SEHEMU YA 154
Kulipokucha siku hiyo aliamshwa na mama yake maana yeye alilala hoi hata habari hakuwa nayo, aliamka na kujiandaa kisha kwenda ofisini, alimkuta shemeji yake yupo ofisini tayari kanakwamba alilala palepale na alikuwa na nguo zile zile za jana, ikabidi aende ofisini kwa shemeji yake kuongea nae vizuri maana zile ofisi zilikuwa za vioo ambavyo vilikuwa vinaonyesha kama bosi yupo au hayupo.
Erica aliingia kuzungumza nae,
“Shemeji vipi? Inaonyesha hukurudi nyumbani kwako!”
“Na kweli sikurudi hata sijui ni jinsi gani nitamuangalia mke wangu”
“Ila mbona jana uliondoka hapa kama unaenda kwako?”
“Unajua nimechanganyikiwa eeh Erica, ni kweli nilikuwa naenda nyumbani kwangu ila nilipofika tu nilimsikia mke wangu akigombana na kile kisichana halafu kwa mbali nikamuona dada yenu Mage anakuja, mmmh namuogopa Yule dada, nikaona hapa balaa ndio nikaondoka sijarudi kabisa nyumbani tena”
“Sasa utaweza kufanya kazi hivyo?”
“Hata sijui, kichwa chote kimenivurugika. Jana nilienda kunywa pombe, na nilizinywa sana ili mawazo yakae sawa”
“Basi, ilitakiwa leo unywe supu kwanza”
“Basi nisindikize Erica, nakuomba na wala sitakwambia tena mambo ya mapenzi”
Kiukweli James alionekana mtu wa kujutia kwa kile alichokitenda, na Erica alikubali kumsindikiza shemeji yake akapate supu kwahiyo ilibidi amuachie maagizo msaidizi wake na kuondoka na Erica.
Walifika kwenye baa kisha akaagiza supu, ikabidi naye Erica aagize supu huku akijaribu kuongea na huyu shemeji yake maana lazima kuna kitu kinachomfanya shemeji yake kuwa katika ile hali,
“Hivi shemeji, kwani humpendi dada?”
“Hapana, nampenda”
“Sasa kwanini unamsaliti?”
“Erica, ngoja leo nikwambie sababu ya mimi kumsaliti dada yako. Mimi ni mwanaume, nahitaji mapenzi yale yenyewe yenyewe kiasi kwamba nikiyapata wala nisitamani mwanamke mwingine. Jamani Erica, dada yako hajui mapenzi kabisa yani hajui kitu hata najuta kuoa mwanamke mshamba kama yeye. Kwa nje anaonekana mjanja ila kumbe mshamba”
“Mmmh jamani! Nyie wanaume hamna shukrani, umepata mwanamke bikra unasema ni mshamba, ila ukipata aliyetangatanga ndio mjanja halafu wakati huo huo mnapenda kuoa mabikra sababu ndio heshima. Ushamba wa dada yangu hauwezi kufanya wewe umsaliti, kumbuka wewe ndio wa kumfundisha mapenzi dada, hivi usipomfundisha wewe atafundishwa na nani?”
“Erica, hujui tu. Nilipoenda ulaya nilijua nikirudi atakuwa amejifunza mambo mengi ila ndio kwanza yupo kama gogo hata hajishughulishi na alivyopata mimba ndio kabisaaa kila ukimshika anadai anaumwa, hivi kuna wanawake wangapi wanaishi vizuri na waume zao na mimba zao? Dadako anadeka sana, yani yeye ndio anapelekea mimi kumsaliti”
“Ila unavyofanya sio vizuri, wewe ndio wa kumbadilisha dada, mwambie hupendi ambavyo anakosa ubunifu nina uhakika dada atajifunza vitu vipya vya kufanya na wewe. Usihangaike nje shemeji yangu, magonjwa mengi sana.”
“Una maneno ya busara sana, hadi natamani wewe ndio ungekuwa mke wangu, yani Bite nilimuoa basi tu”
“Umeanza maneno yako shemeji”
“Sio nimeanza Erica, kiukweli natamani wewe ndio ungekuwa mke wangu. Upo tofauti sana Erica, wewe ni msichana kati ya wasichana ambao sijawahi kukutana nao maishani. Erica ungekuwa aina nyingine ya msichana ungeshatangaza kwenu kuwa nilikutaka kimapenzi ila mpaka leo imebaki kuwa siri yako kwa kulinda penzi la dada yako. Erica kiukweli, mume atakaye kuoa atakuwa amepata mke haswaaa, tofauti na dada yako kitu kidogo lazima aseme nyumbani kwenu hadi najuta kumuoa”
“Mmmh jamani! Ulilazimishwa kwani?”
“Hapana sikulazimishwa ila kuna mwanamke nilikuwa nae kabla ya Bite, alikuwa ni binti wa ukweli ila sikuweza kuoana nae sababu ya itikadi. Na nilivyokutana na Bite, binti mpole basi nikatangaza ndoa maana Yule msichana niliyempenda nae alikuwa ameolewa”
“Mmmh mapenzi bhana, kizunguzungu tu. Kwahiyo wewe ulimpendea nini dada?”
“Kiukweli Bite nampenda akicheka anavyobonyea mashavuni yani hapo roho yangu burudani, ila sikujua kama atakuwa mshamba vile kwenye mapenzi”
“Yani ulimpendea dimpozi tu? Ila kwasasa si unampenda dada kushinda Yule wa zamani?”
“Ndio, nampenda sana Bite halafu nampenda kweli ila kwasasa naomba unisaidie jambo moja tu, naomba wewe uende kwanza nyumbani kwangu. Ongea kwanza na dadako ndio mimi nitakuja maana najua una maneno ya busara na unaweza kumfanya dadako anisamehe na tuendelee vyema kumkuza mtoto wetu”
Erica alikubali na shemeji yake alimuomba muda ule ule aende kwahiyo James alimuombea tu udhuru ofisini,
“Ila shemeji usinywe tena pombe basi”
“Sinywi, ukiongea nae tu vizuri akikaa kwenye mstari niambie nije”
Sawa”
Erica aliondoka pale na kwenda kwa dadake, huku akiwaza kuhusu vitu vingi sana, aliona kuwa mapenzi ni kitu cha ajabu sana kumbe mtu anakwambia anakupenda halafu alimpendaga mwingine ila hayupo nae tena kwahiyo inabidi aishie kukwambia wewe tu anakupenda, ila hakufikiria kama ushamba wa dada yake ndio unamfanya shemeji yake awe msaliti ila ile ni tabia ya shemeji yake ndiomana ameweza kumtongoza hata yeye.