SEHEMU YA 115
Mama Angel na baba Angel walikuwa mahali ambapo baba Angel alichagua ili yeye na mkewe wakae kwa karibu zaidi na kusahau yale yanayowafanya muda wote wasifikirie mambo yao zaidi ya biashara tu wanazofanya,
“Jamani mume wangu si ungeniambia sasa!”
“Aaaah kumbe hujui eeeh! Safari za kushtukizana ndio nzuri mpenzi. Mimi na wewe tunapendana, kwahiyo naweza panga safari yoyote kwa muda wowote kwani najua huwezi kukataa. Je hujafurahia huku mke wangu?”
“Nimefurahi sana yani, mara nyingine watoto nao wanachanganya sana akili, mtu ukipata sehemu kama hii unashukuru sana kwakweli”
Mara simu ya mama Angel ilianza kuita, kuangalia ni ile namba ya siku ile, wasiwasi wake ni kuwa huenda mpigaji wa ile simu ni baba Abdi sababu siku ile ni mkewe aliongea na kwa haraka haraka alihisi ile sauti kama ni sauti ya Fetty vile, basi mumewe akamwambia kuwa apokee,
“Pokea mke wangu, huwezi jua ingawa sikupenda tukiwa huku tusumbuliwe na simu”
Basi mama Angel alipokea, na kama alivyohisi ni kweli baba Abdi ndiye aliyekuwa akimpigia ile simu,
“Oooh asante sana kwa kupokea simu yangu, ujue nimekumiss sana wewe mwanamke”
“Kwani wewe una matatizo gani jamani!!”
“Sina matatizo yoyote, wewe ndio chanzo cha mimi kuoa mwanamke asiyeeleweka, na wewe ndio chanzo cha yule mwanamke kunifanyia dawa mimi hadi nikazaa hovyo, na wewe ndio chanzo cha mpaka sasa siishi kwa amani na mke wangu maana muda wote nakukumbuka na kukutaja sana kwani ungeishi nami najua watoto wangu wangepata malezi mazuri sana”
“Una wazimu wewe”
Kisha mama Angel alikata ile simu na mumewe alimuuliza, ambapo hakutaka kumficha kwani alimwambia ukweli wote,
“Kheee jamani, hivi huyu si ndio kwenye harusi yetu aliongea sana nikajua yameisha mke wangu, bado tu anakufatilia!! Nahitaji kuongea nae kiume”
“Hata mimi namshangaa, eti analalamika maisha yake yameharibika sababu yangu”
“Huyu ni mjinga, maana mtu unaharibu maisha mwenyewe na sio mtu mwingine, kwani wewe umeharibu vipi maisha yake?”
Mama Angel alimwambia mumewe waachane tu na habari hizo na waendelee kufurahia kilichowapeleka kule kwani hakutaka kuongea yaliyopita.
Leo ndio ilikuwa Jumamosi ambayo Samir alienda nyumbani kwa madam Hawa, ambaye alisema kuwa siku hiyo ndio aende akaongee nae vizuri, kiukweli hata yeye huwa haelewi mantiki ya kinachofanywa na yule madam kwahiyo anachukulia kawaida tu, basi alienda kumsikiliza,
“Madam, nimeitikia wito”
“Maisha unayoishi sasa yani mimi nikionekana kama mzazi wako unayaonaje?”
Samir alinyamaza kimya kidogo, kumbe kile alichokuwa akifanyiwa ni kama mtoto wa mwalimu, basi alipumua kidogo na kujibu,
“Nimeyapenda”
“Mbona umewaza sana? Ulikuwa ukifikiria ni kitu gani? Au ulifikiria kuwa nakutaka?”
“Hapana madam”
Kisha madam hawa akacheka na kusema,
“Siwezi katika maisha yangu yote kuwa na mahusiano na kujana mdogo kama wewe, yani maisha ninayokupa shuleni nahitaji ujione kama mtoto wa mwalimu na usome kwa bidii na uache kumfatilia Angel yani ukitaka kufanya ujinga ujue kuwa mama yangu yupo hapa shuleni ananiona. Mimi sikuhitaji kwakweli, na walimu wote wanaelewa kuwa kwanini nafanya hivi, nakuweka vizuri kisaikolojia. Haya niambie kwasasa, unasumbuliwa sana na mawazo ya Angel?”
“Hapana”
“Sawa, mara nyingi huwa unafanya nini?”
“Mara nyingi umekuwa ukinipa zoezi na maswali ya kufanya, kwahiyo nikirudi nyumbani nakosa muda wa kukaa na kuwaza maana asubuhi huwa unahitaji nikupatie hayo maswali, na moja kwa moja huwa unakuja na kuniita darasani kwahiyo nimejikuta nikiwa busy sana”
“Na hiko ndio nilichokuwa nakitaka toka mwanzo, nilitaka wewe ukazanie masomo na sio kitu kingine chochote. Kama ulikuwa unawazo kuwa madam Hawa anakutaka kimapenzi naomba usahau kabisa kabisa, maana mimi nakupenda kama mtoto wangu ndiomana niliongea na mama yako aniruhusu nianze kukulea mwenyewe shuleni ili kukurudisha kwenye mstari, si vizuri kufanya mzazi atupe hela kila siku sababu ya kukuhamisha wewe shule, si vizuri kwakweli mnatuumiza wazazi, niliumia sana wakati mama yako akiongea ndiomana nikabeba jukumu la kuwa nawe bega kwa bega”
“Asante sana madam”
“Sasa nadhani utakuwa huru zaidi maana mwanzoni ulikuwa na mashaka kuwa sijui huyu madam ananitaka sijui nini na nini, ondoka kabisa hayo mawazo maana mimi ni kama mama yako tu”
Basi Samir aliitikia ambapo yule madam alimpa maswali mengine na kuagana nae kuwa arudi kwao.
“Moja kwa moja nyumbani Samir, nitawasiliana na mama yako maana anajua kama ulikuja kwangu”
“Sawa madam”
Basi Samir aliondoka muda ule na kuelekea kwao.