Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

utata.JPG

362

Mapambano yanaendelea…




Saa 4:05 usiku…

DANIELLA aliliegesha gari letu kando ya Barabara ya Bandari (Port Road), takriban mita mia tano kutoka ilipo kambi ya JWTZ Mtwara, nikashuka na kuanza kutembea taratibu kando kando ya barabara ile nikielekea mbele. Mcho yangu yalikuwa makini sana kutazama huku na huko. Na muda huo Daniella alikuwa akiliondoa gari na kuelekea mtaa mwingine, kwenye kituo cha mafuta cha Oilcom.

Ndivyo tulivyokuwa tumekubaliana, kuwa mimi nishuke halafu akaliegeshe gari kwenye kituo cha mafuta kisha arudi kuja kuungana nami kwenye mgahawa mmoja maarufu wa Paradise. Hii ilikuwa mbinu muhimu kwa ajili ya usalama wetu.

Wakati tukitoka nyumbani kwa mzee Othman Mwambe tulikubaliana kuwa twende pale Paradise Café kujipatia mlo na kisha tuelekee kule Naf Beach Hotel kwa ajili ya kupanga mikakati zaidi. Paradise Café ilivuma kwa sifa zake za kuandaa chakula kitamu sana, na pia lilikuwa eneo tulivu lenye ustaarabu mkubwa.

Hata hivyo hatukuwa na muda wa kupoteza, tulipanga kuwepo pale Paradise Café kwa dakika zisizozidi ishirini na tano tu, kwa maana hiyo tulitakiwa kumaliza kula na kuondoka pale Paradise Café si zaidi ya saa nne na nusu za usiku.

Niliendelea kupiga hatua zangu kwa utulivu kisha nikaanza kukatisha barabara ile ya Bandari ili nielekee ng’ambo ya pili ya barabara ulipo ule mgahawa wa Paradise, nikiwa naangaza angaza huku na kule. Macho yangu yalikuwa makini zaidi kuzichunguza sura za watu waliokuwa eneo lile na mijongeo yao.

Mwili wangu ulikuwa mchovu mno kutokana na vyote; pilika pilika za mapambano ya siku mbili bila kupumzika, kukosa usingizi kwa siku mbili tangu lilipotokea tukio la kigaidi kule Capital Social Club Dodoma, na njaa. Vyote hivi vilininyong’onyesha na kunifanya nitembee kwa kujivuta vuta.

Wakati nikiangaza huku na kule mara macho yangu yakaangukia kwa mtu mmoja aliyekuwa amesimama kando ya kioski fulani akionekana kuongea na simu. Alikuwa ni mwanamke mrefu aliyevalia blauzi nyeupe, suruali nyeusi ya dengrizi ya kumbana na viatu vyeusi vya ngozi vyenye visigino msawazo.

Sikufanikiwa kuiona sura ya mwanamke yule ila niliamini kabisa kuwa alikuwa akinitazama kwa wizi wizi kwani aliukwepesha haraka uso wake punde tu nilipotazama upande alipokuwa amesimama. Alikuwa amevalia nywele ndefu za bandia ambazo ziliziba shepu ya kichwa chake na masikio. Pengine ningeviona vitu hivyo vingenisaidia kumng’amua mwanamke huyo.

Hata hivyo, umbo lake refu lenye shepu fulani lilinijulisha kuwa nilikuwa namfahamu. “Ni nani huyu mwanamke, na kwa nini amekwepesha sura yake nisimtambue?” nilijiuliza kwa mshangao. Na hapo nikajikuta nikipatwa na hamu ya kutaka kuiona sura yake japokuwa sikuwa na shaka kiasi cha kunifanya nichukue hatua nzito.

Honi kali za gari zilinigutua kutoka kwenye mawazo yangu, nikaruka kando huku nikigeuka haraka kutazama kule ilikosikika ile honi ya gari. Nikaliona gari dogo aina ya IST la kijivu likinipita kwa mwendo wa kasi huku dereva wake akishusha kioo na kuninyooshea kidole kama ishara ya kunionya niwe makini wakati wa kuvuka barabara.

Mara tu lile gari lilipopita haraka nikayarudisha macho yangu kwa yule mwanamke. Sikumwona! Alikuwa amepotea! Nilitazama huku na huko lakini sikufanikiwa kumwona. Dah, nikaamua kupuuzia na kuanza kukatisha kwenye eneo la maegesho ya magari la Paradise Café nikielekea ndani ya mgahawa ule, huku nikijaribu kudadavua mambo niliyoambiwa na mzee Othman Mwambe.

Nilijaribu kutafakari, iwapo ni kweli mmojawapo kati ya mkuu wa majeshi na mnadhimu wa jeshi ndiye aliyekuwa nyuma ya tukio lile la kutekwa kwa Rais Masinde… je, kwa nini afanye hivyo? Kwa maslahi ya nani? Na nini kilikuwepo nyuma ya tukio lile?

Pale nje ya mgahawa niliwapita watu wawili watatu walikuwa wameosimama wakiwa wamezama katika mazungumzo yao ila wakati nikiwapita watu wale waligeuka kunitazama, sikuwajali. Niliwapita pasipo kuonesha dalili ya kuwatilia maanani ingawa akili yangu ilikuwa makini sana ikijaribu kunusa hatari.

Nilipoingia tu ndani ya mgahawa ule wa Paradise nikajikuta nikikabiliana na macho ya watu waliokuwa wameketi kwa utulivu mle ndani ya ukumbi wakiendelea na starehe zao. Mgahawa ule ulikuwa wa kisasa wenye huduma za daraja la juu, hii ilidhihirishwa na idadi ya watu wengi waliofika pale kwa ajili ya chakula na vinywaji.

Hata hivyo ukumbi ulikuwa mkubwa na hivyo bado kulikuwa na meza nyingi zisizokaliwa na watu. Niliangaza macho yangu huku na huko katika namna ya kutafuta sehemu nzuri ya kukaa na wakati nikiyatembeza macho yangu nikawa nikiwachunguza watu waliokuwa mle ndani ili kujaribu kubaini iwapo kulikuwa na yeyote aliyekuwa akinizingatia sana. Sikumwona.

Nikaiona meza moja iliyokuwa imejitenga ikiwa kwenye kona moja ya ukumbi ule, upande wa kulia. Nikaifuata na kuketi nikijitenga mbali kidogo na watu wengine, huku nikiwa na nafasi nzuri kuona pande zote za ukumbi ule. Mhudumu mmoja wa kike aliniona wakati naketi pale, akanijia haraka huku uso wake ukipambwa na tabasamu la kibiashara.

“Karibu, kaka, sijui ungependa kuagiza nini?” yule dada mhudumu aliniuliza kwa sauti nyororo ya kumtoa nyoka pangoni, sauti iliyotuama vyema ndani ya moyo wangu. Hata hivyo sauti yake na uzuri wake havikuendana. Alikuwa msichana wa kawaida sana machoni kwangu.

“Naomba kwanza niletee supu ya samaki chapchap nipashe tumbo joto wakati ukiniandalia ugali wa dona na kuku wa kurosti…” nilimwambia yule dada mhudumu baada ya kusoma karatasi yenye orodha ya vyakula iliyokuwa juu ya ile meza. “Sijui itachukua muda gani?”

“Sasa hivi tu,” yule dada mhudumu aliniambia huku akiendelea kutabasamu.

“Basi fanya fasta maana nina njaa ya siku mbili,” nilisema huku nikijiweka sawa kwenye kiti changu.

Yule dada mhudumu aligeuka na kuondoka haraka toka eneo lile na wakati huo huo nikamwona Daniella akiingia ndani ya ukumbi ule na kusimama, akayazungusha macho yake kutazama na macho yetu yalipogongana akayahamisha haraka macho yake na kuelekea upande mwingine, wa kushoto, akionekana kutafuta sehemu ya kukaa.

Nikiwa makini kuwatazama watu waliokuwemo mle ukumbini mara nikamwona yule dada mhudumu akirudi pale kwenye meza yangu haraka huku mikononi akiwa amebeba sinia kubwa lenye supu ya samaki.

Alipofika pale kwenye meza yangu aliinama kwa utulivu akilitua lile sinia juu ya ile meza mbele yangu na kitendo kile cha kuinama kidogo kikanifanya nikione kifua chake kilichobeba matiti madogo mfano wa machungwa yenye chuchu nyeusi zilizosimama na kutaka kunitoa udenda.

Nikiwa nimevutiwa kuyaangalia matiti yake, yule dada mhudumu alinishtukia na kuitengeneza vizuri blauzi yake huku akiona aibu. Nilimtazama usoni huku nikitabasamu, tukio lile likamfanya atabasamu kidogo kwa aibu huku akiyakwepesha macho yake pembeni yasikutane na yangu.

Endelea...
 
utata.JPG

363

Alipomaliza kuniandalia akanikaribisha huku akiniuliza kama nilihitaji kinywaji chochote, nikampa noti mbili za elfu kumi kumi kwa ajili ya supu ile ya samaki na ugali wa dona ambao ungekuja baada ya kumaliza ile supu ya Samaki, halafu nikamtaka aniletee na bia moja baridi aina ya Heineken na chenji ambayo ingebaki abaki nayo. Yule dada mhudumu alizipokea zile noti huku akinishukuru sana na kuondoka.

Niliishambulia ile supu kama nzige kutokana na njaa niliyokuwa nayo, maana tangu lilipotokea lile tukio la kigaidi kule Capital Social Club Dodoma sikuwa nimepata chakula cha kueleweka zaidi ya kunywa sharubati tu ambazo hazikusaidia kuizima njaa niliyokuwa nayo.

Ndani ya dakika tano nilikuwa nimeimaliza ile supu ya Samaki na kusasa nilikuwa nakula ugali. Ulikuwa mtamu sana. Wakati nikila macho yangu yalikuwa makini sana kuwatazama watu waliokuwemo mle ukumbini. Ilinichukua dakika zisizozidi kumi kumaliza chakula kisha nikasubiri kama dakika mbili hivi halafu nikawa nakunywa bia yangu taratibu wakati chakula kikishuka tumboni.

Niliitazama saa yangu ya mkononi nikashusha pumzi, nilikuwa bado nipo ndani ya muda tuliokubaliana. Hivyo nikavuta funda jingine la bia huku nikiangaza macho yangu huku na kule. Na kwa kufanya vile nikamwona mwanamke mmoja mrefu akiwa anapunga mkono wake kunielekea na kutabasamu, huku akiita, “Jason!”

Alikuwa mwanadada mrefu mwembamba na mweusi mwenye haiba nzuri ya kuvutia. Nywele zake zilikuwa nyeusi ndefu na alikuwa amezifunika kwa kofia nyekundu aina ya kapelo. Sura yake ilikuwa ndefu na macho yalikuwa makubwa ya kike yaliyoonesha kulegea. Alikuwa amevaa fulana nyepesi nyekundu iliyoyaficha matiti yake. Kiuno chake chembamba kiasi chenye misuli imara kiliizuia suruali yake ya bluu ya kitambaa cha dengrizi na miguuni alikuwa amevaa raba nyekundu.

Alikuwa amening’iniza mkoba wa bluu ulioonekana ulimghalimu fedha nyingi sana na katika vidole vya mkono wake wa kushoto alikuwa amevaa pete mbili za madini ghali ya tanzanite na almasi nyeupe. Nilimtazama yule mwanamke kwa umakini nikijaribu kukumbuka kama nilishawahi kumwona mahali. Kabla sijakumbuka chochote, mwanamke huyo akawa amenifikia.

Alinisalimu akitumia Kiingereza huku akinipatia mkono na kujitambulisha, “I’m Anabella Fernando!

Oh! Nice to meet you, Anabella,” nilimjibu yule mwanadada huku nikimtazama usoni kwa umakini. Nilikuwa nimeshangazwa kuona kuwa yeye alikuwa akinifahamu ila mimi sikumfahamu kabisa. Sura yake ilikuwa ngeni machoni kwangu.

Na kabla sijafungua mdomo wangu kuuliza, Anabella akawahi kuniuliza, “Don’t you feel lonely being alone?” akitaka kujua kama sikuwa nikijihisi mpweke kukaa peke yangu.

Niligundua kuwa namna ya matamshi ya Kiingereza chake yalimwonesha kuwa alikuwa raia wa kutoka katika nchi zinazozungumza Kireno. Kama si Msumbiji basi Angola. Mkononi alikuwa ameshika chupa ya mvinyo aina ya Miami 24.

Nilimtazama kwa mshangao kidogo kwa sababu sikutegemea kuona mwanamke wa aina yake akitumia kinywaji kikali kama kile. Pia nilijiuliza mvinyo ule alikuwa ameupata wapi maana niliamini pale Mtwara hakukuwa na duka lililouza mvinyo ghali kama ule. Nikapatwa na shauku ya kutaka kumfahamu zaidi yule dada.

Kwa tathmini yangu ya haraka nilihitimisha kuwa mwanamke yule alikuwa ni mtu mwenye kipato cha kueleweka.

Why do you like Miami 24 whisky?” badala ya kujibu swali lake nami nilimwuliza kwa nini alipenda mvinyo wa Miami 24, nilitumia lugha yangu safi ya Kiingereza kisicho cha kubabaisha huku nikimtazama kwa tabasamu.

It’s like you, you like Heineken!” Anabella alinijibu kuwa ni kama mimi nilivyopenda Heineken, aliongea huku akitabasamu kisha akaendelea, “Before, I liked beer like you, but I found myself giving up after I got friends who drink Miami 24. Though, I don’t hate beer, but I don’t really enjoy drinking it,” Anabella aliongea huku akinitazama kwa mbwembwe za kike.

Hapo alinieleza kuwa alikuwa mpenzi wa bia kama mimi lakini alijikuta akiachana nazo baada ya kupata marafiki wanywaji wa Miami 24. Hata hivyo hakuzichukia bia ila hakuzifurahia sana.

Nilimtazama kwa udadisi zaidi na hapo nikagundua kuwa alionekana kuzimudu vizuri starehe za dunia kwa namna yake. Hata hivyo swali langu kubwa lililoendelea kuniumiza akili yangu ni kwamba; alilifahamu vipi jina langu?

You haven’t told me how you know my name? Also your accent shows you are not from English speaking countries!” nilimwambia Anabella nikimuuliza alilijuaje jina langu na pia lafudhi yake ilionesha kuwa hakuwa anatoka katika nchi zinazozungumza Kiingereza, nilikuwa bado namtazama kwa udadisi.

Oh! This is impossible!” Anabella alisema kuwa ilikuwa haiwezekani, huku akinitazama kwa mshangao kisha akaongeza, “Does it mean you really forgot me?” akiniuliza kama kweli nilikuwa nimemsahau!

If I’d have remembered you, I’d not have asked you!” nilimjibu Anabella kwa sauti tulivu kuwa iwapo ningekuwa namkumbuka nisingemuuliza.

Kisha niliyatupa macho yangu kumtazama Daniella, nikamwona akiwa ameketi na mwanamume mmoja mtu mzima ambaye tangu alipokuwa akiingia hakuchoka kumtazama, kinywa wazi na ulimi nje huku akiwa na kila dalili ya tamaa ya ngono katika macho yake.

Na sasa mzee huyo alikuwa amehamia kwenye meza ya Daniella na kutandaza vinywaji mezani huku akiongea kama aliyepagawa. Macho yetu yalipogongana nikayaona macho ya Daniella yakinitaka kuwa makini na yakinikumbusha kuwa hatukuwa na muda wa kupoteza pale. Hata hivyo, nisingeweza kuondoka pale Paradise pasipo kulifumbua fumbo lile lililojitokeza.

Why do I know you even though many years have passed since we lost each other!” Anabella aliniuliza kuwa mbona yeye alikuwa ananijua japo ilikuwa imepita miaka mingi tangu tupotezane.

Hisia zangu ziliniambia kuwa Anabella alikuwa anataka kucheza na akili yangu na alikuwa ameamua kupoteza muda makusudi. Alikuwa kama anayeniletea maigizo ambayo alikwisha yafanyia mazoezi kwa muda mrefu. Hilo lilinifanya niamue kujitokeza toka kichakani na kuingia hadharani.

Listen, Anabella… I have a lot of things to do and I can’t force you to tell me if you don’t feel like doing it. Time doesn’t allow me…” nilisema kwa sauti iliyoonesha wazi kuwa nilishaanza kukasirika, nikimaanisha kuwa nilikuwa na mambo mengi ya kufanya na nisingeweza kumlazimisha anieleze kama alikuwa hajisikii maana sikuwa na muda.

Endelea...
 
utata.JPG

364

Kuona vile, Anabella akawahi kuongea, “I am Angolan citizen and I live in Luanda. You and I studied together in Pretoria Technikon in South Africa. But I studied Aspect of Film and Television.” Akimaanisha alikuwa anatokea jijini Luanda nchini Angola na kwamba tulisoma pamoja kule Pretoria nchini Afrika Kusini ila yeye alisomea masuala ya filamu na televisheni.

Nilimtazama kwa umakini lakini bado sikuweza kumkumbuka kabisa. Sura yake ilikuwa ngeni kabisa machoni kwangu. Nilishusha pumzi na kumuuliza kwa sauti tulivu. “Have you come here for a business trip or vacation?” nilikaamisha alikuja Mtwara kwa safari ya kibiashara au matembezi?”

I am here in Mtwara for a short break of my vacation,” Anabella aliniambia huku akinitazama usoni kuwa alikuwepo Mtwara kwa ajili ya mapumziko mafupi ya likizo yake. Tulitazamana na macho yetu yalipokutana kila mmoja akatabasamu na hapo haraka nikajua kuwa alikuwa ni mwanamke wa aina yangu.

Why did you choose Mtwara as a place of vacation instead of big cities like Dar es Salaam, Arusha and Mwanza? Or other East African Cities like Nairobi, Kigali and Kampala?” nilimuuliza Anabella kwa nini aliichagua Mtwara kama sehemu ya mapumziko badala ya miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, au miji mingine mikubwa ya Afrika Mashariki kama Nairobi, Kigali au Kampala. Kisha nilivuta funda la bia.

I have been all over there but the lifestyle here in Mtwara, I can say, has really impressed me,” Anabella aliongea huku akitabasamu kwa aibu, alikuwa akimaanisha kuwa alikuwa amefika huko kote lakini mtindo wa maisha ya Mtwara ulikuwa umemvutia sana.

How?” nilimuuliza Anabella ki vipi maisha ya Mtwara yalimvutia, huku nikimkazia macho.

I don’t even know how to explain it, but I just happened to like Mtwara!” Anabella aliongea huku akiangua kicheko hafifu kilichoniacha njia panda akimaanisha kuwa hata hakujua aelezeje ila alitokea tu kupapenda Mtwara. Na hapo nikajaribu kuyapima maneno yake.

Do you live here?” Anabella aliniuliza kama nilikuwa naishia Mtwara huku akiendelea kunitazama usoni. Namna ya uangaliaji wake ulinifanya kuhisi jambo lisilo la kawaida. Ila kwa wakati huo sikujua ni jambo gani.

Nope. I live in Dar es Salaam. Here Mtwara I have come for a vacation,” nilimwambia Anabella kuwa niliishi Dar es Salaam ila pale Mtwara nilikwenda kwa mapumziko tu.

Doy have family, wife and kids maybe…?” Anabella aliniuliza iwapo nilikuwa nimeoa na nina watoto.

I have no family. I am still single and have no children,” nilimjibu kuwa sikuwa nimeoa wala kuwana watoto, na wakati huo nikijaribu kutafakari maana ya maswali yake.

Why is a handsome man like you not married until now and your age allows it? Besides, you seem financially capable!” Anabella aliniuliza huku akinitazama kwa mshangao akitaka kujua kwa nini nilikuwa sijaoa hadi sasa na umri wangu uliniruhusu. Isitoshe nilionekana nina uwezo kifedha.

Are you married and have children?” nilimtupia swali nikitaka kujua kama yeye alikuwa ameolewa na ana watoto.

Men are unpredictable,” Anabella alimaanisha kuwa wanaume hawatabiriki, alisema huku akiachia kicheko hafifu. Hata hivyo sikuelewa alimaanisha nini kusema vile.

Nilimtazama Anabella kwa umakini huku nikijaribu kumlinganisha na maneno yake. Na wakati nikifanya vile nikajikuta nikivutiwa na mchoro fulani uliokuwa shingoni kwake. Mchoro ule ulichorwa kwa ustadi mno ingawa haukunivutia hata kidogo.

Ulikuwa ni mchoro wa kichwa cha chui milia (tiger) aliyekuwa ameachama kinywa chake wazi. Nikiwa nimeduwaa kuutazama ule mchoro Anabella alionekana kama ambaye hakuvutiwa na angalia yangu hivyo aligeuka katika namna ya kunifanya nisiweze kuuona vizuri ule mchoro.

Ili kumweka sawa nilimuuliza Anabella alikuwa amefikia wapi pale Mtwara, hii ilikuwa ni katika namna ya kumdadisi na hapo nikamwona akiupeleka mkono wake kwenye pochi yake ndogo ya mkononi. Alipoifungua ile pochi akatoa kadi ndogo na kunipa.

Niliipokea ile kadi na kuitazama kwa umakini. Ilikuwa ni kadi ndogo yenye maelezo ya namba ya chumba cha Tiffany Diamond Hotel iliyopo katikati ya Mji wa Mtwara, na chini ya kadi ile kulikuwa na namba za simu.

Muda huo huo niliyatupa macho yangu kumtazama Daniella, nikamwona akinitazama katika namna ya kunisisitiza kwamba tulitakiwa kuondoka. Niliitazama saa yangu na kushtuka. Ilikuwa imetimia saa nne na dakika hamsini na tano. Hii ilimaanisha kuwa tulikuwa tumetumia dakika ishirini na tano zaidi ya muda tuliopanga kuwepo pale. Nikanyanyua bilauri yangu ya bia na kunywa bia yote.

Ni kama Anabella alikuwa ameyasoma mawazo yangu kwani nilimwona akifungua tena mkoba wake na kutoa simu yake ya mkononi. Akabonyeza kidogo na kuweka sikioni, “Where are you? Please come and get me…” akimuuliza mtu wa upande wa pili wa simu ni wapi alikokuwa na kumtaka afike kumchukua kisha akairejesha simu mkobani na kuinuka. “I’m also late. So, let’s all go out, I need to go back to the hotel.” Akimaanisha kuwa alikuwa amechelewa na alitaka kurudi hotelini na hivyo akanitaka tutoke wote.

Tukaongozana kuelekea nje ya mgahawa ule na tulipofika nje akafungua mkoba wake na kutoa bastola! Akaiminya mbavuni kwangu katika namna ambayo haikuweza kuonekana na mtu mwingine, kisha akaniambia, “If you try to do anything stupid, I’ll turn you into a corpse!” akinionya kutofanya jambo lolote la kipumbavu vinginevyo angenigeuza mzoga!

Halafu akaniamuru nielekee moja kwa moja kwenye gari moja lililokuwa limeegeshwa mbali kidogo, kando ya barabara ile ya Bandari, kwenye eneo lenye kiza. Nikatii, tukawa tukitembea kuelekea huko. Wakati huo Anabella alikuwa anaangaza angaza huku na kule kuhakikisha usalama wake, nami kichwani mwangu nikifikiria namna gani ya kumdhibiti maana hakujua kuwa alikuwa anacheza na simba mwenye njaa kali.

Tukazidi kusonga huku nikiupima umakini wake mpaka mahali ambapo kwa mahesabu tulikuwa tumebakiza umbali mfupi kulifikia lile gari ambalo Anabella alikuwa ananipelekea. Nikajifanya kujikwaa na kuyumba kidogo, na hapo Anabella akashtuka na kuielekeza bastola yake kichwani kwangu lakini nikawahi kuudaka mkono wake kisha nikautegua kiustadi, akaiachia bastola!

Kisha nilimdhibiti na kumwamuru twende kule alipokuwa anataka kunipeleka. Hakubisha. Tukaongozana mpaka lilipoegeshwa lile gari aina ya Toyota Alphad jeupe lenye vioo vyeusi. Nikamwamuru agonge mlango, na punde mlango ukafunguliwa na mwanamume mmoja mrefu aliyekuwa amevalia shati jeusi na suruali ya bluu, na kichwani alivaa kofia aina ya kapelo.

Huku nikiendelea kumdhibiti vyema Anabella nilimwelekezea yule jamaa bastola kichwani. Halafu tukazama ndani ya gari lile huku nikiwa makini zaidi. Bastola ilikuwa bado inamwelekea kichwani yule dereva na wakati huo huo nikizidisha kumkaba Anabella mpaka nikasikia akianza kukoroma.

Endelea...
 
utata.JPG

365

Drive your car,” nilimwamuru yule jamaa kuendesha gari bila kujali kama alikuwa anafahamu Kiingereza au alikuwa Mswahili kama mimi, nikimtaka aendeshe gari lake. Bila ubishi akaliondoa gari na baada ya mwendo wa kama mita mia tano hivi tukafika sehemu iliyotulia sana, nikamwamuru kuliegesha gari kando ya barabara. Akafanya kama nilivyomwelekeza.

Who sent you to follow me?” nilimuuliza yule jamaa ni nani aliyewatuma kunifuatilia, nikiwa makini kuhakikisha kuwa hawanichezi shere. Pia sikuwa na wasiwasi sana maana nilijua kuwa Daniella alikuwa sehemu fulani akichunga usalama wangu kwani mchezo mzima alishauona.

No one sent us,” yule jamaa alijibu kuwa hakuna mtu aliyewatuma akizungumza kwa Kiingereza ambacho mara moja nilitambua kuwa alikuwa Mtanzania.

“Usinitanie. Najua mmekuwa mkitufuatilia tangu tufike hapa Mtwara. Niambie Rais mmemficha wapi?” nilimuuliza yule jamaa kwa Kiswahili huku nikimkazia macho.

Jamaa yule akanyamaza akiwa ananitazama kwa dharau. Nikarudia kumuuliza swali langu, hakunijibu, badala yake akaniuliza, “Mbona sielewi unachokisema. Wewe nani aliyekwambia kuwa tumemficha Rais?”

“Jibu nilichokuuliza!” nilimwamuru yule mtu lakini hakuonesha sura ya hofu na badala yake aliachia tabasamu lililojaa dharau.

“Nakubali wewe ni mpelelezi hodari sana lakini nikwambie tu ukweli, kwenye hili hautafanikiwa…” yule mtu alisema na kuongeza, “Wewe na mwenzio mna kazi ngumu sana.”

“Hizo kazi ngumu ndizo tunazopenda!” nilimjibu kwa jeuri kisha nikamfyatulia risasi iliyokichakaza kiganja chake cha mkono wa kushoto aliokuwa ameuinua wakati akiongea.

Akalalama kwa maumivu makali huku akiushika mkono wake uliochakazwa kwa risasi, na wakati huo huo nikimgonga Anabella na kitako cha bastola chini ya kisogo chake, akalegea. Halafu nikamlaza kwenye kiti na kumkwida shati yule mwanamume. Nikamsogeza kwangu. Tukawa tunatazamana.

“Hata kama nikijibu maswali yako haitasaidia kitu,” yule mtu alisema huku akilalama kwa maumivu.

“Mambo ya kunisaidia au kutonisaidia nayajua mwenyewe. Nijibu kabla sijaumwaga ubongo wako,” nilimwambia kwa ukali.

Bado akawa mgumu. Nikampiga kichwa kikali kilichompasua mfupa wa pua yake na kusababisha damu imtoke kama bomba lililopasuka. Akapiga kelele za maumivu huku akiidaka pua yake.

“Mmemficha wapi Rais?” nilimuuliza kwa kufoka. Hakunijibu na badala yake akawa analalama kwa maumivu huku mkono wake wa kulia ukiziba pua. Nikamshtua na aliposhtuka nikamtandika ngumi kwenye pua yake iliyovunjika, akalia kama mtoto.

Nikarudia kumuuliza, “Mmemficha wapi Rais?”

Bado akawa hasemi. Aliendelea kulia tu kwa maumivu makali aliyoyapata. Basi nikaona alikuwa ananipotezea muda wangu, nikaielekeza bastola kichwani kwake nikiwa tayari kumchakaza. Akapiga kelele, “Usiniue nasema!”

“Sema haraka! Usinipotezee muda,” nilimkaripia huku nikiendelea kuielekeza bastola kichwani kwake.

“Mimi sijui alipofichwa Rais. Anayejua ni Kapteni Edwardo Munambo!” yule jamaa alisema na hapo nikamkumbuka yule mtu aliyepambana na Daniella kule kwenye nyumba iliyokuwa nyuma ya Naf Beach Hotel, kabla hajauawa. Hata hivyo sikutaka kuyaamini maneno yake.

“Haiwezekani wewe usijue wakati ninyi nyote ni wamoja. Niambie ukweli, ni wapi mmemficha Rais?” nilimuuliza tena huku nikiendelea kumwelekeza bastola, nikasema kwa ukali, “nahesabu hadi tatu kama husemi ukweli nakipasua kichwa chako.”

“Amefichwa ghalani…” yule jamaa alisema kwa tabu.

“Ghalani wapi?” nilimuuliza lakini hakijibu. Nikamchapa konde kali la shingoni, na hapo akalegea.

Shit!” nilipiga ngumi juu ya dashboard baada ya kugundua kosa langu kuwa nilitumia nguvu nyingi kumwadhibu yule mtu. Sasa sikuwa na uhakika wa kupata taarifa za Rais. Nilihitaji sana kujua Rais alikuwa amefichwa wapi.

* * *



Saa 5:30 usiku…

Zilikuwa zimepita dakika ishirini na tano tangu tutoke kule Paradise Café mimi na Daniella baada ya kupambana na wale wavamizi waliokuja kuniteka. Baada ya kuona walikuwa wamepoteza fahamu niliwasiliana na RSO Mama Komba na kumweleza juu ya wale wavamizi na kumwomba awatume maofisa wake kwenda kuwachukua na kuwahifadhi.

Sasa nilikuwa nimetulia ndani ya gari letu nikifanya utundu wangu kwa kuifungua Ipad yangu ambayo ilikuwa na mfumo maalumu wa utambuzi wa TracerMark, nikawa nabofya hiki na kile kisha nikaingiza code fulani na muda mfupi uliofuata nikawa nimeshazidukua kamera za usalama za Naf Beach Hotel.

Wakati huo tulikuwa tumeegesha gari letu jirani na eneo la viwanja vya wazi vinavyomilikiwa na Veta Mtwara, katika Barabara ya Mailimoja, kama mita mia tatu hivi kutoka ilipokuwa hoteli ile.

Nilipoona nimefanikiwa kuzidukua zile kamera za usalama nikamkabidhi Daniella ile Ipad, sasa alikuwa kama aliyekuwa ameingia kwenye chumba maalumu chenye tarakilishi inayoongoza mfumo mzima wa zile kamera za usalama za hoteli ile, akizidhibiti atakavyo.

Tulikuwa tumekubaliana kuwa Daniella abakie ndani ya gari kuchunga usalama wakati mimi nikielekea chumbani kwetu kuchukua vitu vya muhimu, na iwapo angeona kitu chochote ambacho angekitilia shaka basi angenijulisha mara moja.

Niliteremka haraka toka kwenye gari kisha nikaanza kutembea nikipita kando kando ya barabara nikiyapita majengo kadhaa kisha nikaufikia uzio uliokuwa ukizunguka hoteli ile, nikatazama huku na kule na kisha nikaruka uzio ule na kuingia ndani ya eneo la hoteli nikikwepa kwenda kutokea kwenye Barabara ya Chuno, barabara kubwa inayopita kando kando ya ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Nilipotua ndani ya uzio ule wa hoteli nikatulia kidogo kabla sijaanza kufanya mjongeo wowote, nikatazama huku na kule. Nilijua kwa vyovyote vile kungekuwa na watu walioweka mtego pale hotelini ili kutunasa, kwani katika ulimwengu wa ujasusi hatukutakiwa kumwamini mtu yeyote, hivyo niliamua kuwacheza shere kwa kuwabadilishia mchezo.

Kisha nikaondoka pale na kuanza kuelekea nyuma ya jengo la hoteli ile kulikokuwa na majengo mengine, nilikuwa makini sana kutazama huku na kule kama kungekuwa na chochote cha kukitilia shaka, huku nikipanga kuingia chumbani kwa njia ya kijasusi.

Sikutaka kwenda kuingilia kule kwenye mlango wa mbele kwenye mapokezi ya hoteli na badala yake nilielekea kule nyuma ya hoteli na kulichunguza lile jengo la hoteli, nikagundua kuwa kulikuwa na mlango wa kutokea upande huo wa nyuma. Nikajaribu kuutikisa na kukuta umefungwa, nikatulia kimya nikifikiri mara mbili kipi cha kufanya.

Sikuwa na shaka kabisa kuwa kamera za usalama zilikuwa zinachukua picha za tukio lile lakini pia sikuhofia chochote kwa kuwa udukuzi nilioufanya ulimwezesha Daniella peke yake kuzidhibiti mfumo wa kamera zile kwa muda ule na alikuwa na uwezo wa kufuta picha yoyote ambayo alidhani haikutakiwa kuonekana kwenye kamera zile za usalama ili kutoacha ushahidi.

Nikiwa bado nimesimama pale nyuma mara nikasikia sauti ya nyayo za mtu akija upande ule wa nyuma wa hoteli, nikajibanza katikati ya mabomba mawili ya majitaka yaliyokuwa yanatiririsha majitaka toka juu kuleta chini. Yule mtu alipotokeza tu nikagundua kuwa alikuwa mlinzi wa hoteli ile, na alinipita pasipo kutambua uwepo wangu, na hapo nikaanza kukwea kuelekea juu kupitia yale mabomba ya majitaka.

Endelea...
 
utata.JPG

366

Bahati nzuri chumba chetu hakikuwa juu sana, kilikuwa katika ghorofa ya kwanza tu, hivyo haikunichukua muda kufika usawa wa chumba chetu, pale kulikuwa na kaukuta kalikojitokeza, nikakanyaga na kujisogeza hadi kwenye dirisha la chumba chetu, nikalitikisa kidogo na lenyewe likatii amri, taratibu nikaingia ndani kupitia dirisha hilo kubwa lililoundwa kwa vioo, kisha nikatua ndani ya chumba hicho kwa kunyata bila kufanya kelele yoyote kwani nilijua kuwa lazima kungekuwa na mtego.

Halafu taratibu nikaanza kulisogelea kabati la nguo la ukutani, nilipokuwa mbioni kushika kitasa cha mlango wa kabati hilo ili kuuvuta kengele ya hatari kichwani mwangu ikagonga, nikajiandaa na kuuvuta mlango kwa nguvu huku nikisogea kando. Na hapo mtu mmoja aliyekuwa amejificha ndani ya kabati hilo akajitokeza kwa kasi ili kunishambulia.

Kwa kuwa tayari nilikuwa nimejiweka kando hivyo yule mtu alipojaribu kunirukia akajikuta akipitiliza na kuanguka sakafuni peke yake, alipotaka kusimama akakutana na teke maridadi lililotua kwenye kifua chake na kumrudisha tena sakafuni. Kabla hajainuka nikafyatua teke lingine lililompata kwenye shingo yake na kumfanya agugumie kwa maumivu huku akilegea.

Nikainama haraka na kumkwida shati huku nikimtazama kwa hasira, damu zilikuwa zikimtoka mdomoni na alikuwa akigugumia kwa maumivu.

“Wewe ni nani na nani amekutuma kuingia humu ndani?” nilimuuliza yule mtu. Akabaki kimya. Nikamuuliza tena, safari hii kwa ukali.

“Ah, si-ju-i…” alijibu kwa shida huku akijaribu kujiinua, lakini hakuweza kufanya hivyo.

“Unaniletea utani, eh?” nilimuuliza na kumkanyaga kwa nguvu shingoni kitendo kilichomfanya ashindwe kupumua, akaanza kutupa tupa miguu na mikono kwa kutafuta pumzi.

“U-uu-ta-ni-uua, ng-oo-ja nii- kwa-mbi-i-e,” yule mtu alisema kwa tabu. Nikalegeza mguu kidogo ili kumpa ahueni ya kupumua.

“Haya sema haraka,” nilimwambia huku nikiwa makini kuhakikisha kuwa hanizidi maarifa.

“Cha-me-leo-n,” yule mtu alijibu huku akiwa katika maumivu makali.

“Mpo wangapi mliotumwa kunifuatilia?” nilimhoji.

“Wa-ta-tu, we-weng-ine wa-po nje. Ah… una-unaniu-miza,” yule mtu alilalamika.

“Niambie, Rais mmemficha wapi?” nilimuuliza tena kwa ukali.

“Mi- mi si–sijui,” alijibu.

Muda huo huo mlio wa kuashiria kuwa ujumbe mfupi ulikuwa umeingia kwenye simu yangu ukasikika. Nikajua kulikuwa na ujumbe muhimu sana wa kunipa taarifa maana namba ile ilikuwa mpya ikiwa maalumu kwa ajili ya operesheni ile tu, Operesheni Utata, na ilijulikana na watu wanne tu; Kanali Mjaka, RSO Mama Komba, Daniella na mzee Othman Mwambe, ambaye aliifahamu kwa kuwa niliwasiliana naye kwa namba ile.

Wakati nikihangaika kutaka kuitoa simu yangu mfukoni, pasipo kujua, nikawa nimempa nafasi yule mtu pale chini, akajipindua kwa sarakasi ya aina yake na kusimama wima, nikagutuka na kumrushia teke kali lililokuwa litue kwenye korodani zake lakini akaliona na kulipangua kwa mikono yake huku akibonyea kama anachuchumaa, teke langu likashindwa kufika lilipokusudiwa baada ya kukingwa kwa ustadi mkubwa.

Hapo hapo nikazunguka na kuachia teke lingine lililotua katika paji la uso wake, akapepesuka na kujibwaga sakafuni. Hata hivyo yule mtu alikuwa sugu, kwani alijirusha sarakasi kinyume nyume kutoka pale sakafuni, na wakati huo huo akiichomoa bastola yake toka kiunoni na kuachia risasi mbili zilizonikosa baada ya kujitupa chini sakafuni, nyuma ya kitanda changu. Risasi zikachimba ukutani.

Kisha yule mtu akafanya kosa kubwa sana baada ya kurukia kitandani ili awe juu na kuniona kwa chini, nilikwisha jua nini yule mtu angefanya wakati nilipojitupa chini nyuma ya kitanda, na ndivyo ilivyokuwa. Kabla yule mtu hajafanya alichokusudia, nilijirusha juu huku nikizunguka na kumpiga teke kali la mzunguko, yule mtu akajibamiza ukutani na kuanguka chini kama gunia, roho yake ikaacha mwili.

Nilisonya na kuliendea lile kabati haraka, sikuwa na muda wa kupoteza, nikatoa yale mabegi yetu madogo ya mgongoni na kuchakura haraka haraka nikitoa vitu vichache vya muhimu na kuvitia katika mfuko niliokuwa nao, na wakati nikiyarudisha mabegi yale kabatini nikasikia sauti za vishindo vya hatua za watu wakikimbia nje ya ile korido kuukaribia mlango wa kile chumba chetu.

Nikajua kuwa tayari kazi mpya ilikuwa inanukia. Nilishahisi kuwa jambo la hatari lilikuwa mbioni kunikaribia hivyo sikutaka kusubiri, badala yake haraka nikakatisha kwenye kile chumba na kurukia kitandani nikielekea dirishani huku nikijipa tahadhari. Nilipofika pale dirishani nikasogeza pazia pembeni na kutoka.

Vile vishindo vya watu viliongezeka kwenye ile korido na hatimaye kuja kukomea nje ya ule mlango wa kile chumba chetu kisha ukimya mfupi ukafuata kabla ya kusikia kelele za kitasa cha ule mlango kikichokolewa kwa funguo. Sikutaka tena kusubiri, muda huo huo nilijiachia kwenye yale mabomba ya majitaka na kutua chini kama paka pasipo kufanya kishindo.

Halafu nikatulia kidogo nikipeleleza kama kungekuwa na mtu yeyote eneo lile na niliporidhika kuwa bado nilikuwa salama nikachepuka na kuanza kutembea kwa tahadhari nikiliacha eneo lile na kuelekea nyuma upande wa kushoto kwenye eneo la wazi lililokuwa na miti mingi ndani ya uzio wa hoteli ile.

Wakati nikitembea haraka na kwa hadhari kuelekea kwenye uzio wa hoteli ile nilijiuliza akilini kwangu, kitendo kile cha watu wale kujiamini kiasi kile na kuweka mitego kila sehemu tulipopita kilikuwa kinathibitisha ukweli wa maneno ya mzee Othman Mwambe kuwa, kulikuwa na uwezekano mkubwa kuwa Tiger alikuwa ana nafasi ya juu ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania… kama si mkuu wa majeshi, Jenerali Adam Kalembo basi Mnadhimu wa Jeshi, Luteni Jenerali Gozbert Bundala.

Sasa niliamini kuwa mpango ule wa kutekwa kwa Rais Masinde kwenye makazi yake ulikuwa na mkono wa mtu au watu wenye mamlaka makubwa ndani ya Jeshi na ndani ya kikosi cha ulinzi wa Rais, lakini sikuweza kuelewa lengo la watu hao kumteka Rais lilikuwa nini!

Wakati nikiukaribia uzio wa hoteli ile nilijitahidi kutazama huku na kule katika namna ya kutathmini vizuri mandhari ya eneo lile kwa usalama wa roho yangu. Kisha nikauparamia ule uzio na kurukia nje nikitokea kwenye Mtaa wa Duara, sehemu ambako Daniella alikuwa amelihamishia gari letu na kuliacha likiunguruma taratibu.

Mara tu Daniella aliponiona wakati nikitua katika barabara ya mtaa ule akaliondoka gari kunifuata, aliponifikia akapunguza mwendo, nikaufungua mlango na kurukia ndani ya gari na hapo hapo gari likaondoka kwa mwendo wa kasi huku magurudumu yakichimba barabara. Tukaenda kutokea katika Barabara ya Njombe, hapo akakata kushoto akiifuata barabara ile.

Kisha aliongeza mwendo na ndani ya muda mfupi tukawa tumetokea katika Barabara ya Uwanjani, akakunja tena kuingia kushoto akiifuata barabara ile ya Uwanjani hadi tulipotokea katika Barabara ya Chuno iliyopita kando kando ya Bahari ya Hindi. Kisha alikata tena kushoto kuifuata barabara ile ya Chuno, na muda mfupi baadaye tukapita mbele ya jengo la Naf Beach Hotel kwa mwendo wa kasi.

* * *

Endelea...
 
utata.JPG

367

Ujumbe wa siri…




Saa 6:05 usiku…

“KARIBUNI sana, vijana… karibuni ndani,” Daktari Chitemo alitukaribisha ndani huku akitutazama kwa mshangao na kutupa mikono kwa zamu, kisha akaongeza, “mmenitisha sana kunijia usiku huu bila hata taarifa.”

“Usihofu, mzee… tunatumaini kuwa hapa ni kwetu hivyo tunaruhusiwa kuja wakati wowote,” Daniella alisema.

“Ni kweli, hapa ni kwenu…” yule mzee alisema huku akitukaribisha kwenye makochi, “Lakini…”

“Kama umekubali kuwa hap ani kwetu hakuna tena cha lakini,” Daniella alisema na kutufanya wote tucheke. Kisha tuliketi na kumweleza yule mzee sababu ya ujio wetu pale kwake kuwa tuliamini ndiyo sehemu salama zaidi kwetu kwa usiku huo baada ya kubaini kule Naf Beach Hotel hapakuwa mahali salama tena.

Tuliamua kwenda pale ili kujipanga upya kabla ya kuianza ngwe nyingine ya harakati zetu za kumsaka Rais na kuhakikisha tumempata kabla dunia haijatambua kilichokuwa kikiendelea. Yule mzee hakuwa na kipingamizi, alituelewa. Na kwa sababu nyumba yake ilikuwa kubwa na yenye vyumba vingi, alituonesha vyumba ambavyo tungepumzika.

Kama binadamu wengine, mwili wangu ulijua kuchoka na ubongo wangu ulihitaji mapumziko. Kwani nilipokabidhiwa chumba kilichokuwa na kitanda kipana cha samadari kilichonialika kwa shuka safi zilizotandikwa vizuri na kisha nikaliona beseni la maji likimeremeta kwa usafi juu ya marumaru iliyofurika kila pembe ya ukuta na sakafu; ile hali ya uchovu ikazidi.

Kuoga nilitamani, na kulala nilitamani… ila sasa njaa haikuwa ikinitesa tena! Kwa hiyo sikutaka kujivunga, nilihitaji kuoga na kubadilisha nguo. Nilikuwa mchovu mno na sikuwa nimechafuka tu, bali kuchakaa. Jasho na vumbi mwilini mwangu vilinifanya nijisikie kunuka.

Nikavua nguo zangu haraka na kuingia katika beseni la kuogea, nikajilaza katika maji ya baridi na kukaa humo kwa dakika kadhaa nikiifurahia hali hiyo. Nilitamani niendelee kukaa humo hata kwa saa nzima au zaidi lakini sikuwa na muda huo. Bado tulikuwa na mengi ya kufanya kwenye harakati zetu za kumsaka Rais.

Awali ya yote, tulihitaji kuifungua ile bahasha ya kaki ambayo Daniella aliichukua kwa yule komando mamluki, Kapteni Edwardo Munambo, ili kuona kulikuwa na nini, halafu tukae mbele ya tarakilishi kwa ajili ya kutafuta majibu ya maswali yaliyotusumbua na pia kutafuta taarifa za kiintelijensia juu ya watu ambao tulishaanza kuwatilia shaka.

Nilitumia dakika ishirini kuoga na kuvaa nguo safi, suruali ya kijivu ya kitambaa cha kodrai na fulana nyeusi, kisha nikatoka na kuelekea sebuleni, nikiwa na Ipad yangu. Tulikuwa tumekubaliana mimi na Daniella kukutana pale sebuleni kwa ajili ya kupanga mikakati ya kazi. Muda huo Daktari Chitemo alikuwa ameshajipumzisha chumbani kwake.

Niliketi pale kwenye chumba cha ofisi nikimsubiri Daniella huku nikihisi kuwa akili yangu ilikuwa imepata utulivu wa kutosha wa kuweza kutafakari hili na lile na kutengeneza hoja zenye msingi, na wakati nilipokuwa nikitafakari nikamwona Daniella akija, yeye pia alikuwa ameoga na kubadilisha nguo, sasa alivaa jumpsuit ya rangi ya maruni iliyolichora vyema umbo lake zuri. Nikajikuta nikimeza mate ya tamaa.

Nilipomtazama vizuri sikuona kitu chochote mkononi mwake. Nikamuuliza kama alikumbuka kuichukua ile bahasha ya kaki aliyoichukua toka kwa yule komando mamluki, Edwardo Munambo.

Daniella alirudi haraka chumbani kwake na muda mfupi baadaye akawa amerejea tena pale sebuleni akiwa na ile bahasha mkononi, na hapo akaketi kwenye kochi huku akinikabidhi ile bahasha. Kabla ya kuifungua ile bahasha niliyapitisha macho yangu nikiichunguza kwa juu, kwenye mwanga wa taa ya umeme, hata hivyo sikufanikiwa kuona kitu chochote mle ndani kwani ile bahasha ilifungwa kwa gundi kali na karatasi yake haikuruhusu macho yangu kupenya na kuona ndani.

Nikaichana kwa juu na kuchungulia ndani na hapo nikaiona karatasi ndogo na nilipoitoa nikashangaa kuona haikuwa na maana yoyote kwangu kwani sikuweza kuona chochote kilichoandikwa kwenye karatasi ile.

Katika harakati zangu za ushushushu sikuwahi kukutana na kitu kama kile, hata hivyo Daniella hakuwa mshamba wa karatasi za namna ile na aliniambia kuwa hakuna binadamu mwenye akili timamu ambaye angetumbukiza karatasi isiyo na kitu ndani ya bahasha na kuifunga kwa gundi kali namna ile.

Aliichukua na kuigeuza geuza ile karatasi akiichunguza vizuri na hapo akaachia tabasamu na kuniambia kuwa ilikuwa ni aina fulani ya karatasi inayotumiwa sana na majasusi katika kupashana habari. Karatasi ambayo ili kuweza kuyasoma maelezo ndani yake ilihitajika mtu awe na kalamu ya grafiti.

Alisema kwa kawaida karatasi ya namna ile inapotumwa kwa mhusika hutumwa pamoja na kalamu yake maalumu, na hivyo akaichukua ile bahasha na kuichana na hapo akafanikiwa kuiona kalamu ndogo ya grafiti iliyochongwa vizuri.

Aliichukua ile kalamu kisha akailaza ile karatasi juu ya meza halafu akaanza kuichora chora kwa ule wino wa ile kalamu maalumu ya grafiti katika pembe isiyozidi nyuzi ishirini na tano ili aweze kupata taswira nzuri ya kilichoandikwa ndani ya karatasi ile.

Mwanzoni nilidhani kuwa ile karatasi ingekuwa na mchoro fulani wa siri au ramani ambayo ingehitajika jitahada za kipekee katika kutafsiri ili kuweza kuelewa kwani niliwahi kudokezwa kuwa karatasi za namna hii hutumika kupeleka ujumbe kwa njia ya mchoro. Lakini kadiri Daniella alivyokuwa akiichora chora karatasi ile nikawa naona herufi ambazo zilianza kuunganika na kutengeneza sentensi fulani.

Alizidi kuichora ile karatasi hadi mwisho na alipomaliza nikaona muunganiko wa codes ngumu za N-23 - 11:00. G-WH.164. zilizofuatiwa na sentensi kamili iliyoleta maana ikiwa katika lugha ya Kiingereza ikisomeka; ‘Farmstead is occupied of weeds; wheat must be reaped instantly’

Ukweli zile codes zilikuwa ngumu na sikuwa na ujuzi wa kuzifungua, ila nilijikuta nikijaribu kuutafakari ujumbe ule haraka haraka bila kupata maana yoyote kamili ya kunipa picha ya nini kilichokuwa kikiendelea. Ujumbe ule uliweza kutafsiriwqa kwa Kiswahili kuwa; shamba lilikuwa na magugu, na hivyo ngano ilitakiwa kuvunwa haraka.

Hata hivyo nilijipa muda kidogo huku nikiichunguza chunguza tena ile karatasi lakini sikuweza kuliona jina la mwandishi wala mtumiwaji wa ujumbe ule.

Muda huo Daniella alikuwa akizinakiri zile codes na kuanza kuzifanyia kazi. Yeye alikuwa mtaalamu wa codes. Na baada ya dakika therathini tulikuwa tumepata majibu ya codes zile.

“Novemba 23, saa tano kamili asubuhi, nenda kwenye ghala lililopo kitalu namba 164…” Daniella alisoma majibu ya codes zile.

Endelea...
 
utata.JPG

368

Haraka sana akili yangu ikaanza kupambanua nikijiuliza siku ile ilikuwa tarehe gani, sikuchelewa kupata jibu kuwa ilikuwa Novemba 22… Hii ilikuwa na maana siku iliyokuwa inafuata mtu yule alitakiwa kwenda kwenye ghala lililopo kitalu namba 164 saa tano asubuhi. Ghala hilo lilikuwa wapi na kulikuwa na nini huko kwenye ghala? hili lilikuwa swali la kwanza.

Ili kupata maana tukaanza kujadiliana kuhusu ile sentensi kuwa shamba lilikuwa na magugu, na hivyo ngano ilitakiwa kuvunwa haraka. Katika kujadiliana tuliweza kubaini mambo machache; ‘Shamba kuwa na magugu’ ilimaanisha kuwa sisi tulikuwa tumeingilia misheni ya watekaji hao. ‘Ngano kuvunwa haraka’ ilimaanisha kuwa walipaswa kumwondoa Rais Masinde…

Kumwondoaje? Aondolewe kutoka wapi? Au walipanga kumuua? Dah… kufika hapo akili yangu ilikataa kukubaliana na jambo lile! Mara nikakumbuka mahojiano yangu na yule mtekaji kule Paradise Café pale aliponiambia kuwa Rais Masinde alikuwa amefichwa ghalani. Na hapo moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu.

Ujumbe ule ulimaanisha kuwa kwa kuwa tulikuwa tumeingilia mishezi yao walitakiwa kumwondoa Rais haraka.

Lini? Novemba 23 saa tano kamili asubuhi. Wapi? Kwenye ghala lililopo kitalu namba 164! Halafu apelekwe wapi? Hakuna ajuaye! Dah akili yangu ikajikuta ikipata mtihani mgumu uliohitaji kupatiwa majibu kabla hapajapambazuka. Nilimtazama Daniella nikamwona yeye pia alikuwa amechanganyikiwa kama mimi.

Sasa nilianza kuhisi kuwa kulikuwa na hatari kubwa iliyokuwa ikimkabili Rais Masinde, hivyo tulipaswa kufanya mambo kabla ya muda uliotajwa kwenye ujumbe ule, kabla hakujapambazuka. Si hivyo tu, tulipaswa pia kuwa makini zaidi kuliko kujitumbukiza kizembe katika mkasa huu usioeleweka.

Kulikuwa na kitu kilichoanza kunisukuma moyoni kuwa hatukupaswa kulala usiku huo bali tulitakiwa kuinuka na kwenda kumsaka Rais kabla ya asubuhi… kabla ngano haijavunwa!

Nilipoitazama saa yangu nikagundua kuwa ilikwisha timia saa saba na dakika tano za usiku.

* * *



Saa 7:30 usiku…

Daniella alianza kuambaa na ukuta kuelekea ndani ya nyumba fulani ambayo mwanzoni alikuwa ameingia na kisha akapambana na akina komando Kapteni Edwardo Munambo. Wakati akitembea mimi nilikuwa nyuma yake nikichunga usalama wake. Tulikubaliana kuanzia kwenye nyumba ile harakati zetu za kumsaka Rais Masinde, kila mmoja wetu alikuwa makini, bastola zikiwa mkononi.

Tulifanikiwa kuingia ndani ya nyumba ile baada ya kumzimisha mtu mmoja aliyekuwa akilinda nyumba ile na kisha tukamfunga kamba madhubuti na kumficha kwenye banda moja, halafu tukaanza kukagua chumba kimoja baada ya kingine.

“Jason, nilinde,” Daniella aliniambia wakati tukiingia chumba cha kwanza, kisha akaibana bastola yake kwenye kiuno cha suruali aliyovaa. Chumba kile hakikuwa na chochote cha maana zaidi ya kitanda na vitu vichache tu. Daniella alilifuata kabati lililokuwa ukutani lililokuwa na droo kadhaa, akaanza kufungua droo moja moja, kila alipofungua palikuwa patupu, zaidi ya mataulo na mashuka hakukuwa na jipya.

Kisha tulitoka na kuingia katika chumba kingine mimi nikiendelea kumfuata nyuma, ndani ya chumba kile nako kulikuwa vivyo hivyo, tukaingia chumba cha tatu pia hatukubaini chochote cha muhimu. Tukiwa katika ujia mdogo wa kuelekea maliwato, nilikuwa bado nipo nyuma ya Daniella na bastola mkononi niliikamata vizuri kwa mkono wangu wa kuume tayari kupambana na chochote, Daniella aliyekuwa ametangulia mbele akauona mlango mwingine pembeni.

Akataka kuufuata, nikamzuia kwanza na kufanya uchunguzi baada ya kuhisi kulikuwa na sauti fulani isiyo ya kawaida, kumbe hata yeye alikuwa amehisi jambo kama hilo. Tukasikiliza kwa umakini kisha Daniella akaushika mlango ule na kujaribu kuufungua, ulikuwa umefungwa.

Aliutikisa tena na tena lakini ulionekana kufungwa kabisa, akaichomoa bastola yake toka kiunoni na kukifumua kitasa, mlango ukaachia na mara moja tukagundua kuwa chumba kile kilikuwa ni kama stoo, kulionekana vikorokoro vya ufundi na vitu mbalimbali vilivyolundikana.

Daniella akaishusha bastola yake na kuiweka tena kiunoni, halafu akavuta hatua moja na kufika mlangoni, akasita kuingia na kunusa nusa kama mbwa wa polisi. Alikuwa amehisi kitu na hivyo kabla hajaingia aliamua kutanguliza kwanza mkono wake aone kama kulikuwa na hatari yoyote ambayo ingemshambulia.

Kwa kufanya vile tukabaini kuwa hakukuwa na chochote cha hatari. Daniella alikuwa amefanya vile kwa kuhofia kuwa chumba kile kingeweza kuwa kimetegwa silaha maalumu ambayo mtu yeyote asiye rafiki na nyumba ile akiingia angeshambuliwa na bomu la misumari lakini kama ni mwenyeji angejua nini cha kufanya kwanza.

Baada ya kuridhishwa na hali ya usalama Daniella akaingia mle ndani na mimi nikamfuata nyuma nikiwa makini sana, tukasimama katikati ya chumba kile tukitazama huku na kule. Tukaona mashelfu yaliyopangwa ukutani, tuliyatazama tu kwa kitambo fulani pasipo kugusa kitu, baadaye Daniella akaanza kugusa na kutikisa hapa na pale, mahala fulani chini ya moja ya mashelfu yale akagundua kulikuwa na kipande cha marumaru ambacho kilitofautiana kidogo sana ua lake na vipande vingine.

Ilikuwa kazi ngumu sana kugundua jambo lile kwa mtu wa kawaida, ila kwa macho ya kishushushu ilikuwa kazi rahisi sana. Daniella akakikanyaga kile kipande na mara shelfu moja lililokuwa mbele yake likasogea pembeni taratibu na kuacha mlango mmoja uliofungwa.

Akashika kitasa cha mlango ule na kukinyonga, ule mlango badala ya kufunguka ukafyatuka kwa juu na kuwa kama unaoanguka kwenda ndani taratibu, mbele yake kulibaki na uwazi ambao ulikuwa sawa na chumba kidogo. Tukatazamana kwa mshangao maana nyumba ile kwa nje ilionekana ya kawaida lakini mle ndani tuliona mambo ya ajabu.

“Dah! Utata mwingi!” Daniella alisema huku akishika kiuno chake.

“Ngoja nishuke kwanza na wewe weka ulinzi,” nilimwambia Daniella huku nikimvuka, nikashusha bastola yangu na kuiweka kiunoni na kisha nikaanza kuteremka ngazi kwenye ule mlango nikielekea kule chini. Daniella akaungana nami kuteremka kule chini huku akilinda usalama wangu.

Tuliposhuka tukajikuta tumetokea kwenye chumba kimoja kipana kilichojengwa chini ya ardhi, kilikuwa ni chumba chenye mitambo mingi ya kielektroniki mfano wa studio ya redio.

“Naam, hapa ndipo wanapotumia kunasa mawasiliano yetu na pengine kutuma sehemu fulani,” nilimwambia Daniella baada ya kuiona ile mitambo. Kisha nilimtaka anilinde wakati nikiketi mbele ya mitambo ile na kuanza kufanya utundu wangu nikijaribu kuifungua ili kujua ilikuwa inanasa mawasiliano kutoka wapi na kutuma wapi.

“Utaweza kuioperate kweli hiyo mitambo?” Daniella aliniuliza akinitazama kwa mshangao.

Endelea...
 
utata.JPG

369

“Mimi ni Jason Sizya, linapokuja suala la teknolojia mimi ndo kiboko yao, hii ndiyo kitu iliyofanya niaminiwe kupewa kazi tata na Idara ya Ujasusi,” nilisema katika namna ya kujigamba.

All the best,” Daniella alisema na kukaa kimya. Hakutaka kuongeza neno lingine.

Kwa kuwa nilikuwa nimefanya kazi kwenye taasisi ya SPACE ambayo ilikuwa taasisi maalumu ya Usalama wa Taifa ya kushughulika na masuala yote ya kiteknolojia kama sehemu ya ulinzi wa kimtandao dhidi ya nchi, hivyo nilijiamini kuwa ningeweza kuifungua mitambo ile na kuyabaini mawasiliano yote.

Kabla ya yote niliwasha kwanza kiyoyozi na hapo hewa safi ya ubaridi ikaanza kuingia mle chumbani, kisha nikaanza kubofya hapa na pale na sikuchukua muda nikagundua kuwa ili kufungua mitambo ile na kupata mawasiliano ilihitajika kwanza kufungua codes fulani kwani mitambo ile ilikuwa imefungwa kwa namba maalumu ambazo mpaka ujue mjumuiko wake ndiyo uweze kupata mawasiliano.

Sikutaka kushindwa hasa kwa kuzingatia kuwa nilikuwa nimemtambia Daniella hivyo endapo ningeshindwa ingekuwa kichekesho cha mwaka. Pia nilitambua kuwa ni sisi wawili tu tuliokuwa tunategemewa na nchi kumkomboa Rais, japokuwa polisi na wapelelezi wao nao walikuwa wanafanya upelelezi juu ya tukio lile tata la kutekwa kwa Rais.

Kadiri nilivyocheza na zile codes niligundua kuwa zilikuwa ngumu sana kiasi cha kuanza kunitoa jasho. Daniella aliendelea kunitazama pasipo kusema neno. Kwa kweli ilikuwa kazi ngumu sana, kama vile kutafuta miguu ya nyoka.

Lakini baada ya kucheza na codes zile mara kadhaa hatimaye nilifanikiwa kuzifungua, hata hivyo hadi muda huo sikuwa nimegundua kulikuwa na chaneli ngapi zilizounganishwa kupeleka au kuleta mawasiliano pale kwenye kile chumba.

“Sasa hapa ninachotaka kufanya ni kutafuta kujua mitambo hii inatoa wapi mawasiliano na kupeleka wapi, na nani anayapokea…” nilimwambia Daniella kisha nikaongeza nikielezea kitaalamu, “hapa nitaiunganisha halafu nijaribu kuona codes zake zinavyooana, hapo tutajua upande gani unatuma taarifa kuja hapa na upande upi unapokea taarifa kutokea hapa, hii itakuwa rahisi sana kuwapata watu wetu.”

Daniella aliendelea kubaki kimya akinikodolea macho kwa mshangao maana kwenye masuala yale ya teknolojia alikuwa mtupu kabisa.

Niliziunganisha zile codes na kuiwasha ile mitambo, na hapo runinga kubwa iliyokuwa ukutani ikawaka na ramani ya Tanzania ikatokea huku yakionekana mawimbi fulani madogo madogo na mengine mawili makubwa, ambayo kwa haraka nilibaini kuwa yale mawimbi madogo zilikuwa chaneli za mawasiliano zilizokuwa zikileta taarifa pale kwenye kile chumba na yale mawimbi makubwa vilikuwa ni vituo vilivyokuwa vikipokea mawasiliano kutoka pale kwenye kile chumba.

Kama ramani ile ilivyojionesha, zile chaneli ndogo zilizokuwa zinaleta mawasiliano pale kwenye kile chumba zilikuwa zimetapakaa sehemu mbalimbali katika maeneo ya Dar es Salaam, Dodoma na pale Mtwara, na hii ilidhihirisha kuwa walikuwa wametega vinasa sauti kwenye ofisi kadhaa nyeti za taasisi za ulinzi na usalama, na hivyo taarifa zote za kutoka ndani ya ofisi hizo zilifika pale kwenye kile chumba bila chenga.

Halafu niligundua kuwa yale mawimbi makubwa mawili yaliyopewa utambulisho wa ‘the first wave’ na ‘the second wavei, vilikuwa vituo vikubwa vilivyopokea mawasiliano kutoka pale kwenye kile chumba. The first wave ilikuwa jijini Dar es Salaam na the second wave ilikuwa jijini Dodoma.

Hilo lilikuwa wazi kabisa, ila kazi kubwa ilikuwa kubaini vituo hivyo vilikuwa vipo kwenye majengo gani na nani walipokea mawasiliano hayo! Ningeweza kubaini endapo ningekuwa na muda kwani kazi hii haikuwa ya lelemama, ilihitaji muda wa kutosha wa kucheza na mitambo ile ili kubaini.

Tulipiga picha kila kitu ndani ya kile chumba kwa kutumia simu zetu zilizokuwa na kamera zenye uwezo mkubwa, kisha tukafanya upekuzi ndani ya chumba kile lakini hatukuweza kupata kingine chochote cha kutusaidia. Wakati tukianza kutoka nikaona kitu fulani ukutani kilichovuta umakini wangu.

Kilikuwa pembezoni mwa mlango ambapo kulikuwa kuna kitu kidogo chenye umbo la pembe nne, nikaanza kutafuta swichi fulani na kuiona kando ya ile mitambo ikiwa imefichwa, nilipoibonyeza sehemu fulani ya ukuta ikasogea.

Kiukweli nyumba ile kama ungeitazama kwa nje ungeichukulia kuwa ya kawaida sana na usingeweza kuipa uzito anaostahili. Kwenye macho ya kawaida ya binadamu ilikuwa ya kawaida lakini kiuhalisia ilikuwa kubwa sana kutokana na mambo kadha wa kadha yaliyowekwa katika muundo wa siri.

Baada ya ile sehemu ya ukuta kusogea likaonekana kabati moja lililokuwa limehifadhi nyaraka na makabrasha muhimu. Kulikuwa na mafaili mawili mekundu yaliyoonekana kuwa muhimu sana yakiwa na maandishi; Top Secret.

Niliyachukua nikampatia Daniella ayashike kisha nikaangaza hapa na pale lakini sikuona kitu kingine, tukaanza kutoka nje. Mara nikahisi kusikia sauti fulani, sauti kama karatasi. Nikampa ishara Daniella, halafu tukajigawa, yeye akielekea upande wa kushoto na mimi nikaelekea upande wa kulia.

Wakati nikizunguka upande ule wa kulia nikasikia tena sauti ya kitu kama karatasi nyuma yangu. Haraka nikageuza shingo kutazama. Sikumwona mtu! Nikaendelea mbele huku nikizungusha macho yangu kutazama huku na kule. Sikuona mtu.

Sasa nilikuwa karibu na banda tulilomficha yule mlinzi wa ile nyumba, takriban hatua nne hivi kulifikia lile banda, nikahisi tena sauti ile ya mwanzoni. Haraka nikageuka huku nikinyoosha bastola yangu kuielekeza huko. Sikuona mtu! Niliporejesha tu uso wangu mbele, nikakutana na mwanamume mmoja mrefu akiwa amesimama.

Akili yangu ilifanya kazi haraka sana, lakini yule mtu alionekana kuwa mwepesi zaidi yangu katika kufanya maamuzi, kufumba na kufumbua nikamwona akiwa juu, nikapigwa teke lenye kilo nyingi lililonitupa chini kama peto la pamba!

Nilinyanyuka upesi kwa kujifyatua na mikono yangu. Yule mtu alionekana kutonipa mwanya hata kidogo, akachumpa na kujilaza hewani akijizungusha kama tairi na kuchanua miguu yake, kisha akaachia teke lingine.

Mara hii nililiona, nikainama kidogo kulikwepa, na yule mtu alipotua tu chini, kabla sijakaa sawa, mkono wangu wenye bastola ukapigwa teke lingine, bastola ikarukia mbali. Nikatabasamu nikiamini kuwa sasa nilikuwa nimempata kiboko yangu.

Nilikiri kimoyomoyo kuwa nilikuwa nimekutana na mtu makini mwenye kila aina ya mbinu na ujuzi katika sanaa ya mapigano. Lakini hii haikuniogopesha na badala yake ilinifanya kuwa makini zaidi.

Baada ya kugundua kuwa aina ya upiganaji wa yule mtu ulifanana sana kimtindo na ule niliokuwa nikipenda kuutumia nikajua mchuano ungekuwa mgumu, na hivyo niliamua kuingiza mafunzo kadhaa ya kijeshi niliyoyapata toka kwa makomando kule nchini Misri. Nikatanua miguu yangu na kumwita yule mwanamume kwa ishara.

Kama nilikuwa nimemchukulia poa sasa niliamini kuwa nilikuwa napambana na mtu wa kazi na hivyo kama ningejilegeza Daniella angenicheka. Kwa hesabu za haraka haraka tu niliamini kuwa nilikuwa nammudu yule, kama ni matemebezi basi alikuwa ameingia peku peku kwenye shamba lenye mbigiri na hivyo alipaswa kuvumilia miiba.

Yule mtu alinisogelea kwa kasi huku akikunja ngumi, akarusha mateke mazito ambayo niliyaona na kuyaepa, mateke hayo yakapita kando ya kichwa changu. Akarusha ngumi, akarusha teke, akapiga viwiko, vyote hivyo niliviona, nikavinyima mwelekeo.

Jamaa akashangaa kidogo, na hapo nikawa nimeamsha kichaa chake maana yule mtu alianza kutuma ngumi zake nzito kwa spidi ya ajabu. Vuuuup! Vuuuup! Lakini niliweza kuziepa, zote zikapita! Yule mwanamume akatuma ngumi nyingine na nyingine, na nyingine… nikazikwepa zote kama niliyekuwa kwenye mchezo wa rede.

Jambo lile likamshangaza sana, na baada ya dakika moja na nusu hivi nikawa nimeshamsoma adui yangu, sasa nikaanza kujibu mashambulizi. Nilimwona Daniella akiwa amesimama kando ya ukuta akitutazama kwa umakini. Alikuwa ametuachia ukumbi sisi wawili tuoneshane umwamba.

Sikukutaka kupoteza nguvu, niliamua kupiga maeneo dhoofu kwenye mwili wa yule jamaa. Ncha za ngumi zangu zilitafuta kingo za kwapa za yule jamaa, nikamtia ganzi mikono yake. Halafu nilimpiga pia chini kidogo, katikati ya shingo, penye kashimo kanakotenganisha shingo na kifua, na kisha kummalizia juu ya kitovu.

Ilifikia hatua yule mtu akaonekana kuchoka kwani alikuwa ametumia nguvu nyingi kurusha ngumi zilizokuwa zinaenda patupu. Pia ukijumlisha na ngumi zangu zilizokuwa zinatua maeneo dhoofu basi alishindwa kufua dafu. Alikuwa hoi.

Ni wazi alikuwa ameshindwa kuhimili mapigo yangu na hakutaka kuingia kwenye mikono yangu, hivyo basi alijikakamua kisha akafanya kama aliyetaka kunirukia, nikaepa kidogo na hapo hapo nikamwona akijirusha kwenye ukuta uliokuwa ukiizunguka nyumba ile kwa namna ambayo ilinishangaza kidogo, akadanda juu.

Daniella alipoinua bastola yake kumlenga akawa amechelewa kwani yule mtu alijirusha kwa nje na kukimbia.

* * *

Usichoke, endelea kufuatilia hadi mwisho wa mkasa huu wenye utata...
 
Mkuu Bishop Hiluka naona kama #365 na #366 zimejirudia, pia 366 mwishoni hakuna mwendelezo mzuri kuelekea 367..

Au nina wenge? [emoji1787][emoji1787][emoji1787][emoji1787][emoji1787][emoji1787]
Dah, ni kweli, mkuu, nimesharekebisha na sasa #366 inasomeka vizuri na ina mwendelezo na #367. Halafu nilitaka kutupia nyingine naona tayari wameshachukua umeme wao.

Ahsante sana mkuu Ihayabuyaga, nilikuwa sijaona, macho yananisumbua sana...
 
Dah, ni kweli, mkuu, nimesharekebisha na sasa #366 inasomeka vizuri na ina mwendelezo na #367. Halafu nilitaka kutupia nyingine naona tayari wameshachukua umeme wao.

Ahsante sana mkuu Ihayabuyaga, nilikuwa sijaona, macho yananisumbua sana...
Mambo juu ya mambo taharuki juu ya taharuki!! Asante Bishop bado niko seat ya mbele.
 
Back
Top Bottom