Eneo la kwa Mama John Mbeya liligeuka uwanja wa vita kwa muda jioni baada ya kampeni za CCM kumalizika. Mara baada ya msafara wa Magufuli na viongozi wengine wa CCM kuondoka, gari aina ya Land Cruiser lenye machata ya Sugu 2015 lilipita likisindikizwa na vijana waliokuwa wakishangilia.
Mara baada ya hapo kila bajaj au bodaboda iliyokuwa ikikatiza eneo hilo ikiwa na bendera ya CCM ilikuwa ikishambuliwa kwa mawe huku bendera nyingine zikiporwa. Kuna wakati hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya foleni kuzidi na magari kutotembea ambapo kundi la vijana liliifuata bajaj iliyokuwa imepakia watu waliovalia sare za CCM na kuanza kuwafanyia vurugu na mmojawapo alipojaribu kujibizana nao walimkokota kwenye mtaro na kuanza kumpiga. Baada ya muda umati wa watu ulijaa na mawe yalianza kurushwa huku wanawake na watoto waliokuwa wakirejea majumbani wakilizamika kuanza kukimbia kujiokoa na baadhi kuishia kuanguka mitaroni na bodaboda kukosa kosa kuwagonga watu.
Hii imenisikitisha sana, nadhani inabidi ifikie hatua viongozi wa vyama vyote wapige marufuku vurugu za aina hii kuwe na kuvumiliana kila mmoja afanye kampeni bila kubugudhiwa. Kama alivyosema Mbatia kuwa hawatamshambulia mtu au kumsema yeyote vibaya ni muhimu mbegu hii waipandikize kwa wanachama wa matawi yote. Na Magufuli kasema kuwa hatamsema mtu wao pia waihubiri hiyo kwa wanachama wao ili kampeni ziishe kwa amani.