SEHEMU YA 166
Kufika nyumbani wakamkuta Bahati getini kumbe nae alikuwa akimsubiria Erica baada ya kumkosa hewani kabisa kwa siku kadhaa mfululizo maana Erica alibadilisha laini ya simu, kwahiyo alihisi akifika nyumbani kwao itakuwa rahisi kumuona. James alipomuona Bahati akamwambia mama mkwe wake,
“Eeeh mama, kijana mwenyewe ndio Yule pale anayesumbua akili ya Erica”
“Khaaa si muuza samaki huyu!”
Mama Erica alimfata Bahati kwa hasira sana, na kumkunja kisha James akasogea na kumpiga vibao kadhaa kisha akasema kuwa wasimsikilize chochote kwani huyo ndio mtuhumiwa namba moja, walimpandisha kwenye gari ya James na kwenda nae kituo cha polisi. Kwakweli Bahati alikuwa akishangaa tu, maana hata hakuelewa kuwa imekuwaje kuwaje yeye kushikwa kama mwizi kiasi kile maana hata hakujua kama Erica alipotea.
Walivyofika kituoni, James alishuka na Bahati na kuwaambia wale wamsubirie kwenye gari, James alienda na Bahati kwa mapolisi, na aliimuita polisi mmoja pembeni na kumpa kitu kidogo ili amshikishe adabu Bahati, na Yule polisi pale pale alianza kumshurutisha Bahati.
Kisha James akarudi kwenye gari na kuwaambia wale kuwa Erica atapatikana tu, akaenda kuwarudisha nyumbani, kisha akaondoka.
Mage nae alikaa kidogo tu na kumuaga mama yao, kwani kuna mahali alitakiwa aende,
“Mama naomba uniruhusu tu”
“Sawa, ila hapa sina hata hamu ya kula”
“Ila mama jaribu hata kunywa juisi tu, twende ninavyoondoka uchukue juisi dukani. Badae nitarudi”
Mama Erica alikubali na kwenda na Mage dukani ila kiukweli alikuwa na mawazo sana.
Erica alishtuka kichwa chake kikiwa kizito sana kiasi kwamba hakuna alichoelewa kimetendeka juu yake, akaangaza macho huku na huku akagundua yupo kwenye chumba asichokijua kwani hayakuwa mazingira ya nyumbani kwao, akiwa anashangaa shangaa akamuona Babuu akiingia kwenye kile chumba,
“Ooooh Erica, umezinduka asante Mungu”
Erica alikuwa akishangaa tu na kumuuliza Babuu,
“Kwani imekuwaje? Hapa wapi? Nafanya nini hapa?”
“Erica, hapa ni nyumbani kwangu”
“Nyumbani kwako! Nimekuja kufanya nini hapa?”
“Usiwe na jazba erica, nisikilize kwanza nikwambie”
“Haya niambie”
Aliongea huku akionekana kuchukizwa sana kupelekwa pale,
“Erica, jana nilifika kwenye ile hoteli mliyopanga kwenda na shemeji yako kabla hata ya muda wenu na hadi mnaingia pale nawaona. Sasa shemeji yako alienda kuagiza vinywaji sijui na chakula, nilimuona akiongea na kijana mmoja na kumpa pesa, ilibidi nifatilie ili nijue ni kutu gani. Yule kijana nilimuona akibeba vinywaji ambapo kimoja wapo ilikuwa ni juisi kwenye glasi ila nilimuona akitia kitu kwenye ile juisi, nikafatilia kuona ni nini kinaendelea. Pale mlipokaa vikaletwa vinywaji na chakula, ukaanza kunywa ile juisi ila taratibu ulionekana kuregea hadi kulaza kichwa chako kwenye meza, nikamuona Yule shemeji yako ameinuka. Sikutaka kujua ameenda kufanya nini ila nilichohisi ni kuwa ana lengo baya na wewe, ikabidi nianze kukukokota pale ili nikutoa eneo lile. Tulifika nje nikakodi bajaji tukaanza kuondoka ila shemeji yako akawa anatufata nyuma ikabidi nimwambie Yule dereva bajaji atupitishe njia za panya na tukampoteza mwelekeo Yule shemeji yako. Nilitaka nikupeleke kwenu ila nikakumbuka kuwa mama yako ni mlokole na hatopendezewa kukuona kwenye hali kama ya ulevi, yani Erica ulikuwa kama mtu aliyekuwa pombe saana, ikabidi nikulete hata nyumbani kwangu. Erica hakuna chochote nilichofanya kwako, siwezi kufanya jambo lolote bila ridhaa yako, furaha yangu mimi ni kuona ukizinduka tu”
Erica alijaribu kufikiria na kukumbuka vizuri, akakumbuka pale alipokunywa kinywaji na kuzidiwa na kizunguzungu basi ila mengine hakuyakumbuka ila alitambua kwamba shemeji yake alikuwa na lengo baya kwake,
“Yani Yule shemeji yangu jamani, kweli alitaka kunibaka loh! Asante kwa kuniokoa Babuu, nashukuru sana. Saa ngapi saa hizi?”
“Ni saa sita mchana hii yani hadi nilikuwa na mashaka nikasema usipozinduka nikupeleke hospitali ila nilikuwa nahofia kuwa nitaenda kujielezea nini”
“Mungu wangu, mama atakuwa na wasiwasi balaa, naomba niende nyumbani”
“Hakuna shida, nitakusindikiza ila ngoja unywe kahawa kwanza”
Babuu alimmiminia Erica kahawa na kumpa anywe ili angalau aweke kichwa vizuri,
“Na simu yako iliita sana jana ila nilipoangalia jina niliona Shemeji james, na alikuwa akipiga sana kwahiyo nikaamua kuizima. Samahani kwa hilo kama litakukwaza”
“Hata usijali Babuu, cha msingi umeniokoa toka kwenye mikono ya lile shetani. Yani mtu anatembea na dada yangu, bado haridhiki anataka kunibaka na mimi loh! Sijui wanaume mmeumbwaje!”
“Sio wote bhana Erica, hiyo ni tabia ya mtu hata kuna wanawake wengine wenye tabia hizo”
“Hapana, wanaume nyie sio watu kabisa mna tamaa sana”
“Erica, kumbuka na mimi ni mwanaume pia ila umelala hapa bila kujitambua na sijakufanya chochote. Tumetofautiana wanaume, na hiyo ni tabia ya mtu tu. Huyo shemeji yake itakuwa ndio tabia yake hiyo”
“Sawa ila kwa muda huu nahitaji kumuona mama yangu tu maana najua atakuwa na mawazo sana”
Baada ya hapo Babuu alimsaidia kujiweka sawa Erica kwani bado kichwa chake hakikuwa vizuri. Kisha wakatoka nje na kukodi bajaji ya kuwapeleka nyumbani kwakina Erica.