya miaka 30 na 35, alikuwa amevaa vazi refu jeusi la aina ya abaya (baibui). Miguuni alivaa makubazi mazuri ya kike ya ngozi halisi. Alikuwa mrefu na macho yake yalikuwa mazuri na pua yake ilikuwa ndogo ya kihabeshi iliyopendezeshwa kwa kipini cha dhahabu. Kifua chake kilibeba matiti imara na nywele zake zilikuwa ndefu nyeusi zilizolalia mabegani.

“Samahani, bibie,” nilisema haraka katika namna ya kumwomba msamaha kama vile kosa la kumgonga lilikuwa langu. Wakati huo mwanamke huyo alikuwa ameinama akiziokota haraka haraka karatasi zake na alipoinua uso wake kunitazama, macho yake na yangu yakagongana.

Haraka sana, kwa macho ya kijasusi, nikagundua kuwa macho yake mazuri yalikuwa yameficha ghadhabu, na zaidi yalikuwa yameficha kitu kama dharau na jeuri. Yalikuwa ni macho ya mtu ayenata, mtu anayeamini kuwa yeye ni mtu bora kuliko wengine na anaweza kupata chochote akitakacho au kufanya lolote apendalo. Kwa sekunde kadhaa nikajikuta nikiganda, macho yangu nikiwa nimeyafinya na mdomo ukiwa nusu wazi kwa mshangao na mshituko.

Sura yake ilijaa machoni kwangu na sikutaka kujiuliza mara mbili kama nilikuwa namfahamu mwanamke au la kwani nilijikuta nikiwa natazamana uso kwa uso na Rahma wa Singida, mwanamke ambaye rafiki yangu Majaliwa Nzilwa alinikutanisha naye katika eneo la Chemchem mjini Tabora – kama ilivyowahi kuandikwa kwenye mkasa wa ‘Safari ya Buzwagi’. Kila nilivyomtazama mwanamke huyu sura ya Rahma ilizidi kujaa machoni kwangu.

Ndiyo… nilikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kuwa huyu alikuwa ndiye Rahma wa Singida kama ambavyo kumbukumbu zangu zilinijia. Mwanamke ambaye nilimchukua usiku na kwenda kulala naye nyumbani eneo la Ng’ambo lakini nilipoamka asubuhi nikawa sikumbuki chochote! Kwa mshtuko nilioupata nikajikuta nikimuuliza kwa sauti ambayo nilihisi haikuwa yangu, “Wewe si Rahma wa Singida?”

“Nani?” yule mwanamke aliuliza. Ingawa aliuliza kijeuri lakini uso wake ulikwisha mbadilika ghafla. Uso ulionekana kumwiva na alikuwa akipumua kwa nguvu. Macho yake yaliingiwa na kila dalili ya mshtuko. Na hapo nikagundua kuwa mshituko wake ulikuwa mkubwa zaidi kuliko wa kwangu.

Ingawa tulitazamana kwa nukta zisizozidi tatu lakini ilikuwa kama vile tulikuwa tumetazamana kwa muda mrefu zaidi. Bado akili yangu iliniambia kuwa mwanamke huyo aliyekuwa amesimama mbele yangu ni Rahma wa Singida.

“Wewe ni Rahma wa Singida…” nilisema lakini yule mwanamke akanikatiza.

“Mimi si Rahma,” yule mwanamke alisema huku akiwa amekunja uso wake kisha akaongeza, “Utakuwa umenifananisha.” Halafu akaondoka haraka toka eneo lile pasipo hata kugeuka nyuma.

Nilibaki nimeduwaa pale mlangoni huku nikimsindikiza kwa macho mtu niliyemdhania kuwa ni Rahma wa Singida akiondoka kwa hatua ndefu na za hima. Kitendo kile kikafanya kengele ya hatari kugonga kichwani mwangu, nikaingiwa na hamu ya kutaka kufahamu yaliyojificha nyuma ya pazia kumhusu mwanamke huyo. Mlango wa sita wa fahamu ukaibua hisia za kishushushu ndani yangu na sikutaka kuzipuuzia, hivyo nikasubiri nione angeelekea upande upi ili nimfuate pasipo yeye kujua.

Nikamwona akivuka haraka barabara na kuelekea upande wa pili kwenye maegesho ya magari, halafu akaingia kwenye lile gari la kifahari aina ya Range Rover SV Autobiography LWB la rangi nyeusi lililokuwa limeegeshwa kando ya gari langu. Kwa kuwa alikuwa ameingia kwenye mlango wa nyuma wa lile gari nikawa nimegundua kuwa ndani ya lile gari kulikuwa na mtu au watu wengine wakimsubiri.

Nikiwa bado natafakari hatua za kuchukua nikaliona lile gari likianza kuondoka kwa mwendo wa taratibu likiifuata barabara ya Nnamdi Azikiwe likielekea upande wa Posta Mpya. Sikuwa na muda zaidi wa kupoteza hivyo nikaharakisha kwenda lilipokuwa gari langu na nilipofika nikafungua mlango na kuingia. Muda mfupi baadaye nikaanza safari ya kulifuatilia lile gari aina ya Range Rover jeusi.

Kumfuatilia mtu pasipo kumpa nafasi yoyote ya kunitilia mashaka ilikuwa
moja ya mambo niliyokuwa nimefuzu chuoni na hivyo niliamini kuwa ni jambo ambalo nililimudu vizuri, nikaamua kuliacha lile gari aina ya Range Rover litangulie mbele yangu kwa umbali fulani na hapo nikaanza kazi yangu. Mara nikaliona lile gari likifika pale kwenye mzunguko wa barabara za Nnamdi Azikiwe na Samora, kwenye sanamu ya askari, na kuchepuka kuingia upande wa kushoto likiifuata Barabara ya Samora.

Nami nikakunja kuifuata barabara ile, na baada ya kitambo kirefu kidogo cha safari ile tukaufukia mzunguko mwingine ulioziunganisha barabara za Samora, Uhuru, Nkrumah na Stesheni, kwenye mnara wa saa, nikaliona lile gari likinyoosha kuifuata barabara ya Nkrumah likikatisha katikati ya majengo ya ghorofa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Nikaendelea kulifuata huku nikiyaacha magari matatu katikati yetu nikiwa nimeridhika kuwa waliokuwemo kwenye lile gari aina ya Range Rover mbele yangu hawakuwa wameshtukia chochote kuwa nilikuwa nikiwafuatilia kwa nyuma. Wakati naendesha nilijitahidi vizuri kuidhibiti miguu yangu kwenye pedeli za breki na mafuta, nikipunguza mwendo na kuongeza kila pale nilipohitajika kufanya hivyo.

Hatimaye tulitokea kwenye taa za kuongozea magari barabarani, lile gari likaendelea kuifuata barabara ile ya Nkrumah likizidi kukatisha katikati ya majengo ya Shirika la Nyumba la Taifa. Foleni ya magari iliyokuwa kwenye barabara ile ya Nkrumah ilikuwa inaninyima uhuru wa kuifanya kazi yangu kwa starehe na hapo nikaanza kuvunja sheria kadhaa za barabarani katika kuhakikisha kuwa lile Range Rover mbele yangu halinipotei machoni mwangu.

Hata hivyo umbali huo baina yangu na gari lile aina ya Range Rover haukunisumbua sana. Nilikwishazisoma namba za gari hilo. Hali kadhalika, niliweza kuona vizuri hatua zote ambazo dereva wa gari hilo alikuwa akizichukua kama kuongeza mwendo, kulipita gari lingine au kupinda kona kabla hata ya dereva huyo hajafanya hivyo. Pengine kilichokuwa kikinisumbua wakati huo ni hatua yangu hii ya kuamua kumfuatilia mwanamke huyo niliyemtambua kama Rahma wa Singida kwa sababu tu alionesha mshtuko mkubwa aliponiona!

Ya nini kumfuatilia mtu ambaye hana kosa na huna uhakika kama ni mhalifu kisa tu kashtuka baada ya kukuona? Nilijiuliza. Kisha, nikajicheka kimoyomoyo nilipokumbuka usemi wa mwanamke wa Kiingereza kuwa; “Never marry a Cop”. Yaani usilogwe kuolewa na mpelelezi kwani akikosa mtu wa kumshuku kwa uhalifu ataanza kukushuku hata wewe mwenyewe.

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

134

Wakati huo lile gari aina ya Range Rover lilikuwa linavuka kwenye daraja mtambuko la reli ya kisasa (SGR) katika eneo la Goldstar, eneo ambalo kulikuwa na vurugu za magari hususan daladala, niliendelea kuwa makini zaidi, na wakati nikivuka eneo lile la Goldstar nikaliona lile gari aina ya Range Rover likiwa linafika kwenye taa za barabarani za kuongozea magari katika makutano ya barabara za Nyerere, Msimbazi, Nkrumah na Gerezani.

Kwa kuwa pale kulikuwa na askari wa usalama barabarani akiyaruhusu magari yaliyokuwa yakitoka Barabara ya Nkrumah kupita na hivyo lile gari likavuka likizidi kusonga mbele kwenye Barabara ya Nyerere. Sasa mbele yangu kulikuwa na magari manne, na bahati nzuri sote tukavuka pale kwenye taa baada ya askari wa usalama barabarani kuturuhusu, hivyo nami nikanyoosha kuifuata barabara ile ya Nyerere huku nikiwa bado sijalipoteza lile gari.

Tulisafiri kwenye barabara ile ya Nyerere hadi pale tulipoyafikia makutano ya barabara za Nyerere, Kawawa na Chang’ombe nikaliona lile gari likikunja kulia kuifuata Barabara ya Kawawa, wakati huo huo magari mawili kati ya yale manne yaliyokuwa mbele yangu nayo yakakunja kuifuata Barabara ya Kawawa. Nami nikakunja kuingia barabara hiyo nikizidi kulifuata lile gari.

Kwenye ile Barabara ya Kawawa kulikuwa na foleni kubwa zaidi ya magari, hivyo sote tukajikuta tukienda mwendo mdogo hadi tulipofika kwenye taa za kuongozea magari barabarani za Ilala Boma tukasimama kusubiri taa zituruhusu. Na baada ya kitambo fulani taa zilituruhusu, nikaliona lile gari likinyoosha kuifuata Barabara ya Kawawa huku gari moja kati ya yale mawili yaliyotutenganisha likiingia kushoto kuifuata Barabara ya Uhuru.

Niliendelea kulifungia mkia lile gari, hata hivyo hatukwenda mbali sana mara nikaliona likipunguza mwendo na kisha likachepuka na kuingia upande wa kushoto na kwenda kusimama mbele ya geti la kuingilia Lamada Hotel and Apartments. Sikutaka wale watu wanishtukie kwa wepesi dhamira yangu na hivyo nikaongeza mwendo na kuendelea mbele na safari kama mtu niliyekuwa kwenye hamsini zangu lakini nikiwa makini kulitazama lile gari wakati likiingia ndani ya uzio wa hoteli ile ya Lamada, na nilipofika mbele kidogo kablaa sijalifikia geti la kuingilia Msimbazi Center nikasimama na kuliegesha gari langu kando ya barabara ile ya Kawawa, kisha nikashuka na kuharakisha kurudi kule Lamada Hotel and Apartments.

Nilipofika pale kwenye geti la kuingilia Lamada nikaingia huku nikiwa makini kutazama huku na kule, na hapo nikaliona lile gari aina ya Range Rover SV Autobiography LWB nililokuwa nimelifungia mkia likiwa limeegeshwa mbele ya apartment mojawapo ya jengo la Lamada Hotel and Apartments lenye nyumba nyingi za kupanga. Na wakati huo Rahma wa Singida alikuwa amesimama kando karibu na lango la kuelekea kwenye ngazi akimsubiri mwanamume mmoja mrefu, ambaye kwa mtazamo wa haraka tu niliweza kubaini kuwa alikuwa na asili ya Kisomali, akiwa amesimama kwenye dirisha la dereva na walikuwa wakiongea.

Kisha yule mwanamume wa Kisomali akaagana na yule dereva na kumfuata Rahma wa Singida mahali aliposimama, wakashikana mikono na kuanza kutembea taratibu na kwa utulivu kuelekea kwenye ngazi za lile jengo lililokuwa mbele yao. Hawakuonekana kuwa na mashaka yoyote kwani macho yangu ya kishushushu yalikuwa makini yakizikagua vizuri nyendo zao. Walipanda hadi orofa ya pili na kupotelea kwenye orofa (apartment) ya kwanza ya lile jengo, wakati huo lile gari aina ya Range Rover SV lililowaleta lilikuwa linaondoka.

Nililitazama vizuri lile gari wakati likiondoka lakini sikuwa na haja tena ya kulifuatilia kwa kuwa shida yangu ilikuwa kumpata Rahma, pia nilikwisha zikariri vizuri kichwani mwangu namba za gari hilo. Nikageuka kutazama kule kwenye orofa waliyoingia Rahma wa Singida na yule mwanamume wa Kisomali huku nikijiuliza endapo nibaki eneo lile niendelee na harakati zangu za kumpeleleza Rahma wa Singida au niachane na mpango huo kwanza ili nije pale wakati mwingine.

Hatimaye nikajiambia kuwa nilipaswa kuwa mvumilivu endapo ningetaka mambo yangu yafanikiwe. Hivyo nilisimama kidogo huku nikiyatembeza macho yangu eneo lile katika namna ya kuzikariri vizuri kichwani mwangu namba za orofa waliyoingia Rahma wa Singida na yule mwanamume wa Kisomali, ili pindi nikirudi kwa mara nyingine nisiwe mgeni.

Nilipojitosheleza na kumbukumbu nzuri iliyojengeka kichwani mwangu nikageuka na kuanza kuondoka taratibu eneo lile nikipanga kurudi tena jioni.

* * *



Saa 2:30 usiku…

Nilikuwa nimeketi peke yangu kwenye meza ya pembeni kabisa kwenye eneo maalumu la baa ya Lamada Hotel. Pale baa kulikuwa na wateja wachache walioketi kwa utulivu kwenye meza na wahudumu wachache wa kike, warembo kweli kweli, waliokuwa wanatuhudumia kwa vinywaji.

Eneo lote lilipendezeshwa sana na taa nzuri za rangi mbalimbali zenye mwanga hafifu na kulikuwa na runinga mbili pana zilizotundikwa ukutani moja ikiwa kona hii na nyingine kona ile na zilikuwa zimejikita katika kurusha matangazo ya mpira wa miguu wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Hata hivyo, sauti ya muziki laini wa kubembeleza unaoweza kuacha kumbukumbu ya muda mrefu kwa mtu yeyote baada ya kuondoka eneo lile ilisikika kutoka katika spika zilizotundikwa maeneo fulani kwenye kona za eneo lile na hivyo kuzikonga vizuri nyoyo za wateja waliokuwa pale.

Tangu nilipokaa pale kwa utulivu baada ya kutoridhishwa na ufuatiliaji wangu nilijikuta nikikosa raha kabisa. Ndiyo, Rahma wa Singida alikuwa amefanikiwa kunipiga chenga ya mwili na kupotea mithili ya moshi. Kutoweka kwake pale Lamada Hotel kabla sijampata kulinisononesha sana na ukimya wangu pale baa ulikuwa wa kujaribu kubashiri ni wapi angekuwa ameelekea baada ya kutoka pale Lamada Hotel.

Sehemu kubwa ya mchana wa siku hiyo nilikuwa nimeitumia katika kutengeneza hoja na kuunganisha nukta, nikianzia kule benki ya NBC Posta nilikokutana na Rahma wa Singida, jinsi alivyoonesha kushtuka sana baada ya kuniona na kuondoka haraka… nilivyomfuata hadi pale Lamada Hotel na niliporudi tena jioni nikakuta ameondoka.

Ndiyo, kwa kila hali Rahma wa Singida alikuwa mwanamke wa kawaida kabisa. Ni hisia zangu tu za kijasusi zilizoniambia kuwa macho yake yenye haya yalikuwa yameficha kitu, na hivyo, fikra zangu zikaniambia kuwa Rahma wa Singida alikuwa na jambo lenye kutia shaka ambalo isingekuwa busara kama ningeruhusu linipite. Jambo kubwa. Jambo ambalo kama nisipokuwa makini, nilijiambia, lingenipita. Na huo ulikuwa mwiko mkubwa kwa shushushu.

Kabla, nikiwa nimeketi pale kwenye eneo la baa katika Hoteli ya Lamada tangu saa kumi na nusu nilipofika, nilikuwa nakunywa bia taratibu lakini sikuwa nimemwona Rahma wa Singida wala yule mwanamume wa Kisomali. Niliendelea kuvuta subira hadi ilipofika saa 12:30 jioni hiyo nikaamua kwenda kwenye dawati la mapokezi ambapo nilipokewa kwa bashasha zote na msichana mmoja mrembo aliyeniweka kwenye kundi la watu mashuhuri kutokana na mwonekano wangu nadhifu wenye sura ya kirafiki.

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

235

Kwa kutumia mbinu za kijasusi nilifanikiwa kulifahamu jina la yule mwanamume wa Kisomali aliyekuwa na Rahma wa Singida baada ya kujitambulisha kwa msichana wa mapokezi kama jamaa yake, na sasa nilimfahamu kwa jina moja tu la Abshir. Yule msichana wa mapokezi alikuwa amebabaishwa na utanashati wangu na hivyo akajikuta akiyajibu maswali yangu ya mtego pasipo kuushirikisha ubongo wake, aliniambia kuwa Abshir na mwanamke wake walikuwa wamepata safari ya ghafla na wasingerejea tena pale.

Niliambiwa kuwa Rahma wa Singida na mwanamume wake wa Kisomali walikuwa wameondoka pale Lamada Hotel saa nane mchana – muda mfupi tu baada ya kurejea pale – japokuwa walikuwa wamepanga kukaa pale kwa muda wa wiki nzima na walilipa fedha zote lakini wakaishia kukaa siku mbili tu. Hakuna aliyejua walielekea wapi.

Baada ya maongezi mafupi na yule msichana wa mapokezi nikawa nimekuja na hitimisho moja kuwa Rahma wa Singida na Abshir walishafahamu kuwa nilikuwa nimewafuatilia hadi pale Lamada Hotel, ndiyo maana wakaamua kuhama na kwenda kusikojulikana.

Kwa kweli bado nilikuwa sijapata japo fununu ya nini alichokuwa akikifanya Rahma jijini Dar es Salaam, na sikufahamu Abshir alikuwa nani kwake maana nilifahamu kuwa mume wa Rahma alikuwa mzee mmoja mfanyabiashara wa Kiarabu aliyekuwa akiishi Singida. Hata hivyo sikuwa na ushahidi kamili wa shaka yangu kwani hisia zangu zilikuwa zimetawaliwa na viashiria tu.

Nikiwa bado nakunywa bia yangu kwa utulivu huku nikitafakari kwa kina nikahisi kulikuwa na mtu aliyekuja na kusimama mbele yangu, nikainua uso wangu kumtazama. Na hapo macho yangu yakakutana na macho ya msichana mmoja mzuri niliyemkadiria kuwa na umri wa miaka isiyopungua ishirini na tano na hakuzidi miaka therathini, alikuwa amejipulizia marashi mepesi yaliyofanya hewa iliyonizunguka ijae hisia za mahaba.

Alikuwa mweupe na uso wake uling’ara kwa aina fulani ya poda au mafuta aliyokuwa ameyatumia. Nywele zake ziliachiwa na kujimwaga hadi mabegani mwake, na hivyo kufanya suala la kujua kama alikuwa Mbantu, Chotara au Mwarabu liwe tatizo kidogo. Kilichohitimisha uzuri wake lilikuwa vazi lake. Alivalia vazi la jioni, gauni fupi laini la rangi ya bluu la kumetameta lililoishia juu ya magoti yake na kuufichua vilivyo ubora wa umbile lake refu. Miguuni alivaa viatu vya bluu vya flat visivyo na visigino, na alining’iniza mkoba mzuri wa bluu begani.

Nilipomtazama vizuri nikamwona akiwa ameshika chupa ya pombe kali aina ya John Walker na bilauri ndefu mkono wake wa kulia. Kwa namna ya mwonekano wake sikuona kama alikuwa na jambo lolote na kunifanya nimtilie sana maanani, hivyo sikuyatuliza sana macho yangu kumtazama, nikayahamisha toka juu ya umbo lake la kuvutia na kuitazama saa yangu ya mkononi, ikanionesha kuwa ilishatimia saa mbili na nusu usiku.

Saa nne zilikuwa zimekatika tangu nilipofika hapo Lamada Hotel kumfuatilia Rahma wa Singida. Nikajiuliza kama bado kulikuwa na haja ya mimi kuendelea kuwepo pale Lamada Hotel au niondoke zangu nirudi nyumbani nikapumzike.

Yule msichana alikuwa kama aliyeyasoma mawazo yangu. “Naona hujafurahishwa na ujio wangu,” alisema kisha akaongeza, “Samahani sana kama nimekuvurugia utulivu wako. Nilikuwa nimekaa pale hisia za upweke zikanibana nikashindwa kuvumilia. Ila kama vipi naweza kuondoka…”

“Usijali,” nilisema huku nikimkaribisha. “Karibu…”

Yule msichana akaketi kwenye kiti kilichokuwa jirani na kiti changu huku akinitazama kwa tabasamu na kisha akaamua kujitambulisha, “I’m Zuena Abdul,” aliniambia huku akinyoosha mkono wake kunipa.

“I’m Slim Kubanda,” nilijitambulisha bila wasiwasi kwa jina lisilo langu huku nami nikimpa mkono. Tuliposhikana mikono nikashangaa kuona mkono wake haukuwa legelege kama nilivyotazamia. Ulikuwa mkakamavu karibu sawa na mkono wa mwanamume.

Ooh, Mr. Slim! Jina zuri sana. Nafurahi mno kukufahamu,” Zuena alisema huku akiachia tabasamu. kisha akauliza, “Samahani lakini… wewe ni mkaazi wa hapa Dar es Salaam?”

“Haswa! Mimi ni mkaazi wa hapa hapa Dar es Salaam. Ninaishi eneo hili la Ilala, si mbali kutoka hapa. Je wewe unaishi wapi?” nilijibu pasipo kusita na hapo hapo nikamsaili huku nikimtazama moja kwa moja machoni kujaribu kuyasoma mawazo yake.

“Mimi makazi yangu ni Mombasa nchini Kenya. Hapa Dar es Salaam nimekuja kwa siku chache kwa ajili ya shughuli ya mitindo na mavazi inayoendelea katika Hoteli ya Golden Tulip. Nimekuja hapa Lamada kwa sababu nilitaka kubadilisha hali ya hewa na kutuliza kichwa,” Zuena alisema kwa mbwembwe huku akiyazungusha macho yake kwa maringo.

“Ooh! Kumbe unajishughulisha na masuala ya mitindo na mavazi?” niliuliza huku nikimtazama kwa umakini zaidi nikijifanya kuvutiwa naye.

“Ndiyo, ninajishughulisha na mambo ya ubunifu na mitindo kwa ujumla,” Zuena alisema kwa namna ya kujigamba.

“Nilipokuona nilijua ni lazima ungekuwa mwanamitindo,” nilisema na kumfanya atabasamu. “Unaionaje fani ya mitindo na mavazi hapa Afrika Mashariki hususan Kenya na Tanzania?” nikamuuliza tena.

Zuena alishusha pumzi za ndani kwa ndani, akamimina kidogo ile pombe aina ya John Walker katika bilauri halafu akanywa yote kisha akainua kichwa na kunitazama. Nilistaajabu kidogo, kwani kutokana na umbo lake na jinsi alivyo sikutegemea kama angeweza kutumia kinywaji kikali kama John Walker. Nikajikuta nikipatwa na shauku ya kutaka kumfahamu zaidi.

“Kwa hapa East Africa fani hii ya mitindo bado iko chini japokuwa kuna wanamitindo wazuri na wabunifu wazuri. Wenzetu Ulaya, au hata kule South Africa wamepiga hatua kubwa sana… lakini si mbaya tunazidi kupambana hadi kieleweke,” Zuena alisema huku akicheka kidogo.

“Nimefurahi sana kusikia hivyo, Zuena. Unajua hata mimi hapo awali nilikuwa na ndoto ya kuwa mbunifu ingawa baadaye nikajikuta naangukia katika fani ya upigaji picha… I’m a photographer,” niliongopa na kumfanya Zuena aachie tabasamu pana.

Ooh, are you a photographer! I thought you are a movie actor or something like that… maybe mwanamitindo or Bongo Fleva musician kwa jinsi unavyoonekana,” Zuena alisema kwa mshangao huku akinitazama usoni.

“Sijawahi kuigiza wala kuimba na sina ndoto hiyo. Actually, mimi ni mkurugenzi wa kampuni ya Capital Inc. inayojishughulisha na upigaji picha za matangazo yanayotangaza vivutio mbalimbali vya utalii katika nchi yetu. Hivyo kazi yangu ni kupiga picha, basi!” nilisema kwa mbwembwe na hapo nikamwona Zuena akiangua kicheko hafifu.

To be honest, I’m starting to like you. You’re so fun!” Zuena alisema huku akinitazama kwa namna ya kunihusudu zaidi, kisha akaongeza, “Nimefurahi sana kukutana na wewe… where is your office, I’d like to come there before I leave to Mombasa.”

You’re mostly welcome. Infact, tunadili zaidi na warembo na wanamitindo kama wewe,” nilimkaribisha pasipo kumweleza ilipo ofisi huku nikichombeza, na hapo nikamwona akijiweka vizuri kwenye kiti huku akinitazama kwa macho yaliyojaa shauku.

“Naweza kufaa kwenye kampuni yako?” Zuena aliuliza huku tabasamu usoni kwake likikataa kwenda likizo.

Why not? You’re sexy, brilliant and gorgeous,” niliongea nikizidi kumpamba Zuena. Wakati nikiyatamka yale maneno ya kumpamba nilimwona akiyazungusha macho yake kwa maringo katika namna ya kunithibitishia kuwa sijakosea, yeye ni mzuri.

Kisha tulianza kuongea mambo mengi kuhusu fani ya mitindo na mavazi huku nikijaribu kumpa ushauri wa namna ya kufanikiwa zaidi kwenye kazi yake. Zuena alianza kufunguka kuhusu changamoto za kazi yake na vishawishi walivyokuwa wanambana navyo toka kwa wanaume wabunifu na waandaaji wa matamasha ya mitindo. Katika maongezi yake aliingiza utani jambo ambalo lilinifanya nishindwe kujizuia kucheka. Alionekana mcheshi sana na mwongeaji mzuri, sikujua kama ilikuwa ni tabia yake au ni kwa sababu ya pombe alizokunywa.

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

236

Aidha, aliongea kwa maneno na vitendo. Mara kwa mara mikono yake iliruka na kutua hapa na pale katika mwili wangu. Mara achezee vidole vyangu. Mara mkono utue na kutulia juu ya paja langu. Kama mwanamume rijali sikuwa na uwezo wa kustahimili hali ile na kama nisingekuwa makini nami ningejikuta pia nikiingia katika mchezo wa mikono, nikimshika hapa na pale.

Lakini sikutaka hali ile ijitokeze kwani akili yangu muda huo ilikuwa kikazi zaidi, nilifikiria kuhusu kazi ya kumsaka Rahma wa Singida na Abshir. Ilikuwa inaniuma sana kwa kuwa niliamini kuwa kwa namna moja au nyingine nilikuwa nimeshindwa kutimiza wajibu wangu.

Wakati Zuena akiendelea na mbwembwe zake mara wimbo wa taratibu wa mwanamuziki wa Marekani, Mariah Carey uitwao My All ukaanza kupigwa ukisisika kutoka katika spika zilizotundikwa maeneo fulani kwenye kona za ukumbi ule. Wimbo huo niliupenda sana kwa kuwa sauti tamu ya mwanamama huyo ilikuwa inanisisimua sana mwili.

Nikiwa natafakari kuhusu Rahma nikamwona Zuena akiigida pombe yote iliyokuwemo kwenye bilauri yake kama maji kisha akainuka na kunishika mkono. “Can we go?” (Tunaweza kwenda?) aliniuliza.

“Wapi?” nilimuuliza kwa mshangao huku nikimtazama kwa umakini usoni.

Can we dance?” (Tunaweza kucheza?) Zuena aliniambia huku akiwa bado ameushika mkono wangu akinitazama usoni. “Twende tukacheze bwana.”

Ilinishangaza kuona kuwa pamoja na mwili wangu kusisimkwa na matarajio, roho yangu ilikuwa nzito sana. Hisia fulani za kijasusi, ambazo sikuweza kuzifafanua vizuri ziliashiria shari badala ya heri. Nikashusha pumzi.

Thinking of your wife?” (Unamfikiria mkeo?) Zuena aliniuliza huku akiendelea kunitazama usoni.

Nami nikamtazama usoni na kusema, “I don’t have a wife.” (Sina mke).

Zuena akacheka huku macho yake yakienda moja kwa moja kwenye kidole changu cha mkono wa kushoto chenye pete ya ndoa kisha akauliza, “What’s that ring for?” (Na hiyo pete ni ya nini?).

Nikayapeleka macho yangu kukitazama kidole changu chenye pete ya ndoa na kuachia tabasamu. Japo nilighafirika kidogo lakini sikutaka kuonesha mshtuko. Kisha tabasamu langu likageuka kicheko kidogo na wakati nikitaka kujieleza Zuena akawekea kidole chake cha shahada kwenye mdomo wangu kwa namna ya kunizuia nisiongee.

Never mind… it’s okay,” (Usijali… ni sawa) Zuena alisema huku akiangua kicheko. Na baada ya kile kicheko akanitazama tena machoni, “Kwa hiyo unasemaje, tunakwenda kucheza, au?”

I don’t feel like dancing,” nilimwambia huku nikimtazama usoni kwa udadisi.

Zuena alinitazama moja kwa moja machoni kisha akaangua tena kicheko. “Acha mzaha, Slim. Unajua… leo imetokea kama bahati tu kukutana na wewe… naweza kusema leo ni bahati ya pekee, kwa nini tusifurahie maisha!”

“Dah, kwa leo sijisikii kucheza, labda siku nyingine kwa kuwa bado upo,” nilisema kwa sauti tulivu.

Zuena akaachia tabasamu huku akijinyonga nyonga kwa mbwembwe na kulamba midomo yake katika namna ya kunivutia kimahaba. “Siku nyingine! Lini?”

“Hata kesho. Kwani kuna ubaya?” lilikuwa jibu langu.

“Daah! Kesho tutaonana wapi na saa ngapi? Natamani sana tupate wakati mzuri ili tufahamiane zaidi. Tumekutana na tumefahamiana juu juu tu, nafikiri kuna kila sababu ya kujuana kwa undani kidogo, kama hutajali,” Zuena aliniambia huku akirudi kuketi kwenye kiti. Alionekana kufadhaika kidogo.

Taaluma yangu ya ujasusi ilinifanya kuwa makini mno, niliamini kuwa kupanga muda ni kati ya makosa makubwa. Unaweza kuwa unashirikishwa kupanga muda wa kifo chako. Nikajifanya kufikiria kidogo kisha nikamtazama Zuena usoni, “Ratiba yangu ya kesho inaonesha kuwa mchana nitakuwa na shughuli nyingi, tuombe Mungu…” nilisema huku nikiinua mkono wangu wa kushoto kutazama saa yangu, nikajitia kushtuka kidogo.

“Inakaribia saa tano za usiku. Nikiendelea kukaa na wewe hapa tunaweza tukafika asubuhi. It’s time to go now,” nilimwambia Zuena kwa sauti tulivu halafu nikainuka toka kwenye kiti. Sikutaka kuendelea kukaa pale maana zile hisia zilizoashiria shari badala ya heri ziliendela kunijia.

“Bado hujaniambia zilipo ofisi zako,” Zuena aliniambia huku akiinuka kisha kabla sijasema lolote akatoa simu yake. “Nipe basi namba yako ili nikutafute kesho kujua ulipo na ratiba zako.”

Niliitarajia kauli ya kuombwa namba na nilikuwa nimejiandaa kwa hilo, hivyo bila kusita nikamtajia Zuena namba zangu. Namba ambazo nilikuwa nimezisajili kwa kazi maalumu na kuziingiza kwenye mfumo maalumu wa kiulinzi uliozifanya zisiweze kudukuliwa au kutambuliwa na chombo chochote baada ya kuziwekea msimbo fiche (code number).

Ingekuwa vigumu sana kwa mtu mwingine kutambua mahali nilipo au hata kuingilia mawasiliano yangu. Kama mtu angejaribu kudukua mawasiliano yangu kwa siri asingefanikiwa kwa kuwa taarifa zake zilikuwa zinalindwa. Ingehitaji mtu awe mtaalamu aliyebobea mno kwenye masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano na mwenye ufahamu mkubwa sana wa masuala ya mawasiliano kuweza kuzifungua code number hizo.

“Ahsante, kwa hiyo ofisi zako zipo wapi?” Zuena bado aling’ang’ana kutaka kujua zilipo ofisi zangu huku akizipiga zile namba katika namna ya kutaka kuhakikisha kama zilikuwa namba sahihi, na hapo hapo simu yangu ikaanza kuita mfukoni mwangu.

“Utakaponipigia kesho nitakuelekeza,” nilisema huku nikiitoa simu yangu toka mfukoni na kuzitazama namba za Zuena. Nikabetua kichwa changu kuonesha kuridhika halafu nikaanza kupiga hatua fupi fupi za kuondoka.

“Sawa, naamini bado tutakuwa na muda wa kutosha wa kuongea na kufurahi. Hakika leo nimefurahi sana. I had a very great time with you,” Zuena alisema akinisindikiza kwa maneno wakati naondoka.

“Usijali,” nilisema kisha nikaongeza mwendo nikielekea kwenye lango la kutokea pale Lamada Hotel, nia yangu ilikuwa kwenda kulifuata gari langu kwenye kituo cha mafuta kilichokuwa ng’ambo ya pili ya Barabara ya Kawawa nilikoacha kwa sababu za kiusalama. Sikuwa nimeingia pale Lamada Hotel na gari langu.

Mara tu nilipotoka nje ya lile geti la Hoteli ya Lamada sikutaka kwenda moja kwa moja kule nilikokuwa nimeegesha gari langu, bado hisia mbaya zilizoashiria shari badala ya heri ziliendela kunijia. Nikaamua kujipa tahadhari maana kwenye kazi ya ujasusi kila mtu kwako ni adui na hutakiwi kumwamini yeyote.

Hivyo mara tu baada ya kutoka nje ya lile geti la Hoteli ya Lamada nikashika uelekeo wa upande wa kulia nikawa naambaa ambaa na ukuta wa uzio wa ile hoteli ya Lamada nikitembea kwa mwendo wa tahadhari hadi mwisho wa uzio ule, huku mara kwa mara nikigeuka na kutazama nyuma kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia. Niliwaona watu kadhaa wakitembea lakini sikumwona mtu yeyote niliyehisi kuwa alikuwa akinifuatilia, hivyo niliamini hali ilikuwa shwari.

Nilipofika mwisho wa ule ukuta nikasimama kutathmini hali ya usalama wa eneo lile na niliporidhika nikakata kulia kuufuata Mtaa wa Mafao uliokuwa na mwanga hafifu ukiwa unapita kando ya maghorofa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kanda ya Ilala. Kisha nikachepuka na kuvuka barabara upande wa pili. Nikiwa upande ule wa pili wa ile barabara nikaendelea kutembea kwenye barabara ile yenye mwanga hafifu huku nikimtafakari mwanamke huyo aliyejitambulisha kwangu kama Zuena wa Mombasa.

Nilijikuta nikimweka Zuena wa Mombasa kundi moja na Rahma wa Singida. Sikujua kwa nini nilifanya hivyo lakini hisia zangu ziliniambia hivyo! Hata nilipozidi kujiuliza bado jibu sikulipata ila hisia zangu ziliniambia kuwa kwa kumfuatilia Rahma wa Singida nilikuwa nimejiingiza kwenye mkasa hatari.

Niliendelea kutembea kando ya ile barabara hadi nilipojikuta nimetoka kwenye barabara ya Uhuru iliyokatisha kutoka Buguruni kwenda mjini, eneo la Kituo cha Vijana cha Amana (AVC), hivyo nilipoifikia ile barabara nikaingia upande wa kushoto kuifuata barabara ya Uhuru huku nikiendelea kutembea kwa tahadhari na mara kwa mara nikawa nikigeuka na kutazama nyuma kama kungekuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia.

Bado sikumwona mtu yeyote aliyeonesha kunifuatilia nyuma yangu, hivyo nikaendelea kuamini kuwa hali bado ilikuwa shwari. Nilizidi kuifuata ile barabara ya Uhuru na kulivuka jengo la Mafao linalomilikiwa na NSSF, lililokuwa upande wangu wa kushoto, na soko la Ilala Boma kwa upande wa kulia, nikazidi kunyoosha mbele hadi nilipofika kwenye jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Nikachepuka kuivuka Barabara ya Kawawa hadi upande wa pili wa soko la Mchikichini, nikawa naambaa ambaa na barabara ile nikitembea kando ya soko la Mchikichini kisha nikakata kuingia kulia nikiufuata mtaa mwingine uliokuwa ukielekea eneo la ndani la Mchikichini, kando ya maghorofa ya Mchikichini. Niliendelea kuwa makini nikimchunguza kila mtu niliyepishana naye au aliyekuwa akinijia nyuma yangu.

Niliuzunguka ule mtaa na kwenda kutokea kwenye kituo cha mafuta nilipoacha gari langu, na wakati nikilifikia lile gari nikachepuka kidogo na kujibanza kwenye kona moja ya ukuta wa kile kituo cha mafuta katika namna ya kuchunguza hali ya usalama wa eneo lile na niliporidhika kuwa hali bado ilikuwa shwari nikaelekea kwenye gari langu kwa tahadhari huku mkono wangu wa kushoto ukiwa umekikamata vyema kilimi cha bastola yangu kwenye mfuko wa koti langu tayari kukabiliana na rabsha yoyote ambayo ingejitokeza eneo lile.

Hatimaye nikalifikia gari langu na baada ya kulizunguka kidogo kukagua usalama wake na kuridhishwa nikamfuata mlinzi wa kituo hicho cha mafuta na kumpa noti ya shilingi 2,000 kama asante kisha nikafungua mlango wa dereva na kuingia mle ndani. Bila kupoteza muda nikawasha gari na kuondoka eneo lile huku mawazo mengi juu ya Rahma wa Singida, na Zuena wa Mombasa, yakipita kichwani mwangu.

* * *

Inaendelea...
 
ufukweni mombasa.JPG

237

Shujaa!




Saa 12:15 asubuhi…

KULISHAKUCHA na jua lilikuwa linachomoza lakini katika hayo si kwamba watu wote tulikuwa tumeamka au tunaamka baada ya kulala usiku. Wengine tulijikuta tukiwa macho karibia kila mchana na usiku kwa siku kadhaa. Tukipanga hili na lile na kisha kupangua. Tukiumba hiki na kile na kisha kuvunja. Tukiwaza jambo hili au lile na kisha kuwazua, tukikihesabu hiki na kile na kisha… Dah! Ukweli ni kwamba mambo yalikuwa mengi sana na muda haukutosha.

Zilikuwa zimeshapita siku tano tangu nilipoanza kumtafuta Rahma wa Singida bila mafanikio yoyote. Tangu usiku wa siku niliyotoka katika Hoteli ya Lamada baada ya kumkosa Rahma wa Singida, huku akijitokea Zuena wa Mombasa, sikuweza kupata usingizi, na hiyo nikaamua muda mwingi kukesha sebuleni kwenye tarakilishi yangu maalumu ya kazi nikijaribu kutafuta taarifa juu ya Rahma wa Singida kupitia programu yangu maalumu ya utambuzi isiyoshindwa ya TracerMark.

Katika upelelezi wangu niliweza kufahamu mambo machache sana kumhusu Rahma wa Singida, mambo ambayo hayakuwa msaada kabisa kwenye kile nilichokuwa nikikihisi juu ya mwanamke huyo. Yalikuwa ni mambo ya kawaida. Hata hivyo, hisia zangu bado ziliniambia kuwa kwa vyovyote kulikuwepo aina fulani ya kuhusiana kati ya Rahma wa Singida na Zuena wa Mombasa.

Ni hapo nilipomkumbuka Zuena wa Mombasa, katika kipindi chote cha siku tano hatukuwa tumewasiliana wala kukutana tena, na kama alijaribu kunitafuta kwenye namba za simu nilizompatia asingeweza kunipata. Nilikuwa na sababu za msingi za kutotaka kuwasiliana au kukutana na Zuena kwa muda huo, kwani nilihitaji muda zaidi wa kushughulika na jambo lililonitia wasiwasi. Kuhusu Rahma wa Singida.

Hadi wakati huo nilikwisha fanya ziara ya kutembelea maeneo kadhaa ambayo nilidhani ningeweza kumwona Rahma au pengine kupata lolote ambalo lingemhusisha lakini sikufanikiwa. Rahma alikuwa ametoweka kama moshi uliosambaa hewani. Na nilipofuatilia namba za zile gari aina ya Range Rover SV Autobiography LWB la rangi nyeusi lililowachukua kutoka pale Benki ya NBC ili kujua nani mmiliki wake niliishia kupata taarifa zilizozidi kunichanganya.

Lile gari lilikuwa na namba za bandia na kulikuwa na uwezekano mkubwa kwamba lilikuwa limeibwa toka mojawapo ya nchi za Kusini mwa Afrika hususan Afrika Kusini au Botswana. Hali ile ikanizidishia ile njaa niliyokuwa nayo rohoni, njaa ya kutaka kujua ni kitu gani kilikuwa kinapikika sirini, katika jiji la Dar es Salaam!

Kuna muda nilijikuta nikiachana na suala lile la Rahma wa Singida na kujifikiria mwenyewe. Hivi nilikuwa nimepatwa na nini hata nijikute nikitamani kufuatilia mambo yasiyonihusu ambayo pengine yangeishia kuhatarisha maisha yangu na ya familia yangu? Kitu gani kilichoniambukiza ugonjwa huu? Sasa, kwa mara ya kwanza maishani mwangu, nilijikuta nikiilaani taaluma ya ushushushu na kuilaumu bahati yangu.

Baada ya mawazo hayo nilitulia kwa muda nikiitazama dari. Hapana… Niliitazama lakini nilikuwa siioni. Nilikuwa mbali zaidi, nje kabisa ya chumba hicho; nikiyatazama yote ambayo yalipata kunitokea tangu nijiunge na mafunzo ya kijasusi huko chuoni Zawyet Sidi Abd el-Ati nchini Misri, katika hayo mengi yalikuwa ya kutisha na kutatanisha. Yaliifanya roho yangu iponee chupuchupu japokuwa mwisho wa siku nikaonekana mshindi kati ya yote hayo. Na ni hilo ambalo lilinisumbua, kuona kuwa pamoja na ushindi wangu ulionipatia sifa kuanzia kule chuoni hadi kwenye idara yangu ya ujasusi, bado nilikuwa nimeshindwa kutegua kitendawili rahisi sana, juu ya Rahma wa Singida!

Bado hisia zangu ziliniambia kuwa ili kupata majibu juu ya Rahma wa Singida sikupaswa kabisa kumdharau Zuena wa Mombasa. Nikaamua kuziheshimu hisia zangu maana kwa kila hali, niliona kuwa bado nilikuwa hewani nikielea juu bila ya kuufikia msingi wa mambo. Ni hicho kilichonisumbua sana akili yangu, kujiona niko angani nikielea kama kishada. Ningeweza kufanya chini juu kukitegua kitendawili hiki, walao kwa ajili ya kuitoa roho yangu katika lindi la mashaka. Ila hayo yasingekuwa rahisi kiasi hicho pasipo kuziheshimu hisia zangu.

Sikuhitaji tena kujishughulisha na mambo ya kubahatisha na nisingepoteza muda wangu kutafuta habari za mtu ambaye kimsingi, Rahma wa Singida hakuwa na rekodi yoyote ya uhalifu kwani tayari taarifa zake, kuanzia mawasiliano yake na mitandaoni Facebook hadi Instagram zilishaonesha kuwa hakuwa na chochote cha kutiliwa shaka. Zaidi, sikuwa na wasiwasi juu ya Rahma wa Singida kuhama ghafla toka Hoteli ya Lamada kwa kujua kuwa nilikuwa nimemfuatilia, huenda alikuwa na mashaka na mimi na alifanya vile kwa kuhofia usalama wake.

Kitu ambacho kwa sasa kilianza kuisumbua sana akili yangu ni kushindwa kuoanisha mambo juu ya hisia zangu na mkasa mzima kumhusu Rahma wa Singida. Hata hivyo, nilihitaji kwanza kumfahamu Zuena wa Mombasa kwa gharama yoyote ile kwani namna alivyojileta kwangu na hadithi zake kuhusu fani ya mitindo na mavazi niliweza kubaini mengi kuwa hayakuwa na ukweli wowote.

Hivyo, nikaanza mchakato wa kutafuta taarifa za Zuena wa Mombasa kwenye programu hiyo ya TracerMark ili kwamba, kwa kutumia mawasiliano ya simu ya Zuena wa Mombasa au hata kwa kudukua taarifa kwenye account zake za Facebook na Instagram, huenda ningeweza kupata kitu ambacho kingenitoa kwenye mashaka yangu. Niliamini mawasiliano hayo yangenipunguzia kazi kwa kiasi kikubwa.

“Habari za asubuhi, Baba Junior!” sauti tamu ya Rehema ilinizindua toka kwenye lindi la mawazo. Niligeuka kumtazama.

Rehema alikuwa amesimama kando yangu akinitazama kwa utulivu. Sikujua alisimama pale kwa muda gani. Nilikuwa nimemsahau. Wakati wote ambao nilikuwa nimejawa na mawazo yaliyonipeleka nje kabisa ya kuta za nyumba ile kimawazo, nilikuwa nimesahau kabisa kuwa ndani ya nyumba hiyo nilikuwa naishi na watu wengine.

Muda huo Rehema alikuwa amevaa miwani mikubwa ya kuzia mwanga wa jua na suruali ya Jumpsuit ya rangi ya zambarau iliyolionesha vyema umbo lake refu maridadi lenye kiuno chembamba lakini kilichokuwa imara kikiwa kimebeba minofu ya mapaja iliyokaza kutokana na mazoezi. Miguuni alikuwa amevaa viatu vya rangi ya zambarau vya mchuchumio.

Harufu nzuri ya marashi ghali aliyokuwa amejipulizia mwilini ilitamalaki pale sebuleni na kuzifanya pua zangu zipate uhai mpya na kujaribu kunisahaulisha kwa muda masahibu ya kuwafikiria akina Rahma wa Singida na Zuena wa Mombasa.

“Habari za asubuhi!” Rehema aliirejea tena salamu yake.

Nikamtazama usoni na kuachia tabasamu. Hata hivyo tabasamu langu lisingeweza kumlaghai Rehema. Lilikuwa tabasamu la uchungu lililobeba hasira na maumivu makubwa. Badala ya kumjibu nilijikuta nikiinuka toka pale kwenye kiti nilipokaa usiku kucha nikitafuta taarifa kwenye tarakilishi na kumsogelea Rehema kisha nikamsogezea mdomo wangu kinywani mwake.

Rehema akanikwepa huku akisema, “Kazi njema. Najua una kazi ngumu inayokusumbua na akili yako yote imevurugika. Pambana, baba… tutaonana jioni.” Kisha akaanza kupiga hatua za kuondoka.

Inaendelea...
 
Back
Top Bottom