Walioiba mabilioni ya EPA wafilisiwa
Cassian Malima, Dodoma
Daily News; Friday,August 22, 2008 @00:01
Serikali imekamata mali zote za wamiliki wa kampuni 13 kati ya 22 zilizothibitika kuhusika na uchotaji wa mabilioni ya shilingi kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Rais Jakaya Kikwete aliliambia Bunge jana.
Alisema licha ya kuzuiwa hata kwa magari wanayomiliki watu hao, pasi zao za kusafiria pia zinashikiliwa wasikimbie nje ya nchi. Licha ya hatua hiyo, Rais Kikwete alisema ameiagiza Benki Kuu (BoT) kufunga akaunti hiyo ambayo kwa mujibu wake ina zaidi ya Sh bilioni 130 na fedha hizo ziwekwe katika mfuko mkuu wa serikali.
"Ikitokea mtu ajitokeze kudai (kutokana na EPA) tutamlipa," alisema Rais na kuiagiza serikali kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya dharura ya malipo kama hayo. Aliwasisitizia wananchi kufahamu kwamba fedha hizo si za umma, ni za watu wa nje ambao hawakupelekewa fedha zao.
Pia ameagiza kwamba fedha zitakapopelekwa serikalini baadhi zitumike kuongeza ruzuku ya mbolea na dawa za mifugo. Alisema fedha nyingine zitapelekwa katika Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) zitumike kutoa mikopo ya kilimo na kama sehemu ya mchakato wa kuanzisha benki ya kilimo.
Katika hotuba yake hiyo bungeni iliyoanza saa 6:17 mchana hadi saa 9:42 alasiri, Rais Kikwete alisema amekubali ombi la timu aliyoiunda Januari mwaka huu kuendelea kufuatilia kampuni hizo na kuziruhusu kuendelea kulipa fedha zilizochukuliwa hadi Oktoba 31, mwaka huu.
Timu hiyo inaongozwa na Mwanasheria Mkuu akishirikiana na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). "Ifikapo Novemba mosi asiyelipa… mahakamani, tumewapa fursa ya kutosha," alisema. Kwa mujibu wa Rais Kikwete, hadi timu aliyoiunda ilipowasilisha ripoti ya uchunguzi wao kwake Jumatatu wiki hii ilikuwa 'imewabana' watuhumiwa hao na kuweza kukusanya Sh bilioni 53.7.
Alisema kwa mujibu wa makubaliano na timu, wadaiwa wengine wanapaswa kulipa fedha zitakazofanya kiasi kilichokusanywa kufikia Sh bilioni 64 ifikapo Oktoba 31, mwaka huu. Rais Kikwete hakuzitaja kampuni ambazo wamiliki wake mali zao zimekamatwa.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo, Januari mwaka huu alizitaja kampuni hizo kuwa ni Bencon International, VB & Associates, Bina Resorts, Venus Hotel, Njake Hotel & Tours, Maltan Mining, Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment, Ndovu Soaps, Navy Cut Tobacco, Changanyikeni Residential na Kagoda Agriculture Ltd.
Rais Kikwete alisema hatua kali zimechukuliwa dhidi ya kampuni hizo 13 baada ya kubainika kwamba zilichota Sh bilioni 90.3 kwa kutumia kumbukumbu, nyaraka na hati za kughushi. Juu ya kampuni tisa zilizosalia, Rais alisema zililipwa Sh bilioni 42.6 ambazo pia inaaminika hazikustahili kulipwa kwa sababu hazikuwa na nyaraka zilizoonyesha stahili za malipo hayo, lakini imekuwa vigumu kuhakiki malipo hayo kutokana na ukosefu wa nyaraka.
Rais alisema kamati yake inasubiri taarifa kutoka kwa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) na Polisi wa nchi ambazo Tanzania ina makubaliano ya kushirikiana nao ili kupata taarifa ya kampuni hizo tisa. Ingawa hakuzitaja, kumbukumbu zinaonyesha kampuni hizo ni G&T International, Excellent Services, Mibane Farm, Liquidity Service, Clayton Marketing, M/S Rashtas, Malegesi Law Chambers, Kiloloma and Brothers na Karnel Ltd.
Rais Kikwete alitumia zaidi ya nusu saa kuzungumzia suala hilo la EPA, akianza kwa kueleza historia nzima ya akaunti hiyo aliyosema iliundwa mwaka 1985 wakati taifa likiwa linakabiliwa na matatizo ya uchumi na ukosefu wa fedha za kigeni. Alisema awali akaunti hiyo ilikuwa ikitunzwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa ajlii ya kupokea fedha za malipo ya huduma na bidhaa ambazo wafanyabiashara wa Tanzania walikuwa wakinunua kutoka nje.
Kwa kuwa malipo hayo yalifanyika kwa shilingi ya Tanzania na baadaye kukawa na mlundikano kutokana na kutokuwa na fedha za kigeni, akaunti hiyo ilihamishiwa BoT na wakati fulani ilifikia kuwa na akiba ya Sh bilioni 600, alisema. Aliwaambia wabunge waliofurika kumsikiliza na waliokuwa watulivu, kwamba inaonyesha wizi huo uliwezekana kutokana na akaunti hiyo kutofanyiwa ukaguzi kwa miaka kadhaa kwa kuwa haikuwa mali ya serikali.
Rais alisema ni pale kampuni ya ukaguzi ya nje ya Deloitte & Touche ilipoishtukia akaunti hiyo mwaka juzi na kuamua ndipo ulipotokea mvutano na BoT ambayo iliikatalia na kuitimua. Alisema taarifa hizo zilipomfikia aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji alimwagiza aliyekuwa Gavana ukaguzi uendelee kwa kufanywa na Mkaguzi wa Kisheria ambaye ni Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG).
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kufanya ukaguzi huo uwe huru, iliteuliwa kampuni ya Ernst and Young ambayo ilithibitisha upotevu wa Sh bilioni 133 katika akaunti ya EPA kwa nyaraka za kughushi. Kampuni hiyo ilitoa mapendekezo kadhaa ambayo Rais alisema yamefanyiwa kazi, ikiwamo uundwaji wa timu iliyomkabidhi ripoti Jumatatu na kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Gavana, Dk. Daud Ballali