258
Pamoja na mawazo kuniandama lakini chakula kilishuka vilivyo kutokana na ustadi wa mapishi. Muda mwingi Merina alionekana kunitazama lakini nilikuwa mbali kimawazo. Nilikuwa namfikiria dereva wa teksi iliyonibeba kutoka Serena Beach Resort.
Niliamini kuwa kifo chake ulikuwa ni mwanzo tu wa mlolongo wa matukio ya damu kumwagika kwa ajili yangu. Kama ningekuwa naandika kitabu basi damu ya yule dereva wa teksi ingekuwa ni dibaji. Na hivyo ilikuwa lazima damu hii ilipizwe. Bei ya damu ni damu, na yeyote aliyesababisha kumwagika kwa damu hiyo nilimhitaji kwa udi na uvumba na nisingejisamehe kumwacha mtu huyo aendelee kusheherekea hewa safi ya dunia baada ya kumwaga damu ya dereva asiye na hatia.
Ni watu wangapi wangeendelea kupoteza maisha yao katika sakata hilo kabla sijaupata ukweli? Je, ningeendelea kuwa mtu wa kujificha na kuketi kizembezembe hadi lini nikiwatazama watu wanavyouawa kinyama kwa ajili yangu? Lini ningejibu shambulio?
Ukweli kifo cha yule dereva wa teksi kilinitia uchungu mkali moyoni, na mara nikajikuta nikiwaza kile ambacho sikupenda kukiwaza, kwamba kama nisingeruka na mimi muda huo ningekuwa maiti! Halafu…? Likanijia wazo jingine kuwa pengine yule mwuaji alikusudia kunitisha, kwa nini asitumie risasi kunimaliza pale chini nilipoanguka baada ya kunusurika? Nini kilimfanya aondoke haraka eneo lile? Maswali hayo yalizidi kuniongezea kiu ya kutaka kufahamu nini kilikuwa nyuma ya pazia.
Tulimaliza kula kisha tukashushia na matunda halafu maji baridi. Tukarudi kwenye sofa huku kila mmoja akiwa na kimbaka mdomoni kuondoa masalio ya chakula kwenye meno. Sikuacha kumsifia Merina kwa mapishi. Tukiwa pale kwenye sofa nikakumbuka wajibu wangu na kuanza kumsaili Merina.
“Hivi, Merina, una muda gani pale Serena Beach Resort?” nilimuuliza kwa sauti tulivu.
“Miaka miwili,” Merina alijibu.
“Unapaonaje?” nilimsaili tena huku nikimtazama kwa tuo usoni.
“Kupaonaje kivipi?” Merina aliniuliza huku akishindwa kuuficha mshangao wake.
“Panalipa, au unafanya tu kazi kwa sababu huna mahali pengine pa kwenda kufanya kazi?” niliendelea kumuuliza.
“Panalipa,” Merina alisema kwa kifupi na kushusha pumzi.
“Wanalipa vizuri?” nilimuuliza tena na hapo nikamwona akiangua kicheko hafifu.
“Vipi kwani, unataka kuniondoa hapo uniajiri nini?” Merina alisema huku akicheka.
“Yote yanawezekana,” nilisema huku nami nikicheka kidogo.
“Si mbaya, mshahara wao unanisaidia kwa namna fulani lakini uwepo wangu pale unanipa
connection zinazonisaidia kama hivi unavyoona!” Merina alisema huku akinionesha pale sebuleni.
“
Connection kama zipi?” nilimuuliza na hapo nikamwona akisita kidogo kisha akanitazama usoni kwa umakini zaidi. Nikabadili swali, “Nani mmiliki wa hoteli hiyo?”
“Mmiliki simfahamu ila najua asilimia 45 inamilikiwa na
Aga Khan Fund for Economic Development,” Merina alisema.
“Samahani lakini… kuna wageni wawili jana nimewakuta hapo hotelini, mmoja mwanamume wa Kisomali anaitwa Abshir na mwingine mdada wa Kiarabu anaitwa Rahma, unaweza kuwa unawafahamu?”
“Ab-shi-r… Ra-h-ma…” alisema kama aliyejaribu kukumbuka jambo halafu akatingisha kichwa chache kukataa huku uso wake ukionesha shaka fulani. “Hapana, siwafahamu na wala sikumbuki kusikia majina kama hayo pale hotelini.”
“Yule Msomali mrefu ambaye jana tulipishana pale orofa ya pili wakati unanionesha chumba… unamkumbuka?” nilimuuliza tena huku nikimkazia macho.
“Mh! pale kuna Wasomali wengi kwa hiyo sikumbuki yupi unayemkusudia!” Merina alijibu huku akinitazama kwa tuo usoni.
“
Anyway, labda niulize hivi… kuna wale waliopanga katika chumba nambari 201 jirani na chumba changu wamejiandikisha kwa majina gani?” nilimtupia swali lingine na kumwona akinitazama kwa namna ya mshangao.
“Sikumbuki, kwani vipi?” Merina aliniuliza huku akiniangalia kwa udadisi zaidi machoni. “Naomba uniambie ukweli, Jason… wewe ni nani hasa!
Are you a cop?”
“Kwa nini umeuliza hivyo?” nikamtupia swali huku sauti yangu ikiwa bado tulivu na ya kirafiki.
“Nataka tu kufahamu, maana maswali yako ni ya kipolisi polisi,” Merina alisema huku akitabasamu. “Kama kuna jambo baya linaendelea pale hotelini unaweza kuniambia,
we are friends.”
Kwanza niliachia tabasamu lililozaa kicheko hafifu huku nikiyaondosha macho yangu toka usoni kwa Merina, “Hapana, mimi si polisi.”
“
You can trust me… kama kuna lolote unahitaji kufahamu we funguka tu, ila kama huniamini pia hakuna shida,” Merina alisema huku akitabasamu. “
I can understand…”
“Wala si hivyo…” nilisema na kuachia tabasamu pana.
Muda huo akili yangu ilikuwa inasumbuka iwapo nimweleze ukweli au nisimweleze hasa nilipokumbuka kazi ngumu iliyokuwa mbele yangu, sikuona sababu ya kumficha lakini nilichagua kipi cha kumwambia na kipi nikiache.
“Sina hakika lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa hao watu waliopanga chumba nambari 201 si watu wazuri kabisa. Usiniulize nimeona nini lakini elewa hivyo tu,” nilimwambia Merina kisha nikaongeza, “Naomba uwe makini saana lakini usimwambie mtu, sawa?”
Merina alibetua kichwa chake kukubali huku uso wake ukianza kupambwa na wasiwasi, na hapo hapo nikabadili mada, “Hivi eneo hili kuna
gym kweli?”
“Ipo pale jirani na
Bridge International Academy,” Merina aliniambia huku akielekeza kidole chake upande wa Magharibi.
“Basi nitaomba baadaye unipeleke,” nilimwambia kisha nikaongeza, “Pia n’tahitaji kununua nguo maana nimeona duka fulani la nguo kule barabarani.”
* * *
Saa 12:15 jioni…
Jioni ya siku hiyo ilinikuta nikiwa katika
gym moja eneo lile la Shanzu barabara ya Old Malindi nikifanya mazoezi. Niliamua kufanya mazoezi makali mpaka watu wengine waliokuwemo ndani ya ukumbi huo wa mazoezi wakawa wananishangaa lakini sikujali bali niliendelea na mazoezi yangu na kuhakikisha mwili umetona jasho la kutosha.
Muda wote wakati nafanya mazoezi Merina alikuwa amesimama kando akinitazama kwa namna ya kunishangaa, hakujua kile kilichokuwa kikipita akilini kwangu muda huo. Huenda yeye pia alikuwa na maswali mengi kichwani kwake hasa baada ya mazungumzo yetu pale sebuleni.
Baada ya mazoezi yale makali nilichukua taulo langu dogo nililolinunua kwenye duka la nguo eneo lile na kujifuta jasho taratibu, kisha tukaondoka kurudi nyumbani kwa Merina.
Ilipofika saa moja na nusu Merina alikuwa tayari amekwisha maliza kujiandaa na alipotoka chumbani alinikuta nikiwa namsubiri sebuleni nikiwa tayari nimejiandaa. Nilivaa suti nzuri ya rangi ya kijivu na shati jeusi ambavyo nilikuwa nimevinunua kwenye duka la nguo pale pale Old Malindi Road, Shanzu. Kichwani nilivaa kofia ya kijivu aina ya pama iliyoendana na ile suti.
Merina yeye alivaa vazi la jioni, gauni fupi laini jekundu la kumetameta lililoishia juu ya magoti yake na kuufichua vilivyo ubora wa umbile lake. Miguuni alivaa viatu vyekundu visivyo na visigino, kisha akakamilisha urembo wake kwa kubeba mkoba mzuri mwekundu.
Usiku ule hali ya hewa ya jiji la Mombasa ilikuwa imepoa zaidi tofauti na hali ya joto iliyozoeleka, kulikuwa na manyunyu hafifu ya mvua yaliyoanguka kutoka angani kulikotanda wingu jepesi la mvua. Tulipotoka nje tuliikuta teksi ikiwa inatusubiri, dereva wa teksi ile alikuwa kijana wa makamo aliyefahamiana vyema na Merina kwa kuwa alikuwa ni mteja wake wa kuaminika. Alipotuona akaachia tabasamu.
Inaendelea...