Kwa ujumla nchi hii haina sera wala sheria. Viongozi na watendaji wa Serikali wanafanya mambo kwa unafiki na hulka za kutaka waonekane wazuri kwa kila mtu.
Itawezekana vipi wewe kiongozi au Serikali uonekane mzuri kwa mhalifu na mtu mwema.
Angalia hata suala tu machinga kuzagaa kila sehemu. Mara sijui waondoke, mara sijui wapangwe vizuri, mara sijui watafutiwe maeneo. Kauli zote hizi ni kwa sababu ya unafiki. Badala ya kuangalia sheria, kunakuwa na kauli ambazo hazieleweki ambazo zinawapa shida hata watendaji wa chini.
Sheria kama inasema hairuhusiwi kujenga au kufanya shughuli zozote kwenye vyanzo vya maji na hifadhi ya misitu, inatakiwa iwe hivyo. Kinachofuatia inatakiwa ni usimamizi tu wa sheria, siyo hadithi nyingine.
Sheria kama inasema mifuko ya plastic hairuhusiwi, hairuhusiwi kufanyia biashara au kuweka kitu chochote kwenye barabara au hifadhi ya barabara, inatakiwa iwe hivyo. Kinachofuatia ni taratibu za usimamizi. Hayo mambo sijui watafutiwe maeneo, kuna mtu aliwahi kutafutiwa hata nyumba tu ya kupanga? Si anatafuta mwenyewe?
Unafiki, katiba mbaya inayompa madaraka makubwa kupindukia Rais kiasi cha kila mtendaji kushindwa kufanya kazi mpaka asikie kauli ya Rais ni chanzo cha matatizo mengi. Mkiwa na Rais ambaye maamuzi yake ni ya hovyo, upeo duni au ana hulka ya kujipendekeza, nchi inabakia inayumbayumba tu.