SHETANI RUIDISHA NAFSI ZETU.
MTUNZI:SINGANOJR
SEHEMU YA 118.
The ancient tomb(Kaburi la kale).
Watu wale mara baada ya kuambiwa wamshambulie Hamza na Yonesi , haraka sana walitoa visu vyao na kushika mkononi wakiwa tayari kwa mashambulizi.
Wa kwanza mara baada ya kusogea, Hamza alipiga hatua mbele na kisha kwa ustadi wa hali ya juu alishika mkono wake uliokuwa umeshikilia kisu na kuupindisha na kumfanya yule mtu kujichinja mwenyewe shingoni baada ya mkono wake kuvunjjika.
Huyo alikuwa wa kwanza , wengine mara baada ya kuona mwenzao alivyoshambuliwa haraka haraka walianza kumrushia Hamza visu vidogo kama mishale lakini Hamza alikuwa mwepesi mno , kwani aliweza kumsogeza Yonesi pembeni na wakati huo akikwepa visu vile na ilikuwa ni kufumba na kufumbua alishawasogelea na kuwagusa shingoni na ukawa mwisho wao.
Kwa namna ambavyo alikuwa akipata urahisi wa kudili nao aliweza kugundua watu hao hawakuwa na mafunzo ya hali ya juu , kama ni kundi la kihalifu basi litakuwa daraja C na kazi yao kubwa ni ujambazi.
Yule kiongozi mara baada ya kuona uwezo wa Hamza haraka haraka alichomoa bastora yake kutoka kiunoni na kumnyooshea.
“Ukisogea hatua moja tu nakulipua”Aliongea kwa kuamrisha akiamini katika siraha yake, lakini hata hivyo siraha ile haikumfanya Hamza kuwa na wasiwasi.
“Nyie ni wakina nani na mnachimba nini? Ongea kila kitu,pengine ninaweza kukuacha hai”Aliongea Hamza na yule bwana alianza kshikwa na hofu mara baada ya kuona Hamza hakuwa na wasiwasi kabisa licha ya kumuonyeshea bunduki.
“Tunatokea kundi la
Lemur…. kwanza sipaswi kujibu swali lako kama unavyotaka”Aliongea bwana yule kwa lugha ya kingereza akitaka kusema kila kitu lakini mara baada ya kufikiria katika miiko ya taalauma yake aliona anapaswa kufanya siri juu ya misheni yake.
Hamza alifikiria kwa umakini na kujaribu kuwaza kama ashawahi kusikikia kundu linalojiita kwa jina la mnyama Komba wa bukini(Lemur) ndani ya Afrika , lakini kadri alivyofikiria hakuweza kusikia ikimaanisha kwamba kundi hilo ni dogo mno.
Kwa namna alivyosikia maongezi yao , watu hao walionekana kupewa kibarua kuja kufanya kazi ndani ya eneo hilo , lakini kwa namna moja ama nyingine aliona kwanini alichagua kundi la majambazi ndio waje kumfanyia kazi au na yeye ni mdogo.
“Niambie mlichokuwa mkichimba la sivyo utakufa hapa hapa”Aliongea Hamza akiwa siriasi.
Yule bwana kutokana na usiriasi aliokuwa nao Hamza alijikuta akishikwa na hofu kubwa na kufanya mikono yake kumtetemeka na palepale aliachia risasi kumlenga lakini katika hali ya ajabu iliishia katika mikono ya Hamza.
Na mara baada ya kuishika mkononi alimsogelea yule bwana na kisha kumpatia risasi yake mkononi na kitendo kile kilimpa hofu kubwa mno lakini Hamza hakumchelewesha kwani kitendo cha kupokea ile risasi ilikuwa ni kama mtego wa kumzubaisha kwani palepale alimshika kichwa na kukizungusha na ikawa mwisho wake.
Kitendo kile kilishuhudiwa na wale waliokuwa wakichimba shimo ndani na kutoka chini na walijikuta wakianza kutetemeka kwa woga.
“Tunaomba utusamehe , usutuue tulikuwa tukichimba kwa ajili ya kutafuta Hazina”Waliongea wanaume wale waliokuwa wamechafuka kwa kumwagikiwa na mchanga kwenye nguo zao na kichwani.
“Niambieni kila kitu mnachojua , niko kwenye mudi nzuri hivyo sitomuua mtu”Aliongea Hamza na watu wale mara baada ya kuona bosi wao amekwisha kufa haraka haraka walianza kumwambia Hamza.
Kwa maelezo yao wanasema mwezi mmoja uliopita alitokea mtu nchini Botswana alievalia mavazi ya chuma kama roboti kwanzia miguuni mpaka usoni na kuwataka wazamie nchini Tanzania na kuja kuchimba katika eneo hilo la kilele cha mlima joto na kutafuta kaburi la kale(
Ancient Tomb).
Wanasema ilikuwa ndio misheni yao ya kwanza ya kustaajabisha na hata wao wenyewe hawakuamini kama kweli kulikuwa na kaburi la kale ndani ya eneo hilo na aliwashawishi kwa kuwaambia kutokana na eneo hilo kupata joto nyakati za usiku ni kwasababu chini yake kuna Hazina kubwa iliofichwa miaka mingi sana kabla hata sehemu hio kuishi watu.
Kutokana na mtu huyo alivyokuwa akijiamini na ushawishi wake walijikuta wakiamini na kukubali misheni hio kisha kuanza safari ya kuja nchini Tanzania kwa ajili ya kuwinda Hazina hio ambayo imefichwa ndani ya kaburi la kale.
Lakini moja ya masharti ambayo wamepewa na mwajiri huyo ni kwamba isitokee wakagundulika wanachimba eneo hilo mpaka wamalize kabisa kupata hio hazina , hivyo ndio maana waliua baadhi ya wafanyakazi waliowakuta ndani ya hilo eneo na wakati wafanyakazi wa Dosam wakisogelea hilo eneo walitengeneza maporomoko feki lengo lilikuwa ni kuficha kile walichokuwa wakifanya.
Lakini licha ya wasiwasi wao wakati wa kuanza kazi hatimae waliona kiashiria na kuona ni kweli kile walichoambiwa ni uhalisia lakini kwa bahati mbaya ndio muda ambao Hamza alijitokeza.
Hamza aliingiwa na walakini juu ya jambo hilo , ilikuwa ni mara yake ya kwanza kusikia watu wakisafiri kutoka taifa la mbali kwa ajili tu ya kuja mahali kuchimba kabuli la kale, lakini hata hivyo hakujali sana ili mradi ilikuwa kweli.
“Huyo aliewaajili kuja kuchimba mwonekano wake ukoje?”Aliuliza.
“Kama tulivyosema alikuwa amevalia suti ya chuma na usoni amevaa Mask, lakini kingereza chake na lafudhi anaonekana kama sio mzawa wa lugha hio”Aliongea.
“Ni mwanaume au mwanamke?”Aliuliza
“Anaonekana kuwa mwanaume , mrefu kama mita moja na nukta nane hivi , pia ana mwili mkubwa kama bonge”
“Kuna kitu kingine cha kuniambia?”
“Hakuna , hivyo ndio pekee tunavyojua , Mkuu tunaomba utuache hai , tumekuja tu hapa kama wasaidizi”Wachimba kaburi hao walianza kusujudu wakitaka Hamza awaache hai.
Hamza aliishia kushika vichwa vyao kulia na kushoto .
“Sitaki kujiongezea idadi ya watu nilioua , lakini nani kawaambia muue watu wasio na hatia”Aliongea Hamza na kwa mikono yake yenye nguvu aligonganisha vichwa vyao na kama matikiti vilitengeneza ufa na wakapoteza maisha palepale.
Kitendo kile kilimfanya Yonesi uso wake kufubaa kwa namna Hamza alivyowaua kikatili lakini vilevile kitendo cha Hamza kuidaka risasi.
“Hivi ni kweli ile risasi uliidaka?”Aliuliza akiwa bado haamini.
“Ah.. kwangu risasi ni kama chuma kinachoruka ruka kwa spidi kuliko vyuma vingine, ni siraha ambayo inatumiaka kwa binadamu wa kawaida na kwa mvuna nishati za mbingu na ardhi aliefikia levo ya nafsi inaweza isiwe na uwezo wa kumdhuru , kuhusu mimi kutumia bunduki kunishambulia ni kupoteza muda”Aliongea Hamza.
“Unavyoongea unaonyesha ni rahisi sana, nilishituka wakati alivyokushambulia”
“Nini cha kushituka sasa , wewe ulipaswa kuchukulia kama mdudu anaepaa”Aliongea huku akicheka.
“Unaonekana kama mtu ambae hujaua mtu”Aliongea huku akiangalia maiti zilizozagaa.
Kwa uzoefu wake kama mwanajeshi , kitendo cha Hamza kuuwa kirahisi namna hio ilimaanisha alikuwa ameua sana kiasi kwamba roho na moyo wake umekufa ganzi.
Ukweli ni kwamba alimuona Hamza kama mwanaume ambae ni ngumu kumwelewa , muda mwingine anakuwa muhuni , muda mwingine mwenye kuchekesha na muda mwingine mkatili wa kiwango cha juu sana.
“Yonesi nawezekana kuonekana mkatili kidogo lakini najua kumjali sana mpenzi wangu”Aliongea.
“Mimi sio mpenzi wako”Aliongea Yonesi akiangalia chini akiona aibu za kike.
Hamza wala hakutaka kubishana nae maana baadhi ya vitu vilipaswa pia kueleweka vizuri kwenye moyo wake, Mwanzoni alikuwa na wazo juu ya Yonesi lakini dakika hio ilionekana ni mwanamke huyo ndio amekufa na kuoza juu yake ila tu hasemi na kwasababu hio aliona amuingize kwenye orodha.
“Sidhani kama kuna mtu atakuja hapa usiku huu, unaonaje tukipiga simu na kuwapa taarifa tupo salama?”Aliongea Hamza na Yonesi alikuwa tayari ameshikilia simu muda mrefu.
“Hakuna mtandao hapa”Aliongea na kumfanya na Hamza kutoa simu yake kuangalia na kweli hapakuwa na mtandao kabisa japo eneo hilo mwanzoni lilikuwa na mtandao kutokana na kilele cha pembeni yao kulikuwa na minara ya mawasiliano.
“Nadhani watakuwa wameua mkondo wa mawasiliano kwa hili eneo,ndio maana hakuna mtu alietupigia”Aliongea Hamza.
“Kwahio tunafanyaje, au tunashuka kwanza?”Aliongea Yonesi na kumfanya Hamza kufikiria kidogo na palepale alisogelea lile shimo na kuangalia chini , chini yake lilionekana jiwe kubwa mno(tombstone)kama lichuma ambalo limechongwa, kwa uchakavu wake ilikuwa ngumu hata kutabiria lilikuwa na miaka mingapi ndani ya eneo hilo.
“Haina haja ya kuhatakisha kwenda chini , nina shauku kweli ya kujua kilichopo chini ya ardhi”Aliongea
“Usiniambie unapanga kuingia ndani ya hilo shimo? Tunapaswa kuripoti kwanza”Aliongea Hamza.
“Kama tukiondoka kwenda kuripoti , unajuaje kama hakuna mtu mwingine ambae atawahi na kuja kuingia na kuchukua hio hazina wanayozungumzia? Isitoshe naangalia tu, nini kipo ndani yake”Aliongea Hamza
“Una visingizio sana , kwanini unakuwa na shauku hivyo , kama ni mtego utajuaje?”Aliongea Yonesi akiwa na wasiwasi.
Hamza alishikwa na hali ya kusita palepale , kama angekuwa peke yake asingeweza kuogopa lakini asingemwingiza Yonesi, vipi kama ikitokea tatizo na kushindwa kumlinda.
“Upo sahihi kuna giza kubwa sana , sidhani kama ni vizuri kuingia ndani ya hili shimo”Aliongera Hamza huku akicheka.
“Unacheka nini?”Aliuliza Yonesi lakini hakujibiwa kwani Hamza alimsogelea na kwa kasi alimshika kiuno na mwanamke huyo mara baada ya kuhisi kudondoka alijikuta akipelekea mikono yake na kumshika Hamza shingoni.
“Wewe unafanya nini?”
“Tunarudi chini ya mlima tukakutane na wenzetu”Aliongea Hamza na palepale hakumpa muda Yonesi kufikiria kwani kitendo cha kupiga hatua moja tu alikuwa umbali mrefu mno chni ya korongo na ilikuwa ni kama wanadondoka na kumfanya Yonesi kuanza kupiga makelele ya woga.
“Arhhhh.. Hamza acha ukichaa wako”
Ijapokuwa mlima huo haukuwa mrefu sana, lakini ulikuwa na mita za kutosha ambazo kwa mtu atakaedondoka kwenda chini hakuna uwezekano wa kupona , lakini Hamza yeye alikruka bila ya kujiuliza mara mbili mbili.
Kitendo cha kupunguza wasiwasi alijikuta akigundua hawakuwa wakidondoka , bali ni kama kuna kitu kimewashikilia na kuwafanya washuke kama vile wanaogelea angani.
Kitendo cha namna alivyokumbatiwa na namna anga lilivyokuwa alikwisha kusahau palepale kama alikuwa angani na moyo wake uliojaa mapenzi ulianza kudunda kwa kasi.
Hamza aliishia kutoa tabasamu hafifu wakati akimwangalia mrembo huyo.
Aliruka kwa zaidi ya hatua nne kwa kutua chini na hatimae mpaka kufika chini kabisa ya mlima ndani ya dakika mbili tu na kumshusha Yonesi katika geti la kuingilia kwenye mlima huo.
Baada ya kumshusha chini alimwambia aweke nywele zake vizuri na nguo maana alikuwa amechafuka mno.
“Yonesi nadhani kutokea hapa unaweza kwenda sasa , waambie wenzetu nipo salama na kuna mnyama naaenda kumuwinda kwa ajili ya kitoweo”Hamza mara baada ya kuongea hivyo , palepale aliondoka na kuanza kukimbilia msituni akimuacha Yonesi amechanganyikiwa.
Alisimama pale kwa dakika kama moja hivi na baada ya kushituka alijikuta akipatwa na hasira na muda huo ndio alijua Hamza kamleta hapo na kumuacha ili akaangalie lile kaburi mwenyew.
Aliishia kusugua meno yake kwa hasira na kama kilele cha mlima hakikuwa mbali angerudi mara moja , lakini ni mbali hivyo alishia kugeuka na kuangalia taa za hoteli upande wa nyuma yake na kuanza kupiga hatua za haraka kurudi.
Hamza kwa namna alivyokuwa akikimbia alikuwa kama Chui , kwani ndani ya dakika chache tu hatimae aliweza kurudi katika eneo lile kwa mara ya pili.
Alianza kuangalia kwa kukagua kama kuna mabadiliko na hakuona chochote na palepale alijirusha na kutumbukia ndani ya lile shimo mpaka juu ya jiwe kubwa na kuanza kulichunguza.
Alipangusa kutoa mchanga wake na palepale aliona maandishi ambayo yalimfanya kutoa macho.
“Haya maandishi”Hamza macho yalimtoka kwani maandishi yale yalikuwa yakifanana na lugha iliokuwa katika kitabu alichopewa na Dokta Genesha na kumfanya kushikwa na bumbuwazi la aina yake.
Ile shauku ya kutaka kunyanyua jiwe hilo ili kujua kilichopo ndani yake ilimvaa.
Kwa ufupi ni kwamba jiwe hilo lilionekana kama mfuniko na pembeni yake kulikuwa kumejengwa kwa zenge na kuonekana kama vile ni boksi,lilikuwa ni kaburi halisia ambayo yalitumika enzi za kale.
Sasa swali la kushangaza ni kwamba nani alipanda katika eneo hilo na kuweka kaburi hio, maana kwa makadirio yake na historia nzima ya Tanzania na wenyeji wake pengine enzi ya kale hapakuwahi kuwepo na watu katika eneo hilo.
“Au kuna binadamu ambae ashawahi kuja kujificha huku?”Aliwaza Hamza na kuona inawezekana, isitoshe licha ya historia kuelezea mengi haikumaanisha kila kitu kilielezewa ndio maana watu = bado wanatafuta mabaki ya vitu.
Lakini jambo moja la uhakika aliamini kaburi hilo kwa namna yoyote ile waliolitengeneza hawakuwa watu wa kawaida , mpaka kutumia lugha hio ambayo ni mpaka wakati huo hakuna anaeweza kuitafsiri maana yake kuna uwezekano pia wasiwe watu wa dunia au ni binadamu ambao tamaduni zao zilipotea katika historia.
Hamza palepale alisogeza mchanga pembeni , kwa bahati nzuri ni kwamba watu wale walikuwa wamefanya kazi kubwa mno ya kuchimba hivyo kutengeneza uwazi wa kutosha kuondoa ufuniko.
Hamza mara baada ya kusukuma kwenda pembeni jiwe lile , uzito wake ulimshangaza mno, kwa makadirio yake ya haraka haraka aliamini litakuwa na uzito wa tani nne au tano hivi.
Kama sio kwa nguvu zake ambazo hazikuwa za kawaida , asingeweza kusogeza kabisa.
Kitendo cha kuusukuma ule mfuniko kama wa chemba palepale maporomoko ya mchanga na mawe yalisikika yakidonsoka kuelekea chini.
Hamza licha ya kuona ufuniko huo kama jiwe , lakini bado ilimuwia vigumu kuamini hilo ni jiwe kutokana na uzito wake , ilionekana ni aina ya zege lakini ambalo malighafi zake hazikueleweka.
Kutokana na uzito huo ilikuwa ni kama vile mtengenezaji alijua siku moja kuna mtu ambae atajaribu kutaka kuiba ndio maana akatengeneza uzito mwingi ili iwe ngumu.
Baada ya kutengeneza upenyo alitoa simu yake na kumulika chini na hatimae aliweza kuona kuna ngazi za kuelekea chini , haikuwa chemba kama alivyodhania bali ni kama pango, alijikuta akitabasamu tu kwa uchungu uliojaa fanaka.
Ukweli ni kwamba kama asingewahi kuona
purgatory , basi uwepo wa kaburi hilo kama pango ungemshangaza na kuona jambo ambalo haliwezekani , lakini duinia ilikuwa na magereza ya ardhi , mapangao na makaburi mengi ambayo baadhi yao hayajagundulika kabisa kutokana na kufukiwa na vifusi juu.
Hamza hakuwa na hofu kabisa , hakujua kilichopo chini ya giza hilo ni nini lakini kwa kutumia mwanga wa simu alipiga hatua kuingia ndani,lakini sasa kitendo cha kukanyaga ngazi kushuka chini taa ziliwaka kutokea ukutani.
Hamza alidhani ni umeme , lakini haukuwa umeme , kitendo cha kufungua mlango kwa juu na kuruhusu hewa ya oksijeni kuingia , iliwasha karabai zilizowekwa humo ndani na tukio hilo lilimfanya kuamini mtengenezaji alikuwa mjuzi wa hali ya juu , maana kikawaida kama ni kuwaka ilibidi atumie kiberiti au chanzo chochote cha moto.
Hamza alijikuta akiongeza umakini kwani aliamini kadri eneo hilo kuwa na utaalamu wa hali ya juu ilimaanisha hatari ni kubwa vilevile.
Hamza mara baada ya kutembea kwa mita kama therathini hivi katika njia iliokuwa na tambarare alijikuta akiona michoro mbalimbali iliokuwa kwenye kuta , moja ya mchoro uliomshitua ulikuwa ni wa kusanyiko la watu ambao walikuwa wakimwangalia mwanamke aliekuwa ameangikwa kwenye kitu kama msalaba huku ukiwa na ishara ya kuungua na moto.
Mchoro ule ulimshangaza sana Hamza na kufanya azidi kuumulika na tochi kuuangalia vizuri lakini ulikuwa ni vilevile , watu hao walionekana walikuwa wakionyesha ishara ya chuki kwa yule mwanamke na ilimfanya kuhisi kabisa mwanamke huyo ni kama yule mchawi ambae amemuota kwenye ndoto , ijapokuwa katika hio picha hakuonekana kwa sura lakini mchoro uliashiria kila kitu.
Hamza alipita mchoro ule na kuangalia michoro mingine na wa pili yake aliona picha ya kijana mdogo akipuliza baragumu na nyingine akichezesha vidole kwenye Kinubi.
Kulikuwa na picha nyingi sana na iliomfanya kusimama licha ya kutaka kupotezea ni ya mwanamke na mwanaume waliokuwa wameshikana mikono ikionyesha walikuwa na uhusiano wa karibu , mwanamke alionekana kuwa mzuri na mwanaume alionekana kuwa mtanashati.
“Hizi picha zinamaanisha nini , sidhani kama ni historia ya mtu katika dunia yetu”Aliwaza Hamza huku akiangalia ukale uliokuwa kwenye pango hilo.
Eneo lilikuwa na joto mno lakini kutokana na mwili wake ulivyo aliweza kuhimili joto lake, kuta zake za juu pia zilitengenezwa kwa aina ya ajabu mno , hakujua ni aina gani ya malighafi ambazo zilitumika kuimarisha kuta zake na kufanya zisishikwe kabisa na ukungu wala buibui , kulikuwa na uchafu kidogo sana na harufu ya ukale pekee lakini mazingira hayakuwa kama ya pango, yalikuwa ni kama ya
bunker
Maswali mengi pia yalipita katika kichwa chake na kujiuliza eneo kama hili huyo aliewaajiri kundi la Lemur kalifahamu vipi , kwa alichoona hakuwa akitaka kundi hilo kuingia hapo ndani ila alikuwa akiwatumia kuchimba tu na kwa maana hio alijua ndani kuna ukubwa kabisa wa pango kama hivyo , sasa swali kama eneo hili lilikuwa likionekana la kale namna hio maana yake ni kwamba hakuna binadamu alie hai wa kale ambae anaweza kujua uwepo wake , labda kama iwe ni kwenye vitabu na hata kama ni vitabu ingekuwa ngumu kujua uelekeo sahihi.
“Au ni kwasababu ya hali joto iliokuwa juu ya kilele ndio ilikuwa ishara kubwa?”Alijiuliza Hamza.
Ukweli ni kwamba kichwa chake kilijaa maswali mfululizo na aliona namna pekee ya kuyajibu ni kuendelea kufuatisha njia kwenda ndani zaidi akajionee kilichopo.
Baada ya kutembea kwa mita kama tano hivi kwenda mbele hatimae aliweza kukutana na mlango ambao pia haukueleweka ni chuma ama ni wa zenge , ulikuwa tu ni mlango mweusi kama rami uliokuwa na hali ya kuchakaa.
Hamza mara baada ya kuuchunguza mlango huo na kuangalia kama kuna mtego hakuweza kuona pia hakukuwa sehemu ya kuweza kuufungua .
Hamza alijaribu kwanza kuusukuma lakini ulionekana kufungwa , alipangusa eneo la juu na mkono wake na aliweza kuona mchoro wa pembe nane.
Hamza alishangazwa na mchoro ule, kwani kwa uelewa wake pembe nane siku zote iliwakilisha chanzo cha nishati juu ya uhalisia wa asili ya ulimwengu , yaani hasi na nyanya.
Tofauti na kusukuma mlango , Hamza yeye alisukuma lile eneo lenye pembe nne kwa nguvu na kitendo kile kilimfanya asikie kishindo kikubwa na mlango ule hatimae ulionyesha ishara ya kuachia loki zake.
Ukweli ni kwamba Hamza hakujua hio ndio namna ya kuufungua , alishawahi kusoma sehemu na kuelewa siku zote ukiona mlango umefungwa kwa fumbo la pembe nane basi njia rahisi ya kuufungua maana yake ni kwamba umeamsha mtego wake.
Yaani kwa lugha nyepesi ni kwamba mlango utafunguka kwa njia ambayo ni rahisi lakini haimaanishi kwamba mlango umefunguka ili uingie , maana yake ni kwamba mlango umewasha mitego yake..
Kitu kimoja ambacho kilimpa akili ya kufanya kwa wakat huo kutokana na eneo hilo kutumika akili nyingi katika utengenezaji wake ni msingi wa utengenezaji wake , kwa haraka haraka kutokana na uchunguzi wake na uelewa aligundua eneo hilo lilitengenezwa katika msingi wa uhalisia wa ulimwengu(Nature of reality).
Hivyo Hamza alitaka kwanza kutegua mtego uliowekewa kwenye mlango huo kwa kutumia kanuni za uhalisia wa asili.
Hivyo alichokifanya ni kuzungusha ile pembe nane ambayo aliisukuma kwenda ndani na kisha kaizungusha kulia na kushoto katika masharti maalumu , mara nyingi kutokana na uelewa wake kanuni yake ni kufuatisha mzunguko wa jua.
Kwa maana kwamba mzunguko wa kwanza ni kwenda uelekeo wa jua linakochomoza na kisha kurudi katikati ya mstari na kisha kwenda tena upande wa magharibi.
Sasa kanuni hii maana yake kabla ya kuzungusha lazima ujue ueleo wako na mashariki na magharibi ulivyo ndio uanze kuzungusha.
Hamza alitumia simu kujua uelekeo wake na kisha palepale alizungusha kwenda kuhoto mpaka kwenye mstari na kisha akarudi kwenye mstari na kupeleka kulia na kutoka kulia akarudi kwenye mstari , hivyo hivyo akarudia mara nane na mara ya mwisho tu mlango ulifunguka wenyewe na kuacha eneo lote wazi.
Kwa jinsi mlango huo ulivyokuwa ukijifungua ni kama Hamza anafungua ulimwengu wa kale.
SEHEMU YA 119.
Hisia ambazo alizipata alijua ni kwanini watu wengi walikuwa wanapenda kuchunguza mabaki ya kale.
Mbele ya macho yake kulianza giza zito mno lakini mra baada ya hewa kuingia ghafla tu taa moja moja kwa mtindo wa kufurahisha macho ziliwaka.
Mwonekano wake ulibadilika kutoka kuwa wa matarajio na kuwa wa kuchanganyikiwa na taratibu alianza kushangaa.
Halikuwa kaburi bali ni kama chumba kikubwa sana chini ya ardhi kwa ukubwa wa kiwanja cha basketball, sehemu yote ilikuwa imezingirwa na kuta za mawe makubwa juu na chini huku
angle zake zilikuwa ni za kustaajabisha.
Katikati ya eneo hilo kulikuwa na jiwe kubwa la kuchongwa ambalo lilikuwa kama meza na juu yake kulikuwa na mchoro wa ramani ambao licha ya kuonyesha ni mchoro wa ramani ya dunia lakini ulikuwa na utofauti kabisa na ramani ya kawaida ya dunia , ilionyesha ni ramani ambayo ilichorwa enzi za kale kwa kutenganisha mabara pekee na sio nchi.
Hamza alishawahi shuhudia mahandaki mengi ndani ya dunia lakini ndani ya kaburi hilo kulikuwa na upekee wa aina yake , usanifu wake na mpangilio ulikuwa sio wa akili ya kawaida , hakika ilimshangaza sana, kingine kilichomshangaza ni kwamba eneo hilo lilikuwa la wazi bila ya kuwa na vitu vingi.
Hamza taratibu alitembea kusogea katikati akitaka kupanda eneo ambalo ni kama anapandisha jukwaani sehemu ambayo ilikuwa ni m kama madhabahu flani hivi ili kujua kilichopo juu yake ni nini, kulikuwa na ukimya wa aina yake na kitu pekee kilichoweza kusikika ni kucheza kwa zile taa na kuungua kwake.
Mara baada ya kufika juu kabisa iliokuwa ni kama kijukwaa , Hamza aliinua kichwa chake na kuangalia juu , kulikuwa na vitu kama vishikwambi vya mbao vilivyopangiliwa kwa mtindo wa kuvutia macho na kila kishikwambi kilikuwa na herufi ambazo Hamza aliamini pengine ni majina , lakini kutokana na lugha iliotumika alishindwa kujua ni majina gani, kuna kila hisia zilizomwambia pengine hayo ni majina ya wafu.
Muda uleule aliona kitabu kilichokuwa mwishoni kabisa kwenye kona iliochongoka na alisogea na kushika kile kitabu na kukifungua ndani , kitabu kile hakikuwa cha kawaida kama vitabu vya makatarasi bali vilikuwa kama vipande vyembamba vya mbao vilivyounganishwa pamoja.
Hamza mara baada ya kuangalia kilichoandikwa hakuweza kusoma kabisa kutokana na lugha yake kuwa ileile ambayo hakuweza kuitafsiri, lakini kwa namna mwandiko ulivyoonekana ilikuwa ni kama ni kitabu cha ukoo kwani baadhi ya majina ambayo yalikuwa mwishoni yalikuwa pia katika vile vibao vilivyokuwa vimepangiliwa.
Sasa wakati akiendelea kushangazwa na kitabu hicho ghafla tu alisikia mtikisiko nyuma yake na kumfanya kugeuka kwa kasi na palepale eneo la mlango wa kutokea kwenye eneo hilo kulikuwa na ‘watu’, hapana haikuwa watu bali ni masanamu yaliokuwa na muonekano wa kufanana na mtu ilikuwa ngumu kusema pia ilikuwa masanamu , vinyago au midoli lakini muonekano wao wa kimavazi ni kama vile ni wale wanajeshi wa Kikorea,
Joseon soldiers, waliovalia mavazi ya chuma maarufu kama
Armor au askari wa ki’
terracotta huku mkononi midoli ile ikiwa imeshikishwa mapanga , hayakuwa mapanga feki bali mapanga halisi tena ya kung’aa sana kwa ukali wake.
Hamza hakujua masanamu yale kwanini yamejitokeza ghafla na kuziba njia kwa mbele kama walinzi lakini hakutaka kujali sana maana alitaka kuendelea kutalii ndani ya kaburi hilo , isitoshe hakuwa bado amepata kitu cha maana , kutokana na kwamba licha ya ujenzi wa eneo hilo kushangaza lakini kitu pekee alichoweza kuona ni majina yalioandikwa katika lugha isioeleweka , hakukuwa na kitu kingine zaidi ya uwazi tu.
Sasa wakati anataka kuyasogelea yale masanamu ya kiaskari ili apite upande wa pili kutoka eneo hilo, palepale alijikuta mwili wake ukimsisimka baada ya kuhisi hatari .
“S*t !!”
Hamza alijikuta akiruka kurudi nyuma mara baada ya lile sanamu kuzungusha mkono wake kwa juu na lile panga kutengeneza mjongeo wa kumfyeka.
Jambo lile lilimshangaza mno Hamza , kwani hakuamini yale masanamu mapanga walioshikishwa zilikuwa ni siraha za kufanyia maangamizi na sio mapambo kama alivyowaza, kama sio uwezo wake wa kukwepa angekuwa ashakatwa shingo muda mrefu.
Kwenye maisha yake hakuwahi kuona sanamu ambalo linaweza kuua kama maroboti yenye umeme , maana hata muonekano wao haukuonyesha kabisa kama walikuwa maroboti maana hakukuwa na chanzo cha nishati kutoka kwao zaidi ya kuonekana kama midoli ya kale.
“Nyie ni binadamu au maroboti?”Hamza aliuliza huku akiyaangalia yale masanamu yote mawili ambayo yameanza kuchezesha yale mapanga yao katika muundo wa kustaajabisha ambao ilikuwa ngumu mno kuruka na kupita upande wa pili.
Muda ule Hamza aliweza kusikia mvumo wa vitu kama mashine na minyororo baada ya kutaka kujua mashine hizo ni nini palepale sanamu moja lilisogea upande wake kwa spidi kutaka kumshambulia.
Swala lile lilimshangaza Hamza sana , ijapokuwa alikuwa akisikia mvumo wa mashine kuzunguka kama vile ni treni ya umeme lakini spidi yao ilikuwa kubwa mno.
“Fyuuu fyuuu…!!”
Sanamu zile za chuma staili zao za kurusha panga zao zilikuwa za muunganiko wa ajabu mno na zenye wepesi mkubwa.
Hamza mara baada ya kuona anashambuliwa palepale aliishia kukwepa panga zile kulia na kushoto kwa ustadi wa juu sana.
Hamza hakuwahi kuona mbinu hizo za mashambulizi hapo kabla , lakini haraka haraka alijua lazima hayo yatakuwa mapigano ya kisanaa ya zama za kale na mtu huyo yoyote alietengeneza hilo eneo aliweka mbinu hizo katika hayo masanamu.
Kilichomsaidia muda huo ilikuwa ni wepesi wake wa kukwepa na nguvu la sivyo angekuwa ashapata majeraha kama sio kufa kabisa .
“Arghhhh!!”
Hamza alijikuta akitoa mguno mara baada ya kujaribu kukwepa shambulizi la sanamu lile la kulia na kujikuta akiingia katika mtego wa sanamu la kushoto na kupitishiwa upanga kwenye bega na kama sio kupinda kidogo ingekuwa shingoni.
Ulikuwa utaalamu wa hali ya juu sana na kitu ambacho aligundua kwa haraka ni kwamba masanamu hayo yalikuwa yakilenga sehemu muhimu katika mwili wa binadamu.
Yalikuwa na wepesi wa kushambulia kama binadamu ambae ana mafunzo ya hali ya juu ya kimapigano.
Japo muda huo alikuwa na wasiwasi , lakini alijikuta akishikwa na matamanio makuba yaliojaa mshangao wa uwezekano wa kitu kama hicho , hususani katika mbinu hio ya mapigano iliokuwa ikitumika , kwenye maisha yake alikuwa amekutana na wataalamu wengi wa mapigano , lakini hakuwahi kukutana na mbinu hio.
Hamza alitamani kupita hivyo alitulia kwanza na kuangalia mfumo wao wa kushambulia ulivyo na palepale aligundua sio tu kwamba yalikuwa yakishambulia lakini moja likishambulia lingine lilikuwa likizuia mashambulizi katika muunganiko sahihi kwa asilimia mia moja na kutotengeneza kosa lolote.
Hamza palepale alijiambia hawezi kushindwa akili na masanamu ambayo yanatumia kanuni za mjongeo zilizowekwa ndani yao , hivyo kwa moyo wote aliingia kwenye pambano rasmi, kwanza kabisa alianza kujifunza mbinu yao na kukariri wakati huo huo akitafuta namna ya kushambnlia na yeye tofauti na kukwepa.
Baada ya dakika tano jasho lilikuwa likimtiririka , sio kwasababu alikuwa amechoka lakini ni kutokana na kushindwa kupita kwa kila alivyokuwa akijaribu.
Alijiambia ni afadhali masanamu hayo ulikuwa ni mfumo wa utaalamu wa kimakenikia tu lakini kama ungekuwa uwezo halisia wa binadamu , basi dunia ingetikisika.
Lakini hakuacha kujiuliza ni mtu gani ambae ana uwezo wa kutengeneza kitu ambacho kinazidi hata kanuni za kimakenikia, alijiambia kama ameweza kutengeneza masanamu tu ambayo uwezo wake ni mkubwa hivyo vipi kuhusu yeye mwenyewe si atakuwa juu mara mia yake, kuwaza tu hivyo maini yalicheza kwa hofu.
Hamza alijiambia ngoja ajaribu mara ya mwisho , akiona ameshindwa hana jinsi zaidi ya kutafuta namna ya kukimbia tofauti na kushyambulia
Lakini sasa ni kama yale masanamu yalikuwa yakichochewa kwani spidi yao iliongezeka maradufu , ilikuwa ni kama shughuli yao imeanza rasmi na mfumo wao ulikuwa ukizidi kuwa mwepesi zaidi na zaidi.
Dakika ambayo Hamza aliona amepata upenyo wa kukimbia alizuiwa palepale na kurudishwa nyuma kwenye pambano.
Ilifikia hatua alijikuta akishika kiuno akiwa hajui hata alie ama acheke maana kazidiwa ujanja na masanamu..
“Ma’bro … nimewafanya nini mpaka mnanichukia vyote hivi ..sijawaibia chochote nilikuwa nikiangalia tu”Aliongea Hamza akiwa ameshika kiuno.
Ijapokuwa ameongea hivyo , lakini alijua masanamu hayo hayakujua alichokuwa akiongea.
Clang!!”
Siraha ya lile sanamu ilipanda juu kwenye hewa na kutengenezza upepo uliomfanya Hamza kuruka sarakasi ya kurudi nyuma na wakati anafanya kitendo hicho alijikuta akipata kujua kitu kilichomshangaza .
Mawazo mengi palepale yalipita katika akili yake kama mwanga wa kimondo.
Alichogundua ni kwamba masanamu hayo hayakuwa yakishambulia kutokana na kuwa na akili au kumuona , haikujalisha umetumika utaalamu mkubwa kiwango gani yatabakia kuwa maroboti pekee, kilichomfanya kugundua hilo ni kwamba kitendo chake cha kupanda juu hewani yaliacha kushambulia ikimaanisha kwamba yalikuwa yakishambuilia kwa kufuata uzito wake ulipo chini ya sakafu.
Yaani kwa lugha nyepesi kile ambacho Hamza aligundua ni kwamba eneo hilo ambalo amekanyaga ni kama uzito wake ndio ulitengeneza ufahamu kwa hayo maroboti na kitendo cha kuruka juu yaliacha kushambulia.
Ijapokuwa ilikuwa ni jambo ambalo ni la kufikirika lakini kweli , aina hio ya teknolojia ni kitu ambacho katika dunia ya sasa ni ngumu kufikiria., sasa alijiuliza kama masanamu haya yametengenezwa na watu wa kale alijiuliza walikuwa na akili kiasi gani.
Hamza palepale aliona kwanza athibishe kile ambacho amegundua na kuruka juu kadri awezavyo na ilikuwa ni kweli kitendo cha kuruka juu yale masanamu ni kama yamezubaa ghafla kama vile yameishiwa umeme.
“Hehe.. muda wangu wa kulipiza kisasi sasa”Aliwaza Hamza huku akichekelea gunduzi yake na kutaka kuyaadhibu ipasavyo kwa kumkata kwenye bega lake.
Palepale kwa nguvu zake zote aliruka hewani na kwenda kulilenga na teke moja ya lile sanamu , nguvu ya teke lake hata kama ni gari yenye chuma kigumu ingebonyea.
Lakini sasa kitendo cha Hamza kugonganisha mguu wake na lile sanamu palepale upanga ulifyatuliwa na kumkata Hamza kwenye paja na kumfanya aruke umbali mrefu bila ya kupenda huku akigulia maumivu
Shambulizi hilo lilikuwa kali mno kwake kama vile alikuwa na uadui wa muda mrefu na hayo masanamu.
Lakini hata hivyo hakutaka kukata tamaa , kwani palepale aliruka juu kwa mara nyingine na kuchukulia faida kuzubaa kwao na kisha kulipiga teke sanamu lingine , teke lake lilikuwa na uzito wa tani kadhaa.
Bang!!
Kishindo kizito kiliweza kusikika na kujaza sauti ndani ya handaki hilo lote na kutokana na kutumia nguvu nyingi alijihisi ni kama zimemwishia kabisa.
Hamza licha ya kutumia mbinu ya kuruka juu na kuyapiga aligundua hakukuwa na mabadiliko makubwa kwani yalikuwa na nguvu sio ya kawaida , yalikuwa yakitingishika na kurudi katika mkao wake na kuendelea kushambulia.
Hamza pumzi ilianza kuwa nzito , tokea afike Tanzania hakuwahi kutumia nguvu zake zote katika kupambana., lakini mbele ya masanamu hayo alikuwa ametumia kiwango kikubwa cha uwezo wake kudili nayo tu.
Alijikuta akijihisi ni kama anapatwa na ukichaa kwani hakuwahi kukutana na adui mwiba kama hayo masanamu , lakini hata hivyo alikuwa na uzoefu mkubwa sana wa kimapambano na alijua siku zote adui yako hata kama ana nguvu kiasi gani lazima awe na udhaifu lakini tatizo ni kwamba kadri adui yako alivyo na nguvu maana yake udhaifu wake ni mdogo sana au ni ngumu kuutambua lakini haikumaanisha kwa wakati mmoja kama hakuwezekana.
Hamza aliamua kutulia kwanza na kuangalia sanaa yao ya mashambulizi ili kuona kama kuna kitu ambacho hajakiangalia tokea mwanzo , lakini ilikuwa ngumu kuona kutokana na kwamba hakuwa ametulia , alikuwa akiendelea kukwepa mashambulizi yao ili asiumie zaidi.
Licha ya kwamba alikuwa na uwezo wa kukwepa risasi , lakini mbele ya masanamu hayo alishindwa kukwepa mashambulizi yao yote , kitendo cha kupambana nayo kwa zaidi ya nusu saa ilimfanya kuwa na majeraha mengi mwilini na kumfanya nguo yake kuloa damu. Na aliishia kung;ata meno akijitahidi kuvumilia hayo maumivu.
Hakuwahi kupitia maumivu makali kwa muda mrefu kama hivyo na yote hayo ni kutokana na kukutana na mbinu ya kimapigano ambayo ilikuwa mpya kwake , mbinu ambayo imewekwa katika masanamu hayo , lakini alijua hata kama wanashambulia kwa kanuni kama maroboti lazma kutakuwa na maana iliojificha katika mbinu yao hio ambayo bado hakuwa akiijua.
Pambano hilo lilimkausha nguvu zake kwa kiasi kikubwa mno , kama ingekuwa mapigano ya kawaida alikuwa na uwezo wa kuhimili hata siku saba anapigana na asingechoka , lakini mbele ya hayo maroboti nusu saa tu alikuwa amechoka chakali.
“Wakuu hamjachoka tu”Hamza alijikuta akiuongea bila ya kujali maroboti hayo hayakuwa yakimsikia hata kidogo.
Ukweli ni kwamba hakuwahi kupigika kiasi hicho , yeye aliyashambulia kwa mateke lakini hayakujua hata maana ya maumivu ni nini kutokana na kuwa machuma tu lakini yeye mashambulizi alioyapata yalikuwa yakiuma mno.
Hamza kadri alivyokuwa akiruka juu na kutua chini kwa nguvu ni kama alikuwa akiyachochoa na kusogea kwa kushambulia kwa kasi mno na aliishia kuviringika kulia na kushoto akikwepa mashambulizi y ake.
Kwa ustadi ambayo alikuwa akionyesha pamoja na mashambulizi ambayo yalikuwa yanafanywa na hayo masanamu kama kuna mtu ambae anaangalia angefurahia kweli na kujifunza mengi , hata Hamza mwenyewe alitamani kuwa yeye ndio angekuwa anaangalia.
“Swiiii…!, Swii!!”
Ilikuwa ni milio ya mapanga yakikata hewa ilioweza kusikia na kumfanya aanze kujikatia tamaa kutokana na nguvu zake kuzidi kumwishia na palepale swali lilimjia katika akili yake kama yeye anachoka kushambuliwa kwanin hayo maroboti hayaishiwi nguvu.
Alifikiria katika msingi wa kanuni ya
conservative of energy na kujiambia kwamba hata kama masanamu hayo hayakuwa hai lazima kuwe na chazo cha nguvu yao na sio tu kutegemea uzito wake.
Sasa palepale alijiuliza kama ni hivyo chanzo cha nguvu zao kipo wapi , isitoshe hayakuwa yakila wala kunywa , hayakuwa hata na betri lakini bado yalikuwa yakimkimbiza na kushambulia.
Alijiambia lazima kuwe na chazo la sivyo yasingekuwa na uwezo wa kusogea na kushambulia.
Alijikuta akikubaliana na wazo hilo katika moyo wake lakini hakuwa na muda wa kutosha , aliona anapaswa kutafuta chanzo hicho kabla ya nguvu zake kumwuishia kabisa.
Alikumbuka alikuwa ameyashambulia kwenye shingo , moyo mpaka kihcwani lakini hakukuwa na kitu cha tofauti , lakini kulingana na utengenezaji wake aliamini pengine kuna mlango wa nyuma , aliona hakuna namna ya kuzuia mashambulizi yake bila kujua chanzo cha nishati zake.
Palepale alijiuliza swali kama masanamu hayo yametengenezwa na mtalamu wa mapigano je kwa mpiganaji ni kitu gani kinawakilisha chazo cha nishati?.
Hamza mara baada ya kufikiria hivyo palepale swali hjilo liliweza kujibika katika kichwa chake.
Mafunzo ya kimapigano yalikuwa yakifuata elimu ileile ya
Kinesiology kwamba chanzo cha nguvu za binadamu iwe kiroho au kimwili ni katika kitovu eneo la tumboni, ukienda katika tamaduni za wachina kwa wale wanaojifunz mafunzo kama ya Tai chi na Qigong pia wanatambua Dantian kama kituo cha kati cha uwiano wa nishati ya mwili kwa kutenganisha kiwiliwili cha juu na chini.
Licha ya kugundua hilo alikuwa ameyashambulia kwa kulenga kifuani na kichwani lakini hakuyaletea shida licha ya kuwa vituo muhimu pia vya nguvu za mwili , sehemu pekee ambayo hakugusa ni chni ya kitomvu.
Lakini licha ya ugunduzi huo aliona itakuwa ngumu sana kufikia eneo hilo kimashambulizi kutokana na staili yao ya kurusha panga lakini licha ya hivyo aliamua kushambulia kwa uwezo wake wote.
Mara baada ya kuona masanamu hayo bado yalikuwa yakimshambulia , alichokifanya ni kuruka juu akichukulia faida kuzubaa kwao kutokana na kukosa uzito wake na kisha alienda kushambulia eneo la chini kwa kulenga usawa wa tumbo.
Clang!!
Kitendo cha kupiga eneo lile aliweza kusikia vyuma vikilia , ilikuwa ni sauti ya kwanza kusikia tokea aanze kushambnuliana na masanamu hayo, vilikuwa ni kama kuna vitu vilivyokuwa vikisuguana.
Palepale aligundua hapo ndipo udhaifu wao ulipo maana pailionekana hapakuwa pagumu kama kwingine kwenye miili yao.
Mara baada ya kupata shabaha ya kulenga palepale mpango mwingine uliibuka na kwa haraka haraka aliiendelea kuruka juu na kuendelea kuyashambulia kwa kuyalenga eneo la tumboni.
Sasa kile kitendo cha kushambulia mfufulizo lile lichuma kama
armor ambalo sanamu lile lilivalishwa liliharibika kwa mbele na Hamza mara baada ya kuangalia kwa umakini aliweza kuona kitu cha kung’aa kama vile ni vigoroli vilivyoninginia , ilionekana dhahiri maroboti hayo nishati yao ilikuwa ikitokana na fuwele(crystal) hizo.
Hamza palepale mara baada ya kuona ugunduzi huo aliruka tena na kwa kutumia mkono wake mmoja alinyakua zile fuwele kwa nguvu huku akilipa mgongo lile roboti lingine kumshambulia mgongoni.
“Arghhhhhh..”Alijikuta kitoa mguno mkubwa wa maumivu mara baada ya upanga kumpitia mgongoni na kumkata kiasi kwamba upanga uliacha mifupa yake wazi .
Lakini hata hivyo matarajio yake yalikuwa kama alivyowaza , kwani lile roboti ambalo fuwele yake ya kimadini imeondolewa liliacha kabisa kupigana na lilikuwa ni kama limezima na alichokifanya ni kuondoa lile panga mkononi kwa ngumu na kisha alilielekezea upande wa lile roboti lingine na kisha akakaa pembeni kuona namna linavyomshambulia mwenzake , alifanya hivyo kwa ajili ya kujifunza mbiunu ile ya kimapigano na kwa dakika kadhaa aliweza kuelewa baadhi ya mbinu yake
Baada ya hapo kwa hasira kubwa alianza kushambuliana na lile lililobakia kwa kutumia upanga sasa , ilikuwa rahisi kulitoboa eneo la chini ya tumbo lake kwa nguvu mpaka alipoharibu lile vazi lake la chuma na hatimae aliweza kuona fuwele nyingine na alipeleka mkono na kuichukua na baada ya hapo sanamu lile liliacha kusogea na kuzima kabisa na kama lisingezima Hamza angepoteza shingo kwani upanga ulishamfikia tayari na kumkandamiza.
Baada ya shughuli hio pevu alijikuta akikaa chini huku akihema kwa nguvu na kuanza kucheka kicheko kikubwa kilichojaa uchungu , alijiambia kwamba kama isingekuwa yeye wale wengine wote wangebakia kuwa nyama kama wangeingia ndani ya hilo eneo.
Hamza aliishia kuinua juu zile fuwele ambazo zilikuwa zikitoa mng’ao wa ajabu ndani yake na hakujua zilikuwa zimetengenezwa na nini lakini kwa kushika tu zilikuwa zina hali flani ya kupiga shoti mkononi.
Aliishia kugeuza macho yake kulia na kushoto kuangalia kama kuna kitu kingine lakini hakuweza kuona na aliona hana haja ya kuendelea kupoteza muda kwa kudhania pengine kunaweza kuwa na mtego mwingine ndani ya hilo eneo.
Kwa namna ya kuchechemea huku damu zikiwa zinamtoka alijilazimisha kutoka ndani ya hilo eneo.
Kitendo cha kutoka nje ya kile chumba alianza kusikia sauti ya vitu kama ngurumo zinazotokea nyuma yake.
Palepale wasiwasi ulimwingia na kujiuliza au kulikuwa kumetegwa bomu ndani ya pango hilo , muda ule aliweza kuhisi mtetemeko mkubwa wa ardhi huku mchanga ukianza kumdondokea kutoka juu.
Baada ya kuhisi hatari ya kufukiwa akiwa ndani ya pango hilo kwa uwezo wake wote alikimbia kutoka nje kabisa , lakini kitendo cha kufikia tu nusu y ake aliweza kugundua mawe yalikuwa yakimzibia njia.
Palepale alijua pango hilo lilikuwa likijizamisha lenyewe na kujifunga , aliamini lazima watu ambao walitengeneza hilo eneo , ili kuzuia wezi wasije kuiba na kuondoka walitengeneza ulinzi wa kuwafunika wezi ndani yake wasifanikiwe kutoka nje.
Hamza alijua kabisa kama akifukiwa na mchanga na mawe , itakuwa ngumu kupona hata kama awe hajaumia hivyo kwa haraka sana alitumia uwezo wake wote kuchoropoka katika mawe yaliokuwa yakianza kuporomoka.
Haikuweleweka hata nguvu kazitoa wapi kwani alipita kwa spidi kubwa mno kiasi kwamba jiwe la mwisho kuziba njia halikumkuta na alikoswa kuoswa kwa sentimita kadhaa.
Kitendo cha kuruka juu na kutoka nje eneo lote lilianza kuporomoka kwa juu kuziba shimo lililokuwa chini yake
Kwa jinsi mfuatano huo wa maporomoko ulivyokuwa ukitokea ilikuwa ni kama vile dunia imetengeneza tundu kwenye kwenye kiini chake.
Hamza hakuwa hata na muda wa kuangalia maporomoko hayo maana hakujua ni umbali gani yataishia hivyo alikimbia kushuka chini na kwenda kukaa mbali kabisa na aliishia kushangaa tu kile kilichokuwa kikitokea mbele ya macho yake.
Mpaka hali inakuja kutulia kilichoweza kuonekana ni shimo kubwa juu ya kilele hicho na aliona miaka kadhaa mbele mimea ikisha kuota hakuna mtu ambae atakuja kudhania eneo hilo kulikuwa na pango kubwa chini yake, hata kama wanasayansi wafike tena na kujaribu kufanya utafiti aliona wanaweza wasitoke na majibu , isitoshe shimo lililokuwa chini yake limefunikwa na mawe na sio mchanga , hivyo kama wataamua kuchimba wangetakiwa kupambana kwanza na mchanga mwingi na kisha mawe kitu ambacho ingekuwa ngumu sana na isitoshe lazima wangehitaji sababu ya kufanya hivyo kama watataka kufanya kazi hio kubwa.
Kutokana na jambo hilo Hamza aliweza kupitia uzoefu wa aina yake , aliweza kugundua dunia ina vitu vingi ambavyo vimejificha na binadamu hawafahamu , kwa namna eneo hilo lilivyokuwepo ilikuwa ni ngumu sana kwa binadamu kudhania kulikuwa na kitu kimefichwa chini yake.
Dakika hio hio wakati akitaka kujiandaa kuondoika aliweza kuhisi msisimko wa kusogelewa na kiumbe kisichokuwa cha kawaida na kumfanya vinyweleo vyake kusimama.
Kitendo cha Hamza kugeuka nyuma aliweza kushuhudia mtu aina ya kiumbe cha ajabu kilichokuwa kimesimama mita kadhaa nyuma yake kwenye shina la mti.
Ilikuwa sahihi kusema ni kama kiumbe kutokana na aina ya uvaaji wake , alikuwa ni ngumu kusema mtu yule alikuwa ni roboti au mtu alievalia machuma mwilini , ila muonekano wake ulikuwa mweusi huku kichwani akiwa amevalia helmeti la rangi nyekundu na mbele yake kwenye mdomo palikuwa pamefunguka na kumfanya Hamza kuona ni kama mtu yule anaongea.
Hisia zake zote zilimwambia huyo ni mtu na sio roboti lakini alishindwa kujua ni mtu mwanamke au mwanaume kutokana na suti hio ambayo malighafi yake haikueleweka kama ni ya chuma au madini gani, lakini kutokana na maelezo ya wale watswana alijua lazima huyo ndio mtu alietoa kazi ya kuchimbwa kwa hilo eneo na kwa vyovyote yupo hapo kishari.
Hamza aliishia kujisikitikia kutokana na majeraha aliokuwa nayo halafu adui mwingine anajitokeza mbele yake , aliishia kujiambia kazi imeanza upya.