Simulizi: Nini maana ya mapenzi

Simulizi: Nini maana ya mapenzi

SEHEMU YA 151


Erica alimaliza shughuli alizopangiwa kisha akaaga ili kuondoka, ila alipotoka ofisini tu alimkuta Bahati akimsubiriria nje, na alipomuona alimsogelea na kumkumbatia ila kilichomshangaza ni kumuona Mrs.Peter akiwapiga picha, akaanza kumuuliza Bahati kabla hawajamsogelea huyu mama,
“Vipi umekuja na mama huyu?”
“Aliuliza kila siku nawahi wapi, nikamwambia huwa nawahi kumpitia mke wangu nimrudishe nyumbani kwanza. Ndio akasema leo tuje wote”
“Sasa mbona alikuwa anatupiga picha?”
“Kuhusu picha sielewi, labda ngoja tumuulize”
Walisogea karibu na kumsalimia, Yule Mrs.Peter alianza kujieleza mwenyewe kabla hata hajaulizwa,
“Nimekupiga picha Erica ili kupata picha ya ukumbusho na uthibitisho. Unajua Rahim nilimwambia kuwa nimemuona mumeo akanikatalia katakata kuwa huna mume, sasa leo nataka nimtumie na picha kabisa aone”
Erica alihema kwanza na kumuuliza,
“Khaaa mama, sasa picha za mimi na mume wangu umtumie Rahim za nini?”
“Unajua ulivyoongea hivyo nimekurekodi na nishamtumia? Picha nazo nishamtumia kwani kuna ubaya gani?”
Erica alimuangalia huyu mama na kutamani hata kumnasa vibao.


Walisogea karibu na kumsalimia, Yule Mrs.Peter alianza kujieleza mwenyewe kabla hata hajaulizwa,
“Nimekupiga picha Erica ili kupata picha ya ukumbusho na uthibitisho. Unajua Rahim nilimwambia kuwa nimemuona mumeo akanikatalia katakata kuwa huna mume, sasa leo nataka nimtumie na picha kabisa aone”
Erica alihema kwanza na kumuuliza,
“Khaaa mama, sasa picha za mimi na mume wangu umtumie Rahim za nini?”
“Unajua ulivyoongea hivyo nimekurekodi na nishamtumia? Picha nazo nishamtumia kwani kuna ubaya gani?”
Erica alimuangalia huyu mama na kutamani hata kumnasa vibao.
Huyu mrs.Peter aliona jinsi Erica alivyoonekana kuchukizwa na swala lile, akamuuliza tena,
“Kwani nimefanya vibaya mwanangu?”
Erica alikuwa kimya tu, Yule mama akamuangalia Bahati na kumuuliza
“Eti baba nimefanya vibaya?”
“Hapana mama, naona ni vizuri tu maana mimi na Erica tunapendana sana”
“Asante, ndio nilichokuwa nakitaka, kwaheri”
Yule mama aliondoka na kuwaacha pale wamesimama, ila kiukweli Erica hakuwa na raha hata safari ya kwenda kwa dada yake aliahirisha na kutaka tu kwenda moja kwa moja nyumbani kwao.
 
SEHEMU YA 152


Erica alifika kwao ila mama yake hakumkuta kwa muda huo akahisi labda mama yake amechelewa kwenye vikoba vyake siku hiyo, ila sababu alikuwa na mawazo aliamua kwenda kulala tu, ila hata usingizi wenyewe haukumpata kwani alikuwa na mawazo lukuki, akawaza kuwa pesa ambazo huwa anapewa na Rahim zitakuwa zimefikia mwisho maana akiambiwa tu na mama yake na kutumiwa ushahidi wa picha na sauti yeye atakuwa ameisha kabisa, aliwaza sana na muda nao ulienda ila mama yao alikuwa bado hajarudi hadi akataka kumpigia simu ili ajue tatizo ni nini. Ila wakati anawaza kumpigia simu alisikia sauti yake ikiita, ikabidi aende kumsikiliza,
“Kila siku huwa nasema wanaume ni mbwa jamani tena mbwa kabisa”
“Kwani vipi mama?”
“Si Yule shemeji yako James, kumbe kampa mimba Yule msichana wa kazi, yani sokomoko la huko leo lilikuwa balaa, hujashangaa hujanikuta hapa nyumbani!”
“Nimeshangaa na nikajiuliza kuwa imekuwaje, nikadhani labda upo kwenye kikoba”
“Kikoba wapi? Mambo yalikuwa sio mambo huko, Mage alinipigia simu ndio nikaenda, jamani mwanaume Yule anaonekana mstaarabu kwa nje kumbe mbwa tu”
“Ila mama kwani wanaume wote wapo hivyo?”
“Hakuna mwanaume aliyetulia mwanangu, yani kuhusu usumbufu wa wanaume ni kilio cha kila mwanamke”
“Mmmh mama ila si huwa unawasema makapuku tu, kumbe wenye hela nao hawafai”
“Hakuna cha mwenye hela wala kapuku, yani kiukweli mwanangu mimi hata sielewi kama kuna wanaume wanaishi bila usaliti jamani”
“Wapo mama”
“Hawapo, labda ashushwe toka mbinguni. Usimkatalie mwanaume hata mara moja, uwezi jua mambo anayoyafanya nyuma ya pazia”
“Mmh sawa mama, ila mmeishia vipi kwa dada sasa?”
“Yani Bite alitamani kurudi nyumbani ila nimemshauri kurudi nyumbani sio suluhisho, kwani ni lazima akae hapo na mumewe na wajue ni wapi alikosea mpaka mume wake akamsaliti.”
“Kwahiyo huyo mwenye mimba kaenda wapi?”
“Tumemfukuza, unajua unapokuwa mke wa mtu inabidi ujivike moyo wa ukatili maana ukiwa mpole sana mumeo atawapa mimba hadi kuku na kukuletea nyumbani. Tumemfukuza pale, atajua mwenyewe pa kwenda”
“Na shemeji?”
“Hajarudi hadi tunaondoka ila kwa nilichomfundisha Bite Yule mumewe ataelewa tu. Nawajua wanaume kupita hata wanavyojijua wenyewe”
Erica alimuangalia mama yake anayesema anawajua wanaume sana ila alishindwa kumshauri mwanae kuwa akae karibu na mumewe asiibiwe na msichana wa kazi maana ingewezekana kabisa Bite angejifungulia kwa mume wake na mama yake angekuwa anaenda kumtazama ila kwavile alitulia kwao ilitoa upenyo mkubwa sana kwa mumewe kuwa na msichana wa kazi ukizingatia mume wake mwenyewe ni penda penda.
 
SEHEMU YA 153


Erica aliagana na mama yake na kwenda kulala maana ilikuwa ni saa tano usiku, hakuwa na usingizi sababu ya mawazo ila aliamua kwenda tu kujilaza, ila kabla hajajibembeleza vizuri na usingizi akapokea ujumbe wa kawaida ukitoka kwa Rahim,
“Naomba uingie facebook muda huu”
Ilibidi Erica achukue simu yake na kuingia kwenye mtandao kwani alijua lazima atakutana na lawama sababu Yule mama inaonyesha tayari alishasema, alipoingia tu akakutana na jumbe kadhaa kutoka kwa Rahim, kwanza aliona picha za yeye na Bahati pia akatumiwa zile sauti ya kwanza akasikia yeye akisema “Khaaa mama, sasa picha za mimi na mume wangu umtumie Rahim za nini?” na sauti ya pili ilikuwa ya Bahati na ilisikika, “mimi na Erica tunapendana sana”
Erica alizisikiliza na kumshangaa sana mrs.Peter
“Jamani Yule mama ana mambo ya Kiswahili loh! Sasa kumtumia mwanae picha na sauti ili iweje jamani? Kwani anahisi natoka na mwanae au? Sasa anamchunga hivyo mwanae na kumtafutia wachumba wa nini sasa? Loh mama mswahili sijapata kuona”
Kisha akaendelea kuangalia ujumbe utakaofatia toka kwa Rahim,
“Erica naomba unieleze kuhusu hizo picha na hiyo sauti”
“Rahim hata sijui nikwambie nini”
“Unajua Erica umeniumiza sana, hivi unajua hilo? Umeumiza sana moyo wangu, kwanini kunifanyia hivi? Yani unanifanya mimi kama poyoyo”
“Hapana Rahim usinifikirie vibaya, nadhani tu mama amenielewa vibaya”
“Hivi nyie wanawake mkoje? Mnataka mpewe nini ndio mridhike nyie? Kwenu mwanaume akikupa pesa ni shida, akikupa mapenzi ni shida, hivi mnataka nini haswaa? Kuna kitu hupati kwangu Erica? Nimekwambia ukiwa na shida yoyote niambie nitakusaidia, nimejitoa kwaajili yako Erica halafu wewe unaenda kunifanyia upuuzi huu kweli?”
“Rahim hata sijui nikueleze nini ila mama kanielewa vibaya tu”
“Erica nilishakutahadhalisha kuhusu mama yangu, hata hivyo mama yangu sio chizi kusema akurupuke tu kufanya mambo. Sikutegemea Erica kama ungeweza kudanganywa na kijana mwingine ilihali nakupa kila kitu cha kukuonyesha kwamba nakupenda. Unajua kinachoniuma zaidi ni nini? Ni huyo kijana, nakumbuka nilibishana nae kuwa kati yake na mimi anapendwa nani? Sasa kama mimi na huyo tu hujui umchague nani, je huyo Erick akisema arudi utanifikiria mimi kweli?”
Erica alisoma huu ujumbe mara mbili mbili na kushindwa ajibu vipi ila aliishia tu kutuma meseji,
“Nisamehe Rahim”
“Erica, kuna siku nitakufanyia kitu ambacho hutokuja kukisahau katika maisha yako”
“Jamani Rahim, ndio unafikia huko kweli? Naomba unisamehe maana hata nikikuelezea hautaniamini ila naomba unisamehe”
“Erica umeniudhi haijapata kutokea yani leo umefanya siku yangu iwe mbaya kuliko siku zote, umeniudhi sana Erica hata sijui nifanyeje”
“Naomba unisamehe Rahim”
“Erica, sijui niseme nini ila kwavile nakupenda. Kwasasa lala tu, sina cha kukwambia”
Erica alibaki kuandika jumbe za kuomba msamaha tu bila ya kujibiwa tena huku akiwaza kuwa ni kitu gani kibaya atakachopangiwa na Rahim, hakuelewa ila pia hakujua kama Rahim anaweza kumsamehe na aendelee kuwasiliana nae kama zamani kwani kwa kipindi hiko ni kweli hela ya Rahim ndio iliyokuwa inamtia kiburi.
Akaamua kulala tu maana hata akiendelea kufikiria sana haina maana na muda huo ulikuwa umeenda ilikuwa ni saa nane usiku, halafu kesho yake anahitajika aende kule kwenye mafunzo asubuhi halafu anachelewa hivyo kulala. Ikabidi tu atafute usingizi ingawa kwa nadra, akalala, huku akifikiria kuanza kumuweka moyoni mwake Bahati maana hakujua ni kitu gani Rahim kapanga kwaajili yake, akawaza ile hela aliyopewa na Rahim ile milioni mbili kuwa alifanya vyema kupunguza milioni moja na kumpa Bahati aongezee mtaji ambao ni hela nyingine aliyoipata kwa Rahim ila kwa muda huo alihisi huenda Bahati ndiye mwanaume wa kutengeneza nae maisha.
 
SEHEMU YA 154


Kulipokucha siku hiyo aliamshwa na mama yake maana yeye alilala hoi hata habari hakuwa nayo, aliamka na kujiandaa kisha kwenda ofisini, alimkuta shemeji yake yupo ofisini tayari kanakwamba alilala palepale na alikuwa na nguo zile zile za jana, ikabidi aende ofisini kwa shemeji yake kuongea nae vizuri maana zile ofisi zilikuwa za vioo ambavyo vilikuwa vinaonyesha kama bosi yupo au hayupo.
Erica aliingia kuzungumza nae,
“Shemeji vipi? Inaonyesha hukurudi nyumbani kwako!”
“Na kweli sikurudi hata sijui ni jinsi gani nitamuangalia mke wangu”
“Ila mbona jana uliondoka hapa kama unaenda kwako?”
“Unajua nimechanganyikiwa eeh Erica, ni kweli nilikuwa naenda nyumbani kwangu ila nilipofika tu nilimsikia mke wangu akigombana na kile kisichana halafu kwa mbali nikamuona dada yenu Mage anakuja, mmmh namuogopa Yule dada, nikaona hapa balaa ndio nikaondoka sijarudi kabisa nyumbani tena”
“Sasa utaweza kufanya kazi hivyo?”
“Hata sijui, kichwa chote kimenivurugika. Jana nilienda kunywa pombe, na nilizinywa sana ili mawazo yakae sawa”
“Basi, ilitakiwa leo unywe supu kwanza”
“Basi nisindikize Erica, nakuomba na wala sitakwambia tena mambo ya mapenzi”
Kiukweli James alionekana mtu wa kujutia kwa kile alichokitenda, na Erica alikubali kumsindikiza shemeji yake akapate supu kwahiyo ilibidi amuachie maagizo msaidizi wake na kuondoka na Erica.
Walifika kwenye baa kisha akaagiza supu, ikabidi naye Erica aagize supu huku akijaribu kuongea na huyu shemeji yake maana lazima kuna kitu kinachomfanya shemeji yake kuwa katika ile hali,
“Hivi shemeji, kwani humpendi dada?”
“Hapana, nampenda”
“Sasa kwanini unamsaliti?”
“Erica, ngoja leo nikwambie sababu ya mimi kumsaliti dada yako. Mimi ni mwanaume, nahitaji mapenzi yale yenyewe yenyewe kiasi kwamba nikiyapata wala nisitamani mwanamke mwingine. Jamani Erica, dada yako hajui mapenzi kabisa yani hajui kitu hata najuta kuoa mwanamke mshamba kama yeye. Kwa nje anaonekana mjanja ila kumbe mshamba”
“Mmmh jamani! Nyie wanaume hamna shukrani, umepata mwanamke bikra unasema ni mshamba, ila ukipata aliyetangatanga ndio mjanja halafu wakati huo huo mnapenda kuoa mabikra sababu ndio heshima. Ushamba wa dada yangu hauwezi kufanya wewe umsaliti, kumbuka wewe ndio wa kumfundisha mapenzi dada, hivi usipomfundisha wewe atafundishwa na nani?”
“Erica, hujui tu. Nilipoenda ulaya nilijua nikirudi atakuwa amejifunza mambo mengi ila ndio kwanza yupo kama gogo hata hajishughulishi na alivyopata mimba ndio kabisaaa kila ukimshika anadai anaumwa, hivi kuna wanawake wangapi wanaishi vizuri na waume zao na mimba zao? Dadako anadeka sana, yani yeye ndio anapelekea mimi kumsaliti”
“Ila unavyofanya sio vizuri, wewe ndio wa kumbadilisha dada, mwambie hupendi ambavyo anakosa ubunifu nina uhakika dada atajifunza vitu vipya vya kufanya na wewe. Usihangaike nje shemeji yangu, magonjwa mengi sana.”
“Una maneno ya busara sana, hadi natamani wewe ndio ungekuwa mke wangu, yani Bite nilimuoa basi tu”
“Umeanza maneno yako shemeji”
“Sio nimeanza Erica, kiukweli natamani wewe ndio ungekuwa mke wangu. Upo tofauti sana Erica, wewe ni msichana kati ya wasichana ambao sijawahi kukutana nao maishani. Erica ungekuwa aina nyingine ya msichana ungeshatangaza kwenu kuwa nilikutaka kimapenzi ila mpaka leo imebaki kuwa siri yako kwa kulinda penzi la dada yako. Erica kiukweli, mume atakaye kuoa atakuwa amepata mke haswaaa, tofauti na dada yako kitu kidogo lazima aseme nyumbani kwenu hadi najuta kumuoa”
“Mmmh jamani! Ulilazimishwa kwani?”
“Hapana sikulazimishwa ila kuna mwanamke nilikuwa nae kabla ya Bite, alikuwa ni binti wa ukweli ila sikuweza kuoana nae sababu ya itikadi. Na nilivyokutana na Bite, binti mpole basi nikatangaza ndoa maana Yule msichana niliyempenda nae alikuwa ameolewa”
“Mmmh mapenzi bhana, kizunguzungu tu. Kwahiyo wewe ulimpendea nini dada?”
“Kiukweli Bite nampenda akicheka anavyobonyea mashavuni yani hapo roho yangu burudani, ila sikujua kama atakuwa mshamba vile kwenye mapenzi”
“Yani ulimpendea dimpozi tu? Ila kwasasa si unampenda dada kushinda Yule wa zamani?”
“Ndio, nampenda sana Bite halafu nampenda kweli ila kwasasa naomba unisaidie jambo moja tu, naomba wewe uende kwanza nyumbani kwangu. Ongea kwanza na dadako ndio mimi nitakuja maana najua una maneno ya busara na unaweza kumfanya dadako anisamehe na tuendelee vyema kumkuza mtoto wetu”
Erica alikubali na shemeji yake alimuomba muda ule ule aende kwahiyo James alimuombea tu udhuru ofisini,
“Ila shemeji usinywe tena pombe basi”
“Sinywi, ukiongea nae tu vizuri akikaa kwenye mstari niambie nije”
Sawa”
Erica aliondoka pale na kwenda kwa dadake, huku akiwaza kuhusu vitu vingi sana, aliona kuwa mapenzi ni kitu cha ajabu sana kumbe mtu anakwambia anakupenda halafu alimpendaga mwingine ila hayupo nae tena kwahiyo inabidi aishie kukwambia wewe tu anakupenda, ila hakufikiria kama ushamba wa dada yake ndio unamfanya shemeji yake awe msaliti ila ile ni tabia ya shemeji yake ndiomana ameweza kumtongoza hata yeye.
 
SEHEMU YA 155


Alifika na kumkuta dadake kajiinamia tu, na alionyesha kuwa na mawazo mengi sana. Alimkaribisha ila alikuwa na unyonge wa hali ya juu,
“Pole dada, naelewa matatizo unayopitia”
“Yani acha tu mdogo wangu”
Erica alijaribu kuongea na dada yake kwa maneno ya busara ili hata akirudi mume wake asije akamfanyia hasira,
“Dada najua unavyompenda shemeji na yeye anakupenda, wala usiruhusu shetani ayaingilie mapenzi yenu. Msamehe Yule ni mumeo, akirudi mkaribishe na akipumzika muulize kwa upendo tu kuwa ilikuwaje akafikia hatua ile, unajua na yeye ni binadamu, kila binadamu ana mapungufu yake hakuna aliyekamilika ila usiruhusu shetani kuyavuruga mapenzi yenu. Yani mchukulie huyo msichana kama shetani tu”
Erica alijaribu kumuelewesha dada yake hadi alionyesha kuwa yupo kwenye mstari kisha akamtumia ujumbe shemeji yake kuwa arudi tu nyumbani.
Halafu yeye akamuaga dada yake kuwa anaondoka kwani alitaka shemeji yake akifika apate muda wa kutosha wa kuzungumza na dada yake maana alijua kwa vyovyote vile kama mtoto angesumbua basi angekaa na Yule msichana wa kazi ambaye kazoea kumlea mtoto Yule tokea wapo kwao.
Muda huo aliondoka na kwenda kwa dada yake Mage, na alifika na kumkuta kisha akamsalimia na kuanza kuongea nae,
“Sasa dada kwanini mlifikia hatua ya kumfukuza Yule dada aliyepewa mimba na shemeji?”
“Kwanini aachwe? Kwanza msichana ana kiburi sana Yule, anajisema eti mi mke mwenzio, na sisi tukasema hutujui eeh! Dawa ya kiburi ni jeuri Erica, yani tulivyomtimua pale hajaamini macho yake. Sipendagi ujinga kabisa mimi”
“Ila dada, wewe hujawahi kuletewa mtoto wa nje?”
“Sikia Erica nikwambie kitu, kwasasa sijui kama mume wangu kazaa huko nje ila siwezi sema kuwa namuamini na hawezi kuzaa nje, siwezi sema hivyo. Ila ikitokea nikiletewa mtoto wan je nitamlea tu tena kama mwanangu wa kumzaa ila mama yake huyo mtoto akiwa mstaarabu nitaongea nae kistaarabu hata kuwa na urafiki nae ila akijifanya jeuri yani hatokanyaga hata hapa kwangu kuja kumsalimia mwanae.”
“Mmmh dada, haya kuhusu swala la kuja nyumbani na shemeji mmejipangaje?”
“Tumejipanga ujue, yani mwezi huu hauishi tutakuwa nyumbani tayari. Ila mdogo wangu najisikia kukwambia tu, kuwa makini sana na hawa wanaume maana mwingine anaweza kuonyesha anakupenda kweli kumbe nyuma ya pazia wala hakupendi ila anavutiwa nawe tu sababu ya kitu Fulani”
“Hivi inawezekana mtu akavutiwa nawe kwa kitu Fulani na akaonyesha kuwa anakupenda?”
“Inawezekana ndio, utasikia mwingine nakupendea macho yako, jiulize kwamba hivi niking’olewa macho itakuwaje? Yani hutonipenda tena? Nakupendea miguu yako, hivi miguu ikikatika hutonipenda? Kuna vitu tunatakiwa kujiuliza, mwenye mapenzi ya kweli huwa hana sababu ya kukupenda yani yeye huwa anakupenda tu hata uweje”
Kwa maneno haya ya dada yake yalionyesha kuwa mwanaume pekee anayempenda yeye ni Bahati tu sababu ndio anaonekana anampenda bila kujali sababu yoyote, akaongea ongea pale na dada yake ila akapigiwa simu na Bahati akimuomba akamuonyeshe kitu nyumbani kwao.
“Natumaini sio kwa Yule mmama tena, sitaki kuonana na Yule bosi wako”
“Usijali Erica, ni nyumbani kwetu”
Basi Erica akakubali na kumuaga pale dada yake na kuondoka.
 
SEHEMU YA 156


Alifika hadi mitaa ya kwakina Bahati kisha Bahati akaenda kumchukua na kwenda nae nyumbani kwao, akampeleka mahali ambapo kulikuwa na mabwawa ya samaki,
“Erica nimekuja kukuonyesha kuwa, ile milioni moja uliyoniongezea nilikuja kutengeneza mabwawa ya samaki, na sasa samaki wanaendelea vizuri. Mpenzi wangu Erica tutakuwa matajiri sana sisi”
Bahati akamkumbatia Erica, na ilionyesha alikuwa na furaha sana kwani alikuwa akitabasamu tu, muda kidogo simu ya Bahati ikaita akaipokea na kuongea nayo, alipomaliza alimuangalia Erica na kumwambia,
“Kuna rafiki yangu kaja, sasa yupo stendi na hapa nyumbani hapajui inabidi nikamfate stendi. Sasa twende wote au utabaki unaangalia samaki!”
“Mimi nitabaki tu”
“Sawa, ila sitakawia kurudi, jisikie upo nyumbani kabisa maana hapa ni kwenu pia”
“Sawa”
Erica aliendelea kuangalia wale samaki jinsi wanavyoogelea mule kwenye bwawa.
Gafla alifika dada wa Bahati, Yule ambaye alikutanaga na Erica na kumpiga kibao, alikuwa ameongozana na wadada wengine wawili wa Bahati na mama yao.
Yule dada alimsogelea Erica karibu na kumwambia,
“Yani msichana mpumbavu wewe, umeona mdogo wetu kaanza kupata vipesa umeanza kujipendekeza tena”
Kisha akamuangalia mama yao na kumwambia,
“Mama, ndio huyu msichana aliyesababisha mwanao alale jela mwezi mzima tena hata hakujishughulisha kuja kumuona”
“Khaaa kumbe ndio huyu firauni”
Yule mama alimsogelea Erica na kumnasa kibao, wakati Erica akijishika shavu Yule mama akamsukuma Erica kwenye bwawa la samaki.
 
SEHEMU YA 157

Kisha akamuangalia mama yao na kumwambia,
“Mama, ndio huyu msichana aliyesababisha mwanao alale jela mwezi mzima tena hata hakujishughulisha kuja kumuona”
“Khaaa kumbe ndio huyu firauni”
Yule mama alimsogelea Erica na kumnasa kibao, wakati Erica akijishika shavu Yule mama akamsukuma Erica kwenye bwawa la samaki.
Halafu wakawa wanacheka pale juu, Erica akajitahidi kwa kuhangaika sana na kutoka kwenye lile bwawa la samaki kwa upande mwingine, ila wakamfata na kumvutia pembeni kisha kila mmoja alianza kumshambulia kwa makofi yake, mmoja kati ya wale dada wa Bahati akashauri kwamba aachiwe ameshakoma,
“Akome wapi? Malaya anakomaga? Huyu msichana ni malaya, kasababisha mdogo wetu kaka ndani mwezi mzima, halafu kwa umalaya wake nikamkuta na malaya mwingine wanakumbatiana kumbatiana njiani. Huyu msichana hafai ni kichefuchefu”
Mama Bahati, akamsimamisha Erica pale chini kisha akamuangalia na kumwambia,
“Yani wewe binti naomba uelewe swala moja, kama ulifikiri ya kwamba kuna siku utakuja kuolewa na mwanangu yani isahau kabisa hiyo siku labda niwe nimekufa”
Dada yake akadakia,
“Sio wewe tu mama, labda ukoo mzima wa Bahati tuwe tumekufa. Yani huyu mwanamke hajielewi hata robo, umemuona Bahati kaanza kushika hela vizuri, kaanza kuwa tajiri ukaona hapa ndio umalizie shida zako na familia yako. Umenoa kwakweli”
Erica alikuwa kimya kabisa, kajikunyata kama kikuku kilichonyeshewa na mvua, nguo zote zimelowa, na makofi ya kutosha hadi amebaki na alama usoni, hakujua hata afanye nini kwa muda huo. Yule mama Bahati akamwambia,
“Sasa muda huu fanya upesi uondoke hapa kwangu, sitaki kukuona maana tutakufanya mboga bure. Ondoka”
Erica alianza kukimbia tu na alipotoka nje ya uwanja wa nyumba ile aliiona bodaboda ikipita akaisimamisha na kupanda huku akimuomba ampeleke hadi kwao na hela atampa akifika kwao maana hata mkoba wake ulikuwa chapachapa.
Yule wa bodaboda alimuhurumia na aliona kuwa baridi lingempiga sana ikabidi ampe koti lake avae kisha wakaanza kuondoka.
Njiani akapishana na Bahati anarudi kwao, ila Bahati pia alimshangaa Erica akiwa kwenye bodaboda na kujaribu kuisimamisha ile bodaboda lakini Erica alimwambia Yule wa bodaboda asisimame kwahiyo Yule dereva aliendeleza mwendo tu.
Bahati hakuelewa, akarudi kwao na kumkuta dadake nje akamuuliza kuwa imekuwaje hadi Erica kaondoka,
“Kwani wewe umemuona wapi?”
“Nimemuona kwenye bodaboda halafu kama amevaa koti la Yule mwendesha bodaboda!”
Dadake akacheka na kumwambia,
“Ila wewe sijui una akili gani? Sijui unataka tukwambie kwa lugha gani, Yule msichana ni malaya, tena ni malaya koko. Nadhani anajuana na huyo mwendesha bodaboda maana mi nilikuwa hapa nikashangaa anaongea na simu gafla namuona katoka mara kapewa koti na Yule dereva kavaa na kupanda bodaboda akaondoka. Kwanza msichana hana adabu Yule loh! Hata kunisalimia kaona shida”
“Mmmh dada jamani, Erica anaweza kufanya hivyo kweli?”
“Hebu na wewe kuwaga na akili, unamuona kabisa mwanamke anaondoka na mwanaume mwenzio halafu unabaki kutetea ujinga hapa eti hawezi kufanya hivyo, hebu kuwa na akili basi”
Bahati hakuridhika kabisa na majibu ya dada yake, akasogea pale kwenye bwawa lake la samaki, akashangaa kuona maji kwa pembeni, alijiuliza kuwa imekuwaje lakini alikosa jibu, na akapata wazo kuwa mgtu pekee atakayekuwa na jibu ni Erica tu.


 
SEHEMU YA 158

Erica alifika kwao na kumuuliza Yule bodaboda ni shilingi ngapi,
“Hapana dada, mimi nimekusaidia tu”
“Hii ni biashara kaka yangu sio swala la kunisaidia. Naomba nisubiri hapo mara moja, ikuletee hili koti lako”
Erica aliingia ndani kwao, na kwa bahati hakumkuta mama yake kwahiyo alienda kubadilisha nguo kisha akatoka na hela na kumkabidhi Yule bodaboda pamoja na lile koti,
“Kheee zote hizi, hapana”
“Aaah usijali, umenisaidia sana. Nenda nazo tu, maana hata hili koti lako ingebidi nilifue, ila nakuomba utapitisha kwa wale wafua nguo, nakuomba”
Yule bodaboda akawa anakataa ila Erica alimuomba achukue kisha akachukua na kuondoka zake, halafu Erica alirudi ndani kwao amabapo cha kwanza alienda kuoga maana alihisi mwili wake wote unanuka samaki.
Alimaliza na kukaa chumbani kwake akitafakari,
“Hivi kosa langu haswaa ni nini jamani? Mbona kila ninachoshika hakishikiki? Sina raha ya mapenzi kabisa mimi, hakuna ninachofanya kikafanyika, kila kitu kwangu ni majanga.”
Aliwaza sana kuwa yeye ndiye aliyempa pesa Bahati ila leo hii anaonekana yeye ndio anafuata pesa kwa Bahati, roho ilimuuma sana na kujiona kwa hakika hana bahati na mapenzi kabisa.
Akachukua simu zake kwenye mkoba, na kwa bahati hazikuingia maji ila zilikuwa zimezimika, akaziwasha na alikuwa na mawazo sana huku akijisemea kuwa ni vyema angerudi kwao tu kuliko kupitia alikoitwa na Bahati. Alipokaa kidogo simu yake ikaanza kuita, mpigaji alikuwa ni Bahati kwakweli hakupokea kabisa kwani hakujisikia hata kuongea nae kila akifikiria maneno ya ndugu wa Bahati na vile walivyomfanyia hakuwa na hamu kabisa. Mama yake hata aliporudi alimkuta amelala, ila hakulala kwa raha kwani kiukweli alikuwa na mawazo sana.
Kulipokucha alihisi viungo vyote mwilini vinauma, akagundua ni sababu ya ile misukosuko aliyoipata jana yake, basi akampigia simu shemeji yake na kumtaarifu kuwa anajisikia vibaya na hatoweza kufika ofisini, shemeji yake alimkubalia ukizingatia huwa anampenda kwahiyo hawezi kukataa kuwa asipumzike kwenda ofisini halafu yupo mafunzoni tu sio kazi kamili.


 
SEHEMU YA 159


Kwenye mida ya saa nne asubuhi alikuwa akikereka sana na zile simu za Bahati ambazo alikuwa akipiga kila baada ya dakika chache, akajiandaa kisha akaenda mjini, kwa mara ya kwanza alienda kwenye ofisi za laini na kurudisha ile laini yake ya zamani kabisa, alipokuta hakuna mtu mpya anayeitumia alifurahi sana, akairudisha ile laini na kurudi nyumbani kwao kisha kuiweka kwenye simu. Halafu ile laini yake ya siku zote aliikata kata huku akijisemea kuwa atakuwa Erica mpya, hataki tena ujinga wala masikhara, kwani alihisi kuwa hii laini aliyotafutiwa na George ndio iliongeza mkosi kabisa katika maisha yake.
“Ngoja nikumbuke kwanza, laini hii nilitafutiwa na George halafu alinifanyia vituko sana kiasi kwamba nilijiona sina thamani, kwa mawazo nilikutana na mama yake Rahim na kwa mawazo nilikutana na Bahati halafu watu hawa wote wamekuwa ni changamoto kubwa sana katika maisha yangu, ngoja niangalie ukurasa mpya wa maisha yangu kwasasa”
Ile laini ambayo aliwekewa na Rahim, hakuitumia kupiga zaidi ya kwenye mtandao tu, kwahiyo alikuwa akitumia bando tu la ile simu basi.
Baada ya kubadilisha hii laini aliamua kumpigia simu shemeji yake maana akaona ni vyema kumtaarifu sababu anaweza akamtafuta,
“Kumbe Erica, mbona umebadilisha namba?”
“Ndio nilikuwa nakutaarifu tu kuwa nimebadilisha namba”
“Sawa, ila nikitoka ofisini nakuja kukuona”
“Hapana usijali shemeji, naendelea vizuri”
“Lazima nije nikuone Erica, usinikatalie”
Erica hakuwa na jinsi ila alitaka tu muda atakaokuja shemeji yake basi na mama yake awepo ndani.
Kiukweli mwili wake ulikuwa umechoka choka sana, aliamua kwenda kupumzika, wakati amelala na kujisahau kumbe giza lilishaanza kuingia, akasikia tu mtu akigonga mlango wa ndani kwao kwa nguvu, Erica aliinuka na kwenda kumfungulia, akamkuta ni shemeji yake akiwa anathema halafu alionyesha kuwa na hasira sana,
“Vipi shemeji, kuna nini?”
“Naomba maji kwanza”
Erica akaenda kuchukua maji na kumpa, akayanywa kwa haraka sana kwani ilionyesha alikuwa na hasira vilivyo, kisha akamuangalia Erica na kumuuliza,
“Erica, Yule mbwa umempa nini wewe mpaka anakung’ang’ania hivyo?”
“Mbwa gani shemeji?”
“Si kile kibwana chako, aaargh nitakimaliza mimi”
“Sikuelewi shemeji, imekuwaje?”
“Kwanza mama yuko wapi?”
“Mama, katoka kidogo ila sasa hivi anarudi”
“Nimemkuta nje kwenu hapo Yule bwanako muuza samaki, ndio nimetoka kugombana nae”
“Kwanini umegombana nae sasa shemeji?”
“Sitaki akufatilie”
Erica alimuangalia shemeji yake na kushindwa hata kumtafakari maana anamuonea wivu wa nini sasa, muda kidogo mama yao alirudi na kumkuta James pale na kumkaribisha, wakasalimiana kisha James akasema dhamira yake ya kuja kumuona Erica,
“Endelea na moyo huo huo baba angu, ni wachache sana wanaojali ndugu wa upande wa pili. Kwakweli mwanangu kapata mume”
James mwenyewe alishangaa ambavyo mama huyu hakumkumbusha kabisa kuhusu makosa aliyoyafanya ya kumpa mimba msichana wa kazi, baada ya muda kidogo akaaga maana asingeweza kuendelea na zile mada zake zisizoelewekaga mbele ya mama mkwe wake. Kisha akamuuliza Erica kama ataweza kwenda ofisini kesho yake naye alisema kuwa ataenda. Kisha akaaga tena na kuondoka zake.

 
SEHEMU YA 160

Muda huu Erica alikaa na mama yake na kujaribu kuongea nae vitu vichache vichache kama kumdadisi,
“Hivi mama, mfano mwanamke kaolewa ila familia ya mume hawampendi huyo mwanamke inakuwaje hapo?”
“Mmmh mwanangu huo ni mtihani mkubwa sana, japo wengi wanasema akikupenda mume inatosha ila kiukweli usopopendwa na familia kuna karaha yake, raha ya ndoa upendwe na mume na ndugu nao wakupende hapo utajiona kama upo pepo dogo, ila mume anakupenda halafu ukizunguka huku masimango, ukienda huku masimango yani utaiona ndoa chungu kwakweli. Utasema mume akikupenda inatosha je hutashirikiana na wale ndugu zake kwenye jambo lolote? Yani kiukweli ili furaha itimie basin a wao wakupende hata kama sio wote ila wawepo ambao watakupenda”
“Sasa mtu huwa anafanya nini kupendwa na ndugu wa mume?”
“Hiyo huwa inatokea tu, mwingine ana damu ya kupendwa basi wanajikuta wanampenda ila mwingine ni mume ndio anatakiwa afanye ndugu zake wakupende. Kwani mume ana nafasi kubwa ya kufanya ndugu zake wakupende au wakuchukie, yani hatakiwi kusema mabaya yako kwa ndugu zake, yani hata kama una mabaya basi atafute hata mazuri ya kujitungia ili ndugu zake wakupende”
“Mmmmh mama, ila ndoa ni ngumu sana?”
“Vipi mwanangu unataka kuolewa nini? Ndoa si ngumu ila kabla hujaolewa mchunguze huyo muowaji, maana unaweza kuangukia pua uione dunia chungu.”
“Hapana sio nataka kuolewa ila nauliza tu nijue, hivi ndugu wa mume wakikuchukia kuna namna unaweza fanya wakupende kweli?”
“Mwanangu umechukiwa na ndugu wa mume au? Sikuelewi, na kwanini uchukiwe?”
“Nimeuliza tu mama”
“Basi nitakujibu siku nyingine”
Erica alienda chumbani kwake akawa anajiongelesha mwenyewe,
“Erick, dada yake hataki hata kunitazama mara mbili yani hanipendi kabisa. Kuolewa na huyu ni mtihani maana yeye na dada yake ni wanapatana balaa halafu dada yake hanipendi. Rahim nae mama yake nahisi hataki ukaribu wangu na mwanae maana anafatilia kila njia yangu, na siku akisikia nina mahusiano na mwanae atakuwa mbogo kwakweli. Bahati sasa, mwanaume niliyemuamini kuwa hateteleshwi na chochote, nikaanza kumkabidhi moyo wangu maana na yeye ananipenda sana, ila ndugu zake wote hawataki hata kunisikia, mbona sina bahati na mapenzi jamani! Nina mkosi gani mimi Erica?”
Hakujielewa, akafungua simu yake ile nyingine na kuingia kwenye mtandao, akakutana na jumbe toka kwa Rahim,
“Mbona namba yako nimeipiga haipatikani?”
“Nimebadilisha laini”
“Kwanini?”
Erica alifikiria cha kumwambia Rahim, badae akapata wazo,
“Sitaki tena kuwasiliana na watu wa ajabu ajabu ndiomana nimebadilisha laini”
“Kweli Erica? Kwahiyo Yule Bahati hutowasiliana nae tena?”
“Ndio, siwasiliani nae, nimeanza maisha mapya”
“Kama umeamua hivyo Erica nimefurahi sana ten asana”
“Ndio nimeamua hivyo”
“Niambie zawadi gani unataka?”
Erica akatabasamu kwa kuweza kurudisha moyo wa Rahim tena kwake, yani kwa siku hiyo akawasiliana nae vitu vingi sana kwani ilikuwa ni furaha mno sana kurudisha moyo wa Rahim, hadi anamuaga kulala amejawa na furaha kwenye uso wake, yani kwa muda huo hakujali swala la kusema kuwa mama yake Rahim hampendi wala nini.


 
Back
Top Bottom