Tanzania yatoa majibu na msimamo wake kwa Azimio la Bunge la Ulaya la Mei 8, 2025

Tanzania yatoa majibu na msimamo wake kwa Azimio la Bunge la Ulaya la Mei 8, 2025

TAMKO LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KUHUSU AZIMIO LA BUNGE LA ULAYA


Dar es Salaam, 8 Mei 2025

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea taarifa ya azimio lililopitishwa na Bunge la Ulaya tarehe 8 Mei 2025 kuhusu mwenendo wa mashauri ya kisheria yanayoendelea nchini Tanzania. Wakati Tanzania ikiheshimu uhuru wa taasisi wa Bunge la Ulaya na kuthamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya, inaona ni muhimu kufafanua baadhi ya mambo ya msingi na kusisitiza tena dhamira yake ya muda mrefu ya kuzingatia misingi ya demokrasia, utawala bora, na sheria.

Tangu Machi 2021, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitekeleza mageuzi ya kisiasa na kisheria kupitia dhana ya 4R – Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi, na Ujenzi Upya. Mageuzi haya yameleta mafanikio ya dhahiri ikiwa ni pamoja na kurejesha uhuru wa kisiasa, kupanua haki za kiraia, kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, na kupitishwa kwa sheria mpya za uchaguzi mwezi Machi 2024, zilizowezesha kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Tanzania ni nchi huru inayoongozwa kwa mujibu wa Katiba yake na utawala wa sheria. Masuala yote ya kisheria yanashughulikiwa kwa uhuru na mhimili wa Mahakama ambao ni miongoni mwa mihimili ya dola, kwa mujibu wa sheria za kitaifa na kwa kuzingatia viwango na kanuni bora za kimataifa, ambapo Serikali (Tawala) haina mamlaka ya kuingilia mashauri ya mahakama. Hivyo basi, matamko yoyote yanayodokeza au kuhamasisha Serikali kuingilia mashauri yanayoendelea mahakamani siyo tu kwamba hayafai, bali pia yanakwenda kinyume na misingi ya uhuru wa Mahakama kama ilivyobainishwa katika Katiba ya Tanzania na kama inavyohimizwa na Umoja wa Ulaya.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia ina wasiwasi na mwenendo unaojitokeza kwenye azimio la Bunge la Ulaya ambapo baadhi ya wadau wa kimataifa wanatoa maamuzi kwa msingi wa taarifa pungufu au zenye upendeleo, bila kupitia njia rasmi za kidiplomasia. Mtazamo huu unapotosha na kuwasilisha taswira isiyo sahihi kuhusu hali halisi ya mambo nchini.

Soma Pia: Hoja ya azimio la Bunge la Ulaya kuhusu kukamatwa na hatari ya kunyongwa kwa Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema

Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba baadhi ya maendeleo nchini Tanzania, ikiwemo mashauri mahususi ya kisheria, yanashughulikiwa kwa ukaguzi maalum, huku mafanikio makubwa katika maeneo kama uhuru wa vyombo vya habari, ushirikishwaji wa kisiasa, mageuzi ya uchaguzi, na ujenzi wa amani ya kikanda yakipuuzwa.

Wakati Tanzania ikiendelea kuheshimu haki na utu wa kila mtu kama ilivyoainishwa katika Katiba yake, ni muhimu kufafanua kuwa masuala yanayohusu mwelekeo wa kijinsia yameshaainishwa wazi ndani ya mfumo wa Katiba ya Tanzania, sheria za kitaifa, mila, na desturi za jamii. Tanzania inasisitiza kuwa ushirikiano wowote lazima ujengwe juu ya kuheshimiana kwa misingi ya maadili, ikiwa ni pamoja na kuheshimu mamlaka ya kikatiba, mifumo ya kisheria, na utambulisho wa kitaifa, huku ushirikiano wa baadaye ukilenga vipaumbele vya pamoja katika maendeleo, utawala, ukuaji wa uchumi, na ustawi wa watu.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuthamini ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya na iko tayari kwa mazungumzo ya wazi, yenye heshima, na yanayozingatia ushahidi kuhusu masuala ya maslahi na umuhimu wa pamoja. Hata hivyo, mazungumzo haya lazima yajengwe juu ya uwazi, usawa, kuheshimiana, na uelewa kamili wa uhuru wa taasisi za kila nchi, Katiba zake, pamoja na muktadha wa sheria na utamaduni wa kila taifa.

Tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025, Serikali ya Tanzania inathibitisha tena dhamira yake ya kulinda amani, kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, na kulinda haki na uhuru wa msingi wa wananchi wote kwa mujibu wa Katiba.

Tanzania inakaribisha kuendelea kwa msaada kutoka Umoja wa Ulaya na washirika wote wa kimataifa wanaojitokeza kwa nia njema na uelewa ulio sahihi kuhusu safari ya kidemokrasia ya nchi hii, na wako tayari kushirikiana na wale ambao bado hawajafahamu vya kutosha kuhusu maadili na utamaduni wa Kitanzania.

MWISHO


Imetolewa na:
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI – JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

View attachment 3328439
View attachment 3328440
Mmelipuka kama Bashe. Msije kutia huruma baadae.
 
Sijui kama watakuwa wameelewa hao vichwa maji. Cha muhimu tuache kuomba misaada yo yote kutoka nchi hizo kwank huwa ni ya kinyanyashaji mara zote. Wanatuona sisi bado ni koloni lao.

Hili si suala la misaada tu. Hata bila ya misaada, kuna mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu Tanzania imesaini.

Mikataba hii inaifunga Tanzania kutimiza masharti ya haki za binadamu.
 
Rais SSH kwenye suala hili awe mwangalifu Sana kuchagua upande wa kuegemea, asiwasikilize Wala asifuate Misimamo ya hawa Watu ambao wanaonekana kuwa Wanajipendekeza kwake. Endapo kama kweli bado anaupenda uRais wake basi itamlazimu awe mpole na awe na busara kubwa sana katika mchakato mzima wa kutatua Mgogoro huu uliopo.

Rais SSH asipende kuendeleza Malumbano na hao EU, hao EU wana uwezo mkubwa sana wa kuweza kumhujumu, na anaweza akakwama kabisa katika kutawala nchi hii. Ajifunze kupitia kwa yaliyomkumba Rais Robert Mugabe na Zimbabwe kwa ujumla. Mugabe alihujumiwa na EU, alipata taabu kubwa sana katika kuendesha/kutawala nchi hiyo ya Zimbabwe, na hatimaye matokeo yake aliondolewa madarakani 2017 kutokana madhara ya muda mrefu ya hujuma hizo za EU. Rais SSH asipende kuingia kwenye mtego huo alionasa Mugabe. Hadi leo hii Zimbabwe bado haijatulia kabisa kutokana na Vikwazo vilivyowekwa na EU enzi za Utawala wa Mugabe.

Tatizo kuna mkwe kifua kipana ndio mtawala kwa sasa, anamkwepaje mama yetu ili arudi kwenye senses zake? Labda binti aanze kwanza na anaanzaje? Mama karelax kwa kuwa anaamini kifua kipana ana akili sana kwa kuwa ana mwanae!
 
Hili si suala la misaada tu. Hata bila ya misaada, kuna mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu Tanzania imesaini.

Mikataba hii inaifunga Tanzania kutimiza masharti ya haki za binadamu.
Haki za binadam gani tanzania imekiuka!?
 
Swali si haki za binadamu gani Tanzania imekiuka.

Swali ni haki za binadamu gani Tanzania haijakiuka?
Nisanue haki ambazo tz imekiuka zilizoifanya EU itoke shimoni na kutishia vikwazo
 
Hiki ni Kingereza cha Chatgpt. Tumuone alieandika tuone kama alichoandika ataweza kukiongea!

Anyway , alieandika amepoteza muda. Unaonq kabisa watu hawapo serious na wameshiba kodi
 
Sisi watu wa Medical na Psycholog…. Ukiona mtu anatoa maelezo mengi kama hivo; UJUE ni muongo. The world of technology and social media , si vema kudanganya
 
Nisanue haki ambazo tz imekiuka zilizoifanya EU itoke shimoni na kutishia vikwazo
Nakwambia hivii, swali si haki gani zimevunjwa, swali ni haki gani hazijavunjwa.

Taja haki yoyote ya binadamu ambayo haijavunjwa Tanzania.
 
Andiko linasema EU wanapotosha kwa taqrifa zenye mapungufu. I can bet EU committee is more informed kuliko Samia. Hii taarifa imeandikwa na maafisa wa foreign affairs…. Kwakweli ni aibu
 
"Tanzania inakaribisha kuendelea kwa msaada kutoka umoja wa ulaya na washirika wote wa kimataifa"

... mwisho wa kunukuu...


Kwa kuwa hata pesa ya kufanya uchaguzi nchini ni msaada toka nje, Reforms zitafanyika kwenye katiba na tutapata Tume huru ya uchaguzi na Tundu lissu ataachiwa huru.

Tusubiri 🙏
Ikawe sawa na unenavyo
 
Back
Top Bottom