Oleksiy Vadatursky: Tajiri wa nafaka wa Ukraine auawa katika shambulio la Urusi
Mfanyabiashara mmoja tajiri zaidi nchini Ukraine ameuawa akiwa na mkewe katika shambulizi ‘’kubwa’’ la Urusi katika mji wa kusini wa Mykolaiv.
Oleksiy Vadatursky, 74, na mkewe Raisa walikufa wakati kombora lilipopiga nyumba yao usiku kucha, maafisa wa eneo hilo walisema.
Bw Vadatursky alimiliki Nibulon, kampuni inayohusika na mauzo ya nafaka nje ya nchi.
Pia alikuwa amepokea tuzo ya ‘’shujaa wa Ukraine’’.
Meya wa Mykolaiv Oleksandr Senkevych alisema huenda ni mashambulizi makubwa zaidi ya Warusi katika jiji hilo kufikia sasa.
Kulikuwa na uharibifu wa hoteli, uwanja wa michezo, shule mbili na kituo cha huduma, pamoja na nyumba.
Mykolaiv iko kwenye njia kuu kuelekea Odesa, bandari kubwa zaidi ya Ukraine kwenye Bahari Nyeusi, na imepigwa mara kwa mara tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake tarehe 24 Februari.