Na James Marenga
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema Rais Jakaya Kikwete, amelemewa na kazi na hataweza kuwaletea mabadiliko Watanzania wanayoyatarajia.
Mbowe alisema hayo jana kwenye mkutano na waandishi wa habari, alioufanya nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, kuzungumzia tathmini ya ziara yake, ya kuwashukuru wananchi kwa kumpigia kura aliyoifanya kwenye mikoa kadhaa hapa nchini.
Alisema Tanzania ni nchi kubwa, ambayo haiwezi kuongozwa kutoka eneo moja tu la nchi kama inavyofanywa sasa na serikali ya Rais Kikwete.
Rais Kikwete na Waziri Mkuu wake wamekuwa wakihaha, wanatoka Ulaya wanazunguka mikoani, nchi hii ni kubwa hawawezi kuzunguka na kutoa maagizo yatakayoweza kurekebisha uchumi wa nchi hii peke yao, alisema Mbowe.
Alisema kuendelea kutoa maelekezo ya kuendeleza nchi kutokea Dar es Salaam, kutaendelea kuifanya mikoa kuwa maskini kutokana na ukweli kuwa haitumii vyema rasilimali zilizopo kwenye mikoa hiyo kwa maendeleo yake.
Alisema hivi sasa ni jambo la kusononesha kuona kwamba, mikoa na wilaya hapa nchini imekuwa ikigawanywa katika misingi ya kikabila badala ya kikanda na akasisitiza njia ya pekee ya kuepukana na hilo ni kuanzishwa kwa serikali za majimbo, ambazo chama chake kimekuwa kikipigia kampeni.
Alieleza kushangazwa na hoja zilizokuwa zikitolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kampeni mwaka jana ambazo zilikuwa zikidai kuwa, sera ya majimbo itakuza ukabila wakati ukweli ni kwamba mfumo wa sasa wa mikoa na wilaya ndiyo hasa unaokuza ukabila.
Alisema katika baadhi ya wilaya alizopita wananchi kadhaa aliozungumza nao walionyesha kutowajua wakuu wao wa mikoa na wilaya kutokana na ukweli kwamba watu hao hupata nafasi hizo za kuteuliwa badala ya kuchaguliwa kama itakavyokuwa iwapo majimbo yataanzishwa.
Hivi sasa rais anaweza akateua mtu kuwa mkuu wa mkoa au wilaya kwa sababu ni rafiki yake wa
au ni ndugu yake
Nimepita mahali watu hawamjui mkuu wao wa mkoa wala wa wilaya, kwa sababu watu hao hawakuwachagua, alisema Mbowe.
Akiendelea na mifano alisema kuna sehemu Rais Benjamin Mkapa katika kipindi chake chote cha miaka 10 ya urais wake alifika mara moja tu, jambo ambalo ni ushahidi mwingine unaoonyesha kuwa nchi ni kubwa, ambayo kamwe haiwezi kuongozwa kutoka Dar es Salaam.
Nchi kubwa kama hii, Waziri wa Elimu ndiye anaongoza sekta nyeti kama hiyo. Maamuzi ya elimu kwa nchi yote hii yanatoka Dar es Salaam. Hatuwezi kutegemea mabadiliko ya kweli kwenye sekta hiyo muhimu, alisema Mbowe.
Akirejea sera ya chama hicho ya kugawa nchi kwenye majimbo kwa kuwa na kanda za kiutawala alisema, mikoa mingi imekuwa nyuma kimaendeleo kwa kukosa utaratibu wa kiutawala wa kuamua mipango yao ya kimaendeleo.
CHADEMA tulikuwa tukisisitaza kuundwa kwa kanda, kwa mfano Kanda ya Ziwa ingekuwa na mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga na Mara, kanda hii ingekuwa na uwezo wa kupanga mipango yake hasa matumizi ya rasilimali zilizopo na kujiletea maendeleo.
Pato la mikoa ya Kanda ya Ziwa, hasa linalotokana na dhahabu pekee, ni asilimia 42 ya mapato ya nchi, kama mikoa hii ingekuwa na mikakati mizuri, ingeweza kujitosheleza na wananchi wake wasingalikuwa maskini, alisema.
Mwenyekiti huyo alipinga hoja iliyojengwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa kuigawa nchi kwenye kanda ni kuendeleza ukabila, kwa kusema mikoa hiyo imeundwa na makabila tofauti ambayo si rahisi kujenga ukabila.
Alisema sera hiyo pia ina lengo la kuhakikisha kuwa viongozi kwenye ngazi za mikoa wanatokana na ridhaa ya wananchi, na si uongozi wa kupeana kama inavyofanya serikali ya sasa.
Akizungumzia mkakati wa chama hicho kwa mwaka 2007, alisema kuanzia mwaka huu, chama hicho kinaanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi kwenye ngazi mbalimbali ili kupata viongozi wapya watakaosimamia mikakati ya chama hicho.
Alisema utaratibu utakaotumiwa na chama hicho si kama ule wa CCM wa kuwa na uchaguzi mmoja, watakachofanya ni kuwa na uchaguzi ambao utatoa nafasi kwa wanachama wote, kwa wakati unaofaa kugombea nafasi hiyo.
Mkutano mkuu ulibadilisha baadhi ya vipengele vya katiba, hata mimi nitamaliza muda wangu mwaka huu badala ya 2009, na anaweza kuchaguliwa mwenyekiti mwingine, chama chetu kina demokrasia, alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo alisema chama hicho kimeandaa mpango mkakati wa miaka mitano na kumi, ambayo inalenga kuimarisha chama hicho katika ngazi zote kuanzia matawi hadi taifa.
Tukimaliza ziara ya kuwashukuru wananchi, ziara ambayo tumeipa jina la tumaini jipya, tutahamia kwenye ziara ya ardhini, viongozi watakwenda wilaya kwa wilaya, mkoa kwa mkoa kukitangaza chama na kufungua matawi, kutoa semina na kueleza mkakati wa chama, alisema.
Ziara hiyo alisema itawahusisha wabunge, madiwani wa chama hicho na watendaji wengine na watatumia makabrasha mbalimbali yaliyoandaliwa na chama hicho kwa ajili ya kuelezea mikakati mbalimbali ya chama hicho.
(Tanzania Daima 6/1/2007)