STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
********************
SEHEMU YA THELATHINI NA TISA
SONGA NAYO................
“Kwa hili vijana wanatakiwa kuingia kazini kwa masaa ishirini na manne kwa hali yoyote ile”
“Mr Savato”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Hivi yule mwanamama bado yupo hai?”
“Yupi?”
“Auleria”
“Nahisi bado ni mzima mheshimiwa, kwanini?”
“Kuna kipindi aliwahi kutoa tamko baya kumhusu mke wangu kupitia watu kadhaa nadhani unakumbuka hilo, kama yupo hai huenda kuna muunganiko wa yeye na hili labda?”
“Sidhani, ni mwanamke ambaye alishajikatia tamaa ya maisha tayari sasa inawezekana vipi afanye jambo kama hili?”
“Kumbuka yule amewahi kuwa kanali wa jeshi, ana nyenzo na ana uwezo wa kuwatafuta watu ambao wanaweza kuifanya kazi hii kwa niaba yake?”
“Mheshimiwa unahisi kuna sababu gani ya msingi ya kumfanya yeye afanye yote haya?”
“Hiyo sababu ndiyo ambayo mimi binafsi nahitaji kuifahamu kutoka kwake. Nataka kukutana na Aurelia”
“Hili sio wazo zuri mheshimiwa, kumbuka yule mama anaishi mtaani kule na huwezi kwenda ile sehemi kienyeji tu hivi”
“Hivi unajisikia unacho kiongea wewe? Tunazungumzia maisha ya mke wangu ambayo hayapo tena halafu bado unataka kuniaminisha kwamba natakiwa kutulia? Mr Savato hili jambo haliwezekani abadani”
“Nimekuelewa mkuu, unahitaji kitu gani?”
“Nahitaji Luca Gavin apatikane akiwa hai kwa sasa, kama imeshindikana kufa basi namtaka akiwa hai kabisa, nina mazungumzo naye marefu na maswali ambayo anapaswa kunijibu. Tumia mali yoyote, tumia rasilimali yoyote ile ila hakikisha huyu mtu anapatikana kwa sababu nahitaji kuja kumuua mwenyewe kwa mkono wangu”
“Sawa mheshimiwa” hakuwa na ubavu wa kumzuia tena, muda huo huo msafara uliandaliwa huku juu kukiwa na helikopta za kutosha za jeshi kudumisha ulinzi, mji ulikuwa umechafuka na kutapakaa ulinzi kila mahali huku msako mkali ukiwa unaendelea kila kona kuanzia kwenye lile jengo ambalo ndiko alikuwepo Sarah kuhakikisha muuaji wa mke wa raisi anapatikana mara moja.
Msafara wa raisi ulienda kuishia YOMBO VITUKA, eneo amblo ni uswahilini kabisa na maisha ambayo yanapatikana huko ni yale maisha ya chini. Huko hata ukiwa na miatano una uhakika wa kushiba, hukosi mihogo ya kutosha ukipata na maji basi siku yako inaisha safi kabisa. Msafara huo uligotea nje ya jumba la mwanamama Aurelia huko mtaani wengi wakimjua kama Bi Aisha. Lilikuwa ni jambo la kushangaza kwa watu wengi kuona raisi tena siku hiyo hiyo ambayo mkewe alikuwa ameuawa akiingia ndani ya eneo hilo tena kwa mwanamke ambaye muda mfupi alitoka kuwashangaza wananchi kwa kuwaonyesha kwamba yeye hakuwa kichaa bali alikuwa na akili zake timamu kabisa.
Nje ya jumba hilo walikutana na mlinzi mmoja tu akiwa na gobole mkononi ambaye hakuwaletea upinzani wowote ule, baada ya kuingia ndani ya jumba hilo walikutana na bwawa dogo la kuogelea ambalo lilikuwa kwenye hali ya usafi, mama huyo majira hayo ya jioni alikuwa ameketi pembezoni akiwa anapata kahawa bila wasiwasi hata ule ujio wa raisi haukumshtua kabisa wala kumpa papara aliendelea kunywa kahawa yake. Jambo hilo raisi alilihesabia kama dharau ila aliamua kuwa mtulivu kutaka kujua kitu kilichokuwa kinampa mwanamama huyo jeuri ya kutojali uwepo wa mtu mkubwa kama huyo kwenye taifa nyumbani kwake.
“Ni muda kidogo sijapokea taarifa zako ila mara ya mwisho nilipata habari kwamba una matatizo ya akili kiasi kwamba unazurura mtaani kama kichaa ila nimeshangaza baada ya kugundua kwamba wewe ni mzima wa afanya kabisa na hauonekani kama ni mtu mwenye shida hiyo ambayo wanadai kwamba unayo” raisi aliongea kwa hasira japo alijaribu kulizuia hilo hadharani mkuu wa majeshi akiwa pembeni yake. Raisi alimpa ishara kiongozi huyo wa jeshi awapishe kwani alikuwa na mazungumzo ya siri na mwanamama huyo.
“Nasikia mkeo amekufa alasiri ya leo, nasikitika kwa hilo lakini nikupe pole sana mheshimiwa”
“Unasikitika mke wangu kufa?”
“Ndiyo, ni mke wa raisi wa taifa langu ulitegemea nitafurahia kifo chake?”
“Kama ni wewe umeratibu hili basi lazima ufurahie” mheshimiwa alisogea kwenye kiti cha karibu akaketi alipokuwepo mwanamama huyo.
“Unahisi mimi hapa ambaye kwa sasa sina ramani yoyote ndiye ambaye naweza kuwaza huo ujinga wa kumuua mke wa raisi?”
“Huwa sipendi kuingilia ugomvi wa wanawake ila ni muda najua kwamba wewe na mke wangu hamkuwahi kuwa sawa, sijajua kuhusu historia yenu ya nyuma kwani hata mke wangu hakutaka kuniambia lolote kuhusu wewe ila inaonekana kuna mambo yenu binafsi hayakuwa sawa kwahiyo unaweza kunipa sababu ya msingi ya kunifanya nisiamini kama ni wewe ndiye umehusika kwenye hili?”
“Sina sababu ya kufanya hayo yote George”
“Unaonekana hata hauniheshimu kabisa kama raisi wa taifa hili!”
“Tangu siku ambayo nilijua kwamba wewe ni kibaraka tu ndiyo siku ambayo nilikufuta kama mtu ambaye unastahili heshima”
“Nakujua wewe Aurelia, wewe sio yule ambaye umekuwa unawaigizia watu kuwa kichaa, uliwahi kuwa kanali wa jeshi ila ghafla tu ukaja kuacha halafu baadae nikaja kusikia kwamba wewe ndiye mlezi wa Gavin habari ambazo zimekuwa zikikanushwa vikali sana. Hii ndiyo sababu una kiburi sana hata unapo niona mimi?”
“Mhhhhh mheshimiwa kwanini usiendelee kuwaongoza hao watanzania ambao wengi akili zao ni za kushikiwa? Raia hawana hata uwezo wa kuhoji, hawajui taifa lao linapelekwa wapi wapo wapo tu. Niliamua kukaa mbali na maisha hayo ambayo unayasema wewe lakini kwa sasa nimeamua kupumzika tu huku kama umekuja kuniua basi unaweza ukafanya hivyo na kuondoka kwa sababu naona kama unanipigia makelele tu hapa kwa kutafutiza sababu zisizo na msingi wowote ule” raisi alibaki anamwangalia mwanamke huyo ambaye yeye binafsi hakuwa anamuelewa vizuri.
“Kwahiyo ni kweli kwamba wewe ndiye mlezi wa Gavin?”
“Ndiyo George, yule mtoto nimemlea mimi hapa. Una tatizo juu ya hilo?”
“Naona kabisa mazungumzo yetu yanaenda kuwa marefu zaidi ya nilivyokuwa nafikiria mwanzo. Nilitaka siku moja kukutana na mlezi wake ili niyajue maisha yake yalikuwaje mpaka anajihisi kwamba anaweza kufanya kila anacho kitaka yeye? Leo nina uhakika nitayapat majibu sahihi”
“Au utafanya nini George?”
“Unajua kabisa siwezi kukuacha hai bila kupata kile ninakihitaji kwako”
“Wewe hapo ndo unataka kuniua mimi?”
“Aurelia hivi unaona kama ni maigizo sio?”
“Nisikilize George, wewe hapo Ikulu hauna lolote ambalo ni lako, kuna watu wamekuweka ili kufanikisha mambo yao na wote tunajua hilo. Kama unataka kuyajua majibu sahihi kwanini usiwaulize ambao wamekuweka hapo halafu usije siku nyingine tena nyumbani kwangu ukaanza kunitishia kuhusu kifo wewe ndiye utakuja kufa bila kujali kama ni raisi au vipi” mwanamama huyo alikuwa akijiamini mno, raisi alitoa bastola yake na kumuwekea mama huyo lakini jambo la kushangaza ni kwamba kuna mwanaume mmoja alitokea kwenye paa la nyumba hiyo na kumnyooshea raisi bastola kichwani pia hali ambayo ilipelekea walinzi wote kumnyooshea bastola mwanaume huyo pia.
“Aurelia una uhakika na hili ambalo unalifanya, unajua kijana huyu anahalalisha kuuawa kwako?”
“Mheshimiwa huyo hapo alipo hajali kuhusu kufa kwake lakini kama kuna kijana wako hata mmoja atampiga risasi tambua tu kwamba hakuna mtu hata mmoja kati yenu ambaye anaweza kutoka akiwa hai humu ndani. Wenzako wanaelewa ndiyo maana huwa wanakuja kistaarabu sio kwa sababu wewe ni raisi wa taifa basi unaweza kufanya lolote na kwa mtu yeyote yule hivyo kama hauna mazungumzo na mimi unaweza kwenda” alikuwa anazungumza na raisi wa nchi mithili ya mtu ambaye alikuwa anaongea na kibaka wa mtaani tu mwanamama huyo, raisi alibaki anacheka kwa ghadhabu lakini alimuona mkuu wa majeshi akimuonyesha ishara ya kukataa huenda yeye kuna mambo alikuwa anayajua kuhusu sehemu hiyo ndiyo maana alimpa ishara ya kutofanya kosa lolote.
“Nilijua tu kuna kitu hakipo sawa kuhusu wewe, nilijua tu lazima kuna mkono wako kwenye hili Aurelia. Naenda kufanya uchunguzi kwa sababu kama nitagundua kuna uhusika wako kwenye hili lazima ufe kwa mkono wangu”
“Jitahidi kuwa makini sana mheshimiwa raisi kwa sababu hasira siku zote huwa ni mtaji mbaya na wa hovyo wa watu wajinga na siku nyingine unapo enda kwenye nyumba za watu jitahidi kuwa mstaarabu na mkarimu ili wakupokee vizuri” alitoa elimu kwa raisi mwanamama huyo na kubeba kikombe chake kuelekea ndani, yaani mwananchi wa kawaida alikuwa anampa mgongo raisi kabla hajanyanyuka. Ile aibu na dharau ambayo aliipata kwa walinzi wake kutokana na tukio lile aliiihifadhi moyoni, asingeweza kuiacha iende hivi hivi. Alimuita mlinzi wake na kumpa maagizo ya siri kisha akahitaji waondoke eneo hilo huku akitoa maagizo ya kufanyika kwa maandalizi makubwa mno kwa ajili ya kumpumzisha mkewe kipenzi kwa heshima kubwa ili taifa lije kumkumbuka mwanamke huyo.
*********
Lile jambo la mchana halikuishia pale, raisi asingeweza kudhalilika namna ile halafu akaacha mambo yakaenda hivi hivi. Aliondoka pale huku akiwa anajua kabisa kama angefanya jambo la hovyo pale lazima kungekuwa na matatizo lakini pia hakuelewa sababu ya mwanamama yule kujiamini sana namna ile kiasi kwamba akadai hakuna mtu hata mmoja angeweza kutoka hai pale kama wangefanya jambo la kipumbavu. Alihisi kwamba huenda mwanamama yule alikuwa na watu wa siri ambao walikuwa wamelizunguka eneo lile hivyo alitakiwa kufanya mambo ambayo hakuna mtu angeweza kumshtukia.
Usiku alituma watu eneo lile, walikuwa ni wanaume maalumu ambao aliamini ila kazi lazima waifanye kwa usahihi. Alituma kikosi cha watu kumi wakiwa wanaongozwa na mlinzi wake kwa sababu alikuwa akimuamini mno, alihitaji watu hao waue kila ambaye wangemkuta kule lakini alikuwa akimtaka mwanamama yule akiwa hai na mzima wa afya kabisa kwa sababu kuna mengi ambayo alikuwa anataka kuyasikia kutoka kwake ndiyo maana amri yake ilikuwa ni kwamba mwanamama yule apelekwe kwake akiwa hai.
39 inafika mwisho.
FEBIANI BABUYA.