SHETANI RUDISHA AKILI ZETU
MTUNZI: SINGANOJR.
Regina alikuwa katika mshangao maana ilikuwa ni mara yake ya kwanza kumuona Shangazi akiwa na uwezo wa kuzimisha watu wenye mafunzo ya kininja. Asichokijua Regina ni kwamba Shangazi alikuwa ni mwanajeshi na yupo kwenye maisha yake si kama shangazi yake tu, bali kama mlinzi wake kwa ajili ya kulinda nafsi nyingine iliyolala ndani yake.
“Shangazi, umefikaje hapa?” aliuliza Regina akiwa na mshangao.
“Hata kama wakubwa wa familia wamekwisha kuondoka, jina la familia linatakiwa kudumu. Nimeshindwa kuvumilia kusubiria nyumbani, ndiyo maana nimekuja kwa ajili ya kukupa ulinzi. Hamza pia yupo mwenyewe tu, hivyo si rahisi kukulinda na kudili na adui kwa wakati mmoja,” aliongea Shangazi.
Upande wa Hamza, hakushangazwa na uwezo wa Shangazi hata kidogo. Ukweli ni kwamba alishamuona si mtu wa kawaida tokea siku ambayo anatia mguu katika nyumba ya Regina, ni hivyo tu hakutaka kumchimba kiundani.
“Shangazi, naomba umlinde Regina kwa sasa. Ngoja niende nikawatafute,” alisema Hamza.
“Vipi kuhusu Mzee Wilson?” aliuliza Shangazi.
“Ametutoka tayari.”
“Nini!?” Shangazi alijikuta akitoa macho na mwili wake ulianza kumtetemeka.
“Kuhusu kilichotokea, ngoja Regina atakuambia. Mimi napaswa kuwahi, la sivyo nitachelewa,” aliongea Hamza.
Shangazi aliishia kumwangalia Regina na palepale alimkumbatia kwa nguvu huku machozi yakimtiririka. Alimuonea huruma; anakwenda kumzika bibi yake na baba yake kwa wakati mmoja.
Hamza, licha ya kwamba moyo wake haukutaka kuwaacha wenyewe, kwa wakati huo muda ulikuwa ni mali hivyo alipaswa kuwahi.
Mara baada ya kushuka kwenye lifti, alimpigia Afande Himidu na kumwambia nia yake ya kuwafukuza wahalifu. Afande huyo alimwambia Hamza awahi Gati ya Kigamboni Naval Base atakutana na wanajeshi wa kitengo cha Malibu.
Hamza, mara baada ya kupata taarifa hiyo, hakutaka kuchelewa hata kwa sekunde. Uzuri ni kwamba hoteli ya Dar Lux ilikuwa eneo la Kigamboni, hivyo haikumchukua muda mrefu kufika.
Kitendo cha kukaribia tu eneo hilo, gari SUV ya kijeshi ilisimama karibu yake na mlango ulifunguliwa haraka haraka na mwanaume na mwanamke. Mwanaume alikuwa amevalia kombati za kijeshi rangi nyeusi na koti la kuzuia risasi kifuani, na mwanamke alikuwa amevalia kombati za kijeshi za kikosi maalum cha Malibu. Hawakuwa peke yao; kulikuwa pia na Afande Norbert Geza na baadhi ya wanajeshi wa kikosi chake.
Hamza aliwatupia macho wale waliokuwa wa kwanza kushuka kwenye gari na aliishia kutingisha kichwa baada ya kuona walikuwa na mafunzo ya nishati za mbingu na ardhi, na wote walikuwa wakifuatilia levo ya mzunguko kamili.
“Mr. Hamza...” aliekuwa wa kwanza kuita ni Norbert. Licha ya kwamba siku kadhaa zilizopita alipokea kichapo kutoka kwa Hamza, lakini muda huo ni kama ameweka kinyongo pembeni na sasa alikuwa na macho ya heshima na woga kiasi.
“Ilikuwaje mkachezewa akili? Yaani bado mmegundulika lakini mkaendelea kufuatilia magari yao?” aliongea Hamza.
Kauli yake ile iliwafanya wanajeshi hao kushikwa na soni juu ya kile kilichotokea; dakika ambayo waligundua gari waliokuwa wakiifukuza haikuwa na mateka, walikuwa wamekwisha kuchelewa muda mrefu.
"Wewe ni nani, unadhani una vigezo vya kutoa maoni yako juu ya utendaji wetu kama jeshi?" Aliongea mwanaume ambaye alianza kutoka kwenye gari akitangulizana na mwanamke.
"Mimi kuwa nani sio muhimu kwako. Mmeshajiandaa na boti tayari? Kuna uwezekano wametuacha umbali wa nusu saa na itakuwa ngumu kuwafikia," aliongea Hamza.
"Wewe inakuhusu nini kama tumeita boti ama hatujaita? Na unajuaje wamekimbilia baharini? Kuna uwezekano wamejificha eneo lingine la nchi kavu na wamekudanganya uamini wapo baharini."
"Hivi unadhani hili kundi la roho zinazotangatanga ni wajinga au nyie ndio wajinga? Kama wakiendelea kubakia hapa jijini ni swala la muda tu kukamatika maana hakuna njia watakayopita bila kuonekana. Unadhani kundi la kihalifu la daraja B linaweza kuwa na akili za kijinga namna hiyo?"
"Wewe ni nani kuwa na ujasiri wa kutukana kikosi chetu?" Aliongea yule bwana kwa hasira.
"Afande, huyu ndiye aliyetuma ripoti kwenda kwa Mshauri Mkuu. Ila haijalishi hata kama unafahamiana na Mshauri Mkuu, haimaanishi una mamlaka ya kutunyooshea vidole," aliongeza kwa dharau.
Kapteni Norbert, mara baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, aliingilia kati mara moja. Alijua wanajeshi wenzake hawakuwa wakimfahamu Hamza.
"Hamza, hawa ni makomandoo wa kitengo cha Malibu. Wanafahamika kwa majina yao ya msimbo, Kanali Mwiba na Kanali Barafu. Ndio wanaongoza hii misheni," aliongea Kapteni Norbert kwa upole, akijaribu kutuliza hali.
“Sijali kama nyie ni makanali au majenerali, fanyeni haraka tupate helikopta na boti, la sivyo wakishaingia maji ya kimataifa itakuwa ngumu kuwakamata tena,” alisema Hamza kwa msisitizo.
“Kama wakifikia maji ya kimataifa, maana yake ni mwisho wetu na jeshi haliwezi kuendelea kuwafuatilia,” aliongea Afande Mwiba.
“Watu wamelipua bomu ndani ya ardhi ya Tanzania, wameteka na kuua halafu unasema hujali kama wakikimbilia nje ya mpaka wa Tanzania, au ni kwa sababu mnawaogopa?” Hamza aliuliza kwa hasira.
“Angalia maneno yako, dogo. Usijione kwa sababu unafahamiana na Mshauri Mkuu unaweza kudharau jeshi,” alisema Afande Mwiba huku uso wake ukiwa na hasira mbele ya Hamza.
Wakati huo, geti la kuingia ndani ya gati ya kijeshi lilifunguliwa, na taarifa ya boti kuwa tayari ilitolewa. Hamza hakutaka kupoteza muda; aliongoza njia ili awahi, lakini Afande Mwiba na Afande Barafu walimzuia mbele yake.
“Wewe ni raia tu, huruhusiwi kutufuata kwenye hii misheni. Hatuendi kucheza,” alisema Afande Mwiba akiwa siriasi.
Hamza alijiambia kama sio heshima kwa Afande Himidu, muda huu huyu bwana angekuwa anaugulia maumivu.
“Relax, bro, sihitaji ulinzi wako. Mwili wa baba mkwe wangu upo kwenye mikono ya watekaji, na kwa namna yoyote natakiwa kuurudisha kwa ajili ya kuzikwa,” alisema Hamza, akijiambia angalau Regina apate nafasi ya kumzika baba yake.
“Tuwie radhi, Mr. Hamza. Hili lishakuwa chini ya jeshi tayari, na sio swala binafsi. Hatuwezi kukuruhusu kuongozana na sisi na chochote kikikutokea tukose namna ya kujibu mbele ya Mshauri Mkuu,” alisema Afande Barafu kwa upole.
Ukweli ni kwamba Afande Himidu licha ya kutoa maagizo ya kesi zote zinazomhusu Hamza kufungwa, hakuelezea sababu ni nini zaidi ya agizo la moja kwa moja. Hivyo, Kanali Mwiba na Afande Barafu hawakumchukulia siriasi, walimuona ni mtu wa kawaida tu ambaye hana mafunzo ya kijeshi.
Hamza aliishia kushusha pumzi na hakutaka kuendelea kuelezea zaidi, bali alipiga hatua kuelekea upande wa boti iliko.
“Simama wewe, hujasikia nilichokuwa nikisema?” Aliongea Afande Mwiba kwa hasira mara baada ya kuona Hamza hakuwa na nia ya kumsikiliza onyo lake.
Baada ya kuona Hamza hataki kusimama, alimsogelea kwa kasi na kutaka kumshika kola ya shati. Lakini mkono wa kushoto wa Hamza ulikuwa na kasi mno kwani alimshika Afande Mwiba kiganja chake na kumwangalia kwa macho ya kutisha.
“Ukiendelea kunichelewesha, sitojali kukutupa baharini,” alisema Hamza kwa ukali.
Afande Mwiba hakujua amekamatwa vipi na Hamza. Kitendo kile kama mwanajeshi kilimfanya kuona ni dharau kiasi cha kuanza kupandwa na hasira.
“Kwa mafunzo yako kidogo, ndiyo maana unaleta kiburi mbele yangu, lakini nikuambie, sheria ni sheria. Hata kama unafahamiana na Mshauri Mkuu, haina maana mbele ya sheria. Kikosi changu kipo kwenye misheni, na mimi kama kamanda wa misheni hii nikitoa maagizo, unapaswa kutii,” alisema Afande Mwiba kwa ukali, na ghafla tu msisimko wa nguvu za nishati ya mbingu na ardhi ulianza kujikusanya kwenye mwili wake, misuli yake ikawa migumu kama jiwe.
“Usipoachia kiganja changu, nitauvunja mkono wako kwa shambulizi linalokuja,” aliongea Afande Mwiba kwa sauti kali.
“Kwa uwezo wako mdogo huu, unadhani utaweza hata kunigusa?” Hamza alijibu, huku akiwa hajabadilika muonekano wake hata kidogo.
“Nadhani hujui hata unaongea na nani sasa hivi. Acha kunilazimisha kuwa siriasi, utaumia,” alisema Afande Mwiba, lakini Hamza aliishia kumwangalia kwa kejeli, akijiambia kuwa Mwiba ndiye hajui nani anashindana naye.
“Kanali, achana naye. Kwa ajili ya Mshauri Mkuu, ngoja afanye anavyotaka. Isitoshe, kwa wingi wetu, kundi la nafsi zinazotangatanga hawawezi kuwa tishio,” alisema Afande Barafu, au Kanali Caroline kwa jina lake la kawaida.
Kanali Mwiba alisita kidogo, lakini baada ya kumfikiria Afande Himidu, alijizuia na kuachana na Hamza.
“Ukija kutumbukia baharini, usije kunililia kuomba msaada maana sitokusaidia,” alisema kwa kejeli, na baada ya kauli hiyo alikimbilia kuelekea boti.
“Twendeni. Norbert, wasiliana na Afande Kwavava aendelee kufuatilia baharini kama kuna boti yoyote ya kutilia mashaka,” alisema Afande Caro huku akipiga hatua kusogelea Speedboat.
“Sawa, Afande!” alijibu Afande Norbert kwa saluti na wakati huo akitembea, alikuwa akifanya mawasiliano kwa simu ya upepo.
Hamza, mara baada ya kuingia ndani ya boti, aliishia kuangalia wanajeshi hao walivyokuwa na majigambo, na mdomo wake ulicheza kwa kejeli.
Ilikuwa ni sawa kwao kujisikia wapo juu, kwani wanajeshi wote ambao walikuwa chini ya Kitengo cha Malibu ndio waliaminika kuwa na uwezo wa juu sana kati ya wanajeshi wote. Hii ni kutokana na kwamba mafunzo yao hayakuwa ya kawaida tu; yalichanganya na mafunzo ya nguvu za ziada kama vile kuvuna nishati za mbingu na ardhi.
Hamza, hata hivyo, mpango wake haukuwa kujipatia umaarufu kutoka kwao. Alichokuwa akihitaji kufanikisha kwa muda huo ni kupata mwili wa baba yake Regina na kisha awaue wahusika wote waliotekeleza kifo chake.
Mara baada ya wote kupanda ndani ya boti hiyo ya mwendokasi, iliwashwa na kuanza kushika kasi kuelekea katikati ya bahari ikifukuzia watekaji.
Ilikuwa ni boti ya kijeshi, hivyo ilikuwa na mafuta ya kutosha, lakini vilevile ilikuwa na ya ziada, na sio hivyo tu, kulikuwa na vifaa vya kujiokolea ikitokea dharura.
Hazikupita hata dakika kumi baada ya kutoka katika gati hiyo ya kambi ya jeshi, waliweza kupokea taarifa kutoka kwa Afande Kwavava na kuambiwa kuna boti ya uvuvi inayokimbia kwa kasi kuelekea maji ya kimataifa.
Baada ya taarifa hiyo, dereva wa boti hiyo aliongeza spidi mara mbili kwa ajili ya kuikamatia.
&&&&
Ndani ya boti ya uvuvi iliyokuwa ikitembea kwa spidi kubwa kuelekea katikati ya maji ya kimataifa, Mzee Benjamini, James, na Lamla walikuwa hawatulii kama vile wamekalia kaa la moto.
“Mzee Tui, watu wa Kitengo cha Malibu ni wa aina gani? Ni wanajeshi au polisi?” aliuliza James.
“Kama ni jeshi la kawaida ama polisi, nisingekuwa na wasiwasi namna yote hii. Ukisikia Malibu ni kitengo cha jeshi ambacho wanajeshi wake wana mafunzo si tu ya kupambana kwa silaha lakini pia ya kupambana na nguvu za giza. Mwanzo walikuwa wakikiita Kitengo cha Wachawi ila walikipa jina la Malibu kama heshima kwa Afande Malibu, mmoja wa wanajeshi walioweka historia katika kitengo hicho,” aliongea Mzee Tui, ambaye alikuwa na taarifa zote maana hata yeye alikuwa mmoja wa wanajeshi wa kikosi hicho.
“Kumbe ni hatari hivyo? Isije wakaja na meli za kivita tu?” James aliuliza kwa wasiwasi.
“Hilo haliwezekani, isitoshe tupo kwenye boti ya uvuvi tu,” alijibu Mzee Tui.
“Tui, kama tukishafika katika maji ya kimataifa kwa spidi hii, si inamaanisha mipango yetu yote imefeli, maana itakuwa ngumu kwa sisi kurudi Dar tena?” James aliuliza kwa hofu.
“Kufeli!? Mmepoteza nyie. Hamkujua mipaka yenu. Zidi ya mateka ndiyo maana akajiua. Isije mkawa na mawazo ya kwamba mimi ndiye nimesababisha hii misheni kufeli?” Mzee Tui alijibu kwa hasira.
“Wewe! Kwa hiyo unasema sisi ndiyo tumeifelisha? Yaani tumekubali kukulipa zaidi ya bilioni ishirini za Kitanzania, halafu kazi unataka kufanya nusu nusu?” Lamla aliongea kwa hasira.
“Kazi yenu imekamilika nusu na malipo mlionipatia ni nusu yake. Sidhani mpaka hapa tunadaiana,” aliongea Mzee Tui, na kauli yake iliwafanya Benjamini na wenzake kukamaa miili.
“Mpaka sasa nimepoteza vijana wangu wengi katika hii misheni, na inanifanya nione hata kiasi mlichonipatia ni kidogo kwa ajili ya kulipa fidia kwa familia zao. Hivyo kama msipomalizia kiasi kilichobakia, msije ongea chochote kuhusu kuendelea kuwafanyia kazi na pia kuhusu usalama wenu mtajua wenyewe,” alisema kwa msisitizo.
“Mzee Tui, unamaanisha nini? Kwa hiyo unapanga kutuacha katikati ya bahari wenyewe? Hivi ndiyo mnavyotimiza masharti ya mkataba?” aliuliza Mzee Benjamini kwa hasira.
“Kaa kimya. Kwanza kabisa, tushatimiza kazi yetu yote kulingana na makubaliano. Lakini kutokana na ujinga wenu mmefanya hii misheni kuvurugika. Pili, mpaka sasa hamna uwezo wa kutulipa kiasi kilichobakia na bado mnataka vijana wangu waendelee kuwafanyia kazi. Hamuoni mnakuwa wajinga?” Mzee Tui alijibu kwa ukali.
Benjamini na James walijikuta wakikosa maneno. Walikuwa na wasiwasi na woga mno na hawakuweza kujizuia kumtolea macho Lamla. Walikuwa wakimlaumu kwa kumpandisha munkari Mzee Wilsoni mpaka akachukua maamuzi ya kujimaliza.
“Mnaniangalia nini sasa wakati mlikuwa mkifurahia kumuona Wilsoni anateseka?” alisema Lamla.
“Yaani bado tu unapata ujasiri wa kuongea hivyo. Kama sio uwezo wako mdogo wa kushindwa kumdanganya Bi Mirum, unadhani tungefikia katika hii hali?” aliuliza Mzee Benjamini kwa hasira, lakini hata hivyo walikatishwa malumbano yao na watu waliosogea upande huo.
"Bosi, tumeweza kufanikiwa kufanya mazungumzo na The Shark na tutaweza kukutana nao upande mwingine," alisema mmoja wa vijana wa Mzee Tui.
"Vizuri sana. Endeleeni kuendesha kwa spidi yote. Tukifanikiwa kukutana na The Shark mbeleni, wanajeshi wa Malibu hawawezi kutukamata tena," aliongea Mzee Tui.
"Mzee Tui, The Shark ndio watu gani?" aliuliza James.
"Ni maharamia wa baharini. Kapteni Kenny ni rafiki yangu kwa miaka mingi. The Shark wanafanya shughuli zao katika ukanda wa Bahari ya Afrika Mashariki na Kati na ndio maharamia pekee wanaopatikana kwenye ukanda huu. Kwa msaada wao, Malibu hawawezi kutushambulia tukiwa kwenye maji ya kimataifa maana kuwashambulia The Shark ni kuchokozana na Al-Shabab."
"Hivi kumbe kuna maharamia wa baharini siku hizi?"
"Ndio maana meli nyingi za mizigo zinasafiri na wanajeshi, lakini hata hivyo maharamia hawa wa siku hizi ni tofauti. Mara nyingi hawaibi meli ila wanajihusisha na Black Market, ndio maana nchi hazitilii sana mkazo kuwaondoa," aliongea.
Black Market ni soko la ulimwengu wa giza au underworld market, soko ambalo kila kitu ambacho kinaonekana kuwa haramu au kuvunja sheria kinauzwa. The Shark licha ya kuitwa maharamia, hawakuwa majambazi kamili. Walikuwa ni wafanyabiashara wa bidhaa za kimagendo na haramu ikiwemo madawa ya kulevya na bidhaa zingine. Moja ya sababu kubwa ya The Shark kuogopeka ni kutokana na ushirika wake mkubwa wa kibiashara na makundi ya kigaidi ikiwemo Al-Shabab.
Wakati wakiendelea na maongezi, hatimaye waliweza kuona meli kubwa ya mizigo iliyoizungukwa na boti ndogo ndogo za kivita zilizokuwa na mikonga mikubwa ya mtutu wa kurusha mabomu.
"Ile ndio meli ya maharamia, mbona ni kama meli ya jeshi la nchi?" aliuliza Mzee Benjamini akionyesha mshangao.
Hakutaka kuamini kwamba meli kubwa ile na pia boti za kivita zinazoizunguka ni za maharamia. Mzee huyo kila alipokuwa akisikia neno haramia, alijua ni watu walioamua kuwa majambazi, ambao wanaiba kwa ajili ya kupeleka mkono kinywani.
"Vitu kama hivyo wanatoa kwa Shardbearer’s ambao wanakuwa kama madalali wa vifaa vya kivita vilivyoisha muda wake na taasisi za giza. Unadhani ni kwanini majeshi mengi yanawaogopa?" aliongea Tui.
Dakika chache mara baada ya boti yao kuvuka mpaka wa Tanzania na maji ya kimataifa, hatimaye waliweza kushuhudia bendera juu ya meli ile iliyokuwa na chata kubwa la samaki aina ya papa.
Eneo la deki ya meli hiyo, walionekana watu mbalimbali, weusi na weupe, waliokuwa wamesimama. Walikuwa na mwonekano wa kichafu na kwa jinsi walivyoacha ndevu ni kama hawakutaka sura zao kuonekana.