HADITHI: NAFSI ZILIZO TELEKEZWA
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+
UKURASA WA 49
“Yule sio mtu baki, ni kijana wangu makini kuliko unavyo fikiria wewe. Hizo video ndizo ambazo zimerahisisha zoezi hilo kwenda haraka kabla ya mambo yangu kuharibika kwa huyo kijana ambaye mlikuwa mnamshikilia. Huwa nina namna yangu ya ufanyaji wa mambo yangu hususani kwa watu kama wewe, sijui saa wala dakika ambayo utaamua kunigeuka hivyo hizo video ni ulinzi wako mwenyewe kuhakikisha unanitii na kunisikiliza. Siwezi kuzipeleka popote mpaka siku ambayo utaamua kunisaliti ama kwenda kinyume na vile ambavyo nahitaji iwe Bacia” ilikuwa ni sauti ya kike kutoka upande wa pili. Sauti ambayo ilikuwa inaunguruma kutoka Tanzania.
“Kate umefikia hatua mbaya kunidhalilisha namna hiyo”
“Tuachane na hayo, mmeamua kuchukua hatua gani?”
“Serikali haiwezi kukaa kimya, nimetoa amri watumwe majasusi kupeleleza huko Tanzania”
“Bila shaka wakifika huku wanatakiwa kufa si ndiyo?”
“Ndiyo ila wafe bila kuacha ushahidi wa mwili wala taarifa zozote yaani wasije kupatikana lakini pia wawili miongoni mwao watakuwa ni madouble agent wa Tanzania na Uganda hivyo nina imani hakuna makosa yatafanyika”
“Done” Simu ilikatwa, alikuwa anaongea na Madam Kate ambaye alikuwa nyuma ya huo mpango wa kilicho tokea. Mshauri mkuu wa raisi alikuwa amebanwa kwenye mbavu na mwanamke huyo hakuwa na kauli kwake hivyo alijikuta akiiuza serikali yake kwa mwanamama huyo ili kuendelea kulinda siri zake kwa sababu kama angeenda naye kinyume basi ilikuwa inakula kwake.
Kamanda wa jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es salaam hakuridhishwa na yale maamuzi ya yeye kupokonywa ile kesi kwenye mazingira ambayo hayakueleweka. Hakuridhika na yale maamuzi ila hakuwa na namna ya kuweza kupinga kwa sababu ilikuwa ni amri kutoka juu na halikuwa ombi, alikumbuka asubuhi ya siku hiyo alikutana na afisa upelelezi wa mkoa kuweza kujadili yale ambayo yalitokea husuani mauaji ya kijana wake Julius Mbandu na baadhi ya maafisa upelelezi wengine.
“Bwana Kono najua kabisa kwamba hukufurahi mimi kuichukua hii kesi kwenye mkono wako ila tulipo fikia kwa sasa sidhani kama kuna haja ya sisi kuendelea kulaumiana kwa yaliyo tokea, nadhani jambo la msingi zaidi ni kuweza kukaa chini pamoja na kujua ni kipi ambacho tunatakiwa kukifanya kwani hiki ambacho kinatokea kwa sasa sio jambo la kawaida”
“Kwahiyo umekuja hapa baada ya kijana wako kupoteza maisha ndipo ukaona ninakufaa?”
“Uko sawa kuwaza hivyo na sikulaumu ila kumbuka hii ni nchi na ina utaratibu wake kwenye kesi kama hizi na wewe sio mgeni na huu utaratibu ambao huwa tunaufuata kila linapo tokea tatizo na ulipewa muda kabisa ukashindwa kuutekeleza”
“Nadhani hata wewe ulipewa muda au wewe umefanikisha hilo?”
“Hapana ndiyo maana nipo hapa kuhitaji msaada wako”
“Msaada wangu wakati kesi imesha enda ngazi za juu?”
“Kumbuka nimempoteza kijana wangu tena ameuliwa kwa kudhalilishwa vibaya akiwa karibu kuupata ushahidi, nahitaji kujua kama kuna jambo lolote uliligundua kipindi ambacho ulikuwa unaifuatilia hii kesi, linaweza kunisaidia na nikajua wapi pa kuanzia”
“Sina kitu ambacho nadhani naweza kusema kwamba kitakusaidia, hakuna jambo la maana mpaka sasa zaidi ya mkanganyiko wa udanganyifu wa binti aliye tekwa na watekaji wenyewe”
“Unajaribu kumaanisha nini kusema hivyo?”
“Yule binti kwa mazingira yanavyo onekana sidhani kama ametekwa”
“Kwahiyo?”
“Nadhani alikuwa anajua anacho kifanya”
“Una maana gani kusema hilo?”
“Yule binti kuna namna ndogo tu aliitengeneza sura yake japo hajaibadilisha ila kuna vitu aliongezea usoni vya kuifanya sura yake isitambulike moja kwa moja, yule ni binti ambaye amewahi kuhudumu kwenye ngazi ya jeshi na mafunzo ya ukomando kule Morogoro”
“Bado sijakuelewa, kwamba komando anaweza kutekwa kirahisi tu namna ile?”
“Ndiyo maana nakwambia hajatekwa yule, alikuwa anajua anacho kifanya. Jambo ambalo linaweza kukusaidia ni jina lake, anaitwa Nicola Aidan Semzaba hivyo nadhani msaada wangu unaweza ukawa umeishia hapo”
“Nashukuru sana kwa hilo lakini nina maswali kadhaa bado na kuna kitu nakihitaji kwako” Raymond Kono hakumjibu zaidi ya kubaki anamwangalia mtu huyo ambaye mara ya kwanza aliichukua kesi kwake kwa dharau ila wakati huo alikuwa analilia msaada wake kwa udi na uvumba.
“Aidan Semzaba unamzungumzia mwanasheria wa zamani?”
“Ndo huyo”
“Asante sana kwa hili ila hiki sicho kilicho nileta hapa, jambo ambalo limenileta hapa ni juu ya kifo cha Julius. Mara ya mwisho alienda kumchukua mzee Kazimoto kwa taarifa ambazo nilizipata na baada ya hapo baadae akanipigia simu kwamba ana masaa mawili tu atamleta mtuhumiwa kwangu akiwa mzima kabisa, sikuhoji kujua kwamba mtuhumiwa huyo alikuwa ni nani hasa lakini kwa bahati mbaya ikapatikana maiti yake na sio mtuhumiwa. Kwahiyo nipo hapa ili unisaidie kama utakuwa unajua jambo lolote lile juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea au kuna uhusiano gani kati ya mzee Kazimoto na kifo cha Julius?”
“Hata mimi kesi hii sikufika mbali kiasi kwamba nipate ushahidi wa kutosha ila ni kwamba nahisi Damasi bado yupo hai”
“Hilo haliwezekani, mwili wake uliagwa kabisa na alisimamia mheshimiwa raisi”
“Wewe ndiye unasema haiwezekani, kwamba raisi akiaga kitu ndiyo sababu ya kusema haiwezekani?”
“Lakini tuliuaga hata mwili wake siku ile na baba yake mzazi alithibitisha hilo?”
“Hii ni dunia ya utandawazi, hakuna jambo linashindikana mbele ya sayansi zaidi ya kushindwa kukwepa kifo tu. Kifo ndicho kitu pekee ambacho teknolojia haiwezi kukizuia ila hivi vingine inawezekana kabisa, sitaki kukuaminisha kwa sababu sina uhakika kamili ila naweza kusema Damasi bado yupo hai na huenda hata kifo cha Julius ni yeye amehusika nacho”
“Kama unacho niambia ni kweli, kuna uhusiano gani kati ya Damasi kuwa hai na kumteka huyu mwanamke ambaye umedai kwamba amewahi kupata mafunzo ya kikomando?”
“Hilo ndilo swali ambalo hata mimi sijui napataje majibu yake na nina imani usinge nipokonya hii kesi kwa kebehi huenda ningekuwa nakaribia kupata majibu yake. Nimekusaidia kadri ya uwezo wangu ulipo ishia hivyo naomba uende kwa sasa nahitaji kubaki mwenyewe” kamanda alijitahidi kumpa ushirikiano mwenzake licha ya yye kumfanyanyia ubabe wakati wa kuichukua kesi hiyo. Afisa upelelezi wa mkoa aliondoka akiwa ana maswali mengi kwenye kichwa chake, mwanga mdogo ambao aliupata haikuwa sababu ya yeye kuamini kwamba ndio ulikuwa ukweli kwani hata kesi ilikuwa haipo chini yake tena hivyo kama ni kuliwasilisha jambo hilo kwa wakubwa, alihitaji kuwa na ushahidi wa kutosha mezani ili asikilizwe bila tatizo lakini alikata tamaa kwani bado asingeipata ile nafasi kabisa ni mambo ambayo yalikuwa nje ya uwezo wake tayari.
Kamanda alikuwa anayakumbuka mambo hayo akiwa kwenye gari yake, alikuwa Tambani Mkuruganga wakati huo. Nafsi yake iligoma kabisa kuamini kwamba Damasi alikuwa mfu kwa matukio ambayo yalikuwa yanatokea hivyo kwake aliamini kwamba kuna kitu mzee Kazimoto alikuwa anakijua na anakificha ndiyo sababu usiku huo aliamua kutembelea yalipo makazi ya mzee huyo ili kuanza uchunguzi wake kimya kimya.
UKURASA WA 49 unafika mwisho.