Tanzania Yakubali Kulipa Bilioni 237 ya Fidia Kwa Kuvunja Mkataba Mwaka 2018. Yatanguliza Bilioni 92
Tanzania na kampuni ya uchimbaji madini kutoka Australia, Indiana Resource Limited zimefikia makubaliano ya fidia ambapo Tanzania itailipa kampuni hiyo dola za kimarekani milioni 90 kutokana na kuvunja makubaliano katika Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill uliopo mkoani Lindi. Tanzania imeshatanguliza malipo ya awamu ya kwanza ya dola milioni 35 sawa na bilioni 92.
Haya yameelezwa leo Julai 29,2024 katika taarifa iliyotolewa na kampuni ya Indiana Resouces ambayo inaeleza kuwa kampuni hiyo imekubali kupokea ofa ya Tanzania ya dola milioni 90 sawa na bilioni 237, kiwango ambacho ni kidogo kuliko kile cha awali ambacho Tanzania kiliamriwa kulipa na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).
Mnamo Julai 14, 2023, Tanzania ilitakiwa kuilipa kampuni ya Indiana Resources Ltd, dola milioni 109 ambazo ni sawa na takribani shilingi bilioni 250 baada ya kituo hicho kujiridhisha uwepo wa ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill.
Kampuni hiyo imeeleza kuwa imeamua kukubali kiwango hicho kupunguza mzigo wa gharama utakaotokana na kuendelea na ubishano katika vyombo mbalimbali vya kisheria. Katika makubaliano hayo Tanzania itatakiwa kumalizia kiwango kilichobaki kwa awamu mbili, ambapo mpaka Oktoba 24 itatakiwa kulipa dola milioni 25 na ifikapo Machi 30,2025, itatakiwa kulipa dola milioni 30.
SOURCE: THE CHANZO