Shukrani sana Mkuu nilikuwa nasubiri uchambuzi wako. Mpaka sahivi nimeshindwa kulala sijajua nini kitaendelea huko.
Sifahamu nini kitaendelea, lakini Marekani amewekwa kwenye kikaango kibaya sana: Kuvimbisha misuli ili atunze uso wake mbele ya Ulaya au Kufyata mkia kwa kufanya APPEASEMENT POLICY kama Neville Chamberlain alivyofanya mwaka 1939 baada ya Ujerumani kuvamia Czechslovakia. Akivimba msuli na kufanikiwa, basi atatuma ujumbe hadi Uchina kuhusu kuvamia Taiwan, pia hata kumuogopesha Serbia kuvamia Kossovo.
Ujumbe tunaoupata hapa ni huu: Kama Marekani akishindwa kuilinda Ukraine, unadhani ataweza kuilinda Taiwan ??? Binafsi sina jibu la moja kwa moja, kwasababu mazingira ya kisiasa barani Ulaya na Mashariki ya mbali yako tofauti. Ulaya mataifa mengi hayako na Marekani kwenye baadhi ya sera zake, na tofauti kabisa na zamani, siku hizi Ukomunisti haupo hivyo nchi za Umoja wa Ulaya zinaweza kukaa na kuzungumza na Urusi na kuelewana.
Nchi kama Ufaransa na Ujerumani zinacheza karata vizuri kwasababu zitapata faida kubwa sana endapo Marekani atadhalilika na ushawishi wake kupungua barani Ulaya. Ikumbukwe Umoja wa Ulaya ulitaka kuanzisha jeshi lake tangu miaka ya 50's kipindi cha Jean Monnet na Charles De Gaulle lakini aliyewafitini kufanya hivyo ni Marekani kwa kuleta NATO.
Wafaransa walichukia kiasi cha kufanya vituko hadi kujitoa NATO. Mpaka mwaka majuzi kwenye bunge la Ulaya Nigel Farage alikuwa anamshambulia sana Ulsura Von Deleyen alivyotoa pendekezo la kuanzisha jeshi la Ulaya. Usione Macron na Olaf wanaenda sana Urusi, na kujihusisha sana na Putin, huu mgogoro una maslahi sana kwao. Tena wao ndiyo wana mkono wa juu kuliko Marekani kwasababu Uingereza haimo tenda ndani ya UMOJA WA ULAYA.
Sasa ili Marekani afanikiwe kwenye hili anahitaji azungumze kwa sauti moja na kutenda kwa nguvu moja na wenzake wa nchi za Magharibi (The Atlantic Alliance), lakini bahati mbaya haipo hivo kama zamani. Nchi kubwa ndani ya Umoja wa Ulaya kama Ujerumani na Ufaransa zina maslahi yao binafsi, pia kwao Urusi ni changamoto wanayoweza kuimudu.
Mashariki ya mbali kuna utofauti kidogo na Ulaya. Tofauti na Urusi, Uchina anapambana mataifa mengi ambayo anagombania nayo mipaka, hayana umoja wao, huku yakiendeshwa na rimoti ya Marekani kutoka Washington. Hapa Marekani yuko na mkono wa juu, shida inakuja pale ambapo mataifa haya yote yamefungamana sana kiuchumi na Uchina. Hebu ona:
Ukiitoa Vietnam peke yake, nchi kubwa Mashariki ya mbali kama Japan, Korea-Kusini, Singapore, Ufilipino na Australia wanaongozwa kijeshi na Marekani. Hebu fikiria haya yafuatayo, ndiyo uone jinsi gani Marekani ni muhuni:
1. Japan - Hana jeshi anategemea Ulinzi kutoka Marekani.
2. Korea Kusini - Ana jeshi lakini linaongozwa na Majenerali wa Marekani.
3. Australia - Iko chini ya Uingereza
4. Ufilipino - Lilikuwa ni koloni la Marekani.
NB: Hivyo Marekani anaweza kucheza vizuri na Mashariki ya mbali, kuliko Ulaya kwasababu kule mbali na kuwa na vikosi vya jeshi nchini Ujerumani, hawezi kuwapelekesha wajerumani endapo watamkazia. Pia Ujerumani haina tatizo na Urusi kwasababu wanahistoria ndefu ya pamoja, tofauti kabisa na Japan ambao hawapikiki chungu kimoja na Uchina.
Sasa mpira kapewa Marekani, tuone atachezaje: Maana vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi haviwezi kufanya kazi kwasababu ili vifanye kazi ni lazima nchi zote za Umoja wa Ulaya zikubali kupambana na Urusi, kitu ambacho siyo rahisi, japo kinaweza kutokea.