Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Shusha vitu kaka...huyu karani wa Sizya anataka kuleta mambo meusi...ataaga dunia muda si mrefu.
 
taharuki..jpg

310

Saa 8:15 mchana…

Tulifika katika jengo la Benki ya Alpha tawi la Dar es Salaam, lililokuwa katika mtaa wa India eneo la Mnazi Mmoja, na kuegesha gari letu katika eneo maalumu la maegesho lililokuwa kando kidogo ya jengo hilo. Kuipata benki hiyo halikuwa jambo jepesi hata kidogo kwa kuzingatia kuwa ilikuwa ni benki bado mpya ikiwa imefunguliwa na kuanza kutoa huduma zake jijini Dar es Salaam kwa takriban miezi kumi tu iliyokuwa imepita.

Ni katika benki hii ya Alpha ndipo mtu mwenye jina la Andrew Adonis aliyekuwa akifanya kazi kama meneja wa benki hiyo alipatikana. Na kupitia barua niliyokuwa nimeichukua kule nyumbani kwa SSP Kambi usiku wa siku iliyokuwa imetangulia kulikuwa na maelekezo yaliyokuwa bayana kwa meneja wa benki hiyo tawi jipya la Dar es Salaam, Mr. Andrew Adonis kuhakikisha kuwa SSP Yusuf Kambi anapatiwa mgawo wake kutoka kwenye fedha zilizoingizwa kwenye benki hiyo kupitia akaunti maalumu.

Barua ile iliendelea kueleza kuwa SSP Kambi, kama ilivyokuwa kwa watu wengine ambao orodha ya majina yao ilikuwa imetumwa kwa meneja huyo kwa njia ya barua pepe, wangefika kwa nyakati tofauti kwenye benki hiyo wakiwa na vitambulisho vyao vya kazi, nakara ya barua ya maelekezo (kama ile ya SSP Yusuf Kambi) na hundi zao zilizosainiwa tayari kulipwa mgao wao kutoka kwenye akaunti ile maalumu, lakini ikisisitizwa kuwa shughuli yote ya utoaji wa fedha hizo ilipaswa kufanywa katika mazingira yenye usiri mkubwa sana.

Tulipoingia ndani ya jengo lile la Benki ya Alpha tulitembea taratibu tukiyatembeza macho yetu kuyatazama mazingira ya mle ndani. Haraka sana niliweza kugundua kuwa upande wa kulia kulikuwa na meza ya ukutani ambayo ilikuwa ikitumiwa na wateja wa benki ile kwa ajili ya kuandikia au kujaza taarifa za benki kwenye karatasi maalumu ya kutolea au kuweka fedha.

Mara baada ya kuipita meza ile kulikuwa na viti vingi katika sehemu maalumu ambapo wateja wa benki ile walikuwa wameketi wakisubiri kupata huduma au wakisubiri wakati shida zao zikishughulikiwa na maofisa wa benki ile. Baada ya kuipita sehemu ile mbele kidogo upande ule ule wa kulia kulikuwa na dawati la huduma kwa wateja na msichana mrembo alikuwa ameketi.

Upande wa kushoto mle ndani kulikuwa na vizimba sita vya watoa fedha (bank tellers) wa benki ile vilivyotengenezwa kwa kuta za aluminium na vioo. Ndani ya vile vizimba kulikuwa na wafanyakazi, wake kwa waume, wa benki ile waliokuwa wakiendelea kuwahudumia wateja wachache waliokuwepo kwenye foleni fupi kuelekea vibanda vile.

Tukiwa tumeridhishwa na tathmini ya mandhari ya ndani ya jengo lile la benki taratibu tulielekea kwenye lile dawati la huduma kwa wateja alilokuwa ameketi yule msichana mrembo aliyeonekana kuyazingatia vizuri maadili ya kazi yake kwa kutabasamu mbele ya wateja waliowasili kwenye dawati lake kwa ajili ya kupata huduma.

Msichana huyo alikuwa mweupe kiasi na kwa mwonekano tu niliweza kubaini kuwa hakuwa amezidi umri wa miaka 25. Alivaa sare maalumu ya wafanyakazi wa benki hiyo; suti nzuri ya rangi ya bluu iliyokolea, kwa ndani alivaa shati jeupe lenye kola ya rangi ya bluu na tai ya bluu iliyokuwa na nembo ya benki ile. Miguuni alikuwa amevaa viatu vyeusi vya ngozi visivyo na visigino virefu.

Macho yake yalikuwa makubwa kiasi na legevu kiasi yaliyopambwa na tabasamu laini usoni mwake. Kope zake zilikuwa zimekolea wanja mfano wa mwezi mwandamo. Masikio yake alikuwa ametoga na kuvaa hereni ndogo za madini ya dhahabu na nywele zake zilikuwa fupi alizokuwa amezinyoa mtindo wa low cut.

Tulisita kidogo kumfuata msichana huyo pale kwenye dawati lake, tukasimama kwa utulivu tukimsubiri amalizane kwanza na mteja mmoja, mtu mzima, mwenye asili ya Kiasia ambaye alikuwa akipewa maelekezo ya namna ya kujaza fomu maalumu ya benki hiyo. Mara tukamwona yule mtu akiondoka, na hapo msichana yule aliyahamisha macho yake kutoka kwa mtu yule na kututazama huku akiachia tabasamu pana la makaribisho.

“Karibuni, sijui niwasaidie?” yule msichana alituuliza huku uso wake ukipambwa na tabasamu la kibiashara na alikuwa amechangamka sana kwa kudhani tulikuwa wateja wapya. Tulimsalimia, kisha Luteni Lister akaanzisha maongezi.

“Samahani… tumekuja hapa kwa sababu tunaamini idara yako ya huduma kwa wateja inaweza kutusaidia. Sijui uko tayari kwa hilo?” Luteni Lister alimuuliza yule msichana kwa sauti tulivu ya kirafiki.

“Itategemea na aina ya msaada mnaouhitaji, kama uko ndani ya uwezo wangu sawa, la kama sitaweza kuwasaidia natumaini hamtanilaumu,” yule msichana alijibu huku sura yake ikiwa bado imepambwa na tabasamu pana la kibiashara.

“Shida yetu ni ndogo tu, tunahitaji kuonana na meneja wa benki hii, ndugu Andrew Adonis,” Luteni Lister alimwambia yule msichana huku akiendelea kuifanya sauti yake kuwa ya kirafiki zaidi.

“Meneja?” yule msichana aliuliza kwa mshangao.

“Ndiyo,” Luteni Lister alimjibu yule msichana huku akilegeza sura yake katika namna ya kirafiki zaidi.

Yule msichana alinyamaza kidogo huku akitutazama kwa zamu kama aliyekuwa akitusaili, alionekana kama aliyekuwa anafikiria jambo kisha alipitisha ulimi wake chini ya mdomo wake wa chini.

“Kwani shida yenu ni lazima itatuliwe na meneja tu na si mtu mwingine?” yule msichana alituuliza akiwa bado amechangamka.

Na hapo nikamwona Luteni Lister akitoa kitambulisho chake cha kazi, akamwekea yule msichana mbele ya macho yake, huenda aliona mahojiano hayo yangeweza kuchukua muda mrefu.

“Ni masuala ya kazi, dada yangu,” Luteni Lister alisema huku akimkazia macho yule msichana. Kisha alitutambulisha mimi na Pamela kwa yule msichana.

Yule msichana alishtuka kidogo na hapo nikauona ule uchangamfu wake ukiyeyuka haraka kama siagi iliyotiwa katika kikaango cha moto. Kisha aliupitisha tena ulimi wake chini ya mdomo, safari hii haraka haraka, halafu akameza funda la mate kutowesha koo lake ambalo bila shaka lilikauka ghafla.

“Unaitwa nani?” Luteni Lister alimuuliza yule msichana kwa sauti tulivu ya chini lakini iliyosikiwa vizuri na yule msichana.

“Naitwa Rahma Sufiani Mango,” yule msichana alijibu huku sura yake ikiwa imepambwa na woga.

Okay, Rahma, tunahitaji kuonana na meneja wako, sijui utatusaidiaje?” Luteni Lister aliendelea kuongea kwa sauti ya kirafiki huku akikirudisha kitambulisho chake mfukoni.

Rahma hakuna na namna isipokuwa kutuelekeza zilipokuwepo ngazi za kuelekea juu kwenye ofisi ya meneja wa benki ile, tukamshukuru na kuzifuata zile ngazi za kuelekea juu kisha tukaanza kuzikwea hadi sehemu ya juu na kuufikia mlango wa ofisi ya meneja wa benki uliokuwa mkono wa kushoto mara baada ya kumaliza kupanda ngazi.

Endelea kufuatilia...
 
taharuki..jpg

311

Luteni Lister aligonga mlango wa ofisi ya meneja taratibu kisha akakishika kitasa na kukinyonga halafu akausukuma, ukafunguka. Tukajitoma ndani na kumkuta mwanamume mmoja mtu mzima lakini umri wake usingekuwa zaidi ya miaka hamsini. Alikuwa chotara, kwa mwonekano tu alionekana kuwa na asili ya Kigiriki, mrefu mwenye nywele ndefu na alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha kiofisi cha utukufu nyuma ya meza kubwa ya ofisi. Mara moja tukatambua kuwa yule ndiye Andrew Adonis.

Juu ya ile meza kulikuwa na tarakilishi kubwa ya mezani, trei dogo lenye ngazi tatu kwa ajili ya kuwekea nyaraka za ofisi, simu ya mezani, mhuri na kidau cha wino pamoja na mafaili kadhaa mbele yake. Upande wake wa kushoto kulikuwa na meza nyingine ndogo na fupi ya mbao ambayo juu yake kulikuwa na mashine ya kurudufu (photocopier) na scanner.

Andrew Adonis alikuwa mnene mwenye kitambi cha ukwasi na macho yake yalikuwa makubwa lakini yenye hila yakiwa nyuma ya miwani mikubwa ya macho. Uso wake ulikuwa wa duara na ndevu zake zilizoanza kuwa na mvi alikuwa amezinyoa vizuri kuuzunguka mdomo wake. Alivaa suti nzuri ya kijivu na koti lake la suti alikuwa amelitundika nyuma kwenye kiti chake cha ofisi kinachoweza kuzunguka nyuzi mia tatu sitini na hivyo kuusanifu vizuri mwonekano wake mpya wa fulana ya kaba shingo nyeusi ya mikono mirefu.

Ofisi ya meneja, kama zilivyokuwa ofisi nyingi za kisasa, ilikuwa kubwa yenye mpangilio mzuri wa samani za ofisini huku sakafu yake ikifunikwa kwa zulia maridadi la rangi nyekundu. Upande wa kulia wa ile ofisi kulikuwa na dirisha kubwa la kioo lililofunikwa kwa pazia jepesi. Na kando ya dirisha lile kulikuwa na rafu kubwa ya chuma yenye droo tano. Pembeni kulikuwa na seti moja ya makochi laini ya bluu ya sofa yaliyoizunguka meza fupi ya kioo iliyokuwa na majarida na vipeperushi vinavyohusiana na huduma zilizokuwa zinatolewa na ile benki.

Upande wa kushoto wa ile ofisi kulikuwa na jokofu dogo la vinywaji baridi. Pia ndani ya ile ofisi kulikuwa kiyoyozi kilichokuwa kikisambaza hewa safi iliyokinzana na hali ya joto kali ya Jiji la Dar es Salaam.

Yule meneja alipotuona akasita kidogo kuendelea kufanya alichokuwa akikifanya kwenye tarakilishi yake na kisha kuiegemeza mikono yake juu ya meza kabla ya kutukaribisha huku uso wake ukiwa hauoneshi tashwishwi yoyote. “Karibuni.”

“Ahsante,” tuliitikia kwa nidhamu kama ilivyo kwa mtu yeyote mgeni aingiapo katika ofisi nyeti. Tukamsalimia yule meneja wa benki, kisha Luteni Lister akmuuliza, “Bila shaka wewe ndiye Mr. Andrew Adonis?”

“Naam! Naitwa Andrew Adonis, ni meneja wa benki tawi hili la Dar es Salaam. Sijui mna shida gani?” yule meneja alisema kwa kujiamini.

Badala ya kumjibu Luteni Lister alitoa kitambulisho chake huku akijitambulisha na kututambulisha huku kila mmoja wetu akitoa kitambulisho chake na kumwonesha yule meneja. Baada ya hapo tuliulizana maswali mengine ya kutuwezesha kufahamiana zaidi, kisha Luteni Lister akaingia moja kwa moja kwenye suala la msingi.

“Tunajua una kazi nyingi sana, hivyo tusingependa kukupotezea muda mwingi, tutajitahidi kujieleza kwa kifupi sana,” Luteni Lister alimweleza meneja huyo wa benki.

“Hakuna tatizo, tunaweza kuzungumza,” Andrew Adonis alisema huku akitutazama kwa wasiwasi kidogo ingawa sauti yake ilidhihirisha wazi kuwa alikuwa ameingiwa na hofu.

“Mr Andrew, tunahitaji msaada wako mdogo kuhusu barua hii,” Luteni Lister alisema huku akiifungua ile bahasha kubwa niliyoitoa nyumbani kwa SSP Kambi na kutoa ile barua ya maelekezo iliyokuwa ndani ya ile bahasha na kuitupa pale mezani karibu na yule meneja wa benki.

Kuona vile yule meneja wa benki akaichukua ile karatasi na kuanza kusoma maelezo yaliyokuwa ndani yake. Muda wote macho yetu yalikuwa makini sana kuzitazama nyendo za yule meneja wa benki. Na kadiri yule meneja wa benki alivyokuwa akizidi kuyapitia maelezo kwenye ile barua ndivyo mikono yake ilivyokuwa ikizidi kutetemeka. Mwishowe alionekana kumaliza kuyapitia maelezo kwenye ile barua na kuiweka pale juu ya meza huku uso wake ukiwa umepoteza kabisa utulivu wake sambamba na vitone vya jasho jepesi vikichomoza kwenye paji la uso wake.

“Sasa, maofisa, mnataka niwasaidie nini kwenye hii barua?” yule meneja wa benki auliza kwa wasiwasi huku akitutazama kwa zamu.

“Tunahitaji ushirikiano wako tu kwa kujibu maswali yetu,” Luteni Lister aliongea kwa utulivu huku akimtazama yule meneja wa benki kwa makini.

Kitambo kifupi cha ukimya kikafuata huku yule meneja wa benki akibaki mdomo wazi kwa mshangao wakati mawazo mengi yakipita kichwani mwake. Ni dhahiri mshtuko alioupata meneja yule ulikuwa mkubwa na ulionekana wazi usoni mwake huku akionekana kama mtu aliyekuwa akifikiria kutimua mbio ingawa mazingira ya kufanya vile hayakuwepo.

“Ushirikiano upi mnaouhitaji kutoka kwangu?’’ hatimaye yule meneja wa benki alijikaza na kuuliza kwa sauti ya kupwaya, baada ya kubabaika kidogo.

“Ushirikiano wa kutupatia taarifa zote muhimu unazozifahamu… tunafahamu kuwa unatumika na watu wenye mamlaka zaidi juu yako na kutokana na mazingira uliyo nayo huwezi kukataa. Hata hivyo hiyo haimaanishi kuwa hufahamu kinachoendelea na humfahamu kabisa mtu aliyetoa maagizo haya…” Luteni Lister alimwambia yule meneja wa benki kisha akatutazama na kuyarudisha macho yake kwa yule meneja wa benki.

“Ofisa, naona mnataka kuniweka katika wakati mgumu sana. Kwa sababu mimi, kama Andrew Adonis, sina tatizo kabisa na hilo lakini sheria za benki haziniruhusu kutoa siri za wateja. Kimsingi, mteja anaweza kuifikisha benki mahakamani endapo atagundua taarifa zake zimetolewa bila ridhaa yake,” alilalama yule meneja wa benki.

“Lakini vipo vifungu vya sheria vinavyoturuhusu kuishughulikia akaunti yoyote ya benki pale inapoonekana kuhusihwa na utakatishaji wa fedha. Tupo tayari kukulinda wewe na maslahi yako kama utakuwa muwazi na kutupa ushirikiano wa kutosha katika kumfichua mtu au watu waliopo nyuma ya mtandao huu mchafu,” niliingilia kati nikiongea kwa msisitizo.

Yule meneja wa benki alinitazama kwa kitambo kidogo, alionekana kusita sana na kuinamisha kichwa chake akionekana kuzama kwenye lindi la fikra.

“Ni suala dogo tu, Mr. Andrew, tunahitaji ufahamu kuwa tuna uhakika kuwa fedha zinazotajwa kwenye hii barua ambazo zinatakiwa kugawanywa kwa watu fulani tayari zimeshaingizwa kwenye benki yako. Tunachotaka kujua zimetoka kwa nani na ni nani aliyekupa maagizo haya?” nilimuuliza tena yule meneja wa benki baada ya kumwona akiwa amejiinamia tu pasipo kufanya lolote.

“Sijaona fedha yoyote ya kiasi kikubwa iliyoingia kwenye benki yangu, lakini… hata kama fedha hiyo ingekuwa imeingia taratibu za kibenki haziniruhusu kutoa taarifa za akaunti ya mhusika kwa mtu mwingine isipokuwa kwa idhini ya mhusika tu,” yule meneja wa benki alisema baada ya kufikiria sana kisha aliunyanyua mkono wake kuitazama saa yake ya mkononi.

Kuona vile Luteni Lister akaitoa ile hundi yenye jina la Yusuf Kambi na kuitupia pale mezani karibu na yule meneja wa benki huku akiongea kwa utulivu akijitahidi kuidhibiti hasira yake kifuani. “Najua itakuwa ngumu kwako kusema ukweli ila nisingependa tukaumizana na kutiana ulemavu halafu ndiyo useme, kwa hiyo tuokoe muda… huenda hujui uzito wa jambo hili ndiyo maana unajaribu kuficha taarifa hizi za utakatishaji wa fedha.”

Yule meneja wa benki aliitazama ile hundi kwa makini pale mezani na kuonekana kuingiwa na mshtuko mkubwa zaidi baada ya kupitia hundi ile.

“Hatuhitaji kutumia nguvu ila kama utataka tukifikishane huko, haina shida… tutakupeleka sehemu maalumu ya mahojiano na huko unaweza kujikuta ukitoa taarifa hizo kwa maumivu makali mno, wakati hapa huhitaji maumivu kutueleza…” Luteni Lister aliongea kwa utulivu huku akimtazama yule meneja wa benki kwa macho makali. Kisha akaongeza, “Naamini hili ni jambo dogo tu, tuoneshe cash flow ya hii benki inayoonesha miamala ya fedha zilizoingizwa na kutolewa katika kipindi cha miezi mitatu.”

Nilimtazama yule meneja wa benki kwa umakini na nilichokishuhudia mbele yangu ni hofu na mshtuko mkubwa uliojengeka usoni kwake.

Okay…!” yule meneja wa benki aliitikia kwa shida huku hofu kubwa ikiwa imemshika na muda mfupi uliofuata aliifungua ile tarakilishi yake ya ofisini pale mezani, mimi na Luteni Lister tukasogea na kusimama nyuma yake. Pamela alibaki amesimama kando ya mlango akiwa makini sana kama simba jike anayewinda.

Endelea...
 
taharuki..jpg

312

Ile tarakilishi ilipofunguka yule meneja wa benki, kwa mikono ya kutetemeka, alifungua mafaili kadhaa na kulifikia faili lenye rekodi za miamala ya fedha zilizoingia na kutoka kwenye ile benki. Muda wote macho yetu yalikuwa makini yakiichunguza taarifa ile.

Tuliporidhika nayo Luteni Lister alimtaka yule meneja wa benki aichape ile taarifa. Yule meneja wa benki alisita kidogo lakini macho yake yalipokutana na macho ya Luteni Lister hofu ikamwingia tena na hapo akalazimika kufanya vile alivyoagizwa kwa kuiamuru tarakilishi yake kuichapa ile taarifa ya benki kwenye mashine ya kurudufu ambayo pia ilitumika kama printa.

Mara baada ya ile taarifa ya benki kuchapwa Luteni Lister aliichukua haraka na kuipitia katika namna ya kuichunguza kama angeweza kupata taarifa yoyote ya kumsaidia. Mimi pia niliipitia haraka haraka na kugundua kuwa kulikuwa na miamala mingi iliyofanywa kwenye ile benki kwa kipindi cha miezi mitatu iliyokuwa imepita. Miamala mingi ilikuwa imefanywa na kampuni ambazo kwa namna moja au nyingine hazikupaswa kutiliwa shaka kutokana na aina ya biashara ambazo kampuni hizo zilifanya. Miamala mingi ilikuwa yenye fedha za kawaida.

Katika kuendelea kuchunguza nikajikuta nikivutiwa na akaunti moja ambayo ilikuwa imetumika kufanya muamala wa fedha nyingi sana za kigeni kwa mara moja. Akaunti hiyo ilikuwa na jina la Kangaroo Group. Nilipoichunguza nikagundua kuwa, kupitia rekodi zilizokuwa kwenye taarifa ile ya benki akaunti ile ilikuwa ni mpya kabisa kwani hapakuonekana rekodi nyingine zilizoonesha kuwa akaunti ile ilikuwa ikitumika huko siku za nyuma.

Luteni Lister naye alikuwa ameliona hilo na kunitazama usoni huku akikunja sura yake na kuminya midomo. Lilikuwa jambo la kustaajabisha sana ingawa lingeweza kuaminika vile vile. Tulipoichunguza kwa umakini ile taarifa ndipo shaka juu ya kile tulichokuwa tukikihisi ikazidi kuongezeka. Muamala wa fedha nyingi mno ulikuwa umefanywa kupitia akaunti ile katika siku mbili tu zilizokuwa zimepita.

Haraka sana hisia zangu zikanipeleka kwenye kufikiria juu ya matukio mawili, kwanza lile jaribio lililoshindwa la kutaka kuniua kule Soko la TX Kinondoni; na pili tukio la mlipuko wa bomu pale kwenye jengo la Alpha Mall. Na hapo nikatambua kuwa muamala huo ulikuwa umefanyika siku moja tu baada ya tukio lile la kigaidi. Nikahisi vinyweleo vya mwili wangu vikisimama huku kijasho chepesi kikinitoka mwilini baada ya kugundua kuwa lile jina la akaunti hiyo lilifanana na jina la akaunti iliyokuwa kwenye ile hundi niliyoipata kule nyumbani kwa SSP Kambi!

Kwa sekunde kadhaa nilijikuta nikiwa nimeganda kama sanamu huku nikiendelea kuikodolea macho taarifa ile ya benki kwenye ile karatasi. “Okay, tunahitaji kupata bank statement ya hii akaunti,” nilimwambia yule meneja wa benki huku nikimsogezea karibu ile karatasi na kumwonesha kwa kidole changu kwenye lile jina la akaunti ya Kangaroo Group.

Yule meneja wa benki alilikodolea macho lile jina la akaunti kabla ya kusita huku akiinua uso wake na kunitazama kwa shaka.

“Nahitaji hii taarifa ya kifedha ichapwe!” nilimwamuru yule meneja wa benki huku nikimkazia macho kumaanisha kile nilichokuwa nikikisema.

Yule meneja wa benki aliyahamisha macho yake kutoka kwangu na kumtazama Luteni Lister na mwisho akamalizia kwa Pamela halafu akashusha pumzi ndefu kama aliyetoka kukimbia mbio ndefu. Kisha akainama tena kwenye tarakilishi yake mezani na kuanza kushughulika nayo na baada ya muda mfupi ile taarifa ya kifedha ya akaunti ya Kangaroo Group ikawa imechwapwa kwenye karatasi ikionesha kiasi cha fedha, saa, tarehe, mwezi na mwaka ambao muamala ule wa fedha nyingi kwenye ile akaunti ulikuwa umefanyika.

Jambo moja la kushangaza ni kuwa fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ile zilionekana kuwa zilikuwa zimetokea kwenye benki mama iliyokuwa nchini Afrika Kusini. Niliikodolea macho ile taarifa ya kifedha ya kampuni ya Kangaroo Group huku nikishindwa kuamini kile kilichokuwa kwenye zile karatasi.

“Ni nani boss wa kampuni hii ya Kangaroo ambaye anahusika na fedha hizi?’’ nilimuuliza yule meneja wa benki, hata hivyo alibaki kimya akinitumbulia macho tu kisha alitingisha kichwa chake kuonesha kuwa alikuwa hafahamu chochote.

“Kukaa kimya hakutakusaidia kitu, Mr Andrew Adonis, kwani ni vizuri ukawa muwazi na kutueleza ni nani anayehusika na ugawaji wa mabilioni haya ya fedha nyingi kiasi hiki huku akisisitiza mambo haya yafanyike kwa usiri mkubwa. Na kwa nini amegawa fedha hizi?” Luteni Lister aliingilia kati huku akimkazia macho yule meneja wa benki.

“Kwa kweli mimi simfahamu kwa sababu hata barua hii ya maelekezo nilikuwa sijaipata,” yule meneja wa benki alisema kwa sauti ya unyonge.

Mara moja nikakumbuka jambo na kumwambia yule meneja wa benki kuwa yeye alikuwa ametumiwa nakala laini (soft copy) ya barua yenye orodha ya watu wote waliohitajika kugawiwa fedha hizo, kwa njia ya barua pepe, nikamtaka afungue email yake ambayo ilikuwa na orodha ya majina ya watu wote waliokuwa wakihusika katika mgawo wa fedha hizo. Yule meneja wa benki alionekana kusita sana huku akionesha woga mkubwa mno.

Luteni Lister alimtazama kwa macho makali. “Hivi unapenda kuhangaika na kuteseka eh? Maana tunatumia ustaarabu kukuuliza lakini hutaki kuonesha ushirikiano!” Lister alisema kwa msisitizo huku akimtaka yule meneja wa benki kufungua barua pepe yake kama alikuwa hapendi matatizo zaidi. Macho ya Luteni Lister na sauti yake viliashiria ukweli wa kile alichokuwa akikisema.

“Labda nikwambie ukweli, sisi hatuna shida na wewe. Tunajua wewe ni kibaraka tu unayepewa maagizo. Tuna shida ya kuiona orodha ya watu wote wanaotakiwa kugawiwa fedha hizi na kulijua jina la mtu anayegawa hizi fedha, basi!” nilimweleza yule meneja wa benki kwa sauti tulivu.

Yule meneja wa benki alinitazama kisha akaachia tabasamu, lakini tabasamu lake halikuwa la furaha bali lilibeba kitu fulani, kitu mfano wa hofu kubwa.

“Maofisa, nadhani hamfahamu hatari mnayoitafuta kwa kutaka kupambana na mtandao huu mpana mno wa watu wenye nguvu zote za kimamlaka, kiuchumi, kiulinzi na hata kwa kiukatili!” yule meneja wa benki alisema kwa sauti ya majonzi.

“Kazi za hatari ndizo tunazozipenda wala usiwe na wasiwasi na sisi, wewe tupatie orodha ya watu wote wanaotakiwa kugawiwa fedha na jina la mtu anayegawa hizi fedha halafu hayo mengine tuachie wenyewe,” nilimwambia yule meneja wa benki kwa kujiamini.

“Halafu mimi?” yule meneja wa benki aliuliza huku akinitazama usoni.

“Wewe tutakulinda, hakuna mtu yeyote atakayeweza kukudhuru,” nilimwambia kumtoa hofu. Akacheka.

“Kunilinda…? Hamuwezi kunilinda na wala siwezi kuwa huru kamwe maisha yangu yote,” yule meneja wa benki alisema kwa unyonge.

“Kwa nini unasema hivyo?” nilimuuliza huku nikimkazia macho.

“Kwa sababu najua… pindi unapoingia au kuingizwa ndani ya mtandao huu basi familia yako yote inajulikana. Watu wako wa karibu na marafiki zako wanajulikana. Huwezi kuwa huru labda uwe umekufa! Njia pekee ya mimi kuepukana na haya yote ni kifo tu. Kwa hiyo kama kweli mnataka kunilinda inabidi nife halafu ninyi mjilinde wenyewe,” yule meneja wa benki alisema kwa huzuni. Kisha akaongeza.

“Sina haja ya kuwaambia huu mtandao una nguvu kiasi gani au unahusisha watu gani ila mtakuja kuona wenyewe, na wakati huo mtakuwa mmeshachelewa.”

“Tuamini, hakuna yeyote anayeweza kukudhuru kama utakuwa upande wetu. Kwa nini usishirikiane nasi kwa kutupatia taarifa tunazozihitaji halafu uone uwezo wetu wa kuusambaratisha mtandao huu!” Pamela alisema kwa mara ya kwanza tangu aingie mle ndani.

Yule meneja wa benki alimtazama Pamela kwa kitambo huku akionekana kufikiria kidogo kisha akasshusha pumzi na kuinamia kwenye ile tarakilishi kisha akaanza kushughulika nayo huku mikono ikimtetemeka, aliifungua barua pepe yake na baada ya muda mfupi ikawa imefunguka. Akaifungua ile nakala laini ya barua iliyotumwa ambayo ndiyo ilikuwa na maelekezo na orodha ya watu wote waliotakiwa kupewa mgawo wa fedha.

“Najua sina maisha, mimi ni mtu wa kufa tu. Lakini sina haja ya kufa na taarifa hizi. Ingalau niwapatie mnachokitaka ili mjaribu kuukata mbuyu ambao naamini hamtauweza…” yule meneja wa benki alisema kwa huzuni huku akiiamuru tarakilishi yake kuichapa ile barua.

Luteni Lister aliichukua haraka ile barua yenye maelekezo na orodha ya majina yote ya watu waliotakiwa kupata mgawo wao wa fedha, akaitazama kwa muda na kuachia mguno ulionifanya nami niyapeleke macho yangu kuitazama barua hiyo. Niliyapita maelezo haraka haraka na nilipofika kwenye ile orodha ya majina kumi na nane ya watu waliotakiwa kupata mgawo wa fedha nikajikuta nikipigwa na butwaa.

Mwili wangu ulikuwa kama uliopigwa na shoti mbaya ya umeme na akili yangu ilikataa kabisa kukubaliana na kile nilichokuwa nikikisoma kwenye ile barua. Hali ile ikasababisha jasho jepesi lianze kunitoka mwilini huku mapigo ya moyo wangu yakienda mbio isivyo kawaida. Muda huo yule meneja wa benki alikuwa anatweta.

Nikiwa bado nimezama kwenye kuyasoma yale majina kumi na nane ya watu waliotakiwa kupata mgawo wa fedha nikashtushwa sana na kitendo cha Pamela ambaye alikuwa ameruka juu kumwendea yule meneja wa benki pale kwenye kiti chake lakini alikuwa amechelewa. Sauti kali ya risasi ikasikika. Nilipogeuza shingo yangu kutazama upande huo nikakishuhudia kichwa cha yule meneja wa benki kikifumuliwa na risasi moja tu kutoka kwenye bastola yake aina ya 22 Caliber Revolver aliyokuwa ameididimiza kinywani mwake.

Niliushuhudia mwili wa yule meneja wa benki ukitikisika kidogo tu kwenye kile kiti chake cha ofisini kabla ya kutulia huku roho yake ikiwa mbali na mwili. Alikuwa ameamua kujiweka huru kama alivyodai mwenyewe baada ya kujua kuwa alikuwa ametoa siri hatari za mtandao ule haramu.

* * *

Mambo yanazidi kunoga, usiache kuzifuatilia harakati hizi za Jason Sizya...
 
Asante mkuu, huyu wini na koba nna waswas nao sana ila i miss rehema n am curious abt zainab
Bishop Hiluka pa1 sana mwamba[emoji120]
Duh story imefikia Patamu. Pamoja
Bishop Hiluka
hongera mkuu
kazi nzuri saana
Du mkuu uko vizuri, kazi umeipanga vyema visa na matukio viko vizuri.straight forward umeitumia ipasanyo .umeshift kutoka love mpaka ujasusi. Pongezi Sana bishop.kila season ina vionjo vyake. Nilikuwa nasoma kimyakimya ila imenibidi nikometi leo
UTAMU KOLEA MKUU SHUSHA VITU
Yeah kila episode ina matukio ya kipekee aseee

Hujawahi kuniangusha bishop,nzuri sana!
Kana kwamba naingalia
Shusha vitu kaka...huyu karani wa Sizya anataka kuleta mambo meusi...ataaga dunia muda si mrefu.
Comments zikiwa km hv ni faraja mno kwa mwandishi anajua yes tuko pa1[emoji120]
Bishop Hiluka twende sawa kaka mkubwa...
Karibuni tuendelee kuzishuhudia Harakati za Jason Sizya, japo kwa mwendo mdogo mdogo, lakini naamini tutafika tunakokwenda.
Imesemwa na wahenga kuwa: "Mwendo si kitu jambo la maana ni kujua uendako"...
 
Back
Top Bottom