Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA AROBAINI
SONGA NAYO................

Uswahilini mara nyingi watu hawakeshi kwa sababu hawana ubavu wa kutumia usiku kucha. Uswahilini shughuli nyingi huwa zinaisha saa sita au saa saba ya usiku watu wanaenda kulala, hakuna kumbi nyingi za starehe za kuwafanya wakeshe, tatizo ni kipato kidogo. Hivyo usiku kulikuwa na watu wa kuhesabu nao wengi ni wale ambao walikuwa wanatoka kwenye starehe maeneo mengine wakiwa wanarudi lakini pia walikuwepo wachache ambao hawakuwa na makazi kabisa.
Huo ndio ulikuwa wakati mzuri kabisa wa kuvamia ndani ya eneo hilo kwenye nyumba ya mwanamama huyo ambaye alidaiwa kuwa mama wa Gavin Luca. Wanaume kumi walikuwa makini kupiga hatua kadhaa kuelekea kwenye nyumba ya mama huyo lakini walipatwa na mshtuko kwa sababu wakati wanafika hapo walikuta geti lipo wazi kabisa halijafungwa na taa za kwenye hiyo nyumba zilikuwa zimezimwa. Juu kulikuwa na wingu la mvua ambalo liliambatana na ngurumo kadhaa ambazo ziliwafanya watu kulala fofofo hususani kwa wale ambao usiku huwa ni sehemu ya kuzisahau shida zao.

Muda mfupi tu mvua ilianza kushuka ikiwa imeambatana na radi, ilipiga radi moja kali umeme ukawa umekata mtaa mzima kukawa kiza totoro. Kikosi cha hao wanaume kilikuwa kinaongozwa na Hussein Damoga ambaye ndiye alikuwa mlinzi mkuu wa raisi, wanaume hao walizidisha umakini baada ya umeme kukatika na mvua kuanza kushuka. Mvua na giza haikuwa sababu ya wao kuwa na hofu zaidi ila iliwaongezea hofu ila jambo ambalo liliwapa mashaka ni kukuta geti la hiyo nyumba lipo wazi, ilikuwa ni ishara ya wao kusubiriwa kama sio kuingizwa kwenye mtego.

Waliingia mpaka ndani na kutulia huku wakianza kujigawa pande mbili tofauti ili waanze kuizunguka hiyo nyumba. Wakati wanaendelea na mambo yote hayo juu ya paa la hiyo nyumba alikuwa amesimama mtu ambaye alikuwa amevaa kanzu nyeusi na kiatu cheusi chepesi. Alijifunga kitambaa cheusi kichwani pamoja na usoni hakuwa akionekana kabisa sura yake, mikono yake yote miwili ilikuwa nyuma kabisa ya kiuno chake imekutanishwa na katikati ya mikono hiyo kulikuwa na upanga mkali ambao ulikuwa ulikuwa umetolewa kwenye ala yake tayari.
Aliwaona watu hao tangu wakiwa mbali mpaka wanafika hapo ila aliwasubiri waweze kufika wazungumze kwa mapana. Kundi la kwanza ambalo lilipita upande wake lilikuwa na wanaume watano, mwanaume mmoja ambaye alikuwa nyuma alihisi kama kuna kitu kinakuja hewani, wakati anahitaji kugeuka alihisi kuna kitu kinaipapasa shingo yake wakati anajiandaa kupiga makelele, shingo ilitobolewa vibaya wakati huo upanga ulizama kwenye moyo wake na kutolewa. Alikufa akiwa kimya bila kutoa sauti wala mlio wa kuwashtua wenzake ambao waliendelea kutembea kwa tahadhari wakiwa na silaha zao kali.
Wanaume hao walisimama baada ya mtu kupita juu yao kwa sarakasi na kutua mbele, wakati anatua yule wa mbele alikutana na upanga wa shingo, ulitokezea mpaka nyuma ukatolewa, hakuwa na uhai wakawa wamebaki watatu. Hakuna hata mmoja ambaye alipewa hata nafasi ya kuweza kupiga risasi, kasi ambayo alikuwa anaitumia mwanaume huyo ilikuwa inatisha mno, ajijigeuza hewani ambapo alitua pembeni ya mwanaume mmoja kwa mguu wa chembe ya moyo wakati huo aliachia silaha yake na upanga kwenda kwa wale wawili ambao walikuwa wamebaki. Upanga na shilingi vilizama kwenye shingo za wale mabwana wakabaki wanahangaika kuweza kujitoa kwenye hali hiyo, ile shilingi ilikuwa inatumiwa na mwanaume mmoja tu pekee Gavin Luca hivyo bila shaka alikuwa ni mwenyewe kwenye lile eneo.

Alibeba upanga wake na kuzunguka kwa wale wengine ambao walibakia, mwanaume aliyekuwa nyuma kabisa alipiga kelele na kutamka kwamba;
“Tumevamiwa” ila muda ambao alitamka haukuwa rafiki kwake, na bahati nzuri kwao wakati anatamka hilo umeme ulikuwa unarudi hivyo wote walipo geuka walikuwa wanamuona mwanaume huyo akiwa mbele yao. Gavin alikuwa ameibana shingo ya yule mwanaume kiasi kwamba hakuwa na uwezo wa kufurukuta, aliuzungusha upanga kwa mbele na kuupitisha mithili ya mtu ambaye alikuwa anachinja kuku. Alikitoa kitambaa chake usoni ndipo hata Hussein aliogopa na kushtuka, hakutarajia kukutana na bwana huyo hilo eneo.
Hayo wakati yanatokea wanaume wale kwa kushuhudia mwenzao anauawa walianza kumshambulia kwa risasi lakini hazikufua dafu kwa sababu alikuwa anamtumia yule mwenzao kama ngao
“Stop, huyu tunamhitaji akiwa hai” aliongea Hussein kwa sauti ya mamlaka ila wakati hilo linafanyika Gavin aliutupa ule mwili wa mwenzao kuelekea kule walipo. Hawakuwa tayari kuacha mwili wa mwenzao udondoke kabisa chini hivyo walifanya jitihada za kuweza kuudaka, mmoja alisikika akitoa sauti ya kilio, upanga ulikuwa umepenya kwenye tumbo lake na bwana yule alikuwa anakuja kama mizimu ikawalazimu kuutupa mwili wa mwenzeo na kumkwepa. Alichelewa mmoja ambaye aliguswa kwenye mguu wake, hakutararajia hivyo akarushwa vibaya, alifuatwa akiwa hewani na kushindiliwa ngumi za kifuani mpaka anafika chini kifua kilikuwa kimepasuka akiwa anavuja damu hovyo.
Mmoja ambaye alikuwa vyema hakusikia alihitaji kupiga risasi mpaka pale aliposhtuka anaipiga risasi shilingi ambayo ilikuwa inakuja kwake kwa kasi kubwa kiasi kwamba ikaachia cheche ambazo zilimuumiza macho akalazimika kuyafumba, alipokuja kuyafumbua alikuwa anatazamana na Gavin mbele yake uso kwa uso ambaye alizamisha vidole vyake kwenye macho yake na kuyanyofoa, alitoa kisu kidogo kwenye kiuno chake na kukizamisha kwenye kichwa cha yule bwana hadithi yake ikawa inaishia hapo. Gavin alirudi taratibu kwa yule ambaye alikuwa anajinyonga kwa sababu upanga ulikuwa umeingia kwenye tumbo lake, alipigiza mguu wake kwenye kichwa cha yule mwanaume ambacho kilipasuka vibaya na kumfanya Hussein kuyafumba macho. Gavin alinyanyuka akiwa anauchomoa upanga wake bila wasiwasi na kumgeukia Hussein.

“Sina imani kama kulikuwa na ulazima wa mimi na wewe kukutana kwenye maisha yetu yote ila mmelazimisha nifanye hivi siku ya leo. Kuna muda najisikia vibaya kuua hawa viumbe dhaifu bila sababu maalumu ila nahisi ni njia rahisi zaidi ya baadhi ya watu kunielewa. Nenda kwa huyo kiongozi wako mwambie kama akija kuthubutu tena kwenye maisha yake yote kuja karibu na huyu mwanamke basi ndiyo itakuwa siku yake ya mwisho kukaa Ikulu. Kuna jambo anajaribu kulificha kwangu basi nitalijua muda mfupi ujao ila mpe onyo, hatakiwi kuja karibu na huyu mwanamke kwenye maisha yake yote mpaka siku anakufa” ilikuwa ni sauti nzito ya Gavin Luca mwenyewe kwenda kwa Hussein ambaye alikuwa na silaha yake mkononi ila hakuw ana la kufanya.
“Siwezi kukuacha uende Gavin, ni lazima ukutane na raisi umwambie hayo maneno mwenyewe”
“Kama kutakuwa na ulazima wa mimi kukutana naye basi hana haja ya kunitafuta kwa sababu nitamtafuta kwa muda wangu”
“Huwezi kukutana na raisi kwa wakati ambao unataka na kwa namna ambayo unaitaka wewe, yule sio mhuni wa mtaani, yule ni raisi wa hili taifa. Umeua hawa vijana mbele yangu halafu kirahisi tu unafikiri nitakuacha uende?”
“Unamaanisha kwamba wewe hapo ndo unataka kunizuia mimi?”

“Hakuna mahali unaenda Luca na kama sio kuhitajika kuwa hai basi ningekuua mwenyewe leo hii” Hussein aliirusha silaha yake kuelekea mahali ambapo alikuwepo Gavin huku akiwa anakuja kwa hatua zake nzito ambazo zilisindikizwa na matone mengi ya mvua. Gavin aliurusha upanga wake juu kwa nguvu kubwa akiwa anaikunja ngumi yake, mifupa ilisikika wakati ngumi hiyo inakunjwa. Hussen alitua karibu na uso wa Gavin ambaye aliinama na kujivuta kidogo kwenye maji, buti la Hussein lilitua karibu na bega lake lakini aliudaka huo mguu ambao ulikutana na ngumi nzito kwenye buti.
Hussein aligeuka na mguu mmoja ambao ulikuwa chini akamkosa Gavin usoni. Wakati anatua mguu mmoja ukiwa unauma kwa kukutana na ile ngumi, Hussein alijikuta anaelea baada ya mwanaume huyo kuzunguka na teke kali la chini ambalo liliuzoa mguu wake, Hussein hakuwa fala alijigeuza ilia asidondoke vibaya ila hakuwa na bahati kwa sababu alikutana na mguu mzito kwenye kifua chake kiasi kwamba akatapika damu nyingi mdomoni na kutua chini kama kitenesi.
Alipata maumivu makali yasiyo elezeka, aliguekia upande mingine kwa kasi baada ya kuona kivuli kinashuka pale alipokuwa amelala. Alikoswa na goti ambalo lilitua kwenye ardhi na kufanya ardhi kutetemeka kwa kiasi chake, alijizungusha kwa sarakasi ili asimame ila hakuendana kasi na mtu ambaye alikuwa anapigana naye, alikutana na ngumi tano kwenye kifua chake ambazo zilimrudisha tena alipokuwa na wakati huu alitema damu mbali huku kifua kikiwa kinawaka moto isivyokuwa kawaida.
Alisimama na kugeuka nyuma yake, Gavin alikuwa hatua kadhaa kutoka kwake, alianza kuogopa huku akirusha ngumi. Alijitikisa baada ya kuhisi kama haoni vizuri, mtu aliyekuwa mbele yake hakuwepo tena ni kama alipishana na kivuli ndipo akakumbuka kujishika sikio lake akakutana na damu, alishtuka na kuanza kutetemeka akiwa anarudi nyuma, sikio lake moja lilikuwa limedondoshwa chini. Alipo liona ndipo maumivu yakaanza kutawanyika kwenye mwili wake, aliunguruma kwa sauti inayo umiza na kuanza kukimbia eneo hilo, nani angempa nafasi ya kuweza kuondoka bila ruhusa? Hakuna.
Alidondoka baada ya ule upanga kuzama nyuma ya mguu wake, Gavin alimsogelea na kuuchomoa kwa hasira ambapo ulimletea maumivu makali mno.
“Siku nyingine jifunze kuwa msikilizaji mzuri kuliko kuwa muongeaji. Nakuacha hai kwa sababu unatakiwa kutumika kama mfikisha ujumbe kwa huyo mtu ambaye amekutuma uje hapa muda huu kuvamia kwenye hii nyumba, vinginevyo ulitakiwa kufa” aliirusha shilingi yake moja eneo hilo baada ya kumkita Hussein na buti la kiuno ambapo alihisi kitakuwa kimevunjika, alipita na kidole kimoja kwenye mkono wa bwana Hussein kisha akatoweka hapo. Hussein alipitia maumivu makali mno ambayo yalimfanya kupoteza fahamu muda huo huo.


***
Baada ya hayo yote kutokea, muda mfupi baadae zilionekana gari kadhaa za jeshi zikiingia hilo eneo ambapo yalikuwepo makazi ya mwanamama huyo Bi Aisha. Ndani ya gari alikuwepo mkuu wa majeshi, licha ya kuwa na hasira kali na mwanamama huyo alipewa onyo la kutofanya jambo la hovyo kwake hiyo ingepelekea hata yeye mwenyewe kuipoteza familia yake kwahiyo alikuwa amefika hapo kutoa taarifa ya kukamilisha kazi ya kuweza kumuua mke wa raisi lakini pia alihitaji kuzungumza na mwanamama huyo kwa sababu alielewa kwamba ndiyo ilikuwa njia rahisi zaidi ya kuweza kumpata Gavin.
Macho yake yaliona mambo tofauti na yale ambayo alikuwa anatarajia kukutana nayo hilo eneo, geti lilikuwa wazi hivyo waliingia lakini hapakuonekana kuwa sawa. Baada ya kuingia tu aliona miili ya watu kwenye mkono wake wa kulia ikalazimu kuelekea sehemu hiyo, watu hao waliuawa vibaya na kikatili mno lakini kama kawaida shilingi haikuwahi kukosa kwenye mazingira kama hayo hivyo alimujua mhusika alikuwa nani ambaye alifanya jambo hilo ila kitu pekee ambacho hakikuingia kwenye akili yake ni kwamba hao wanaume ambao walivamia hilo eneo walikuwa ni akina nani na walitumwa na nani?

Akiwa anawaza na kuigagua hiyo miili, kijana wake mmoja alimuita aweze kwenda kuona upande wa pili, baada ya kufika huko yalikuwa ni yale yale lakini mtu ambaye alikutwa hapo ndiye alimpa umakini. Hussein Damoga, aliwahi kuwa komando miaka ya huko nyuma ila baadae alikuja kujiunga na kitengo maalumu kwa ajili ya ulinzi wa raisi mpaka baadae akafanikiwa kuwa mlinzi wa raisi ambaye alikuwa madarakani. Licha ya kuwa kwenye hali mbaya lakini bwana huyo alionekana bado anapumua hivyo alikuwa hai, mkuu wa majeshi alitoa amri kwa kijana mmoja kumuwahisha hospitali mtu huyo haraka na ahakikishe anapona, yeye hakuona kama ulikuwa ni muda wa kuweza kurudi kulala tena bali ulikuwa ni wakati wa yeye kuweza kuyapata majibu ya maswali yake ambayo yaliishia njiani.

Arobaini inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA AROBAINI NA MOJA
SONGA NAYO................

Jambo hilo ndilo lilimfanya usiku huo huo kusafiri mpaka Kibaha Maili moja, huko ndiko alifanikiwa kumficha mzee Hasheem huku akimpatia walinzi na wafanyakazi wa kike warembo ambao muda wote walihakikisha mzee huyo anapata kile ambacho anakihitaji. Ulikuwa ni usiku mzito lakini alihitaji mzee huyo aamshwe, jambo ambalo alikuwa nalo lisingeweza kusubiri mpaka asubuhi ndipo waongee ilikuwa ni mhumu wamalizane nalo muda huo kabla mambo hayajaanza kuwa magumu zaidi.
“Unanisumbua na usiku saivi wakati unajua kabisa nilikuwa nateseka kulala kule gerezani na wakati huu natakiwa kufidia yale mateso” alifoka mzee huyo akiwa anajifunga vizuri nguo yake ya kulalia akiwa anaisogelea meza ambayo ilitakiwa kutumika kwa ajili ya kufanyia mazungumzo.
“Jambo ambalo limenileta hapa sio la kulala”
“Ni wewe umemuua mke wa raisi?”
“Ndiyo”
“Alikupa nani hiyo kazi?”
“Aurelia”
“Kuna jambo gani ambalo linakupa hofu kiasi kwamba unatekeleza kile ambacho anakuagiza yeye?”
“Sipo hapa kuanza kukupa mambo yangu binafsi mzee na unalijua hilo”
“Nakusikiliza”
“Leo raisi alienda kumtisha Aurelia na baadae nadhani alituma watu kwa ajili ya kwenda kumuua” mzee huyo alisikitika kidogo.
“Ni raisi ndo kafanya hivi?”
“Ndiyo”
“Na kimetokea nini?”
“Mimi nimerudi usiku huu ili nimwambie nimeifanya kazi yake kwa usahihi lakini sijampata ndipo nikakutana na matatizo kwenye ile nyumba yake”
“Mmepoteza vijana wangapi?”
“Wewe unajuaje kama tumepoteza vijana?”
“Hakuna mtu anaweza kumgusa yule mwanamke Gavin akiwa mzima wa afya kwa sababu anaweza kuua kila mtu”
“Wamekufa tisa na mmoja ambaye ni mlinzi mkuu wa raisi yupo kwenye hali mbaya sana anaonekana amemuacha makusudi kabisa”
“Kwamba raisi amemtuma mlinzi wake eneo lile?”
“Ndiyo”
“Hivi hawa viongozi wananchi huwa wanawachaguaje? Kiongozi gani hana hata uwezo wa kufikiria mara mbili kabla ya kutumia mihemko kufanya maamuzi ya kipuuzi namna hiyo?”
“Kwa hilo sijui mwisho wa siku ndiye bosi wetu hatuna namna, mimi kuna mambo nataka kuyafahamu sina muda wa kusubiri, tunako elekea haya mambo yanaenda kuwa mabaya sana”
“Kwanza anayetakiwa kujiwazia sana kwa sasa ni huyo raisi wako kwa sababu Gavin hawezi kuacha hili lipite, hakuna mtu aliyewahi kumtishia mama yake akamuacha akiwa hai. Mlitakiwa kutumia zaidi akili bwana Savato na tunako elekea ni kwamba unanihitaji sana nikiwa hai kwa sababu sikuoni ukiwa na maisha marefu huko mbele”
“Nataka kujua kwamba Gavin haya mambo anayafanya mwenyewe au kuna watu wengine nyuma yake? Kwa mpangilio wa matukio ni kama inashindikana kabisa kimahesabu kuyatekeleza kwa wakati mmoja”
“Oooh usiniambie umekuja hapa kuhitaji nikumalizie simulizi ya maisha yake”
“Hiyo ndiyo sababu nipo hapa, najua unahisi kwamba naweza kuyabeba maisha yako lakini kwa sasa siwezi kwa sababu naona kabisa wewe ndiye akili yangu ya mwisho iliyo bakia na wewe ndiye unaweza kuwa msaada mkubwa kwangu kuliko mtu yeyote yule hivyo naomba sana unimalizie maelezo ya maisha yake ili niweze kutembua kwamba ni sehemu ipi ambayo inabakia wazi ili nianze kubeba tahadhari mapema”
“Gavin hayupo mwenyewe, kuna vijana wake ambao anafanya nao kazi na mmoja miongoni mwao ndiye mlinzi wa mama yake. Wakati raisi anaenda kwake leo mmewakuta walinzi wangapi?”
“Tumemkuta mmoja mbaye alitufungulia geti, ila mwingine alijitokeza baadae baada ya raisi kumnyooshea bastola mama huyo naye bila uoga akamnyooshea bastola raisi”
“Unaona kosa ambalo mmelifanya bwana Savato?”
“Kivipi?”
“Ukiwa vitani usidharau watu, siku zote watu hatari ni wale ambao huwa wanaonekana wa kawaida mbele ya macho ya wajinga”

“Unamaanisha nini kusema hivyo?”
“Unamkumbuka huyo mmoja ambaye unasema kwamba aliwafungulia geti?”
“Ndiyo”
“Alibeba silaha gani kwenye mkono wake?”
“Kama sikosei ni gobole lile”
“Yule ndiye mlinzi wake”
“Hapana, ni kijana wa kawaida yule tena mfungua geti na hata kama angekuwa hivyo basi asingekuwa anatumia silaha ya kipuuzi namna ile kumlinda yule mama”

“Mhhhhhhh nina uhakika haujui hata kile ambacho unakizungumza wewe, hivi kwa akili yako unahisi kwamba Gavin ni mpuuzi kumuacha yule mwanamke kuishi kwenye mazingira kama yale bila kuwa na uhakika na usalama wake? Yule ndiye mwanamke ambaye amemlea yeye hivyo hawezi kuruhusu mtu kumgusa kijinga kama ambavyo unafikiria wewe ila mwanamke yule amewekwa pale kama chambo kwenye safari ya kumtafuta mtu ambaye alitoa amri ya ile familia kuuawa na kama jina lako limefika kwenye mikono ya Luca kwamba nawewe ulihusika basi fanya ambalo unaliweza kuhakikisha kwamba anakufa kabla hajakufikia au uwe na majibu mazuri ya kumpa na kumshawishi aweze kukuacha hai” mzee Hasheem baada ya kuongea alitoa tablet ambayo ilikuwa kwenye droo kwenye meza hiyo na kuifungua video moja huku mkuu wa majeshi akiwa makini kumsikiliza;

“Huyu ndiye kijana ambaye wewe mwenyewe uliniambia kwamba pekeyake alimvamia waziri wa mambo ya ndani tena mchana wa juakali, kwenye hiyo video ukiangalia unaona kabisa kwamba hata hauna kabisa vijana wenye uwezo wa namna hii. Huyu Othman chunga ni miongoni mwa vijana wake na huyu ndiye huwa anawaongoza Gavin anapokuwa mbali kwahiyo huyo ambaye unasema kwamba alilegea mlangoni ndiye mwenzake na huyu Othman sasa umepata picha aina ya watu ambao unaingia nao vitani bwana mkubwa”
“Wapo wangapi wa namna hii”
“Mimi binafsi sijui kwa sasa kwa sababu ni muda sijapata taarifa zao”
“Sasa umejuaje kwamba huyo kijana wa getini ndiye alikuwa yeye?”
“Wakati mnaondoka hapo ulimuona tena?”
“Hapana, wakati tunaingia ndiye alifungua geti ila wakati wa kuondoka hakuwepo”
“Unahisi kwanini?”
“Alikuwa anasubiri mfanye kosa moja tu awaibukie kwenye uhalisia wake, wanavaa nguo nyeusi kama maninja na ndio utambulisho wao mkubwa lakini kiongozi wao huwa ana utofauti kwenye kufanya matukio yake kwa sababu yeye ana shilingi ambayo ndiyo utambulisho wake lakini ukiacha shilingi aina ya mauaji ambayo yeye huwa anayafanya ni tofauti”
“Bado haujanijibu kwamba umefahamje kwamba wa getini ndiye alikuwa mlinzi wake”
“Huwa wanafanya hivyo, kuna mtu mmoja ambaye huwa wanaamini kwamba hata maadui wakifika hawatamzingatia kwa namna anavyo jiweka kwahiyo ukifanya kosa tu anaondoka na maisha yako ndiyo maana ulivyo nielekeza tu nikajua huyo ndiye kwa sababu siku zote huwa wanafanya hivyo”
“Na unajua wanako patikana?”
“Wapo kila sehemu bwana Savato hata kwako watafika ni suala la muda tu”
“Ebu naomba tuanzie tulipo ishia wakati tupo ndani ya gereza”
“Wapi unataka tuanzie?”

“Baada ya kuzaliwa kwa wale mapacha ndipo tuliishia, nahitaji kujua kile kitu kwamba ni kwanini ilikuwa vile, kwanini ilifanyika siri na baadae hao mapacha waliishi vipi mpaka kutuletea huu muunganiko wa Gavin Luca”
“Unataka kuniua baada ya hapa?”
“Naonekana kama nipo hapa ili kuuua?”
“Sikuamini”
“Ningeweza kukutesa ukaniambia kwa ulazima, hivyo mpaka nakuja hapa ili tuongee kistaarabu ujue kabisa nakuhitaji. Mtu ambaye alinipa maagizo ya kukutafuta wewe mpaka sasa anajua kabisa kwamba umekufa jambo ambalo ni hatari kwangu siku akigundua kwamba upo hai lakini nakuweka hai kwa sababu naona tunaweza kufanya kazi siku za hapo mbeleni natakiwa kujitengenezea njia yangu kwa sababu nahisi hawa wote yakinifika kichwani sitawaona tena” mzee Hasheem alihema ili kuendelea na simulizi ya maisha ya mwanaume wa kuitwa Gavin.

“Kuzaliwa kwa wale watoto kuliongeza furaha kubwa lakini pia kulileta majukumu mapya kwenye familia kwa sababu Lucas alitakiwa kuanza kuangalia pande mbili za shilingi, moja ilikuwa ni pande yake yeye lakini upande mwingine ulikuwa ni kwa ajili ya familia yake. Kumbuka bwana yule hakuwa na maelewano mazuri na baadhi ya watu na alijua kabisa biashara yake ilimpatia maadui wengi kila kona wengine wakiwa viongozi wa serikali ambao hawakuwa upande wake hivyo alijua kwamba kuna siku ingekuja kufika mambo yangeenda vibaya ndiyo maana akataka kujiandaa mapema.
Aliamini siku moja familia yake ingekuja kuingia kwenye matatizo makubwa ndiyo maana kwanza hakutaka kabisa mkewe aweze kufahamika kwa watu kumlinda yeye pamoja na mkwewe ambaye alikuwa waziri mkuu bwana Hassan hivyo kwa ajili ya kulinda hilo akaamua kuwatenganisha watoto hao wawili. Sasa alitakiwa kuwatenganishaje? Ndipo hapa ulikuja mpango wa pili wa kumpata mama mlezi wa mtoto mmoja na jina ambalo lilitua mezani lilikuwa ni jina la Aurelia Vicent ambaye alikuwa kanali wa jeshi kipindi kile.

Sehemu ya arobaini na moja inafika tamati.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA AROBAINI NA MBILI
SONGA NAYO................


Mama huyu alikuwa mjamzito wakati mkewe na Lucas ni mjamzito ila kitu kilicho takiwa kufanyika ni wakati mama huyu anajifungua ndipo abambikiziwe mtoto asiyekuwa wake na angekuja kuambiwa baadae. Walijua hilo haliwezekani bila kumshirikisha mumewe wa ndoa ambaye alikuwa ni mfanya biashara hivyo Lucas alienda mwenyewe kumuomba bwana yule ambaye walikuwa na mahusiano mazuri kibiashara kwamba jambo hilo lifanyike mpaka mkewe akitoka hospitali ndipo aje aambiwe ukweli juu ya yule mtoto na angeelezwa sababu ya mambo hayo yote kuweza kutokea.
Mama wa wale mapacha hakutaka kabisa kuwa mbali na mtoto wake hata mmoja ila hakukuwa na namna nyingine zaidi ya jambo hilo kufanyika kwa sababu ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuwafanya wawe salama ndipo wagagawanyishwa mmoja akapewa kanali wa jeshi Aurelia ambaye mpaka leo unamfahamu na ndiye ambaye umetoka huko kwake na huo ukawa mwanzo kabisa wa mtoto mmoja kuishia kwenye mikono yake.
Baada ya mwaka mmoja kupita mama yule alifuatwa na wenye mtoto kuja kuelezwa ukweli, ukweli ulikuwa ni kwamba mtoto mmoja hakuwa wake bali yeye alipewa tu na mama wa mtoto alikuwa anahitaji baada ya muda awe anakutana na mwanae kwa sababu alikuwa akiishi kwa taabu mno. Ilikuwa ni ngumu kumshawishi kanali kulielewa jambo hilo mpaka alipoitwa daktari ambaye alikuwepo siku watoto wanazaliwa ndiye alithibitisha baadae kwa taabu akaja kuwaelewa baada ya kupewa sababu za msingi za kufanya hivyo na mtoto huyo kila mtu alimjua kama ni wa kanali hata serikali ilijua kabisa kwamba yule mtoto ni wa kanali hivyo hakukuwa na shida yoyote juu ya jambo lile.

Taarifa zilianza kuvuja kwa watu kwamba Lucas ana mtoto mmoja japo hakuna ambaye alijua kuhusu mtoto huyo. Habari hiyo ilianza kufanyiwa uchunguzi na baadhi ya watu kwa sababu wanajua kabisa kwamba udhaifu wa mwanadamu yeyote yule upo kwenye familia, hakuna mwanaume mjanja mbele ya familia yake hivyo wangeitumia hiyo kama fimbo ya kudili na bwana huyo barabara. Zaidi ya hapo watu walitamani kujua mwanamke ambaye alikuwa amezaa naye huyo mtoto lakini pia hakuna mtu alifanikiwa kulitambua jambo hilo kwa sababu alikuwa akilindwa isivyokuwa kawaida.
Miaka ilianza kusogea taratibu maisha yakiendelea, aliendelea kuwa na ukwasi wa kutosha na taifa lilifanikiwa kuanza kurudi kwenye hali yake kwa msaada mkubwa ambao aliutoa. Alikuwa shujaa wa kila mtu, alikuwa mtu ambaye kila binadamu kabla ya kuanza shughuli zake ila asubuhi ni lazima amfanyie maombi bwana huyo kwa sababu alionekana kuwa malaika ambaye alitumwa na Mungu kufanya hiyo kazi.
Baada ya muda kwenda, yule mtoto ambaye alikuwa analelewa na kanali alibebwa na kutolewa kabisa Tanzania, hakuna mtu aliwahi kujua mahali ambako alienda lakini kuna mtu mmoja ambaye alikuwa na taarifa za kijana huyo ambaye siye mwingine ni babu yake yule waziri mkuu na huyo ndiye ambaye anajua ni nani alikuwa anazunguka na huyo mtu kwenye hii dunia na ndiye ana siri nyingi zaidi za mtoto huyo. Maisha yaliendelea kama kawaida huku mtoto mmoja akiwa anasoma vyuo vya nje kwa siri kwa sababu jambo hilo halikutakiwa kujulikana kwani ingekuwa ni hatari.

Akiba za kila hatua ya maisha yako zinaishi pamoja na matendo yako ambayo unayatenda mwanzo. Bila shaka unakumbuka kwamba kuna yule raisi ambaye alitolewa madarakani na Lucas nilikwambia kwamba alikuwa anaishi, sasa yule bwana hakufa kama ambavyo vyombo vya habari vilitangaza, bwana yule alikuwa hai ila aliamua kufeki kifo kwa ajili ya kulipa kisasi. Alidhalilishwa kama raisi kupigishwa magoti, hakuna mtu ambaye alihitaji kumheshimu tena baada ya pale sasa kulikuwa na sababu gani ya yeye kutolipa kisasi? Aliamini kisasi kilikuwa ni haki yake na kila ambaye alihusika na jambo lolote lile juu yake basi alitakiwa kulipa sawa sawa na yale ambayo aliyatenda.
Huyu bwana alikuwa ni raisi hivyo alikuwa na kila rasilimali ambayo aliihitaji, alikuwa na pesa nyingi mno kwa sababu wakati akiwa madarakani alikuwa ni miongoni mwa watu ambao waliihujumu serikali vya kutosha. Ile pesa yake alihitaji kuitumia kwa ajili ya kulipa kisasi ndipo alifanikiwa kuanzisha umoja wa watu wasiokufa THE IMMORTALS, yaani hao ni wanadamu ambao waliamini kwamba wao hawafi kabisa, kwanini? Ni kwamba ukiwaua watano basi wanakuja kumi na baada ya hapo wanapotea tena wanakuja kurudi na kuua watu wako wengi zaidi ya mwanzo.
Mara ya kwanza inadaiwa kwamba bwana huyu alikurupuka kiasi kwamba ilibaki kidogo apatikane lakini akafanikiwa kuondoka kabisa na kutoroka. Aliingia kwenye vita ya moja kwa moja na muuza madawa huyo japo hakuwahi kutokea hadharani ili ajulikane kwamba ni yeye, lengo lake alikuwa anataka kummaliza Luca kisha abebe kila kitu kiwe kwenye himaya yake aanze kuitawala Afrika na kufanya hilo alipanga kuua familia nzima ya Lucas lakini aligundua kwamba hakuwa na uwezo wa kushindana na mtu huyo ambaye alikuwa bilionea, alikuwa analindwa mpaka na wahuni wa mtaani hivyo hiyo vita ilipelekea kupoteza watu wake wengi mno naye akafanikiwa kutoroka na hakuonekana tena baada ya pale, aligundua kwamba aliingia na panga kwenye vita vya kutumia silaha nzito hivyo alitakiwa kujipanga na ndipo alipotea kwa muda mrefu mpaka baadae ambapo alirudi na kufanikiwa kuudondosha utawala wa Lucas ila kwa mara ya pili aliamua kutumia akili zaidi ya nguvu na ndizo ambazo zilimlipa.

Ilitumika miaka mingi yeye kujiandaa ili kumuangusha bwana Lucas bila kuutoa uitambulisho wake wa zamani na hilo ndilo ambalo limetokea. Jambo la kwanza ambalo alilifanya ni kuhakikisha THE IMMORTALS inakuwa na watu wengi wenye nguvu, alihakikisha anawapata watu wenye uwezo ndani ya Tanzania wanakuwa upande wake na anawaendesha, sasa hawa watu alikuwa anawapata vipi? Alikuwa anatumia njia ya kuwaweka madarakani na kuwapa nafasi, watu wengi ukitumia udhaifu wao kuwashika inakuwa ni rahisi kuwaongoza na ndicho alikitumia, alielewa kwanza watu wengi wana tamaa ya kuwa na nguvu kimadaraka basi akawapa hizo nafasi.

Kwenye kuwatengeneza watu wake na kuwapa nafasi kama hizo hata wewe kwa baadae ulikuja kuingia kwenye hiyo mipango na safari yako ikawa inaanzia hapo kuingia kwenye uongozi ukiwa jeshini kijana mwenye uwezo wa kawaida tu, sasa wewe kwanini uliingizwa kwenye huo mfumo? Kwa sababu ulikuwa ni rahisi mtu kuweza kukuendesha, mtu mwenye akili wewe anaweza kukuendesha atakavyo kwa sababu kitu pekee ambacho unakijua ni kujivunia na kujigamba juu ya nafasi uliyokuwa nayo.
Alianza kupenyeza watu wake kwenye mfumo wa Lucas bila yeye mwenyewe kujua, watu wake wengi alikuwa amewapenyeza kwenye nafasi kubwa serikalini, watu wake wakawa wanaliendesha taifa na moja ya mazao yake ni huyu raisi ambaye yupo madarakani, huyu raisi haya mambo yote anayaelewa vizuri kabisa ndiyo maana baada ya kuingia Ikulu alikuteua wewe hapo kuwa mkuu wa majeshi ukihisi umeipata nafasi hiyo kwa bahati mbaya ila haukuelewa kwamba wewe ni zao la watu ambao wana mipango ya kukutumia kutekeleza kila wanakihitaji na siku ikitokea wakajua kwamba umeenda nao kinyume basi niamini mimi hautamaliza hata masaa matano lazima utakufa kwa sababu mfumo wa huyu mtu ni mkubwa na mgumu na ndio ambao unaendesha hili taifa.
Lucas miaka ilivyokuwa inazidi kwenda ndivyo alivyokuwa anazidi kujisahau kabisa, kujisahau kwake likawa tatizo la kuiingiza familia yake kwenye matatizo kwa sababu mwenzake alikuwa anawaza kila anapokwenda kulala kulipa kisasi juu yake, mwenzake alikuwa anamuwazia mabaya kwa siku zake zote za masaa ishirini na manne, yeye hakujua. Wakati huo mtoto wake ambaye alikuwa anamlea yeye alikuwa mkubwa, alikuwa ni msomi mzuri tu lakini hata siku moja hakuwahi kukutanishwa na ndugu yake mpaka walipokuwa watu wazima ndipo walikuja kukutanishwa kwa mara ya kwanza na kukutana kwao ikawa furaha kwa wawili wale. Hawakuwa mapacha tu bali ilikuwa ni kama kopi ya mmoja, walikuwa wanafanana kwa kila kitu ila walipishana kwenye tabia.

Austin ambaye ndiye alikuwa mkubwa alikuwa mstaarabu na msomi mkubwa lakini huyu mmoja Gavin, yeye miaka yake mingi hakuitumia shule bali aliitumia kuzunguka sehemu mbali mbali za ulimwengu ndiyo maana kidogo hakuwa akiujua ule ustaarabu ambao ulitukuka kama ndugu yake. Baada ya kukutanishwa bado hawakutakiwa kuwa karibu kwa sababu ilikuwa ni hatari na ambaye alikuwa anaonekana ni mmoja tu ambaye alikuwa mtoto wa Lucas ambaye naye hakuwa akiishi Tanzania hivyo bado ni watu wa kuhesabu ambao walikuwa wanajua juu ya uwepo wa mtoto huyo hivyo wakati watu wanapandikizwa kwake moja ya vitu vya mhimu ambavyo walitakiwa kuvipatia taarifa ni maisha halisi ya familia hiyo hususani mtoto kwa sababu ndiye angekuwa udhaifu mkubwa wa hiyo familia.

Taarifa zilipojaa kwenye meza sasa walianza kutafutwa wauaji ambao ni wataalamu wa kufanya hizo kazi, moja kati ya watu ambao walihusika kwa ukubwa ni yule komando kutoka Israeli ambaye alifukuzwa kwao kwa ajili ya uhalifu na alipofika hapa akawa anahitaji kuwa raia wa Tanzania lakini akapewa sharti kwamba kama anahitaji kuwepo Tanzania basi anatakiwa kukubali kuifanya kazi moja kisha baada ya hapo engepewa uraia bila hivyo asingepewa msaada basi akawa hana namna zaidi ya kukubali kufanya hiyo kazi. Kazi yake ilikuwa ni kumtafuta mtoto wa Lucas na kumuua na mtoto ambaye alitakiwa kufa alikuwa ni Austin baada tu ya kutua ndani ya mipaka ya Tanzania.
Mwanaume huyo aliifanya kazi hiyo kwa usiri mkubwa huku akiwa anasaidiwa na viongozi wa serikali kupata taarifa mpaka alipofanikiwa kumpata kijana Austin ambaye alikuwa ni pacha wa Gavin Luca. Sasa hapa kuna mkanganyiko kidogo ambao sijakueleza hapo juu, wakati maisha yanaendelea kuna taarifa zilivuja kwamba mtoto huyo wa Lucas miaka ambayo aliitumia nje ya nchi aliitumia kufanya mazoezi makali na mafunzo ya kutisha na wengi waliamini kwamba bwana huyo alimtengeneza huyo mwanae ili aje kumlinda kutoka kwa wale watu ambao wangekuwa maadui zake hivyo waliambiwa kwamba wanatakiwa kwenda kwa tahadhari juu ya mtoto huyo na ndiyo sababu mojwapo ambayo iliwafanya wamtumia komando huyo ambaye hakuwa mtanzania ili hata kama dili hilo lingekuja kuharibika basi walielelewa kabisa kwamba watampoteza mtu huyo na kuitupilia mbali hiyo kesi hivyo kusingekuwa na habari yoyote kuhusu mtu ambaye alikuwa mhusika mkuu kwenye ule mpango.
Mtu ambaye alitumwa kuifanya hiyo kazi ni kijana wa Kiisraeli ambaye anadaiwa kuwa na utanzania kiasi anaitwa Yosef Biton. Huyu bwana ndiye ambaye alikuja kufanikisha kazi ya kumuua Austin wao wakijua wamemuua ni Gavin kwani hawakujua kama wapo wawili ama kuna mtoto anaitwa Austin jina ambalo lilivuja kwao ni hilo la Gavin. Kwa bahati ambayo ilikuwa ni mbaya ni kwamba wakati hii mipango inatengenezwa ni mtoto mmoja tu ambaye alikuwepo Tanzania ila Lucas alizipata habari za kutafutwa kwa familia yake iweze kuuawa ikamlazimu kuongeza umakini. Taarifa hizo pia zilimfikia Gavin, wakati huo alikuwa anaishi Afrika ya kusini ikamlazimu kurudi nyumbani baada ya kusikia familia yake ipo kwenye hatari na jambo ambalo alilifanya baada ya kurudi ni kumficha kaka yake ambaye ndiye alikuwa ni Kurwa hivyo ambaye alianza kuonekana ni yeye. Mwanaume huyo alirudi ili kuhakikisha anailinda familia yake kwa namna yoyote ile hivyo wakati anatafutwa hata yeye akaanza kuwatafuta wale ambao walikuwa wanaisaka familia yake.
Kwenye lile sakata aliwapoteza wanaume miamoja ambao walikuwa na lengo la kumuua yeye na familia yake, kuwapoteza watu wale kukafanya jina lake kuwa maarufu kwao kwa sababu walijua aina ya mtu ambaye walikuwa wanadili naye hakuwa mtu wa kawaida ikawalazimu kutumia nguvu ya ziada kupitia watu wao ambao walikuwa kwenye mfumo wa familia ya Lucas kumteketeza ila haikuwa rahisi mpaka siku moja ambapo miongoni mwa watu ambao walikuwa wakiishi na familia alipo itoa siri ya uwepo wa Gavin mahali fulani pa siri ambapo alikuwa analindwa na ulinzi mkali.
Yosef alipewa watu kadhaa wa kufanya nao kazi ndipo akaenda huko, simulizi ambayo alikuwa amepewa ni kwamba Gavin alikuwa ameua watu wao zaidi ya miamoja hivyo alitakiwa kuwa makini mno lakini wakati anampata alimkuta bwana huyo yupo kawaida jambo ambalo lilimchanganya pakubwa. Austin alikutwa akiwa amelewa, hakuwa akijitambua vizuri hivyo walimtesa isivyokuwa kawaida mpaka mwisho Yosef akamuua kijana huyo kwa risasi kwa mkono wake mwenyewe baada ya kumpa mateso makali na kutokomea akijua amemaliza kazi. Baada ya kukamilisha jambo lile mwanaume yule alitoroka Tanzania na kwenda kuishi Afrika ya kusini kwa siri ili jambo hilo lisije kuvuja hata siku moja.
Sasa kwa kipindi hicho wakati haya mambo yanaanza kutekelezwa ndipo hata wewe ulipo ingizwa kwenye huo mchezo na bila shaka ndio muda ambao wewe ulienda kukutana na kujuana ana kwa ana na Aurelia aliyekuwa kanali wa jeshi ila kwa wakati ule alikuwa ni bosi wako na mtu ambaye alikuwa anatumika kukufundisha wewe mambo mengi kuhusu jeshi. Aliwahi kuwa bosi wako ila baadae ukaja kumsaliti bwana Savato ndiyo maana wanadamu hatuaminiki kwa kiasi kikubwa kwa sababu sisi wanadamu ni watu wa tofauti kiasi kwamba hata kuaminika kwetu limekuwa jambo gumu sana.


Sehemu ya arobaini na mbili inafika tamati.

FEBIANI BABUYA.
 
Back
Top Bottom