Simulizi ya kipelelezi: Jiji la kamari (gambling city)

Simulizi ya kipelelezi: Jiji la kamari (gambling city)

Kesho tunaianza wikiendi hivyo nitaleta episodes 5 za simulizi hii ili mkomae nazo.

Lakini kesho hiyo hiyo tunaianza simulizi mpya ambayo inaitwa BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)

Naomba support yako kubwa ya likes, comments pamoja na support ya kununua ikikupendeza ili tuendeleze gurudumu hili pamoja.

See you tomorrow [emoji872]

CIAOView attachment 3016756
[emoji119][emoji119] mhm lazm tukusupport bro ...!!
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 61
“Hii sio biashara yako daktari, nadhani kazi yako ni kuyaokoa maisha yake tu kisha utapata malipo yako na baada ya hapo uweze kutoweka hapa”
“Sawa nitahitaji msaada wako umvue hizo nguo umsafishe vizuri kisha umvalishe nguo safi nimfanyie uchunguzi ili nisije kupoteza muda wa kuanza kuitibu maiti maana mtu mwenyewe sidhani kama yupo hai huyo” daktari huyo aliongea kwa dharau sana na ilikuwa kawaida yake kitu ambacho kilimfanya James amwangalie kwa jicho kali sana lakini kwa wakati huo alitakiwa kuwa mpole maana kama angeleta ujuaji alikuwa anaingia kwenye hasara ya maisha.
Daktari huyo baada ya kufanya vipimo, alisogea pembeni na kuketi kwenye kiti huku akiinama na kusikitika sana kitu ambacho kilimfanya James kuingiwa na wasiwasi mkubwa sana na kutamani kusikia lolote kutoka kwa daktari huyo.
“Ni bora umwache afe”
“Whaaaaat?”
“Hilo ndilo litakuwa jambo bora zaidi kwake”
“Unamaanisha kwamba yupo hai”
“Ndiyo”
“Kuokoa watu ndiyo kazi yako, sasa kivipi daktari useme kwamba mgonjwa anatakiwa kufa?”
“Huwezi kunielewa na sijali kuhusu yeye kuwa hai au kufa, mara nyingi mimi naangalia malipo yangu tu” James alimwangalia sana daktari huyo kisha akacheka kwa nguvu sana.
“Hivi una hata wazo kwamba kwanini nimekubali kulipa kiwango kikubwa sana cha pesa hivi ili huyu mtu aishi?”
“Hiyo siyo biashara yangu kujua, huyo ni gaidi na mimi nafanya kazi yangu kwa ajili ya pesa tu basi. Akifa, asipokufa hainihusu”
“Kama unahitaji hiyo pesa basi hakikisha huyo mtu anaishi na kama akifa basi hakuna kitu utakipata bwana daktari. Uchaguzi ni wako uwe tajiri ndani ya usiku mmoja au kiburi kikufanye uyakose haya mamilioni ya pesa”
“Kikubwa kama nalipwa pesa yangu sina shida sana kumtibu ila unajua kwanini nimekwambia ni bora angekufa tu?”
“Nakusikiliza”
“Yupo kwenye hali mbaya sana na inaonekana kuwa hai mpaka sasa ni kwa sababu tu mwili wake umezizoea sana hali ngumu hivyo unaweza kustahimili kwa muda mrefu ila mtu wa kawaida alitakiwa kuwa amekufa muda mrefu sana. Amepoteza damu nyingi sana ambapo inatakiwa kumuongezea damu pia baada ya kujua grupu lake ni lipi ila hata hivyo tutakuwa tunabahatisha tu maana sina uhakika kama atafanikiwa kuishi”
“Ndo hicho tu kimekufanya utake afe?”
“Hapana”
“Ila”
“Kama itatokea akafanikiwa kuishi, basi inaweza kumchukua hata miaka miwili kuja kuweza kufumbua macho kwa mara nyingine tena. Kama hilo likitokea basi kuna miaka mingine ya yeye kuweza kuanza kurudisha nguvu za mwili wake baada ya kufumbua macho, hapa nazungumzia uwezo wake wa yeye kuja kusimama tena maana mwili wake ni kama umepooza. Hili la kusimama linaweza kuchukua mpaka miaka mitano au zaidi na kama akifanikiwa kusimama na kuanza kutembea mwili wake utakuwa dhaifu sana kwenye maisha yake yote ambayo atayaishi labda kama kutatokea muujiza mwingine ila sina imani na sijui inaweza ikachukua muda gani haya yote kuweza kufanyika maana ameumizwa vibaya sana na amechelewa kupata msaada ukizingatia viungo vyake vyote vipo kwenye hatari ya kuacha kufanya kazi na ikifikia hatua hiyo basi kunauwa hakuna namna tena ya kuweza kuyaokoa maisha ya mtu”
“Kivipi mtu anaweza kuwa hai kama baadhi ya viungo vya mhimu kama moyo na pua havionyeshi uhai wa mtu husika?”
“Na hapo ndipo inakuja pointi ya msingi kwamba mamilioni ya watu wanazikwa wakiwa bado wapo hai kabisa na huenda hii ni siri ambayo sisi madaktari huwa hatutaki kabisa dunia ije kuujua ukweli”
“Unamaanisha nini?”
“Mtu mpaka ithibitishwe kwamba amekufa inatakiwa viungo vyake vyote vya mwili viache kabisa kufanya kazi, kama kuna viungo hata vichache vinafanya kazi kwenye mwili wake inawezekana mtu huyo kupona. Kuna wakati unakuta mtu kidole tu ndicho kinaonyesha uhai kama mtu akipata matibabu ya hali ya juu anaweza kuishi, kuna watu unakuta kila kitu hakifanyi kazi ila sikio tu ndilo linapumua. Na kuna muda kuna viungo ambavyo vipo ndani ya mwili na wewe huwezi kuviona kwa macho yako unakuta vipo hai lakini mtu anazikwa kwa sababu watu wanashindwa kuujua ukweli”
“Kama ukiwa karibu na maisha yetu sisi ya kuishi na wagonjwa huenda utakuja kuyajua mambo ya kutisha sana na huenda sisi ni miongoni mwa watu ambao ni watenda dhambi wakubwa kuliko hao wanasiasa ila hakuna daktari atakuja kukueleza hili. Sio kila daktari yupo hivi kuna muda inatokea tu ni ukosefu wa vifaa husika au ukosefu wa wataalamu walio bobea ndiyo maana unaonaga matajiri wengi inaweza kuonekana kwamba amekufa na watu wakatangaziwa lakini baadae unaambiwa amepona, unajua kwanini? Kwa sababu huwa wanaitwa watu walio bobea na kila aina ya vifaa vikubwa kiasi kwamba kile sehemu ya mwili wake inachunguzwa kwa umakini mkubwa sana kijana wangu”
“Kwanini unaniambia yote haya dokta?”
“Kwa sababu unanilipa vizuri sana hivyo unastahili kusikia mengi usiyo yajua ila kama ungekuwa umenilipa pesa kidogo basi ningeandika tu ripoti kwamba mtu wako amekufa hivyo sipo tayari kuikosa bilioni moja pesa ambayo itanifanya nitanue kwa sababu tu ya mtu ambaye hatuhusiani kwenye maisha. Sijali kwa sababu anatafutwa hiyo sio biashara yangu, mimi naangalia pesa tu ndugu yangu siuzi sura mjini hapa” daktari huyo aliongea mambo mazito na ya kutisha sana ambayo yalionekana kumpeleka mbali sana kimawazo James juu ya namna wanavyokuwa wanayatenda mambo ya kutisha sana.
“Okoa maisha ya huyu mtu ni mhimu kuliko hata maisha ya raisi wa nchi na kuhusu damu usijali nitamchangia mimi maana group langu ni O hivyo naweza kumchangia yeyote yule” daktari alimwangalia sana mwanaume huyo huku akiwa anatabasamu.
“Kikubwa kama pesa yangu inasoma sina shida kabisa ila huwa napenda sana wakati nafanya kazi niwe naziona pesa kwenye meza” James hakuongea kitu alitoka kwenye hicho chumba na kurudi akiwa na begi la pesa za kimarekani ambalo aliliweka juu ya meza na daktari huyo alizigusa gusa huku akiwa anatabasamu sana akivaa vazi lake jeupe ili aweze kuifanya kazi kama ambavyo alitakiwa kuifanya.
Yalitumika masaa nane kuweza kumfanyia mwanaume huyo oparesheni kali sana na kuongezewa damu ambapo baada ya muda huo ambao ulikuwa ni mchana wa siku ya pili daktari huyo alithibitisha kwamba yeye binafsi alikuwa ameimaliza kazi yake na huko ambako kungeendelea basi haikuwa biashara yake kabisa hivyo alitakiwa kubeba ujira wake kisha atoweke ndani ya eneo hilo haraka sana. James aliweza kumuuliza daktari huyo vitu vya kuvifanya pamoja na dawa za kununua kwa muda ambao atakuwa anamhudumia mgonjwa wake na baada ya kuelekezwa alimgeukia daktari huyo.
“Dokta unataka kuwahi nyumbani?” alimuuliza wakati daktari huyo akiwa anabeba begi la pesa
“Ndiyo, nafikiri biashara yetu imeishia hapa na niseme kwamba nimefurahi sana kufanya kazi na wewe maana sijawahi kukutana na mteja wa maana kama wewe kwenye maisha yangu. Ukipata watu wengine kama huyu mgonjwa wako basi usisite kuniita muda wowote, namba yangu unayo” majivuno yalikuwa sehemu ya maisha ya daktari huyo ambaye aliongea kwa mbwembwe sana akiwa anaanza kuzipiga hatua zake kwenda nje.
“Tunafanyaje kuhusu huyu gaidi sasa?” kauli hiyo ilimshtua sana na kumfanya aweze kugeuka
“Hiyo sio biashara yangu kijana”
“Kwa sasa ishakuwa yako kwa sababu ushamjua na unajua alipo”
“Unataka kufanyaje kuhusu hilo?”
“Siwaamini sana wanadamu dokta”
“Kwahiyo utaniua”
“Nadhani hilo ndilo jibu sahihi, ni mtu ambaye ni mwepesi sana kutoa siri ndiyo maana kwa sababu ya pesa tu ukaamua kutoa siri zenu madaktari je unahisi napaswa kukuamini mtu kama wewe?”
“Kijana nadhani bado haujanijua”
“Kuwajua watu sio kazi yangu, kazi yangu ni kuua” mwanaume alichomoa bastola kwa kasi ya ajabu kwenye kiuno chake na kumtandika risasi daktari huyo kwenye paji lake la uso
“I don’t trust humans” aliongea akiwa anausogelea mwili huo ili akautoe hapo akiwa na maana kwamba hakuwa mtu ambaye alikuwa anawaamini kabisa wanadamu.

Nchi ilikuwa imechafuka, watu walikuwa wamepoteza kabisa imani na kila kitu wakiamini kwamba kama raisi wa nchi aliweza kuuawa basi mtu yeyote yule angeweza kufa ndani ya nchi yao. Mchana wa siku hiyo watu walikuwa wanazunguka na mabango kila sehemu huku polisi wakiwa wana kazi kubwa sana yakuwatuliza. Viongozi wa mataifa mbali mbali ambao walikuwa na uhusiano mzuri na nchi ya Tanzania walikuwa wanaingia Tanzania kuweza kutoa pole kwa yale mazito ambayo yalikuwa yametokea lakini pia kusaidia kutoa msaada pale ambapo wangehitajika.
Wananchi walikuwa wanataka kujua kuhusu usalama wao na hao magaidi ambao walikuwa wameanza kuishtua nchi, waliamini kwamba kama kuna gaidi aliweza kuuawa basi hakuwa pekeyake lazima kulikuwa na wenzake ambao wangejitokeza muda wowote na kuleta madhara makubwa lakini licha ya hayo yote kuweza kuendelea hakuna taarifa yoyote ile ambayo ilitoka kutoka serikalini tangu raisi Denis Kijazo aweze kutoa habari mbaya ya kifo cha raisi Teodensia Mpanzi ambaye alisemekana kuwa msaliti na alihitaji kuliingiza taifa kwenye matatizo makubwa sana.
James alikuwa anaangalia taarifa ya habari kwa umakini sana kujua kama kulikuwa na habari yoyote ile mbaya kwa upande wake huku akiwa na mawazo sana maana mtu ambaye alikuwa amebaki naye wa kumtegemea ndiye huyo alikuwa kitandani na ilidaiwa kwamba anaweza kuchukua miaka kadhaa mpaka kufanikiwa kuja kusimama tena. Tangu jana yake hakuwa amebadilisha nguo zake zaidi ya koti tu pekee hivyo akahitaji kubadilisha zingine kisha apumzike maana alikuwa amechoka sana.
Wakati anashika suruali yake alishangaa anakutana na kitu kigumu mfukoni na baada ya kuangalia kwa umakini aligundua kwamba kulikuwa na kikaratasi kifupi chenye maandishi machache. Aliwaza kwamba ni namna gani aliweza kukipata kikaratasi hicho, alitabasamu baada ya kugundua kwamba ni lazima Bilali alikiweka hakukuwa na mwingine wa kuweza kufanya jambo kama hilo. Baada ya kuikunjua karatasi hiyo na kuisoma vizuri alituliza kwanza akili, ilikuwa inamuelekeza kazi ambayo alikuwa anatakiwa kuifanya siku hiyo hiyo.

61 inafika mwisho.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 62
Yalikuwa ni maelezo ya kumuelekeza alipokuwepo mwanamke ambaye alikuwa ni mhimu sana kwa Max, alimuomba James kwamba kama asipo fanikiwa kumpata Max basi ahakikishe kwamba mwanamke huyo anakuwa salama kwa namna yoyote ile kwa sababu Max aliahidi kumlinda huyo mrembo ambaye jina lake alifahamika kama Ariana. Maelezo yote ya namna ya kumpata yalikuwa yanaonekana vizuri sana ndani ya karatasi hiyo na kilichokuwa kimebakia ni utekelezaji tu.
Usiku maeneo ya Salasala James alikuwa pembezoni mwa mjengo ambao ulikuwa unamilikiwa na mwanamke huyo na hakutaka kabisa kuua mtu maeneo hayo hivyo alirusha gesi ndani ya geti ambayo haikuwa pana sana. Moshi wa gesi ulisambaa sana ndani ya eneo hilo mlinzi mmoja mmoja akwa anashuka chini na baada ya hapo aliingia ndani ambamo alimkuta mwanamke huyo amelala, alimgusa shingoni na kumbeba kisha kutoweka naye mpaka sehemu ambayo alikuwa amemhifadhi Max.
Asubuhi Ariana alishtuka akiwa kwenye chumba ambacho alikuwa ana uhakika kwamba hakikuwa chake, hilo ni jambo ambalo lilimshtua sana kiasi kwamba alianza kujikagua kama alikuwa salama kwani alianza kuogopa kwamba huenda alikuwa amebakwa ila baada ya kujikuta yupo salama alihema kwa nguvu sana na kuanza kuhangaika kugonga kwa nguvu mlango ambao ulikuwa mbele yake akiamini kwamba mtu ambaye alikuwa karibu na eneo hilo angeweza kuja kumfungulia.
Baada ya muda kidogo kupita kuna mwanaume ambaye hakuwahi kumuona kwenye maisha yake yote akiwa amebeba sinia ambalo lilionekana kuwa na supu aliingia hapo.
“Nimefikaje hapa?”
“Nilikuja kukuchukua jana kwako”
“Na walinzi wangu?”
“Saivi watakuwa wameamka maana niliwazimisha tu”
“Ungekuwa unataka kunibaka nadhani ungekuwa umenifanyia hivyo nikiwa nimelala, unaweza ukanipa sababu ya mimi kuwa hapa?”
“Ni kukufanya uendelee kuwa hai”
“Wewe ni nani ambaye unajali mimi kuwa hai na nitakuwa hai kutoka kwa nani ambaye anakuja kuniua?”
“Kunifahamu mimi haina umuhimu sana kwako ila kusema nani anataka wewe ufe ni kila mtu”
“Mimi sina ugomvi na mtu yeyote yule unahisi ni mtu gani anaweza kutaka mimi nife?”
“Unahisi mpaka uwe na sababu ya msingi ya kuuawa ndipo unaweza kufanyiwa hivyo?”
“Umeaua watu wangapi kwenye maisha yako?”
“Siwezi hata kuhesabu”
“Kwahiyo unataka kuniua na mimi?”
“Ningetaka kufanya hivyo ningekuua muda mrefu sana”
“Unataka nini kwangu?”
“Unahisi mimi najali sana kuhusu maisha ya mtu zaidi ya watu wangu wa karibu ambao nimewapoteza? Umeniuliza nimeua watu wangapi kwenye maisha yangu? yes, huenda mamia ya watu kwa sababu kuua ndiyo kazi yangu. Mimi sijawahi kuishi kwa amani kama wewe hapo ambaye muda wote unalindwa. Tangu nianze kufanya hizi kazi, mimi ni kupishana na mapanga tu na risasi muda wote kuhakikisha watu ambao wanatusaliti wanakuwa salama halafu unaanza kunikaripia kwamba mimi nataka nini?” mwanaume aliongea kwa ukali sana akiwa anabamiza chini sinia ambalo lilikuwa kwenye mkono wake kisha akamshika mkono mwaamke huyo na kumpeleka kwenye chumba kingine ambapo juu ya kitanda kulikuwa na mwili wa mtu ambaye alikuwa anatumia mashine kupumua.
“Unamfahamu yule aliye lala kitandani pale?” Ariana alisogea kwa kujivuta sana akiwa anatetemeka kwa uoga kwani hakuwa mzoefu kwenye mambo kama hayo. Baada ya kuiona ile sura alishtuka sana na kurudi nyuma.
“Unaweza ukaniambia kwamba umeshtuka kwa sababu yupo hai au umeshtuka kwa sababu unajua kwamba ni gaidi?” mwanaume alikuwa akiwa anamsogelea mrembo huyo ambaye mpaka wakati huo ni kama alikuwa njiapanda asielewe ni kipi ambacho alitakiwa kukifanya.
“Nchi nzima inamtafuta kama gaidi na anadaiwa kuhusika na mauaji ya raisi na bado unataka kuniaminisha nini? Kwahiyo umenileta mimi kuja kumuona huyu mtu? Na kwanini yupo hai? Huenda ndiye alimuua kaka yangu kisha akaja kunirubuni” Ariana naye alitamka kwa ukali sana huku chozi likiwa linamtoka kwa huzuni sana.
“Yeah sasa nimeanza kuelewa kwamba ni kwanini kuna baadhi ya makomando kama mimi huwa wanaamua kuisaliti nchi hii na kuchagua pesa na maisha mazuri. Kuna wananchi kama nyie hamstahili kabisa kuwa hai wala kulindwa na watu kama sisi kwa sababu tunajitoa kwa kila kitu, tunayatoa maisha yetu na kuwatoa sadaka tunao wapenda na malipo ya pekee ambayo tunayapata kutoka kwa wananchi kama wewe ni matusi na dhihaka kwa sababu mna akili za kijinga ambazo mwanasiasa yeyote yule anawaambia kitu ambacho mnaanza kuwadharau hata watu ambao wanawalinda”
“Bibie mimi sijali kuhusu usalama wako, I don’t give a https://jamii.app/JFUserGuide kama unaishi au unakufa, kwangu sina hasara yoyote ila huyo kijana mdogo ambaye unamwona amelala pale ndiye ambaye mpaka sasa amenifanya mimi kuja kukukomboa wewe kwa kuilinda ahadi ya kaka yako ambayo alimuahidi ila kama ningekuwa mimi nisingekusaidia mwanamke mwenye jeuri kama wewe. Umefika hapa bila hata kujua hali yake, bila hata kujua nini kilitokea unaanza kumbebesha lawama kijana ambaye ameyatoa maisha yake kwa ajili ya taifa hili? Hapa mimi sijakuweka kama mateka ila nilihitaji kukuweka salama kwa ajili yake ili siku akija kuamka akuone ila unaweza kwenda kwako na ukaendelea na maisha yako na hautakuja kutuona tena kwenye haya maisha mpaka dunia inafika mwisho” mwanaueme aliongea maneno machungu sana na yenye kugusa sana kwenye kwa mwanamke huyo ili kama alihisi kwamba labda mtu huyo alikuwa amemteka basi ajue hakuwa sahihi.
Watu hao walikuwa wamepitia mambo mengi sana na wakati huo angalau angeuliza yaliyo tokea yeye anaanza kumhisi mtu huyo kwamba ni msaliti kwake ila alishtuka sana baada ya mwanaume huyo kujitambulisha kama komando kwenye maelezo yake. James alifungua milango ya jumba hilo yote kwa rimoti ambayo ilikuwa kwenye mkono wake kisha akatamka kwa sauti kali sana.
“Go and never come back” ilikuwa kauli ya kiume haswa wakati akiwa anatoka kwenye chumba hicho akiwa na hasira kali sana. Mwanaume alirudi ndani ya nusu saa baadae na kushangaa uwepo wa mwanamke huyo akiwa amejikunyata pembezoni mwa kitanda.
“Unataka nikurudishe mwenyewe?”
“Siondoki”
“Whaaat?”
“Mpaka nijue kipi kinaendelea, nahisi nipo porini nimetelekezwa na sijui niende wapi. Ghafla tu naletewa taarifa za kifo cha kaka yangu na mtu ambaye sikuwahi kumfahamu kabla nikaamua kumuamini, mtu huyo huyo ghafla nakuja kujua kwamba ni gaidi na amemuua raisi wa nchi na mamlaka za ulinzi zinatanganza kwamba amekufa lakini ghafla mtu huyo huyo nakuja kumkuta akiwa hai bado huku ukiniteka na kunifikisha hapa bila mimi kujua. Bado tu unataka nikuamini na kufanya unacho kitaka wewe?”
“Wewe unataka kujua nini bibie?”
“Kila kitu” James hakuwa na namna zaidi ya kumsimulia kila kitu na mambo yote ambayo yalikuwa yametokea mpaka wao kuishia hapo. Ariana alijikuta mpaka anatokwa na machozi maana mambo hayakuwa mepesi kama alivyokuwa anahisi yeye.
“Unataka kuniambia kwamba mmesalitiwa na nchi?”
“Yeah na wanajua kwamba Max amekufa kwa sababu wamemzika kabisa ni basi tu alikuwa mtu wa kazi ndiyo maana mpaka sasa anaishi. Ubaya wa hawa watu huwa wanaua hadi watu wanao kuzunguka na wewe unahusika moja kwa moja kwenye hili wanamini kwamba kwa baadae kunaweza kukawa na uzao wa visasi ndiyo sababu huwa wanaua kila ambaye anakuhusu”
“Sasa tunafanyaje?”
“Hakuna kurudi nyuma tena, kama unataka kuishi basi sahau kila kitu ambacho umekiacha kwenye maisha yako”
“Unamaanisha nisahau biashara zangu? Nisahau nyumba na kila kitu”
“Kila kitu ila kama unaona hivyo vitu ni mhimu sana kuliko maisha yako unaweza ukavifuata”
“Ni maisha gani ambayo naenda kuyaishi mimi?”
“Kuhusu pesa sio shida ila uhai wako ndicho kilikuwa kitu cha mhimu zaidi lakini yule aliye lala pale maisha yake yana thamani kuliko mtu yeyote yule hapa nchini”
“Kwanini?”
“Kwa sababu ndiye mtu pekekee ambaye anaweza kumaliza kila kinacho endelea hapa nchini”
“Itamchukua muda gani kulala pale na kuja kusimama tena?”
“Sijajua ila ni miaka”
“Na maisha yangu mimi yatakuwaje?”
“Una bahati sana kumpata mwanaume kama huyo kwenye maisha yako kuna watu hawawezi kutunza ahadi kiasi hicho kama alivyofanya yeye hivyo kama unaweza basi usije ukampoteza huyo mwanaume na kama ukipata nafasi kuwa mke kwake na uwe mtu wa karibu yake kumpa furaha siku akija kuamka, wanaume kama hao ni mmoja kwenye mamilioni” maneno ya mwanaume huyo yalimgusa sana kiasi kwamba alitabasamu huku akiwa anayatoa machozi akiwa anamsogelea mwanaume huyo ambaye alikuwa kitandani. Alijitoa kwa kila kitu kuweza kutimiza ahadi ambayo alikuwa amemuahidi kaka yake na huyo alikuwa kwenye hiyo hali kwa sababu ya kusalitiwa na watu ambao walikuwa wanahitaji kuendelea kuiweka nchi kwenye mikono yao kama walivyokuwa wanataka wao. Alimkumbatia kwa mahaba sana mtu huyo.
“What is next?”
“Tunaondoka nchini usiku wa leo”
“Whaaaat?”

62 inafika mwisho.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 63
“Hii ndiyo njia pakee ya sisi kuwa salama kutoka kwa hawa watu” Ariana alichoka kwani yalikuwa ni maamuzi ya haraka mno ila hakuwa na namna ya kupinga kwani alipewa nafasi kama alitaka kuishi basi alitakiwa kuwa na watu hao ila kama alikuwa anataka kufa basi aliruhusiwa kuweza kuondoka ndani ya eneo hilo.


MIAKA YA SASA
Karistus Dikson aliogopa sana kwa mambo ambayo yalimkuta usiku huo. Kwanza bado hakuwa anaaamini kama kuna mtu anaweza kumvamia kirahisi sana namna ile na kufanya ambacho alikipenda mbele yake kwa sababu alikuwa ni mwaaume wa kazi sana ila alipigika kama mtoto mdogo na alijua kabisa kwamba watu wenye uwezo wa kufanya hivyo mbele yake walikuwa ni wa kuhesabika.
Pia kitu kilimshangaza ni hisia zake juu ya kurudi kwa mwanaume ambaye alimzika kwa mikono yake mwenyewe, ila kauli ambayo ilibaki pale chini aliamini kabisa kwamba haikuwa ya mtu mwingine bali Donald Daniel kwa sababu ni kauli ambayo aliwahi kumtamkia yeye mwenyewe kwa kinywa chake. Swali lake kama hilo jambo lilikuwa ni kweli, alijiuliza kwanini mtu huyo aweze kumuacha hai? Kwa mambo ambayo alimfanyia huko nyuma alitakiwa kuuawa na mtu huyo tena kikatili sana. Hayo mambo yalikuwa ni magumu sana kwake kuufanya moyo wake utulie kitu ambacho kilianza kumtisha sana kiasi kwamba akakosa kabisa imani ya kila ambacho kilikuwa kinaendelea kwenye maisha yake.
Jambo la mwisho ilikuwa ni begi ambayo iliibiwa, ni begi ambayo ilionekana kubeba nyaraka za siri sana ambazo hakutakiwa kuzipoteza kwa gharama yoyote ile vinginevyo ingekuwa hatari sana kwake na kwa bahati mbaya sana hakujua huyo mtu alizichukua kwa sababu ipi na angeweza kumpatia wapi. Mwanaume alikuwa anayawaza hayo yote akiwa anakimbia kwa kasi sana kuweza kupotea eneo ambalo alikuwa amekutana na mwanaume ambaye alichukua begi lake.
Alifika mpaka sehemu ambayo alikuwa amepaki gari yake, aliingia na kutoweka kwa kasi sana huku akiwa anaonekana kuwahi maeneo fulani. Safari yake ilimfikisha mpaka kwenye godauni moja ambalo lilionekana kuwa la muda mrefu sana na baada ya kufika hapo hakukaa sana baada ya kumsalimia mlinzi aliyekuwa mlangoni aliingia ndani na kuchukua koleo kubwa mbili na jembe kisha akaondoka kwa kasi sana na gari yake bila kujulikana kwamba alikuwa anaelekea wapi.
Safari yake ilienda kuishia kwenye barabara ya Mpiji Magohe, aliendesha gari yake mpaka msituni sehemu ambayo alikuwa ana uhakika kwamba alimzika Max waweza kumuita DONNY au Donald Daniel (Double D). mwanaume baada ya kufika maeneo hayo alikutana na nyasi ndefu sana maana ni miaka kumi na miwili ilikuwa imepita tangu tukio hilo liweze kufanyika hapo, alifukua na kuchimba haraka haraka huku akiwa anahema sana. Alimaliza kuchimba sehemu hiyo mpaka chini kabisa lakini alikutana na udongo tu, alihakikisha kila kona ya kaburi hilo lakini hakukuwa hata ishara ndogo ya kwamba kuna mtu waliwahi kumzika maeneo hayo wala kuonyesha kama kulikuwa hata na mabaki yoyote zaidi ya udongo wa kawaida tu na mchanga kiasi.
Alikaa humo humo ndani akiwa anaogopa sana, alisikitika sana na kuhisi kuna jambo baya sana lilikuwa linakuja kwenye maisha yake, jambo ambalo abadani asingeweza kulikwepa au kulikimbia.
“Yupo hai. Sasa aliishije na kwanini ameniacha mimi hai? Huenda kuniacha mimi hai ni hatari zaidi ya kama angefanikiwa kuniua na lazima kuna mambo mabaya sana yanaenda kutokea. Uko wapi Max?” mwanaume alijiuliza maswali mengi sana mwenyewe na kuweza kujishauri kile ambacho alikuwa anahisi kwamba huenda kinaenda kutokea huku akiwa anamuita mwanaume huyo kwa hasira saa kujua ni wapi alipokuwepo ili aweze kumtafuta. Hakuwa na namna zaidi ya kunyanyuka na kutoweka hilo eneo Dax maana hakukuwa na msaada wwote ule wa kupata chochote kile ambacho alikuwa anakihitaji.
Dax hakuwa na uhakika na maamuzi yake lakini alitakiwa kuhakikisha anafanya jambo kabla mambo hayajaharibika hivyo wakati huo alikuwa anahitaji akamweleze ukweli bosi wake maana ni bora kama angeongea mwenyewe kuliko mtu huyo kama angekuja kujionea mwenyewe au kuambiwa na mtu mwingine.
Ndani ya kasino moja kubwa sana walikuwa wamekutana matajiri kadhaa wakiwa wanazungumzia mambo ya biashara zao na kwenye kundi la hao matajiri alikuwepo Denis Kijazo umri ukiwa umesogea sana. Yeye ndiye ambaye alikuwa kiongozi wa wafanya biashara hao ambapo walikuwa wamepata mwekezaji wa madini kutoka nje ya nchi hivyo kabla hajapewa mkataba na serikali wao ndio walikuwa wanakubaliana naye kwanza kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa kwenye upande wao.
Wakiwa katikati ya kikao hicho walisikia kelele za vurugu mlangoni, Dax aliingia hapo na kuwakuta walinzi mlangoni ambapo aliwaambia kwamba anahitaji kukutana na bosi lakini wanaume hao walimwambia kwamba alitakiwa kusubiri mpaka kiongozi huyo amalize kikao kwani alikuwa anazungumza na wageni wake mambo ya mhimu sana lakini mwanaume wa kazi alisistiza kwamba yeye alikuwa na jambo la mhimu zaidi kuliko hata hiyo biashara ambayo walikuwa wanaifanya humo ndani hivyo alitakiwa kumuona bosi wake haraka sana. Licha ya hayo yote bado watu hao waliendelea kumkatalia yeye kuweza kuingia ndani na hapo ndipo alianza kuwarushia ngumi kali na mbaya sana mithili ya watu ambao hakuwa akiwafahamu kabisa.
Baada ya kelele hizo kuwa kubwa Denis Kijazo alitoka mwenyewe na baada ya kumuona tu kila mtu alitulia kimya kama hawakuwa wao kwa sababu walikuwa wanamuogopa sana mzee huyo.
“Umeanza kunywa pombe mpaka hujielewi kiasi kwamba unanidhalilisha mbele ya wageni wangu?” aliongea kwa sauti yake ya upole ambayo ilikuwa kali sana ndani yake.
“Hapana bosi”
“Una kipi cha kujitetea?”
“Nina habari mbaya sana naomba maliza huo mkutano na hao watu waambie mkutane wakati mwingine”
“Umechanganyikiwa?”
“Hiki ninachotaka kukwambia kinaweza kufanya hata hiyo biashara kufa”
“Whaaaaat?”
“Bosi nipo tayari kwa adhabu yoyote ile kama ukikuta ni jambo la kitoto hili ambalo nataka kukwambia” Denis Kijazo alimwangalia kwa hasira sana kijana wake huyo huku akiwa anatabasamu na kuingia ndani ambako kulikuwa kunafanyika mkutano. Baada ya dakika moja wageni wake alitoka mmoja mmoja na kumruhusu kijana huyo aingie huku akiwa haongei zaidi ya kumkazia macho na kumtaka aweze kusema hicho ambacho alidai kuwa nacho. Dax alipiga magoti kwanza kwa sababu hicho ambacho alikuwa anataka kukiongea alikuwa na asilima nyingi sana kwamba mtu huyo asingeweza kumuacha hai ni lazima angemuua.
“Mzigo umepotea”
“Usiniambie mzigo wangu”
“Ndio huo bosi”
“Niletee bastola hapa” aliongea kwa sauti kali sana kuelekea kwa walinzi ambao walikuwa mlango ni kilikuwa kitendo cha sekunde kadhaa tu kuweza kuletewa bastola kwenye mkono wake.
“Bosi kabla haujafanya chochote naomba unisikilize sana kwa sababu huenda kunisikiliza litakuwa jambo la busara zaidi na kuweza kujua kwamba ni wapi tulipaswa kuanzia” mzee huyo alikuwa anamtazama kwa hasira ana kitu ambacho kilimpa taarifa kwamba ni kama aliruhusiwa kuongea.
“Max bado anaishi” aliongea akiwa anatetemeka sana huku akiwa na wasiwasi usiokuwa wa kawaida.
“So?”
“Yeye ndiye ameuchukua mzigo na kwa sasa upo kwenye mkono wake”
“Unaweza kwenda”
“Bosi”
“Huyo mtu alishakufa miaka kumi na miwili ambayo imepita, leo unaniletea habari za yeye kuwa hai na kupotea na mzigo wa mhimu sana ambao unaweza kunipoteza hapa nilipo na bado unataka uendelee kunidanganya hapa? Nakupa masaa mawili tu kazilete hizo nyaraka kabla sijaamua kuanza kuzitafuta mimi mwenyewe” bosi wake alihisi kijana wake alifanya uzembe mwenyewe ila akaamua kusingizia kuhusu mtu huyo ikiwa ni kama njia ya kuweza kujisafisha kutoka kwenye hilo asijue kwamba huo ndio ulikuwa ukweli wenyewe.
“Nimefukua kaburi lake. Ni kweli anaishi na hakufa kama tunavyo amini sisi”
“Whaaaaat?”
“Nakumbuka kauli yake ya mwisho aliwahi kuniambia kwamba ipo siku angerudi nadhani alimaanisha kweli”
“Mwili wake ulikuwa na risasi ngapi wakati yanafanyika hayo yote?”
“Kwa kumbukumbu zangu kama zipo sawa ni risasi sita”
“Halafu ukamzika?”
“Ndiyo bosi”
“Halafu badae anakuja kuishi tena?”
“Ndiyo bosi”
“Hayo maelezo yako wewe unayaelewa?”
“Bosi najua hili jambo ni gumu sana kuweza kuniamini ila ni ukweli nadhani kuna mtu atakuwa alihusika kwenye kulitelekeza hili”
“How?”
“Nilimzika akiwa mzima ili afe kwa mateso makali na majuto sana na baada ya kumaliza niliondoka pale na vijana ila kwa mlolongo huu ulivyo ni lazima siku ile wakati namzika kulikuwa na mtu au watu wengine ambao walikuwepo pale na huenda ndio ambao walimsaidia kuishi”
“Unajua ni jambo gani ambalo ni hatari zaidi duniani Dax?”
“Pesa bosi”
“Hapana, pesa sio hatari kama watu wanavyosema, pesa huenda ndiyo inatumika kuipunguza hatari kubwa licha ya kuhusika pia kutengeneza hatari hizo hizo lakini duniani kitu hatari zaidi ni uongo. Uongo huwa unaanza kuuaminisha ubongo kwamba kila kitu kipo sawa, kwamba jambo hili ni zuri sana unatakiwa kuliamini. Uongo unaleta burudani kubwa sana lakini unaweza kuharibu ubongo moja kwa moja lakini pia uongo ndiyo silaha kubwa sana kwenye siasa na kuitawala dunia kwa sababu ulimwengu unapewa taarifa za uongo kwa ajili ya faida fulani iwe ni kiuchumi au kwa namna yoyote ile lakini mimi sipendi mtu kuwa muongo kwangu kwani kunaweza kuwa na madhara makubwa sana kwa baadae”
“Nakumbuka miaka kumi na miwili ulinihakikishia kwamba umehakikisha mtu huyo amekufa kabisa na havuti pumzi tena, ukanipa uhakika kwamba kila kitu kipo sawa tuendelee na maisha mengine na kwa sababu nilikuwa nina imani na wewe nikaamua kukuamini na kuachana na habari hizo lakini leo unakuja kunipa taarifa kinyume chake unataka nikufanye nini bwana mdogo? Unajua thamani ya mzigo ulio upoteza na madhara yake yatakuwaje? Sijali kuhusu nani kuishi na nani kutoishi ila kwa sasa nahitaji mzigo upatikane haraka sana vinginevyo nakuua” mzee huyo alikuwa anaongea kana kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile ila macho yake yalikuwa kwenye hasira kali sana na yalikuwa yanawaka moto ndani yake.

63 inafika mwisho.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 64
Baada ya kijana huyo kutoka humo ndani alipasua pasua meza yake kwa hasira kali ambazo alikuwa nazo baada ya kuambiwa mambo ambayo kwake hayakuwa mema kabisa, ilikuwa ni ishara mbaya sana. Aliifungua tai yake na kuitupa kisha akamimina pombe kali sana na kuigida yote, akaketi kwenye meza ambayo ilikuwa na simu hapo, aliipigia namba moja kwenye simu hiyo ikawa inaita lakini wakati anasubiri simu hiyo iweze kupokelewa upande wa pili simu yake ya mkononi ilianza kuita na namba ambayo ilikuwa inapiga ilionekana kutokea Marekani ila alijua kwamba anahezewa tu. Aliipokea kwa wasiwasi sana
“Hello bwana Denis Kijazo” ilisikika sauti nzito sana kutoka upande wa pili.
“Nani wewe?”
“Usiwe na haraka sana mzee wangu, nina maelekezo mafupi sana kwako”
“Yapi?”
“Jiue mwenyewe kabla sijakukamata au nenda kwneye vyombo vya habari ueleze kila ambacho umekifanya tangu uingie kwenye siasa, ukifanya hivyo mimi nitakuacha na maisha yako na sitakugusa kabisa ila kama itakuwa ni ngumu sana kuchagua moja kati ya haya machaguo mawili basi mimi nitakusaidia kuweza kuyachagua” mwanaume huyo ambaye hakujulikana hakuwa na haraka kabisa wakati wa kuyatoa maelezo hayo, alitulia kusikiliza jibu la mheshimiwa huyo.
“Hahah hahaha hahahah nadhani bado wewe ni mgeni ndani ya hili jiji”
“Hata wewe hili jiji ulilidandia tu bwana kijazo na ukataka kuligeuza lionekane lako kwa nguvu, au nakosea?”
“Wewe ni nani?”
“Muda sio mrefu sana utanijua”
“Wanaume huwa wanakutana uso kwa uso wanapofanya mazungumzo kama haya, unajisifia huku umejificha nyuma ya simu? Jitokeze nikufahamu kama wewe mwanaume kweli”
“Ni bahati kwako tunaongea kwenye simu kwani kama tungeonana kama unavyotaka wewe basi ungerudi kwako ukiwa na mkono mmoja na mguu mmoja tu pekee hivyo wewe ndiye unatakiwa kushukuru kwa hili la kuongea na mimi kwenye simu na sio ana kwa ana. Nadhani umenielewa kile ambacho nilikwambia hivyo unatakiwa kuanza kukifanyia kazi wakati huu na nakupa masaa ishirini na manne tu uwe umefanya maamuzi yako ya mwisho” simu ilikatwa baada ya kupewa hayo maelekezo. Hayakuwa ya muda mrefu sana lakini yalikuwa yanaeleweka vizuri, alishangaa sana mtu ambaye alikuwa anatoa amri kila siku eti naye alikuwa anatishiwa kwenye simu.
“Max, hahahahahah hahahaha kama ulifanikiwa kuishi kwa kuzikwa, saivi nitakutia kwenye mafuta ya moto nishuhudie ukiwa unaungua kwa macho yangu halafu kama utapona tena basi nitakuacha uendelee na maisha yako” mzee huyo alitamka kwa hasira sana akiwa anatoka eneo hilo ambapo walinzi walikuwa makini sana kuhakikisha anakuwa salama wakati wote.


Mwanaume ambaye alimvamia Dax hakuwa mbali na lile eneo wakati umeme unarudi na Dax anajikuta yupo mwenyewe pale. Mwanaume huyo hakuwa mwingine, mawazo ya Dax yalikuwa sahihi kabisa, kipindi hicho mvua ikiwa inayesha kwa kasi sana maeneo hayo Max alikuwa juu ya paa moja la nyumba akiwa amesimama na begi mkono mmoja na mkono mwingine alikuwa amelishika shoka jipya kabisa.
Alikuwa hapo akiwa anamtazama mwanaume mwenzake jinsi alivyokuwa akihangaika pale chini tena akiwa mwingi wa wasiwasi sana na ile karatasi ambayo alikuwa anaisoma. Dax aliondoka kwa kukimbia kwa kasi sana na kila ambacho alikuuwa anakifanya DONNY alikuwa akimshuhudia na wakati huo alikuwa ameitoa mask yake usoni, uso ulikuwa wazi unanyeshewa na mvua. Baada ya kukamilisha kitu ambacho kilimpeleka ndani ya hilo eneo alitoweka haraka sana na kwenda mahali ambako hakuna aliyekuwa anajua.
“Kiongozi” ilikuwa sauti ya mwanaume ambaye alienda kumpokea Max wakati anaingia ndani ya jumba moja la ghorofa tatu. Mtu huyo alionekana kuwa mkubwa sana kwake ila alionyesha hali ya kumheshimu sana mtu huyo.
Walikuwa ndani ya Mbezi Beach karibu kabisa na ufukwe wa bahari, huko ndiko walikokuwa wanaishi watu hao. Mwanaume baada ya kupokelewa mzigo huo, waliondoka wakiwa wameongozana kuelekeaa kwenye lifti ambayo iliwapeleka mpaka vyumba vya chini kabisa. Aliyekuwa amempokea Max alikuwa ni mwanaume wa kazi James masalia ya DRAGON BOYS na ndiye ambaye alimuokoa Max na kumfanya aendelee kuipata pumzi ya bure kabisa.
“Nimemuacha hai”
“Kwanini”
“Kwa sababu yeye kuwa hai sisi tunapiga hatua ya mbali zaidi, kama ningeamua kumuua basi ningepata mzigo lakini kile ambacho nimekidhamiria nisingeweza kukifanikisha”
“Unataka kuniambia una mpango upi mwingine?”
“Nilitaka huyu afikishe taarifa kwao kwamba mimi nipo hai na bado ninaishi”
“Kwahiyo umejitambulisha kwake?”
“Hapana, kuna ujumbe nimeuacha na nina imani ameelewa umetoka kwa nani kwa sababu ameondoka pale akiwa anatetemeka sana na ile kauli niliyo iandika pale ni yeye pekee ndiye ambaye aliwahi kuisikia kutoka kwenye kimywa changu”
“Nadhani umekosea sana kufanya hawa watu watambue kwamba bado upo hai”
“Hicho ndicho nilikuwa nakitaka, nataka watu hawa wapate mshtuko mkubwa sana na hilo litakuwa moja kati ya anguko lao kubwa mno na hizi nyaraka zipo kwenye mikono yetu kwa sasa hivyo kazi itakuwa rahisi kuimaliza. Kuchanganyikiwa kwao kutafanya waanze kufanya mambo kwa presha sana na hatutawapa nafasi nyingine ya kuweza kujiandaa mpaka presha yao ije kuisha kazi imesha isha kisha sitataka tena kukaa ndani ya nchi hii. Nitaondoka moja kwa moja”
“Sawa kiongozi lakini umeumia”
“Usijali ni jeraha dogo sana hili James”
“Kwahiyo kwa sasa unafuata mpango gani?”
“Tutazipitia hizo nyaraka zote na baada ya hapo anaanza kufa mmoja mmoja kila ambaye anahusika nazo”
“Hata raisi?”
“Yeah, lazima nimuue”
“Huoni kama itaibua mambo mengine ambayo yanaweza kuleta wasiwasi kwa wananchi?”
“Ni bora wapate shida kwa muda mfupi kuliko kuwa watumwa kwa maisha yao yote”
“Jifute damu hizo na ubadilishe hayo mavazi haraka” James aliongea kama ishara ya kumwambia kwamba alitakia kujiweka vizuri kwani kulikuwa na ugeni ndani ya nyumba hiyo. Max alimwangalia sana mwanaume huyo.
“Whaaaaaat? James, Noo” aliongea akiwa anamsogelea na kumkaba shingo yake kwa nguvu na hasira kubwa sana.
“I’m sorry boss” mwanaume huyo alitamka kuomba samahani kwa kile ambacho kilikuwa kinaendelea.
“Kwanini umeruhusu familia yangu ije huku?”
“Sio mimi ni mkeo ndiye kataka hivyo kwa sababu mwanao alikuwa anagoma hata kwenda shule bila kukuona wewe”
“This is one of the biggest mistake James”
“Nadhani unapaswa kuongea na mkeo kuhusu hili” mwanaume aliiondoka hapo kichwa kikiwa kimepata moto sana, alivaa vizuri na kujiweka kwenye hali ya usafi kisha akapanda juu sebuleni ambapo baada ya kufika tu alipokelewa na sauti ndogo na laini sana yenye furaha tele.
“Dady” ni binti yake ambaye alikuwa anaitwa Naima ndiye ambaye alimkimbilia kwa furaha sana na kumkumbatia baba yake. Alimpokea mwanae kwa furaha sana na kumbeba huku akiwa anamzungusha hewani kwani alikuwa anampenda isivyo kawaida na hakuwa tayari kuona kitu chochote kinasogea katikati ya mwanae na mkewe.
Akiwa amembeba mwanae na kucheka nae kwa furaha sana kwenye kona moja alimuona mwanamke mrembo sana akiwa ameegamia kona hiyo na kumtazama mwanaume huyo kwa furaha kubwa sana isiyo isha hamu. Alikuwa anainjoi kumuona baba na mwana wakiwa kwenye furaha kubwa furaha ambayo yeye hakuipata huko nyuma lakini kwa wakati huo alikuwa anaipata kupitia mumewe na mwanae. Ilikuwa inamkumbusha mwanamke huyo mrembo kwamba duniani hata kama utakuwa na nini ila hakuna kitu bora kuizidi familia, familia ndiyo kila kitu na familia ndipo zilipo baraka za furaha kwa mwanadamu yeyote yule.
Mwanaume baada ya kuinua macho yake na kumwangalia mwanamke huyo alitabasamu, mkewe alikuwa anazidi kuwa mrembo kila siku moja ilivyokuwa inasogea mbele. Alimwachia mwanae na kumwambia akacheze mezani angeenda kumchukua tena na wakati huo alisogea sehemu ambayo alikuwepo mkewe na kumbeba kwa furaha sana huku wakipigana mabusu ya kuonyesha jinsi walivyokuwa wamekumbukana sana.
Alimbeba mkewe mpaka chumbani ambapo alihakikisha anampatia haki yake kama mume na baada ya hapo alihitaji waweze kuongea na kujua sababu ambayo imemfanya mwanamke huyo kumfuata maana alimkataza kabisa kufanya jambo kama hilo na ingekuja kuwa hatari kubwa sana kwa familia yake ndiyo maana alitaka wabaki kuishi huko huko nje ya nchi.
“Kwanini mmekuja Tanzania tena?”
“Ni kwa sababu nakupenda sana mume wangu, mimi sikuwa tayari kuishi maisha ya upweke tena kwenye maisha yangu. Hii miaka kumi na mbili ambayo nimekuwa karibu yako ndiyo miaka yangu bora zaidi kuwahi kuishi na kujihisi kama mwanadamu, kila siku nimekuwa nahitaji kuwa karibu na mume wangu tangu siku ya kwanza nimegundua kwamba nafsi yangu inakuhitaji siku zote sasa unahisi ningewezaje kuishi mwenyewe? Mwanao kila akiamka asubuhi alikuwa amezoea kukuona na angekuita kwa furaha sana ndipo aende shule kitu ambacho kimekuwa tofauti sana kwa huu mwezi mzima, kila akiamka swali la kwanza ni yuko wapi baba, amegoma hata kwenda shule muda wote analia anataka kukuona baba yake, unahisi mimi ningefanya nini mume wangu? Nakupenda sana” mwanamke ambaye alikuwa anayaongea hayo maneno alikuwa ni Ariana, dada yake Siza ambaye Max aliachiwa majukumu ya kuweza kumlinda.
Huyo ndiye alikuwa mkewe na alimzawadia mtoto mmoja wa kike Naima ambaye mpaka wakati huo aliikamilisha furaha ya wao kuwa na familia ambayo walitamani sana kuiita familia bora lakini mbele yao kulikuwa na mambo makubwa sana na ya kutisha mno ndiyo maana Max aliogopa sana baada ya kujua kwamba familia yake ilikuwa imerudi tena ndani ya nchi. Mwanaume hakuongea jambo lolote tena zaidi ya kumkumbatia mkewe kwani aliyo yaongea yalikuwa ya kweli na aliyaongea kwa uchungu mkubwa isivyo kawaida.

64 inafika mwisho.
 
HADITHI: JIJI LA KAMARI (GAMBLING CITY)
MTUNZI: FEBIANI BABUYA
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
WHATSAPP: 0621567672
AGE: 18+

Episode 65
“Nitawalinda kwa gharama yoyote ile” aliongea akiwa anamuacha mkewe apumzike baada ya kupitiwa na usingizi na ndipo akarudi kwa James.
“Kwa muda gani ulijua kwamba watarudi?”
“Siku mbili”
“Kwanini haukuniambia?”
“Alinisisitiza sana kwamba kama ningekwambia basi asingenisamehe kamwe kwenye maisha yangu maana ningekuwa nahatarisha hali ya mtoto”
“James unajua mpaka hivi ninavyozungumza kuna watu huenda wana picha za mwanangu na mke wangu?”
“Unahisi wanaweza wakawa wamehisi kwamba kuna mtu mgeni amefika ndani ya nchi?”
“Denis Kijazo kila taarifa za nchi hii anaweza kuzipata kwa dakika kumi tu pekee unahisi mke wangu wakati anaingia pale uwanja wa ndege hakuna kitu ambacho watakipata kutoka kwake?”
“Niliangalia sana usalama wa kamera pale sidhani kama inawezekana kuna tatizo lolote”
“Mimi nilifanya kazi ndani ya shirika letu la kijasusi, najua una uwezo mkubwa sana kwenye mitandao ila ninacho kizungumzia hapa ni kitu tofauti kabisa. Sehemu kama zile huwa zina kamera za siri sana ambazo ili kuzifungia ni mpaka ujue kwamba zipo na najua haukuwa ukijua kuhusu jambo hilo je una imani bado kwamba kutakuwa na uhakika wa usalama wao na wako pia?”
“Nisamehe sana kiongozi”
“Huu sio muda wa kuombana msamaha ila ni muda wa kujua kwamba ni kitu gani tunatakiwa kukifanya baada ya hapa. Nina imani kwamba picha zao, mke wangu na mwanangu mpaka sasa kuna watu wanazo kitu ambacho litakuwa suala la muda tu kufanikiwa kutufikia hivyo tunatakiwa kuifanya kazi hii kabla ya wao hawajafanya lolote lakini kuna ombi moja ambalo ninalo kwako”
“Nahitaji kuimaliza kazi hii na nashukuru sana kwa mchango wako mkubwa mpaka sasa tupo wote ila kwa sasa naomba uilinde familia yangu.”
“Hii tayari ishakuwa familia yangu hivyo hakuna mtu hata mmoja ambaye atafanikiwa kuigusa kama mimi bado nipo hai na kama mtu huyo atataka kufanya hivyo basi anatakiwa kuhakikisha kwamba mimi nakufa kwanza” wanaume hao walikumbatiana kisha kila mtu akaingia kwenye majukumu yake ya kawaida japo Max alikuwa ni mtu mwenye wasiwasi sana.
Kurudi kwa Max ilikuwa ni habari mbaya sana kwa Denis Kijazo lakini habari mbaya zaidi ni kwamba kijana wake alipoteza mzigo wa mhimu sana ambao kwa maelezo yake alidai kwamba ungeweza ukampoteza kabisa duniani. Nyaraka ambazo ziliibiwa zilikuwa ni mhimu sana kwake na ndiyo maana alimpa Dax masaa ishirini na manne tu awe amefanikiwa kuzipata vinginevyo angedili naye mwenyewe. Alikuwa yupo kwenye gari yake anaelekea Ikulu ambako alionekana kuwa na mazungumzo ya mhimu sana na mheshimiwa raisi wa taifa la Tanzania.
Akiwa kwenye gari aliichukua simu yake na kujiweka sawa kisha akaipiga kwa kijana wake ambaye alikuwa anamwamini sana. Simu hiyo ilikuwa inaelekea Ngarenaro ya chini Jengo la saba sehemu ambako ilikuwepo ngome yake ya siri ambayo ilikuwa inamuingizia mabilioni ya fedha. Simu ilimkuta Ted akiwa amekaa na vijana wake wakiwa wanafunga mahesabu ya pesa, aliipokea haraka sana na kusogea pembeni ili kuweza kumsikiliza bosi wake.
“Mzigo ambao Max alienda kuuchukua kwa yule mzee umepotea na upo kwenye mikono ya Max”
“Hilo haliwezekani bosi, huyo mtu alikufa miaka kumi na mbili iliyopita”
“Hata mimi nilijua hivyo ila kwa sasa kinachotakiwa ni mzigo kupatikana kisha ndo tuanze kujua kwamba huyu mtu aliponaje wakati alizikwa. Nadhani unajua ni kipi ambacho unatakiwa kukifanya lakini kabla haujafanya jambo lolote pitia kamera zote za uwanja mkubwa wa ndege ambao unapokea watu kutoka pande zote za dunia kisha kama kutakuwa na kitu utakipata utanipa taarifa”
“Sawa mkuu” Ted alikata simu na kuhema kwa nguvu sana, hiyo kazi haikuonekana kwamba itakuwa nyepesi sana japo haikuwa inampa mashaka maana alizoea sana kufanya kazi za namna hiyo. Alirudi kwa vijana wake na kumuita Kenedy pembeni ambaye naye alikuwa akimwamini sana.
“Mimi leo natakiwa kwenda Dar es salaam kuna tatizo kubwa sana limetokea. Nyaraka za mhimu sana za bosi ambazo zinaweza kumpoteza zimepotea hivyo natakiwa kwenda kuhakikisha zinapatikana na hii sehemu naiacha kwenye mikono yako ila na wewe unatakiwa kuja Dar es salaama haraka sana hesabu zikikamilika”
“Unajua ni nani amezichukua?”
“Yeap, ni Max”
“Unamaanisha yule mlinzi wa zamani wa raisi Teodensia Mpanzi ambaye alizikwa”
“Kuhusu kuzikwa unasema wewe ila yupo hai na tunatakiwa kujua kwamba ni wapi yupo, anataka kufanya nini na alikuwa wapi mpaka ajitokeze baada ya miaka hii kumi na miwili?” Maelezo ya Ted yalimchanganya sana Kenedy, ni kama alikuwa anasimuliwa simulizi za zamani ambazo zisingekuwa kweli ila kwa bahati mbaya sana alitakiwa kukubaliana na huo ukweli ambao alikuwa anapewa wakati huo.
“Kwahiyo ni kipi kinafuata kwa sasa?”
“Tunatakiwa kuangalia marejeo ya video za pale uwanja wa ndege kwa miezi kadhaa nyuma ila nataka za kuanzia leo kisha zingine zifuate” ilikuwa ni amri ambayo mara moja ilianza kutekelezwa hapo. Walisogea kwenye chumba cha kazi ambacho kilikuwa na komputa nyingi sana na kuna vijana ambao walikuwa hapo wakiwa makini sana kucheza na komputa hizo.
Walikuwa makini sana kwenye kukagua kila hatua na kila mtu ambaye alikuwa anapita eneo hilo taarifa zake zote zilikuwa zinajitokeza kwenye komputa hizo kitu ambacho kiliwarahisishia sana kazi wanaume hao. Walizipitia kwa muda mrefu sana na mara ghafla walimuona mwanamke mmoja mrembo sana akiwa na mtoto.
Ted ambaye alikuwa ameanza kusinzia kutokana na kukaa muda mrefu alishtuka sana baada ya kumuona mwanamke huyo akahitaji watu hao wasimamishe hapo kwanza.
“Stop” aliongea akimpa ishara mwanaume mmoja kuweza kuirudia video hiyo na kuikuza picha ya mwanamke huyo pamoja na mwanae. Jina lake lilikuwa linasoma mrs Howartson kutokea ndani ya nchi ya Marekani, kwake jina halikuwa na shida sana ila kitu ambacho kilimshtua ni mtoto ambaye alikuwa na mwanamke huyo, mtoto alikuwa anafanana sana na mtu ambaye aliamini kwamba alikuwa anamfahamu sana.
Mwanaume alisogea mwenyewe kwenye komputa nyingine ambayo ilikuwa pembeni yake na kuandika jina la Max. zilikuja taarifa za mtu huyo kwa sababu alikuwa maarufu sana na alidaiwa kuwa ndiye gaidi hatari zaidi wa taifa la Tanzania kwa kumuua raisi miaka kadhaa ambayo ilipita. Aliikuza picha ya mwanaume huyo akaikuza na ya mtoto kisha akawa anaangalia kwa zamu zamu kama kufananisha kitu. Baba na mtoto walikuwa wanafanana vitu vingi sana kama ungewaangalia kwa umakini mkubwa na ndiyo sababu ambayo ilimshtua sana baada ya kumuona mtoto huyo akiwa na mama yake.
“Yes, nimekupata Max”
“Mkuu unamaanisha nini?”
“Hii ni familia yake, huyo mwanamke mrembo ni mkewe na huyo binti mrembo ni mwanae wa damu. Mchezo huu unaenda kuwa mrahisi sana na mimi siku zote ndiye huwa nazichanga karata kwenye huu mchezo”
“Unataka kufanya nini?”
“Binadamu yeyote yule duniani hata kama atakuwa mgumu au katili kiasi gani, udhaifu wake mkubwa huwa ni familia. Mbele ya familia hata watu wa kutisha huwa wanapiga magoti wakiomba watu wao wanao wapenda waachiwe. Kama tukiipata familia yake basi niamini mimi atakuja yeye mwenyewe popote ambapo nitahitaji aje na kwa sasa nataka nishuhudie anavyokuja kufufuka tena kwenye mikono yangu” Ted aliongea kwa furaha sana akiwa anaangalia mpaka mwanamke huyo anavyotoka ambapo alienda kupokelewa na mwanaume mmoja ambaye alikuwa anamsubiria kwenye gari moja ya kifahari sana.
Alimpokea mwanamke huyo kwa heshima na kumpandisha kwenye gari hiyo na mtoto kisha akaondoka eneo hilo akionekana kuwa makini sana huku mbele yake kukiwa na gari moja na nyuma yake kukiwa na gari nyingine na hao wote walikuwa ni walinzi ambao walitakiwa kumlinda mwanamke huyo na mtoto.
Ted alibaki anamtazama huyo mwanaume kwa umakini mkubwa sana ambaye alikuwa anamlinda mke wa max akifahamaika kwa jina la mrs Howartson. Aliikuza na picha ya mwanaume huyo akiwa kama anaifananisha pia na alikuwa ana uhakika kwamba aliwahi kuiona mahali japo ni zamani sana. Kumbukumbu zake zilimrejesha ule usiku ambao walikuwa kwenye nyumba ya Madilu Mpagazi walipokutana na DRAGON BOYS, huyo ndiye pekee ambaye alifanikiwa kuishi na alimdharau sana kwa kipindi kile lakini ndiye alikuwa chanzo cha mambo yaote hayo kutokea.
“Ooooh shiiit! Nilifanya kosa kubwa sana kumuacha hai huyu mjinga na nahisi kwamba yeye ndiye ambaye alimsaidia Max kutoka kwenye kifo hivyo natakiwa kurudi Dar es salaam haraka sana na kama kuna kitu mtagundua basi mtatakiwa kunitaarifu haraka sana hawa watu natakiwa kuwaweka kwenye mkono wangu kwa muda mchache sana ujao”
“Sawa mkuu” wate waliitikia wakati huo mwanaume huyo alikuwa anatoka ndani humo na vijana kadhaa ili kuweza kusafiri mpaka ndani ya jiji la Dar kwenda kuikamilisha kazi ambayo alikuwa ameianza na bosi wake alihitaji yeye aimalize mapema sana.


IKULU
Bado ilikuwa ipo chini ya Justin Mtadei, mwanaume ambaye aliingizwa hapo baada ya kifo cha Teo akiwa kama ameikaimu nafasi yake na miaka ile ya kwanza haikuhesabika kama yake ndiyo maana mpaka wakati huo alikuwa kwenye hicho kiti akiwa anaimalizia miaka yake ya kula mema ya nchi. Siku hiyo alitembelewa na bosi wake ambaye ndiye alimuweka kwenye hicho kiti ili kuweza kulinda maslahi yao kwa ujumla na kuhakikisha kwamba mambo yao yanaenda vyema na kuhusu watanzania hawakuona kama ni biashara ambayo ilikuwa inawahusu.
“Karibu sana kiongozi, imekuwa ni muda mrefu sana tangu uweze kunitembelea hapa”
“Huwa sioni sababu ya msingi kuzunguka kwenye hili eneo kama mambo yangu yanaenda vizuri hivyo ukiniona nakuja hapa basi ujue kwamba kuna sehemu mambo hayapo sawa”
“Nini shida kiongozi?”
“Max bado anaishi”
“Nambie unanitania bosi” raisi aliongea kwa wasiwasi hata lile tabasamu lake lilipotea kabisa kwenye uso wake.

65 inafika mwisho.
 
Back
Top Bottom