SEHEMU YA 74
Roma Alikuja kusimamisha gari Makongo juu, Edna alishangazwa na Roma kumleta hayo maeneo , lakini hakujali sana , alitaka kuona mwisho wake.
Baada ya Roma kusimamisha gari ,alishuka na Edna pia hivyohivyo , jua siku ya leo halikuwa kali sana na kulikuwa na dalili ya mvua.
“Wife tutatembea kidogo mpaka hapo mbele , kuna mgahawa mzuri tu”
“Sasa kwanini usingesimamishia gari hapo?”
“Edna hivi lini ushawahi kuchukua mazoezi hata ya kutembea?”Aliuliza Roma na Edna hakuweza kujibu hilo swali , kwani ni kweli katika maisha yake hakuwa ni mwenye kuchukua mazoezi , hata ya kutembea , alikuwa ni mwenye kutembea na usafri kila mahali na hata kazini hakuwa akipanda ngazi , alikuwa akitumia Lift.
“Unatakiwa kuchukua mazoezi kwa ajili yaAfya yako na huu ni mwanzo , tutatembea mpaka kwenye mgahawa na kurudi kwa mguu pia”Aliongea Roma na Edna alishindwa aongee nini , kwani hata kama angegoma alikuwa akimjua Roma na isitoshe alikuwa na ufunguo.
Mtaa huu haukua na watu wengi sana kama maeneo ya Tegeta, lakini watu waliokuwepo ndani ya huu mtaa hawakuaacha kumkodolea Roma na pisi yake kali.
Dakika chache mbele kama kumi na tano hivi waliweza kufika ndani ya mgahawa mmoja maarufu kwa kuuza nyama za kuchoma unaofahamika kwa jina la ARIFU, haikueleweka Roma alipafahamu vipi hapo mpaka kujua huo mgahawa na Edna alitamani kumuuliza Roma lakini alishindwa.
Waliingia ndani ya mgahawa huu , huku wateja wa mgahawa huu wakiwaangalia , hii sehemu ilikuwa na makelele mengi na kumfanya Edna asiipende , lakini kwa Roma yeye aliona kawaida tu , kwani kwanza alikuwa amezoea kula sehemu kama hizi na pia alifanya makusudi kumleta Edna ndani ya eneo hili la mgahawa.
Mbele kabisa ya mgahawa huu kulikuwa na mdoli mkubwa mweupe uliowekwa mbele ya mlango na kufanya eneo hili kupendeza Zaidi , ilionesha mmiliki wa hapa ndani alikuwa mwanamke.
Roma leo alishangazwa sana na Zogo ambalo lipo ndani ya hii sehemu kwa siku ya leo , huku kwa mbele wakionekkana wazungu na baadhi ya wabongo wakiwa wamezunguka meza.
“Roma..!”Ilikuwa ni sauti ya kike ambayo ilimfanya Roma kugeuka na baada ya kukutanisha macho na mwanamke mtu mzima hivi mweupe shombeshombe alievalia Aproni alitabasamu.
“”Mama Aisha nimekuja kukutembelea na mke wangu leo”Aliongea Roma na kumfanya mwanamama huyu mtu mzima kushangaa na kumwangalia Edna , ni kama hakuwa akiamini kama Roma ana mke kama huyo.
“Jamanii! Umepataje mke mzuri kama huyu Roma?”Aliuliza Mama huyu huku akimshika Edna mikono na kumfanya Edna atabasamu na kujisikia vizuri ,kwake hii ni mara ya kwanza kwa Roma kumtambulisha kama mke na ndio kilichomfanya kujisikia vizuri.
Roma na Mama Aisha mmiliki wa Mgahawa huu , walionekana kufahamiana sana , jambo ambalo lilimfanya hata Edna kutaka kujua ukaribu wao ukoje.
“Mama Aisha pale ni nini kinaendelea?”Aliuliza Roma baada ya kuona kuna zogo sana , kwa watu waliozingira meza na mama Aisha akatabasamu.
“Kuna mchezo wa kushindana kula nyama unaendelea pale, nimejaribu kutoa shindano leo kama kuvutia wateja”Aliongea Mama Aisha na kumfanya Roma na Edna watabasamu kwa pamoja.
“Mshindi anapatiwa zawadi gani?”
“Unataka ukajiunge nini?.Mshindi ni chakula bure kwa wiki nzima”Alijibu na Roma alitoa macho.
“Mama Aisha na mimi nataka kushindana kwenye hilo shindano , lakini nikishinda sitaki chakula maana itakuwa ngumu mimi kuja mpaka huku , unaonaje huo mdori hapo , nikishinda inakuwa zaiwadi ya mke wangu”Aliongea Roma na kumfanya Edna ashangae na Mama Aisha alitabasamu.
“Kwakua leo ni siku ulionitambulisha kwa mkeo, basi nakubaliana na ombi lako, isitoshe mdoli wangu ni mzuri na unaendana na mkeo”aliongea Mama Nasra na kumfanya Roma atabasamu na kisha akamwangalia Edna na kumkonyeza , lakini Edna aliishia kushangaa na matendo ya Roma.
Roma alimshika mkono Edna na kwenda mpaka upande ambao kuna meza na mama Aisha alimtambulisha kama mshiriki wa shindano kwa siku hio na akajitokeza mtu kwa nia ya kutaka kushindana na Roma na Roma alimwangalia mshindani wake na kutabasamu , lakini pia hata kwa mwenzake alimwangalia Roma na kisha akamdharau na kuona huyu lazima amshinde.
“Nikishinda pambano , sitaki nyama za bure wala chakula , bali nitachukua ule mdoli kama zawadi kwa mke wangu”
Aliongea Roma kwa sauti na kufanya kundi la watu wamwangalie Edna na kisha wakashangilia kwa kupiga makofi na kumfanya Edna atabasamu kwa Aibu , ila kwa Roma hakuwa kabisa na aibu Zaidi ya kumkonyeza Edna.
Sahani tano za vipande vya nyama ya ng`ombe ya kuchoma vilipangwa na dakika za kumaliza sahani zote zilikuwa ni kumi na tano , zilikuwa ni dakika chache sana ambazo Mama Aisha alikuwa ameweka kama moja ya sheria za Pambano ,Roma alimuona mwanamama huyu kufanya jambo hilo makusudi ili watu wasishinde , ila alijiambia leo lazima ashinde kwa namna yoyote ile ili kumpa zawadi mke wake.
Baada ya maandalizi ya pambano kuanza,Mtoto wa mama Nasra alitoa sauti kuashiria pambano kuanza na hapo hapo Roma na Mshindani wake Shombeshombe walianza kula kwa haraka sana ,Roma alikuwa akila taratibu kitendo kilichofanya washabiki kushangaa na staili ya kula , ni kama Roma alikuwa akimpa nafasi ya ushindi bwana Shombeshombe.
Edna licha ya kwamba mwanzoni aikuwa hakubaliani na shindano hilo ,kwani aliaona kama jambo la aibu , lakini sasa Roma ashaingia kwenye mchezo na alitaka awe siriasi , alitaka kumpiga kibao ale , haraka mwenzake anamshinda.
“Roma kula bhna ,,, atakushinda”Aliongea Edna baada ya kukosa uvumilivu na Roma alimwangalia na kisha akatabasamu na kumkonyeza.
Na muda huu watu walikuwa wakimshangilia Shombeshombe kwa kumaliza sahani ya kwanza , na walimuona Roma kama hatoweza kumfikia kwa namna yoyote ile , Roma aliona shabiki yake alikuwa ni mke wake pekee.
Roma baada ya kuona mpinzani wake kafikisha sahani ya kwanza na ya pili kufikia nusu , alianza kuchukua nyama mbilimbili na kutumbukia mdomoni , yaani Roma alikuwa akitafuna mara moja ilikuwa imepita , spidi ambayo alikuwa akitumia haikuwa ya kawaida na jambo hili likamuacha Edna na watu wa hapo ndani kwa mshangao na ndani ya dakika moja na nusu Roma alikuwa ashamaliza Sahani ya kwanza na sasa alikuwa akienda ya pili.
Shombeshombe alimwangalia Roma kwa namna anavyokula haraka na kujikuta akitumbua macho na kusahau kama yupo kwenye pambano , alishangazwa na ulaji huo wa Roma na kujiuliza huyu ni mnyamaa au ni binadamu , ile anakuja kushituka ,Roma alikuwa akimalizia sahani ya tatu.
Mashabiki wote walihama kwa Shombeshombe na kuja upande wa Roma huku Edna akiwa ni mwenye kushangaa m kwa mambo ambayo Roma alikuwa akiyafanya.
Ndani ya dakika saba tu Roma alimalizia nyama ya mwisho na kisha akamwangalia mke wake na kumkonyeza , Mama Nasra aliekuwa pembeni yake alijikuta akishangazwa na uwezo huo wa Roma , alikuwa ni kama mtu aliekuwa mbele yake hajawahi kukutana nae .
Watu walishangilia huku wakimwangalia Roma kwa macho ya kiulizo na kujiuliza ni mtu gani huyu anaweza kula nyama kwa kuitafuna mara moja na kumeza.
“Mama Aisha siku nyingine unapaswa kuweka zenye mifupa”Aliongea Roma aliekuwa akimalizia kutafuta nyama ya mwisho , huku shombeshombe na wengine wakiendelea kumwangalia Roma.
“Hahaha… umenishangaza sana leo”
Aliongea Mama Aisha kuku akielekea mlangoni kutoa mdoli uliokuwa kwenye mlango,mwanamama huyu alionekana kujutia kuweka Mdoli wake rehani , lakini alikuwa ashaweka ahadi , alichukua ule mdoli na kisha akampatia Roma ambaye alikuwa akitabasamu na kisha baada ya Roma kupewa mdoli wake alimkabidhi Edna.
“Wife Zawadi yangu kwako kama mumeo”Aliongea Roma na kumfanya Edna kushindwa kuzuia tabasamu , ni kweli zawadi hio ilikuwa ya thamani Zaidi kwa Edna.
Na hata Roma mwenyewe siku nyingi alikuwa akiwaza ni zawadi gani ambayo napaswa kumpatia Edna , lakini alishindwa kung`amua , kwani mke wake alikuwa na kila kitu , kama ni maua alikuwa nayo yamejaa na yote yamenunuliwa na pesa , sasa yeye baada ya kuona pambano hilo na Mdoli mlangoni aliona hio ndio nafasi nzuri kwa kumpatia Edna zawadi.
Mama Aisha aliwapa chakula cha bure kizuri na baaada ya wawili hao kula kumaliza walitoka ndani ya mgahawa hupo wa ARIFU kutembea kueleka walipokuwa wameacha gari.
Edna alionekana kama mtoto kwa namna ambavyo alikuwa amebeba mdoli wale wa Rangi nyeupe na masikio ya pink.
“Umefahamiana vipi na yule mama?”Alivunja ukimhya Edna mara baada ya wawili hawa kuingia kwenye gari na kuanza safari ya kurudi .
“Nilikutana nae Mikumi nikiwa njiani kuja Dar, alikuwa ameharibikiwa na gari yake njiani nikamsaidia kuitengeneza na akanipatia lift kama malipo”.
“Wewe huko Mikuni ulikuwa upo kwenye gari au ulikuwa unatembea?”
“Nilikuwa natembea , sikuwa hata na hela”Aliongea Roma na kumfanya Edna kushangaa.
“Na wewe ulikuwa ukitokea wapi?”
“Nilikuwa nikitoka Mwanza wife”Edna alishangaa Zaidi.
“Kwa hio unamaanisha ulitembea kutoka Mwanza Mpaka Mikumi”
“Hehe..Wife unashangaa nini , hujawahi kusikia watu wanatembea kutoka Kigoma huko mpaka Dar”Aliongea Roma na kumfanya Edna aone ni kweli , lakini bado alibakia na maswali.
*****
Ilikuwa ni siku nyingine kabisa ya asubuhi , Abu alionekana akiingia kazini kama kawaida , lakini siku hii akionekana kuwahi tofauti na siku zingine.
Baada ya kuegesha gari yake , moja kwa moja aliingia kwenye Lift ya jengo hili kwenda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi yake.
“Boss..!!”Aliita Isack aliekuwa na wasiwasi na kumfanya Abuu aliekuwa akitembea kwenda kwenye ofisi yake asimame na kumwangalia.
“Kuna nini?”
“Kuna Jambo ambalo halipo sawa”
“Kivipi?”
“Nimejaribu kufatilia muwekezaji ambaye Chairman jana alisaini nae makataba ndani ya kampuni yetu”
“Sasa nini hakipo sawa?”
“Muwekezaji anatoka kampuni ya Athena Trading Company”Aliongea Isack na kumfanya Abu atoe macho huku akichukua kishikwambi mbacho Isack ameshikilia mkononi , na baada ya Abu kuangalia kwa umakini alijikuta akitetemeka mikono.
“Ni macho yangu , au hii ni sahihi Isack?”
“Ni Sahihi kama unavyoona ,mpaka sasa Athena ana asilimia hamsini za hisa ndani ya kampuni na ni rahisi kusema ndio mmiliki wa JR group mpaka sasa”Aliongea Isack na Abu alishindwa kuongea chochote , alionekana kuchanganyikiwa na alichokifanya ni kughairisha safari ya kuingia kwenye ofisi yake na kurudi alikotoka.
Ndani ya madakika kadhaa hivi Abubakari Hamadi CEO alionekana akiingia Masaki nyumbani kwa baba yake , huku akionekana mwenye haraka kweli.
Ndani ya sehemu ya kuegesha magari kwa muda Gari ya RollRoyce ilionekana hapo ndani , lakini kwa Abu alishindwa hata kuona.
Nyumba ilionekana kutulia mno na hili halikumpa Abuu shida , alienda moja kwa moja mpaka ilipo ofisi ya baba yake Mlezi na ile anafungua tu mlango , alimuona Mzee Alex akiwa hayupo peke yake , bali alikuwepo Matrida mtu ambaye hawakua wakipatana kabisa ,Matrida alimgeukia Abu na kutabasamu , huku Mzee Alex akimwangalia Abu na kusikitika na kisha akaendelea na kile alichokuwa akifanya , Mzee huyu alikuwa akisaini karatasi ambayo hakuwa akijua inahusiana na nini.