Article nyingine kuhusu Mambo ya Mikataba ya Madini:
Kwa uelewa huu kipengele cha 15% kiliondolewa tangu 2004... hivyo tunahitaji data kama kipengele hicho bado kiko kwenye mkataba wa sasa huu unaoleta utata!
Serikali inafanya marekebisho katika sekta ya madini ili kupata faida na mapato zaidi kwa ajili ya wananchi wake.
Katika marekebisho hayo, Serikali imeshafanya majadiliano na kukubaliana na kampuni za Barrick Tanzania Limited (inayomiliki migodi ya Bulyanhulu ulioko wilayani Kahama, Tulawaka ulioko wilayani Biharamulo; na North Mara ulioko wilayani Tarime) na Resolute Tanzania Limited (inayomiliki mgodi wa Golden Pride ulioko wilayani Nzega) ili kuyawezesha kampuni hizi kulipa kodi na ushuru stahili kwa Serikali.
Katika majadiliano hayo kampuni hizi zimekubali kuondolewa kwenye mikataba baadhi ya vivutio vya ziada ikiwa ni pamoja na nyongeza ya asilimia 15 kwenye mtaji wa uwekezaji ambao haujarejeshwa/kukombolewa (15% additional capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure). Hatua hii itawezesha kampuni hizi kukomboa gharama zao za uwekezaji mapema na hivyo kulipa kodi ya mapato (corporate tax). Endapo kipengele hicho kisingeondolewa, kungekuwa na uwezekano mkubwa wa kampuni hizo kutolipa corporate tax.
Serikali bado inaendelea na majadiliano na kampuni ya Geita Gold Mine Limited inayomiliki mgodi wa Geita ili nayo ikubali kufuta kipengele hiki kwenye mkataba wake. Hata hivyo, Serikali tayari ilisharekebisha kipengele hiki cha 15% additional capital allowance on unredeemed qualifying capital expedicture, kilichokuwa kwenye Sheria ya Kodi ya mwaka 1973 ambayo ilifanyiwa marekebisho. Sheria ya Kodi ya mwaka 2004 haina kipengele hicho tena, hivyo mikataba mipya ya madini haitakuwa na kipengele hiki.
Pamoja na suala la ulipwaji kodi ya mapato (corporate tax), kampuni hutakiwa kulipa kodi na ushuru mbalimbali ikiwemo mrabaha. Mrabaha wa asilimia 3 kwa madini ya dhahabu na madini mengineyo; na asilimia 5 kwa madini ya almasi na vito hulipwa Serikalini bila kujali kama kampuni inapata hasara au faida tofauti na kodi ya mapato (corporate tax) ambayo hulipwa baada ya kampuni kupata faida kwa kuondoa gharama za uendeshaji na uzalishaji. Kodi nyingine zinazolipwa na kampuni za madini ni pamoja na kodi ya zuio (withholding taxes) kodi za ajira (PAYE); ushuru wa forodha, stamp duty; ambapo ushuru ni pamoja na ada ya pango (annual rent), ada ya maombi na utayarishaji wa leseni za utafutaji (application and preparation fee); na ada za leseni mbalimbali za biashara ya madini.
Katika jitihada za Serikali za kuhakikisha sekta ya madini inachangia ipasavyo kijamii na kiuchumi inafanyia marekebisho Sera ya Madini ya mwaka 1997. Aidha, Sheria ya Madini ya mwaka 1998 nayo inafanyiwa marekebisho ili kuhakikisha usimamizi wa sekta ya madini unaihakikishia Serikali na wananchi wake mapato zaidi kutokana na rasilimali ya madini.