SHETANI RUDISHA NAFSI ZETU
MTUNZI: SINGANOJR
SEHEMU YA 53/52
Tuliishia Bibi yake Regina ametembelea makao makuu ya kampuni na kuzidiwa Ghafla.
Endelea sasa.
Licha ya kwamba Mirium kuonekana amepoteza fahamu lakini ilionyesha ni kiasi gani alikuwa katika maumivu makali , uso ulipoteza nuru kabisa na ulikuwa umejikunja kana kwamba alikuwa akisikia maumivu makali.
Hamza mara baada ya kumuona mzee huyo alijua moja kwa moja ni vipindi vya mwisho mwisho vya ugonjwa huo na muda wowote anaweza kuondoka.
Lakini namna ambavo Regina alikuwa akilia na alivyowekewana ahadi na bibi yake kwa ajili ya kutoka nae Out , aliona kama akifa mapema Regina atakumbwa na majuto na huzuni kubwa , hivyo mara baada ya kuingia garini aliliendesha kama kichaa na ilimchukua dakika ishirini kufika hospitalini.
Mara baada ya Manesi kumchukua upande wa Regina alikuwa ni kama mpira ulioisha upepo wakati akikaa kwenye benchi.
Hamza alijua hata aongee neno la kumfariji halitokuwa na maana kwa muda huo hivyo na yeye alikaa pembeni yake kimya akimpa kampani.
Muda nao haukusimama,sekunde baada ya sekunde dakika zilisogea na hatimae usiku ukaingia.
Regina aliejichokea aliinua uso wake na kuangalia saa na hakuweza hata kujua muda umesogea vipi kwa kasi namna hio , kwani ilikuwa imetimia saa mbili kamili za usiku tayari.
Aligeuza uso wake na kumwangalia Hamza na alimuona kuwa na utulivu huku mikono akiwa ameikunja kifuani.
Hamza muda huo alikuwa ni kama sanamu kutokana na mkao wake , ilikuwa ni kama anaogopa kupiga kelele.
“Unaweza kutangulia ili uwahi chakula cha usiku kabla ya muda haujapitiliza”Aliongea Regina kwa upole huku macho yake yakiwa na majimaji kama mtu anaetaka kutoa machozi.
“Hata wewe hujakula chakula cha usiku bado”
“Sijisikii kula , huna haja ya kuendelea kubaki na mimi hapa , ninaweza kubakia mwenyewe tu”
Aliongea na kumfanya Hamza kuvuta pumzi nyingi na kuzishusha na kisha alishika bega lake.
“Kama umechoka unaweza kuegamia hapa , niwe feki au halisi bado cheo changu ni mpenzi wako”
“Haina haja , sijachoka hata hivyo”Aliongea huku akigeuka na kuangalia pembeni na kumfanya Hamza kuishia kutoa tabasamu kuonyesha kumwelewa na kisha aliegamia ukuta.
“Japo sina kumbukumbu za kutosha wakati nikiwa mtoto , lakini napata nusu nusu ya kumbukumbu za maisha yangu nikiwa mdogo , nakumbuka nikimuona mama yangu akiwa katika hali ya maumivu makali.. natamani kukumbuka kila kitu lakini bado nashindwa kuona kila kitu lakini licha ya kumbukumbu kidogo nilizokuwa nazo nahisi maumivu makali ambayo hayavumiliki kila dakika na saa ninapojiwa na kumbukumbu kuhusu mama yangu”Aliongea Hamza na kumfanya Regina kumwangalia Hamza kwa shauku.
“Huna kumbukumbu zote za utoto wako?”Aliuliza Regina na Hamza alitingisha kichwa kukubali.
“Mama yako amekufaje , pia hukumbuki?”
“Sikumbuki kabisa ninachokumbuka ni hisia nilizopata na kumbukumbu chache za mama yangu kuwa katika maumivu makali mpaka kukata roho, sikumbuki zaidi”.
Regina alijikuta akishindwa kujizuia na kushikilia sketi yake , ijapokuwa alimuona Hamza akiongea katika hali ya utulivu lakini alijisikia vibaya katika moyo wake kusikia maneno hayo.
“Ninachomaanisha ni kwamba najua ni hisia gani unazopita muda huu na nataka kukupunguzia mzigo”
Regina aliishia kuinamisha kichwa chake tu na hakuongea neno , upande wa Hamza pia hakuongea neno zaidi na alifunika macho yake akiwa ameegamia ukutani akisubiri.
Dakika kumi mbele aliweza kuhisi kitu kikiyagusa mabega yake na kumfanya afungue macho na kuangalia na hakuweza kujizuia kutabasamu mara baada ya kuona ni Regina aliejiegamiza kwake.
Regina alionekana kuwa na waswasi kana kwamba hakutaka Hamza kumwelewa vibaya.
“Usinifikirie vibaya , nimechoka kidogo tu”
“Ndio najua”
Baada ya hapo hakuna alieongea na walisubiria kwa namna hio mpaka lisaa lingine likapita na hatimae mlango wa cha ICU ulifunguliwa na bibi yake Regina alitolewa
“Dokta vipi hali ya bibi?”Aliuliza Regina mara baada ya kumkimbilia dokta na manesi waliokuwa wakimtoa bibi yake.
“Tumejitahidi kadri ya uwezo wetu lakini niseme tu hali yake ya inazidi kudhoofu kadri dakika zinavyosogea na muda wowote anaweza kuondoka, mnapaswa kujiandaa”Aliongea Dokta huyo wa kike wa makamo na kisha aliungana na kundi lake na kuendelea na safari
Regina aliishia kumwangalia bibi yake kwa huzuni wakati akitolewa ICU kwenda wodi za VIP.
Haikuchukua dakika nyingi na Shangazi alifika kutokea nyumbani na mara baada ya kusikia Mirium hana muda mrefu alijikuta akishikwa na huzuni.
“Baba bado tu hajafika?”Aliuliza Regina.
“Yupo mkoani kwa wakwe zake”Aliongea Shangazi akiwa katika hali ya huzuni kidogo.
“Oh..!
Regina alijikuta akikosa neno , ni kama alitegemea kitu kama hicho hivyo hakutaka kuwaza zaidi na kujipa matumaini hewa.
“Regina nitakaa hapa hospitalini kwa siku kadhaa na madam , inabidi mteseka kwa siku kadhaa wenyewe nyumbani”Aliongea.
Regina hakuwa na pingamizi , isitoshe alikuwa na majukumu makubwa sana ya kuendesha kampuni hivyo muda wa kukaa hospitalini ulikuwa ni mdogo mno.
Wakati huo Bibi Mirium ambae amewekewa Oksijeni aliweza kufumbua macho yake taratibu kivivu na kwa ukungu wa macho aliweza kuwaangalia watu hao watatu waliokuwa mbele yake.
“Regina …!”Aliita.
“Bibii!!”
Regina mara baada ya kusikia jina lake linaitwa alikimbilia kitandani kwa haraka na kwenda kushikilia mikono ya bibi yake huku akiwa ameinama.
“Bibi mimi hapa”Aliongea Regina huku akitabasamu.
“Mjukuu wangu nataka uniahidi kitu kimmoja…”Aliongea huku mikono yake ikionekana kumtetemeka na kauli yake ilimfanya Shangazi na Hamza kukunja sura kiasi maana ilionekana kabisa ni maneno ya mwisho mwisho.
“Bibi nakusikiliza , niambie tu.”
“Niahidi kwanza utafanya ninachokuambia”
“Bibi sijawahi kwenda kinyume na ahadi , bibi usiwe na wasiwasi nakuahidi”
“Hapo sawa .. nataka ufunge ndoa na Hamza hata kama ni ya serikali”Aliongea hatimae.
Dakika ambayo Regina aliyasikia maneno hayo macho yake yalichanua kwa mshagao huku uso wake ukiwa katika hali ya kutokuamini , ilikuwa ni kama vile nafsi imeuacha mwili wake.
Upande waShangazi alionekana kuwa katika tafakari ya kina huku akimwangalia Hamza.
Ijapokuwa Hamza aliikuwa ametegemea hilo lakini hakuamini bibi huyo atatumia dakika zake za mwisho kumtaka Regina kufanya jambo hilo.
Ukweli ni kwamba katika hali aliokuwa nao ilikuwa ni jambo lisilokuwa la kawaida kuongea , lakini ilionekana kutokana na uzoefu na ugumu mzee huyo aliopitia ndio maana akaongea hivyo.
Alionekana akijua hakuwa na muda wa kusubiri Regina aamue mwenyewe kuolewa na Hamza ndio maana alitaka kitendo hiko kifanyike kabla hajakata roho.
Upande wa Hamza na yeye alikuwa akimwangalia Shangazi na kwa jinsi alivyokuwa akimuona alijiambia tu lazima kuna maneno ambayo Shangazi ameongea kwenda kwa Bibi Mirium, isitoshe licha ya kumuonaShangazi kuwa kama mama wa nyumbani lakini siku ya kwanza tu kumuona alijua sio mtu wa kawaida.
“Bibi unapaswa kupumzika , unajichosha zaidi ukiongea”Aliongea Regina akitaka kuingilia anachotaka kusema bibi yake kwa mara ya pii.
Lakini Mzee huyo alimshikilia Regina kwa nguvu zake zote huku akijitahidi kumkazia macho, alionekana kuwa siriasi mno kile ambacho anataka Regina kufanya.
“Niahidi hapa hapa kama utakubali ninachokuambia”
Regina alijikuta akiingiwa na hisia mchanganyiko , ilikuwa ni hisia za maumivu , majonzi , kuchanganyikiwa, aibu na uoga.
Baada ya dakika moja ya ukimya aliishia kutoa tabasamu la kukubal.
“Nakuahidi nitafanya hivyo lakini swala la ndoa ni la makubalianyo ya watu wawili , Hamza anaweza asikubali”Aliongea Regina na kisha alimgeukia Hamza na kumpa ishara ya kukataa.
Hamza alimwangalia Regina namna alivyokuwa siriasi akimpa ishara za kukataa na alijikuta akisita kidogo.
“Mimi sina tatizo , nakubali ndoas”Aliongea
“Wewe..!!”
Regina alijikuta akifoka katika hali ya aibu na hasira kwa wakati mmoja huku akijimbia Hamza anawaza nini.
Bibi Mirium mara baada ya kusikia kauli hio kutoka kwa Hamza alijikuta akipandisha kifua na kukishusha kwa nguvu na kumwachia Regina, ilikuwa ni kama kila anavyovuta pumzi na kupumua ameongeza mwaka mmoja wa kupumua.
“Vizuri …nyie wote ni watoto wazuri na nataka kuwaona mkiwa pamoja kwa kifungo cha ndoa”
Hamza aliishia kuvuta pumzi huku akimwangalia Regina kwa kumuonea huruma , kumbukumbu za kile ambacho Yulia alimwambia kilimjia na aliona pengine ndio maana bibi yake Regina anafosi wafunge ndoa.
“Naenda kupunga kidogo upepo hapo nje , kama unataka tuongee utanikuta”Aliongea Hamza na kisha bila ya kujali alitoka nje mpaka eneo la maegesho ya magari na kwenda kuegamia kwenye mtende na kukodolea macho mwezi huku akionekana kuwa katika mawazo.
Alijikuta akiingiza mkono kwenye mfuko na kutoa simu yake na alienda upande wa namba za simu na alijikuta akiiangalia namba ya Eliza kwa muda na kisha alienda katika namba ya Dina na kuiangalia na alijikuta akirudisha simu mfukoni.
Swali lilikuwa moja tu , vipi kama kweli atafunga ndoa na Regina , Eliza atachukuliaje swala hilo? , si ataumia mno , vipi atakubali kuendelea nae , vipi kuhusu Dina.
Lakini jibu lilikuwa ni ndio, akimuoa Regina atamuumiza mno mpenzi wake Eliza , ni kweli hakuwa akimpenda Regina kiviile na pengine ni kutokana na kutokumjua kwake kwa muda mrefu , lakini mahesabu yake ni kama yalikuwa yakimwambia alimuona Regina kwanza kabla ya kumuona Eliza , pili Regina alionekana kuhitaji ulinzi mno kulingana na maadui zake pamoja na kile alichokifahamu kuhusu Regina kuwa na ugonjwa wa akili , haya yote ndio yaliomsababishia kusema ndio , lakini bado moyo wake ulikuwa mzito mno kila alipokuwa akimfikiria mpenzi wake Eliza.
Hamza alionekana kuwa na wasiwasi pia kwa wakati mmoja , hakufika Tanzania kwa ajili ya kufunga ndoa bali alifika Tanzania kwa ajili ya kumfahamu Mzee ni nani, wasiwasi wake hakujua katika misheni yake hio ni hatari za aina ngapi ataweza kupitia maana Mzee hakuonekana kuwa mtu wa kawaida.
“Kwanini umekubaliana na alichosema bibi?”Aliuliza Regina ambae alionekana kuwa katika hasira na kumfanya Hamza kumwangalia Regina kwa muda bila ya kutoa jibu , ni kama aikuwa akimchunguza lakini upande wa Regina alionekana alikuwa akitaka majibu.
“Kuna sababu gani ipi nyingine , nimeamua kujipandisha cheo kutoka kuwa Boyfriend mpaka kuwa Mume , naamini mshahara wangu utaongezeka mara mbili”Aliongea Hamza.
“Hebu geukia huko kwanza , sipo hapa kutaniana na wewe”Aliongea Regina huku akiona aibu kidogo.
“Hebu ingia kwenye gari tutafute eneo lolote tule chakula , hata kama njaa huna mimi njaa ninayo , tutaongea huku tunakula, sitanii”Aliongea Hamza akiwa siriasi na kumfahya Regina kuingia ndani ya gari kihasira hasira .
Hamza hakujali ubora wa Mgahawa kwa muda huo alijali kushibisha tumbo lake tu hivyo aliendesha gari na kwenda kupaki katika Mgahawa mdogo tu lakini ulionekana kuwa na mazingira safi na ilikuwa bahati Regina hakuwa na pingamizi.
Mmiliki wa mgahawa huo pamoja na wafanyakazi wake mara baada ya kuona gari hio ya Lexus ambayo imekaa kama zile zinazoendeshwa na wanasiasia waliishia kumkazia macho Regina na mmoja ya wafanyakazi hao ni kama alimfahamu Regina.
Walishangaa maana mgahawa wao ulikuwa ni wa hadhi ya wateja wa kawaida na sio matajiri, isitoshe hawakuwa na vyakula vya aina nyingi.
Hamza mara baada ya kukaa aliuliza ni chakula gani kinapatikana na mhudumu alimwambia.
“Vipi unaonaje tukiagiza Tambi na rosti ya mainu , unapenda?”
“Kwanini sipendi , dada niwekee hizo tambi na maini tu ila usiweke mchuzi mchuzi wenye vitunguu naomba na pilipili, pia utaniletea juisi ya embe ya Cereals”Aliongea Regina na kumfanya bosi wa mgahawa huo kutingisha kichwa huku akitoa tabasamu ni kama vile anaifurahia sauti ya Regina kama sio kumuonea wivu kutokana na uzuri wake.
Hamza alijikuta akinyamaza kimya, kwa jinsi Regina alivyochangamka ni kama alikuwa mzoefu wa migahawa ya namna hio na ilimfanya kumwangalia kwa tabasamu.
“Unaniangalia nini?”
“Sijakuangalia , ila kuna muda nakuona kama malaika uliemuasi Mungu”
“Unaongea upuuzi”Aliongea Regina huku akiona uvivu wa kujibishana na Hamza.
Dakika kadhaa waliletewa chakula na kutokana na njaa kila mtu alijikuta akiwa bize na chakula , muda huo Regina aliona midomo yake ilikuwa imejaa mafuta na kabla hata hajatafuta namna ya kujifuta Hamza alikuwa ashamchomolea tishu na kumpatia.
Regina aliishia kumwangalia Hamza kwa macho makavu kwa sekunde na kisha aliichukua ile tishu na kujifuta midomo.
“Ongea sasa kwanini umemkubalia bibi ilihali mimi sitaki”Aliongea Regina.
“Niongee nini tena , wakati kama huu bibi akiwa katika hali nzuri kidogo tunapaswa kwenda kujisajili na kupata cheti cha ndoa , isitoshe babe siwezi kubadili dini kwa ajili yako hehe”
“Acha kujipelekesha kimawazo , siwezi kuolewa na wewe”
“Lakini ushamuahidi bibi yako tayari na nimekubali mbele yake”
“Lakini wewe si una mpenzi wako?”
“Upo sahihi nina mpenzi na tupo hatua nzuri lakini hili lisikupe shida nitadili nalo mwenyewe”Aliongea Hamza na kumfanya Regina kuvuta pumzi nyingi na kuzishusha na muonekano wake ulizidi kuwa wa kikauzu.
“Ngoja nikuambie tu , mimi sijawahi kuamini maswala ya ndoa kabisa na tokea nikiwa mdogo nilijiapiza sitokuja kuolewa”
“Kwanini unasema hivyo , usiniambie ni kwasabqabu ya baba yako?”Aliuliza Hamza na Regina aliishia kuwa kimya kuonyesha ndio sababu.
Hamza alihisi kumwelewa Regina , isitoshe alikuwa ni mtoto wa nje ya ndoa.
“Sio kwasababu ya baba tu , ila nyie wanaume hamuaminiki kabisa , angalia kama wewe sasa hivi una mpenzi tayari na anaonekana kukupenda lakini bado unataka tufunge ndoa , unadhani ni kitu kizuri kwa mpenzi wako?”Aliongea Regina na kauli ile ilimfanya Hamza kutingisha kichwa kukubaliana nae.
“Nadhani sasa ushanielewa ninachomaanisha , hivyo achana na hayo mawazo kabisa , sina mpango wa kuolewa, kwangu mimi kuzikamilisha ndoto zangu naona kuna maana zaidi kuliko kuingia katika ndoa zilizojaa mateso”
“Unadanganya?”Aliongea Hamza.
“Kwanini nikudanganye?”
“Namaanisha hunidanganyi mimi ila unajidanganya mwenyewe”Aliongea na kumfanya Regina kukosa neno lakini kushangaa zaidi kutaka kujua Hamza anachomaanisha.
“Kama kweli huamini swala la ndoa basi unao uwezo wa kuolewa na yoyote yule, sio mimi tu hata awe James , kuna msemo wa kingereza wanasema ‘The more you care the more you will resist’ , kwa lugha nyepesi kama kweli ungekubali kuolewa na mtu yoyote ili kumridhisha bibi yako basi ni kweli hujali na huamini swala la ndoa”
“Sio kweli”Regina alikataa na kumfanya Hamza kumwangalia Regina na macho ya ki uchunguzi kana kwamba anajairbu kuangalia kilichopo ndani ya moyo wake.
“Basi ngoja nikuulize swali?, kwanini siku hizi umeanza kujilemba , kwanini umekuwa makini sana na mavazi yako na kwanini muda mwingine unakua mchangamfu na muda mwingine unakuwa kauzu mbele yangu?”Aliuliza Hamza na kumfanya Regina uso wake kuwa mwekundu.
“Unadhani nafanya hayo yote kwa ajili yako?, nafanya kila ninachotaka”
“Kama ni hivyo kwanini ulikasirika mimi kutokurudi nyumbani usiku na ukakasirika zaidi kutokana na kutorudi na nguo ulizonipa , kwanini umenisamehe kirahisi vile baada ya kukupiga vibao , kwanini unaonyesha hali ya kunitegemea katika baadhi ya vitu?”
“Sija.. umenielewa vibaya Hamza”
Regina alijikuta akishindwa kuwa na neno sahihi la kuongea na alijikuta akikwepesha macho yake na Hamza , mapigo ya moyo yalikuwa yakimwenda mbio mno na kauli za Hamza kusema ukweli zimemfanya kuhisi hali ya kupaniki.
“Regina!”Aliita Hamza na kumfanya Regina kumwangalia.
“Sikia kama kweli hujali ndoa basi hupaswi kuweka matarajio yoyote yae katika ndoa , kwasababu ndoa ni neno tu na hata cheti cha ndoa siku zote ni ushahidi tu wa kimaandishi , usidhanie kwasababu watu wanatambulika kama mke na mume na wanatambulika furaha wanayo au wanapendana, chukulia mfano baba yako na mama yako wa kambo, hivi unadhani wanafuraha kwasababu ni wanandoa?”
“Mama yako hakuwa ameolewa lakini alikuwa tayari kukuzaa ikimaanisha hakujutia kuzaaa na baba yako licha ya kutokuwa ndani ya ndoa , unadhani kama angekuwepo hai sasa hivi akikuangalia angejiona ni mwanamke mwenye laana kukuzaa nje ya ndoa?”
Maneno ya Hamza yalimfanya Regina machozi kuanza kujitengeneza katika mboni za macho yake.
“Tokea dakika ambayo mtoto anaanza kulia baada ya kuzaliwa moyo wake hupevuka palepale na hauna tofauti yoyote na wa mtu mzima , ili mradi una moyo na ni binadamu basi uwe ndani ya ndoa au nje ya ndoa haimaanishi kwamba huwezi kupenda, ndoa kama ndoa sio tatizo , tatizo ni watu , au nasema uongo?”
“Kupenda… kupenda… kwahio kwa mawazo yako unadhani nakupenda, hebu acha ukichaa wako”Aliongea Regina kwa hasira.
“Sawa unaweza kuniona kama kichaa na kunichukulia kama kichaa lakini kwa niaba ya kile anachopenda kuona bibi yako katika nyakati za mwisho wa uhai wake na kwa ajili ya wafanyakazi wote wa kampuni ya Dosam , tunapaswa kujiandikisha ili kupata cheti cha ndoa , kulingana na mtazamo wako hujali kabisa maswala ya ndoa na kwa mantiki hio kujisajili kama wanandoa haiwezi kukuathiri isitoshe utakuwa umepiga ndege wawii kwa jiwe moja , utamfurahisha bibi yako na utaikoa kampuni isiende kwenye mikono ya watu wasio na nia nzuri”
“Sitaki maswala ya ndoa fullstop”Aliongea Regina huku akigonga meza kabisa kutilia mkazo na kufanya baadhi ya wateja kumwangalia mrembo huyo na kujiuliza kuna nini mpaka kuonekana kuwa na hasria.
Regina hakuendelea kubakia ndani ya mgahawa huo , aliichukua mkoba wake na kuondoka haraka haraka
Hamza hakujali gharama ya chakula alitoa noti tatu za elfu kumi na kuziweka mezani na kumkimbilia Regina ambae alikuwa akilisogelea gari.
“Regina nitaendesha mimi?”Aliongea Hamza lakini Regina alimsukuma na kisha alifungua mlango wa dereva na kuingia.
“Sitaki kukuona tena , ondoka”
Regina alijihisi kuchanganyikiwa sio kwasababu Hamza alikosea ni kwasababu kila alichoongea Hamza ulikuwa ukweli ambao alikuwa katika vita nao.
“Bosi umesahau funguo za gari ninazo mimi?”
“Nipe funguo”Aliongea Regina mara baada ya kugundua hakuwa na funguo na anataka kuwa dereva.
Hamza mara baada ya kuona namna alivyokuwa siriasi aliishia kuzunguka upande mwingine na kuingia kwenye gari na kisha alimkabidhi ufunguo.
“Toka kwenye gari”
“Sitoki, kama nilivyosema kesho naenda kuaga ubachela”
“Wewe endelea tu kunichokoza”
“Nitakuchokoza mpaka uwe mke wangu”Aliongea Hamza.
Ukweli ni kwamba sio kama alikuwa akitaka sana kumuoa Regina bali aliona ndio njia pekee ya kumsaidia kwa wakati huo , ki ufupi hakuwa na jinsi na ili kufanya hivyo alitaka angalau kuonekana siriasi,ijapokuwa Regina anakataa lakini yeye ndio njia ya kutatua tatizo.
Regina aliishia kumwangalia Hamza kwa dakika kadhaa huku akijiuliza ni mkosi gani amejiingiza mpaka kukutana na Hamza, licha ya kwamba mwanzoni mpango wake ni kumridhisha bibi yake angalau kuwa na boyfriend feki lakini muda huo alijihisi kukosa amani kabisa, aliishia kuwasha gari na kulitoa ndani ya eneo hilo kurudi nyumbani.
“Regina mimi sio mtu mbaya ki hivyo , ukifikiria vizuri utaona nimekuokoa ulivyotekwa , hebu fikiria stori inavyonoga mtu akisikia namna shujaa Hamza alivyomuokoa mwanamke mrembo katika mikono ya watekaji , hili kitalaamu tunasema ni Penzi la papo kwa papo”
“Tunalikaribia daraja la Kigamboni , unadhani nashindwa kulitumbukiza gari baharini na wote kupotea, wewe endelea kuongea”
“Damn .. acha kuniogopesha namna hio .. siongei tena”
Regina hakuwa mkataa ndoa bali alikuwa anaiogopa ndoa , ki ufupi wengi wanaosema ni wakataa ndoa mara nyingi wanaona aibu kusema wanaogopa ndoa.
“Usinikodolee macho angalia pembeni”Regina hakuweza kuhimili macho makali ya Hamza
Muda ambao Hamza anaangalia pembeni kama alivyoambiwa hisia mbaya zilimvaa muda uleule mara baada ya kuona pikipiki ambayo ilikuwa nyuma yao kwa muda mrefu.
Ilikuwa ni Ducat 1299 igales inayovuma kwa uwezo wake wa mbio na kusafiri kilomita nyingi, thamani yake ilikuwa sawa tu na BMW X3 au zaidi , sasa juu ya pikipiki hio kulikuwa na wanaume wawili ambao wamevalia helmeti nyeusi na kufanya sura zao zisionekane.
Kilichomfanya Hamza kuhisi hali isiokawaida ni kutokana na msisimko wa nia ovu ya kimauji iliowavaa watu wale ni hisia ambazo mtu wa kawaida hawezi kuzipata.
“Regina simamisha gari”Aliongea Hamza mara baada ya kuona usalama wao ndani ya gari ni mdogo.
“Unataka nini tena?”
“Kuna watu wanatufuatilia , haraka simamisha gari pembeni”Aliongea Hamza.
“Tunafuatiliwa…!”Regina palepale akili yake iliamka na kukanyaga breki lakini mara baada ya kuikanyaga uso wake ulifubaa.
Hamza palepale aligundua kuna kitu hakipo sawa na alimgeukia na kumwangalia.
“Nini tatizo?”
“Breki hazifanyi kazi”Aliongea Regina na kumfanya Hamza kukunja ndita na palepale alijua watu ambao wapo kwenye pikipiki mmoja wao ameshikilia kifaa kinachofanana na simu kwenye mkono wake.
“Wanatumia kifaa maalumu kudhibiti mfumo wa kielektroniki wa gari , naona wanatumia mbinu hii kutusababishia ajali ili ionekane ni ajali ya kawaida kabisa baada ya uchunguzi”
SEHEMU YA 34.
Regina mara baada ya kusikia kauli hio mikono yake iliokuwa imeshikilia usukani wa gari ilianza kutetemeka , isitoshe alikuwa msichana na ni ngumu kwake kuhimili mshituko wa namna hio
“Kwahio tunafanya nini , gari halipunguzi mwendo na tunakaribia mataa mbele yetu?”
Hamza alijikuta akiinua macho mbele na kugundua kweli mbele yao wanazikaribia Traffic light na magari ambayo yalikuwa yakitoka Kariako kwenda Mbagala yalikuwa mengi mno na pili katika lane yao kulikuwa na magari mbele yao ambayo pia yanapunguza mwendo , kama wakiendelea hivyo hivyo basi ni hakika watayagonga magari yaliokuwa mbele yao.
“Achia usukani , nitaendesha mimi rudi nyuma”
“Lakini siwezi kutoka hapa kirahisi”Aliongea Regina lakini Hamza bila ya kuchelewa kwa mkono mmoja alimnyanyua kutoka katika siti ya udereva na kumrushia katika viti vya nyuma ya gari , bahati nzuri gari yao iliikuwa SUV hivyo Regina hakujigonga na Hamza alimshika Regina makalio na kumsukumizia mpaka kwenye siti.
“Aiyaaa… umenigusa wapi!!?”
Regina licha ya kujua yupo hatarini alishindwa kujizuia kwa namna Hamza alivyomsukumiza kwa kumshika kalio.
Hamza hakutaka kujali zaidi na alishika sterling kwa mikono yake miwili na kuweka umakini kwenye kuendesha.
Gari ilikuwa ikiserereka kwa spidi kubwa mno na Hamza alijitahidi kadri ya uwezo wake kuyakwepa magari na kwenda mbele zaidi kiasi ambacho alifanya madereva kuanza kupaniki, ilikuwa ni upepo tu aliokuwa akiacha kila alivyopokuwa akipita gari.
Jambo zuri aliweza kulikunja gari vizuri na kuingia katika barabara ya dharula na bahati ilikuwa yake maana aliweza kupita mataa bila ya kugongana na gari.
Kitendo cha kupita tu Hamza aling’ata meno kwa hasira na kisha alikanyaqga pedeli na kuongeza mwendo zaidi.
“Wewe umekuwa kichaa , kwanini unakanyaga mafuta?”Aliuliza Regina kwa kupaniki asijue Hamza anafanya nini
“Wale watu kwenye pikipiki wameshikilia rimoti na inafanya kazi kwa umbali wa mita ishirini mpaka arobaini hivi, hivyo najaribu kuwaacha kwa zaidi ya huo umbali ili isifanye kazi ndio maana nimeongeza spidi zaidi”
“Kumbe! , wewe umejuaje sasa?”
“Wewe unadhani kama sina uwezo kwanini bibi yako analazimisha nikuoe?”Aliuliza Hamza na kumfanya Regina kugeuka yai.
“Ongeza umakini barabarani”
Kitendo cha kumaliza sentensi hio alichoweza kusikia ni sauti ya Ziii.. ziii..Ziii , gari ilikuwa imebadilika mngurumo wake na sasa ni kama ni mnyama aliekuwa akinguruma huku tairi zikisuguana na barabara.
“Argghh..!!”
Regina katika maisha yake hakuwahi kuwa katika hali kama hio , gari kwenda katika spidi ya hali ya juu mno na hakutaka kuangalia mbele zaidi ya kukizika kichwa chake
Uwezo wa Hamza wa kuendesha ulikuwa ni wa viwango va juu, baada ya kuingia katika daraja la Kigamboni aliongeza spidi zaidi kwa nguvu kabisa na gari ilichomoka kama mshale, mara baada ya kuangalia kwenye kioo alitoa tabasamu na palepale kwa nguvu alikanyaga breki na zilikubali.
“Creeek!!!”
Mataili ya magari yaliishia kuacha michirizi katika barabara ilioambatana na moshi , ilikuwa ni kama vile ndege inatua na hatimae aliweza kwenda kupaki gari pembeni mita kadhaa na daraja hilo katika stairi ya mshazari.
Kitendo cha gari kukanyaga breki na Hamza alivyoisimamisha gari katika mzunguko ilimfanya Regina kushikwa na kichefuchefu kikali , ijapokuwa mchakato wote ulifanyika kwa sekunde tu lakini ulikuwa sio wa kawaida kwake.
Wale watu kwenye pikipiki waliona hali sio nzuri na mpango wao ni kama umefeli hivyo kwa haraka waligeuza pikipiki wakidhamiria kukimbia.
Lakini Hamza hakuwa na mpango wa kuwaacha kabisa na alifungua mlango haraka na kutoka na kisha alianza kuikimbiza ile pikipiki na kadri alivyokuwa akikimbia mwili wake ulianza kubadilika.
Dereva wa ile pilipiki haikueeweka alikumbwa na nini lakini alijikuta akiyumba na kuisababisha pikipiki ile kuteleza na ikamshinda uzito na wote pamoja na aliempakia walidondoka chini na kabla hata hawajanyanyuka Hamza alikuwa ashawafikia tayari.
Muda huo hata Regina aliweza kutoka nje ya gari na kumkimbilia Hamza na kwenda kujificha nyuma yake.
“Nani kawatuma?”Aliuliza Hamza akiwa siriasi lakini yule dereva kwa utalamu alipiga sarakasi na kusimama na muda huo huo alichomoa Bunduki zile za kuwachomea sindano wanyama(Trangulizer gun) na kutaka kumfyatulia Hamza lakini Hamza alikuwa mwepesi mno kwani aliruka na teke na kumpiga kwenye mikono yake na kuifanya idondokee pembeni.
“Kama hamtaki kuongea nitawafanya muongee wenyewe”Aliongea.
Yule mwingine alionekana kuumia na alishindwa kusimama na Hamza aliamua kudili na yule aliesimama na kwa haraka alimsogelea na kumshika na kisha aliondoa ile helmeti na sasa aliweza kuona sura yake,alikuwa ni muafrika mwenye asili ya kisomali na alikuwa amevalia Heleni nyeusi.
Hamza alishangazwa na kitendo kile na kwa haraka haraka alimsogelea na yule mwingine aliekuwa akigulia maumivu na kutoa helmeti yake na wote kwa pamoja walikuwa wamevalia heleni japo yule mwingine alikuwa ni Mwafrika asilia.
“Nyie ni maninja kutoka kundi la Black Eared Snake!, inaonekana kuna watu kweli wamedhamiria kutuua”Aliongea Hamza akimaanisha watu hao ni kundi la maninja la Nyoka mwenye masikio meusi.
Kitendo cha Hamza kuongea neno hilo wale watu walijikuta wakishituka na kushangaa hawakuamini Hamza angeweza kuwatambua.
“Black Eared Snake ndio nini?”Aliuliza Regina.
“Ni kundi la maninja kutoka nchi ya CAR , ni kundi daraja C , ijapokuwa uwezo wa maninja wao hauwezi kuhesabika wa juu lakini wana mbinu nyingi za kusababisha mauaji , ndio kundi la kininja namba moja Afrika”Aliongea Hamza akimwelezea Regina kwa lugha nyepesi kwamba kundi hilo linatokea Afrika ya Kati.
Japo Regina hakuelewa maana ya kundi daraja C lakini alichojua muda huo hali ilikuwa ni ya hatari mno.
“Mmetumwa na familia ya Mzee Benjamini?”Aliuliza Regina.
“Usiulize maswali , ijapokuwa ni kundi daraja C lakini wanaongozwa na sheria kali za kininja , sheria kubwa ya ninja yoyote ni kutomtaja mwajiri wake”
“Kwahio tunafanyaje, tunawaacha waende?”
Hamza alifikiria kidogo na aliona asingeweza kuwaua wakati huo ambao Regina alikuwa mbele yake , alikuwa na uwezo wa kuwaua na kupoteza miili yao kimazingara lakini hakutaka maswali kutoka kwa Regina.
“Pigia simu polisi watakuja kudili nao”Aliongea Hamza na Regina alikubali lakini kabla simu haijapokelewa wale manijja walionekana kutafuna vitu huku wakiwa wamekaza sura.
Hamza hakutaka hata kuwazuia kwani aliona pia ni moja ya njia ya kutatua tatizo.
Dakika mbili tu wale manijja walitema damu nyeusi na kufariki palepale mbele ya Regina.
“Mamaaaa..!!!”
Regina alijikuta akipiga ukulele na pasipo ya kujua upande wa pili polisi alikuwa ashapokea simu yake.
“Hello , nini tatizo!!?”Hamza mara baada ya kuona Regina ameshikwa na mshituko alichukua simu na kutoa maelekezo kwa poilisi, upande wa pili wa polisi walionekana kushangaa maana ni kama hawakuwa wakiamini walichoambiwa , lakini hata hivyo walisema wanafika muda si mrefu.
Regina aijikuta akichuchumaa pembeni ya barabara huku akionekana ni kama ameshikwa na kichefu chefu.
Ilibidi Hamza kumsogelea na kisha alimshika bega kwa namna ya kumtuliza , mwanamke huyo ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuona mtu akijiua kwa staili hio hivyo ilikuwa haki yake kushituka.
Dakika chache baadae Polisi waliweza kufika eneo la tukio na kutokana na muda ulikuwa umeenda sana Hamza alimchukua Regina na kuingia ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea nyumbani .
Lakini sasa kitendo cha dakika chache tu za kuendesha sikio la tatu la Hamza liliweza kunasa sauti ya kitu kubip ndani ya gari , kama hakuwa mtu mzoefu asingeweza kugundua kitu hicho.
Ilikuwa ni bomu , ilionekana ndani ya gari lao kulikuwa kumetegwa bomu kama mpango B.
Hamza hakuwa hata na muda wa kumwambia Regina nini kinachoendelea na haraka sana alijifyatua kutoka katika siti yake na kuelekea upande wa Regina alipo na kumbeba juu juu akimtanguliza mbele yake , kitengo cha kufyatuka kwenye gari walisukumizwa na presha ya msukumo wa bomu na kwenda kutua kwenye majani upande wa pili wa barabara huku gari yao ikiteketea kwa moto mkubwa.
Kiikuwa kitendo cha sekunde chache mno kufanyika kuanzia kufunguliwa mkanda mpaka kutolewa nje ya gari na mlipuko kutokea na kuja kutua chini akiwa hajaumia.
Mlipuko ule uliyafanya masikio ya Regina kupatwa na ukiziwi wa ghafla na kengele za masikio kugonga , ilimchukua dakika kadhaa mpaka akili yake kurudi katika uhalisia.
Regina hakuamini alikuwa ameokoka katika mlipuko huo wa gari , Hamza angechelewa kidogo tu wangekuwa tayari ni maiti.
“Hamza… Hamza..!!”
Regina alijikuta akiita kwa nguvu mara baada ya kuzidi kulemewa na uzito wa mwili wa Hamza uliomlalia kwa juu , lakini licha ya kuita hakukuwa na majibu na alijikuta akimeza mate mengi na kujitoa katika mwili wake kwa kumsukuma pembeni..
Mara baada ya kuona mgongo wa Hamza machozi yalianza kumtoka bila ya kujua , aliweza kujua Hamza alitumia mwili wake kumkinga na presha ya mlipuko.
Regina alikuwa ameshikwa naBumbuwazi na maswali mengi yalipita katika kichwa chake na kujiuliza inamaana yeye ni wa muhimu mno kwa Hamza mpaka kujitoa kwa namna hio kumlinda.
Alijikuta akipotezea mawazo yale na kwa haraka sana alimtingisha Hamza kuamka.
“Hamza amka , nakuomba usife , fungua macho yako..”Regina alijikuta akipaliwa mpaka na mate na alijikuta akianza kutafuta simu yake ili kupiga simu lakini simu hakuwa nayo na alijikuta ni kama kuchanganyikiwa kumemvaa.
Dakika hio hio watu ni kama walisikia mlipuko huo na walianza kusogelea eneo hilo kwa kasi na Regina alianza kupiga kelele kuomba msaada.
“Regina..!!”
Alijikuta mwili wake ukimtetemeka mara baada ya kushikiliwa mkono wakati akitaka kuamka kwenda kuomba msaada lakini Hamza alionekana kuamka.
“Nipo hapa , unaendelea , hali yako ikoje?”
“Mbaya sama nadhani siwezi kuishi tena”Aliongea kinyonge.
“Uisongee hivyo huwezi kufa , ngoja niombe msaada tukupeleke hospitalini”Aliongea huku akisimama.
“Haina haja , mpaka nikifika hospitalini nitakuwa nishakufa”
“Acha kuongea kuniogopesha, huwezi kufa”
“Namuona Israeli mtoa roho mbele yangu , Regina nisamehe siwezi kukuoa kama bibi yako alivyosema”Aliongea Hamza
“Hapana usife , umesema mwenyewe unataka unioe, huwezi kufa leo, kesho tunatakkiwa kwenda kusajili ndoa yetu , naomba usife jamani”
Regina hakujua hata maneno yanatokea wapi lakini aliona ndio mbinu ya kumbembeleza Hamza asipoteze uha.
“Upo tayari tuandikishe ndoa yetu?”
“Ndio nipo tayari .. please Hamza naomba usiniache..”Aliongea na alijikuta akianza kulia kwa kwikwi.
“Kwakuwa umekubali mwenyewe , basi nimeghairi kufa mpaka siku nyingine”Aliongea Hamza huku akimwangalia Regina na tabasamu la uchokozi.
Regina mara baada ya kusikia kauli hio alijikuta akimwangalia Hamza na kumkuta hakuwa na dalili yoyote ya kuonyesha yupo kwenye maumivu.
Hamza alikaa kitako huku akipangusa mikono yake na kumwangalia Regina huku akimcheka.
“Kwahio Regina kesho ndio siku yetu ya kuuaga ubachela sio?”
Regina alijikuta akiwa haamini alikuwa akichezewa akili na Hamza muda wote , kadri alivyokuwa akimwangalia ile huzuni aliokuwa nayo ilianza kubadilika na kuwa na hasira kali, alijikuta akiona kipande cha zege pembeni na bila ya kujiuliza mara mbilimbili alikichukua na kumlenga nacho Hamza kichwani.
“Holly shit!!!”
Hamza alijikuta akifyatuka kama mshale akikwepa kipande kile ambacho kilienda kutua mtaroni.
“Hamza nitakuua …!!!”Aliongea huku akirusha ngumi za kike kwa hasira lakini Hamza aliishia kuidaka mikono yake na kumkumbatia kwa nyuma.
Shida halikuwa kumbatio tatizo ni mikono ya Hamza iliposhikilia katika eneo la kifua la mrembo huyo.
Hamza aliweza kuhisi kitu kilaini katika mikono yake na hakuweza kujizuia na kuuliza.
“Regina kumbe upo vizuri kiasi hichi”
“Wewe mpuuzi niachie”
Regina uso wake ulikuwa umeshika moto alitamani kujirusha kwenye mtaro.
“Sawa ila sijafanya makusudi”Aliongea Hamza huku akimuachia.
“Halafu kingine kwanzia kesho unakwenda kuwa mke wangu hivyo haijalishi wapi nina gusa”
“Kafie mbali huko , siwezi kuwa mke wako”
“Umeahidi mwenyewe zaidi ya mara mbili kama nikiendelea kuishi tutaenda kujiandikisha , kama bosi wa kampuni kubwa sidhani ni vizuri kwenda kinyume na ahadi yako unatoa mfano mbaya kwa wafanyakazi wako”
“Umenitega kwa kunidanganya , niliongea vile nikajua unakufa kweli”
“Kama upo tayari kuoana na mimi wakati nakaribia kufa si vizuri zaidi nikiwa hai maana utafurahia zaidi matunda ya ndoa , hata hivyo tuachane na hayo kwanza hata nikikuelezea huwezi kuelewa nini maana ya Matunda ya ndoa”
“Wewe..!!”
Regina alijikuta akipiga miguu chini kwa hasira na kuanza kupiga hatua kurudi barabarani.
Ukweli ni kwamba alishasahau kabisa kama walipata ajali ya gari lao kulipuka , ilionekana makusudi ya Hamza kumchezea akili yamemshushia presha kabisa ya swala zima la ajali.
“Mke unaenda wapi tena?”
“Naenda nyumbani”Aliongea Regina alijua hawezi kumfanya chochote Hamza hivyo hakuona haja ya kuendelea kujibishana nae , kuhusu maswala ya gari yao kulipuka aliona awaachie polisi wafanye kazi yao.
Dakika kadhaa tu wote waliweza kufika nyumbani na Regina mara baada ya kuingia ndani na kukumbuka Shangazi hayupo aliona ni kama kuna hali ambayo sio ya kawaida na alijikuta akigeuka na kumwangalia Hamza lakini alishangaa kumuona amekaa kwenye ngazi akionekana kufikiria.
“Wewe unafikiria nini?”
“Nawaza namna ya kudili na hawa watu ambao wanatusababishia ajali kila siku , sidhani kama nisiposhughulika nao mapema wanaweza kuacha”Aliongea Hamza na kumfanya Regina kumshangaa , dakika kadhaa zilizopita mwanaume huyo alionekana kuwa kama kichaa lakini sasa hivi amegeuka na kuwa siriasi.
“Kama unatengeneza hela nyingi jua kuna ambao hawana uwezo wa kutengeneza hizo hela , hivyo ni kawaida kuwa na maadui, nimejiandaa kwa vitu kama hivi ndio maana sipati shida hata vikitokea”
“Wewe unapaswa kuzingatia kufanya biashara na mimi nitazingatia namna ya kukulinda”
“Kwahio unapanga kufanya nini?”
“Regina hivi unadhani wale wajinga wametumwa na familia ya Mzee Benjamini au kuna maadui wengine ambao hatuwajui, sidhani ni swala la kawaida kukodi maninja hatari kama wale nje ya nchi kwa ajili yetu”
“Siwezi kujua ila familia ya James ndio maadui zangu wakubwa”
“Mpaka wameenda mbali kukodi majina kutoka Afrika ya kati!!?”
“Siwezi kujua kama kuna adui mwingine au lah”Aliongea Regina na kumfanya Hamza kutingisha kichwa.
“Usikurupuke kutaka kulipa kisasi , haijalishi una nguvu kiasi gani ni ngumu kushinda watu wengi”
Regina aliona swala la kuweza kuokoka katika ule mlipuko ilikuwa bahati lakini upande wa Hamza haikuwa swala la bahati.
“Naona ushaanza kuchukua cheo cha mke kwa namna unavyotoa ushauri”Aliongea Hamza akitabasamu kizembe na kumfanya Regina kugeuka na kuelekea juu chumbani kwake
Hamza mara baada ya kukaa sebuleni kwa dakika kadhaa hakuelekea tena ndani bali alitoka nje na kufunga mlango na kisha kuondoka
*******
UHALISIA NDANI YA NDOTO 04:30am
Licha ya mwanamke yule kuungua na ule moto wa maajabu na kufariki lakini kicheko chake na laana alizokuwa akiongea wakati wa kuungua zilikuwa bado zikisikika kama vile ni mwangwi unaojirudia rudia katika masikio ya watu.
Watu wale waliokuwa wakishangilia yule mwanamke mchawi kuchomwa moto walijikuta wakipatwa na woga kutokana na kitendo kile cha kuendelea kuzisikia zile sauti licha ya kwamba tayari amekwisha kuungua na kufariki.
Kusanyiko lile baada ya yule Askofu aliehusika kumuunguza yule mwanamke na moto wa nuru kuondoka walimfuata nyuma na kuingia katika kanisa kubwa na kuanza kusali kwa kutubu.
Licha ya kila mtu kutawanyika Hamza alijikuta akiwa amesimama katika eneo lilelile bila ya kupiga hatua , kilichokuwa kikimshangaza ni kwamba bado akili yake ni kama ilikuwa ikiyaona macho ya yule mwanamke yakimwangalia , haikuwa hivyo tu ule moto ambao ulimuunguza yule mwanamke bado alikuwa akihisi nguvu yake.
Alikuwa katika mshituko mkubwa mno kwa kile kilichotokea , kiasi cha kusahau kabisa nafsi yake na akili yake ipo katika mwili ambao sio wake
“Hii nguvu ni ya kimaajabu mno”Aliwaza Hamza.
Tofauti na kuogopa kama ilivyokuwa kwa watu wale ambao hakuwa akiwajua lakini yeye alikuwa ameshikwa na tamaa kubwa ya nguvu ile alioweza kuiona na kujiuliza anawezaje kujifunza uwezo ule.
Muda huo alijikuta akishikwa mkono kitendo kilichomshitua na kumwangalia aliemshika.
“Jamani Luther , Asante Mungu wa nuru , Asante Mungu wa nuru kwa kumuokoa na mateso kama ya baba yake , kijana mdogo kama huyu anastahili rehema za Mungu”
Hamza alijikuta akivutwa kutolewa katika eneo lile na yule mwanamke huku akiongea kila aina ya maneno ya shukrani kwa Mungu wa Nuru.
Alikuwa Mzungu , ukweli ni kwamba kila mtu aliekuwa akimuona kwake alikuwa ni Mzungu.
Hamza alijaribu kunyanyua mdomo ili kuongea lakini mdomo ulikuwa mzito mno na bado alikuwa katika mshangao wa kuitwa Luther, alitaka kuuliza yeye ni nani na kwanini ana mwili wa kizungu.
Hamza aliendelea kushangaa zaidi mara baada ya kuingizwa katika nyumba ndogo na mwanamke wa makamo wa kizungu ambae alikuwa akitaja kila aina ya shukrani kwenda kwa Mungu.
Kitendo cha kushangaa na kujishangaa kilimfanya yule mwanamke kumwangalia Hamza na kuendelea kutokwa na machozi.
“Luther ugonjwa wa akili umekutesa mno , hebu jiangalie ulivyokonda..”Aliongea yule mwanamke huku akimwangalia Hamza.
Hamza bado alikuwa na maswali , hakujua kilichokuwa kikiendelea ni nini lakini alijua kitu kimoja hakuwa ni Hamza bali alikuwa ni Luther, aliogopa pia kuongea kwa kuonekana labda watamjua yeye ni Hamza katika mwili wa Luther.
“Alisa usiongee sana na Luther, ndio kwanza amepona na lazima atakuwa na uchomvu , Ivani msaidie mama yako twende nyumbani”
Hamza aligeuza macho yake na kumwangalia mwanaume wa kizungu mwenye nywele nyeupe akiongea , alikuwa na kama miaka hamsini hivi kwenda sitini hivi , licha ya kuwa na ndevu nyingi lakini ilionyesha katika ujana wake alikuwa na mwonekano mzuri.
“Asante Shangazi , nipo sawa bado tu najihisi kizunguzungu”Hamza aliongea lakini aliongea nje ya hiari yake , ilikuwa ni kama kuna kitu ambacho kilikuwa kikimsukuma kuongea hivyo.
Yule kijana ambae alikuwa amemleta Hamza kuangalia mchawi akichomwa moto alikuwa amemshikilia mwanamke huyo wa kizungu aliefahamika kwa jina la Alisa.
“Luther nimefurahi sana kukuona hali yako inatengemaa yule mchawi amestahili , amekutesa sana”
“Wakati ule anahamia na kuwa jirani yako alionekana kama mwanamke mrembo sana mstaarabu mpaka nilipatwa hadi na wazo la kuhakikisha John anakuwa mke wake lakini alikuwa ni mchawi, tulimshuhudia mara kadhaa akifukua miili ya watu kutoka makaburini ili kufanyia majaribio ya kichawi , Asante sana Mungu kwa kumfanya akamatawe na ushahidi wakati akifukua mwili kaburini , nashindwa hata kufikiria kama angefanikiwa katika uchawi wake ni watu wangapi wangeathirika”
Hamza aliendelea kusikiliza yale maneno ya Alisa kwa umakini na sasa ni kama anapata mwanga , yule mwanamke alikuwa mchawi na alikamatwa na ushahidi akiroga kwa kufukua maiti makaburini ndio maana akachomwa moto.
Kutokana na mwanamke yule kuwa jirani yake na yeye pia alichukuliwa kama mshirika wa uchawi na yule mwanamke na kuanza kuhojiwa na ilionekana mahojiano hayakuwa ya kawada , kuna nguvu za ziada ambazo zilikuwa zikitumika na ndio kilichomfanya Luther kupoteza fahamu, ilimfanya Hamza kudhania pengine Luther alikuwa akishirikiana katika maswala ya ulozi na yule mwanamke ndio maana alikuwa akimwangalia sana.
Yule mwanamke Alisa alionekana kuongea mfululizo kana kwamba alikuwa akisimulia tukio zima la namna mwanamke yule alivyokamatwa na namna ambavyo pia Luther alihusishwa katika swala hilo mpaka kuachiliwa.
Yule mwanaume mwenye nywele nyeupe alimwangalia Hamza na muda uleule alionekana kutabasamu na kumshika bega.
“Yupo hivyo , unapaswa kumzoea”Aliongea na kumfanya Hamza kutingisha kichwa.
“Alisa alikuwa mwanamke mrembo sana wakati wa ujana wake lakini mara baada ya kumzaa John alibadilika sana na kuwa kama hivi , mpaka sasa naweza kusema amekuwa sio mshindani wangu tena likija swala la kuongea”Aliongea yule mzee kwa kingereza.
Upande wa Hamza bado hakuzingatia mazungumzo yao ni kama alikuwa akiwaza kutaka kujua alikuwa wapi na kwanini nafsi yake ipo katika mwili ambao sio wake.
“Joeli mwanaume aliekuwa na nguvu na hamasa ya juu ya kutimiza ndoto zake za kuwa msanii mkubwa sasa hivi amegeuka na kuwa mlevi”Aliongea Alisa
“Aalto ni jiji ndani ya nchi ya Zaburi , watu wasiohesabika wanafika kwa ajili ya kutimiza ndoto zao lakini je ni wangapi ambao wamefanikiwa , isitoshe Alisa nimeacha kuwa mlevi tokea siku John aliopata kazi”
“Asante Mungu , nadhani unajua namna tulivyoweka matumaini yetu kwa John na Ivan , John amekuwa mtoto mzuri kwetu ameweka juhudi kubwa na sasa ameweza kuchaguliwa na kujiunga na jeshi , kama ataweza kuamsha karama ya damu yake na kutambulika ataweza kupewa cheo cha Ubwana na wengi watamheshimu”Hamza alimsikia yule mwanake Alisa akiongea na upande wa yule mwanaume aliefahamika kwa jina la Joeli alitingisha mabega na yule mwanamke aliefahamika kwa jina la Alisa alionekana kujishtukia na kumwangalia Hamza.
“Luther nisamehe , sijamaanisha kwamba wewe huna uwezo , ulitakiwa kupitia mafunzo kidogo wakati ulipokuwa mdogo”Aliongea yule Alisa lakini ni kama radhi yake haikuwafanya kazi.
“Luther hana shida na naamini ataweza kuibeba ndoto yangu na kuwa msanii mkubwa”Aliongea yule Joeli.
“Ndio nataka kuwa msanii mwanamuziki mkubwa”
Hamza alijikuta akisema bila ya kufikiria huku akicheka na kumfanya yule mwanamke kuvuta pumzi ya ahueni na kuanza kuongea tena kila neno ambalo lilimjia mdomoni na ilimfanya Hamza kuelewa mji huo na ulimwengu huo kitu alichojua ni kwamba yupo katika jiji lililofahamika kwa jina la Aalto ndani ya nchi ya Zaburi.
Hamza muda huo licha ya kujua nafsi yake ipo katika mwili ambao sio wa kwake lakini ukweli alijikuta ni kama alikuwa akiangalia TV kwa kupitia VR na kumfanya awe katika mazingira yale matukio yanapotokea.
Nafsi yake muda huo ilikuwa ikimwambia lazima afahamu yupo wapi , kama yupo kwenye ulimwengu mwingine lazima ajue yupo ulimwengu gani , kama ni kumbukumbu za maisha lazima azifahamu ni kumbukummbu gani ambazo zimemleta katika mazingira ya namna hio , mazingira ambayo ni ya kale kabisa lakini yenye kujaa maajabu na hata kama ni ndoto lazima ajue kwanini anaota ndoto ya namna hio.
Hamza alijikuta akishituka mara baada ya kutingishwa kwa nguvu na akiwa katika hali ya kuhema alijikuta akifumbua macho yake na pembeni yake alikuwa amesimama Regina.
“Amka wewe , nenda kaoge na kisha badilisha mavazi yako”Aliongea Regina aliekuwa amesimama akimwangalia Hamza namna alivyojiachia bila ya kujifunika shuka kutoka kiunoni na kufanya kifua chake kuwa wazi pamoja na mwili uliovimba kutokana na mazoezi , alijikuta akishindwa kujizuia na kuanza kuona aibu za kike.
Alijiambia ndio maana Hamza anaonekana kuwa na maamuzi ya haraka kutokana na kuwa na mwili wenye mazoezi.
Aliona mwili wa Hamza haukuwa wa kawaida kabisa na aliushangaa kana kwamba hakuwahi kuona mwili wa mwanaume.
Hamza upande wake ni kama hakupenda kutoka ndotoni , ukweli ni kwamba siku kadhaa nyuma alihofia ile ndoto lakini mara baada ya kuota zaidi ya mara nne ni kama alianza kupata shauku ya kuendelea kuota , kwake ni kama alikuwa akiangalia tamthilia akiwa ndotoni , kiichomfurahisha ni kwamba ndoto hio ni kama ilikuwa ikijua wapi aliishia kuota kwani ilianza palepale na kuendelea lakini sasa mara baada ya kuona kumekucha ilimshangaza, aligeuza macho upande wa eneo la swichi kuangalia labda ule mshumaa wa nuru umechomekwa kwenye umeme lakini hakukuwa na mshumaa na aliona kabisa ameota bila ya msaada wa kitu.
“Regina kwanini umeingia chumbani kwangu bila ya kugonga?”Aliuliza Hamza.
“Nimegonga mara kibao hufungui ndio maana nikaingia , fanya haraka nataka tukachukue cheti cha ndoa”Aliongea Regina na kumfanya Hamza kufunua shuka bila ya kujali alikuwa amevalia boksa tu.
Regina hakutegemea Hamza alikuwa na boksa tu na baada ya shuka lile kumtoka mwilini kilichoonekana ni eneo la mbele la Hamza kuwa na hamasa kubwa ya mapambano.
“Ah!!.. unafanya nini ?”Regina alijikuta akigeuka na kuangalia pembeni huku mapigo ya moyo wake yakienda kasi mno.
“Hii ni swala la kibaiolojia , kuna haya gani ya kushituka wakati ni ishara nzuri kuonyesha nina afya nzuri”Aliongea Hamza
“Huoni aibu?”
“Nione aibu ya nini ndani ya chumba changu , Regina unaonekana kuwa na mchecheto mno kwenda kuchukua cheti cha ndoa asubiuhi asubuhi, hukulala nini?”
“Sitaki bibi kuwa na wasiwasi kabla ya kuondoka , usifikirie mbali ni cheti tu ila maisha yetu yatabakia vilevile, nimekaa chini na kufikiria na nimegundua bibi anachotaka ni kuona cheti tu na hajasema hatuwezi kuachana hapo baadae , baada ya mkataba wako wa kazi kuisha tunaweza kuachana na kila mtu akaendelea na mambo yake”
“Kuna haja ya kwenda mbali hivyo , kuna haja ya kuichukia ndoa kiasi hicho?”
“Sijasema naichukia ndoa nachukia kufunga ndoa na mtu kama wewe”Aliongea na kumfanya Hamza kuvuta pumzi ya masikitiko huku akimwangalia mwanamke huyo akizipiga hatua kutoka chumbani kwake.
“Regina kwasababu umekuja kuniamsha chumbani kwangu , unaonaje na mimi nikiwa nakuja chumbani kwako kukuamsha , itakuwa ni kuamshana kwa zamu”
“Ole wako uingie chumbani kwangu”Aliongea Regina na kutoka nje.
Upande wa Hamza wakati akijiandaa kwenda kuoga simu ilimfanya aghairi kwa dakika kadhaa na kisha kuchukua kujua nani anampigia asubuhi asubuhi hio , baada ya kuangalia na kuona jina ni la Dina alijikuta akitoa tabasamu la uovu na moja kwa moja alikumbuka ukatili aliofanya usiku.
“Mrembo nini maana ya kupiga simu asubuhi yote hii”
“Unaniuliza nini , umefanya nini wakati nikiwa nimelala?”Sauti upande wa pili ilionekana kuwa na hasira mno.
INAENDELEA GRUPU WATSAPP 0687161346.