312
Ile tarakilishi ilipofunguka yule meneja wa benki, kwa mikono ya kutetemeka, alifungua mafaili kadhaa na kulifikia faili lenye rekodi za miamala ya fedha zilizoingia na kutoka kwenye ile benki. Muda wote macho yetu yalikuwa makini yakiichunguza taarifa ile.
Tuliporidhika nayo Luteni Lister alimtaka yule meneja wa benki aichape ile taarifa. Yule meneja wa benki alisita kidogo lakini macho yake yalipokutana na macho ya Luteni Lister hofu ikamwingia tena na hapo akalazimika kufanya vile alivyoagizwa kwa kuiamuru tarakilishi yake kuichapa ile taarifa ya benki kwenye mashine ya kurudufu ambayo pia ilitumika kama
printa.
Mara baada ya ile taarifa ya benki kuchapwa Luteni Lister aliichukua haraka na kuipitia katika namna ya kuichunguza kama angeweza kupata taarifa yoyote ya kumsaidia. Mimi pia niliipitia haraka haraka na kugundua kuwa kulikuwa na miamala mingi iliyofanywa kwenye ile benki kwa kipindi cha miezi mitatu iliyokuwa imepita. Miamala mingi ilikuwa imefanywa na kampuni ambazo kwa namna moja au nyingine hazikupaswa kutiliwa shaka kutokana na aina ya biashara ambazo kampuni hizo zilifanya. Miamala mingi ilikuwa yenye fedha za kawaida.
Katika kuendelea kuchunguza nikajikuta nikivutiwa na akaunti moja ambayo ilikuwa imetumika kufanya muamala wa fedha nyingi sana za kigeni kwa mara moja. Akaunti hiyo ilikuwa na jina la
Kangaroo Group. Nilipoichunguza nikagundua kuwa, kupitia rekodi zilizokuwa kwenye taarifa ile ya benki akaunti ile ilikuwa ni mpya kabisa kwani hapakuonekana rekodi nyingine zilizoonesha kuwa akaunti ile ilikuwa ikitumika huko siku za nyuma.
Luteni Lister naye alikuwa ameliona hilo na kunitazama usoni huku akikunja sura yake na kuminya midomo. Lilikuwa jambo la kustaajabisha sana ingawa lingeweza kuaminika vile vile. Tulipoichunguza kwa umakini ile taarifa ndipo shaka juu ya kile tulichokuwa tukikihisi ikazidi kuongezeka. Muamala wa fedha nyingi mno ulikuwa umefanywa kupitia akaunti ile katika siku mbili tu zilizokuwa zimepita.
Haraka sana hisia zangu zikanipeleka kwenye kufikiria juu ya matukio mawili, kwanza lile jaribio lililoshindwa la kutaka kuniua kule Soko la TX Kinondoni; na pili tukio la mlipuko wa bomu pale kwenye jengo la Alpha Mall. Na hapo nikatambua kuwa muamala huo ulikuwa umefanyika siku moja tu baada ya tukio lile la kigaidi. Nikahisi vinyweleo vya mwili wangu vikisimama huku kijasho chepesi kikinitoka mwilini baada ya kugundua kuwa lile jina la akaunti hiyo lilifanana na jina la akaunti iliyokuwa kwenye ile hundi niliyoipata kule nyumbani kwa SSP Kambi!
Kwa sekunde kadhaa nilijikuta nikiwa nimeganda kama sanamu huku nikiendelea kuikodolea macho taarifa ile ya benki kwenye ile karatasi. “
Okay, tunahitaji kupata
bank statement ya hii akaunti,” nilimwambia yule meneja wa benki huku nikimsogezea karibu ile karatasi na kumwonesha kwa kidole changu kwenye lile jina la akaunti ya Kangaroo Group.
Yule meneja wa benki alilikodolea macho lile jina la akaunti kabla ya kusita huku akiinua uso wake na kunitazama kwa shaka.
“Nahitaji hii taarifa ya kifedha ichapwe!” nilimwamuru yule meneja wa benki huku nikimkazia macho kumaanisha kile nilichokuwa nikikisema.
Yule meneja wa benki aliyahamisha macho yake kutoka kwangu na kumtazama Luteni Lister na mwisho akamalizia kwa Pamela halafu akashusha pumzi ndefu kama aliyetoka kukimbia mbio ndefu. Kisha akainama tena kwenye tarakilishi yake mezani na kuanza kushughulika nayo na baada ya muda mfupi ile taarifa ya kifedha ya akaunti ya Kangaroo Group ikawa imechwapwa kwenye karatasi ikionesha kiasi cha fedha, saa, tarehe, mwezi na mwaka ambao muamala ule wa fedha nyingi kwenye ile akaunti ulikuwa umefanyika.
Jambo moja la kushangaza ni kuwa fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ile zilionekana kuwa zilikuwa zimetokea kwenye benki mama iliyokuwa nchini Afrika Kusini. Niliikodolea macho ile taarifa ya kifedha ya kampuni ya Kangaroo Group huku nikishindwa kuamini kile kilichokuwa kwenye zile karatasi.
“Ni nani boss wa kampuni hii ya Kangaroo ambaye anahusika na fedha hizi?’’ nilimuuliza yule meneja wa benki, hata hivyo alibaki kimya akinitumbulia macho tu kisha alitingisha kichwa chake kuonesha kuwa alikuwa hafahamu chochote.
“Kukaa kimya hakutakusaidia kitu, Mr Andrew Adonis, kwani ni vizuri ukawa muwazi na kutueleza ni nani anayehusika na ugawaji wa mabilioni haya ya fedha nyingi kiasi hiki huku akisisitiza mambo haya yafanyike kwa usiri mkubwa. Na kwa nini amegawa fedha hizi?” Luteni Lister aliingilia kati huku akimkazia macho yule meneja wa benki.
“Kwa kweli mimi simfahamu kwa sababu hata barua hii ya maelekezo nilikuwa sijaipata,” yule meneja wa benki alisema kwa sauti ya unyonge.
Mara moja nikakumbuka jambo na kumwambia yule meneja wa benki kuwa yeye alikuwa ametumiwa nakala laini (
soft copy) ya barua yenye orodha ya watu wote waliohitajika kugawiwa fedha hizo, kwa njia ya barua pepe, nikamtaka afungue
email yake ambayo ilikuwa na orodha ya majina ya watu wote waliokuwa wakihusika katika mgawo wa fedha hizo. Yule meneja wa benki alionekana kusita sana huku akionesha woga mkubwa mno.
Luteni Lister alimtazama kwa macho makali. “Hivi unapenda kuhangaika na kuteseka eh? Maana tunatumia ustaarabu kukuuliza lakini hutaki kuonesha ushirikiano!” Lister alisema kwa msisitizo huku akimtaka yule meneja wa benki kufungua barua pepe yake kama alikuwa hapendi matatizo zaidi. Macho ya Luteni Lister na sauti yake viliashiria ukweli wa kile alichokuwa akikisema.
“Labda nikwambie ukweli, sisi hatuna shida na wewe. Tunajua wewe ni kibaraka tu unayepewa maagizo. Tuna shida ya kuiona orodha ya watu wote wanaotakiwa kugawiwa fedha hizi na kulijua jina la mtu anayegawa hizi fedha, basi!” nilimweleza yule meneja wa benki kwa sauti tulivu.
Yule meneja wa benki alinitazama kisha akaachia tabasamu, lakini tabasamu lake halikuwa la furaha bali lilibeba kitu fulani, kitu mfano wa hofu kubwa.
“Maofisa, nadhani hamfahamu hatari mnayoitafuta kwa kutaka kupambana na mtandao huu mpana mno wa watu wenye nguvu zote za kimamlaka, kiuchumi, kiulinzi na hata kwa kiukatili!” yule meneja wa benki alisema kwa sauti ya majonzi.
“Kazi za hatari ndizo tunazozipenda wala usiwe na wasiwasi na sisi, wewe tupatie orodha ya watu wote wanaotakiwa kugawiwa fedha na jina la mtu anayegawa hizi fedha halafu hayo mengine tuachie wenyewe,” nilimwambia yule meneja wa benki kwa kujiamini.
“Halafu mimi?” yule meneja wa benki aliuliza huku akinitazama usoni.
“Wewe tutakulinda, hakuna mtu yeyote atakayeweza kukudhuru,” nilimwambia kumtoa hofu. Akacheka.
“Kunilinda…? Hamuwezi kunilinda na wala siwezi kuwa huru kamwe maisha yangu yote,” yule meneja wa benki alisema kwa unyonge.
“Kwa nini unasema hivyo?” nilimuuliza huku nikimkazia macho.
“Kwa sababu najua… pindi unapoingia au kuingizwa ndani ya mtandao huu basi familia yako yote inajulikana. Watu wako wa karibu na marafiki zako wanajulikana. Huwezi kuwa huru labda uwe umekufa! Njia pekee ya mimi kuepukana na haya yote ni kifo tu. Kwa hiyo kama kweli mnataka kunilinda inabidi nife halafu ninyi mjilinde wenyewe,” yule meneja wa benki alisema kwa huzuni. Kisha akaongeza.
“Sina haja ya kuwaambia huu mtandao una nguvu kiasi gani au unahusisha watu gani ila mtakuja kuona wenyewe, na wakati huo mtakuwa mmeshachelewa.”
“Tuamini, hakuna yeyote anayeweza kukudhuru kama utakuwa upande wetu. Kwa nini usishirikiane nasi kwa kutupatia taarifa tunazozihitaji halafu uone uwezo wetu wa kuusambaratisha mtandao huu!” Pamela alisema kwa mara ya kwanza tangu aingie mle ndani.
Yule meneja wa benki alimtazama Pamela kwa kitambo huku akionekana kufikiria kidogo kisha akasshusha pumzi na kuinamia kwenye ile tarakilishi kisha akaanza kushughulika nayo huku mikono ikimtetemeka, aliifungua barua pepe yake na baada ya muda mfupi ikawa imefunguka. Akaifungua ile nakala laini ya barua iliyotumwa ambayo ndiyo ilikuwa na maelekezo na orodha ya watu wote waliotakiwa kupewa mgawo wa fedha.
“Najua sina maisha, mimi ni mtu wa kufa tu. Lakini sina haja ya kufa na taarifa hizi. Ingalau niwapatie mnachokitaka ili mjaribu kuukata mbuyu ambao naamini hamtauweza…” yule meneja wa benki alisema kwa huzuni huku akiiamuru tarakilishi yake kuichapa ile barua.
Luteni Lister aliichukua haraka ile barua yenye maelekezo na orodha ya majina yote ya watu waliotakiwa kupata mgawo wao wa fedha, akaitazama kwa muda na kuachia mguno ulionifanya nami niyapeleke macho yangu kuitazama barua hiyo. Niliyapita maelezo haraka haraka na nilipofika kwenye ile orodha ya majina kumi na nane ya watu waliotakiwa kupata mgawo wa fedha nikajikuta nikipigwa na butwaa.
Mwili wangu ulikuwa kama uliopigwa na shoti mbaya ya umeme na akili yangu ilikataa kabisa kukubaliana na kile nilichokuwa nikikisoma kwenye ile barua. Hali ile ikasababisha jasho jepesi lianze kunitoka mwilini huku mapigo ya moyo wangu yakienda mbio isivyo kawaida. Muda huo yule meneja wa benki alikuwa anatweta.
Nikiwa bado nimezama kwenye kuyasoma yale majina kumi na nane ya watu waliotakiwa kupata mgawo wa fedha nikashtushwa sana na kitendo cha Pamela ambaye alikuwa ameruka juu kumwendea yule meneja wa benki pale kwenye kiti chake lakini alikuwa amechelewa. Sauti kali ya risasi ikasikika. Nilipogeuza shingo yangu kutazama upande huo nikakishuhudia kichwa cha yule meneja wa benki kikifumuliwa na risasi moja tu kutoka kwenye bastola yake aina ya
22 Caliber Revolver aliyokuwa ameididimiza kinywani mwake.
Niliushuhudia mwili wa yule meneja wa benki ukitikisika kidogo tu kwenye kile kiti chake cha ofisini kabla ya kutulia huku roho yake ikiwa mbali na mwili. Alikuwa ameamua kujiweka huru kama alivyodai mwenyewe baada ya kujua kuwa alikuwa ametoa siri hatari za mtandao ule haramu.
* * *
Mambo yanazidi kunoga, usiache kuzifuatilia harakati hizi za Jason Sizya...