STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
********************
SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA
SONGA NAYO................
Ilikuwa imebakia hatua ndogo sana kufanikiwa kumdondosha kabisa Lucas pale alipokuwepo lakini ilishindikana baada ya jambo kubwa kuukumba Ulimwengu. Dunia iliingia kwenye vita baridi, vita vikaathiri uchumi kuanzia soko la dunia na kila sehemu, hali ikaanza kuwa mbaya na miongoni mwa nchi ambazo ziliathirika sana ilikuwa ni Tanzania kwa sababu inategemea zaidi kuagiza kuliko kutoa vitu vyake nje. Vitu vilikuwa ghali sana kuvipata, ikapelekea benki ya nchi kuanguka vibaya, hali ikawa ngumu, wananchi wakaanza kulalamika kila upande wa nchi, ni matajiri tu ambao walikuwa wana uwezo wa kuzimudu gharama za maisha.
Vilio vilitanda kila kona, kila mtaa, kila wilaya na kila mkoa, watu walimlilia raisi aweze kuwasaidia, hakuwa na huo uwezo wa kuwasaidia mamilioni ya watu wakati hata akiba ya benki kuu ilikuwa ya kusua sua. Licha ya kubana matumizi lakini bado haikutosha kuifanya hali iwe kawaida kama mwanzo, sasa nchi ikawa inaingia kwenye njaa kali mno na hali mbaya, hakuna aliyejali kuhusu mipango miji tena. Watu walijisaidia popote pale, takataka zingezagaa kila sehemu, watu wakaanza kuuana kugombania mikate na kazi, wababe ndio ambao walikuwa na nafasi ya kuweza kuwa na uhakika wa kujaza matumbo yao kwa wanyonge ikawa ni tatizo jipya.
Wananchi wakawa hawaelewi ni nani angewapa msaada na huko kwenye soko la dunia vitu vikawa vinazidi kupanda kila kuitwapo leo, hata zile nchi ambazo zilikuwa zinategemewa kwamba ni watoa misaada wakuu kwa Tanzania zikapotea. Ni kama nao walikuwa wanapambana na hali zao ama waliamua kuaacha watanzania wapate somo la kujitegemea, wasitegemee misaada kila siku na kutia tia huruma, wajifunze namna ya kuishi wakiwa wenyewe. Raisi angefanya nini na yeye ndiye ambaye alikuwa anategemewa kutatua tatizo? Hakuna na njia nyingine zaidi ya njia moja ambayo kwake ilikuwa ni ngumu kuipita.
Alitakiwa kwenda kuomba msaada kwa Lucas aweze kulisaidia taifa, kwake ilikuwa ni ngumu kwa sababu alikuwa na kisasi naye moyoni, ni yeye ambaye alikuwa anataka kumpoteza mwanaume huyo lakini kwa wakati huo ni Lucas ambaye alikuwa ameshika kisu chenye makali. Hakuwa na namna ya kufanya, misaada yote ya nje ilikatwa na hakuna kiongozi wa taifa kubwa hata mmoja ambaye alikuwa anapokea simu zake ndipo akakubali yaishe, akaamua kwenda kumuomba msaada Lucas aweze kumsaidia. Wakati haya yanafanyika wewe ulikuwa mpuuzi tu mmoja Medrick na sina uhakika kama ulikuwa umeanza hata mazoezi yako ya kwanza.
Ilikuwa ni aibu lakini pia ndiyo ilikuwa njia pekee ya yeye kama raisi kuweza kuwajibika kulisaidia taifa lake, vyombo vya habari vilihitajika ikiwa ni kama takwa la Lucas, kwa sababu raisi huyo aliwahi kumuonyeshea kiburi na dharau alimtaka apige magoti na kuomba msaada mbele ya watanzania wote wamuone. Haikuwa kwa sababu ya kiburi tu lakini hao wawili walikuwa na mambo yao binafsi kumbuka kwamba raisi huyo alikuwa anapambana sana kuweza kumpoteza kabisa Lucas hivyo hata yeye alipopata nafasi ya kumnyoosha, alitaka kumuonyesha ni nani bosi wa kweli kati yao.
Raisi huyo alipiga magoti mbele ya vyombo vya habari akiomba msaada kwa Lucas tena alilazimika kusafiri mpaka kule Lucas Villa. Jambo hilo lilimpatia kisasi kizito mno kwenye moyo wake, raisi kupigishwa magoti na mwananchi ambaye hata hata nafasi yoyote ile? Kwake ilikuwa ni moja kati ya jambo la aibu kuwahi kumkuta lakini hata hivyo ilisaidia pakubwa kwa sababu Lucas alikubali kutoa pesa za kimarekani dola bilioni kumi kwa ajili ya kuingizwa kwenye bajeti ya taifa kuanza kuandaa mazingira ya kuwasaidia wananchi kwa muda mrefu.
Hakuishia hapo tu lakini pia ili aingize pesa hizo kwenye akaunti ya benki alimtaka raisi huyo aweze kujiuzulu kwenye nafasi yake, yalikuwa ni maamuzi magumu lakini ilikuwa ni lazima yafanyike kwa ajili ya usalama wa taifa zima. Hadharani kwenye vyombo vya habari raisi wa nchi alitangaza kuweza kujiuzulu nafasi yake tena kwa aibu ya kumpigia magoti mtu. Baada ya pale ndipo pesa ilidhinishwa na kwenda kuleta mabadiliko makubwa ndani ya taifa kwa ujumla.
Natron Vinza baada ya kukumbana na ile aibu kubwa alishindwa kuishi mbele ya macho ya watu, alipotea kabisa kwenye masikio ya watu na baada ya miezi sita kupita bwana yule alidaiwa kwamba alikutwa amekufa kwa kujiua mwenyewe baada ya kuzidisha madawa ya kuongeza nguvu kwenye mwili wake. Ile hadithi mbaya ikawa imeishia pale baada ya kifo chake lakini sio kweli kwamba hadithi ile iliishia pale bali ule ulikuwa ni mwanzo wa hadithi mpya ya kutisha" maelezo ya mzee Hasheem ya muda mrefu yalimchanganya Medrick Savato ambaye alikuwa makini muda wote kusikiliza kwa usahihi kabisa. Ulikuwa ni muda mrefu kidogo tangu akae hapo kuweza kusimuliwa historia nzima ya maisha ya Gavin Luca ila kwa wakati huo aliona kabisa kwamba kulikuwa na haja kubwa ya kuweza kuuliza.
"Mzee wangu umeniacha kidogo hapo, umesema kwamba aliyekuwa raisi wa wakati alikufa kitu ambacho ni sahihi kabisa kwa sababu ilikuwa ni taarifa kubwa kwa taifa zima ila unapo sema kwamba ule ulikuwa ni mwanzo ya hadithi ya kutisha unamaanisha nini?" mzee Hasheem alitabasamu akiwa anamwangalia mkuu wa majeshi ambaye bila shaka alikuwa amenogewa na simulizi ile.
"Kijana wangu dunia yetu ina kila aina ya viumbe, kuna vile ambavyo vinaishi kama ambavyo maisha yanataka viishi na kuna vile ambavyo vinaipinga asili yaani hivi vinaishi kutokana na sheria zao vyenyewe. Isingekuwa bahati mbaya mtu alikuwa raisi halafu kirahisi tu ajiue kwa vidonge wakati ana uhasama na mtu, wewe unaona hilo linakuingia akilini kweli?" swali la mzee huyo lilimuacha mkuu wa majeshi akiwa ametumbua macho, kiuhalisia hakuelewa hapo angeongeza kitu gani.
"Hapana bwana, yule bwana hakufa kama ambavyo aliuaminisha uma bali alimuua mtu mwingine akamfanyia plastic surgery akamuweka kwenye nafasi yake hivyo yule mtu ambaye alikufa hakuwa yeye"
"Unamaanisha nini mzee?"
"Mpaka hii leo Natron Vinza ni mzima"
"Whaaaaaat?"
"Yeah ni mzima na ndiye bosi wako wewe hapo"
"Bila shaka mzee umeshaanza kuchoka"
"Kijana wangu tatizo mnaendeshwa na mihemko akili zenu mnazitumia kukaangia mayai tu na kuwavimbia watu mtaani, watu kama wewe wanatumika kwenye maeneo mengi sana na watu wenye akili kwa sababu anajua wewe unapenda maujiko anakupa nafasi ili uweze kutekeleza mambo yake kisha akaiona huna faida anakuua. Nina uhakika wewe mwenyewe unajua kabisa kwamba una uwezo mdogo mno haukutakiwa kuwa hata kwenye hiyo nafasi ambayo upo ndiyo maana licha ya upuuzi wako wote bado raisi huwa anakulinda. Unaijua sababu ya msingi ya wewe kuwekwa hapo?" Medrick alibaki ametumbua macho asielewe kile embacho kilikuwa kinaendelea ni kama alikuwa ndotoni halafu mtu akamuamusha ghafla na kumtaka aelezee jambo fulani kwa ufasaha, asingeweza kufanya hivyo bila akili yake kutulia kwanza.
"Unamaanisha Natron Vinza bado anaishi?"
"Yeah ni mzima wa afya kabisa"
"Unaweza ukanieleza sehemu ya kumpatia tafadhali?"
"Hilo sio jukumu langu, mtu ambaye amekupa taarifa za wewe kunipata mimi huku ndiye unapaswa kwenda kumuuliza atakujibu kila kitu kwa sababu anajua mambo yote haya" bwana Savato alibaki anacheka kwa hasira na uchungu mkubwa. Taarifa ambazo alikuwa nazo juu ya hiyo kazi alijiona kwamba anazo nyingi sana ila baadae aligundua kwamba hakuwa na taarifa zozote za mhimu ambazo alikuwa anazijua, sasa kwanini afichwe miaka yote hiyo huku akiwa ni mmoja wa watu ambao waliwafanyia watu hao kazi kwa moyo mmoja? Hakuwa na jibu, alijiona kama takataka asiye na thamani mkuu wa majeshi.
"Unaweza ukaniambia kuhusu maisha ya Lucas na mkewe mjamzito baada ya pale?"
"Mhhhhhh una haraka sana CDF, wakati haya mambo yanatokea ya raisi kuigiza kifo chake mwenyewe tayari mke wa Lucas alikuwa amejifungua. Hapa ndipo kuna siri kubwa ambayo iliuchanganya ulimwengu mzima na ni watu wachache ambao tulikuwa na taarifa hizi, Glady alijifungua watoto wawili wa kiume mapacha ila ambaye ulimwengu ulikuja kumjua ni mmoja tu pekee mmoja hakuwahi kujulikana na hapa ndipo inaanzia historia ya maisha ya hicho kiumbe ambacho wewe uliamini kwamba umekiua"
"Unamaanisha miongoni mwa hao watoto wawili mmoja wao ndiye Gavin Luca?"
"Siwezi kukujibu hilo swali Medrick"
"Mzee wangu sipo hapa kwa ajili ya kukubembeleza" Medrick aliongea kwa hasira huku akiwa anaitoa bastola yake, alifika sehemu ambayo binafsi alikuwa anahitaji zaidi kupata taarifa zake, ilikuwa ndiyo sehemu sahihi ya kuanza kumtambua Gavin Luca.
"Weka bastola pembeni, mimi ndiye mtu pekee ambaye naweza kukupatia taarifa ambazo unazihitaji hivyo unanihitaji zaidi nikiwa mzima wa afya na sina tatizo lolote lile. Natambua ahadi yako ni ya uongo kusema kwamba utaniua mimi pekee na wafungwa wengine utawaacha hivyo ninacho kitaka mimi nahitaji kutoka hapa nikiwa hai, nahitaji kuonana na Gavin Luca kabla sijafa hivyo ua wengine kisha utoke na mimi nikiwa mzima na unipeleke sehemu nzuri nikaishi kwa raha" maada ilibadilika kabisa kutoka kwenye kinywa cha mzee huyo kiasi kwamba hata Medrick mwenyewe alibaki ameduwaa kama haamini kile ambacho kilikuwa kinatokea ndani ya eneo hilo. Aliishia kucheka kwa hasira.
Ishirini na sita inafika mwisho.
FEBIANI BABUYA.
Sent from my SM-A107F using
JamiiForums mobile app