Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

utata.JPG

341

Yuko wapi!




Saa 12:53 asubuhi…

NILIINGIA ofisini kwa mkuu wangu wa kikosi maalumu kilichoshughulika na operesheni hatari (SOG), Kanali Othman Mjaka, dakika saba kabla ya saa moja, muda ambao nilitakiwa kufika hapo, nikitokea Julius Nyerere International Airport. Kwa haraka niliyokuwa nayo sikuweza hata kupita nyumbani kwangu Upanga ili nijimwagie maji na kubadilisha nguo kwani nilikuwa nimechafuka sana.

Ofisi ya Kanali Othman Mjaka ilikuwa nzuri sana na pana ikiwa na mazingira nadhifu na yaliyovutia kwa mpangilio wa samani za kisasa za ofisini, ilikuwa na zulia zito jekundu sakafuni na meza ndefu ya ofisini yenye viti ishirini. Viti kumi upande wa kushoto na viti vingine kumi upande wa kulia.

Mle ndani ya ofisi kulikuwa na ukimya mzito ulionifanya nisikie sauti ya hatua zangu mwenyewe wakati nilipokuwa nikitembea kukatisha katikati ya kile chumba nikielekea kule mbele kwenye meza alikokuwa ameketi Kanali Mjaka.

Aiwa katika umri wa miaka 52, Mkuu huyo wa SOG alikuwa ameketi kwa utulivu kwenye kiti chake kikubwa cha kiofisi cha ngozi halisi cha kuzunguka na chenye magurudumu madogo, nyuma ya meza yake kubwa ya ofisini mwisho wa ofisi ile upande wa kulia. Uso wake ulikuwa umesawajika kidogo ila macho yake yalikuwa makini kupitia taarifa fulani kwenye kishkwambi chake alichokuwa amekishika mkononi pasipo kuniangalia pamoja na kuwa alitambua kuwa nilikuwa nimeingia ndani ya ofisi yake.

Kanali Mjaka alikuwa mfupi na mnene kiasi, mweupe sana mwenye ule weupe wa kichotara akiwa mchanganyiko wa damu ya Kishirazi na Kiarabu. Kwa kuwa alitokea Pemba hivyo wengi walipenda kumwita Kanali Mpemba.

Sura yake ilikuwa ya mviringo iliyoonesha utulivu, na macho yake yalikuwa makubwa yenye uchovu lakini yaliyojaa kiburi na yenye kila dalili ya kuonya. Asubuhi ile alikuwa amevaa suti ghali ya kijivu ya single button, brand ya Piacenza kutoka Italy na miwani mikubwa myeupe ya macho.

Kanali Mjaka alikuwa ameipata nafasi ya kuongoza kikosi hiki maalumu cha siri cha kushughulika na operesheni hatari kutokana na umahili wake kwenye operesheni za kijasusi, alikuwa ofisa nguli, mwenye elimu na uzoefu wa hali ya juu katika kazi za kijasusi.

Licha ya kushiriki katika operesheni lukuki ndani ya nchi pia alikuwa amefanya kazi katika nchi kadhaa za Ulaya na Mashariki ya Kati, na kukamilisha malengo ya Idara ya Ujasusi kwa ufanisi mkubwa. Hadi muda huu Kanali Mjaka alikuwa na takriban miaka therathini katika Idara ya Usalama wa Taifa, na muda huo ulimwezesha kujenga rekodi ya utendaji bora kulinganisha na umri wa kati aliokuwa nao.

Nilipofika mbele ya meza yake nilisimama kwa ukakamavu huku nikimtazama kwa wasiwasi kidogo, kwa namna alivyokuwa nilihisi kabisa kuwa mambo hayakuwa shwari hata kidogo. Nilimsalimia kwa adabu huku nikiendelea kumtazama usoni kwa wasiwasi kidogo.

Hakuhangaika kuniangalia wala kunijibu na badala yake aliniashiria kwa mkono kuwa nivute kiti niketi halafu yeye akaendelea kutazama katika kile kishkwambi chake pasipo hata kunitazama, huku uso wake ukiwa umesawajika kidogo na mawazo yake yakionesha kuwa mbali na kile chumba. Sikushangaa hata kidogo kwa tabia ile kwani mara nyingi huyu mkuu wetu alikuwa haitikii salamu na sisi tulikwisha mzoea.

Kwa takriban dakika kumi Kanali Mjaka aliendelea kuzama kwenye taarifa alizozisoma kwenye kile kishkwambi chake pasipo kunitazama au hata kunieleza chochote jambo lililoniacha njia panda. Kwa jinsi ukimya ulivyokuwa umetawala mle ofisini nilitambua kuwa hali ile haikutokana na uzito wa taarifa aliyokuwa akiipitia kwenye kile kishkwambi bali ilitokana tu na dharau zake. “Wana tabu sana hawa watu wafupi!” Niliwaza.

Nikiri kuwa sikuwa nikimchukia kabisa huyu Mpemba, badala yake nilimu-admire sana kutokana na rekodi yake iliyotukuka ya utendaji kazi wake ndani ya Idara ya Ujasusi. Hata hivyo hiyo haikuondoa ukweli kuwa Kanali Mjaka alikuwa mmoja kati ya watu waliojisikia sana na waliokuwa na dharau nyingi katika hii dunia! Pengine ni kwa sababu ya nafasi yake ndani ya Idara ya Ujasusi, rekodi yake na usomi wake.

Baada ya dakika zile kumi za ukimya mzito ndani ya ile ofisi nilianza kukosa uvumilivu na fundo la chuki lilianza kunikaba kooni, nikiwa bado njia panda mara mlango wa ofisi ile ukagongwa mara moja na mgongaji huyo akaufungua na kuingia pasipo kusubiri kukaribishwa, kwani hata kama angegonga mara mia moja asingejibiwa. Nikageuza shingo yangu kutazama kule mlangoni na hapo nikamwona mwanadada mmoja mrefu na mweupe mwenye haiba ya kuvutia akiingia.

Sura yake ilikuwa ndefu na macho makubwa ya kike halafu malegevu. Pua yake ilikuwa ndefu na mdomo wake ulikuwa na kingo pana na alikuwa na vishimo vidogo mashavuni mwake. Nywele zake nyeusi ndefu na laini alikuwa amezifunga kwa nyuma na alikuwa amevaa fulana nyepesi nyeupe iliyoyaficha vyema matiti yake imara yenye ukubwa wa wastani na juu yake alikuwa amevaa suti, shati na suruali, ya kitambaa very expensive cha dengrizi ya rangi ya bluu mpauko brand ya Brunello Cucinelli.

Kiuno chake kilikuwa chembamba kiasi chenye misuli imara kikiwa kimeizuia suruali yake na miguuni alikuwa amevaa buti ngumu nyeusi za ngozi. Mgongoni alikuwa amebeba begi dogo jeusi la safari, ambalo bila shaka lilikuwa na vifaa vyake vyote muhimu kwa kazi za kijasusi.

Kwa sekunde chache macho yangu yalikataa kabisa kuamini kuwa taswira ya mrembo yule aliyeingia iliyokuwa mbele ya macho yangu ilimwakilisha ofisa usalama aliyekuwa na mbinu na ujuzi wa hali ya juu katika kazi za kijasusi na komando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania… Luteni Daniella Palangyo.

Asubuhi hii Daniella alikuwa katika mwonekano wa kupendeza ulioanza kuichanganya akili yangu na kuamsha hisia fulani zisizoelezeka mwilini mwangu. Mtikisiko wa umbo lake refu na zuri la kike wakati akizitupa hatua zake kama mlimbwende aliyekuwa kwenye jukwaa la kugombe taji la dunia, akija pale nilipoketi ulizidisha hisia zangu na hamu ya kutaka kubanjuka naye, ili nione kama uzuri ule ulikuwa hadi ndani au nje tu. Maana isijekuwa uzuri wa mkakasi ndani gome la mti!

“Daniella!” nilijikuta nikimwita kwa mshangao uliochanganyika na furaha na kusahau kabisa, kwa muda, kama nilikuwa nimechukizwa na tabia ya Kanali Mjaka.

“Jason!” Daniella naye aliniita kwa mshangao huku akiharakisha kuja pale nilipoketi na kunikumbatia kwa furaha. Tukakumbatiana.

Endelea...
 
utata.JPG

342

Katika hali ile ya kukumbatiana ikazifanya pua zangu zilakiwe na harufu nzuri ya manukato aliyojipulizia mwilini mwake, ambayo sikuyajua jina lake lakini yalikuwa manukato yenye kuhamasisha ngono… dah, sikuwa na uhakika na hilo lakini ndivyo akili zangu zilivyoniambia. Tuliendelea kukumbatiana kwa sekunde kadhaa huku kila mmoja akionekana kusahau uwepo wa mkuu wetu, Kanali Mjaka, mle ofisini.

Kisha Daniella aliniachia na kunitazama kwa umakini usoni kama mama amtazamaye mwanawe aliyekuwa amepotezana naye kwa miaka mingi. Nilipomtazama usoni nikagundua kuwa alikuwa analengwalengwa na machozi, ya furaha.

“Nimefurahi sana kukukuta hapa, Jason,” Daniella alisema na kushusha pumzi, kisha akaonekana kama kashtuka na kumtazama Kanali Mjaka. Akamsalimia kwa adabu.

Kama kawaida yake, Kanali Mjaka hakuhangaika kumjibu na badala yake alimwashiria kwa mkono kuwa avute kiti aketi, yeye akaendelea kutazama katika kile kishkwambi chake pasipo hata kututazama. Mimi na Daniella tukatazamana na kutabasamu.

“Habari za makao makuu Dodoma?” Daniella aliniuliza huku akizitazama nguo zangu kwa udadisi jinsi zilivyochafuka.

“Za Dodoma si mbaya lakini si nzuri kabisa!” nilijibu kwa kifupi huku nikishusha pumzi. Nilijua kuwa tayari alikwisha pata taarifa ya kile kilichokuwa kimetokea jijini Dodoma.

“Nimesoma mtandaoni kuhusu kilichotokea usiku wa kuamkia leo pale Capital Social Club, wengi wanachukulia tukio lile la club hiyo kupuliwa kwa mabomu kuwa la kigaidi. Unadhani inaweza kuwa hivyo?” Daniella aliniuliza huku akinitazama usoni kwa umakini.

“Sina uhakika lakini nina hisia hizo hizo…” nilisema.

“Kwa kuwa ulikuwa Dodoma, unaweza kuwa umenusa chochote?” Daniella aliniuliza tena.

Nilitingisha kichwa changu taratibu huku nikivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu na kukunja sura yangu huku nikimtazama Daniella kwa umakini zaidi. “By the way, niliambiwa na wewe ulikuwa mbioni kuja Dodoma.”

“Ilikuwa nije leo jioni, lakini…” Daniella alisema kisha akasita baada ya kumsikia Kanali Mjaka akikohoa kama ishara kututaka tunyamaze na tumsikilize, na wakati huo huo akisafisha koo lake, sote tukamtazama huku umakini wote tukiuhamishia kwake.

“Jason! Najua utakuwa unafahamu vizuri kuhusu kilichotokea Dodoma usiku wa kuamkia leo na unaweza kuwa na maelezo mazuri ya kutusaidia kujua chanzo cha tukio hilo, na pengine tayari unazo fununu za uvundo somewhere. Kwa kweli kilichotokea Dodoma kimeishtua sana Idara na serikali na hata dunia, maana ni ndani ya miezi mitatu tu nchi yetu inayoaminika kuwa kisiwa cha amani inakumbwa na matukio mawili makubwa ya kigaidi…” Kanali Mjaka alisema na kufanya nywele zangu zisimame kwa kauli yake. “Japo hatujapata taarifa rasmi lakini tukio la Dodoma limesababisha idadi kubwa ya watu kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa…”

Mara moja akili yangu ikarejea jijini Dodoma, nikawakumbuka akina Almasi, Sofia na Amanda, na kujiuliza iwapo walikuwa miongoni mwa watu waliopoteza maisha au wao walikuwa wamesalimika? Hata hivyo sikuwa tayari kupokea taarifa zozote mbaya kumhusu Almasi, au Sofia, wala Amanda ambaye nilikuwa nimemfahamu kwa muda mfupi sana.

Nikiwa bado nawaza Kanali Mjaka akanitaka nimweleze kwa mapana kuhusiana na tukio lile la Dodoma na jinsi nilivyolifahamu. Kwa uangalifu mkubwa nilimweleza nikianzia tangu mimi na rafiki zangu tulipotoka nyumbani kwa Almasi, mkurugenzi wa jiji, tukaelekea Maisha Club kabla ya kuondoka hapo na kwenda Capital Social Club, na jinsi nilivyoanza kumtilia shaka mtu mmoja na baadaye nikapambana naye kule chooni, na hadi nilipotoka nje ya club yakatokea yale yaliyotokea.

Baada ya maelezo hayo nikamweleza Kanali Mjaka jinsi nilivyoingiwa na shaka kuwa huenda mimi ndiye niliyekuwa mlengwa wa tukio lile la kigaidi, lakini pia namna nilivyoshangazwa baada ya kugundua kuwa watu wote waliokuwa wakinikaribia walikuwa wanauawa kimya kimya, hii ilimaanisha kuwa kulikuwa na mtu au watu walioufahamu mpango mbaya dhidi yangu na hivyo walikuwa wakinilinda!

“Bahati mbaya sana mpaka sasa hivi niongeapo bado sina hata fununu ya nini lilikuwa kusudio la watu waliofanya tukio hilo la kigaidi, na nani aliyekuwa akinilinda,” nilisema na kushusha pumzi.

Muda wote wakati naelezea kuhusu tukio lile la Dodoma, Kanali Mjaka na Daniella walikuwa kimya wakinitazama kwa mshangao mkubwa. Kisha Kanali Mjaka alishusha pumzi. “Duh! Pole sana…” alisema na kuendelea, “Lakini hili si jambo nililokuitia hapa. Kuna kazi nyingine kubwa sana ya kufanya, ambayo hatujui, huenda inaweza kuwa na link na tukio hilo.”

Kanali Mjaka alisema na hapo akili yangu ikaanza kuwaza mbali, nilijiuliza ni kazi gani hiyo kubwa ya kunitoa usiku usiku kwenye majukumu yangu ya kuhakikisha kuna usalama jijini Dodoma? Ndivyo tulivyofundishwa. Ilitupasa kuwaza ya mbele hata kubashiri kwa mantiki pale tulipoona kulikuwa na haja ya kufanya hivyo. Halikuwa kosa. Ila sikuweza kuwaza sana kwa maana nilipaswa kuweka akili na masikio yangu kwenye kinywa cha mkuu wangu wa kazi.

“Hapa tuongeapo mheshimiwa Rais ametoweka usiku wa kuamkia leo na walinzi wake watatu wameuawa huku mkewe akijeruhiwa na kukimbizwa hospitali…” Kanali Mjaka alisema kisha akanyamaza akitutazama kwa zamu mimi na Daniella kwa namna ya kutusoma.

Ilikuwa habari mbaya sana iliyonijia ghafla asubuhi ile, kama pigo la kisu ambalo lilipenya mwilini na kuujeruhi moyo wangu. Kati ya yote niliyoyatarajia asubuhi hii baada ya kuitwa haraka ofisini na mkuu wangu, jambo hili, la kutoweka kwa Rais, halikuwamo kabisa akilini mwangu. Kwa jumla, taarifa hii ilikuwa kama ni yenye kunisimanga au kunidhihaki. Nilikuwa nimeshtushwa sana, lakini nilipomtupia jicho Daniella nikamwona akiwa hana mshtuko ila alikuwa makini sana kumsikiliza Kanali Mjaka. Na hapo nikatambua kuwa tayari alishakuwa na taarifa hizo.

“…alikuwa kwenye ziara ya siku tatu katika mikoa ya Lindi na Mtwara, na kesho Jumatatu ilikuwa amalize ziara yake na kisha aelekee jijini Dodoma kujiandaa kuwakaribisha marais wenzake wa Nchi za Commonwealth kwa mkutano wa Ijumaa, lakini mpaka sasa tuongeapo hatujui yuko wapi! Ila tunajua kuwa ametekwa,” Kanali Mjaka alisema kwa huzuni.

Kauli hiyo ilitosha kunitoa macho kwa mshangao. Nikajitengeneza vyema kwenye kiti changu na kumtazama tena Daniella, ambaye muda wote alikuwa mtulivu sana. Hata hivyo kupitia macho yake niligundua kuwa mawazo yake yalikuwa yamebeba kisasi na ghadhabu na yalionesha kuwa mbali na kile chumba.

“Taarifa za kutoweka kwa Rais zimeshatangazwa?” nilimuuliza Kanali Mjaka kwa wasiwasi.

“Hapana. Taarifa haijatangazwa rasmi lakini hatutaweza kuficha kwa muda mrefu, lazima tu itajulikana…” Kanali Mjaka alisema kisha akanyamaza tena na kututazama mimi na Daniella kwa zamu, halafu akaendelea, “Makao makuu ya Idara ya Ujasusi yametupa sisi kazi ya kumtafuta Rais, lakini wamekwenda mbali zaidi kwa kutaka ninyi wawili ndiyo mwende Mtwara na popote mnakodhani Rais anaweza kuwepo mkamtafute. Kama amekufa muuletee hapa mwili wake, ila msisahau vichwa vya wote waliohusika!”

Endelea...
 
utata.JPG

343

Kwa sekunde kadhaa nilihisi ubaridi wa aina yake ukinitambaa mwilini na moyo wangu ukiyasahau mapigo yake na yaliporudi nikavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu.

“Kwa taarifa yenu, hamkuteuliwa ninyi wawili kwa sababu nyingine yoyote ila ni baada ya kuwekwa kwenye mizani na kuonekana mnafaa kwa kila hali. Kwa sababu hiyo mkurugenzi mkuu ana uhakika wa kuona kazi ikitendeka kwa weledi na kwa kufuata misingi na kanuni za Idara ambayo imewaamini kuwabebesha jukumu hili. Ni wajibu wenu kudhihirisha kwamba hatujakosea kuwaamini,” Kanali Mjaka aliongeza.

Mimi na Daniella tulitazamana, na macho yetu yalipokutana niliweza kutambua kuwa muda huu Daniella hakuwa na macho ya kawaida. Nilikuwa na hakika niliona kitu katika macho yake, kitu kisichoelezeka, kitu kilichoonesha waziwazi yeye ni nani katika dunia hii. Macho ambayo yalikuwa na dalili zote za kwamba alikuwa na nia, sababu na uwezo wa kuifanya kazi ile. Nikashusha pumzi.

Kisha Kanali Mjaka alitueleza kwa kirefu kirefu kazi tuliyokuwa tunapaswa kuifanya, na namna tulivyotakiwa kuifanya. Mengi ya maelezo yake yalirejea Amri ya Kazi (Operation Order).

“Jambo la muhimu mnalotakiwa kufanya kwa weledi wa hali ya juu ni kuangalia nyendo za maofisa wote mtakaowakuta huko Mtwara na kufanya nao kazi ili kutambua endapo kuna wasaliti. Ni jukumu letu kufanya hivyo, na kwa umakini wa hali ya juu ili tusije tukachezwa shere halafu tukaaibika,” Kanali Mjaka alisisitiza.

Mimi na Daniella tulitazamana tena kisha kwa pamoja tukabetua vichwa vyetu kukubaliana na maneno yake.

“Jambo lingine ni kwamba mmeruhusiwa kufanya, ingawa mnatakiwa kuwa makini sana, ni ku-recruite informers mtakaodhani wanafaa kuwasaidia katika kazi yenu…”

Hayo na mengine mengi tuliyoeelezwa na mkuu wetu wa kikosi yalituingia vyema na kututia hamasa ipasavyo. Tulimwahidi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuijengea nchi yetu heshima. Kwa ujumla hakuna kati yetu aliyeonesha wasiwasi wa kubeba mzigo tuliobebeshwa.

Sote tulikuwa tumepitia mafunzo ya kijeshi yanayojumuisha matumizi ya silaha za moto, mbinu za kujilinda kwa mikono mitupu, ujasiri, ukusanyaji wa taarifa za kiitelejensia katika mazingira magumu, kuajiri watoa habari, kufanya upelelezi wa kipolisi, uchunguzi wa maeneo ya tukio, na sheria ya ushahidi. Kwa kifupi tulikuwa tumekamilika.

“Je, kuna taarifa zozote za awali za kutusaidia kujua wapi pa kuanzia kazi yetu?” nilimuuliza Kanali Mjaka.

“Kuna taarifa kwenye ofisi ya RSO wa Mtwara kuhusu kuhusishwa kwa maofisa watatu, mmoja ni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wawili ni vijana wetu kutoka Idara ya Ujasusi, kuwa washukiwa wa tukio hilo. Watu hawa wametoweka na hawajulikani walipo na sasa Idara ya Usalama wa Taifa kwa kushirikiana na Polisi imewatawanya maofisa katika kila sehemu ambayo tunadhania kuwa wanaweza kuwepo. Tumeweka vizuizi katika njia zote zinazoingia na kutoka Mtwara na hivyo kufanya suala la wao kutoka ndani ya mkoa huo kuwa gumu,” Kanali Mjaka alisema.

Kanali alitueleza hatua zaidi zilizokuwa zimechukuliwa, kuwa utaratibu wa haraka ulikuwa umefanyika baada tu ya kupata taarifa za kutoweka kwa Rais kwa kudhibiti mipaka yote (entry points) ili watu waliofanya tukio lile wasiweze kuvuka kwa urahisi. Na pia hatua zaidi zilichukuliwa baada ya taarifa za tukio la jijini Dodoma ambapo iliagizwa kucheleweshwa kwa ndege za abiria katika viwanja vya ndege vyote nchini ili kuwapa maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na Polisi muda wa kufanya upekuzi wa ziada kwa abiria waliokuwa wanaondoka nchini.

“Maadui wa nchi yetu wamegundua Tanzania inatamba kwa amani hali inayosaidia kwa kiasi kikubwa kupata maelfu ya watalii katika mbuga za wanyama na vivutio vingine vilivyoko nchini. Tukio la Dodoma na hata hili la Mtwara yana lengo la kutia doa nchi yetu na kushusha si tu biashara ya utalii lakini pia heshima ya nchi hii na kuyafanya mataifa megine yatudharau na idhaniwei kuwa sasa Tanzania si mahali salama, hivyo mkutano wa Commonwealth uliopangwa kufanyika nchini upelekwe katika nchi nyingine…” Kanali Mjaka alisema kwa huzuni.

Kikao chetu kilichukua muda wa dakika hamsini tu na mwisho Kanali Mjaka alitukabidhi hati ya maagizo ya kazi tuliyotakiwa kuishughulikia kama alivyokuwa ameelekeza. Hati hiyo iliyojulikana kama ‘SIMU’ ilikuwa imeletwa kwa mfuko maalumu (private bag) kutoka makao makuu ya Idara ya Ujasusi ikiwa imefungwa katika mafumbo (codes).

Hati tuliyopewa haikuwa nyingine bali ilikuwa na maagizo yale yale maalumu tuliyopaswa kuyashughulikia ili kufanikisha kazi ile ngumu na ya hatari ya kumtafuta Rais, ambayo ilianza kuniumiza kichwa kabla hata sijaianza. Ni hati ambayo ilimaanisha kuwa tulikuwa tumepata kibali maalumu kutoka kwa mkurugenzi mkuu wa Idara ya Ujasusi kufanya chochote tulichodhani kingetusaidia kumpata Rais, hata kama ni kuua.

Licha ya umachachari wangu hakuna kitu kigumu kilichokuwa kikinisumbua siku zote kama mwanzo. Nilikuwa naumiza sana kichwa changu na wakati mwingine kuichukia kazi yenyewe nilipokuwa katika kuusaka mwanzo wa kitu chochote kile. Safari hii tena nilikuwa nimeingizwa katika kuutafuta mwanzo wa mkasa huu wenye utata… dah, damu ilianza kunichemka na kwenda mbio kwenye mishipa yangu ya damu.

“Sasa nendeni ofisini kwa katibu muhtasi kuna ofisa atawapa OP na usafiri wa kuwafikisha mahali popote mnapotaka na kisha atawapeleka airport. Mnatakiwa kuondoka saa nne asubuhi hii kwa ndege maalumu kwenda Mtwara, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa itakuwa inawasubiri kiwanjani… naomba operesheni hii ifanyike haraka sana, mheshimiwa Rais apatikane, akiwa hai au mwili wake, kabla ya Ijumaa na wote waliofanya hivi wapatikane,” Kanali Mjaka alimaliza na kuturuhusu kuondoka.

Tuliinuka na kupiga saluti kisha tukatoka ndani ya ofisi ya mkuu wa kikosi, tukaelekea ofisini kwa katibu muhtasi wake, Bi Aziza Msojo. Daniella alitangulia na alikuwa akitembea kwa ukakamavu tofauti na alivyoingia. Pale ofisini kwa katibu muhtasi tulimkuta ofisa mmoja akisubiri. Aziza alipotuona tu akamweleza jambo na hapo tukamwona akisimama halafu akatusalimia na kujitambulisha jina lake, nasi tukamfahamisha majina yetu.

“Mkuu ameniagiza niwape hizi OP na usafiri wa kuwafikisha mahali popote mnapotaka kwenda,” yule ofisa alitueleza huku akitukabidhi bahasha nyeupe za OP (operation fund), kila mmoja ya kwake. Bahasha zile zilikuwa zimeandikwa majina yetu. OP ni neno la ki-idara lenye maana ya “fedha za kufanyia kazi”.

Na bila kupoteza muda tulimuaga Aziza na kufuatana na yule ofisa kuelekea kwenye gari maalumu lililoandaliwa kwa ajili yetu, tukakubaliana kuwa gari litupeleke kwanza nyumbani kwangu Upanga nikajiandae kwa safari kwa kuwa Daniella alikuwa tayari amekwisha jiandaa na safari ile kwa kuchukua vitu vyake muhimu.

“…au wewe unaonaje?” Daniella aliniuliza kwa sauti tulivu ya chini wakati tukiwa tumeketi kwenye viti vya nyuma ndani ya gari aina ya Mercedes Benzi jeupe lenye vioo vyeusi.

Kwa kweli sikujua ni nini Daniella alikuwa ametoka kuongelea kwa kuwa wakati huo mawazo yangu yalikuwa mbali sana. Nilikuwa na mambo mengi yaliyonitatanisha, kwanza ilikuwa kuhusu tukio la Dodoma ambalo hadi muda ule lilikuwa limeniacha na sintofahamu. Pia nilijaribu kuwaza ni akina nani waliokuwa na uthubutu wa kufanya tukio kubwa kama kumteka Rais ambaye alikuwa na ulinzi wa hali ya juu!

Nilimtazama kwa mshangao huku nikiitika kuonesha kuwa sikuwa nimemsikia, yeye akanitazama kwa namna ambayo iliniacha kabisa njia panda, kisha akaachia tabasamu ambalo pia sikuelewa lilikuwa na maana gani. Uzoefu wangu kwa wanawake wa aina yake ukaniacha njia panda.

* * *

Dah, sasa kila kitu ni utata mtupu, ilianza Dodoma na sasa Mtwara, sijui nini kitafuata. Usikose kufuatilia...
 
View attachment 2403656
343

Kwa sekunde kadhaa nilihisi ubaridi wa aina yake ukinitambaa mwilini na moyo wangu ukiyasahau mapigo yake na yaliporudi nikavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu.

“Kwa taarifa yenu, hamkuteuliwa ninyi wawili kwa sababu nyingine yoyote ila ni baada ya kuwekwa kwenye mizani na kuonekana mnafaa kwa kila hali. Kwa sababu hiyo mkurugenzi mkuu ana uhakika wa kuona kazi ikitendeka kwa weledi na kwa kufuata misingi na kanuni za Idara ambayo imewaamini kuwabebesha jukumu hili. Ni wajibu wenu kudhihirisha kwamba hatujakosea kuwaamini,” Kanali Mjaka aliongeza.

Mimi na Daniella tulitazamana, na macho yetu yalipokutana niliweza kutambua kuwa muda huu Daniella hakuwa na macho ya kawaida. Nilikuwa na hakika niliona kitu katika macho yake, kitu kisichoelezeka, kitu kilichoonesha waziwazi yeye ni nani katika dunia hii. Macho ambayo yalikuwa na dalili zote za kwamba alikuwa na nia, sababu na uwezo wa kuifanya kazi ile. Nikashusha pumzi.

Kisha Kanali Mjaka alitueleza kwa kirefu kirefu kazi tuliyokuwa tunapaswa kuifanya, na namna tulivyotakiwa kuifanya. Mengi ya maelezo yake yalirejea Amri ya Kazi (Operation Order).

“Jambo la muhimu mnalotakiwa kufanya kwa weledi wa hali ya juu ni kuangalia nyendo za maofisa wote mtakaowakuta huko Mtwara na kufanya nao kazi ili kutambua endapo kuna wasaliti. Ni jukumu letu kufanya hivyo, na kwa umakini wa hali ya juu ili tusije tukachezwa shere halafu tukaaibika,” Kanali Mjaka alisisitiza.

Mimi na Daniella tulitazamana tena kisha kwa pamoja tukabetua vichwa vyetu kukubaliana na maneno yake.

“Jambo lingine ni kwamba mmeruhusiwa kufanya, ingawa mnatakiwa kuwa makini sana, ni ku-recruite informers mtakaodhani wanafaa kuwasaidia katika kazi yenu…”

Hayo na mengine mengi tuliyoeelezwa na mkuu wetu wa kikosi yalituingia vyema na kututia hamasa ipasavyo. Tulimwahidi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuijengea nchi yetu heshima. Kwa ujumla hakuna kati yetu aliyeonesha wasiwasi wa kubeba mzigo tuliobebeshwa.

Sote tulikuwa tumepitia mafunzo ya kijeshi yanayojumuisha matumizi ya silaha za moto, mbinu za kujilinda kwa mikono mitupu, ujasiri, ukusanyaji wa taarifa za kiitelejensia katika mazingira magumu, kuajiri watoa habari, kufanya upelelezi wa kipolisi, uchunguzi wa maeneo ya tukio, na sheria ya ushahidi. Kwa kifupi tulikuwa tumekamilika.

“Je, kuna taarifa zozote za awali za kutusaidia kujua wapi pa kuanzia kazi yetu?” nilimuuliza Kanali Mjaka.

“Kuna taarifa kwenye ofisi ya RSO wa Mtwara kuhusu kuhusishwa kwa maofisa watatu, mmoja ni wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wawili ni vijana wetu kutoka Idara ya Ujasusi, kuwa washukiwa wa tukio hilo. Watu hawa wametoweka na hawajulikani walipo na sasa Idara ya Usalama wa Taifa kwa kushirikiana na Polisi imewatawanya maofisa katika kila sehemu ambayo tunadhania kuwa wanaweza kuwepo. Tumeweka vizuizi katika njia zote zinazoingia na kutoka Mtwara na hivyo kufanya suala la wao kutoka ndani ya mkoa huo kuwa gumu,” Kanali Mjaka alisema.

Kanali alitueleza hatua zaidi zilizokuwa zimechukuliwa, kuwa utaratibu wa haraka ulikuwa umefanyika baada tu ya kupata taarifa za kutoweka kwa Rais kwa kudhibiti mipaka yote (entry points) ili watu waliofanya tukio lile wasiweze kuvuka kwa urahisi. Na pia hatua zaidi zilichukuliwa baada ya taarifa za tukio la jijini Dodoma ambapo iliagizwa kucheleweshwa kwa ndege za abiria katika viwanja vya ndege vyote nchini ili kuwapa maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na Polisi muda wa kufanya upekuzi wa ziada kwa abiria waliokuwa wanaondoka nchini.

“Maadui wa nchi yetu wamegundua Tanzania inatamba kwa amani hali inayosaidia kwa kiasi kikubwa kupata maelfu ya watalii katika mbuga za wanyama na vivutio vingine vilivyoko nchini. Tukio la Dodoma na hata hili la Mtwara yana lengo la kutia doa nchi yetu na kushusha si tu biashara ya utalii lakini pia heshima ya nchi hii na kuyafanya mataifa megine yatudharau na idhaniwei kuwa sasa Tanzania si mahali salama, hivyo mkutano wa Commonwealth uliopangwa kufanyika nchini upelekwe katika nchi nyingine…” Kanali Mjaka alisema kwa huzuni.

Kikao chetu kilichukua muda wa dakika hamsini tu na mwisho Kanali Mjaka alitukabidhi hati ya maagizo ya kazi tuliyotakiwa kuishughulikia kama alivyokuwa ameelekeza. Hati hiyo iliyojulikana kama ‘SIMU’ ilikuwa imeletwa kwa mfuko maalumu (private bag) kutoka makao makuu ya Idara ya Ujasusi ikiwa imefungwa katika mafumbo (codes).

Hati tuliyopewa haikuwa nyingine bali ilikuwa na maagizo yale yale maalumu tuliyopaswa kuyashughulikia ili kufanikisha kazi ile ngumu na ya hatari ya kumtafuta Rais, ambayo ilianza kuniumiza kichwa kabla hata sijaianza. Ni hati ambayo ilimaanisha kuwa tulikuwa tumepata kibali maalumu kutoka kwa mkurugenzi mkuu wa Idara ya Ujasusi kufanya chochote tulichodhani kingetusaidia kumpata Rais, hata kama ni kuua.

Licha ya umachachari wangu hakuna kitu kigumu kilichokuwa kikinisumbua siku zote kama mwanzo. Nilikuwa naumiza sana kichwa changu na wakati mwingine kuichukia kazi yenyewe nilipokuwa katika kuusaka mwanzo wa kitu chochote kile. Safari hii tena nilikuwa nimeingizwa katika kuutafuta mwanzo wa mkasa huu wenye utata… dah, damu ilianza kunichemka na kwenda mbio kwenye mishipa yangu ya damu.

“Sasa nendeni ofisini kwa katibu muhtasi kuna ofisa atawapa OP na usafiri wa kuwafikisha mahali popote mnapotaka na kisha atawapeleka airport. Mnatakiwa kuondoka saa nne asubuhi hii kwa ndege maalumu kwenda Mtwara, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa itakuwa inawasubiri kiwanjani… naomba operesheni hii ifanyike haraka sana, mheshimiwa Rais apatikane, akiwa hai au mwili wake, kabla ya Ijumaa na wote waliofanya hivi wapatikane,” Kanali Mjaka alimaliza na kuturuhusu kuondoka.

Tuliinuka na kupiga saluti kisha tukatoka ndani ya ofisi ya mkuu wa kikosi, tukaelekea ofisini kwa katibu muhtasi wake, Bi Aziza Msojo. Daniella alitangulia na alikuwa akitembea kwa ukakamavu tofauti na alivyoingia. Pale ofisini kwa katibu muhtasi tulimkuta ofisa mmoja akisubiri. Aziza alipotuona tu akamweleza jambo na hapo tukamwona akisimama halafu akatusalimia na kujitambulisha jina lake, nasi tukamfahamisha majina yetu.

“Mkuu ameniagiza niwape hizi OP na usafiri wa kuwafikisha mahali popote mnapotaka kwenda,” yule ofisa alitueleza huku akitukabidhi bahasha nyeupe za OP (operation fund), kila mmoja ya kwake. Bahasha zile zilikuwa zimeandikwa majina yetu. OP ni neno la ki-idara lenye maana ya “fedha za kufanyia kazi”.

Na bila kupoteza muda tulimuaga Aziza na kufuatana na yule ofisa kuelekea kwenye gari maalumu lililoandaliwa kwa ajili yetu, tukakubaliana kuwa gari litupeleke kwanza nyumbani kwangu Upanga nikajiandae kwa safari kwa kuwa Daniella alikuwa tayari amekwisha jiandaa na safari ile kwa kuchukua vitu vyake muhimu.

“…au wewe unaonaje?” Daniella aliniuliza kwa sauti tulivu ya chini wakati tukiwa tumeketi kwenye viti vya nyuma ndani ya gari aina ya Mercedes Benzi jeupe lenye vioo vyeusi.

Kwa kweli sikujua ni nini Daniella alikuwa ametoka kuongelea kwa kuwa wakati huo mawazo yangu yalikuwa mbali sana. Nilikuwa na mambo mengi yaliyonitatanisha, kwanza ilikuwa kuhusu tukio la Dodoma ambalo hadi muda ule lilikuwa limeniacha na sintofahamu. Pia nilijaribu kuwaza ni akina nani waliokuwa na uthubutu wa kufanya tukio kubwa kama kumteka Rais ambaye alikuwa na ulinzi wa hali ya juu!

Nilimtazama kwa mshangao huku nikiitika kuonesha kuwa sikuwa nimemsikia, yeye akanitazama kwa namna ambayo iliniacha kabisa njia panda, kisha akaachia tabasamu ambalo pia sikuelewa lilikuwa na maana gani. Uzoefu wangu kwa wanawake wa aina yake ukaniacha njia panda.

* * *

Dah, sasa kila kitu ni utata mtupu, ilianza Dodoma na sasa Mtwara, sijui nini kitafuata. Usikose kufuatilia...
Kweli ni utata,naamini utatuletea tena baadae bishop!
 
[emoji120][emoji120] ukiacha wewe uliyecomment, na wengine wawili Boogman na kitomari xxiv walio-like naona wengine wamesusa kiaina[emoji17]...
Mkuu tunakufuatilia mnooo ktk huo utata...jamaa yetu si ndio kaitwa Dar...we kamua tu tuko pamoja...mie nataka kujua ni nani aliyekuwa na bastola ya kiwambo aliyekuwa anamuokoa Sizya kutoka kwa wakola wa SMG.
 
utata.JPG

344

Hekaheka…




Saa 4:00 asubuhi…

TULIFUNGA mikanda ya viti vyetu, ndani ya ndege ya kisasa kabisa aina ya Supersonic XB-1 ya kukaa watu 15 tu, kilikuwa kikwangua anga kipya kabisa mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutoka Kikosi namba tisini na mbili (92KJ) Ngerengere. Tulikuwa tumepanga tuingie Mtwara kwa mtindo wa aina yake. Ndani ya ndege ile tulikuwemo watu wanne tu; mimi, Daniella, rubani mkuu na msaidizi wake.

Mimi na Daniella tulikuwa ndani ya mavazi tofauti na tulivyozoeleka, mimi nilitupia kanzu ghali ya rangi ya samawati, makubazi ya ngozi ya rangi nyeusi yenye mkanda katikati unaotenganisha kidole gumba na vidole vingine na kichwani nilivalia kofia ya kushonwa na mkono ya rangi nyeusi, bila kusahau tasbihi ya rangi ya kijani niliyokuwa nikiichezesha chezesha mkononi. Ungeniona ungedhani nilikuwa Shekhe wa Mkoa fulani mwenye unyenyekevu na utiifu mkubwa kwa Mola wangu. Haha!

Daniella yeye alitupia hijabu moja matata sana iliyomfunika na kuacha sehemu ndogo ya uso tu, na kutokana na rangi yake ungeweza kudhani alikuwa Mwarabu kutoka Oman. Chini alivaa viatu fulani vyeusi visivyo na visigino, vilikuwa viatu simple tu. Kama ungebahatika kutuona ungedhani ni Ustadh na Ustadhat.

Tulifanya hivi kwa kuwa kabla hatujatoka nyumbani kwangu kuelekea Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) tayari machale yalishatucheza, tukajionya kusafiri kikawaida kwa kujiamini hasa kutokana na tukio lenyewe la kutekwa Rais ambaye alikuwa na ulinzi wa hali ya juu, hizo zilikuwa ni salamu kwetu na kwa yeyote ambaye angefuatilia jambo hilo kuwa tulikuwa tunapambana na genge kubwa la waharifu ambao walikuwa na ujuzi na maarifa makubwa.

Hivyo tuliamua kubadilisha mwonekano wetu, kabla hatujaenda nyumbani kwangu Upanga tulipitia kwanza Kariakoo, Msikiti wa Kwamtoro ambao upo karibu na Soko Kuu la Kariakoo, hapo tukanunua mavazi hayo. Halafu hatukuishia hapo tu, pia tulibadili mawazo, badala ya kwenda moja kwa moja Mtwara tulikata shauri ya kuishukia Lindi halafu kutoka hapo tungeenda kwa njia ya barabara hadi Mikindani.

Kabla hatujaianza safari yetu Daniella alikuwa amewasiliana na rafiki yake, Kapteni Cassian Luhanga, aliyekuwa katika kituo cha kazi hapo Lindi, na kumwomba msaada wa kutupatia gari ambalo lingetufikisha Mtwara kwenye kazi fulani maalumu.

Ilikuwa ni safari ya dakika 25 tu kutoka jijini Dar es Salaam mpaka kwenye Kiwanja cha Ndege cha Lindi-Kikwetu katika eneo la Mbaja nje kidogo ya Mji wa Lindi. Tulikubaliana na marubani wa ndege yetu kufanya jambo hilo kuwa siri yetu. Tuliposhuka tukafanya haraka kutoka nje ya kiwanja, hatukuwa na muda wa kupoteza, nje ya kiwanja kile tulimkuta Kapteni Luhanga tayari amekwisha fika hapo kiwanjani kutupokea.

Kwanza hakuweza kumtambua Daniella kutokana na mavazi aliyovaa hadi pale alipoguswa bega na kisha Daniella akamsemesha ndipo aliposhtuka na kututazama kwa mshangao mkubwa.

“Kapteni Luhanga, kutana na rafiki’angu Jason Sizya ambaye pia ni mwenzetu,” Daniella alianza utambulisho bila kuchelewa kwani tayari Kapteni Luhanga alikwisha anza kunitumbulia macho yaliyojaa maswali.

“Jason, kutana na Kapteni Luhanga. Huyu ni rafiki yangu, kuna wakati tulikuwa idara moja kule 92 KJ, Ngerengere. Kwa hivi sasa yeye yupo hapa Lindi,” Daniella akaniambia.

Mimi na Kapteni Luhanga tulisalimiana kwa kushikana mikono halafu Kapteni Luhanga akatuongoza alikoacha gari lake aina ya Nissan Patrol la Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Kwenye gari lile tulimkuta dereva aliyekuwa na cheo cha Koplo, tukamsalimia na kisha tukaingia ndani ya gari na safari ya kuelekea Mtwara ikaanza. Niliitazama saa yangu nikagundua kuwa ilikuwa imeshatimia saa nne na nusu juu ya alama.

Na hapo nikakumbuka kumpigia tena simu mke wangu Rehema kumjulisha kuwa nilikuwa nimefika salama na kuanzia muda huo nisingepatikana kwenye namba ile simu kwa sababu za kiusalama. Nilipomaliza nikaizima simu yangu na kuchomoa miwani yangu yenye vioo vya giza, nikaifuta kwa kitambaa laini na kuivaa kuzidi kuficha wajihi wangu.

Daniella naye akaizima simu yake, maana ndivyo tulivyokuwa tumekubaliana ili hata tukitafutwa tusiweze kupatikana hadi pale ambapo tungekuwa tumeshafika Mtwara na kujipanga.



Mimi na Daniella tukiwa amekaa viti vya nyuma ndani ya lile gari macho yetu yalikuwa makini kuangaza huku na kule kupitia vioo ya madirishani ili mradi kuchunga usalama wetu. Hakutaka kuanza kupoteza mpambano mbele ya adui zetu hata kabla bado mechi haijaanza.

Wakati safari ikiendelea nilikuwa nikimtazama Daniella kwa kuibia maana… japokuwa tulikuwa tukienda kwenye kazi ngumu na ya hatari lakini tamaa yangu juu mwili wa Daniella haikunitoka kabisa. Ukweli Daniella alikuwa na uzuri wa shani. Ilikuwa vigumu hata kumwelezea. Nilibakia kumsifu Mungu kwa uumbaji wake huu uliotukuka.

Kwa mwendo wa gari letu tulitumia saa moja na dakika therathini tu tukawa tumeshawasili Mikindani, tukiwa tumesafiri umbali wa kilomita 115 kutoka Kiwanja cha Ndege cha Lindi hadi hapo Mikindani, eneo lililokuwa kilomita kumi tu kabla ya kuingiaa Mtwara Mjini.

Hapo Mikindani tuliachana na Kapteni Luhanga na mara tu gari lile la jeshi lilipoondoka kurudi Lindi tukakodi bodaboda tukikaa mshikaki na kumweleza dereva atupeleke Naf Beach Hotel, Mtwara Mjini. Ilituchukua dakika 28 kufika kwenye hoteli ya Naf yenye hadhi ya nyota 3 iliyokuwa ufukweni katika makutano ya Barabara za Chuno na Mailimoja, na Mtaa wa Duara.

Hoteli ilikuwa na ghorofa tatu na eneo kubwa lililopakana na majengo ya VETA Mtwara. Tulidhani kuwa mahali hapo pangetufaa. Tukamalizana na dereva wa bodaboda kisha tukatokomea ndani ya jengo la hoteli hiyo. Bahati nzuri tulipata chumba kimoja kilichokuwa na vitanda viwili bila shida yoyote, katika ghorofa ya kwanza. Tukajiandikisha kama Mr & Mrs Halfan Jongo kutoka Bagamoyo.

Tulichukua chumba kimoja makusudi japokuwa tulitambua hatari ya kufanya hivyo endapo adui angegundua maficho yetu, na kupiga ndege wawili kwa jiwe moja.

Tulipolipia chumba chetu tu, tukaanza kunusa nusa kama mbwa wa polisi, kuikagua nyumba nzima ili kujiridhisha usalama wake. Kwa kufanya vile tuliweza kugundua kuwa ndani ya jengo lile kulifungwa mfumo wa kamera za ulinzi (CCTV) uliokuwa unarekodi matukio yote hapo hotelini. Tukaangaliana na kujikuta tukitabasamu kisha tukaingia chumbani kwetu kuweka vitu vyetu na kuweka vitu sawa chumbani.

Humo chumbani nako tulijipa kama dakika 10 za kukagua usalama wa chumba hicho, tukihofia tusije tukawa tumejiingiza kwenye mdomo wa mamba bila wenyewe kujua na kisha tukaja kulia kilio cha kusaga na meno.

Na baada ya kujiridhisha na usalama wa eneo lile, tulibadilisha mavazi na kuvaa suti maridadi kisha tukatoka na kuelekea katikati ya Mji wa Mtwara, Barabara ya Tanu, zilipokuwa ofisi za Mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa wa Mtwara (Regional Security Officer - RSO), maana hatukuwa na muda wa kupumzika. Tulitakiwa kuwashtukiza adui zetu mapema kabla hawajatushtukia na kasheshe kuanza.

_____


Endelea...
 
utata.JPG

345

Dakika kumi baadaye tulikuwa ndani ya teksi tuliyoikodi pale hotelini Naf Beach ili itupeleke Kanisa la Pentekoste (FPCT). Hatukutaka kuelekea moja kwa moja zilipo ofisi za RSO wa Mtwara. Tulipotoka Naf Beach Hotel teksi ile ikaingia Barabara ya Mailimoja tukayavuka majengo ya Veta Mtwara, moja kwa moja hadi tulipofika mwisho wa eneo la viwanja vya Veta tukaingia kulia.

Hapo tukaendelea na barabara ile tukiivuka mitaa kadhaa iliyokatisha barabara na kwenda kukutana na Barabara ya Maendeleo iliyokuwa ikikatisha kutoka kulia kwenda kushoto, tukaingia kushoto tukiifuata barabara ile huku tukiyapita majengo kadhaa ikiwemo Shule ya Sekondari ya Shangani, hadi tulipokutana na Barabara ya Jamhuri, hapo dereva akaingia upande wa kulia akiifuata barabara ambayo sikuijua jina lake iliyotupeleka hadi kwenye Kanisa la Pentekoste (FPCT).

Hapo kanisani tulishuka na kumlipa dereva wa teksi fedha yake na tulipohakikisha ile teksi imeondoka na kupotelea mitaani, tukakodi bodaboda iliyotutoa hapo, tukaingia kushoto tukiifuata barabara moja kubwa iliyotupeleka hadi Barabara ya Tanu, na hapo ile bodaboda ikaingia kulia, tukamwelekeza yule dereva wa bodaboda sehemu ya kutushusha, jirani na majengo ya ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Mtwara.

Kutoka hapo tukavuka barabara na kuyafuata majengo fulani ya serikali, mojawapo ya majengo hayo ndipo zilipokuwa ofisi za RSO Mtwara. Wakati tukishuka toka ndani ya teksi ilikuwa imeshatimia saa nane na dakika kumi na tano za mchana. Tukaanza kukatisha viwanja vya majengo yale tukielekea eneo la mapokezi ya ofisi za RSO.

Mara tu tulipoingia eneo lile nikagundua kuwa kulikuwa na maofisa mbalimbali wakiwemo wa Usalama wa Taifa, JWTZ, Polisi na Uhamiaji walioonekana kuwa walitoka kwenye kikao kizito. Niliweza kuwatambua kutokana na sare zao za kazi. Mara macho yangu yakatua kwa mwanadada mmoja mrefu aliyevaa suti maridadi ya rangi ya zambarau iliyowiva, na mara macho yetu yalipokutana akashikwa na hamaki huku tabasamu la hakika likichomoza usoni mwake.

Nilishikwa na mduwao wa sekunde kadhaa huku nikimkodolea macho ya kutokuamini kuwa niliyekuwa nikimwona mbele yangu alikuwa mwanausalama machachari na ofisa mwenye mbinu maalumu, Pamela Mkosamali, ambaye miezi mitatu nyuma tulifanya kazi bega kwa bega katika operesheni hatari iliyokuja kuufichua mpango hatari uliokuwa umeandaliwa na mtandao hatari wa kigaidi, kama ilivyosimuliwa kwenye mkasa uitwao ‘Taharuki’.

Operesheni ambayo baada ya kuikamilisha sote watatu, mimi, Pamela na Luteni Lister tukapelekwa katika kikosi maalumu cha kushughulika na operesheni hatari (SOG) ila baada ya mwezi mmoja nikasikia kuwa Pamela alikuwa amepangiwa majukumu mengine katika sehemu nyingine, na kuanzia hapo tukawa tumepotezana na sikujua alikuwa wapi!

“Kha! Jason!” Pamela alikuwa wa kwanza kuniita kwa uchangamfu wa hali ya juu huku akiwa ameshikwa na furaha isiyoelezeka.

“Hakika ndiyo mimi. Waswahili hawakukosea waliposema milima haikutani…” nilimwambia Pamela kwa sauti tulivu huku usoni nikiumba tabasamu na nilipomfikia nikamkubatia kwa nguvu pasipo kujali macho ya mshangao kutoka kwa baadhi ya maofisa waliokuwa eneo lile.

Wengi wao walinitazama kwa makini huku dhahiri wakionekana kushindwa kunielewa. Niliwasalimia na wote wakaitikia na kuendelea na hamsini zao. Daniella pia alianza kuchangamkiana na baadhi ya maofisa, hasa wa kijeshi, aliofahamiana nao.

“Vipi mbona uko huku?” nilimuuliza Pamela kwa sauti ya chini huku nikimtazama usoni kwa mshangao.

“Kwa sasa kituo changu cha kazi kipo huku Mtwara, nina nafasi fulani nyeti kwenye Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Mtwara,” Pamela aliniambia kwa sauti ya chini huku akigeuka kuwatazama wale maofisa wengine kuona kama walikuwa wanatufuatilia.

Pamela alikuwa mjanja sana kwa kushtukia kuwa maongezi yetu eneo lile yangeweza kuvuta umakini wa maofisa wengine. Hivyo haraka akanionesha ishara kuwa niingie kwenye mlango fulani wa kioo na kwenda kumsubiri kwenye ukumbi mdogo.

Bila kupingana na wazo lake nikafanya vile na nilipokuwa nikiingia mle ndani nikamwona Daniella na maofisa wengine wakiwa bado wanazungumza. Hata hivyo nilishukuru Mungu kwa kuwa hakuna aliyejisumbua kunitazama wakati nilipokuwa nikipiga hatua zangu kwa utulivu katikati ya korido pana kuelekea kwenye ukumbi mdogo uliozungukwa na kuta kubwa za vioo uliokuwa upande wa kushoto wa lile jengo.

Ile korido niliyoingia ilikuwa ikitazamana na milango miwili ya ofisi na mwisho wa korido ile kulikuwa na ngazi za kuelekea ghorofa ya juu. Nilipofika katikati ya ile korido nikausukuma mlango ule na kuingia ndani na kutokea kwenye ukumbi mdogo wa mikutano wenye jumla ya viti kumi na nne vilivyoizunguka meza moja ndefu ya umbo mstatili. Ukumbi ule ulikuwa umezungukwa na kuta kubwa za vioo visivyoonesha waliomo ndani au nje ya ukumbi ule na mapazia marefu kwenye madirisha makubwa mawili.

Nikiwa mle ndani ya ule ukumbi niliyatembeza macho yangu taratibu kutathmini mandhari yale. Hali niliyoikuta mle ndani ilinitambulisha kuwa kulikuwa kumefanyika kikao Kizito muda mfupi tu uliokuwa umepita. Mbali na ile meza kubwa ya mikutano iliyozungukwa na viti kumi na nne kulikuwa na runinga pana iliyokuwa ukutani, projector, na picha mbili kubwa moja ya Rais Dk. Albert Masinde na ya pili ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere, zilizotundikwa ukutani. Zaidi ya vitu hivyo hakukuwa na ziada nyingine.

Niliizunguka ile meza ndefu na kuvuta kiti kimoja, nikaketi. Muda huo huo nikamwona Pamela akiingia haraka huku akiwa katika uso wenye tabasamu la bashasha, kisha akaja na kuvuta kiti akiketi mbele yangu. Hata hivyo sikuona tashwishwi yoyote usoni kwake ingawa alijitahidi kwa kila hali kutabasamu.

Pamela alikuwa msichana mzuri na mrembo mwenye umbo lenye mvuto wa aina yake lakini vile vile alikuwa mcheshi na aliyethamini sana utu.

“Habari za Dar es Salaam, Jason?” Pamela aliniuliza kwa sauti laini ya kubembeleza huku akinilegezea macho kabla ya kuangua kicheko hafifu cha kimahaba.

“Dar es Salaam ni kwema, ila mimi nilikuwa Dodoma. Nadhani umesikia kilichotokea huko?” niliongea kwa utulivu huku nikimtazama usoni.

“Dah, nimesikia. Mbona mwaka huu majanga!” Pamela aliongea kwa sauti dhaifu iliyopwaya kisha akanyamaza na kunitazama kidogo kama aliyekuwa anafikiri kitu cha kuongea. Kisha akaongeza, “Hata huku Mtwara mambo si shwari kabisa!”

“Nafahamu na ndiyo maana tupo hapa…” niliongea kwa utulivu huku nikimtazama kwa umakini usoni.

“Leo asubuhi Kanali Mjaka alinidokeza juu ya ujio wako kwa njia ya simu, kwa kweli nilifurahi sana niliposikia kuwa watu wawili wamekabidhiwa jukumu hili na mmoja wapo ni wewe. Kwa kweli najua upele umempata mkunaji na majibu yatapatikana haraka ingawa pia sitarajii kuwa kazi itakuwa nyepesi.” Pamela aliongea kwa sauti tulivu ya chini.

“Ina maana Kanali Mjaka anafahamu kuwa upo huku Mtwara?” nilimuuliza Pamela kwa udadisi huku nikimtazama usoni kwa makini.

“Kwa nini asijue wakati ni yeye ndiye aliyependekeza niletwe huku?” Pamela alisema na kushusha pumzi. “Si unajua kwa sasa kuna uhalifu mwingi sana unaendelea maeneo haya ya mpakani mwa Msumbiji!”

“Una muda gani tangu uletwe huku?” nilimuuliza Pamela huku mawazo mengi yakianza kupita kichwani mwangu.

“Takriban miezi miwili sasa…” Pamela alinijibu huku akinitazama kwa jicho la mahaba.

“Sifahamu kabisa halafu hata Kanali Mjaka hajanidokezea kabisa kama upo huku!” nilimwambia Pamela huku nikionesha mshangao.

Pamela aliachia tabasamu hafifu usoni mwake huku akinitazama kwa namna ambayo sikuweza kupata tafsiri yake mara moja, na kabla hajasema lolote mlango wa ule ukumbi wa mikutano ukafunguliwa. Ofisa mmoja, kijana wa rika langu, akachungulia na kutuona, akaachia tabasamu na kututaka radhi kwa kukatisha maongezi yetu kisha akaniambia kuwa nilikuwa nasubiriwa ofisini kwa RSO.

Endelea...
 
utata.JPG

346

Sikutaka kumkosea adabu RSO, ambaye kwa cheo cha ki-idara alinizidi mbali tu, nikaagana na Pamela huku tukikubaliana kuonana tena kisha nikainuka na kumfuata yule ofisa, akanipeleka ofisini kwa RSO. Mle ndani ya ofisi ya RSO Mtwara nilimkuta Daniella akiwa ameketi kwa utulivu akiongea na RSO, Victoria Komba, maarufu kama Mama Komba.

Mama Komba alikuwa mwanamama shupavu ambaye alikuwa akiheshimika mno kwa uwezo wake mkubwa wa kusimamia operesheni, kuhamasisha maofisa waliokuwa chini yake kufanya kazi kwa bidii na weledi, na kutoa ushauri bora kwa viongozi wa juu. Sifa hizo pamoja na nyingine nyingi ndizo zilizofanya akabidhiwe dhamana ya kusimamia usalama wa mkoa huo.

Mama Komba hakuwa mrefu wala mfupi bali alikuwa na kimo cha wastani. Sura yake nzuri iliyoambatana na umbo lake la kuvutia, iliwafanya wanaume wengi kumwona kama mfanyabiashara fulani au mwanasiasa. Mama Komba alizitumia vyema sifa hizi katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku, akiiwakilisha vyema Idara ya Usalama wa Taifa kila mahali alipokwenda.

Kama ungebahatika kukutana naye mitaani bila shaka usingeamini kuwa ni mmoja wa watu muhimu mno katika Idara ya Usalama wa Taifa.

Kabla ya yote nilianza kwa kumtaka radhi Mama Komba kwa kuingia katika mkoa wake kwa njia ya kijasusi, njia ambayo pengine yeye hakuitarajia japo sisi tuliona ndiyo njia bora zaidi kwa ajili ya usalama wetu. Mama Komba alikuwa mtu mwelewa sana, alituelewa na hapo tukaanza kikao chetu kwa ajili ya kupashana taarifa za kiintelijensia.

Mama Komba alinikabidhi faili fulani jekundu, nikalipokea na kulifungua kwa shauku, halafu nikalipitia kimya kimya kwa takriban dakika tano nikiisoma taarifa ya awali kuhusu tukio lile la utekaji, kisha nikainua uso wangu kumtazama Mama Komba, wakati huo akili yangu ilikuwa ikijaribu kuyatafakari yale niliyoyapitia haraka haraka. Halafu nikataka kumpatia Daniella lile faili lakini akaniashiria kuwa tayari alikwishaipitia taarifa ile.

This is a brutal kidnapping,” nilisema kwa uchungu mkubwa huku hasira zikianza kuchipua moyoni mwangu, nikimaanisha kuwa ulikuwa ni utekaji mbaya sana.

Yeah! Taifa have betrayed our country,” Daniella aliniunga mkono akisema kuwa Taifa (mkuu wa kikosi cha siri cha ulinzi wa Rais) alikuwa ameisaliti nchi yetu. Kisha akaongeza, “They have betrayed democracy.”

Badala ya kunisaidia, sasa taarifa ile ya awali ilionesha kuivuruga akili yangu. Ndiyo, ilikuwa ni taarifa ya awali iliyoonesha jinsi utekaji huo ulivyofanyika, lakini bado ilikuwa katika mafumbo. Kitu kikubwa nilichoambulia ni kwamba utekaji nyara ulihusisha makomando hatari wasiopungua kumi, ambao utaifa wao ulikuwa bado haukujulikana, walivamia makazi ya Rais baada ya kuhujumu mfumo muhimu wa mawasiliano ya kiusalama.

Taarifa ilizidi kueleza jinsi makomando hao waliokuwa wamejifunika nyuso zao walipovamia kwenye makazi ya Rais katika Ikulu ya Mtwara, wakifyatua risasi za onyo, kupiga kelele na kumnyooshea Rais bunduki kifuani. Kisha alivutwa hadi kwenye gari moja aina ya Jeep Wrangler jeusi na haikueleweka alipelekwa wapi.

Uvamizi huo ulifanyika kupitia baharini, angani na ardhini, na kwamba makomando hawa waliingia nchini kwa kutumia meli iliyosadikiwa kuwa ilimilikiwa na kampuni ya Intersnack Cashew Company ya Vietnam ambayo ilikuwa mnunuzi mkuu wa korosho za Mtwara na kuzisafirisha hadi nchini Vietnam. Ni meli hii pia ilituhumiwa kubeba silaha nzito za kijeshi zilizotumika kwenye utekaji na waliziingiza baada ya kudanganya kwa kuwajulisha mamlaka ya bandari kuwa mzigo huo ulikuwa ni pembejeo na vifaa vya kilimo kwa wakulima wa korosho.

Silaha zilizotumika katika tukio lile ni bunduki kubwa aina ya US Barrett M82 ambazo taarifa ilisema kuwa katika majeshi yetu hatukuwa na silaha za aina hiyo ila kulikuwa na uwezekano mkubwa kwamba zilikuwa zikitumiwa na magaidi Kaskazini mwa Msumbiji katika Jimbo la Cabo Delgado.

US Barrett M82 ni bunduki kubwa itumiwayo na wadunguaji, ilitengenezwa chini ya jina la Barrett Firearms na inatofautiana na silaha za kawaida za wadunguaji kwa kuwa inaweza kuhimili teknolojia nzuri na kudhoofisha risasi za adui kutoka umbali mkubwa na salama. Hii silaha inaweza kufanya uharibifu zaidi kwa maadui kuliko kurusha risasi kutoka mbali.

Imetengenezwa katika namna ya kustahimili hali ya baridi, ina breki ya mdomo wa mtutu na kamera mbili za za kipekee. Pia ina uwezo wa kujisamamia katika kupunguza joto lake wakati inapotumiwa kwa muda mrefu.

Taarifa iliendelea kudadavua kuwa mkuu wa kikosi cha siri cha ulinzi wa Rais (Secret Service), Yusuf Assad Taifa, ndiye aliyeongoza genge hilo la magaidi kumteka nyara Rais, na kwamba Rais alionywa mapema na ofisa mmoja wa Secret Service, William Shamte, kuhusu usaliti wa Yusuf Taifa na tishio linalowezekana kwa maisha yake.

Hata hivyo Rais alipuuza onyo la Shamte na hatimaye akatekwa nyara usiku wa saa sita na robo wakati akiwa amejipumzisha. Wakati wa harakati za utekaji huo wa Rais, Yusuf Taifa ndiye aliyekuwa kikwazo kwa walinzi wa Rais, akiwemo William Shamte, waliojaribu kwa kila hali kupambana na makomando hao hatari ili kumwokoa Rais, na ni yeye aliyewaua walinzi hao watatu kabla ya kuelekeza mtutu wa bunduki kwenye kifua cha Rais Albert Masinde.

Taarifa zaidi zilidai kuwa baada ya Rais kushuhudia mauaji ya walinzi wake watatu yakifanywa na mkuu wa kikosi cha ulinzi wa Rais basi hakutaka makuu, aliamua kujikabidhi mwenyewe mikononi mwa watekaji hao ili kuokoa umwagaji damu zaidi...

Taarifa ilimaliza kwa kueleza hatua ambazo Idara ya Ujasusi Mkoa wa Mtwara walikwisha chukua wakishirikiana na Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, na kuwa walikuwa wanamshikilia meneja wa bandari aliyeidhinisha mzigo wa silaha ulioingizwa na meli ya ya Intersnack Cashew Company ya Vietnam kwa kudhani ni mzigo wa pembejeo na vifaa vya kilimo kwa wakulima wa korosho, na kuwa kutokana na mshtuko alioupata alikuwa amelazwa, chini ya ulinzi mkali, katika Hospitali ya Ligula ambayo ni Hospitali Mkoa wa Mtwara.

Baada ya maelezo ya taarifa ile tuliendelea na kikao kwa dakika zisizopungua therathini hivi tukijadili kila suala tuliloona ni muhimu kufuatia hali tete iliyokuwepo mkoani humo. Kubwa kuliko yote lilikuwa suala la kuzidisha ulinzi na usalama katika maeneo tuliyodhani yalipaswa kulindwa zaidi.

Kwa bahati mbaya mpaka wakati huo tulikuwa hatujapata fununu ya watu waliofanya tukio lile la kumteka Rais zaidi ya kuambiwa kuwa mkuu wa Secret Service, Yusuf Taifa alishiriki. Hatukujua waliomteka Rais walikuwa wamekusudia kufanya matukio gani mengine, maeneo gani, na kwa wakati gani! Kwa sababu hiyo ulinzi wa hali ya juu ulihitajika katika maeneo yote muhimu, si kwa Mtwara tu bali pia katika maeneo mengine nyeti zikiwemo Ikulu za Dar es Salaam na Dodoma.

Jambo lingine tulilolitazama kwa kina lilikuwa suala la wahamiaji haramu waliokuwa wamejazana mkoani Mtwara kutoka nchi za Malawi na Msumbiji, wengi wa watu hawa walikuwa wameingia nchini kwa njia za panya, wakajichanganya na Watanzania na kufanya biashara, au kazi za kuajiriwa bila ya kufuata taratibu husika. Suala hili lilikuwa nyeti kwa sababu tulihisi watu hao wangeweza kutumika kufanya jambo hilo.

Sambamba na hilo, lilikuwepo pia ongezeko kubwa la watu waliokuwa wakifanya biashara haramu na vitendo vya kigaidi, wakitokea Kaskazini mwa Msumbiji katika Jimbo la Cabo Delgado.

Ili kudhibiti hali hiyo tulimshauri Mama Komba ifanyike operesheni maalumu ya kuwatambua wageni wote walioingia mkoani humo kihalali na kiujanjaujanja (wahamiaji haramu) kwa kushirikiana na maofisa uhamiaji, polisi na kitengo maalumu cha idara kinachoshughulika na udhibiti wa wageni, ikiwa sehemu ya uchunguzi wa kuwapata wahalifu, si lazima wahalifu hao wawe ni wale waliofanya tukio la kumteka Rais.

Pia sote tulikubaliana kwamba tukio la kumteka Rais na kuua walinzi watatu lilitia doa taasisi zetu za ulinzi na usalama nchini, na tulipaswa kushughulikia suala la kupatikana Rais haraka iwezekanavyo kabla halijagundulika.

Na mwisho tulishauri kuwa uchunguzi mpya ufanyike bila kuzingatia uchunguzi wa awali uliokwisha fanyika maana tulihisi kuwepo kwa mambo yaliyofichika kwenye uchunguzi wa awali na hivyo kufanya upelelezi kuwa mgumu. Na uchunguzi huo tuliamua kuufanya wenyewe na ukamilike ndani ya siku mbili.

“Sasa tunahitaji kuonana na huyo meneja wa bandari aliyelazwa katika Hospitali ya Ligula. Hapo ndipo tunapoanzia uchunguzi wetu,” Daniella alisema.

Muda huo huo simu iliyokuwa mezani kwa RSO ikaanza kuita kwa kelele. Haraka Mama Komba akanyanyua kikonyo chake na kukipeleka sikioni. “Hallo!” aliita kwa sauti kavu.

Baada ya kusikiliza kwa sekunde chache akatutazama na kusema, “Tayari nimeshaonana nao na sasa wapo hapa ofisini kwangu…” halafu akanyoosha mkono wake kunikabidhi kikonyo cha simu. “Ongea na Kanali Mjaka,” aliniambia.

Nilipokea kile kikonyo cha simu, nikaongea kwa dakika chache na mkuu wangu wa kikosi nikimweleza kwa nini tuliamua kuzima simu zetu na tahadhari zote tulizozichukua hadi kufika hapo, kisha nikamweleza hatua tulizoanza kuzichukua. Mazungumzo yetu yalichukua dakika tano. Simu ilipokatwa ilikuwa imeshatimia saa tisa na robo, nikakumbuka kufanya jambo muhimu kabla hatujaenda Hospitali ya Ligula.

Nikawataka radhi RSO Mama Komba na Daniella na kutoka haraka, nikavuka Barabara ya Tanu na kuelekea upande wa pili wa barabara nikiifuata barabara nyembamba nikiyavuka majengo ya Idara ya Uhamiaji mkoani Mtwara. Majengo yale yalikuwa mkabala na majengo ya Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani, kisha nikafika kwenye jengo ambalo kulikuwa na Benki ya CRDB pamoja na ofisi za NHIF Mtwara na Vision Medics Company Ltd.

* * *

Picha ndo kwanza linaanza. Usikose kufuatilia kujua kilichojili...
 
Back
Top Bottom