Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
Kongole kwa mwandishiSTORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
********************
SEHEMU YA THELATHINI NA TANO
SONGA NAYO................
“Kuna namna naona inatakiwa tuachane na mawazo ya kumtafuta huyu mtu kwanza bali tujue sababu za msingi ambazo zinamfanya ayafanye haya yote”
“Unahisi ni yeye kafanya haya?”
“Shilingi ndio utambulisho wake inaonekana hivyo ni yeye”
“Ni yeye ambaye alitakiwa kuwa amehusika na mauaji ya jaji mkuu mstaafu, inakuwaje ndani ya usiku mmoja yeye mwenyewe awe afrika ya kusini?”
“Kuhusu jaji mkuu nina uhakika sio yeye”
“Umelijuaje hilo Tigana?”
“Kwa sababu tangu nianze kuona mauaji yake, hakuna sehemu anaruhusu mtu wake ajiue mwenyewe hivyo huyo mama ameuawa na watu wake mwenyewe” kila mtu alimpa umakini Tigana kujua anacho kimaanisha kwa sababu alikuwa na hisia kali mno.
“Unataka kusemaje?”
“Kama ameenda Afrika ya kusini maana yake alihitaji kumjua mtu fulani ambaye huenda angemuongoza mpaka kwa Emilia. Kuna uwezekano mkubwa Emilia anawajua watu kadhaa ambao Gavin anawatafuta hivyo ingekuwa hatari kwao na kuimaliza hatari hiyo wakaamua kumuua ili akirudi amkose”
“Una uhakika na hili?”
“Hisia zangu zinanituma hivyo, kuna mnyororo wa watu wengi wakubwa wanaonekana wanatafutwa na huyu bwana”
“Kwahiyo unashauri nini Tigana?”
“Kwa hili ambalo limetokea maana yake kwa sasa atakuwa kwenye ndege ambayo inatua muda sio mrefu JNIA hivyo tunatakiwa kusimamisha kila kitu tukajaribu bahati yetu kama tunaweza kumpata. Kama tukifanikiwa kumkamata basi huenda haya yatafika mwisho na tutajua sababu ya yeye kuwa hivi kwa wakati huu”
“Are you sure?”
“Hisia zangu zinaniambia hivyo kiongozi” Walikuwa wanamwamini sana Tigana hivyo walipewa amri ya kuwahi mara moja uwanja wa ndege kumkamata Gavin ambaye waliamini wakati huo alikuwa kwenye ndege kurudi Tanzania baada ya kufanya mauaji hayo ya kutisha huko Afrika ya kusini. Je ni kweli alikuwa kwenye ndege na walikuwa wanaweza kumpata Gavin?
**********
SOUTH AFRIcAN AIRWAYS.
Ndiyo ndege ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu na majasusi kutoka ndani ya shirika la kijasusi la TIGI la Tanzania, ndege hiyo ilikuwa imeondoka masaa mawili yaliyokuwa yamepita ndani ya jiji la Jozi wakati wao wanapata taarifa juu ya mauaji ambayo yalifanya ndani ya jiji hilo. Baada ya kuipata taarifa hiyo walighairi kila kitu na kuamua kufanya zoezi la kubahatisha kwenda kumkamata Gavin kwa sababu walijua ni lazima alisafiri na ndege hiyo.
Wanaume hao watano walikuwa wamejipanga kwenye maeneo tofauti wakijifanya wapo hapo kwa ajili ya kupokea wageni wao huku wengine wakiwa wanajifanya kama walinzi wa eneo hilo kuhakikisha kila ambaye anapita hapo wanamuona na kama wangemuona mtu wao basi hawakutakiwa kupoteza muda zaidi ya kuondoka naye japo walijua zoezi hilo halikuwa rahisi kama ambavyo lilikuwa limeandikwa kwenye makaratasi ndiyo maana walibebwa wote watano ili kukiwa na ulazima wa kutumia nguvu za zaida isije kula kwao mtu mwenyewe alikuwa anaishi kama mzimu.
Zilikuwa ni dakika kumi na tano zimebakia ili ndege hiyo ambayo ilikuwa inatumia masaa yasiyo pungua matatu kutoka Jozi kufika Dar es salaam ili iweze kutua, muda huo hao wanaume walikuwa ndani ya uwanja huo wa ndege mkubwa tayari wakiwa makini kwa kila kitu kilichokuwa kinaendelea ndani ya hilo eneo bila kuwashtua watu au kuleta mtafaruko ama tafurani ya aina yoyote ile kwenye hilo eneo.
Hatimaye ndege ilitua na baada ya muda watu walianza kupita wakipishana huku na huko, wenyeji walikuwa wanashangilia wageni wao kufika huku wakiwapokea kwa bashasha na furaha ila wao walikuwa makini kupiga kila hatua kuhakikisha mtu wao haondoki ndani ya hilo eneo bila kupatikana. Watu walizidi kuwa wengi ila muda ulivyokuwa unazidi kwenda ndivyo walikuwa wakizidi kupungua taratibu mpaka walipo isha wote wakabaki wachache ambao walienda migahawani kupata chakula na wapendwa wao. Jambo la kushangaza ni kwamba mpaka abiria wanaisha hapo hawakumuona mtu wao huku kila mtu akiwa na picha yake mkononi.
“Nini kimetokea hapa?” Aliongea Tigana akiwa anaangaza kila upande baada ya kukutana na wenzake.
“Huenda hajasafiri” aliongea Jaden Mrisho
“Hapana, alijua kabisa kwamba kungekuwa na tatizo kama hili lazima kungekuwa na kizuizi kwenye viwanja vya ndege na washukiwa wa kwanza wangekuwa wageni maana yake hata yeye angekuwa hatarini kuweza kugundulika hivyo lazima amekuja na hii ndege ya mapema baada tu ya kufanya mauaji” Alieleza crispin Mkono.
“Kwa maana hiyo ni lazima alifika na kuchukua chumba karibu kabisa na uwanja wa ndege ili awahi kuondoka. Sina imani kama huyu bwana ni binadamu kama sisi” Sylvanos aliongea akiwa anasikitika.
“Hapana, ni mahesabu tu watu wa hivi wapo duniani ila ni wachache ndiyo maana wakifanya vitu huwa vinaonekana kuwa vya ajabu na wengine wakiamini kwamba haviwezekani. Swali la msingi ni kwamba kama alikuwepo hapa kapitaje? Na kama kapita tupo hapa maana yake yeye anatufahamu vizuri tu” Bariki baada ya kuongea hivyo ni kama kuna kitu kilipiga kwenye kichwa chake, alihisi kwamba aligongana na abiria mmoja wakati anageuka kumuangalia mtu huyo alitabasamu na kuweka mkono wake mmoja kifuani kama ishara ya heshima ila hakuelewa kama alikuwa ni yeye au siyo.
Alikimbia mpaka nje lakini hakuna ambacho alikiona wenzake wakiwa wanamshangaa bwana huyo
“Nahisi nimepishana naye” Aliongea Bariki
“Umejuaje?”
“Twendeni kwenye chumba cha kamera haraka” walikuwa na kibali cha mkurugenzi hivyo kwao kila kitu kilikuwa rahisi tu, waliingia ndani ya chumba hicho na kuanza kurudisha matukio yote nyuma ili waone kama mtu huyo alifanikiwa kutoka nje na alitokaje. Bariki alibaki anacheka kwa alicho kiona huku akiwa anatikisa kichwa
Kwenye ile video ya kwenye kamera, alipishana na shekhe mmoja ambye alikuwa amevaa kwa heshima mno, ndevu zilitengenezwa vizuri lakini ziliwekwa za kizee kidogo hivyo shekhe huyo alikuwa anaonekana kama mzee kiasi. Kwenye mkono wake mmoja alikuwa na fimbo ya kutembelea huku mkono mwingine ukiwa na begi jeusi la mkononi. Kichwani alikuwa na balakashea na miwani, alionekana kuwa mtu safi.
Huyo ndiye ambaye yeye Bariki aligongana naye na mtu huyo akaonyesha ishara ya kuomba msamaha huku akitabasamu kisha akaenda zake lakini kwenye mkono wake alikuwa na kitu kama kadi, haikuwa kadi bali kilikuwa kitambulisho cha Bariki. Baada ya kupishana pale yule bwana alitokomea zake kwenye gari ambayo haikuwa na namba hata moja ya usajili na bila shaka kuna mtu ambaye alikuwa kwenye ile gari akimsubiri kwani yeye baada ya kuingia kwenye ile gari hakukaa mbele bali nyuma hivyo kuna mtu ambaye alikuwa anamuendesha. Bariki alitabasamu ila moyoni alikuwa na hasira sana.
Tigana Mdachi alisogea kwenye skrini hiyo na kuirudisha nyuma ile video wakati mtu yule akipishana na Bariki, alitaka kuona ni kwa namna gani mtu huyo alifanikiwa kumuibia kitambulisho mwanaume huyo wa kazi bila hata yeye mwenyewe kushtuka! Alicho kiona yeye kilimtisha, vidole viwili ndivyo vilifanya ile kazi, kasi ambayo ilitumika kukibeba kile kitambulisho ilimfanya kuhisi hilo tukio lilihusiana na njia za giza.
“Binadamu gani ana uwezo wa kuwa na kasi ya namna hii?” alikuwa anaongea huku akiwa anairudia mara mbili mbili.
“Dunia inatuhakikishia kwamba bado tuna mengi ya kujifunza Tigana, kuna watu ukikutana nao unaweza kuona ni heri hata ukafa tu dunia uwaachie wenyewe. Watu wanaofanya haya matukio usiombe ukutane naye kwenye mazingira mabaya halafu ukawa mwenyewe, anakuua na hakuna mtu atakuja kujua kwamba uliwahi kuishi. Kama ameweza kumuibia Bariki bila hata yeye kujua kwa muda mfupi namna ile maana yake uwezo wake huyu umevuka kwenye ile hali ya ubinadamu, hii ni hatari kwa mwanadamu wa kawaida kuwa na nguvu za namna hii, anatakiwa kuzuiliwa mapema kabla hajawa hatari zaidi kwa watu wengine” Jaden Mrisho aliongea huku akiwa anaangalia dirishani kuona namna dunia ilivyokuwa inaenda kasi.
“Kwa hapa tulipo fikia tunamhitaji Princess sana na bosi anatakiwa kulijua hili”
“Ni ngumu kumrudisha kazini, amesimamishwa kazi kwa miaka miwili”
“Nina uhakika akiwa kiongozi wetu tulifanya makubwa sana ni wakati wetu wa kumpigania aweze kurudi kazini, ni mwanamke ndiyo lakini uwezo wake hapa sisi wote hatuna kwenye upande wa akili na sasa nguvu hazina msaada mkubwa zaidi ya akili ndizo ambazo zinahitajika zaidi”
“Upo sahihi Tigana, nadhani hilo linatakiwa kufika ofisini mara moja wakati huu”
“Lakini binafsi kuna jambo limenishangaza, kama amebeba kitambulisho maana yake ni kwamba hatujui ila ametuhisi ndiyo maana amekibeba ili akapate uhakika” Bariki aliongea jambo hili akiwa anamaanisha kabisa
“So, una shauri nini?”
“Kwa sasa turudi ofisini, tukae na kuandaa huu mpango upya kwa kuunganisha matukio yote ambayo tumeyapata huko tulikokuwa kufanya kazi hii halafu Malkia wetu arudishwe tuingie kazini mpaka huyu mtu apatikane na naahidi kwamba nitamtia mkononi na siku ambayo nitakutana naye nina imani atajuta” Bariki aliongea jambo la maana na kujisifia
“Bariki chunga ulimi wako ndugu yangu” Bariki hakumjibu Mrisho zaidi ya kuondoka hilo eneo kwani hawakuwa na jambo lingine la kufanya baada ya kumkosa mtu wao aliyekuwa amewapelekea hapo.
Sehemu ya thelathini na tano inafika tamati hapa.
FEBIANI BABUYA.
Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
Shukrani mkuuKongole kwa mwandishi
SaluteSTORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
********************
SEHEMU YA THELATHINI NA TISA
SONGA NAYO................
“Kwa hili vijana wanatakiwa kuingia kazini kwa masaa ishirini na manne kwa hali yoyote ile”
“Mr Savato”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Hivi yule mwanamama bado yupo hai?”
“Yupi?”
“Auleria”
“Nahisi bado ni mzima mheshimiwa, kwanini?”
“Kuna kipindi aliwahi kutoa tamko baya kumhusu mke wangu kupitia watu kadhaa nadhani unakumbuka hilo, kama yupo hai huenda kuna muunganiko wa yeye na hili labda?”
“Sidhani, ni mwanamke ambaye alishajikatia tamaa ya maisha tayari sasa inawezekana vipi afanye jambo kama hili?”
“Kumbuka yule amewahi kuwa kanali wa jeshi, ana nyenzo na ana uwezo wa kuwatafuta watu ambao wanaweza kuifanya kazi hii kwa niaba yake?”
“Mheshimiwa unahisi kuna sababu gani ya msingi ya kumfanya yeye afanye yote haya?”
“Hiyo sababu ndiyo ambayo mimi binafsi nahitaji kuifahamu kutoka kwake. Nataka kukutana na Aurelia”
“Hili sio wazo zuri mheshimiwa, kumbuka yule mama anaishi mtaani kule na huwezi kwenda ile sehemi kienyeji tu hivi”
“Hivi unajisikia unacho kiongea wewe? Tunazungumzia maisha ya mke wangu ambayo hayapo tena halafu bado unataka kuniaminisha kwamba natakiwa kutulia? Mr Savato hili jambo haliwezekani abadani”
“Nimekuelewa mkuu, unahitaji kitu gani?”
“Nahitaji Luca Gavin apatikane akiwa hai kwa sasa, kama imeshindikana kufa basi namtaka akiwa hai kabisa, nina mazungumzo naye marefu na maswali ambayo anapaswa kunijibu. Tumia mali yoyote, tumia rasilimali yoyote ile ila hakikisha huyu mtu anapatikana kwa sababu nahitaji kuja kumuua mwenyewe kwa mkono wangu”
“Sawa mheshimiwa” hakuwa na ubavu wa kumzuia tena, muda huo huo msafara uliandaliwa huku juu kukiwa na helikopta za kutosha za jeshi kudumisha ulinzi, mji ulikuwa umechafuka na kutapakaa ulinzi kila mahali huku msako mkali ukiwa unaendelea kila kona kuanzia kwenye lile jengo ambalo ndiko alikuwepo Sarah kuhakikisha muuaji wa mke wa raisi anapatikana mara moja.
Msafara wa raisi ulienda kuishia YOMBO VITUKA, eneo amblo ni uswahilini kabisa na maisha ambayo yanapatikana huko ni yale maisha ya chini. Huko hata ukiwa na miatano una uhakika wa kushiba, hukosi mihogo ya kutosha ukipata na maji basi siku yako inaisha safi kabisa. Msafara huo uligotea nje ya jumba la mwanamama Aurelia huko mtaani wengi wakimjua kama Bi Aisha. Lilikuwa ni jambo la kushangaza kwa watu wengi kuona raisi tena siku hiyo hiyo ambayo mkewe alikuwa ameuawa akiingia ndani ya eneo hilo tena kwa mwanamke ambaye muda mfupi alitoka kuwashangaza wananchi kwa kuwaonyesha kwamba yeye hakuwa kichaa bali alikuwa na akili zake timamu kabisa.
Nje ya jumba hilo walikutana na mlinzi mmoja tu akiwa na gobole mkononi ambaye hakuwaletea upinzani wowote ule, baada ya kuingia ndani ya jumba hilo walikutana na bwawa dogo la kuogelea ambalo lilikuwa kwenye hali ya usafi, mama huyo majira hayo ya jioni alikuwa ameketi pembezoni akiwa anapata kahawa bila wasiwasi hata ule ujio wa raisi haukumshtua kabisa wala kumpa papara aliendelea kunywa kahawa yake. Jambo hilo raisi alilihesabia kama dharau ila aliamua kuwa mtulivu kutaka kujua kitu kilichokuwa kinampa mwanamama huyo jeuri ya kutojali uwepo wa mtu mkubwa kama huyo kwenye taifa nyumbani kwake.
“Ni muda kidogo sijapokea taarifa zako ila mara ya mwisho nilipata habari kwamba una matatizo ya akili kiasi kwamba unazurura mtaani kama kichaa ila nimeshangaza baada ya kugundua kwamba wewe ni mzima wa afanya kabisa na hauonekani kama ni mtu mwenye shida hiyo ambayo wanadai kwamba unayo” raisi aliongea kwa hasira japo alijaribu kulizuia hilo hadharani mkuu wa majeshi akiwa pembeni yake. Raisi alimpa ishara kiongozi huyo wa jeshi awapishe kwani alikuwa na mazungumzo ya siri na mwanamama huyo.
“Nasikia mkeo amekufa alasiri ya leo, nasikitika kwa hilo lakini nikupe pole sana mheshimiwa”
“Unasikitika mke wangu kufa?”
“Ndiyo, ni mke wa raisi wa taifa langu ulitegemea nitafurahia kifo chake?”
“Kama ni wewe umeratibu hili basi lazima ufurahie” mheshimiwa alisogea kwenye kiti cha karibu akaketi alipokuwepo mwanamama huyo.
“Unahisi mimi hapa ambaye kwa sasa sina ramani yoyote ndiye ambaye naweza kuwaza huo ujinga wa kumuua mke wa raisi?”
“Huwa sipendi kuingilia ugomvi wa wanawake ila ni muda najua kwamba wewe na mke wangu hamkuwahi kuwa sawa, sijajua kuhusu historia yenu ya nyuma kwani hata mke wangu hakutaka kuniambia lolote kuhusu wewe ila inaonekana kuna mambo yenu binafsi hayakuwa sawa kwahiyo unaweza kunipa sababu ya msingi ya kunifanya nisiamini kama ni wewe ndiye umehusika kwenye hili?”
“Sina sababu ya kufanya hayo yote George”
“Unaonekana hata hauniheshimu kabisa kama raisi wa taifa hili!”
“Tangu siku ambayo nilijua kwamba wewe ni kibaraka tu ndiyo siku ambayo nilikufuta kama mtu ambaye unastahili heshima”
“Nakujua wewe Aurelia, wewe sio yule ambaye umekuwa unawaigizia watu kuwa kichaa, uliwahi kuwa kanali wa jeshi ila ghafla tu ukaja kuacha halafu baadae nikaja kusikia kwamba wewe ndiye mlezi wa Gavin habari ambazo zimekuwa zikikanushwa vikali sana. Hii ndiyo sababu una kiburi sana hata unapo niona mimi?”
“Mhhhhh mheshimiwa kwanini usiendelee kuwaongoza hao watanzania ambao wengi akili zao ni za kushikiwa? Raia hawana hata uwezo wa kuhoji, hawajui taifa lao linapelekwa wapi wapo wapo tu. Niliamua kukaa mbali na maisha hayo ambayo unayasema wewe lakini kwa sasa nimeamua kupumzika tu huku kama umekuja kuniua basi unaweza ukafanya hivyo na kuondoka kwa sababu naona kama unanipigia makelele tu hapa kwa kutafutiza sababu zisizo na msingi wowote ule” raisi alibaki anamwangalia mwanamke huyo ambaye yeye binafsi hakuwa anamuelewa vizuri.
“Kwahiyo ni kweli kwamba wewe ndiye mlezi wa Gavin?”
“Ndiyo George, yule mtoto nimemlea mimi hapa. Una tatizo juu ya hilo?”
“Naona kabisa mazungumzo yetu yanaenda kuwa marefu zaidi ya nilivyokuwa nafikiria mwanzo. Nilitaka siku moja kukutana na mlezi wake ili niyajue maisha yake yalikuwaje mpaka anajihisi kwamba anaweza kufanya kila anacho kitaka yeye? Leo nina uhakika nitayapat majibu sahihi”
“Au utafanya nini George?”
“Unajua kabisa siwezi kukuacha hai bila kupata kile ninakihitaji kwako”
“Wewe hapo ndo unataka kuniua mimi?”
“Aurelia hivi unaona kama ni maigizo sio?”
“Nisikilize George, wewe hapo Ikulu hauna lolote ambalo ni lako, kuna watu wamekuweka ili kufanikisha mambo yao na wote tunajua hilo. Kama unataka kuyajua majibu sahihi kwanini usiwaulize ambao wamekuweka hapo halafu usije siku nyingine tena nyumbani kwangu ukaanza kunitishia kuhusu kifo wewe ndiye utakuja kufa bila kujali kama ni raisi au vipi” mwanamama huyo alikuwa akijiamini mno, raisi alitoa bastola yake na kumuwekea mama huyo lakini jambo la kushangaza ni kwamba kuna mwanaume mmoja alitokea kwenye paa la nyumba hiyo na kumnyooshea raisi bastola kichwani pia hali ambayo ilipelekea walinzi wote kumnyooshea bastola mwanaume huyo pia.
“Aurelia una uhakika na hili ambalo unalifanya, unajua kijana huyu anahalalisha kuuawa kwako?”
“Mheshimiwa huyo hapo alipo hajali kuhusu kufa kwake lakini kama kuna kijana wako hata mmoja atampiga risasi tambua tu kwamba hakuna mtu hata mmoja kati yenu ambaye anaweza kutoka akiwa hai humu ndani. Wenzako wanaelewa ndiyo maana huwa wanakuja kistaarabu sio kwa sababu wewe ni raisi wa taifa basi unaweza kufanya lolote na kwa mtu yeyote yule hivyo kama hauna mazungumzo na mimi unaweza kwenda” alikuwa anazungumza na raisi wa nchi mithili ya mtu ambaye alikuwa anaongea na kibaka wa mtaani tu mwanamama huyo, raisi alibaki anacheka kwa ghadhabu lakini alimuona mkuu wa majeshi akimuonyesha ishara ya kukataa huenda yeye kuna mambo alikuwa anayajua kuhusu sehemu hiyo ndiyo maana alimpa ishara ya kutofanya kosa lolote.
“Nilijua tu kuna kitu hakipo sawa kuhusu wewe, nilijua tu lazima kuna mkono wako kwenye hili Aurelia. Naenda kufanya uchunguzi kwa sababu kama nitagundua kuna uhusika wako kwenye hili lazima ufe kwa mkono wangu”
“Jitahidi kuwa makini sana mheshimiwa raisi kwa sababu hasira siku zote huwa ni mtaji mbaya na wa hovyo wa watu wajinga na siku nyingine unapo enda kwenye nyumba za watu jitahidi kuwa mstaarabu na mkarimu ili wakupokee vizuri” alitoa elimu kwa raisi mwanamama huyo na kubeba kikombe chake kuelekea ndani, yaani mwananchi wa kawaida alikuwa anampa mgongo raisi kabla hajanyanyuka. Ile aibu na dharau ambayo aliipata kwa walinzi wake kutokana na tukio lile aliiihifadhi moyoni, asingeweza kuiacha iende hivi hivi. Alimuita mlinzi wake na kumpa maagizo ya siri kisha akahitaji waondoke eneo hilo huku akitoa maagizo ya kufanyika kwa maandalizi makubwa mno kwa ajili ya kumpumzisha mkewe kipenzi kwa heshima kubwa ili taifa lije kumkumbuka mwanamke huyo.
*********
Lile jambo la mchana halikuishia pale, raisi asingeweza kudhalilika namna ile halafu akaacha mambo yakaenda hivi hivi. Aliondoka pale huku akiwa anajua kabisa kama angefanya jambo la hovyo pale lazima kungekuwa na matatizo lakini pia hakuelewa sababu ya mwanamama yule kujiamini sana namna ile kiasi kwamba akadai hakuna mtu hata mmoja angeweza kutoka hai pale kama wangefanya jambo la kipumbavu. Alihisi kwamba huenda mwanamama yule alikuwa na watu wa siri ambao walikuwa wamelizunguka eneo lile hivyo alitakiwa kufanya mambo ambayo hakuna mtu angeweza kumshtukia.
Usiku alituma watu eneo lile, walikuwa ni wanaume maalumu ambao aliamini ila kazi lazima waifanye kwa usahihi. Alituma kikosi cha watu kumi wakiwa wanaongozwa na mlinzi wake kwa sababu alikuwa akimuamini mno, alihitaji watu hao waue kila ambaye wangemkuta kule lakini alikuwa akimtaka mwanamama yule akiwa hai na mzima wa afya kabisa kwa sababu kuna mengi ambayo alikuwa anataka kuyasikia kutoka kwake ndiyo maana amri yake ilikuwa ni kwamba mwanamama yule apelekwe kwake akiwa hai.
39 inafika mwisho.
FEBIANI BABUYA.
Amina kiongoziHakika umetubless,Mungu akubariki mkali wa hizi kazi.🙏