Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #701
290
“Je, kuna lolote ambalo umeliona si la kawaida katika miezi ya karibuni kuhusu dada yako?” nilimuuliza huku nikiyatuliza macho yangu kwenye uso wake.
Dk. Uledi alisita kidogo na kushusha pumzi kama aliyekuwa anafikiria jibu, pengine alikuwa akijaribu kuvuta picha. Akatingisha kichwa chake kukataa.
“Lakini nahisi hapa kuna tatizo moja. Nimesikia mahali kuwa dada yako alikuwa ametengana na mumewe. Unaweza kuniambia ni kitu gani kilichowatenganisha?”
“Siwezi, kwa sababu sijui chochote. Dada yangu hakupenda kuweka mambo ya familia yake wazi ndiyo maana wengi wamekuja kufahamu kuwa yeye na mumewe wametengana baada ya kifo chake. Lakini hata kama ningejua sidhani kama ningeweza kukwambia ili ukaitangazie dunia,” Dk. Uledi alisema na kushusha pumzi.
“Nafahamu kuwa Waziri Ummi alikuwa mtu mwadilifu sana asiyeweza kumvumilia mtu asiye mwadilifu… je, unadhani labda mumewe alikuwa na makandokando jambo lililosababisha hata wakatengana?”
Kwa mara ya kwanza Dk. Uledi aliachia tabasamu. “Ni kweli Ummi hakuwa mwanamke wa kumvumilia mtu mwenye makandokando lakini sidhani kama mumewe alikuwa hivyo.”
“Zipo tetesi kuwa Rashid Mrutu ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wa mihadarati, kuna ukweli wowote juu ya hilo?” nilimuuliza Dk. Uledi huku nikimtazama kwa umakini.
Dk. Uledi alisita kidogo kabla hajasema, “Hizo ni tetesi na zitabaki kuwa tetesi.”
“Na inaonekana kuwa lile bomu lililolipuka pale Alpha Mall lilikuwa limekusudiwa kumuua Waziri Ummi, hili unalisemaje?” nilimuuliza tena Dk. Uledi, na hapo nikamwona akishtuka kidogo.
“Kwa vipi?” Dk. Uledi aliniuliza huku akinikazia macho.
“Mazingira yanatia shaka. Kifo cha waziri kimetokea wiki tatu tu tangu kijana wake Fikiri Mrutu afe kifo cha kutatanisha, halafu bomu lenyewe lililipuka muda mfupi tu tangu afike pale Alpha Mall hali inayoashiria kuwa wauaji walimfuatilia au kukusudia yeye. Wewe unasemaje?”
“Dah, nahisi kuwa maswali yako yalipaswa kuulizwa na polisi na si mwandishi wa habari kama wewe,” lilikuwa jibu la Dk. Uledi.
“Ni kweli lakini mwandishi mzuri ni yule anayewatangulia polisi kubaini mambo, si kusubiri taarifa ambazo mara nyingi huwa zimechujwa sana na kukosa ukweli,” nilimwambia Dk. Uledi. Hata hivyo hakuwa tayari kunieleza hisia zake…
_____
Sasa nilikuwa nimetulia ofisini kwangu nikiwa na magazeti yale nikizipitia habari kuhusu shambulio la bomu lililosababisha kifo cha Waziri Ummi Mrutu. Katika yote niliyoyasoma au kuyasikia kitu kimoja kilikuwa dhahiri, kama alivyoandika mwandishi wa gazeti la Rindima kuwa; Waziri Ummi hakustahili kufa kifo hiki.
Dhana hii ilinipa kitendawili kigumu sana kukitegua hasa nikizingatia ukweli kuwa muuaji au wauaji wake wangeweza kutumia njia nyingine kumuua lakini badala yake wakaamua kutumia njia ya bomu ambalo liliua pia watu wengine wasiokusudiwa.
Wakati wanahabari waking’ang’ana na tukio ambalo kwa mujibu wa kazi yao lilikuwa la kusisimua, wanausalama tulikuwa katika wakati mgumu kuliko wakati mwingine wowote ule. Tulihangaika kimwili na kiakili, jasho likitutoka, hasa kwa kutokujua wapi pa kuanzia na wapi pa kuishia.
‘Waliolipua bomu hilo walikusudia kutoa ujumbe gani?’ Ni swali la kwanza kabisa ambalo lilivisumbua vichwa vya wanausalama. Tuliteseka zaidi kwa kutokuwa na jibu rahisi kwa swali hilo. Hivyo, maswali yaliyofuatia yalikuwa; ‘Ni nani, au kundi gani lililofanya ugaidi huu?’; ‘Sababu na malengo yao ni ipi?’; ‘Na wangenufaika vipi na kitendo chao?’ Yote haya yalipita katika kila kichwa cha mwanausalama na kutuchanganya zaidi.
Bila ya jibu lolote kwa maswali hayo liliibuka lile kubwa zaidi ambalo si kwamba lilivisumbua tu vyombo vya ulinzi na usalama bali pia lilivitisha sana; ‘Je, tukio hili ni mwanzo au mwisho wa makusudio ya magaidi hao?’
Hadi wakati huo nikiwa nimeketi ofisini kwangu tayari vyombo vya ulinzi na usalama vilikuwa katika hali ya hadhari. Hakukuwa na ndege iliyoruka toka nje au ndani ya nchi bila kupitiwa na macho ya rada za vyombo hivi. Mipaka yote pia ilidhibitiwa huku ikihakikishwa kuwa hakuna shambulio lolote toka nje ambalo lisingedhibitiwa kwa nguvu zote.
Nilikuwa nimemsikia msemaji wa polisi akisema kuwa taarifa ambazo ziliwafikia toka nchi adui na rafiki zilionesha kutokuwepo kwa fununu yoyote ya nchi yoyote, au kundi lolote la kigaidi kujihusisha na tukio hili. hali hii ilizidi kuwachanganya wakuu wa vyombo vya usalama kama ambavyo kila mtu alivyochanganywa!
Nilishusha pumzi na taratibu niliachana na magazeti yale na kukizungusha kiti changu cha ofisini nilichokikalia kwenda upande wa kushoto sehemu kulipokuwa na rafu yenye vitabu, majarida mbalimbali na mafaili, na hapo nikaweka kituo nikiyatembeza macho yangu kudadisi kama kungekuwa na chochote ambacho kingenisaidia katika kufanyia kazi zangu. Wakati nikitafakari simu yangu ya mkononi ikaanza kuita.
Niliitazama vizuri na kuliona jina la Tunu Michael kwenye kioo cha simu, nikashusha pumzi na kuminya midomo. “Hallo, mkuu!” nilizungumza kwa sauti tulivu mara tu nilipoipokea ile simu na kuiweka kwenye sikio langu.
“Vipi umefikia wapi?” Tunu aliniuliza
“Bado nachakata taarifa, baadaye nitaziwasilisha kwako,” nilimjibu.
“Jitahidi maana wakuu wananiuliza tumefikia wapi. tunazo siku tatu tu za kufanikisha jukumu letu. Pia kuna jambo nimelipata nadhani linaweza kuwa msaada mkubwa katika kuwafikia adui zetu,” Tunu alisema. “Naomba tuonane saa kumi na mbili na nusu jioni. Nitakueleza baadaye wapi tukutane.”
“Sawa, mkuu,” nilisema na hapo Tunu akakata simu.
Baada ya simu ya Tunu kukatwa mara ile simu ya mezani mle ndani ofisini nayo ikaanza kuita. Nikaunyanyua ule mkonga wa simu na kuuweka sikioni huku macho yangu yakiutazama mlango wa kuingilia mle ndani.
Sauti laini ya kike kutoka upande wa pili wa ile simu ilinitanabaisha kuwa mzungumzaji alikuwa Radhia Jumanne, mfanyakazi wa mapokezi.
“Hallo, Radhia!” niliongea kabla Radhia hajaniambia dhumuni la simu ile baada ya kuisikia sauti yake.
“Bosi, kuna mtu anahitaji kukuona,” sauti nyepesi ya Radhia ilipenya kwenye ngoma ya sikio langu.
“Ana shida gani?” nilimuuliza Radhia kwa wasiwasi.
Endelea...