HADITHI: NAFSI ZILIZO TELEKEZWA
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+
UKURASA WA 70
“Sina imani na Aaliyah, ebu mfuatilie kwa ukaribu kila hatua ambayo anaipiga kisha utakuwa unakuja kuripoti kwangu. Fuatilia ujue anajua nini, anakutana na nani, muda mwingi anashinda wapi? Ila hakikisha hajui kwamba unamfuatilia kwa sababu akikukamata sidhani kama atakusame na mimi sitaingilia kwenye hilo, kwahiyo ukikamatwa you are on your own” hakusubiri jibu upande wa pili akaikata simu hiyo.
Saa moja jioni Aaliyah alikuwa anarudi nyumbani kwake ambako alikuwa akiishi. Alikuwa anaishi eneo la Kawe karibu na vilipo viwanja wa Tanganyika Parkers, ilikuwa ni hatua ya dakika kumi tu mpaka kufika eneo hilo ukiwa unatembea kwa mguu. Nyumba yake ilikuwa ya siri, hakuna mtu ambaye aliwahi kumjua mmiliki zaidi ya kuonekana gari ikiingia eneo hilo na kutoka. Jioni hiyo alikuwa na mengi ya kuyawaza kichwani mwake hususani kwa kazi ambayo alikuwa nayo mbele yake, hakujua aanzie wapi na aishie wapi kwani watu ambao walikuwa wanamtuma ndio hao hawakuonekana kuwa waaminifu kwake hata kidogo.
Baada ya kuingiza gari yake ndani, alifungua mlango wa nyumba kubwa lakini nyumba haikuwa sawa, hisia zake ziliufanya moyo wake kwenda kwa haraka hali ambayo ilimfanya atazame vizuri kila sehemu kama kulikuwa na dalili zozote za uwepo wa mtu kwenye hilo eneo lakini hakuona hata hivyo hakutaka kukaa kijinga, aliichomoa bastola yake na kuiweka sawa huku akiwa anaelekea ghorofa ya juu taratibu. Baada ya kuingia ndani alishangaa kuona kuna mtu ndani ambaye alistarehe kama yupo kwake, mkononi mwake alikuwa na gazeti, juu ya meza akiwa anaweka juisi kwenye bilauri anainywa taratibu huku anapitia gazeti lake.
“Nyoosha mikono juu” aliongea kwa jaziba, alihisi ni dharau kwake mtu kuvamia nyumba yake kirahisi namna hiyo.
“Nina muda mchache wa kuongea na wewe hivyo weka hiyo bastola yako chini kwa sababu kuna mahali natakiwa kuwepo” ilisikika sauti nzito kwenye masikio yake mtu huyo akiwa anaachia gazeti ambalo lilimfunika uso wake, uso kwa uso alikuwa anakutana na Edison mwenyewe kwa mara ya kwanza kabisa kwenye maisha yake. Alibaki ameduwaa asiamini mtu huyo alifikaje na kuingia ndani, ni mtu ambaye alitamani kupata nafasi ya kuweza kukutana naye na kufanya naye mazungumzo na hakujua angempatia wapi kwa sababu alikuwa anaishi kwa siri ila wakati huo alikuwa amejileta mwenyewe ndani kwake. Aliangaza kila upande kuangalia kama labda kulikuwa na watu wengine ila aligundua kwamba alikuwa ni mmoja tu pekee.
“Umeingiaje humu ndani?”
“Nimepasua dirisha lako la nyuma nikaingia kirahisi tu. Tuachane na hizi habari za kitoto ambazo hazijanileta hapa, nilitakiwa nikuue wewe hapo lakini kuna mtu alinishauri unaweza kuwa msaada kwangu kwa baadae. Je hilo ni jambo la uhakika?”
“Kwanini umechagua kuishi maisha ya namna hii EDISON?”
“Acha kujifanya una uchungu na maisha yangu bibie, jikite kwenye swali ambalo nimekuuliza”
“Mimi mpaka sasa sijui nipo upande upi, miaka yote nimefanya kazi kwa kujituma lakini nakuja kugundua kwamba hata mkubwa wangu wa kazi ananidanganya! Imeniuma sana”
“Ulikuwa miongoni mwa watu ambao walikuwa wanaisaka roho yangu kwa udi na uvumba, nafikiri ni suala la muda tu kabla hawajaanza kukutengenezea kesi na kukuwinda, utaelewa aina ya maisha ambayo nimeyaishi miaka yote hii na ladha yake inakuwaje”
“Kwa sasa unahitaji kufanya kitu gani?”
“Nataka kuuteketeza hii jamii yao ya siri yote mpaka wote wafe”
“Hilo ni jambo gumu kwa sababu hujui nani yupo upande wako na nani hayupo nawe”
“Hata wewe haupo upande wangu?”
“Unahisi kirahisi tu naweza kumuamini mtu ambaye taifa zima lilikuwa linamtafuta kama gaidi kwa kuhusika na mauaji ya wenzake tisa? Unataka nimuamini mtu ambaye ameigiza kifo chake na sasa watanzania wanaenda kujua kwamba umekufa? Unataka nimuamini mtu ambaye amemtoa sadaka mwanasheria ili yeye aishi? Nitakuwa binadamu wa ajabu sana”
“Sikuja hapa kukubembeleza, nimekuja hapa kwa sababu ni maelekezo ambayo nilipewa na Jack ila nadhani mimi na wewe hatuwezi kuwa sehemu moja hivyo kuanzia sasa nakuhesabia kama adui yangu na nakuahidi huenda wakati ujao tutakutana sehemu ambayo itanilazimu kukuua” Edison alinyanyuka baada ya kuongea maneno hayo na kutaka kuondoka lakini alisikia sauti ya bastola ikikokiwa kwa mara nyingine tena, hakuogopa bali alimsogelea Aaliyah pale kwenye sofa na kumuinamia.
“Nina uhakia umelisoma faili langu vyema ila bado haujawahi kuniona kwa macho yako hadharani, mimi sio binadamu wa kuanza kujibizana na binti wa kike kama wewe na usije ukathubutu kuninyooshea hii bastola tena kwenye maisha yako yote kwa sababu nitakuua” Aaliyah hakukubaliana na huo ukweli wa kutishiwa nyau wakati alikuwa na mikono yote miwili, alimvuta Edison ghafla na kumtia kichwa cha uso akihitaji kumwekea bastola kichwani ila kitu alifanywa hata yeye alibaki anajutia.
Mkono wake ulidakwa na kuteguliwa kwenye bega, alipigwa ngumi ya taya akiwa ameshikiliwa mkono ulioteguka. Kibao kilipita kwenye shavu lake akahisi amebugia kitu kwenye mdomo wake. Wakati huo alikuwa amesimama, kupigwa kwake kulifanya ayumbe yumbe hali ambayo ilifanya apigwe na mguu wa kwenye goti akataka kudondokea mbele, alikutanishwa na kisigino cha uso ambacho kilimzoa mpaka kwenye kabati ambalo lilikuwa pembeni, kabati lilivunjika. Edison alisogea pale kwenye kabati akiwa anamwangalia mwanamke huyo mtata.
“Huwa sipendi kupiga piga wanawake ndiyo maana nimekupiga kwa kukudekeza ila hili ni onyo la mwisho. Huapo kwenye listi ya watu ambao nawahitaji labda kama nitalikuta jina lako huko mbele au kama utaingia katikati ya njia yangu kwa kigezo cha kudai kwamba unatimiza kazi yako hivyo hili liwe mwanzo na mwisho mimi sijali lolote kuhusu sheria binti” alimatamkia kwa msisitizo, aliisogelea bastola akatoa risasi zote na kuipasua. Edison akawa anatoka taratibu kwenda mlangoni lakini aliisikia sauti ya majuto ikimuita
“Stop please!” Aaliyah aliongea akiwa anajinyanyua kwa maumivu.
“Naweza kufanya kazi na wewe” alijibu akiwa anaunyoosha mkono wake mpaka ulipo kaa sawa.
“Kipi kimeyabadili mawazo yako?”
“Kwa sababu watu ambao niliwaamini wameivunja imani yangu”
“Unataka kulisaliti shirika lako?”
“Yeah kama ambavyo jeshi na serikali vilikusaliti wewe”
“Kwahiyo kwa sasa ndo umejua kwamba nilisalitiwa?”
“Ndiyo, sitaki kurudia makosa kama hayo”
“Kwahiyo unataka kufanya nini?”
“Nitaifanya hii kazi ya kuudondosha umoja huu pamoja na wewe, nitazitafuta taarifa za ndani kwa bosi na nikizipata tu basi nitakupatia kila kitu cha ndani ili tuiteketeze kuanzia ndani”
“Kazi yako kubwa kwa sasa ni kuhakikisha unajifanya upo nao bega kwa bega kwa sababu nahitaji ufuatilie nyendo za bosi wako kila mahali, ujue anafanya nini, anakutana na nani na kwa sababu zipi”
“Hilo naweza kulifanya lakini vipi kuhusu maisha ya mwanasheria?” Edison aliiangalia saa yake ya mkononi
“Atakuwa ameshakufa saivi”
“Unawajua walio mteka?”
“Ni hawa hawa ambao nawatafuta kwa sababu walijua alishakuwa hatari kwao, sikutaka hili litokee lakini aliniwekea dawa ya usingizi hivyo akanitoroka, wakati nashtuka nilikuwa nimechelewa”
“Kwahiyo unataka kuniambia kwamba hata raisi anaweza kuwa mhusika ndiyo maana amempoteza mtu huyu makusudi kwa kigezo cha kutekwa?”
“Usiwaamini viongozi wako kupitiliza. Fanya nilicho kuagiza”
“Nikiwa na taarifa za kukupa nakupata wapi?”
“Nitakutafuta mwenyewe”
“Kwahiyo na wewe haujui ni wapi alipo Irina Espanovich?” Edison alimwangalia Aaliyah kwa umakini bila kumpatia jibu, mwanamke huyo alikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mama yake mzazi hivyo kuliweka wazi jambo hilo ingekuwa hatari kubwa hususani kwa mama yake kwani hakutaka mwanamke huyo aingie matatizoni kabla hajakutana naye na kufanya mazungumzo. Alitamani awe mtu wa kwanza kabisa kumpata kwa sababu alikuwa na mengi ya kumuuliza mwanamama huyo ambaye hakuwahi kuonyesha kujali kuhusu uwepo wake huku yeye ndiye akiwa kinara wa kutafutwa kwake nchini.
UKURASA WA 70 unafika mwisho.